Ulezi wa Yatima ambaye Nasaba yake ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Ulezi wa Yatima ambaye Nasaba yake Haijulikani.

Question

Je, inajuzu kwa familia kuwalea watoto wasiojulikana nasaba zao kama vile inavyojuzu kuwalea mayatima wanaofahamika nasaba zao? Na je, thawabu zake ni kama za kumlea mtoto yatima?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Iwapo familia itabeba jukumu la kumlea mtoto yatima mwenye nasaba inayojulikana na hana mlezi, au mtoto ambaye nasaba yake haijulikani ili akuwe katika familia hiyo, apate malezi yake na kuhudumiwa kama mmoja wa watoto wa familia hiyo, kama ni kuziba pengo la yale aliyoyakosa mtoto huyu kama vile mazingira ya familia, basi hii inazingatiwa kuwa ni kazi nzuri ya kujitolea na inalenga kuwawekea watoto mazingira bora waliyoyakosa kutoka familia zao, kwa ajili ya kuwalinda wasipotee, na ni kazi ya kuwafanya wawe waja wema katika jamii zao na kuinufaisha.

Katika hadithi tukufu aliyoipokea Imamu Muslim katika sahihi yake na Tirmidhiy kutoka kwa Abu Hurayra, Mtume saw alisema : “Mlezi wa yatima au mtoto mwengine basi mimi na yeye tutakuwa kama hivi peponi.” Aliashiria kwa vidole vyake viwili, cha shahada na cha kati.

Na yatima ni yule ambaye baba yake amekufa ilhali ni mtoto mdogo hajabaleghe, basi yeye ni yatima hadi abaleghe, akibaleghe tu basi sifa ya uyatima inaondoka.

Na sababu ya kuhimiza ulezi wa mtoto yatima ni kwa kuwa hana baba. Na wataalamu wa mambo ya Imani, katika maneno yao wamesema kuwa njia ya Imani miongoni mwa njia za sababu, kwamba miongoni mwa aina za Imani ni kuambatanisha hukumu ya kitu na sifa inayoenda na kitu hicho. Daima ukarimu unanasibiana na elimu, na upuuzi unanasibiana na ujinga. Inajulikana kwamba wenye akili hupangilia hukumu kwa mambo mnasaba, na sheria ya Kiislamu haitoki nje ya vitendo vya wenye akili. Na imezoeleka kuwa sheria inazingatia minasaba bila ya kuipuuza. Na iwapo mtu anafuatanisha hukumu katika tamko lake kwa sifa inayofaa basi ni aghalabu ya dhana hapo ni kuizingatia hukumu hiyo. [Rejea: Sharh Al Kawakeb Al Muneer Li Al Fatuhiy Uk, 515, Ch. Matbaat Al Sunnah Al Muhamadiyah]

Yakithibitika haya basi tunasema: Ikiwa sababu ya kumlea yatima ni kutokuwa na baba, basi sababu hii ipo pia kwa yule ambaye nasaba yake haijulikani kwa kuwa anaathirika zaidi kinafsi na katika mambo ya maisha ambayo yanahitaji uangalizi wa hali ya juu, kwani yatima baba yake anajulikana na hapati aibu kwa kufariki baba yake, na pia ana familia na jamaa ambao wanaweza wakaja kumshughulikia siku yoyote.

Ama ambaye nasaba yake haijulikani, yuko hatarini kutengwa na jamii, kwa kuwa hana baba wala ndugu wa karibu wanaosubiriwa kumshughulikia au kumwulizia, na wala hana hata jamaa mwenye uhusiano naye. Maana ya asili ya kilugha ya neno “yatima” inamgusa mtoto ambaye nasaba yake haijulikani –nayo ni upweke– maana ambayo inakusanya maana maalumu ya neno “yatima” kwa mwanadamu -nayo ni kutokuwa na baba– lakini pia yeye hana familia wala ndugu wala watu wa karibu wa ukoo. Kwa mantiki hiyo, mtoto ambaye nasaba yake haijulikani anaingia katika maana ya yatima kisheria, kwa kuwa hana baba na hana hata ndugu. Kwa hivyo, kumlea mtoto huyu ni katika mambo ya fadhila ambayo Mtume saw ameyahimiza, na mwenye kuyafanya anapata malipo makubwa.

Kutokana na hayo; hakika ulezi wa yatima ambaye nasaba yake haijulikani ni jambo lenye kupendeza kisheria, na atakayefanya hivyo atapata thawabu za kumlea yatima, na kwa kuwa yeye hana ndugu kabisa, basi mwenye kumlea atapata thawabu za ziada.
Na Mwenyezi Munga Mtukufu ni mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas