Kumeza Makohozi Mchana wa Mwezi wa...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kumeza Makohozi Mchana wa Mwezi wa Ramadhani kwa Aliyefunga.

Question

 Nini hukumu ya aliyefunga kumeza makohozi mchana wa mwezi wa Ramadhani ambapo mtu huona uzito mkubwa kuyatoa na kuyatema?

Answer

 Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

Neno Swaumu na Swiyaamu ni visuokomo viwili kwa kitenzi kimoja (Swaama yaani alifunga), inasemwa: alifunga, anafunga, kufunga na kadhalika, na maana ya kufunga (Saumu) katika lugha ni kujizuia, na mtu anaitwa mfungaji kwa sababu ya kujizuia vinywaji, vyakula na tendo la ndoa. Na mnyamazaji huitwa mfungaji kwa sababu ya kujizuia na mazungumzo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika kisa cha Maryam amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake: {Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Napindi ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu.} [MARYAM 26]

Na Saumu kisheria ni: kujizuia na vyakula kwa mfumo maalumu, yaani ni kwa kufuata masharti, nguzo na kutokuwepo vizuizi.

Na miongoni mwa nguzo za Saumu ni kujizuia na vyakula, nayo ni: kufika kooni kwa chakula hicho kutoka katika njia ya wazi, kwa kukusudia, kutaka, na kujua uharamu wake.

Maana ya chakula si athari yake kama vile harufu, bali ni chakula chenyewe, kwa hivyo hafungui mtu kwa kunusa harufu ya chakula, au kwa kuwasili ladha ya chakula katika koo yake, na hivyo pia hata kama alizamia majini na akapata ubaridi wa maji hayo katika tumbo lake.

Si sharti kuwa kitakachoingia kooni kiwe kingi au kiwe ni katika vyakula, bali hata kichache –kama punje ya ufuta– au kikawa kitu kisicholiwa –kama kwa mfano mchanga– basi kitaharibu Saumu.

Kinachokusudiwa kwa neno “tumboni” ni ndani ya tumbo. Na maana yake ni njia iliyo wazi: mapito ya kimaumbile ya asili katika mwili wa binadamu na ambayo huzingatiwa ni njia ya kupitisha kitu kutoka nje ya mwili na kuingia ndani ya mwili huo. [Hashiyat Al Bijirmiy ala Al Iqnaiy, 378/2, Ch. Dar Al Fikr]
Inatajwa katika kitabu cha [Al Minhaaj, cha Imamu An Nawawiy na ufafanuzi wake (Nihayat Al Muhtaaj) kwa mwanachuoni Al Shams Al Ramliy, 165, 166/3 Ch. Dar Al Fikr] katika kuongelea yanayoharibu funga: "(Na) Kujizuia na (kufika kitu chenyewe) na ukisema kama vile punje ya ufuta na kisicholiwa kama vile kijiwe (na kuwasili tumboni) kwa makusudi, kwa kujua uharamu wake na kutaka. Na athari za kitu hazimo katika maana ya kitu chenyewe, kama vile upepo kwa kuunusa au kuuvuta, na ubaridi wa maji na ufukuto wake kwa kuyagusa. Na maana ya tumboni, ni kuwa kama mtu alitumia dawa kwa ajili ya matibabu kwenye jeraha lake juu ya nyama za mguu wake au paja, na dawa hiyo ikawasili hadi ndani ya ubongo wake au nyama zake, au aliingiza sindano katika ngozi, hivyo haviiharibu Saumu kwa kutofika kwake tumboni.

Mwanachuoni Al Khatteeb Al Sherbeniy anasema katika kitabu cha: [Al Iqnaai, 378/2, Ch. Dar Al Fikr - pamoja na Hashiyat Al Bijirimiy-] alipoongea katika yanayoharibu Saumu pia: "(kitu kilichofika) hata kama kitakuwa kidogo kama punje ya ufuta (kwa makusudi) kwa kutaka kwake na kwa kujua uharamu wake (hadi katika sehemu yeyote ya tumboni) kupitia njia za wazi, iwe ilikuwa ikuzuia dawa au chakula au hapana, kama vile ndani ya koo au tumbo au utumbo (na) ndani ya kichwa."

Na miongoni mwa yanayoungana na kufika kitu tumboni; ni swala la kumeza makohozi: na makohozi ni mabaki mazito yatokayo kwenye ubongo au tumboni nayo ni mazito. [Rejea: Al Musbaah Al Muneer, cha Al Fayumi; kidahizo cha (N, Kh, Ain) Ch. Al Maktabah Al Elmiyah, na Hashiyat Al Qaliyobi alaa Sharh Al Mahaliy Lil Al Minhaaji 70/2, Ch. Dar Ihiyaa Al Kutub Al Arabiyah].

Na kumeza makohozi hakubatilishi Saumu, isipokuwa yakifika kwenye uwazi wa kinywa (midomoni)- yaani: sehemu ya kutokea herufi za Haa na Khaa- na mwenye saumu akayaachia hali ya kuwa ana uwezo wa kuyatema hadi yakafika tumboni. Na maana hayo ni: Na iwapo makohozi hayo yatapanda kutoka kifuani kwa mfano na yakawa hayajafika midomoni katika eneo la wazi kama mdomo na kisha akayameza basi hayatabatilisha Saumu yake, na pia iwapo yatafika kiwango cha wazi na kisha akayatema au yalifika kiwango cha uwazi na wala hakuweza kuyatema, kama walivyokubaliana na maana hiyo wanachuoni wa madhehebu ya Shafiy na Hanbaliy.

Imamu Al Ramliy Al Shafiy akasema katika kitabu cha: [Nihayat Al Muhtaaj 164,165/3]; "Na iwapo matapishi yatamshinda… basi si vibaya… na vivyo hivyo kama mtu aliyavuta makohozi na kisha akayatema basi si vibaya kufanya hivyo (kwa usahihi wake) iwe ameyavuta makohozi hayo kutoka ubongoni mwake au tumboni mwake, kwa kukariri kufanya hivyo kwa mujibu wa haja ya kufanya hivyo, basi inaruhusiwa kufanya hivyo.

Na ya pili: yanayoibatilisha Saumu; kama vile kujigogoa (kujitapisha). Na ametumia tamko lake: (iwapo atayavuta) kama aliweza kuyatema pamoja na kuteremka kwake yenyewe au kutokana na mafua makali, basi si vibaya kama ilivyoamuliwa, na iwapo kama yangelibakia pale yalipo basi hayaibatilishi Saumu kama ilivyoamuliwa na wanachuoni. Na iwapo mtu atayameza baada ya kutoka na kuwa wazi basi atakuwa amefungua kama ilivyoamuliwa na wanachuoni. (na kama yangeteremka kutoka ubongoni na yakafikia kiwango cha kuonekana mdomoni) ni kwamba yalimiminika kutoka katika ubongo kupitia tundu hadi kufikia mdomoni juu ya koo (basi aizuie njia yake na ayateme) iwapo ataweza kufanya hivyo ili chochote kati ya makohozi hayo kisifike tumboni... (na iwapo atayaacha huku akiwa na uwezo wa kuyazuia) na hadi (basi yakafika tumboni basi atakuwa amefungua bila shaka) kwa sababu ya uzembe wake.

Na ya pili: haibatilishi Saumu; Na kama hayajafika katika kiwango cha uwazi mdomoni –napo ni sehemu ya njia ya herufi “khaa” au yanatokea katika kiwango cha wazi na hakuweza kuyang'oa na kuyatema haidhuru."

Na mwanachuoni Ibn Hajar Al Haitimiy Al Shafiy akasema katika kitabu cha: [Tuhfat Al Muhtaaj 400/3, Ch. Dar Ihyaa Al Turaath Al Arabiy]: "(Na kama makohozi hayo yaliteremka kutoka ubongoni mwake hadi kufikia kuonekana mdomoni...basi na ayakatishie njiani na kuyatema) kiasi kitakachowezekana hadi kisifike chochote kati yake tumboni, (na ikiwa atayaacha hali ya kuwa ana uwezo) wa kuyatema na (yakafika tumboni) inamaanisha kuwa yalipitia kiwango kilichotajwa (basi bila shaka atakuwa amefungua); kwa uzembe wake, tofauti na kwamba iwapo yatakuwa hayajafikia kiwango cha kuonekana mdomoni, ikiwa ataweza kuyatema na iwapo yatafikia kiwango hicho na akashindwa kuyatema".

