Ni nani wenye kuitumikia zaka

Egypt's Dar Al-Ifta

Ni nani wenye kuitumikia zaka

Question

Nini maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wanaozitumikia} [Suratu TAWBA, aya ya 60], na ina maana gani katika zama zetu?

Answer

Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad s.a.w, watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

Wenye kuitumikia zaka (watumishi wa Zaka) ni moja ya aina nane za wanaostahiki kupewa zaka ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu ameainisha katika Quraani Tukufu ambapo alisema: {Sadaka hupewa (watu hawa): Mafakiri na Masikini na Wanaozitumikia na Wanaotiwa nguvu nyoyo zao (juu ya Uislamu) na katika kuwapa Uungwana watumwa na katika kuwasaidia Wenye deni na katika (kutengeneza) Mambo aliyoamrisha Mwenyezi Mungu na katika (Kupewa) Wasafiri (walioharibikiwa). Ni faradhi inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi (na) Mwenye hikima}[AT TAWBA, 60]. Neno “wenye kuitumikia” maana yake ni watu ambao kazi yao ni kukusanya sadaka. Watumishi wa zaka ambao wanakusanya zaka kwa kuichukua kutoka kwa wenye wajibu wa kutoa zaka ili kuwapa wenye kustahiki.

Al-Tabariy alisema kuelezea njia hii ya zaka: “wenye kuitumikia” ni wanaojitahidi kuichukua kutoka kwa wenye kuitoa na kuwapa wanaostahiki, “wenye kuitumikia” wanakuwa na fungu maalum kutokana na kazi yao wawe matajiri au masikini. Na Maakil bin Ubeiduallah alisema: nilimwuliza Al Zuhariy kuhusu maana ya “wenye kuitumikia” akasema: "wenye kazi ya kuchukua zaka kutoka kwa anayewajibika na kuwapa wanaostahiki", naye Qatada alisema: "waliokusanya na kujitahidi kutekeleza kazi hiyo". Na Ibn Zayed alisema: "anayeshughulikia ukusanyaji wa zaka" [Tafseer Al-Tabariy, 4/130, Muasasat Al-Risala].

Na Ibn Abi Hatem alisema katika tafsiri ya kauli ya Allah S.W. “wenye kuitumikia”: “Ibn Abbas alisema: “wenye kuitumikia” ni wale wanaofanya kazi ya kukusanya sadaka” [Tafseer Ibn Abi Hatem, 6/1821, Ch. Mak-tabat Nidhar Mustafa Al-Baz].

Al Qurtubiy alisema: “wenye kazi ya kukusanya sadaka ambao mtawala huwapeleka kukusanya mali ya sadaka kwa niaba yake. Bukhari alipokea kutoka kwa Abi Humeid As-Saaidii alisema: Mtume S.A.W. alimpa mtu mmoja wa kabila la Azd aitwaye Bin Lutbiyyah kazi ya kukusanya sadaka za Bani Salim. Mtu huyo aliporejea baada ya kutekeleza kazi yake, Mtume S.A.W. alimwuliza kafanya nini” [Tafseer Al-Qurtubiy, 8/177, Ch. Dar Al-Kutoob Al-Misriya].

Imamu Al-Taher bin Ashur alisema: “(wenye kuitumikia) maana yake ni wale wanaofanya kazi kwa ajili yake; kwa ajili ya kukusanya sadaka, na hapa herufi (a’la (asili yake ni “kwa ajili” kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {na “Anakutakieni” kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kuwa Amekuongozeni, ili mpate kushukuru}[AL BAQARAH, 185]; yaani kwa ajili ya kukuongozeni, na maana ya kazi hapa ni jitihada na huduma, na wale wanaoshughulikia kukusanya zaka ya mifugo. Kuchagua herufi (a’ala) hapa kunaashiria asili ya maana yake ya madaraka; yaani wale wanaofanya kazi kwa bidii kwa ajili ya kuikusanya; kwani hawa daima huchoka katika kufanikisha kazi hiyo kubwa” [Al-Tahriri wa Al-Tanweer, 10/235, Ch. Al-Dar Al-Tunisia].

Tena haishurutishwi katika wenye kuitumikia zaka kuwa wenye ufukara waweze kupata sehemu ya mali; kwani wanaipata (sehemu hiyo ya mali) kwa ajili ya kazi yao, si kwa ufukara wao.

Ibn Majah alipokea kutoka kwa Abi Saidi Al-Khudariy alisema: “Mtume s.a.w. alisema: sadaka haijuzu (kutolewa) kwa wenye utajiri isipokuwa kwa watu wa aina tano; … kisha akataja (miongoni mwao) mwenye kuitumikia zaka”.

Wanachuoni walihitalifiana kuhusu kiwango wanachokipata wenye kuitumikia kutoka mali ya zaka; madhehebu ya Hanafi walisema: anapewa kwa kadri ya kazi yake, anapewa yeye na wasaidizi wake lakini isizidi nusu ya mali ya zaka anayoikusanya hata kama kazi yake ni nyingi” [Rejea: Al-Hidaya pamoja na maelezo ya Fat-h Al-Qadir, Ibn Al-Hamam, 2/16, Ch. Al-Amiriya].

Madhehebu ya Shafiy na Hanafiy walisema: Imamu ana haki ya kumwajiri mwenye kuitumikia kwa malipo maalumu ikiwa kwa muda maalumu au kwa kazi maalumu. Kisha Madhehebu ya Shafiy walisema: "mwenye kuitumikia hapewi zaidi ya mali ya zaka iliyokusanywa na ikiwa anastahiki malipo zaidi basi anapewa hiyo ziada kutoka Baytul-Mal, tena inajuzu kwa Imamu ampe malipo yake moja kwa moja kutoka Baytul-Mal" [Al-Majmuu’ Al-Nwawawiy, 6/187, Ch. Dar Al Fikr].

Al-Tabariy alisema: wenye kutoa fatwa walihitalifiana katika kiwango ambacho anapewa yule mwenye kuitumikia, baadhi yao walisema: anapewa thumni yake. Na Adh-hak alisema: wenye kuitumikia wanachukua thumni ya mali ya sadaka iliyokusanyika, naye Mujahid alisema: wanachukua thumni, na wengine walisema: wanachukua kiwango kinachokuwa sawa na kazi yao; ambapo alisema Ibn Zayed: mwenye kuitumikia anapewa malipo akiifanya madhubuti; kwani Omar R.A. alikuwa hawapi wenye kuitumikia thumni ya mali ya zaka lakini alikuwa anawakadiria malipo kutokana na kazi yao [Tafseer Al-Tabariy, 14/130].

Al-Qurtubiy alisema: “Maulamaa walihitalifiana katika kauli tatu kuhusu kiwango ambacho wanapewa wenye kuitumikia. Mujahid na Shafii walisema: wanapewa thumni. Ibn Omar R.A. na Malik: wanapewa kiasi kinachokuwa sawa na kazi yao, nayo ni rai ya Abu Hanifa na wenzake wasemao: wanapewa ujira kutokana na kazi yao; kwani wao wamejitolea wakati wao kwa ajili ya masilahi ya mafukara, kwa hiyo inalazimika kuwatosheleza wao na wanaowasaidia, kama mke anayemhudumia mumewe, basi matumizi yake mwenyewe na ujira wa watumishi wake mmoja au zaidi ni juu ya mumewe. Aidha kuwatosheleza wenye kuitumikia kunakuwa sawa na riziki ya kadhi. Kundi la tatu: wenye kuitumikia wanapewa ujira wao kutoka Baytul Mal, ambapo alisema Ibn Arabiy: nayo ni kauli thabiti ya Malik bin Anas iliyopokelewa na Ibn Abi Aues na Daoud bin Said bin Zanbu’a, ingawa hoja yake si nzito; kwani Mwenyezi Mungu amebainisha sehemu yao katika Qurani kwa uwazi. Na kauli sahihi ni kujitahidi tu katika kiwango cha ujira …” [Tafseer Al-Qurtubiy, 8/177].

Katika zama zetu kamati ya zaka iliyoruhusiwa na Imamu (mtawala) inakuwa na hukumu sawa sawa na wenye kuitumikia; kwani inashughulikia kukusanya zaka kwa niaba ya Imamu, basi inajuzu kwa kamati hii kuwapa watumishi wake wenye kushughulikia hii kazi ujira kutoka mali ya zaka, ama wana kamati wenye kuendesha mambo hayo (wasio kusanya wenyewe) hawawi na haki ya kuchukua mali; kwani wanawakilisha wenye kutoa zaka katika hili jambo, na wakili hana haki ya kupewa kutoka zaka.

Kutokana na yaliyopita; wenye kuitumikia zaka ni wanaoshughulika kukusanya mali ya zaka nao ni watumishi wa kamati ya zaka katika zama zetu wanaofanya kazi ya kukusanya mali ya zaka kutoka kwa wenye wajibu wa kutoa zaka sio waasisi wa kamati.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi.
 

Share this:

Related Fatwas