Tofauti Baina ya Uwepesishaji na U...

Egypt's Dar Al-Ifta

Tofauti Baina ya Uwepesishaji na Urahisishaji katika Fatwa.

Question

Je, kuna tofauti yoyote kati ya uwepesishaji na urahisishaji katika fatwa?

Answer

 Namshukuru Mwenyezi Mungu, na sala na amani ziwe juu ya bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, familia yake, masahaba wake, wafuasi wake. Ama baada ya hayo.

Imepokelewa kutoka kwa wanavyuoni kukemea urahisishaji katika fatwa, na mara nyingi jambo hili huwachanganya baadhi ya watu mpaka wakalichukulia kemeo la wanavyuoni katika urahisishaji na uharamishaji wake kama ni kisingizio cha kukemea uwepesishaji wa fatwa. Na katika jambo hili kuna uchanganyaji kati ya mambo mawili tofauti katika sifa zake maalum pamoja na hukumu zake. Kwahivyo basi, kuna tofauti kubwa kati ya urahisishaji na uwepesishaji. Na kama ambavyo ukemeaji wa urahisishaji ulivyopokelewa kutoka kwa wanachuoni, pamepokelewa pia kutoka kwao kuwa wanapendelea zaidi kuwawepesishia watu na kuafuata njia ya kisheria kwao, kwa namna ambayo inawawia ugumu kuitekeleza, kwahiyo wanachuoni wanatofautisha kati ya mambo haya mawili ingawa kilugha yanakaribiana. [1 / 499-500, Muasasatul Risalh- Beirut]: Neno “urahisi” ni kinyume cha ugumu au uzito”.

Na uwepesishaji katika sheria ni: kutunga hukumu katika sura ambayo inachunga haja ya anayetungiwa na uwezo wake katika kutekeleza amri na kujiepusha na makatazo bila ya kupuuzia misingi mikuu ya utungaji sheria. Rejea: [Madhaahir Taysiyr fir Sheria Islamiyya, Kamal Abu El-Maati uk.7, tasnifu ya kupata shahada ya uzamivu, Chuo Kikuu cha Al-Azhar, Cairo, 1975.].

Kutoa Fatwa ni kumbainishia mwulizaji hukumu ya kisheria kwa kutumia dalili katika matukio au hukumu za kisheria zinazomtatanisha. Rejea [Sharhu Muntaha Al-Iradat 3/482, Aalam Al-Kutabu].

Fatwa ni kumbainishia mwulizaji hukumu ya kisheria katika tukio fulani, na kubainisha huku lazima kuwe kwa kutumia dalili za kisheria.

Kazi ya Mufti ni kumwelezea muulizaji hukumu ya kisheria, na swali huwenda likawa ni katika maswali ya zamani ambapo wanachuoni wamejitahidi katika kutoa fatwa katika swali hilo, au huwenda likawa ni swali jipya hakuna aliyewahi kulitolea ufafanuzi, kwahiyo linahitaji jitihada. Na katika hali zote mbili, Mufti anapaswa kujitahidi sana ili kufikia hukumu ya kisheria inayofaa kwa swali hilo, iwe kwa kupendekeza moja ya kauli za wanaojitahidi au kwa jitihada yake mwenyewe na mtazamo wake katika dalili na matini za wahyi au kwa kutoa fatwa kwa kutumia kanuni za wanachuoni na misingi ya madhehebu ya wanaojitahidi. Na vyoyote itakavyokuwa basi anatakikana kuchunga lengo la sheria tukufu ambalo ni kuangalia masilahi na hali za waja duniani na akhera, kwa kutowapa uzito katika utekelezaji, kwa sababu wajibu katika Uislamu unaambatana na uwepesishaji na unafuu.

Katika Quraani tukufu na Sunna ya Mtume saw kuna matini za waziwazi zinaonesha kuwa ndani ya Uislamu kuna hali ya uwepesishaji, matini ambazo zinapinga ugumu, uzito na madhara kwa waja wenye jukumu la kisheria. Pamoja na hayo, waja hao wameamrishwa kufanya upole na uwepesishaji kwa nafsi zao na kwa wengine, na wa kufanya hivyo zaidi ni wanachuoni, kwani wao ndio wajumbe wa kufikisha risala ya Allah, na watu huwakimbilia wao kutaka kujua maarifa ya hukumu za Allah na wanayotakikana kuyafanya.

Mwenyezi Mungu anasema: {Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito} [ALBAQARAH: 185], Al-Khazen alisema katika tafsiri yake [1/156, Dar Al-fikr- Beirut]: “Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini, imesemwa: mtu akitakiwa achague kati ya mambo mawili, basi akichagua jepesi lao, Mwenyezi Mungu hulipenda zaidi kuliko lingine”.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.} [AL MAIDAH: 6].

Imamu Al-Razi alisema katika tafsiri yake Mafatihul Ghaibu [11/139, Darul Kutub Al-Alamiah- Beirut]: “Jua kuwa aya hii ni msingi mkubwa na muhimu katika Uislamu, na madhara yanakatazwa kabisa, na aya hii inathibitisha hivyo: {Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini.} [AL HAJJA: 78], na dalili nyingine ni aya hii: {Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito} [AL BAQARAH: 185], na dalili kutoka hadithi za Mtume SAW ni: "Hakuna madhara wala kudhuriana katika Uislamu", na kuondoa madhara ni jambo linalopendeza katika akili, kwa hivyo kuondoa madhara ni wajibu, kwa mujibu wa kauli ya Mtume S.A.W.: "Wanayoyaona Waislamu ni mazuri, basi pia ni mazuri kwa Mwenyezi Mungu".

Imepokelewa na Bukhari na Muslim katika hadithi zao kutoka kwa Anas RA kwamba Mtume SAW alisema: "Fanyeni wepesi wala msiwatie (watu) uzito, na toeni habari za furaha, wala msiwakimbize watu".

Al-Minyaawi alisema katika kitabu cha [Faidhu Al-Kadiir 6 / 462-461, Al-Maktabatul Tujariyah Al-Kubrah]: “(Fanyeni wepesi) maana yake: Fanyeni wepesi kwa ajili ya watu kwa kutaja mambo yanayowawezesha kukubali mawaidha siku zote; ili yasiwe mazito kwao na wakakimbia utekelezaji wa mambo ya dini. Na uwepesishaji katika elimu hupelekea kukubali utiifu, kutaka kuabudu na kurahisisha elimu na kazi, (msiwatie (watu) uzito) yaani msiwe wakali, licha ya kuwa kuamuru jambo lolote maana yake ni kukataza kinyume chake, lakini Mtume S.A.W. ametaja (msiwatie (watu) uzito) kwa ajili ya kuthibitisha maana iliyotajwa. Al-Kirmani alisema hivyo, na wanavyuoni wengine walisema: Mtume SAW amesema hivyo ili aonyeshe lengo lake ni kupinga kuwatia watu uzito, na angekuwa kasema (Fanyeni wepesi) tu, basi kauli hiyo ingefaa. Na maimamu wameafikiana na mtazamo huu miongoni mwao Al-Nawawi na wengineo”.

Bukhari katika sahihi yake kutoka kwa Abu Hurayra R.A. alisema: Bedui mmoja alikojoa msikitini, watu wakataka kumpiga, Mtume S.A.W. akasema: "Hebu mwacheni na mwageni ndoo ya maji katika sehemu ya mkojo. Nyinyi mmetumwa kwa ajili ya kufanya wepesi na hamkutumwa kuwafanyia watu uzito".
Al-Menyaawi alisema katika kitabu cha [Faidhul Qadir 2/573]: “... amesisitiza uwepesishaji kwa kutaja kinyume chake nacho ni kufanya uzito akasema: "hamkutumwa kuwafanyia watu uzito" neno “kutumwa” limetajwa hapa kwa njia ya kuazima, kwa sababu Mtume ndiye aliyetumwa, lakini waislamu wamemwakilisha katika kufikisha wito wa Kiislamu kwa watu wengine, kwa hivyo wametumwa kupitia Mtume S.A.W., yaani wameamuriwa na Mtume S.A.W., na jukumu lao ni “Fanyeni wepesi wala msiwatie (watu) uzito”, Mtume S.A.W. amesema hivyo pale Abu Al-Khuaisera Al-Yamani au Al-Aqraa ibn Habis alipokojoa msikitini”.

Kutoka kwa Jabir R.A. amesema: Mtume S.A.W. amesema:. “Nimetumwa kwa dini iliyo sawasawa, na anayekiuka Sunna yangu basi si katika mimi (ameacha kunifuata)”, ameitoa Al-Khatib, alisema Al-Minyaawi katika [Faidhul Qadir 3/203]: Hadithi hii ina njia tatu, na inawezekana isifike daraja ya hadithi nzuri.

Al-Minyaawi anasema akielezea hadithi hii 3/203: “.. (na anayekiuka Sunna yangu) maana yake njia yangu, yaani amewafanyia watu uzito na amewatatanisha katika mambo ya kidini, basi mtu huyo hakunifuata katika mambo niliyotumwa kama vile upole, ulaini, kutenda haki na kusamahe watu. Al-Harali alisema: Hakika Mtume ametumwa kwa dini iliyo sawasawa, na uwepesishaji ambao hauna aibu yoyote {kwa sababu aangamie wa kuangamia kwa dalili zilizo dhahiri} [ AL ANFAAL 42]. Na wanavyuoni wa madhehebu ya Shaafiy wamefahamu kupitia hadithi hii kanuni inayosema “ugumu huleta urahisi”.

Kutoka kwa Bukhari na Muslim, kutoka kwa Abu Huraira R.A., Mtume S.A.W. alisema: “Laiti nisingeliwaonea taabu watu wa umma wangu ningeliwaamrisha kupiga msuwaki wakati wa kila Sala”. Al-Hafidh Ibn Abdul Barr alisema katika [Al-Tamhiid 7/199, Wizara ya Wakfu na Mambo ya Kiislamu-Morocco]: “Hadithi hii inathibitisha fadhila za msuwaki na uzuri wake, pia ina dalili ya uwepesishaji katika mambo ya dini, na lenye uzito linachukiza. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema {Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito} Je, huoni kwamba Mtume S.A.W., hakupewa uchaguzi kati ya mambo mawili ila alichagua ambalo ni jepesi kati yao likiwa halina dhambi?, lakini kama likiwa ni dhambi Mtume anakuwa mbali nalo kuliko watu wote”.

Imamu Muslim amepokea katika Sahihi yake "kutoka kwa mama wa waumini Aisha, R.A. alisema: nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. anasema, katika nyumba yangu hii: Ewe Allah, mwenye kusimamia jambo la umma wangu akawafanyia uzito basi na yeye mfanyie uzito, na mwenye kusimamia jambo la umma wangu akawafanyia wepesi, basi na yeye mfanyie wepesi.". Hadithi hii inamhimiza mwenye kutoa fatwa asiwatie watu uzito, bali awe na upole na uwepesishaji kama ikiwepo ruhusa na hakuna dhambi katika uwepesishaji huo. Kutoka kwa Bukhari na Muslim katika Sahihi zao "kutoka kwa mama wa waumini Aisha R.A. alisema: Mtume S.A.W. akitakiwa achague kati ya mambo mawili, basi alikuwa akichagua jambo jepesi zaidi kuliko yote kama halikuwa na dhambi, lakini kama likiwa na dhambi, basi Mtume SAW anajiepusha zaidi kuliko watu wote)). Katika riwaya nyingine kutoka kwa Aisha, R.A. alisema: "akitakiwa achague kati ya mambo mawili, alikuwa hachagui ila jambo linalopendwa kwake nalo ni jepesi zaidi kuliko yote, kama halikuwa na dhambi, lakini kama likiwa na dhambi, basi Mtume S.A.W. anajiepusha zaidi kuliko watu wote). Imepokelewa na Ahmad katika Musnad wake.

Al-Hafidh Ibn Abdul Barr alisema katika [Al-Tamhiid 8 / 146-147]: “Hadithi hii ina dalili ya kwamba mtu anapaswa kuacha mambo mazito ya dunia na Akhera, na kuacha kuyasisitiza kama hakuna dharura, na daima anatakikaka kuelekea katika urahisi, kwa sababu urahisi katika mambo yote hupendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu anasema: {Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito} [AL BAQARAH: 185], pia inamaanisha kuchukua ruhusa ya Mwenyezi Mungu, Mtume wake na ruhusa ya wanavyuoni kama ikiwa hakuna kosa la wazi. Tulipokea kutoka kwa Muhammed bin Yahya bin Salam kutoka kwa baba yake alisema: mwanachuoni anapaswa awaelekeze watu ruhusa na wepesi kama hakuna madhambi ndani yake. Kutoka kwa Muammar alisema: Elimu ni kusikia ruhusa kutoka kwa mwanachuoni mwaminifu, ama uzito kila mtu anaupamba”.
Na anayezitazama hukumu za kisheria anaona kwa uwazi kwamba hukumu hizi zimejengeka kwa uwepesi na kuwaondolea shida wenye jukumu la kisheria, na jambo hili ni moja ya faida ya sheria za Kiislamu, ukilinganisha na mambo ya kabla ya sheria ya Mwenyezi Mungu, kama ilivyoelezwa katika aya inayoelezea sifa za Mtume wa Uislamu, Nabii Muhammed S.A.W.: {Ambao kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiye soma wala kuandika, wanayemkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anayewaamrisha mema na anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.} [AL AARAF: 157], kwa hivyo wanavyuoni wameamua kanuni: “uzito huleta wepesi”, na wameichukulia kanuni hii ni moja ya kanuni tano kuu za sheria ambazo fiqhi ya Kiislamu imeanzishwa juu yake. [Rejea: Al-Ashbah wa Al-Nadhair Li Al-Suyuti, uk 7- 8, Darul Kutub Al-Elmiya]. Pia wameidhinisha kanuni nyingine, mhimili wake mkuu ni uwepesishaji, kama kanuni isemayo "Asili ya vitu ni Halali hadi pale dalili itakapojuulisha juu ya uharamu wake", na kanuni isemayo “Hakikatazwi kitu chenye hitilafu ya maoni kati ya wanachuoni lakini hukatazwa kile ambacho wanachuoni wote wamekubaliana hivyo.” Na kanuni isemayo “ Kanuni kuepekana na hitilafu ni jambo linalopendeza”. n.k