Na mwanachuoni Al Bahutiy Al Hanbaliy akasema katika kitabu cha; [Kashaaf Al Qinaa 329/2, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]: "Ni haramu kwa mwenye kufunga (kumeza makohozi) iwapo atayakusanya mdomoni mwake kwa ajili ya kufungulia kinywa, na mtu aliyefunga (atakuwa amefungua) kwa makohozi hayo iwapo atayameza (iwe yalitokea tumboni mwake, kifuani au katika ubongo wake baada ya kufika mdomoni mwake), kwa sababu makohozi hayo hayatokei mdomoni, ni kama matapishi."

Baadhi ya wanachuoni wameruhusu suala hili la makohozi; kwa hivyo basi wanachuoni wa Madhehebu ya Hanafiy wameyataja katika mambo ambayo hayaharibu funga; imesemwa katika kitabu cha; [Tanweer Al Abssaar washarhhuhu Al Dur Al Mukhtaar 400/2. Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah- pamoja na Sharh Ibn Abdeen-]: "(Au makohozi hayo yaliingia ndani ya pua yake kisha akayavuta na kuingia kwenye koo yake na hata kama yatateremka kutoka kichwani hadi kwenye pua yake…. (hata kama ni kwa makusudi) tofauti na Shafiy kwa yule anayeweza kuyatema, anapaswa kuchukua tahadhari hiyo".

Na hiyo ni katika yale yanayokubaliwa katika madhehebu ya Maalikiy; mwanachuoni Al Kharashiy anasema katika kitabu cha; [Sharh Al Muktassar 250/2, Ch. Dar Al Fikr]: "Na kilichoamuliwa ni kuwa hakuna kulipa Saumu kwa sababu ya kumeza makohozi, na hata kama ungelikuwepo uwezekano wa kuyatema, hata kama baada ya kufika makohozi hayo kwenye ncha ya ulimi wake.

Mwanachuoni Al Adawi amesema katika kitabu chake (Hashiyatahu) "Na kilichochaguliwa ni kuwa hakuna kulipa Saumu kwa sababu ya kumeza makohozi. Ibn Rushd, Assbagh amesimulia kutoka kwa Ibn Al Qaasim katika makohozi kwamba hakuna kulipa Saumu kwa kumeza makohozi kwa makusudi"

Na vile vile riwaya ya Imamu Ahmad; mwanachuoni mkubwa Ibn Qudamah wa Madhehebu ya Hanbaliy amesema katika kitabu cha; [Al Mughniy 17/3, Ch. Dar Ihyaa Al Turaath Al Arabiy]: "Na iwapo mtu atameza makohozi basi kuna riwaya mbili, ya kwanza: atakuwa amefungua. Amesema Hanbali: nimemsikia Abu Abdillahi akisema: mtu akitoa makohozi kisha akayameza basi atakuwa amefungua, kwa sababu makohozi yanatokea kichwani na mate yanatokea mdomoni, na iwapo atatoa makohozi kutoka tumboni mwake kisha akayameza atakuwa amefungua. Na haya ni madhehebu ya Imamu Shafiy: kwani mtu huyo alikuwa na uwezo wa kujiepusha nayo (kwa kuyatema), na ni kama damu, nayo hayatoki mdomoni, nayo ni kama matapishi.

Na riwaya ya pili: Hafungui kwa kumeza makohozi; amesema Imamu Ahmad katika simulizi ya Al Marrwaziy:- Hulazimiki kulipa iwapo utameza makohozi hali ya kuwa umefunga, kwani ni kawaida kuwa kwake mdomoni na wala hayatokei nje, nayo ni kama mate.

Na kutokana na hayo: Mtu anapaswa kujiepusha na kumeza makohozi kwa kiasi awezacho iwapo amefunga. Na ikiwa atakuta kuna ugumu na uzito wa kujiepusha nayo au akapatwa na wasi wasi, basi wakati huo anaweza kufuata madhehebu ya wanachuoni walioruhusu kufanya hivyo na hawakuzingatia kuwa kumeza makohozi ni miongoni mwa yanayobatilisha Saumu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas