Ustaarabu wa Kiislamu na Misingi ya...

Egypt's Dar Al-Ifta

Ustaarabu wa Kiislamu na Misingi yake ya Kiungu katika Quraani na Sunna.

Question

Ustaarabu wa Kiislamu unajengeka kwa misingi gani ya kiungu kwa mujibu wa Quraani tukufu na Sunna tukufu?

Answer

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

1- Hakika Uislamu ni dini ya mwisho ya kiungu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake S.A.W. waliimarisha misingi imara ya ustaarabu wa Kiislamu kwa kuufurahisha ubinadamu. Marehemu Profesa Shauqiy Dhaifu Mkuu wa Taasisi ya Kiarabu anasema misingi hiyo inagawika katika misingi ya kiakida, misingi ya kijamii na misingi ya kimaadili, pamoja na kumtukuza mwanadamu kwa kumtahadharisha yanayoyavuruga maisha yake kati ya yaliyokatazwa na yaangamizayo. Na kama misingi hii ya kiungu ingelipangilika katika maisha ya mataifa basi pangeliimarika nguzo za Uislamu, na udugu wa kibinadamu ungelienea kila sehemu kwa kuyajumuisha makundi yote bila kubagua kundi lolote, wala kuitenga nchi yoyote, wala bara lolote.
2- Na hapa tutaelezea kwa ufupi misingi hiyo mitatu; misingi ya kiakida, misingi ya kijamii na misingi ya kimaadili. Na tutafafanua kila kitengo kivyake vyake kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na idadi ya misingi hiyo kwa sehemu zake tatu ni sabini na tatu, marehemu Profesa Shauqiy Dhaif ameeleza hayo katika utafiti wake wenye thamani (Ustaarabu wa Kiislamu katika Quraani na Sunna) unaozungumzia kiujumla misingi ya kiungu katika ustaarabu wa Kiislamu.

3- Sehemu ya kwanza: Misingi ya Kiakida: Kiini cha akida ya Kiislamu ni kumpwekesha Allah s.w, kumpwekesha huku ni katika dhati, sifa, matendo, na katika ibada zote, na misingi ya kiakida inasimamia yanayofuata: 1- Wahyi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. 2- Quraani Tukufu. 3- Mwenyezi Mungu Mtukufu. 4- Mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake. 5- Mtume Muhammad S.A.W. 6- Sunna ya kinabii. 7- Uislamu na Imani. 8- Swala na Zaka. 9- Saumu na Hija. 10- Dalili za Mwenyezi Mungu za kimaumbile. 11- Uislamu wa Ulimwengu wote. 12- Ushauri na Makubaliano. 13- Kujitahidi. 14- Uwepesi. 15- Uwastani. 16- Uhuru wa Kidini na Usamehevu. 17- Uadilifu. 18- Elimu. 19- Akili. 20- Kubatilisha uzushi, uchawi na ukuhani. 21- Hukumu na kadari. 22- Uchamungu. 23- Kutegemea 24- Khofu na woga. 25- Toba. 26- Msamaha.

4- Sehemu ya Pili: Misingi ya Kijamii: 1- Adabu ya maamkizi na kupeana mikono. 2- Kuomba idhini na adabu ya mabaraza. 3- Kuamrisha mema na kukataza mabaya. 4- Kuwafanyia wema wazazi wawili na jamaa. 5- Haki za Wanawake. 6- Undugu. 7- Usawa. 8- Kufanya kazi. 9- Sadaka. 10- Uaminifu. 11- Kutekeleza ahadi. 12- Haki. 13- Jihadi dhidi ya maadui. 14- Msamaha. 15- Upole. 16- Kuliwaza na kumpendelea mtu. 17- Huruma kwa binadamu na mnyama. 18- Kumkirimu yatima. 19- Kumkirimu jirani na mgeni. 20- Kuwatembelea wagonjwa, kuhudhuria mazishi na kuyazuru makaburi. 21- Kufanya kheri.

5- Sehemu ya Tatu: Misingi ya Kimaadili: 1- Usafi na nia. 2- Utukufu. 3- Ukweli na nasaha. 4- Unyenyekevu na haya. 5- Kutosheka. 6- Upole. 7- Uvumilivu. 8- Kuficha siri na kusitiri makosa ya mkosaji. 9- Kukinai. 10- Kuridhia riziki. 11- matendo mema. 12- Kumshukuru Mwenyezi Mungu. 13- Halali na Haramu. 14- Kuacha uzinifu. 15- Kuacha riba. 16- Kuacha mvinyo na kamari. 17- Kuacha dhulma. 18- Kuacha kiburi na majivuno. 19- Kuacha ushahidi wa uwongo. 20- Kuacha husdu. 21- Kuacha uwongo. 22- Kuacha kiapo cha uwongo na upuuzi. 23- Kuacha udanganyifu, kuepuka hadaa, kulaani na kutukana 24- Kuepukana na dhana mbaya na upelelezi. 25- Kuacha kuteta na usengenyaji. 26- Kuacha dharau na matusi.

6- Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpeleka Mtume wake kwa risala tukufu ya kiungu, na akampeleka kwa watu kama mtoaji wa habari njema na mwonyaji, mwongozaji na ni taa iangazayo, na kutoka kwake S.A.W. waislamu wakachukua Sunna zake zilizokusanya hadithi zake zinazobainisha aya za Quraani tukufu, na zinazokamilisha sheria ya Kiislamu, basi Uislamu umejengwa juu ya nguzo sita; kushuhudia upweke wa Mwenyezi Mungu, Kumwamini Mtume wake Muhammad S.A.W. na risala yake, kutekeleza Sala kwa kumtakasa Mwenyezi Mungu, kutoa Zaka kwa masilahi ya umma wote na kwa kila mwenye shida na aliyenyimwa, na kufunga mwezi wa Ramadhani kwa ajili ya kuisafisha nafsi na kutekeleza ibada ya Hija.

7- Na imani inakusanya: Kumwamini Mwenyezi Mungu, siku ya mwisho, malaika, vitabu vya mbinguni na manabii, na kutoa sadaka kwa wenye haja, pia inakusanya kutekeleza faradhi, kutekeleza ahadi na subiri njema, na Mwenyezi Mungu ameuweka ulimwengu huu kwa mbingu zake, sayari na ardhi kwa mimea yake kuwa chini ya uangalizi wa mwanadamu ili azingatie katika mfumo wake, maumbile yake na siri zake, kisha akili yake imwongoze kwamba Mwenyezi Mungu ni mmoja na ndiye aliyevitengeneza kwa uwezo wake na hekima yake.

8- Kwa hivyo, Ustaarabu wa kiislamu ni ustaarabu wa akili na daima hutumia akili. Anasema Mwenyezi Mungu hakika yeye amedhalilisha kila kitu katika ulimwengu kwa ajili ya kumnufaisha mwanadamu na kufichua kanuni zake za kisayansi zilizofichikana ndani yake. Na Anarudiarudia kwamba aliumba ulimwengu na sayari zake na kila kitu kilichomo ndani yake, na Mwanyezi Mungu alimtuma kila Mtume kwa watu wake isipokuwa bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad S.A.W. ambaye alimtuma kwa watu wote mashariki ya ardhi na magharibi yake kuwafahamisha Uislamu, kwani Uislamu ni dini ya kimataifa, na umataifa wake unabainika kwa kuwalingania watu wa vitabu vya mbinguni ili waufuate kwa kusahihisha dini zao. Na Uislamu umewataka waislamu kuwapatia watu wa dini nyengine katika nchi zao uhuru wao wa kidini katika kutekeleza ibada zao, na wazilinde nafsi zao, nyumba zao za ibada, mali zao na waishi pamoja nao maisha mazuri.

9- Na katika mazingira haya ya Kiislamu na kistaarabu, watu wenye dini tofauti walikuwa wakikutana katika vikao vyao vya elimu kwa ajili ya mijadala ya kidini pamoja na mazungumzo, -si kama inavyotokea hivi sasa katika vituo mbali mbali vya runinga, miongoni mwa wale ambao hawamiliki akili ukiongezea na mfumo, elimu na dalili- na wakijadiliana katika dini na imani zao kwa uhuru kamili.

10- Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake waliwaamuru waislamu kuchukua ushauri katika hukumu, na makubaliano ya wanachuoni yalikuwa ni chanzo cha tatu katika sheria ya Kiislamu baada ya Quraani na Sunna, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamejaalia kujitahidi katika kuzitambua hukumu katika matawi ya dini ni faradhi juu ya kila mwislamu, kwa hivyo kujitihidi ni chanzo cha nne katika sheria ya Kiislamu baada ya Quraani, Sunna na makubaliano ya wanachuoni.

11- Na wepesi ndio kiini hasa chenye uimara katika Uislamu na sheria yake. Na daima, Mtume S.A.W alikuwa akinasihi kutokuwa na msimamo mkali katika dini na alikuwa akiruhusu sana kuwarahisishia waislamu, na Mtume S.A.W. alikuwa akikasirika anapojua kuwa mmoja wa masahaba wake anajilazimisha asiyoyaweza, na wala hachukui ruhusa miongoni mwa ruhusa za Mwenyezi Mungu, na Mtume S.A.W. anasema: "Dini ni nyepesi siyo nzito".

12- Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wametoa wito wa uwastani katika ibada ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ameuita Umma wa Kiislamu ni Umma wa wastani yaani uko kati na kati baina ya uzidishaji na upunguzaji katika dini: na Mtume S.A.W. asema: "Ingia katika dini kwa upole".

13- Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake waliwaamuru waislamu wasimlazimishe mtu yoyote kuingia katika Uislamu, na Quraani tukufu ikateremsha kanuni kuu, waislamu waliitekeleza katika zama zao zote, {Hakuna kulazimishwa (mtu kuingia) katika dini} [AL BAQARAH 256], na sadaka katika Uislamu haziwahusu mafakiri wa waislamu tu, bali zinawajali mafakiri wasio waislamu kama mafakiri wa waislamu, kuwatendea vizuri mateka wao, pamoja na usamehevu wa Kiislamu ambao hakuna dini nyingine au Umma mwengine katika zama za kale au sasa umeutambua.

14- Na ustaarabu wa Kiislamu unaitukuza akili na elimu. Nao ni ustaarabu wa kielimu na kiakili tena kwa kiwango cha juu. Na madai ya wagomvi wa Uislamu eti Uislamu unawalingania waislamu kuamini kwa nguvu si kweli, kwani aya za Quraani zinakariri kwamba mwanadamu ni mwenye hiari, na atahisabiwa kwa matendo yake yote aliyoyatenda duniani.

15- Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamewahimiza waislamu mara kwa mara kumcha Mwenyezi Mungu, kumwabudu Mwenyezi Mungu ipasavyo, kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makazo yake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wakawahimiza waislamu kumtegemea yeye kwa ukweli, na Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake S.A.W. wakamsisitiza mja kuogopa adhabu ya Mola wake na kumwogopa, na Mwenyezi Mungu anafungua milango ya msamaha kwa atakayetarajia msamaha kwa nia njema, bila ya kujali aina au ukubwa wa dhambi za mtu huyo, na kwa mfano huo, Mwenyezi Mungu anafungua milango ya msamaha kwa atakaetubu bila ya kujali aina au ukubwa wa dhambi za mtu huyo, na Mtume S.A.W. anasema; "Mwenyezi Mungu hufurahishwa sana na toba ya mmoja wenu…" Hadithi.

16- Na pamoja na misingi ya kiakida ya kistaarabu ipo misingi ya kijamii ya kistaarabu kwa ajili ya masilahi ya ubinadamu na Umma wa Kiislamu, ikiwemo Uislamu kutaka kueneza salamu baina yao, salamu ambayo wanaikariri katika Sala tano, na Uislamu ndiyo dini ya kwanza iliyotoa wito wa amani tangu karne kumi na nne. Na ili kutilia mkazo wito huo Mwenyezi Mungu alijaalia amani ni jina miongoni mwa majina yake mema, na aliita pepo kwa Nyumba ya amani, na Uislamu unapendelea ukunjufu na kupeana mikono wakati ndugu wanapokutana, na unaweka maadili ya kistaarabu kwa mtu anaemtembelea mtu katika ziara yake hiyo, na umemwekea maadili kama hayo anapoingia vikaoni na namna ya kukaa na kuzungumza ndani ya vikao hivyo. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anawaamuru waislamu kuunda kundi la watu wanaoamrisha mema na kukataza mabaya. Kutokana na wingi wa waislamu alijaalia hayo kuwa mikononi mwa watawala kuyatekeleza na kuyasimamia. Na katika Quraani tukufu, Mwenyezi Mungu anaambatanisha amri ya kuabudiwa yeye na amri ya kuwatunza wazazi na kuwafanyia wema kwa ajili ya kuwaheshimu. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanarudia mara kwa mara wito wa wema huo na wema kwa mke, watoto na jamaa ili kutia mkazo mahusiano ya familia.

17- Na Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake mbora wa viumbe S.A.W. wamemwajibisha mwanamume kuchunga haki nyingi za mwanamke, Mola amesema kuwa wao wote asili yao ni moja nayo ni Adam kwa ajili ya kuwaweka pamoja na kuliwazana. Na kweli Mwenyezi Mungu amemruhusu mwanamume kuoa zaidi ya mwanamke mmoja, lakini hiyo kwa lengo la kuepuka madhara ya kijamii, na Uislamu umejaalia kwa mwanamke haki kamili ya kuendesha mali zake, haki ambazo hazipati katika dini nyingine na staarabu nyingine, na umemwajibisha mke awe na huruma na mapenzi kwa mumewe.

18- Na Uislamu umeweka misingi imara ya undugu baina ya waislamu. Kwa hivyo mwislamu humfanyia wema nduguye mwislamu na humsaidia kwa kumlea kijamii na kiuchumi, na kwa mfano huo Uislamu umeanzisha misingi kamili ya usawa baina ya waislamu, basi hakuna tofauti kati ya tajiri na fakiri katika maisha, pia hakuna tofauti baina yao katika Sala, Saumu na Hija na mengineyo kama haki na wajibu isipokuwa Zaka, kwa sababu Zaka ni wajibu juu ya tajiri kwa masilahi ya fakiri, na usawa huo kiujumla katika Uislamu unajaalia waislamu ni Umma mmoja wanategemeana wenyewe kwa wenyewe.

19- Na Uislamu unakataza mara kwa mara ukosefu wa ajira na uzembe, na unamtaka mwislamu kufanya kazi, na kuchuma vyakula vyake kwa halali ili mtu asiwe mzigo kwa jamii na ili watu wasishindwe kumsaidia anayehitaji miongoni mwao, na Mtume S.A.W. alisisitiza juu ya kuwaonea huruma wafanyakazi na kuwapa ujira ulioukubaliwa, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameusia kuwapa sadaka maskini, mayatima na wajane, na Mwenyezi Mungu amejaalia sadaka ni mkopo kwake wenye thawabu marudufu hadi mara mia saba, na ameweka utaratibu kwa anayetoa sadaka ili maskini asifanyiwe maudhi.

20- Uislamu na sheria yake umesisitizia juu ya uaminifu wa mwislamu na kumtaka ahakikishe kuwa anafikisha amana kwa mhusika na kwa wakati wake uliopangwa, na iwapo ataikanusha amana hiyo basi hiyo itakuwa ni hiana na dhambi kubwa sana. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake walitoa wito wa kutekelezwa ahadi, ahadi ya Mwenyezi Mungu katika ibada yake, ahadi ya mke na watoto katika kuwatunza, ahadi ya watu katika mahusiano, na ahadi ya madola katika mikataba, na kwa mfano huo Uislamu umetaka kutendewa haki katika ibada ya Mwenyezi Mungu, na kutekeleza haki za familia, jamii na Umma, na Mwenyezi Mungu amejiita kwa jina “HAKI” ili kujitukuza, na Uislamu ulijaalia jihadi dhidi ya maadui ni faradhi juu ya kila mwislamu ili kulinda dini yake, nchi yake na umma wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wametukuza kitendo cha kusamehe kosa bila kujali ukubwa wa kosa hilo, na ukahimiza upole na huruma katika mazungumzo kwa ajili ya kuwapenda watu, na mwislamu amtolee nduguye mwislamu salamu, furaha pamoja na maneno mazuri.

21- Na Uislamu umejaa huruma katika sheria yake, waislamu wanaoneana huruma, wanashikamana na nyoyo zao zinajaa upole na huruma si kwa binadamu tu bali hata kwa wanyama. Basi haijuzu kwa mwislamu kumbebesha mnyama wake mzigo mzito au kumuumiza, na Uislamu umehimiza kumfanyia wema yatima, kumlea na kusimamia mali yake kwa wema, na Mwenyezi Mungu amemkanya mlaji mali ya yatima kwa kumwadhibu kwa kuingia motoni, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wakamwusia mgeni, kumkaribisha vizuri na kumkirimu, pia wakamwusia jirani na kuheshimu haki zake za ujirani. Na ili kuimarisha mafungamano ya mshikamo baina ya waislamu, Mtume S.A.W. ametuusia kutembelea wagonjwa ili kuimarisha mapenzi pamoja na mgonjwa na jamaa zake. Pia amewausia kushiriki katika mazishi na Sala ya maiti kama ni njia ya kuwaliwaza wafiwa, na Mtume S.A.W. alikuwa akizuru makaburi na akiomba heri kwa maiti ili kupata mazingatio, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake mara kwa mara waliwahimiza watu kuwafanyia mema ndugu zao waislamu, na pia maadui zao washirikina, kwani Uislamu ni dini ya kimataifa inawakusanya watu wote chini ya bendera yake.

22- Na misingi hiyo ya kijamii katika ustaarabu wa Kiislamu inaimarisha misingi ya kimaadili ya kistaarabu. Mwenyezi Mungu na Mtume wake wametaka kusafishwa nia katika ibada yake na katika kazi zote njema zinazofanywa na waislamu. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake wanamuusia mwislamu kuwa na hisia za utukufu, na kujivunia heshima yake na daima asitamke isipokuwa jambo la kweli na alidhihirishe na wala asichelee lawama ya mtu yoyote. Na wanamhimiza mwislamu kushikilia ukweli daima, na kutoa nasaha bora kwa anayeomba nasaha, na maimamu wawape nasaha waislamu wanapohitajia katika mambo yanayoimarisha masilahi ya Umma.

23- Na Uislamu umetukuza unyenyekevu kwani huimarisha mapenzi kati ya mwislamu na nduguye mwislamu, basi yeye hamfanyii kiburi wala hajikwezi juu yake hata kama atakuwa na utajiri wa kiasi gani au kutoka katika familia ya hali ya juu, bali anamwonea huruma na kumnyenyekea kwa unyenyekevu mzuri unaothibitisha undugu ambao Mwenyezi Mungu na Mtume wake waliutaka kwa waislamu. Na Mtume S.A.W. ameusia kuwa na haya ambayo humfanya mwislamu kujiepusha na machafu na kujipamba na mazuri, na Uislamu umetuhimiza kutosheka kwa kujizuia na vile visivyokuwa halali miongoni mwa vilivyoharamishwa, na umeusia upole, kujizuia na hasira, kuvumilia na kuficha siri.

24- Na Mweneyezi Mungu Na Mtume wake S.A.W. walisifu kukinai, na kwamba mwislamu anaridhia kichache na maisha ya chini, na hakodolei macho utajiri wa matajiri akitamani awe kama wao, kwani utajiri wa kweli sio katika utajiri wa mali bali ni utajiri wa nafsi kwa kumcha Mwenyezi Mungu.

25- Na Mwenyezi Mungu anataja riziki katika Quraani mara kwa mara, riziki ni kile anachokipata mtu kwa kazi yake kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake ya msingi na maisha yake. Na hii ndio riziki ya wazi kwa ajili ya manufaa ya miili, na inakabiliana na riziki ya ndani kwa manufaa ya akili na nyoyo kama vile kumcha Mwenyezi Mungu ambako hulisha akili. Na mwislamu anapaswa kuridhia riziki anayopewa na Mwenyezi Mungu kwani yeye ni mwenye amri yote, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamemhimiza mwislamu kufanya matendo mema kati ya ibada ya Mwenyezi Mungu na kuyashikia mafunzo ya sheria yake, tabia njema, matendo mema, kuwafanyia wema maskini na wenye haja, na kila jambo linalomsaidia mwislamu kujiimarisha miongoni mwa kazi njema na thawabu yake kamili ataikuta kwa Mola wake.

26- Na mambo yaliyopigwa marufuku ni sehemu ya ustaarabu wa Kiislamu. Na asili ya vitu ni halali isipokuwa vile ambavyo sheria imesema kuwa ni haramu. Kwa hivyo basi, kwa mfano vyakula ni halali isipokuwa vile ambavyo Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W. wamevizuia kwa dalili kuwa ni miongoni mwa vyakula vibaya vilivyotajwa katika suratu AL MAIDAH, kama maiti, damu na nyama ya nguruwe. Pamoja na haya yaliyopigwa marufuku, kuna vyakula vyengine marufuku ameviharamisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kuinua maisha ya mwanadamu na kuyatahadharisha kutokana na madhambi yaangamizayo, hasa uzinifu ambao ni dhambi kubwa zaidi, riba, ulevi na kamari.

27- Na Mtume S.A.W. ameonya dhulma na adhabu yake Siku ya Akhera, akisema kuwa dua ya mtu aliyedhulumiwa haina kizuizi kati yake na Mwenyezi Mungu, na miongoni mwa madhambi makubwa ni kiburi na majivuno. Na kiburi ni kujikweza mbele ya watu na kuhisi kuwa uko juu yao, kama asemavyo Mtume S.A.W. kwamba: "Haingii peponi atakayekuwa na chembe ya kiburi moyoni mwake". Na kujiona na majivuno ni mtu kuonesha kiburi kwa namna alivyo au kwa adabu yake, elimu yake na kwa kujikweza na kwamba yeye yuko juu ya watu wote. Na miongoni mwa madhambi makubwa ni kutoa ushahidi wa uongo. Na jambo hili ni batili kwa kauli na kwa vitendo ambapo mtu hutoa ushahidi dhidi ya mtu mwingine kwa kuzusha maneno, na Quraani imeambatanisha dhulma na kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu}, kisha akasema baadaye: {Na wale ambao hawashuhudi shahada za uwongo na wanapopita penye upuuzi hupita kwa heshima (yao), [AL-FURQAN 68, 72]

28- Na miongoni mwa madhambi makubwa ni husda; Nayo ni mtu kutamani neema ya mwenzake itoweke au imwendee yeye kinyume cha mwenzake, na hii ni kinyume cha “Ghibtwa”(furaha) yaani mtu kutamani neema ambayo anaiona kwa mtu mwingine bila ya kutamani imuondokee mtu huyo, na miongoni mwa madhambi makubwa ni uongo, udanganyifu, kughushi, kuwadhania watu mabaya, kuwateta na kuwasengenya watu na madhambi mengine na maasia ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyakataza.

29- Kiufupi hiyo ndio misingi ya kiungu ya ustaarabu wa Kiislamu ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume wake wameiweka katika dini ya Uislamu, dini ya mwisho katika dini za Mwenyezi Mungu, ili kumwokoa mwanadamu kutokana na kutumbukia katika upotofu na ukiukaji wa maadili, na kumrejesha katika uongofu, mshikamano, ushirikiano na mapenzi. Na waislamu wote katika zama hizi wanapaswa kurejea katika kushikamana na maisha yao kwa misingi hii kama walivyofanya wale wema waliopita. Basi ulimwengu mashariki na magharibi ulijisalimisha kwao na waliishi maisha mazuri pamoja na wakazi wote wa nyumba zilizofunguliwa kwa muda wa karne nyingi, ambapo Uislamu ulieneza amani, usalama na maendeleo kwa watu wote.

30- Na lazima tuamini kwamba misingi hiyo ya kistaarabu ambayo Mwenyezi Mungu ameuzawadia ulimwengu katika dini ya Uislamu dini ya mwisho, lazima ienee siku fulani katika maisha ya mataifa duniani, mashariki na magharibi. Na inamwokoa binadamu kutokana na tamaa za mali, majanga ya ngono na kupotoka kimaadili, na humrejeshea roho yake kiungu, na watu wote wakaishi katika nchi zao katika hali ya kupendana, maisha ya undugu, amani, wema, uadilifu, huruma, kutosheka, kusamehe, upole, usamehevu, kuliwazana, pamoja na kujizuia na mambo yote yaliyokatazwa na tabia mbaya zenye madhara.

Marejeo: Marehemu Profesa Shauqiy Dhaif, Alhadhaaratu Al-islaamiyya minal Quraani wa Sunna, Kairo, Dar El Maarif 1997, (Uk. 3-11).


 

Share this:

Related Fatwas