Ustaarabu wa Kiislamu na Misingi ya...

Egypt's Dar Al-Ifta

Ustaarabu wa Kiislamu na Misingi yake ya Kiakida

Question

Ni ipi Misingi ya Kiakida katika Ustaarabu wa Kiislamu?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Kwa mujibu wa marehemu profesa Shawkiy Dhaif, mkuu wa taasisi ya lugha ya Kiarabu, misingi ya kiakida katika ustaarabu wa Kiislamu inajengeka kwa misingi ifuatayo:
1- Wahyi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. 2- Quraani Tukufu. 3- Mwenyezi Mungu Mtukufu. 4- Mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake. 5- Mtume Muhammad S.A.W. 6- Sunna ya kinabii. 7- Uislamu na Imani. 8- Sala na Zaka. 9- Saumu na Hija. 10- Dalili za Mwenyezi Mungu za kimaumbile. 11- Uislamu wa Ulimwengu wote. 12- Ushauri na Makubaliano. 13- Kujitahidi. 14- Uwepesi. 15- Uwastani. 16- Uhuru wa Kidini na kuvumiliana. 17- Uadilifu. 18- Elimu. 19- Akili. 20- Kubatilisha uzushi, uchawi na ukuhani. 21- Hukumu na kadari. 22- Uchamungu. 23- Kutegemea 24- Khofu na woga. 25- Toba. 26- Msamaha.
Na tutaelezea kwa idhini ya Mwenyezi Mungu misingi ya kiakida kwa urefu.
1- Wahyi kwa Mtume Wa Mwenyezi Mungu S.A.W. : Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na haikuwa kwa mwanadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humfunulia ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hekima} [SHUWRA 51]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Hayakuwa haya ila ni ufunuo uliofunuliwa. Amemfundisha aliye mwingi wa nguvu.} [ANNAJM 4-5]. Na Mtume S.A.W. alisema: " Alharith Bin Hishaam alimwuliza Mtume S.A.W. wahyi unakujiaje?, Mtume S.A.W akasema, baadhi ya nyakati hunijia kama mlio wa kengele nao ndio mkali zaidi kwangu mimi, ninapozinduka nakuwa nishafahamu kilichosemwa, na wakati mwingine hujitokeza mtu kama malaika akanisemesha na nikazingatia anachokisema. Bi Aisha alisema nilimwona Mtume unamteremkia wahyi katika siku yenye baridi kali kisha akiondoka huyo aliyemjia Mtume hutokwa na jasho katika uso wake". [Kutoka kwa Aisha, Hadithi ya 475 kwa Bukhariy, na ya 2333 kwa Muslim]. Na kuna aya na hadithi nyingi ambazo zinaelezea Wahyi kwa Manabii na Mitume, na miongoni mwake zinaelezea njia tatu anazozitumia Mwenyezi Mungu kuwapa Wahyi Mitume na Manabii wake, nazo ni; Ilhamu, Maneno kutoka nyuma ya pazia au kuja kwa malaika. Na Ilhamu ni kile anachokikuta Mtume katika nafsi yake yu macho au ndotoni.
2-Quraani Tukufu: Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Quraani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizowazi za uwongofu na upambanuzi”. [BAQARAH 185], pia Amesema: “Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika elimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipokuwa wenye akili.”. [AALI IMRAAN 7].
Na Quraani tukufu imemteremkia Mtume S.A.W kwa hatua kulingana na matukio na hali kwa miaka ishirini na tatu, na Quraani ni jina la maneno yote aliyofunuliwa Mtume S.A.W, yaliyoandikiwa Msahafuni, wenye sura mia na kumi na nne, mwanzo wake ni Suratu Fatiha na mwisho wake ni Suratu Annaas, Quraani ina majina mengi ambayo Allah s.w ameyataja katika aya zake, lakini mashuhuri zaidi ni jina “Quraani”. Miongoni mwa majina hayo ni: 1- Kitabu, Allah S.W. anasema: “Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye amemteremshia mja wake Kitabu, wala hakukifanya kina upogo”. [ALKAHF 1]. 2- Alfurqan, Allah S.W. anasema: {Ametukuka aliyeteremsha Alfurqan kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote.} [AL FURQAN]. 3- Wahyi, Allah S.W. anasema: “Sema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi hawasikii wito wanapo onywa.”. [AL ANBIYAA 45]. 4- Tanziyl (uteremsho), Allah S.W. anasema: “(Tanziyl) Uteremsho huu umetoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.} [FUSWILAT 2].
Na aya ni kiwango fulani cha maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, inaweza ikawa ndefu kama aya ya deni katika Suratu Baqarah, au fupi kama aya ya 64 Suratu Rahmaan {Za kijani kibivu.} “مُدْهَامَّتَانِ”.
Na Suratu ni kiasi maalum cha aya za Quraani zinazojulikana mwanzo na mwisho, na Suratu yenye aya chache ni yenye aya tatu kama Alkawthar, na Suratu Baqarah ni ndefu ina aya mia mbili na thamanini na sita. Ama majina ya Suratu na mpangilio wa aya ni kutoka kwa Mtume Muhammed S.A.W.
Na aya za Muhkam ni aya za imani na sheria ya Kiislamu kwa maamrisho yake na makatazo yake, na aya za mawaidha na yanayohusiana na visa vya Manabii. Na kuna aya za mifanano kinyume ya aya Muhkam, na aya hizo ni chache ukilinganisha na aya Muhkam. Aya zenye mfanano zinajulisha maana zenye kufanana. Na tunaweza kuzifasiri aya “Muhkam” kwa kuwa maana zake ziko wazi kwa kusikia, ama zenye mfanano zinahitaji kufikiri na kuzingatia sana, mfano aya za kuumbwa kwa ulimwengu na aya zinahosiana na Mola mtukufu. Kama kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Arrahmani, Mwingi wa Rehema, aliyetawala juu ya Kiti cha Enzi.”. [TAHA 5].
Na Quraani Takufu ni kitabu cha Mwenyezi Mungu chenye miujiza kwa maelezo yake na ufasaha wake. Mwenyezi Mungu anasema: “Sema: Wangelikusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Quraani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.”. [ISRAA 88]. Wangelikusanyika watu na majini ili walete mfano wa Quraani hii katika balagha na ufasaha wake kwa kuelezea ibada ya Mwenyezi Mungu, kumpwekesha kwa utukufu wake, au uumbaji wake wa ulimwengu, au kufufuliwa na kukusanywa, au kuhusu sheria ambayo inawaletea watu furaha duniani na akhera, au kuhusu maadili na mawaidha wangeshindwa. Na wanadamu wameshindwa na wataendelea kushindwa kuleta mfano wa aya za Quraani.
3- Mwenyezi Mungu Mtukufu: Mwenyezi Mungu anasema: “Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee. Mwenyezi Mungu Mkusudiwa. Hakuzaa wala hakuzaliwa. Wala hana anayefanana naye hata mmoja.} [AL IKHLAS 1-4], pia anasema: “Lau wangelikuwamo humo miungu wengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingelifisidika. Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa Arshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayoyazua.” [AL ANBIYAA 22]. Na Mwenyezi Mungu anasema: “Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.”. [ASH SHUURA 11].
Na neno (Allah) ni jina maalumu la Mwenyezi Mungu linalomaanisha yeye peke yake katika uungu wake usio na mipaka, jina hili linakusanya maana zote za majina yake matukufu, na yale yanayofikirika miongoni mwa ukubwa wa utukufu, ukubwa wa kusifiwa, utakatifu wake, ukamilifu wake, na ubwana wake. Na (Al Ahad) yaani (mmoja) ni miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na unasisitiza upweke wa Mwenyezi Mungu katika pande zote; dhati, sifa, vitendo na ibada.
Ama upweke na umoja wa yeye mwenyewe alivyo kunamaanisha kuwa yeye ndiye anayejitosheleza kwa kuwepo kwake, na kuwepo kwake ni kwa tangu na tangu, naye ndie aliyeuumba uwepo wote na viumbe vyake vyote, na kwamba yeye ni mmoja asiye na mshirika, na kwamba kila atakayemuabudu asiyekuwa yeye atakuwa ni mshirikina aliyekufuru na anastahiki kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu pia adhabu yake kali. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na husamehe yasiyokuwa hilo kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika amezua dhambi kubwa.”. [AN NISAA 48].
Na upweke wa sifa ni kumtakasa Mwenyezi Mungu kutokana na sifa za viumbe kama watu, kwani yeye yu peke yake katika nafsi yake, na sifa zake zilizokuja katika Quraani Tukufu zinaoonesha utukufu wa Mwenyezi Mungu, kama vile mwenye kusifika na kila sifa njema, mwenye utukufu, mtakatifu aliyetakasika na sifa zote chafu. Na miongoni mwa sifa zake zinaonesha uumbaji wake wa ulimwengu na uwepo kama vile: mtengenezaji, mtia sura na muumbaji. Na zipo zinazoonesha uwezo wake wa kiungu kama vile: mwenye uwezo wa kufanya, mwenye nguvu juu ya kila kitu na mwenye kuyaendesha mwenyewe mambo yake. Na miongoni mwa sifa hizo huonesha ujuzi wake Mungu kama vile: Mjuzi wa kila kitu, mwenye kuyajua yaliyo dhahiri na mwenye hekima. Pia miongoni mwake zioneshazo huruma ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kama vile: mwenye huruma, mwingi wa rehma, mwenye kurehemu, pamoja na sifa zake zenye daraja ya juu, naye Mwenyezi Mungu ni mwenye kukusudiwa kwa maombi na haja mbalimbali, yeye peke yake, kwani yeye ndio kimbilio na mafikio, naye ndiye anayeombwa msaada na uokovu, kila kitu kipo mkono mwake naye amekishikilia, na kila kiumbe humwelekea Mwenyezi Mungu katika hali ya kuhisi unyonge na haja zake.
Na Mwenyezi Mungu lililotakasika jina lake anasema: “Lau wangelikuwamo humo miungu wengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingelifisidika. Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa Arshi (Kiti cha Enzi) na hayo wanayoyazua.”. [AL ANBIYAA 22]. Kama kungelikuwa na miungu mingi basi pangelazimika mungu awe na sifa zake maalumu za uungu wake kama utashi usio na mipaka na uwezo kamili wa kufanya atakalo, na kwa hivyo kusababisha ukinzani kati ya miungu hiyo kwa uwezo na utashi. Allah s.w anasema: “Mwenyezi Mungu hana mwana yoyote, wala hanaye mungu mwengine. Ingekuwa hivyo basi kila mungu angelichukua alivyoumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengine. Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazomsifu.”. [MUUMINUN 91].
Kila mmoja wao angelitaka kuwashinda wengine na kuwa juu yao, basi pangetokea mgongano wa utashi wa kila mmoja wao na kupelekea ulimwengu mzima kuangamia, lakini mandhari ya ulimwengu yako chini ya macho ya muumba mmoja yanaonesha mpangilio wa hali ya juu, jambo ambalo linapelekea kuwa muumba ni Mungu mmoja asiye na mfanowe wala wa kushindana naye. Na upweke wa Mwenyezi Mungu ni msingi wa dini zote za mbinguni, na Quraani Tukufu inathibitisha akida hiyo, na anayeamini kuwa Mwenyezi Mungu ana mshiriki au ana mfano au ana mwana basi amemkufuru na anastahiki adhabu yake kali.
4- Mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake: Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.} [AAL IMRAAN 31]. Na Mtume S.A.W akasema: "Mwenyezi Mungu anasema: Yoyote atakayemfanyia uadui mja wangu basi nitamtangazia vita, na ninapenda zaidi mja wangu kujikurubisha kwangu kwa jambo ambalo nimemfaradhishia, na mja wangu bado anaendelea kujikurubisha kwangu kwa Sala za sunna ili nimpende, na nitakapompenda basi nitakuwa mimi ndio sikio lake analosikilizia, na jicho lake anaoloonea, na mkono wake anaoutumia kujipatia nguvu, na mguu wake anaoutumia kutembea, na akiniomba nitampa na akitaka nimkinge na jambo baya basi nitamkinga, isipokuwa mimi husitasita kutokana na nafsi ya muumini anayeogopa kifo, kwani mimi (kwa ajili hiyo) huchukia kumtendea jambo baya." [Imetolewa na Al Bukhariy 6137 kutoka kwa Abu Huraira].
Hakika mwislamu anapaswa kumpenda Mwenyezi Mungu kwa dhati yake, na kwa ukamilifu wake katika kuumba kwake ulimwengu na nidhamu yake inayoenea duniani, na ukamilifu wake katika sheria ya Kiislamu, na rehema na heri yake kwa binadamu iliyoenea duniani. Na mapenzi hayo yanamlazimisha mwislamu kumtii Mwenyezi Mungu Mtukufu katika amri na makatazo yake, kujiepesha na mambo aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, kumwabudu ibada ya haki, kuwajibika katika aliyokuja nayo Mtume S.A.W., akimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwongoza katika dini hii iliyonyooka, akimshukuru kwa neema zake ambazo hazina kifani, wakati huo Mwenyezi Mungu humwongezea mapenzi makubwa, na ni mapenzi ya aina gani haya! Ni mapenzi ya Mweyezi Mungu ambayo hayana mfanowe kwani yamezungukwa na kuandikiwa usamehevu wa Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu huyamiminia ukarimu wake, hakika hadithi Qudsi iliyotangulia inaonesha mahaba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu yasiyo na kifani kwa waja wake wema.
5- Mtume Muhammad S.A.W.: Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Na mwitaji kumwendea Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na taa yenye kutoa nuru. Na wabashirie Waumini ya kwamba wana fadhila kubwa inayotoka kwa Mwenyezi Mungu.”. [AL AHZAB 45-46], pia anasema: “Hakika amekwishakujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.”. [TAWBAH 128]. Na Bi Aisha R.A alisema: Tabia ya Mtume S.A.W ilikuwa ni Quraani, je, husomi katika Quraani kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na bila shaka una tabia njema kabisa.”. [QALAM 4]. [Imetolewa na Ahmad 24545].
Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu alimsifia Mtume wake katika Quraani Tukufu kwa sifa nyingi, basi akamsifia kuwa ni shahidi, kwani yeye ni shahidi kwa sheria yake juu ya sheria za dini zote za mbinguni zilizotangulia, kwani amekuja na sheria ya mwisho inayotawala sheria zote, na yeye ni shahidi juu ya Umma wake siku ya Kiama. Mwenyezi Mungu anasema: “Na tukakuleta wewe (Nabii Muhammad) uwe shahidi juu ya huu (Umma wako)”. [ANNISAA 41]. Pia Mwenyezi Mungu alimsifu Mtume Muhammad S.A.W kuwa ni mtoaji wa habari njema, kwa maana kuwa ni mpashaji wa habari za kuwafurahisha wale wenye kuufuata Uislamu na wanamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na alimsifu kuwa yeye ni mwonyaji wa wale wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwamba mwisho wao ni motoni na adhabu kali. Mtume rehma na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, ni mlinganiaji kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake hana mshirika, na Mtume S.A.W ni taa iangazayo inayoongoza haki na sheria ya Allah, pia inaangaza katika pahali penye giza, kama nuru ya asubuhi inayoangaza baada ya usiku wenye giza.
Na Mwenyezi Mungu amewakirimu waarabu katika aya ya sura ya TAWBA kwa kuwa aliwatumia Mtume miongoni mwao na kutoka nasaba yao halisi anawasomea Quraani kwa lugha yao. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Hakika amekwishakujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.”. [TAWBA 128], Kwani Mtume S.A.W anajisikia uchungu Umma unapopatwa na shida na dhiki, kwa hivyo sheria ya Uislamu ilikuwa nyepesi kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.” [BAQARAH 185]. Na imethibitika kutoka kwa Bi Aisha R.A. alisema: " Mtume S.A.W alikuwa akiacha amali huku akiwa anapenda kuifanya, kwa kuchelea watu wasije wakaifanya kisha ikafaradhishwa juu yao" [Imetolewa na Bukhariy 1067, na Muslim 718]. Kutokana na hayo, Mtume S.A.W alikuwa anawakataza masahaba wake kuuliza sana. [Imetolewa na Bukhariy 6108, na Muslim 593 kutoka kwa Almughira Bin Shuuba].
Naye S.A.W anawajali waumini na anatilia maanani kuongoka kwao, na alikuwa mpole kwao kwa kiasi cha juu cha upole na mwingi wa huruma kwao kwa kiwango cha juu kabisa cha huruma, kwa hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika haki ya Mtume S.A.W. “Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukishakata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaomtegemea.” [AAL IMRAAN 159]. Na anayashuhudia hayo mtumishi wake bwana wetu Anas Bin Malik R.A. anayesema: "Nimemtumikia Mtume S.A.W kwa muda wa miaka kumi tukiwa Madina nami nikiwa kijana, si kila mtu yuko kama vile anavyotamani rafiki yangu niwe kwake, hata siku moja Mtume hajathubutu kunambia hata neno dogo la kuniudhi na hakusema kwanini umefanya hivi? Au kwanini hukufanya hivi?" [Imetolewa na Abu Dawud 4774, na Tarmidhiy 2015, na alisema hadithi hii ni nzuri na sahihi].
Mwenyezi Mungu Mtukufu ametutaka tumfanye Mtume S.A.W. kuwa ni kigezo chema katika kauli zake, vitendo vyake, na hali zake zote. Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika nyinyi mnayo ruwaza (kigezo) njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.” [AL AHZAB 21],
Imefaradhishwa kwa waislamu wamfuate daima kwa kila anachowausia na kuwahamasisha miongoni mwa misingi ya imani, ushujaa, kutosheka, kutekeleza ahadi, kumlinda mwanamke, kuamrisha mema na kukataza mabaya, kuwahurumia waislamu, kusitiri nyuchi zao, kuwafanyia wema wazazi wawili, na ndugu, uaminifu, usafi wa nia, kuyakimbilia yenye kheri ndani yake kwa ajili ya umma wa Kiislamu pamoja na kushikamana na fadhila za akili na kupiga vita uchawi, ukuhani, bidaa, urogaji, na kupiga vita udhalimu na kuharamisha uzushi na uongo..... n.k.. Kwa sababu hiyo Imamu Ibn Hazm anasema katika kitabu che [Al Akhlaaq wa Sira]; "Anayetaka heri ya siku ya mwisho, hekima ya dunia, uadilifu wa mwenendo, kuwa na aina zote za maadili mema na kupata mambo mazuri yote, basi amwige Muhammad S.A.W Mtume wa Mwenyezi Mungu, na atumie maadili yake na mwenendo wake kadiri atakavyoweza.". Ewe Mwenyezi Mungu Mtukufu tuwezeshe kumfuata Mtume S.A.W.
Na maadili mema ni msingi miongoni mwa misingi ya sheria ya Mtume S.A.W, Sunna yake na wasifu wake. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Na hakika wewe una tabia tukufu.”. [AL QALAM 4]. Maadili ni mkusanyiko wa mambo yenye kujumuisha uzoefu, tabia njema za kuigwa, na ni ushahidi wa kiungu usiokuwa na ushahidi mwingine kama huo. Mtume S.A.W alikuwa ana tabia njema kwa sababu tabia yake ilikuwa ni Quraani yenyewe kama alivyosema Bibi Aisha R.A.
Wanachuoni, wasomi na watafiti wengi wameandika masomo mengi na mbalimbali kuhusu maadili ya Mtume S.A.W na walijaribu kuyaandika hayo kwa ujumla au baadhi ya sehemu, na miongoni mwa masomo hayo ni kitabu cha "Maadili ya Mtume S.A.W" kilichoandikwa na Imamu Alhafidh Abi sheikh Al-Assfahaaniy, na kitabu cha "Alkhuluk Alkaamil" kilichoandikwa na ustaadhi Muhammad Ahmad Jad Elmawla, na vitabu vingi vingine. Na tunaweza kusema kwamba yaliyowasilishwa na wanachuoni wasufi ni maelezo mafupi ya maadili ya Mtume Muhammad S.A.W.
6- Sunna ya Mtume S.A.W: Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Nasi tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, wapate kufikiri”. [AL NAHL 44], na Akasema: “Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.” [NISAA 59].
Mtume S.A.W anasema: "Niacheni kwa yale niliyoyaacha kuwaambia. Hakika wale waliokuwa kabla yenu waliangamia kutokana na kuuliza kwao na kutofautiana kwao na mitume yao, ninapokuzuieni jambo basi liepukeni, na ninapokuamrisheni jambo basi lifanyeni kwa kadiri mtakavyoweza" [Imetolewa na Bukhariy 6858, na Muslim 1337, kutoka kwa Abu Huraira].
Na Ukumbusho (wahyi) alioteremshiwa Mtume S.A.W. ni Quraani tukufu, na Sunna tukufu inaifafanua. Ama maelezo ya Mtume S.A.W yanayofafanua hukumu za Quraani na makatazo yake yameitwa kwa jina la HADITHI au SUNNA, na maana ya HADITHI kilugha ni mpya, kinyume cha kuukuu. Na katika istilahi ya wanachuoni wa hadithi ni kila kilichopokelewa kutoka kwa Mtume S.A.W. maneno, vitendo, kukiri au sifa ya kimaumbile, au sifa za kimaadili kama upendo, ukarimu, kusamehe na usamehevu, na alikuwa mwingi wa kusamehe anapoweza, Na kukiri maana yake ni Mtume saw kuridhia kauli au kitendo kilichofanywa mbele yake. Na Sunna asili yake kilugha ni mila na njia. Na katika istilahi ya wanachuoni wa hadithi maana yake ni: desturi au njia (mfumo) ya Mtume S.A.W. katika kufanya jambo, na masahaba wakalifanya katika zama ya Mtume S.A.W. na baada ya kifo chake.
Kutokana na umuhimu na muhimili mkubwa wa Sunna ya Mtume, paliasisiwa msingi mkuu kwamba asili ya sheria za Kiislamu ni: Kitabu na Sunna, au Quraani Tukufu na Sunna tukufu. Na Sunna ya Mtume ni ubainisho wa Quraani tukufu na ufafanuzi wake, pia inatunga sheria katika hukumu nyingi sana ambazo hazikupatikana ndani ya Quraani tukufu, mchango wake hauishii tu katika kukibainisha kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu, bali inajitosheleza pia katika kutunga sheria na hukumu mbali mbali. Na kwa hiyo Mtume S.A.W aliusia ifanyiwe kazi Sunna yake kama inavyotakikana. Kutoka kwa Aryaadh Bin Saaria R.A. alisema: "Siku moja Mtume S.A.W. alituswalisha kisha akatuelekea upande wetu na kutupa mawaidha ambayo yalikuwa mazito na sote tukatokwa na machozi na nyoyo zetu zikawa na unyenyekevu na mmoja wetu akasema, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mawaidha haya yanaonekana kama ni ya kutuaga, je unatuusia kitu gani? Mtume S.A.W. akasema: nakuusieni kumcha Mwenyezi Mungu, na kumsikiliza na kumtii hata kama ni mtumwa wa kihabeshi. Hakika atakayeishi baada yangu ataona hitilafu nyingi sana, basi mlazimike kufuata Sunna (mwenendo) wangu na mwenendo wa masahaba wangu waongofu, shikamaneni na Sunna hii na mjitahidi kuitekeleza. Na jiepusheni na mambo ya kuzushwa kwani kila lenye kuzushwa ni uzushi na kila uzushi ni upotofu." [Imetolewa na Abu Dawud 4607, Tirmidhiy 2676, na Ibn Majah 42].
Na pia imethibiti kutoka kwa Aryaadh Bin Saaria kutoka kwa Mtume S.A.W. amesema: "Je mmoja wenu aliyeketi katika kiti chake kikubwa anadhani kuwa Mwenyezi Mungu hakuharamisha kitu isipokuwa ndani ya Quraani?, tambueni kuwa nami naapa kwa Mwenyezi Mungu hakika nimetoa mawaidha, nimeamrisha na nimekataza vitu mbali mbali, na hakika (mawaidha, maamrisho na makatazo yangu) ni sawa na ya Quraani. [Imetolewa na Abu Dawud 3050].
Na katika hadithi sahihi nyingine, Mtume S.A.W. amesema: "Mimi nimepewa Quraani na mfanowe (Hadithi) pamoja nayo hawezi mtu aliyeshiba akiwa katika kiti chake anawaambieni kuhusu Quraani hii kuwa mtakayoyakuta ndani yake miongoni mwa yaliyo halali basi yahalalisheni na mtakayoyakuta ndani yake kuwa ni haramu basi yaharamisheni." [Imetolewa na Abu Dawud 4604, Tirmadhiy 2664, na Ibn Majah 12 kutoka kwa Almeqdaam Bin Maad Yakrib]
Kwa hivyo Hadith hizi zinatuelezea wazi na kutufafanulia umuhimu wa Sunna (mwenendo wa Mtume), na zinaikosoa misimamo inayokanusha Sunna na kuwa kwake Hoja kwa waislamu, kwa kudhani tu, na misimamo hiyo inakosea kwa kudhani kuwa eti ni lazima kuchukua au kutohoa hukumu kutoka katika Quraani tukufu peke yake.
7- Uislamu na Imani. 8- Sala na Zaka. 9- Saumu na Hija. 10- Dalili za Mwenyezi Mungu za kimaumbile. 11- Uislamu wa Ulimwengu wote. 12- Ushauri na Makubaliano. 13- Kujitahidi. 14- Uwepesi. 15- Uwastani. 16- Uhuru wa Kidini na Kuvumiliana. 17- Uadilifu. 18- Elimu. 19- Akili. 20- Kubatilisha uzushi, uchawi na ukuhani. 21- Hukumu na kadari. 22- Uchamungu. 23- Kutegemea 24- Khofu na woga. 25- Toba. 26- Msamaha.
Marejeo : Marehemu Profesa Shawkiy Dhaif “ Alhadhaaratu Islaamiyya Minal Quraani Wa Sunna”, Daaru Maarif 1997.

Share this:

Related Fatwas