Maadili ya Kislamu na Sifa Zake.
Question
Zipi sifa za maadili ya Kiislamu ?
Answer
Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
Maadili katika Uislamu yana sifa maalumu zinazoyajaalia kutafautiana na maadili ya falsafa na nadharia zote za ulimwengu - Mhadhiri na mkuu wa zamani wa kitengo cha falsafa ya Kiislamu katika kitivo cha Daarul-Uluwm Profesa Abdulhamiyd Madkuwr anaeleza baadhi ya sifa za maadili ya Kiislamu kama ifuatavyo :
Kwanza: Uwezekano wa kupatikana kiukweli.
Pili: Kujinyima, kumpendelea mwingine na kupinga ubaguzi.
Tatu: Huruma na rehma.
Nne: Nia na kazi.
Tano: Udhibiti na uhuru.
Sita: Kigezo chema chenye kutekelezeka.
Saba: Ukamilifu wa chanzo.
Nane: Maumbile timilifu.
Tisa: Kukirimu.
1- Uwezekano wa kupatikana kiukweli: Hakika Quraani inapoonesha misimamo yake katika mambo ya daawa kwa haki, kheri na wema haitosheki kwa kuonesha nadharia tu na kutaja misingi tu bali inaongezea yanayojulisha uwezekano wa kutokea duniani, na jambo hilo ndio lengo kati ya malengo ya visa vingi vya Quraani vinavyosimulia vigezo vyema vya tabia njema hasa vinavyohusiana na visa vya Mitume, visa ambavyo vimewazungumzia wao na wafuasi wao walioharakia kuwaamini. Mitume hii imekuwa mifano mizuri katika haki, kuvumilia matatizo, kuamini ahadi ya Mwenyezi Mungu na walikuwa mifano mizuri katika utiifu, ahadi, kuridhia majaaliwa ya Allah S.W. na kushukuru neema za Mwenyezi Mungu. Na hapa tutaashiria kisa cha Nabii IBRAHIM na kuitikia kwake yale aliyomwaamrisha Allah sw katika ndoto ambayo ni kumchinja mtoto wake, na kisa cha Yussuf A.S na kuvumilia kwake mtihani kutoka kwa Allah S.W. mpaka Allah S.W. akampa neema zake, pia Nabii Suleiman kushukuru neema ya Mwenyezi Mungu, na subira ya Nabii Ayubu kutokana na mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na pia wachawi wa Firauni kumwamini Mola wa Mtume Mussa na kushikilia kwao juu ya haki licha ya vitisho vya Firauni dhidi yao kwa kuwasulubu na adhabu kali .
2- Aidha visa vya Quraani vimeonya mabaya na tabia mbaya ili watu wajiepushe na mambo hayo. Miongoni mwa visa hivi ni kisa cha mwenye bustani mbili kilichosimuliwa katika Suratu Kahf, na kisa cha wamiliki wa bustani kilichotajwa katika Suratu Qalam, na kisa cha mtu aliyemwahidi Mwenyezi Mungu kutoa sadaka na wema halafu akenda kinyume na ahadi yake pamoja na Mwenyezi Mungu, na kisa hiki kimetajwa katika Suratu Tawbah. Haya yote yanamaanisha kwamba maadili ya Uislamu hayaning’inii hewani bali yanakusanya pamoja nadharia na utendaji .
3- Na utekelezaji bora wa maadili haya unapatikana katika tabia za Mtume Muhammad S.A.W aliyesifiwa na Mwenyezi Mungu katika kauli yake {Na bila shaka una tabia njema kabisa} [AL QALAM 4]. Na masahaba waliochukuwa mafunzo yake waliopata daraja kubwa kwa Allah S.W. na kwa watu waliendeleza vizuri sana maadili haya baada ya Mtume S.A.W.
4- Pili: Kujinyima, kumpendelea mwingine na kupinga ubaguzi: Hakika maadili katika Quraani Tukufu yamekemea sana ubaguzi, na yamesifu tabia ya kumpendelea mwingine. Maadili katika Uislamu hayakuwa kama maadili wakati wa ujinga kabla ya Uislamu, katika wakati huo maadili yalijengeka kwa chuki za ukabila. Uislamu ukasahihisha fikra hizo potofu, na Uislamu haukujaalia kumnusuru mwislamu kwa kabila lake bali umejaalia nusura kwa waislamu wote, kwani waislamu wote ni ndugu katika Uislamu. Allah S.W. anasema {Hakika Waumini ni ndugu} [AL HUJURAAT 10]. Kisha Uislamu haukujaalia nusura kwa haki na batili bali umejaalia nusura katika haki tu. Na Uislamu umejaalia mwislamu kumnusuru ndugu yake mwislamu kwa kumkinga na dhuluma na kumwepusha na uadui. Na katika utukufu wa tabia za Kiislamu ni Uislamu kuwataka waislamu kutenda haki na uadilifu hata na maadui zao. {Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda}. [AL MAAIDAH 8].
5- Tatu: Huruma na rehma: Ikiwa maadili ya Kiislamu yanajengeka kwa udugu, kumpendelea mwingine na uadilifu, basi pia yanajengeka kwa huruma na rehma, na huruma hii inajumuisha wanadamu wote na wanyama. Ni vizuri hapa kutaja hadithi ya Mtume S.A.W : “Mwanamke mmoja aliingia motoni kwa sababu ya kumfingia paka mpaka akafa bila ya kumlisha chakula wala kumnywesha, amemfunga bila ya kumwachia kujitafutia chakula atakachokipata juu ya ardhi”. [(Bukhary hadithi ya 3295, Muslim hadithi ya 2242 kutoka kwa Ibn Omar]. Na kauli yake S.A.W “Katika kumfanyia huruma yoyote mwenye ini (kiumbe) kuna malipo” [Imetolewa na Bukhary hadithi ya 2234, na Muslim hadithi ya 2244 kutoka kwa Abu Hurayra] .
6- Maadili ya Kiislamu yanazuia maudhi, kisha maadili haya yanapanda ngazi na kuwa ya ushirikiano, huruma na kumpendelea mwingine. Na kwa hivyo watu wengine si maaadui kwa mtu yeyote ambaye wanataka kumuua, au kumnyang’anya uhuru wake kama alivyosema SARTAR alipotuletea taswira ya kwamba kuna watu wengine ambao wapo kwa ajili ya kumpokonya mtu uhuru wake ambao ndio asili ya kuwepo kwake na uhalisia wa uwepo wake, au wawe kizuizi cha kuzifikia nyenzo na malengo na hili ni jambo ambalo linatufichulia mtazamo uliojaa hali ya kukata tamaa na giza tetere na mnyemeleo unaotia shaka shaka na hofu ya kudumu inayojitokeza kila wakati, kwani mtu katika Uislamu huwaangalia wengine wasio kuwa waislamu kama ndugu, na wao pia humuona yeye hivyo hivyo, na hasa pale wanapokomaa kimaadili kama utakavyo Uislamu na hivyo kupelekea kufikiwa kwa kiwango cha juu cha ushirikiano, upendo na kuthaminiana. Na ukosoaji huu unahusu mwelekeo wa manufaa pia, kwa namna ambayo ameifikia mmoja kati ya vigogo wake ambaye ni mwanafalsafa BENTAM kwa kuyatanguliza maslahi ya mtu juu ya maslahi wengi pale yanapokinzana, kisha haya yanafanana pia na yale aliyoyasema mwanafalsafa wa kimagharibi ajulikanae kama, HOBS alisema kwa maneno yake kwamba binadamu kwa ndugu yake binadamu ni mbwa mwitu, na kwamba chuki kati ya watu, wao kwa wao, ni kama asili au mambile yao .
7- Kutokana na hayo yaliyotangulia, tunaweza kukataa waliyoyasema baadhi ya wataalamu kuhusu maadili ya Kiislamu kwa kujidai kwamba yanakosa fikra ya udugu wa kibinadamu, na tuhuma hizi hutupelekea kueleza matini zilizotangulia ambazo zinathibitisha kuwa Uislamu unajali sana udugu wa kibinadamu na unalingania huruma na rehma kwa viumbe vyote.
8) Nne: Nia na kazi : Uislamu umetilia maanani sana katika wasia wake wa kimaadili kuhusu nia, na ukajaalia matendo kufungamana na nia: “Hakika matendo yanafungamana na nia, na kila mtu atalipwa kutokana na nia yake, basi yule ambaye kuhama kwake ni kwa ajili ya Allah na Mtume wake basi kuhama kwake ni kwa ajili ya Allah na Mtume wake, ama yule ambaye kuhama kwake ni kwa ajili ya kuipata dunia au mwanamke amuoe basi kuhama kwake ni kwa yale aliyoyaendea”. [Imepokelewa na Bukhary hadithi ya kwanza kutoka kwa Omar bin Khattab].
9- Uislamu umejaalia nia ni asili ya kunyooka kazi ya kimaadili. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu anakubali amali ya mtu anayeitakasa nia yake kwa Allah S.W., hata kama hajaitimiza lakini nia yake ni kuifanikisha. Haya yamefafanuliwa na hadithi ya Mtume S.A.W. “Kutoka kwa Mtume S.A.W.: Mtu mmoja alisema nitatoa sadaka usiku huu, akatoa sadaka yake kwa kumpa mzinifu mwanamke, watu wakasema kwamba amempa sadaka mzinifu usiku, yule mtu akasema: Ewe Allah shukrani ni zako juu ya mzinifu na nitatoa sadaka tena, akatoa sadaka yake kwa kumpa tajiri, watu wakazungumza tena kwamba sadaka yake kampa tajiri, akasema: Ewe Allah shukrani ni zako juu ya tajiri na nitatoa sadaka tena, akatoa sadaka yake kwa kumpa mwizi, watu wakaanza kuzungumza tena amempa sadaka yake mwizi, akasema Ewe Allah shukrani ni zako juu ya mzinifu, tajiri na mwizi. Akamjia mtu (usingizini) akaambiwa: Sadaka yako imekubaliwa. “Ama sadaka yako uliyompa mzinifu, huenda ikamtosheleza na kuacha uzinzi, na sadaka uliyompa tajiri, huenda ikamkumbusha na kuanza kutoa alichompa Allah, na sadaka uliyompa mwizi, huenda ikamtosheleza na kuacha wizi”. [Imepokelewa na Muslim, hadithi ya 1022].
10- Ama wale ambao hawajali kusafisha nia wala kuitakasa kutokana na kujiona na unafiki basi amali zao hazikubaliwi, bali watapata dhambi badala ya thawabu: {Sema: Je! Tukujulisheni wenye hasara katika vitendo (vyao)? Hao ambao bidii yao (hapa duniani) imepotea bure katika maisha ya dunia, nao wanafikiri kwamba wanafanya amali njema!}. [AL KAHF 103-104]. Mtume S.A.W anasema: “Hakika mja anafanya matendo mema, basi Malaika wanapanda na daftari lake na kuliweka mbele ya Mwenyezi Mungu, Allah S.W. atasema: litupeni daftari lake kwani hakufanya matendo hayo kwa kutafuta ridhaa zangu. Halafu anawaambia Malaika: Mwandikieni mtu fulani haya na haya, mwandikieni haya na haya, Malaika watasema: Ewe Mola wetu! Hakika mja huyu hakufanya kitu. Mwenyezi Mungu atasema: Hakika yeye amenuia kutenda mema”. [Al-iraaqiy alisema katika Takhrij Al-Ihyaa 4\162: Imetolewa na Aldarqatniy kutoka kwa Anas, na kwa mapokezi mazuri].
11- Uislamu haujatilia umuhimu nia peke yake licha ya kukiri umuhimu wake, na umemtaka muumini kutia nia njema katika amali njema. Na ndio maana Uislamu umejaalia amali njema daima inafungamana na imani katika aya nyingi, kama kauli yake Allah S.W: [Na wabashirie walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo mito kati yake] [AL BAQARAH 25]. Hii ni dalili kwamba njia ya wema haipatikani tu katika nia njema pekee wala katika undani wa amali pekee bali hupatikana kwa yote kwani haiwezekani kutegemea moja bila ya jingine.
12 – Na Uislamu katika kukiri thamani ya nia, umekiri pia umuhimu wa kazi ya kimaadili. Bila shaka nia ni kipengele muhimu katika mchakato mzima wa maadili. Na Uislamu umejiepusha na madhehebu ya maadili yanayohimiza matokeo tu kama madhehebu ya ladha, furaha na manufaa, kwani kwa kupuuzia kwake nia, hushindwa kutathmini tabia ya kiukweli na pia umihimu wake unajikita juu ya mitindo tu bila ya malengo, na huporomosha utukufu na utakatifu wa tabia unaotakikana .
13– Pamoja na Uislamu kutilia umihimu nia, pia umechunga matokeo ya nia, kwani matokeo yana nafasi kubwa katika kutengeneza amali ya kimaadili. Na binadamu hawezi kufanya kazi kwa bidii bila ya lengo maalumu. Kutokana na hayo, kuna uhusiano mkubwa baina ya kumili au nia au makusudio na matokeo ya kazi.
14 – Tano: Udhibiti na uhuru: Uislamu unawataka wafuasi wake kuwa na maadili ya Kiislamu yanayokusanya pande mbili udhibiti na uhuru. Maana ya udhibiti hapa ni kila jambo lina mipaka maalumu katika vyanzo vikuu vya Uislamu, ambapo hulindwa kutokana na ghasia na upotoshaji. Halafu mwislamu anatekeleza jambo hilo kwa nguvu zake, uwezo wake na hali yake. Kwa mfano katika mambo ya ibada, Mwenyezi Mungu amefaradhisha ibada juu ya kila mwislamu mwenye uwezo, asipotenda anakuwa mpungufu, halafu ukafungua mlango mpana wa ibada ya hiari ili kila mwislamu azidi kumtii Mwenyezi Mungu kwa urahisi wake. Na hali hii inapatikana aidha katika maadili. Muumini anapaswa kujiepusha na haramu mpaka imani yake iwe imara moyoni, na haitoshi kujiepusha na haramu bali pia aache baadhi ya Mubah ili asitumbukie katika haramu.
15– Na kwa sifa hiyo, Uislamu unatofautiana na yale madhehebu mengine ya kimaadili yanayojengeka juu ya msingi wa uhuru usio na mipaka, na kauli za baadhi ya wanafalsafa wa kileo wa kimagharibi na wafuasi wa falsafa zinamfanya binadamu ajiwekee mazingira ya tabia na ajichagulia anayoyataka bila ya kutekeleza amri.
16– Sita: Kigezo chema chenye kutekelezeka: Kigezo chema katika maadili ya Kiislamu kinasifika kwa kuwa kinakusanya mfano mwema wenye kutekelezeka. Maadili katika Uislamu hayatosheki tu katika kigezo chema peke yake ili watu wasije wakashindwa kutekeleza kwa mujibu wa maumbile yao na hali zao za kinafsi, na hayatosheki kwa upande wa kutekelezeka tu ili watu wenye nyoyo za ari kubwa wasinyimwe kupanda katika majukwaa ya hadhi, bali maadili haya yamekusanya mambo mawili kwa pamoja. Uislamu umempa binadamu haki ya kujitendea haki na kujinusuru anapokumbwa na maudhi au uadui. Uislamu umekiri haki hii kwa wafuasi wake na haujawanyima kwa kuwa unatambua hisia za kimaumbile ambazo zinampatia haki kwa kulipiza uadui. Allah S.W. anasema: {Na ambao wanapofanyiwa jeuri hujitetea} [ASHURAH 39]. Uislamu baada ya kukiri jambo hilo kwa mwenye haki hii, ukafungua mlango wa kusamehe na ukapendelea mtu kusamehe na suluhu ili apate fadhila za Allah S.W. na malipo yake bora. [Na malipo ya ubaya ni ubaya ulio sawa na (ubaya) huo, lakini anayesamehe na kusuluhisha ugomvi , ujira wake uko kwa Mwenyezi Mungu, bila shaka Yeye hawapendi madhalimu] [ASHURAH 40]. Kisha Quraani Tukufu inabainisha kuwa daraja hiyo hawaifikii ila wenye imani imara. [Na wale wanaolipiza kisasi baada ya kudhulumiwa, hao hakuna njia ya kulaumiwa. Bali lawama iko juu ya wale wanaodhulumu watu na wakawafanyia jeuri katika ardhi pasipo haki, hao ndio watakaopata adhabu iumizayo. Na anayesubiri na kusamehe (atalipwa wema wake). Bila shaka hilo ni katika mambo makubwa ya kuazimiwa kufanya]. [ASHURAH 41-43].
17– Saba: Ukamilifu wa chanzo: Vyanzo vya maadili ya Kiislamu vinarejea kwa Mwenyezi Mungu kama ulivyo Uislamu ambao unarejea kwake. Yaani vyanzo vyake ni kwa Allah anayesifika kwa ukamilifu, mjuzi wa kila kitu, mwenye hekima, huruma, kheri na haki kamilifu. Allah S.W. anasema {Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu chochote, lakini watu wanajidhulumu (wenyewe) nafsi zao. (wamepewa mianga ya maarifa hawataki kutumia}. [YUNUS 44]. Na Mwenyezi Mungu anawaita waja wake kwa huruma na upole: "Enyi waja wangu, hakika nimeharamisha dhulma juu ya nafsi yangu na nimeijaalia kuwa haramu baina yenu, basi msidhulumiane". [Imepokelewa na Muslim, Hadithi ya 2577 kutoka kwa Abu Dharri]. Uhusiano wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake haukomi tu kwa kuwakataza dhulma bali unapindukia rehma zake kwao. {Mola wenu amejilazimisha rehema}. [AL ANAAM 54]. Allah S.W. katika sheria zake hajaishia tu katika huruma bali anawashughulikia waja wake kwa fadhila zake, wema wake na ukarimu wake, aidha anawasamehe makosa yao na kuwasamehe madhambi yao, pia anawazidishia mema na anawaingiza peponi waja wake kwa rehma zake kutokana na matendo yao mema. Halafu sheria zake hazina uzito wala ugumu. {Na wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika dini}. [AL HAJ 78].
18– Ikiwa sheria ya Mwenyezi Mungu inasifika kwa usamehevu huu, basi mwenye kuamini na kuridhia sheria hii anapaswa kukubali amri za maadili kutoka chanzo hiki kwa kuridhia, maadili ambayo yanakataa chuki, yanatuletea upole na yanalenga kutupa kheri. Ikiwa Allah S.W. ndio chanzo cha maadili ya Kiislamu basi maadili haya yanatofautiana na maadili katika falsafa nyingine ambazo vyanzo vya maadili ni akili kama falsafa ya Kant au ni jamii kama falsafa ya Ogest Kont, Dorkayem, Livery Brel n.k. Aidha maadili ya Kiislamu yanatafautiana na maadili ya Arosto ambaye hajazidisha fadhila yoyote ya kimaadili kwa Miungu, mtazamo wake haukuwa na faida yoyote isipokuwa ni muono tu.
19– Kwa kuwa sheria ya Kiislamu ni chanzo cha maadili, basi haina maana kwamba imemnyima mwislamu matunda ya akili na ujuzi wa kibinadamu kiujumla katika yanayohusiana na maadili au mambo mengine ikiwa matunda hayo hayapingani wala hayagongani na maamuzi ya sheria ya Kiislamu. Dalili ya hayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu: {Ambao husikiliza kauli (nyingi zinazosemwa), wakafuata zile zilizo njema. Hao ndio aliowaongoa Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye akili.} [AZ ZUMUR 18].
20– Nane: Maumbili timilifu: Mtazamo wa dini ya Kiislamu unaeleza kuwa binadamu amezaliwa hali ya kuwa ana uwezo wa kufanya kheri na shari. {Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake}. [AS SHAMS 8]. Aidha mwanadamu anaweza kuchagua njia yake katika maisha kwa kuwa Mwenyezi Mungu amemjaalia nguvu na vitendea kazi vya kumwongoza na kumwelekeza. {Na tukambainishia njia zote mbili (iliyo njema na iliyo mbaya)}. [AL BALAD 10]. Na mwanadamu mwenye maumbile ya hekima yuko karibu zaidi na kheri kuliko shari, kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtunukia utukufu. {Na hakika tumewatukuza wanadamu na tumewapa vya kupanda barani na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewatukuza kuliko wengi katika wale tuliowaumba kwa utukufu ulio mkubwa}. [AL ISRAA 70].
21– Tisa: Kukirimu: Mwenyezi Mungu amemkirimu mwanadamu kwa kumuumba mwenyewe, na akawaamrisha Malaika wamsujudie, na akamchagua kuwa kiongozi duniani, na akamwandaa kuchukua amana. Na katika kumkirimu mwanadamu kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu, Mwenyezi Mungu amemuumba binadamu hali ya kuwa hana kosa wala dhambi. Binadamu anaanza maisha yake akiwa msafi bila ya kubeba makosa na madhambi ya wengine. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na kwamba mtu hatapata ila yale aliyoyafanya}. [AN NAJM 39] .
22 – Uislamu unatofautiana na msimamo wa Uyahudi na Ukristo kuhusu binadamu, Taurati inazungumza kwamba Adam na mke wake Hawa wanabeba laana ya hatia kwa sababu ya kumwaasi Mwenyezi Mungu, pia inasema kuwa laana ya ardhi inatokana na dhambi yao. Ama Ukristo unazingatia fikra ya kurithi dhambi ni miongoni mwa sifa zake tangu itikadi zake zilipozidishwa na Polis. Wakristo wanaitakidi kwamba Yesu ni Mwokozi wa wanadamu kutokana na kosa la dhambi ambalo wanadamu wamelirithi kutoka kwa Adam, maelezo yao yanakwenda kinyume na Quraani iliyoweka wazi na kufafanua kila kitu. Quraani inahakikisha kuwa dhambi ya Adam ni dhambi yake yeye kama yeye, inamhusu yeye peke yake. Na Mwenyezi Mungu alimsamehe Adam baada ya kutubia.: {Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake Mlezi alimkubalia toba yake, hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba na Mwenye kurehemu.}. [AL BAQARAH 37]. Kisha Toba hii ilikuwa dalili kwamba Mwenyezi Mungu amemteua Adam na amemchagua. {Kisha Mola wake Mlezi akamteua, na akamkubalia toba yake, na akamwongoa.} [AT TAWABAH 122].
23– Ama kizazi cha binadamu, Mwenyezi Mungu anakihukumu kwa ukurasa mweupe bila ya kuwa na dhambi kinapozaliwa, na hakihusiki na dhambi ya Adam. Mtu analipwa kutokana na vitendo vyake, na huwekwa mbele ya macho yake ahadi ya Allah pamoja na Adam. {Tukasema: Shukeni nyote; na kama ukikufikieni uongofu utokao kwangu, basi watakaofuata uongofu wangu huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika}. [AL BAQARAH 38]. Na jambo hilo kwa hakika linaafikiana na uadilifu unaosimamiwa na maadili ya Kiislamu.
24 – Mwisho: Hizi ni baadhi ya sifa za maadili ya Kiislamu ambayo chanzo chake ni Quraani na Sunna ya Mtume S.A.W. Sifa hizo zinatekelezeka ndani ya Uislamu, wala hazitekelezeki katika nadharia nyingine kwa ukamilifu huu, kwa sababu maadili ya Kiislamu ni pambo la Mwenyezi Mungu. {(Uislamu) ni pambo la Mwenyezi Mungu (alilotupamba). Na ni nani aliye mzuri kwa kupamba kuliko Mwenyezi Mungu ? Na sisi tunamuabudu yeye tu”. [AL BAQARAH 138]. Uislamu unajumuisha masilahi ya mtu na masilahi ya jamii, na huunganisha dunia na akhera katika mfumo usiopingana wala kugongana, na unajengeka kwa uadilifu na kumpendelea mwengine.
Marejeo : Profesa Abdulhamed Madkour, Diraasaat Fiy Ilmu Akhlaaq, Alqaahira : Daar ALhaaniy, 1426 H \ 2005, Uku. 112-126.