Haki za Binadamu Zinazohusiana na M...

Egypt's Dar Al-Ifta

Haki za Binadamu Zinazohusiana na Mali

Question

Haki za Binadamu Zinazohusiana na Mali

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Mali katika sheria ya Kiislamu ni kila kinachomilikiwa kikawaida, na inajuzu kuchukuliwa thamani yake kikipotea. Inasemekana: ni kila chenye manufaa, pia inasemekana: jina la mali haliwi isipokuwa kwa kitu chenye thamani ya kuuzwa na kikiharibiwa ni lazima kulipwa thamani yake.

Wanachuoni waliafikiana juu ya heshima ya mali; haijuzu kuipora au kuiteka au kula mali za watu kwa batili hata zikiwa chache kwa mujibu wa maneno Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala msiliane mali zenu kwa batili} [BAQARAH, 188].

Mali ni mojawapo ya makusudio matano ya kisheria ambayo sheria ya Kiislamu inayachunga na kuunda hukumu za kifiqhi zinazoyalinda, kuyadhamini na kuyakuza kwa kupitia kundi la sheria zinazodhibiti matendeano ya mali “miamala ya fedha” kwa ajili ya kuleta masilahi ya mtu na jamii (kwa maelezo zaidi kuhusu suala la mali katika sheria ya Kiislamu rejea: [Al Mausu'a Al Fiqhiya; 36/31-42].

Kwa upande mwengine, mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu una baadhi ya matini za haki zinazofaa kuingia katika kusudio hilo la kisheria “mali”, kama vile:

• Haki za kiuchumi na za wafanyakazi.
• Haki ya kumiliki.
Haki za kiuchumi na za wafanyakazi.
Hakika maliasili kwa aina zake zote na ulimwengu wote ni ufalme wa Mwenyezi Mungu Mtukufu Anayesema: {Ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo humo vyote} [AL MAIDAH, 120]. Naye Mwenyezi Mungu Amempa binadamu haki ya kuzitumia mali ambapo Amesema: {Na amefanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, vyote vimetoka kwake} [AL-JATHIYAH, 13].

Kwa hiyo, kila mwanadamu ana haki ya kupata riziki yake kwa njia za kihalali, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Basi nendeni katika pande zake zote na kuleni katika riziki zake}[AL-MULK, 15].

Uislamu uliweka vidhibiti vya kisheria na hukumu zinazoongoza shughuli za kiuchumi, miongoni mwa vidhibiti hivyo: kuharamisha ghushi, Mtume S.A.W. alisema: "Adanganyaye hatokani nasi" [Ibn Majah], aidha Uislamu uliharamisha kuuza kwa udanganyifu na ujinga, na umeharamisha kuhodhi mahitaji ya watu ya lazima, Mtume S.A.W. alisema: "hahodhi ila mkosaji", pia Uislamu umeharamisha riba, kila jambo la kupata faida bila ya kuangalia shida ya watu, kumiliki mali bila ya kutoa Zaka zake za fedha, kuuza vilivyoharamishwa na kufanya israfu wakati wa kutumia mali.

Aidha suala la kutojuzu kuteka mali ya mtu binafsi linaambatana na haki za kiuchumi; Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wala msiliane mali zenu kwa batili} [AL BAQARAH, 188].

Kuhusu haki za wafanyakazi, Uislamu umeeneza wito wa “kufanya kazi kwa manufaa ya jamii”, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na sema (uwaambie): Tendeni mambo mazuri} [AT TAWBA, 105]. Ama haki ya mfanyakazi, basi lazima achukue ujira juu ya kazi yake na aishi maisha mazuri (yanayokubalika) bila ya kumdhalilisha, bali lazima mfanyakazi apate haki ya kulindwa pamoja na malezi ya kijamii. Mtume S.A.W. alisema: "mpeni mfanyakazi ujira wake kabla ya kukauka jasho lake".

Mkataba wa kimataifa wa kazi za binadamu ulitaja masuala ya haki za wafanyakazi kwa kusema:
• Kila mtu ana haki ya kupata kazi, ana uhuru wa kuchagua kazi, ana haki ya kufanya kazi katika hali nzuri za kimaisha tena ana haki ya kulindwa.

• Watu wote wana haki ya kupata ujira unaolingana na kazi bila ya kumbagua yoyote kati yao.
Hakika Uislamu unakubali maisha ya kujitegemea tena haukiri hali ya kuishi bila ya kuwa na kazi, kwani Manabii wote walikuwa wanafanya kazi kwa mikono yao ili wachume riziki, kwa hiyo Uislamu unajali sana kazi. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na itakapokwisha Sala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu} [AL-JUMUA, 10].

Mtume S.A.W. alisema: “Hakika kuna aina ya madhambi miongoni mwa madhambi ambayo hayafutwi isipokuwa kwa kutafuta riziki”.

Na amesema “Chakula bora anachokula mtu ni kile kinachotokana na kazi ya mkono wake, na Nabii Daud alikuwa anakula kutokana na kazi ya mkono wake”.

Jamii ya Kiislamu haitakiwi kuwa na nguvu isiyo kuwa na faida au tabaka la kijamii linalolitegemea tabaka lingine, kwani Mtume S.A.W. alisema: "Ni bora mtu achukue kamba yake na aende majabalini kukata kuni, na arejee na mzigo wa kuni mgongoni mwake, auuze na kisha amtegemee Mwenyezi Mungu, kuliko kuwaaomba watu ambao wanaweza kumpa au kumnyima"

Masahaba walitambua maana hizo zinazopandisha thamani ya kazi wakazitekeleza juu yao wenyewe.

Mfano mwema wa kuigwa katika suala hilo ni jambo walilolifanya Muhajirina wakati wa kuhama kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu kutoka Makka kwenda Madina wakaacha biashara zao, mali zao na kazi zao nyuma yao. Answaar walikuwa tayari kuwashirikisha katika mali zao bure kwa ajili ya kunusuriana na kusaidiana katika wema lakini Muhajirina walikataa, wakataka wachume riziki zao kwa mikono yao, basi baadhi yao wakafanya kazi katika biashara na wengine walilima ardhi za Answaar wakapata fungu la zao [Sahih Muslim, juzuu ya 4, uk. 387, 388].

Uislamu haukuishia kutoa fursa za kazi kwa watu tu, bali ukadhamini ujira unaowafaa, aidha ukatilia mkazo jambo la kutochelewesha kuwapa ujira wao, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na (viumbe) wote watakuwa na daraja (zao mbali mbali) kwa yale waliyoyatenda, na ili (Mungu) awalipe (malipo ya) vitendo vyao; nao hawatadhulumiwa} [AL-AHQAF, 19].

Mtume S.A.W. alisema: “mpeni mfanyakazi ujira wake kabla ya kukauka jasho lake”.
Na amesema Mtume S.A.W: "Watu watatu mimi ni mgomvi wao siku ya Malipo: Mtu aliyenipa kisha akafanya hiyana, na mtu aliyeuza bila ya kupima anachokiuza na kisha akala alichokipata, na mtu aliyemwajiri mtumishi na mtumishi huyo akatekeleza kazi yake na mwajiri akagoma kumlipa"

Basi mwajiri ana jukumu la kujali wafanyakazi wake kwa mujibu wa maneno ya Mtume S.A.W. “Kila mmoja wenu ni mchungaji na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga” [Bukhari na Muslim, Bukhari, juzuu ya 3, uk. 157]. Hili ni onyo kwa wanaochelewesha kutoa ujira wa mfanyakazi.
Uislamu unamjali kikamilifu mfanyakazi na kutomwacha peke yake ili mwajiri asije kumtesa au kumtaabisha, bali Uislamu ukadhamini kiwango cha raha kwake, kuhifadhi nguvu yake na kujali afya yake, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Mwenyezi Mungu haikalifisha nafsi yoyote ila yaliyo sawa na uweza wake} [BAQARAH, 286].

Na mtu akikosa kazi, basi Uislamu unailazimisha nchi kumsaidia kuishi mpaka apate kazi, na jambo hilo ni mojawapo ya milango ya Zaka; kwani wanaokosa kazi hao ndio mafakiri, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {(Wapewe hizo sadaka) mafakiri waliozuiwa katika njia za Mwenyezi Mungu, wasioweza kwenda huku na huko katika ardhi (kufanya kazi ya kutafuta riziki); asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao (na kuomba). Utawafahamu (kuwa wahitaji) kwa alama zao (zinazoonyesha ufakiri, lakini) hawawaombi watu wakafanya ung’ang’anizi. Na mali yoyote mnayoitoa, basi kwa yakini Mwenyezi Mungu Anayajua} [BAQARAH, 273].

Na imepokelewa kutoka kwa Imamu Ahmad kwamba Mtume S.A.W amesema: "mtu yeyote atakayepewa jukumu la kutuongoza sisi katika jambo letu na akawa hana makazi basi na apate makazi, na kama hana mke aoe na kama kipando na apate kipando hicho (kutoka katika hazina ya fedha ya waislamu)"

Haki ya kumiliki:
Uislamu ulikiri haki ya kumiliki mali binafsi pamoja na kuweka hukumu zinazoweza kuhifadhi mali hizo, na Quraani Tukufu ilikataa mara nyingi jambo la kula mali za watu, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi mlioamini! Msiliane mali zenu kwa batili} [AN NISAA, 29].

Lakini Uislamu haukujaalia haki ya kumiliki bila ya mipaka, bali Uislamu ulikubali na kukiri haki hiyo iliyowekewa sharti ili mwenye mali awe mdhamini na mwaminifu juu ya mali zinazokuwa mkononi mwake, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu Aliyekupeni} [AN-NUR, 33].

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu Amefaradhisha Zaka juu ya Waislamu watoe kutoka mali zao, kisha Amempa mtawala haki ya kuchukua mali zaidi ya kiwango cha Zaka kutoka mali za Waislamu katika hali ya dharura; kama vile masilahi ya wote kuepusha madhara na lawama pamoja na kutunza masilahi ya Waislamu. [Rejea: Sayed Qutb: Al-Adaalatul Ijtimaaiyah Fil Islaam, uk. 101, 102]

Uislamu ulikiri suala la umiliki kwa aina zake mbili; umiliki binafsi na umiliki kwa pamoja. Kwa hiyo, haijuzu kwa mwenye madaraka kuvamia mali ya mtu binafsi, hali kadhalika haijuzu kuchukua mali yake kuiweka kama ni manufaa ya wote ila ikiwa dharura kwa masilahi ya Waislamu, basi anaweza kuchukua mali kama akikubali au akikataa lakini lazima ampe fidia ya thamani yake, kwani masilahi ya Umma yako mbele ya masilahi binafsi.

Umiliki wa mali binafsi katika Uislamu ukiwa ni nyumba au mali ya kuhamishika tena halali, umetokana na njia halali za kuchuma mali, basi ni jambo linafohamika katika dini.

Uislamu unakubali umilikaji, bali unaelekeza watu kuchuma mali kwa njia halali, na Uislamu umempa mtu uhuru wa kutumia mali yake kwa namna atakayo ikiwa kwa mauzo, hiba au wasia n.k. sharti achunge haki za wengine na asiwaletee madhara.

Vile vile Uislamu umeiwekea mali mazingira ya ulinzi, kinga, utulivu na ukuaji, na umeweka mipaka juu ya wale wanauchupa mipaka.

Wanavyuoni wengi walipata dalili za kisheria juu ya uhalali wa umilikaji binafsi kutokana na maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Yeye ndiye Aliyekuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi} [BAQARAH, 29].

Aya hiyo ina dalili ya kuwa vitu vyote duniani ni manufaa kwa mwanadamu aliyeruhusiwa kuvitumia kukidhi haja zake na aweze kuendelea kuishi lakini kwa mujibu wa mipaka ya uadilifu. Aidha wanavyuoni walipata dalili nyengine kutokana na Aya hiyo nayo ni kwamba asili katika kila kitu ni uhalali mpaka ipatikane dalili ya kukiharamisha.

Pia katika Quraani na Sunna kuna dalili nyingi zinazounga mkono umiliki binafsi. Miongoni mwa Aya zinazohusisha mali kwa watu ni maneno Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Niache mimi na niliyemuumba peke yangu. Na nikamjaalia awe na mali nyingi} [AL-MUDDATHTHIR, 11,12], na Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni yaliyobaki katika riba, ikiwa mmeamini. Na kama hamtafanya (hivyo), basi fahamuni mtakuwa na vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkiwa mmetubu, basi mtapata rasimali zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe} [BAQARAH, 278, 279].

Aidha Quraani Tukufu iliwataka watu walinde mali zao na wazitetee, na imeweka adhabu dhidi ya yule anayeifanyia uadui mali ya mtu. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Hakika wale ambao wanakula mali ya mayatima kwa dhuluma, bila shaka wanakula moto matumboni mwao; na wataungua katika huo Moto (wa Jahanamu) uwakao}. [AN NISAA, 10].

Hekima ya kuidhinisha miliki za watu: Hakika mali kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu ni kitu cha lazima kwa maisha ya kibinadamu na kitu kinachosaidia kuwepo jamii na kuianzisha, kwa hiyo binadamu akijitahidi kukipata, basi ni jambo linaloambatana na maumbile na desturi yake kwani mali ni riziki, na kwa mali binadamu anatosheka na mahitaji yake, kwa hiyo suala la kutafuta na kupata mali ni jambo la wajibu ili kuepukana na maangamizo.

Pia jukumu binafsi linamfanya mtu awe tayari kumiliki na kufanya mkataba, na kutokana na hayo sheria iliweka umiliki binafsi kuwa ni ukweli uliothibiti na mfumo wa kimsingi katika uchumi wa Kiislamu. Na kwa kutekeleza hayo, kunapatikana jambo linalohusiana na maumbile ya kibinadamu na njia inayosaidia kukuza na kuendeleza hali ya mtu pamoja na kuboresha uwezo wake kwa masilahi yake na jamii, ili hayo yote yawe sababu ya kukua jamii na kuepukana na maangamizo. Suala la kujiepusha na maangamizo ni wajibu wa kibinafsi katika maisha ya mtu, suala hilo linaloambatana na umiliki binafsi, kwa hiyo jambo la kuhifadhi umiliki binafsi ni wajibu.

Mali zinazoingia ndani ya umiliki binafsi:
Wanachuoni wa sheria ya Kiislamu wanaigawa mali katika sehemu tatu kwa mujibu wa kukubali kwake kumilikiwa, nazo ni:

• Kisichokubali kumilikiwa wala kumilikiwa na watu au makundi ya watu, nacho ni kitu kinachowekwa kwa manufaa ya umma; maana haijuzu kumiliki au kumilikisha ilhali kiliwekwa kwa manufaa ya wote, kwani ni mali za umma kama vile; misikiti, ngome, mito, barabara za umma.
• Kisichokubali kumilikiwa ila ikikuwepo sababu ya kisheria kama vile; wakfu wa Mwenyezi Mungu na nyumba zilizomilikiwa na Beytu maali (hazina ya Waislamu), basi haijuzu kummilikisha mtu ila kwa kuwepo sababu ya kisheria.
• Kinachokubali kumilikiwa bila sharti isipokuwa zile sharti zilizowekwa na elimu ya misingi ya fiqhi, na hiyo ni sehemu ya msingi kwani mali katika asili yake inakubali kumilikiwa na kumilikishwa ila ikikuwepo sababu ya kisheria inayozuia kuimiliki au kuimilikisha.

Tukiangalia haki ya umilikaji, tutakuta kwamba iliwekwa kwa kuhakikisha masilahi ya pande mbili; mwenye kumiliki na jamii yenyewe, na ikitokea madhara kwa upande mmoja italazimika kufanya uwiano baina ya faida itakayotarajiwa na madhara yatakayoifuata. Na ikiwa masilahi ya mwenye haki yakiwa na uzito, basi haki yake inathibitika, na ikiwa madhara yake kwa wengine yana uzito zaidi, basi haki yake itanyimwa kwa ajili ya kuepusha madhara. Kwa hiyo, sheria ya Kiislamu iliwapa watu haki ya kuangalia vitendo vya mtu katika mali yake binafsi, bali iliwalazimisha kutekeleza wajibu kwa kutunza masilahi na haki yake kutokana na kosa la ubinafsi.

Uislamu uliweka vizingiti vya kidini kuhusu umilikaji ili kuepusha migogoro ya kimasilahi, na ili kuleta faida ya pamoja kwa namna zifuatazo:

• Uislamu umezingatia kuhuisha ardhi iliyokufa, kwani ni sababu mojawapo ya kumiliki ardhi ili kuiimarisha nchi na kupanua mipaka ya ardhi zinazolimwa, na kuhamasisha watu wafanye kazi, ila Uislamu uliweka sharti ya muda wa miaka mitatu kuhuisha, kwa hiyo inawajibika juu ya mwenye kupata haki ya kuitumia ajitahidi alime ndani ya muda huo kwani muda huo ukimalizika bila ya kuihuisha ardhi, basi anapewa mtu mwengine.
• Uislamu ulimkataza mwenye haki ya kutumia mali yake asizitumie haki zake vibaya, asilete madhara kwa wengine.
• Aidha Uislamu unamtaka mwenye kumiliki wakati wa kuuza mali yake amtangulize mshirika wake na jirani yake. na hii ni haki ya jirani ya kumiliki mali kwa kumpa nafasi ya kuinunua mali hiyo kwa masharti maalumu.
• Uislamu umemuwekea mipaka ya haki mmiliki wa mali mwenye uwezo wa kufanya chochote katika mali yake hiyo, na akawa hana haki hiyo baada ya kufa kwake isipokuwa katika theluthi moja tu ya mali yake.
• Uislamu umekataza kuuza ardhi ya wakfu, kwani ni kwa ajili ya manufaa ya umma, na ukawapa watu haki ya kuitumia ardhi hiyo bila ya kupata haki ya kuimiliki.

Kuondoa sifa ya umilikaji bila ya ridhaa ya mwenye kumiliki:
Asili katika uhamishaji wa umilikaji ni kuwepo ridhaa; haijuzu kwa mtu kuchukua kitu kutoka mwengine bila ya ridhaa yake hata kama ana haja nacho isipokuwa chakula. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi mlioamini! Msiliane mali zenu kwa batili. Isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. (Hiyo inajuzu) wala msijiue (wala msiue wenzenu) Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukuhurumieni} [AN NISAA, 29]. Naye Mtume S.A.W. alisema: "Haijuzu kwa mtu kuchukua mali ya mtu mwengine ila kwa ridhaa yake".

Lakini Uislamu umeruhusu kisheria kuondoa umilikaji wa mwenye kumiliki bila ya ridhaa yake kwa manufaa ya umma na kuwaepushia madhara watu wengine, iwapo tu kuwepo kwa faida itakayoyerejea kwa mmiliki ambayo itaendelea kuwepo kwa kuwepo Mali hiyo mikononi mwake kuna madhara machache wanayoyapata wengine kwa kuendelea hali hii. Kwani Mtunga sheria aliruhusu kuondoa sifa ya umilikaji binafsi katika hali maalumu kwa masilahi ambayo hayatatokea ila kwa kuondoa ile sifa. Kwa hiyo Wataalamu wa Usuul walisema kwamba tabia ya haki ya mtu binafsi katika Fiqhi ya Kiislamu ni haki ya pamoja siyo ya ubinafsi; kwani manufaa ya umma yanawekwa mbele ya haki ya mtu binafsi, na hiyo ni maana ambayo Al Shat-biy aliibainisha kuwa ni “haki ya Mwenyezi Mungu” ambapo alisema: mila – nazo ni haki na miamala – ni haki ya Mwenyezi Mungu kwa upande wa kuchuma riziki na kupata manufaa; kwani haki ya wengine inalindwa kisheria na mtu hana chaguo la kuichukua au kuiacha, kwani ni haki ya Mwenyezi Mungu. Na asili katika suala hili ni kuweka manufaa ya umma mbele ya manufaa ya mtu binafsi, na mwenye kumiliki hatapata madhara makubwa kwani anapewa fidia iliyo sawa na thamani ya umilikaji wake, na thamani hukadiriwa kwa ujuzi wa wasomi wenye uzoefu na waadilifu.

Baadhi ya wanachuoni walisema kuwa kupanua misikiti ni suala linaloambatana na manufaa ya wote ili usiwape watu shida, na kama msikiti ukiwabana watu(Msikiti ni mdogo haukidhi mahitaji ya watu) na pembeni ya msikiti kuna ardhi ya mtu, basi inachukuliwa kwa lazima kwa kulipwa thamani, na kuchukua huku kwa lazima kunajuzu. Na mfano mzuri wa hali hii ni utanuzi wa msikiti wa Makka.

Lakini haijuzu kuchukua mali ya mtu bila ya kumpa fidia ya thamani yake hata ikiwa kwa ajili ya manufaa na masilahi ya umma, bali inawajibika kumpa fidia kutoka hazina ya Waislamu, na ikiwa hazina hiyo haina mali, basi mtawala anaweza kuwalazimisha wenye uwezo na nyadhifa za juu walipe mali inayotakikana kwa haja ya nchi, na hiyo inakuwa kwa mizani iliyo sawa; wote wanashirikiana na kila mmoja kwa uwezo wake.
Rejea: Kitengo ya Tafiti za Kisheria katika Idara ya Fatwa ya Misri.
 

Share this:

Related Fatwas