Al-Shatby anasema katika [Al-Muwafakat 4 / 350-351, Dar Ibn Affan]: “Nafasi, uwepesishaji, kuondoa uzito, na upole yanaonekana katika uhalali wa ruhusa za tohara; kama vile, tayammum, kuondoa hukumu ya najisi ikiwa kuiondoa kwake kuna ugumu, kufupisha katika sala, kutolipa Sala kwa aliyezimia, kukusanya sala, kusali katika hali ya kukaa kitako na kulala, mgonjwa na msafiri wanaruhusiwa kufungua Saumu, na pia vitendo vingine vya ibada. Quraani ikielezea baadhi ya maelezo kama vile Tayammum, kupunguza Sala na Kufungua saumu basi ndio ishaelezea, laa si hivyo basi matini za kuondosha madhara zinatosha, na mwenye kujitahidi atumie kanuni hiyo na kuruhusu kwa mujibu wake, na Sunna ndio bora zaidi kutumika katika hali hiyo. (Katika Nafsi) pia uwepesishaji unaonekana katika nafasi nyingi, ikiwa ni pamoja na ruhusa; kama vile kula nyamafu kwa mwenye dharura, uhalali wa kuliwaza kwa Zaka, nk, na kuhalalisha uvuvi ingawa hakuna kumwaga damu kama katika kuchinja. (Katika uzazi) inaruhusiwa kufunga ndoa, ambapo hakuna kiwango maalum cha mahari kwa kila ndoa, kujuzu kwa talaka wakati wa mizozo, inaruhusiwa kutoa talaka mara tatu tu, Khul’u n.k. (Katika mali) pia inaruhusiwa mkopo na upanuzi katika kuhifadhi pesa kama akiba ambazo ni ziada juu ya haja, na kufurahia mambo mema ambayo ni halali pasipo na kutumia kwa fujo au kwa ubakhili. (Katika akili) inaruhusiwa kufanya jambo ambalo limechukizwa kama dharura ikiwepo kama vile kuchelea kuidhuru nafsi katika hali ya njaa na kiu, maradhi n.k, yote hayo yanafuata kanuni ya kuodoa madhara, kwa sababu mengi yao yanatokana na jitihada ya wanavyuoni, na hadithi za Mtume zimeonyesha mambo yanayotakiwa kuigwa”.

(Urahisishaji katika fatwa) maana yake ni mufti awe na haraka katika fatwa pasipo na kuangalia, au bila ya kuthibitisha kupitia vitabu, au kutoa fatwa kwa ajili ya matamanio yake, au kufuata mbinu ambazo ni haramu. Na kufanya hivyo ni haramu bila ya pingamizi.

Imamu Al-Nawawi katika kitabu cha [Al-Majmuu 1 / 79-80, Al-Muniriyah] akitofautisha kati ya urahisishaji na uwepesishaji kwa watu ili kuwaondolea mambo mazito, anasema: “Hairuhusiwi urahisishaji katika fatwa, na anayejulikana kufanya hivyo asiulizwe fatwa, na aina za urahisishaji katika fatwa ni: kutoa fatwa bila ya kuthibitisha na kuangalia vizuri, lakini kama alikuwa anajua fatwa hii kabla ya hivyo, basi hakuna tatizo lolote kuitoa, na wanavyuoni waliotangulia walikuwa wakifanya hivyo, pia miongoni mwa aina za urahisishaji katika fatwa ni mufti kufuata mbinu Haramu au Makruhu kwa ajili ya malengo mabaya, kushikilia mambo yenye shaka ili kumnufaisha mtu, au kutia uzito kwa anayetaka kumdhuru. Ama anayetoa fatwa kwa nia safi na kufuata mbinu zisizo na shaka kwa ajili ya kumwepusha mtu na kosa la kiapo basi ni jambo zuri. Wanavyuoni waliotangulia wamefanya hivyo, kama Sufyaan ambaye alisema: elimu kwetu ni ruhusa pasipo na shaka yoyote, ama kutia uzito basi kila mmoja anaweza kutenda vizuri”.

Kutokana na yaliyotangulia hapo juu: inadhihirika kwamba ipo tofauti kubwa kati ya urahisishaji na uwepesishaji katika kutoa fatwa, urahisishaji kunatokana na upungufu na kasoro katika utafiti, nayo ni aina ya uzembe na matumizi mabaya kwa hivyo hukumu yake ni haramu, lakini uwepesishaji unatokana na elimu ambayo ni thabiti, utambuzi wa malengo ya kisheria, dalili zake na njia za kutofautisha baina yao, kuelewa hali za watu, mahitaji yao na hali zao halisi, basi uwepesishaji ni aina ya misingi ya kielimu inayosomwa vizuri kupitia wanavyuoni wa Kiislamu na maimamu wa fiqhi, kwa hivyo, fatwa ya mufti huyo inakuwa katika duara la Sunna au Wajibu kwa mujibu wa hali halisi ilivyo.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas