1- Urithi wa Kiislamu, Maana na Ist...

Egypt's Dar Al-Ifta

1- Urithi wa Kiislamu, Maana na Istilaahi Kama ni Chombo cha Kuuelewa Urihi huo.

Question

 Je, maana na Istilaahi zina mchango gani kama chombo cha kuuelewa urithi wa Kiislamu?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Maana na Istilaahi ni moja kati ya vipengele ambavyo kwa dhana yetu ni ufunguo wa urithi wetu, na wakati tunaposoma vitabu vya urithi ni lazima tulirejeshe suala la Istilaahi akilini mwetu. Na Istilaahi hizo zinagawanyika katika sehemu nyingi, tunapaswa kuzifahamu vizuri. Na Ili tulielewe suala hili kwa undani, ni lazima turejee kwa kile kinachoitwa suala la Hali ya kitu.

Hali ya kitu hapa ina maana ya kukifanya kitu kikabiliane na kitu kingine, yaani, kiangaliane na kitu kingine, kwa sababu watu wanapokubaliana juu ya Istilaahi moja hali hiyo ina maana ya kwamba wanakubaliana juu ya kuweka neno fulani kwa ajili ya maana fulani. Utaratibu huu una mgogoro katika lugha, hakuna uhusiano maalumu kati ya herufi na maana, lakini ni uhusiano uliowekwa na watu. Hakuna uhusiano kati ya herufi za neno “simba” na mnyama mwenyewe, ambapo kama mtu mmoja akisema "Simba", watu wote wataelewa kwamba anamzungumzia huyo mnyama wa porini ambaye mwenye umbile maalumu. Basi ni kitu gani kilichotokea ili kuwekwa neno hilo katika maana hiyo?

Tofauti ilijitokeza kati ya wanavyuoni waliobobea katika elimu ya misingi ya lugha kuhusu kulipa neno maana, kati ya wale waliyosema kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeyapa maneno maana zake, na dalili yao ni kauli ya Mwenyezi Mungu {Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote} [AL BAQARAH 31], na kati ya kauli ya wengine ambao wanasema kwamba wanadamu ndio waliotengeneza lugha. Na kuna wale waliosema kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeweka misingi na sheria za lugha, kisha baada ya hapo, binadamu akaunda njia za utekelezaji wa sheria hizi na utengenezaji wa misamiati mingi pia, wakati ambapo wengine hawakujibu chochote juu ya swali hili, bali walisema: hatujui kama Mwenyezi Mungu au mwingine yoyote asiyekuwa Mwenyezi Mungu tukufu ndiye aliyeweka lugha. Na Tayari tumekwishaashiria hayo hapo kabla, kwa undani zaidi.

Tumeshaona pia hapo kabla, kwamba lugha –hata kama zimewekewa maneno yenye maana –lakini sheria ikaja na kutohoa katika matamshi hayo ya lugha, maana zake mbali mbali za kilugha na kuwa na maana nyingine maalumu zinazokusudiwa na Sheria. Na tumekwishatoa mifano –hapo kabla –kuhusu tofauti kati ya hali hizi mbili: hali ya tamshi kwa upande wa maana yake kwa wanavyuoni wa lugha, na hali ya kikanuni, kama vile hali tamko lililoletwa na Sheria ya Mwenyezi Mungu.

Na pia imegundulika kuwa makundi mengi ya watu yameweka maana tofauti katika neno moja, kila mmoja amefanya hivyo kwa mujibu wa ubobeaji wake. Tunaona kwamba wabobeaji wa elimu ya misingi–kwa mfano- wameweka neno “asili” kwa maana ya kipimo kinachotumiwa, wakati ambapo neno “asili” katika lugha lina maana ya chanzo cha kitu, huku neno hilo hilo kwa wanachuoni wa fiqhi –katika tamko lao: Zaka ya Mali haitolewi kwa asili na kwa tawi –kwa maana kuwa neno "asili" linakusudiwa baba, mama, babu na bibi. Kwa hivyo basi, kila kundi la wanavyuoni linajiwekea maana maalumu kwa ajili ya neno maalumu, na hii ni hali ambayo wanavyuoni wameiita “Istilaahi ”.

Istilaahi: “ni kuliwekea neno maana maalum kwa wanavyuoni wenyewe”, na hali hiyo inaitwa "Mjulikano Binafsi", nao ni maana maalum inayojulikana kwa mafundi, wanavyuoni au watu wa sanaa fulani. Kuna "Mjulikano wa kiujumla", nao ni ule unaojulikana kwa watu wa eneo au nchi fulani, lakini haupo katika lugha wala katika sheria. Kwa mfano Neno "mnyama anayetambaa"–kwa mfano –maana yake hasa kwa Wamisri ni "punda", lakini katika lugha lina maana ya kila kinachotambaa ardhini kwa miguu yake, bali si hivyo tu, lina maana ya kila kitu kitambaacho kwa ujumla, na kwa hiyo binadamu –kutokana na maana ya kilugha- ni miongoni mwa wanyama wanaotambaa, lakini kama mtu yoyote - nchini Misri- akimwambia ndugu yake kuwa ni “Daabah” kwa maana ya kiumbe kama viumbe wengine ardhini wanaotambaa, basi mtu huyo atazingatia kuwa ametukanwa, kwa kuitwa punda kwa sababu ya kujulikana kwa neno hilo nchini Misri.

Na hivyo ndivyo ilivyo, kama tukitaka kuzungumza kuhusu sanaa fulani miongoni mwa sanaa za urithi wetu, ni lazima kwetu tufahamu na kuelewa Istilaahi zilizowekwa mbele na wanavyuoni au wanasanaa kwa ajili ya maana maalumu. Kama hatukufanya hivyo, maana zitaingiliana na tutapoteza mengi mazuri.

Haiwezikani kupata ufahamu ufaao, isipokuwa tukizijua Istilaahi za sanaa tunazozizungumzia, kwa mfano, neno “Jinsi”, ambalo limo katika mlango wa “kuuziana” linatumika kwa njia mbili tofauti katika mantiki na katika fiqhi. Tukitaka kuonesha maana yake katika mantiki, tutapata kuwa, “Ni neno kusanyishi liachikwalo kwa wengi wanaotofautiana katika ukweli wa jibu la swali; ni kitu gani?” Kama vile “Mnyama”, neno hili hutumika kwa binadamu, simba na twiga, wakati ambapo neno "Aina" Katika mantiki lina maana ya “neno jumuishi linalopachikwa kwa wengi walio sawasawa katika ukweli wake katika jibu la swali; ni kitu gani?” kwa hivyo Neno “mwanadamu” linaashiria maana ya aina kwa wanavyuoni wa Mantiki.

Ama kuhusu wanachuoni wa fiqhi, wao wametumia neno “Jinsi” katika maneno yao kama lilivyotumika neno “Aina” kwa wanavyuoni wa Mantiki, na kwa hivyo basi jinsi -kwa mujibu wa wanachuoni wa fiqhi- ni kila kinachokuwa na muungano wa wahusika wake hata kama wahusika hao watatofautiana vyeo. Kwa mfano “ngano” ni “jinsi” ingawa kutakuwa na tofauti za ukubwa na aina zake, wakati ambapo ni “Aina” kwa wanavyuoni wa Mantiki.

Kutokana na hayo, kama mwanafunzi amesoma matini ya kifiqhi tuliyonayo na akalichukulia neno “Jinsi” kwa namna aliyojifunza katika somo la Mantiki, basi hichi kitakuwa kizuizi cha yeye kutoelewa vyema, na jumla ya sentensi iliyo mbele yake ingekuwa ngumu na ngeni, na hasa pale anaposoma: kuwa kuuza kitu kwa kitu kinachofana nacho hairuhusiwa isipokuwa kwa masharti mawili: Ulinganifu na Uwepo wake. Ulinganifu una maana ya kwamba kama nikitaka kuuza "ngano" kwa ngano lazima niuze kipimo kwa kipimo kinacholingana. Na Uwepo maana yake ni hivi sasa, au wakati huo huo. Na maelezo haya yamechukuliwa kutoka katika Hadithi ya Mtume S.A.W: "Dhahabu kwa dhahabu na fedha kwa fedha, na ngano kwa ngano, shairi kwa shairi, tende kwa tende na chumvi kwa chumvi, mfano kwa mfanowe (Huu ni ulinganifu) mkono kwa mkono (na huu ndio Uwepo) na atakayeongeza au akaomba nyongeza basi hakika atakuwa amefanya Riba, na kwa hivyo basi, mpokeaji na mtoaji wanalingana (katika Riba).

Na huu ni utendeanaji usiokuwapo ambapo Mtume Muhammad, S.A.W. aliuzungumzia kwa lengo la kuzuia kisingizio cha aina yoyote, ambapo Mtume Muhammad, S.A.W. alitaka bei zisiongezeke katika masoko, kwa hivyo akaharamisha kujipendelea na kuchelewesha malipo ya bidhaa za msingi, na alitaka kuwepo uthibitisho wakati wa makabidhiano ili watu walinde bei za bidhaa zao na wala masikini asidhurike. Ni kama vile Mtume amesema: na anaetaka kufanya hivyo basi na afanye hivyo jambo ambalo mtu mwenye akili hawezi kulifanya. Inakuwa kama vile amesema: msithubutu kufanya hivi hata mara moja; ni sawa sawa iwe kwa kutanguliza malipo au kwa kuyachelewesha.

Kwa hivyo, kama tukisoma hukumu za hali hizi, yaani riba ya kujiongezea na riba ya kuahirisha malipo, na tukawa na utulivu wa uelewa kuwa “Jinsi” ni kitu ambacho ndani yake kuna aina mbali mbali, basi tungelifahamu kwamba hairuhusiwi kuuza ngano kwa shairi kwa kuongeza ujazo, na uelewa huu ni kosa kwa sababu inaruhusiwa kuuza shairi kwa ngano kwa kuongeza ujazo. Na katika hadithi hiyo hiyo Mtume, S.A.W. anasema: “Kama aina hizi ni tofauti, basi uzeni kama mnavyotaka, lakini iwe mkono kwa mkono,”. Yaani kama ikiuzwa ngano kwa ngano, inahitajika kukamilika kwa masharti mawili: Ulinganifu na Uwepo, lakini kama ikiuzwa ngano kwa shairi, basi linahitajika sharti moja tu; nalo ni Uwepo, kwa maana kuwa mtu anatoe kilo moja ya ngano kwa kilo mbili za shairi, katika wakati huo huo.

Na hivi ndivyo ilivyo, kama tutasoma masuala ya Fiqhi bila kuwa na mzinduko katika Istilaahi za wanachuoni wa Fiqhi, basi pengine hatutaelewa chochote, au huwenda tukaelewa uelewa usio sahihi, bali hii naweza kupelekea kusoma kinyume na lengo la waandishi.

Suala jingine linalohusiana na Istilaahi mbali mbali, nalo ni kuhusu Istilaahi zilizowekwa na wataalamu wa ujuzi husika. Kwa mfano, Wanavyuoni wa madhehebu ya Shaafiy, wao wameunda maneno yao kwa kutumia njia maalumu, na hivyo, wakati wao walipomuiga Imamu Shaafiiy ambaye ni Muasisi wa madhehebu hayo, wao wameyaita maneno yake kuwa ni “Tamko lake”, iwapo mwanachuoni wa Fiqhi ya Madhehebu ya Shaafiiy akisema: “Katika jambo hili, kuna mitazamo miwili”, maana yake ni kwamba Imamu Shaafiiy mwenyewe ametoa fatwa mbili tofauti katika suala hilo moja.

Hata hivyo, madhehebu ya Imamu Shaafiiy na mengine hayakuishia kwa Maimamu tu, bali baada ya maimamu, ambapo yamehudumiwa na ndio sababu ya kuendelea kuwepo hadi leo, baadhi ya wanachuoni wakachukua hatua ya kuyatumikia madhehebu yote na watu wa madhehebu fulani na wafuasi wa imamu wao wakawa na maneno katika madhehebu yake na Istilaahi katika maneno yao zinazotafautiana na maimamu wenyewe. Na kwa ajili hii wafuasi wa Imamu Shaafiiy walipoandika hayo kutoka kwao yaliitwa “Alwaj-hu (Mwelekeo)”, kwa hivyo basi, inaweza kuwa katika jambo maalumu kuna rai mbili za Maimamu wawili miongoni wa Maimamu wa Madhehebu ya Shaafiiy waliokuja baada ya Imamu Shafi mwenyewe, na hapa rai hizo mbili huitwa “mielekeo miwili” (waj-haan).

Na iwapo jambo moja litakuwa na rai mbili kwenye Madhehebu basi maswali ya uhusiano kati ya hali hizo mbili huibuka, na hapa kuna aina mbili za uwezekano: wa kwanza- ni kwamba pawepo tofauti kubwa baina yao na hoja ya kila rai ya mmoja wao ina nguvu, lakini rai ya mmoja wao in nguvu na hoja zaidi kuliko ya mwengine, au panakuwapo rai mbili katika jambo moja maalumu na kwa kiwango cha nguvu za hoja kinachofanana kati ya pande mbili.

Na hapo ndipo zinapojitokeza hali nne katika mwonekano huu: ya kwanza -ni rai mbili zinazonasibishwa na Imamu husika, moja kati ya rai hizo ina nguvu na ya pili ina nguvu zaidi, au mojawapo ina nguvu na ya pili ni dhaifu, na rai mbili zinanasibishwa na waliyokuja baada ya Imamu huyo, au ni mielekeo miwili ya jambo moja ambalo kati ya mielekeo hiyo kuna nguvu, na mielekeo hiyo mmoja wao una nguvu na mwingine ni dhaifu. Na hapa ndipo unpaojitokeza mchango wa Elimu ya Istilaahi, ambako wanachuoni wameipa jina maalumu kila hali na ukawa msingi katika vitabu vyao.
Hali ya kwanza: maoni kwamba nguvu za kutofautiana katika kauli hizi huitwa “Wazi zaidi”; kwa maana kwamba kuna rai mbili za Imamu: moja kati ya rai hizo ina nguvu na nyengine ina nguvu zaidi, basi rai iliyo na nguvu zaidi wanaiita “Wazi zaidi”, ambapo nyengine huitwa “Kinyume cha iliyo wazi zaidi”.

Ama katika Hali ya pili, ambayo tofauti ndani yake inapungua; kwa maana kwamba kuna rai mbili zinazonasibishwa na Imamu husika: moja kati ya hizo ina nguvu na nyingine ni dhaifu, basi wao huiita rai yenye nguvu “Mashuhuri”, na rai nyingine iliyo kinyume cha mashuhuri ni dhaifu. Katika hali ya kuwepo mitazamo miwili kati yake ipo nguvu.

Hali ya tatu: mtazamo ulio na nguvu huitwa "Sahihi zaidi”. Na katika hali ya kuwepo mitazamo miwili, mmoja kati yake una nguvu na mwengine ni dhaifu, basi mtazamo ulio na nguvu huiitwa “Sahihi”.

Hii ina maana kuwa sisi tuna Istilaahi nne mbele yetu wanazozitumia katika maneno yao kuelezea hali fulani, na kuna nyingi nyingine. Imamu Al-Nawawi katika kitabu chake [Al-Minhaaj] mwanzoni mwake amewafundisha watu njia hii, na akasema kwamba mtu atasema kadhaa wakati kadhaa na atasema kadhaa wakati kadhaa, na akabainisha Istilaahi nyingi.

Kuna mwendelezo wa suala la Istilaahi maalumu, mwendelezo huu hauhusiani na –maneno tu – bali unahusiana na watu na vitabu. Kwa mfano, kama mwanachuoni mmoja wa Tafsiri ya Quraani tukufu akitaja jina la kubandikwa la “Kadhi” atakuwa anamuashiria Imamu Al-Baidhawi, ambapo wanachuoni wa Tafsiri ya Quraani wamezoea kumwita kwa jina hili, lakini kama likikutwa jina kama hilo katika elimu ya Akida (Elmu-Lkalam), basi hakika jina hili litakuwa linamuashiria Imamu Abu Bakr Al-Baqlani. Na iwapo kama wanachuoni wa madhehebu ya Fiqhi ya Imamu Shaafiy watalitaja jina hili basi wao watakuwa wanamkusudia Al-Kadhi Hussein wa madhehebu hayo hayo, wakati ambapo jina hilo hilo hukusudiwa Abu Yaala Al-Faraa kwa wanavyuoni wa madhehebu ya Imamu Ibn Hanbal.
Na hali hiyo hiyo hujitokeza kwa kutajwa jina la “Imamu”, linapotajwa katika vitabu vya fiqhi ya madhehebu ya Shaafiy basi hukusudiwa Imamu Al-Juwaini, wakati ambapo wafuasi wa Misingi ya Asili humkusudia kwa jina hilo, Imamu Al-Razi. Na kama pakitajwa “Al-Shaikhan” katika elimu ya hadithi basi hukusudiwa Imamu Bukhari na Muslim, lakini katika fiqhi ya madhehebu ya Shaafiy hukusudiwa Al-Rafii na Al-Nawawi kwa neno hilo hilo moja.

Elimu haikamiliki ila kwa kuvitambua vitu hivi kwa ajili ya kurasimisha marejeo, kuelewa hoja na kwa ajili ya kuyapanga maneno. Kwa mfano, kama utasoma kitabu cha fiqhi ya madhehebu ya Shaafiy na ukataka kurasimisha marejeo ya maneno yanayohusishwa na Al-Kadhi, basi unapaswa kujua ni nani anayekusudiwa kwa jina hilo la kubandikwa, hivyo basi, ili usije ukachanganya mambo: Je, utaelekea kwa yupi katika hawa? Al-Kadhi Al-Baidhawi au Al-Kadhi Hussein au Al-Kadhi Al-Faraa..? Na kwa upande wa Imamu je? Utaelekea kwa yupi kati ya hawa? Al-Juwaini au Al-Razi?

Kwa kuwa ni lazima kufahamu vizuri Istilaahi za watu tunalazimika vile vile kufahamu Istilaahi za vitabu. Neno “Al-Nihaya” kama likitajwa katika vitabu vya Shaafiy maana yake ni kitabu cha “Nihayatul Matlab fi Maarifatul Madhhab” cha ImamuAl-Juwaini, na kama watasema: “Al-Muharir” nacho ni kitabu cha Al-Rafii, hata kama kuna vitabu vingine katika Fiqhi hiyo hiyo vinavyoitwa Al-Muharir au Al-Nihaya, basi kinachokusudiwa katika hali zote hakibadiliki.

Na kama wakisema, “Al-Majmuu” basi hicho ni kitabu cha Imamu Al-Nawawi. Jambo lingine linahusiana na Istilaahi na ambalo tunaliona katika vitabu vya wanavyuoni waliokuja baadaye na madhehebu yao, nalo ni kuenea kwa kile kilichoitwa “uchongaji wa maneno”. Na neno “uchongaji” linatumika katika lugha kwa maana ya uundaji wa neno moja linalotokana na maneno mengi.

Kwa mfano tunaposema “KWA JINA, LA MWENYEZI MUNGU, MWINGI WA REHEMA, MWENYE KUREHEMU” tunatohoa ndani yake neno moja “Basmalah”, au tunaposema: “adaama –llaahu azzaka, (Mwenyezi Mungu akudumishie cheo chako)” tunatohoa neno moja ambalo ni “Dam-azah”, au tunatohoa kutoka katika maneno yafuatayo: “laa haulaa walaa quwwata illaa billaahi” (Hakuna hila wala uwezo isipokuwa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu) yanakuwa “Alhauqalah”, na mfano wa hayo. Na inasemekana kwamba uchongaji wa herufi unatokana na kusikia tu, maana kwamba haturuhusiwi kujichongea herufi ovyo, lakini pamekuwapo mazoea kwa baadhi ya watu kujichongea maneno, kwa mfano wanasema kwa yoyote aliyemaliza masomo yake katika kitivo cha “Darul Uluum” huitwa “Dar-amian” na kadhalika. Na hata katika lugha ya mitaani Wamisri wanasema: “Maalihish", na wakati neno hili limetoholewa kutokana na maneno ya: (maa alaihi shaiun) kwa maana "hana kitu chochote", kusudio hasa ni: “halaumiwi”.

Waandishi hawakusimama katika ukweli kwamba uchongaji wa herufi unatokana na kusikia, kupima au kuweka mipaka ya lugha, bali waliutumia uchongaji huo katika mwandiko pia, kutokana na kuandikwa sana katika vitabu, na watu kupendelea hivyo, kwahivyo ikawa imeenea katika uandishi wa fasihi na wakawa wakiandika neno “Hiinaidhin kwa kutumia herufi “H”, na wakaandika “Al-Dhahir kwa herufi hizi “Al-Dh”, na “Al-Musanif” kwa kifupi chake “Al-Mus”. Kama ukiangalia maandiko ya kale yaliyoandikwa kwa mikono, ukikuta “H”, basi ujue kwamba mtunzi anakusudia “Hinaidhin (na wakati huo)”. Na wanafunzi walipojikuta mbele ya uchongaji huu wa herufi, walikuwa wakizisoma kama zilivyo ili wasijekusahau maana yake, na uchongaji huu wa herufi ukawa unaenea kwa watu wa kawaida. Pia kuna baadhi ya maneno yaliyochongwa yamepotea, kwa hivyo basi, wakachelea wasije wakayapoteza yaliyobakia, na baadhi yao wakashindwa kuzielewa maana zake na kisha yakaanza kuchanganyika.

Pamoja na herufi hizo herufi “Haa” inayotajwa katika mapokeo ya hadithi kwa maana ya “Haadathani, yaani ameniambia”, na inatumika hapa kwa maana ya kubadilika kwa mapokeo, yaani ni ishara ya mwanzo wa mapokeo mapya ya hadithi yanayotofautiana na yaliyotangulia kabla yake.

Na Ibnu Al-Salaah anaelezea hayo kwa kirefu katika utangulizi wake, akisema kwamba: hakika wanavyuoni wameuboresha uchongaji huo wa herufi, na ukawa kwao kama ni elimu ya Istilaahi katika majina ya watu na vitabu, wakamwita Buhkari kwa kufupisha herufi “kh” na wakamwita Muslim kwa kifupi kwa kutumia herufi “M” na Ibn Majah “H” na Al-Bayhaqi “Heq”. Na katika kitabu cha “Al-Jaami Al-Sagheir” cha Al-Suyuti wakaashiria katika hadithi yenye sifa ya “Hasan, yaani nzuri” kwa kutumia herufi “H”, na kuhusu hadithi iliyo sahihi wanatumia “S” wakati ambapo hadithi ya mapokezi dhaifu wanatumia “Dh” kwa kifupi.

Pia wanachuoni hao waliutumia uchongaji pia katika majina ya watu. Mwandishi wa kitabu cha “Jaamiu Al-Fusulaini” cha madhehebu ya Abu Hanifa ameandika kurasa nyingi ili kuelezea herufi zinazohusu watu na vitabu. Wakati katika madhehebu ya Shaafiy tunakuta machapisho na matini nyingi zina herufi sawa na hizo, wakatumia ufupisho wa “Sim” ili kuashiria Ibn Al-Qasim Al-Abadi, na wakatumia “Haj alisema” wakimaanisha Ibn Hajar, na: “Mar” wakiashiria Mohamed Al-Ramliy, na: “Ram” wakiashiria AL-ShihabAl-Ramliy.

Kwa hivyo, ni lazima zieleweke herufi hizo na pia zisomwe kama zilivyo kulingana na makusudio yao, au laa sivyo tutapata mawazo ya kupotoshwa. Kwa mfano, kama mmoja wa wasomaji hakuelewa maneno ya, “Sim alisema”, na akaanza kufungamanisha baina ya maneno yaliyopokelewa katika matini ambayo: “amesema Sim” kwa kufungamanisha na sumu ambayo inauwa watu na kisha kupelekea pengo kubwa kati ya msomaji na kitabu au mwandishi wa kitabu hicho, jambo ambalo linadhihirisha unyeti mkubwa wa suala la Istilaahi.

Suala muhimu lifuatalo ni suala la Istilaahi, ni kwa yale yanayohusiana na uainishaji. Kwa hivyo, Istilaahi za kifiqhi ni hukumu za kisheria, nazo zina mchango wa kimsingi katika fiqhi ya Kiislamu. Waislamu wameshughulikia sana maana hizo, hivyo wameshughulikia sana elimu ya mantiki na wakaiita “mtumishi wa elimu”, ambapo waliifikiria ni kama mtumishi wa elimu nyingine za kisheria kwa sababu ya mchango wake katika suala la maana, pia kwa sababu suala la maana katika akili ya Mwislamu, na katika akili ya mwanasheria, na katika akili ya mwenye kujitahidi ni mkusanyiko wa hukumu za kisheria.

Wakati wowote maana hiyo inapotajwa kwa mwanachuoni humuwezesha kuainisha halali na haramu. Na kutokana na utukufu wa suala la kuainisha halali na haramu kama ni uamuzi wa Mola wa ulimwengu wote, - kama alivyoita Ibn Al-Qayyim –basi utukufu wa jambo hili umekuwa mkubwa mno.
Kwa kuwa mwanadamu humzungumzia Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi kuna haja ya kuwepo mwanachuoni mwenye tahadhari na uangalifu mkubwa. Na kwa ajili hiyo, maana hizo lazima ziwe na umakini mkubwa na udhibiti kwa kiasi kinachowezekana kutokana na uwezo wa mwanadamu. Na tunapaswa kutotoa chochote midomoni mwetu isipokuwa yanayotolewa na maamuzi ya kisheria.. Na kwa hivyo basi, maana ya riba, kuuza, Jihadi na mkopo n.k ni miongoni mwa hukumu za kisheria.

Pia watu wa kale walizoea kuandika matini katika pambizo, na kuandika kinachojulikana kama pambizo ndani ya jedwali, hivyo yaliyo nje ni kitabu pamoja na maelezo yake, na yaliyo ndani ni pambizo, kama vile pambizo ya Sheikh Al-qalyubiy, na pambizo ya Sheikh Amira. Kama tukisoma maneno yaliyo nje ya matini hii hii tutaona: “sehemu ya kuuza”: nayo ni kama kauli yake nimekuuzia kitu hiki kwa thamani hii, kisha mnunuaji akasema, nimekinunua kitu hiki kwa thamani hii, basi mauziano yatakuwa yamekamilika kati ya muuzaji na mnunuzi – na hali hizo zina masharti na mfumo wake yatakayofuatia baadaye –.”

Mwanzoni mwa karne ya ishirini, wanavyuoni walijaribu kutumia alama za uandishi, na Ahmed Zaki Pasha,wakati huo akijulikana kwa jina la shekhe wa Uarabu, alitunga kitabu kuhusu jambo hilo, kwa sababu alama za uandishi zina faida kubwa katika ufafanuzi wa maana iliyokusudiwa kupitia upangaji wa sentensi, jambo ambalo ni muhimu mno wakati tunaposoma au tunapochapisha vitabu hivi mara nyingine, kwa ajili ya kuondoa utata.

Tukamilishe matini: “inayotumika katika mkataba wa kuuziana,” tunakuta kwamba ameanza kwa masharti kama wanavyuoni wengine, kwa sababu ni muhimu zaidi, na kwa sababu ya kutokubaliana kwake, na amelielezea “sharti” kinyume na kuelezea kwake katika kitabu cha “Sharhu Al-Muhadhab” cha Al-Ghazali, na kitabu cha “Sharhu Al-Muhadhab” ambacho ni “Almajmuu” cha Al-Nawawi. Ambapo aliyaelezea maneno haya matatu kwa kutumia neno “nguzo”, na tumesema –hapo kabla - kwamba maneno haya: (“nguzo” na “masharti”) yanaungana kwa kuwa kwake ni sehemu ya kitu kimoja, lakini nguzo zinakuwa ndani na masharti yanakuwa nje.

Mwandishi aanza kufafanua matini: “nayo ni kauli yake” yaani kauli yake yeye -maana ya kuuza kwa upande wa maana ya kisheria- kama kwamba anasema: maana ya kuuza kwa upande wa sheria ni kama kauli yake: nimekuuzia kitu hiki kwa thamani hii. Na amemtambulisha kwa mfano wa tamko lake: “wewe” na kwa hivyo basi, maana hapa inathibitishwa kwa mfano. Na alisema, “na alimtambulisha kwa mfano pasi na mpaka.” Mpaka unaokusudiwa hapa ni mpaka wa kimantiki. Anaendelea kusema: “kwa sababu mfano huo ni wazi zaidi”, yaani kwa sababu mfano uko wazi zaidi ya mpaka huo.

Anaendelea kusema: “ishara ni kama kauli.” Hii ni maana mpya, na anakusudia uuzaji wa mtu ambaye hana uwezo wa kusema kwa mfano, kama vile bubu, naye huuza na hununua hadi akatimiza mahitaji yake ya kimaisha. Ishara anazozitowa bubu ni sawa na maneno, na hivyo zinachukua hukumu za maneno ya kawaida yanayoeleweka. Kwa kuwa mkataba wa mauziano unaweza kufanyika kwa maneno, basi pia unaweza kufanyika kwa ishara za bubu (ambazo zinachukua nafasi ya maneno). Na anasema: “Na ishara ni kama kauli, na njia nyingine zisizokuwa maneno ya kuuziana ni sawasawa na maneno ya kuuziana”– maana ya hayo ni kwamba maneno yasiyo ya kuuza yanayomaanisha kutimiza kuuza yanachukua hukumu zile zile za maneno ya kuuza. Tunaona kwamba hata kama tutakosea kuyasoma maneno hayo hatutafunga mlango wa kuyaelewa vyema.

Na kauli yake: “(nimekuuzia) kitendo hicho kinahusiana na mtu anayezungumzwa (nafsi ya pili) kwa ujumla, haitoshi kwa kuashiria hivyo kwa kutumia kiungo kimoja tu kama kichwa chake”; maana wakati unapotaka kuzungumza na mtu mwengine kuhusu kuuziana haiwezekani kuzungumza naye kwa misamiati inayowakilisha viungo vya binadamu, kwa kuashiria kwake, kama kauli yako: nimeuuzia mkono wako, au nimekiuzia kichwa chako. Anaendelea akisema:“kitendo hicho kinahusu mtu anayezungumzwa (nafsi ya pili) kwa ujumla, haitoshi kwa kiungo kimoja tu kama kichwa chake, iwapo atakusudiwa mtu mzima. – yaani maneno hayo hayaruhusiwi kutimiza mkataba wa mauzo, kwa ajili ya kuepusha mgongano kati ya watu, na kadhi atakuwa na wasiwasi kuhusu hukumu yake iwapo maneno kama hayo yatatumika. Anaendelea akisema: “Sheik wetu Al-Ramliy amependelea usahihi wa mkataba huo kwa kutumia nafsi (ili kutilia mkazo katika kauli)”. Maana ya hayo ni kwamba nafsi ni miongoni mwa maneno yanayotilia mkazo katika lugha, tunasema: mtu amekuja nafsi yake (yaani yeye mwenyewe), na kauli hiyo ni kauli ya Al-Ramliy.

Anaendelea kusema: “Na Sheikh wetu Al-Ziyadi” [anaashiria hapa kwa “Z” katika matini], “kwa usahihi wa mkataba huo kwa kutumia neno la mkono kwa nia ya mtu mzima, basi akimpinga”. Kitendo “akimpinga” kinamaanisha kwamba mwandishi anampinga Sheikh Al-Ziyadi katika kauli hiyo.
“Wala haitoshi kumkusudia mtu mwengine asiyehusika na mkataba wala haiwezekani kumwashiria mtu mwengine pia” - yaani, haitoshi katika mkataba huo kuzungumza na mtu mwengine asiyehusika na mkataba huo, na wala haiwezikani kumwashiria mtu mwengine pia, kama kwamba muuzaji anakaa na anazungumza na mtu mmoja japokuwa anamkusudia mwengine, hapa anataka kuonesha tukio litakalowajulisha mashahidi kuwa lengo lake ni kuhifadhi mali ya watu na kwa mujibu wa ugomvi kati ya viumbe vya Mwenyezi Mungu, kwa hivyo hukumu zote zimepangika kutokana na akili ya mwanachuoni wa Fiqhi, naye anataka kutekeleza hukumu hizo ili azilinde haki za Mwenyezi Mungu na haki za viumbe wake.

Anaendelea kusema: “haitoshi kumkusudia kwa maneno asiye na akili, wala haitoshi kumwashiria mtu mwengine, wala kumkusudia mwengine kwa jina la wazi”. Hii inaashiria kwamba akusudie mtu mwengine asiyehusika na mkataba kwa jina lingine, vile vile wala kuegemeza kwa asiyezungumza naye, kama vile, aseme “nimemuuzia mwakilishi wako” au “Mwenyezi Mungu amekuuzia.”Kupitia uchunguzi huu, wanavyuoni walitaka kuepuka matumizi mabaya ya mikataba, ambayo baadhi ya watu wanaweza kuyafanya, basi ni lazima mkataba uainishwe kwa ajili ya kuepuka kila aina ya migogoro au kutofahamu vizuri, ambapo mmiliki hawezi kuwa peke yake katika mkataba huo kinyume na mikataba mingine inayofanana na mkataba wa kumwacha huru mtumwa.

Na hapa tunafikia mwisho wa safari yetu ambayo pevu. Katika safari hii tuliivaa akili ya Mwislamu wa zamani, na tumeona ndani yake falsafa na sehemu za juhudi na mihangaiko yake mikali kwa ajili ya kutumikia Quraani, Sunna na Dini, na kuendelea kwake, na aliyekuja akaendeleza juhudi za aliyemtangulia kwa kujali na kuheshimu kwa upande mmoja, na kwa kukosoa na kufanya marejeo na kurekebisha, kukamilisha na kupunguza kwa upande wa pili, na kuendelea na mwelekeo wa kupambana na mwingine katika mawazo na misingi yake, kwa hekima na mazungumzo ambayo yamefuata nguzo zote na masharti kama tuitavyo: “Utaalamu” na “Utafiti wa kitaalamu” na “mfumo wa kitaalamu”.

Tufanye hivi labda Mwenyezi Mungu ataujaalia urithi huu kwa kumleta anayeuthamini vizuri, na atakayefanya jitihada na kuyatumia mawazo yake, ili Uislamu usimame kama unavyotakiwa kusimama, na Ustaarabu wa Kiislamu urejeshe elimu zake, maadili yake, ubora wake na uzuri wake tena. .

Chanzo: “Atwariyqu Ilaa Fahmi Turaathi’, Mufti wa Misri, Profesa Ali Juma.

Share this:

Related Fatwas