Haki na Uchungaji Wake

Egypt's Dar Al-Ifta

Haki na Uchungaji Wake

Question

Ni njia gani iliyo sawa ya kufuatwa na muislamu wa sasa ya kuchunga haki, na hasa haki za wazazi wawili na ukoo?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Dini ya Kiisilamu ni Dini yenye uongofu uliokamilika, imeweka uhusiano madhubuti kati ya mja na Mola wake, uhusiano kati ya binadamu na binadamu mwenzake na pia imeweka uhusiano kati ya mtu na mazingira aliyoumbiwa, ni sawa ayaone au asiyaone.
Na mipaka kati ya mtu na mwingine hutafautiana kwa kutafautiana aina ya mtu, na nafasi ya ukaribu wa kiukoo, ukaribu wa kimaeneo, utafauti wa umri, kizazi na elimu.
Wenye haki katika wanadamu ni wengi wakiongozwa na wazazi wawili, kisha ndugu wa nasaba. Na mazungumzo yetu tutazungumzia kuhusu masuala wawili ili muda usiwe mrefu.
Kwanza: Wema kwa wazazi wawili: Watu wenye haki kubwa sana kwa mtu ni wazazi wake wawili, kwa mwenye akili haifichikani kuwa wazazi wana nafasi ya pekee isiyosemekana, na hata kama itaandikwa kuhusu wazazi basi kalamu haitaweza kuandika fadhila nyingi kuhusu wazazi, na itawezaje kuandika hali ya kuwa wazazi hawa ndio sababu ya kuwepo kwao ulimwenguni na ni nguzo ya maisha yao?
Wazazi wametumia kila aina ya nguvu, ni sawa ziwe za kimwili au kiroho kwa ajili ya kuwalea watoto wao, na kuvumilia matatizo na mashaka ya aina mbali mbali, kitu ambacho hakivumiliki kwa mtu mwengine yeyote isipokuwa wazazi.
Kwa ajili hiyo, Uislamu ukawapa wazazi cheo kitukufu kinachostahiki shukrani. Na kukiri upendo ni jambo la lazima. Na kufaradhishia watoto juu ya kuwatendea haki wazazi wawili ni jambo ambalo Mwenyezi mungu mtukufu hakuwajibisha kwa yeyote isipokuwa kwa wazazi wawili, kiasi ambacho hata Mwenyezi Mungu amelinganisha utiifu wao na wema kwao ni sawa na ibada yake (Mwenyezi Mungu) na kumpwekesha yeye, akasema: {Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzeeni, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na useme nao kwa msemo wa hishima.} (AL ISRAA. 23). Kwa ajili hii Mwenyezi Mungu ameidhinisha utiifu kwao ni katika mambo yamuwekayo mja karibu sana naye (Mwenyezi Mungu) na kuacha kuwatii ni katika makosa makubwa sana baada ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu.
Wanachuoni wa kiislamu na mfasiri wa Quraani tukufu Abdallah bin Abbas (R.A) anasema: “Aya tatu zinakwenda sambamba na Aya tatu zingine, mojawapo haikubaliwi pasina kuwepo nyingine; {Na mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume. Mkigeuka, basi hakika ni juu ya Mtume wetu ni kufikisha (Ujumbe wake) kwa uwazi tu.} [ATAGHAABUN.12]. Yeyote atakamtii Mwenyezi Mungu na kuacha kumtii Mtume (S.A.W) basi hatakubaliwa. {Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na inameni pamoja na wanao inama}. [AL- BAQARAH. 43]. Anayesali bila ya kutoa zaka basi sala yake haikubaliwi. {Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio}. [LUQMAAN: 14) Anayemshukuru Mwenyezi Mungu na kuacha kuwashukuru wazazi wake basi hakubaliwi.
Na kwa ajili hiyo Quraani imetaja mara kwa mara kuwatendea wema na hisani na kuhadharisha tabia ya kuwatupa mkono na kuwafanyia ubaya kwa namna yoyote. Mwenyezi Mungu anasema: {Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na waliomilikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanaojifakharisha} [AN NISAA: 36) na akasema: {Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwatii. Kwangu Mimi ndio marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda}. [AL ANKABUUT: 8) na akasema pia {Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Na kwangu Mimi ndiyo marudio} [LUQMAAN: 14].
Ama kwa upande wa hadithi za Mtume (S.A.W) nazo zimesisitiza ulazima wa kuwatii na kukataza kuwatendea ubaya, kwa mfano, Mtume (S.A.W) anasema: “Radhi za Mwenyezi Mungu zipo katika kuridhia wazazi wawili, na hasira zake zipo katika hasira zao (wazazi wawili)” [Bayhaqi].
Imepokewa na Amru bin Al-As amesema: Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (S.A.W) akasema nimekuja kukuunga mkono kuhusu Hijra na nimeaacha wazazi wangu wanalia, Mtume (S.A.W) akamwambia: “Rudi kwao, na ukawafurahishe kama ulivyowaliza”. [Abu Daudi].
Kutoka kwa Muawiya bin Jahima Asalami: Kuwa alimuomba Mtume (S.A.W) kushiriki naye katika jihadi. Mtume akamuamrisha arudi na kuwafanyia wema wazazi wake, na Muawiya aliposhikilia kuwa anataka kushiriki katika jihadi, Mtume (A.S.W) akamwambia “ole wako, kuwa na mzazi wako kisha tena utaipata pepo” [Ibn Majah].
Na sheria imemuita mtoto kama ni chumo la mzazi wake, imepokewa kutoka kwa Mtume (S.A.W) amesema: “Hakika chumo bora ni lile achumalo mtu kwa mikono yake, na hakika mtoto wake ni katika chumo lake.” (Nisai) ana akasema “Hakika watoto wenu ni katika chumo lenu, basi kuleni kutoka katika machumo ya watoto wenu.” [Daudi].
Na pia masahaba na waliowafuata baada yao walielewa vyema jambo hili, kutoka kwa Ataa amesema, nilimwambia: “Mama yangu ameapa kwa kunikataza nisisali sala yoyote ya Sunna (nikishamaliza kusali sala za lazima) na wala nisifunge isipokuwa funga za lazima kwa ajili ya kunionea huruma.” Akasema: Timiza kiapo chake. [Ibn Shayba].
Na Sheikh Dardir anasema katika kitabu cha; [Sharhu Swaghir]. “Lazima kuwatii wazazi wawili, hata kama ni washirikina na waovu kwa matendo au wanatamka maneno mabaya, na wema wao ni kwa kusema nao kwa upole na kwa mapenzi, kwa kuwaambia mambo mema yanayohusu dini na yenye manufaa nao katika dunia na akhera bila ya kuwainulia sauti, na kama ni kipofu -hata kama ni kafiri- ampeleke kanisani na kumbebea akihitajiacho na kumtimizia akitakacho katika sherehe zao… mpaka akasema: “ wazazi wawili hufanyiwa utiifu hata katika mambo yenye kuchukiza. [Hashiyatu Swawiy ala Sherhi Swaghiyr, 4/ 739-740.
Wema kwa wazazi huwa kwa maneno mazuri yenye kuonesha upendo na mapenzi nakujiepusha na maneno makali yenye kuwakasirisha, na kuwaita kwa unyenyekevu kwa mfano “Ewe mama.. ewe baba,” na kuwaambia yenye manufaa nao katika dunia na akhera na kuwafundisha yenye kuwafaa na wanayoyahitaji katika mambo ya dunia, kuishi nao kwa wema, na kuwatendea kila linalokubalika kisheria, kuwatii kwa yote wakuamrishayo katika mambo ya lazima na yenye kupendeza, na kuacha yasiyofaa kisheria, na wala haitakikani kuwaacha mbali wakati mutembeapo, sembuse kuwatangulia (masafa marefu), isipokuwa kwa dharura. Na kama utaingia walipo basi huruhusiki kukaa isipokuwa kwa ruhusa yao, na ukaapo huruhusiki kusimama isipokuwa kwa ruhusa yao. Na ikitokezea kufanya haja (kwa sababu ya utu uzima walionao au ugonjwa) basi hutakikani kuonesha ishara ya kuwa ni uchafu kwa kuwa hilo litawauma sana. Kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu anasema {Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na waliomilikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifaharisha,} [AN NISAA: 36]. Ibn Abass amesema: Mwenyezi Mungu amekusudia kuwafanyia upole na kuwa laini kwao na wala kusiwe na ugumu na wala kuwaangalia kwa jicho kali na hata kunyanyua sauti.
Na miongoni mwa wema kwao: Ni kuwa usiwatusi na kuwakera na kuwaudhi kwa aina yoyote ile, kwani kufanya hivyo ni katika makosa makubwa yasiyo na shaka.
Imepokewa na Muslim kutoka kwa Abdallah bin Amru kuwa Mtume (S.A.W) amesema “Hakika ya madhambi makubwa sana ni mtu kumtusi mzazi wake.” Wakasema: “ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu je inawezekana mtu kumtusi mzazi wake?” akasema: “Ndio, mtu anamtusi mzazi wa mwenziwe na yeye anamtusi baba yake (Anamrudishia tusi) na anamtusi mama (Wa mwenziwe) na yeye anamtusi mama yake (Anamrudishia tusi). [Muslim].
Na katika mapokezi mengine. “Hakika katika madhambi makubwa ni mtu kumlaani mzazi wake” ikasemwa: "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, iweje mtu kumlaani mzazi wake? Akasema: “Kumtusi baba wa mtu naye (Huyo mtu aliyetusiwa baba yake) anamtusi baba yake (Mtukanaji). [Bukhari]
Na miongoni mwa wema kwao ni: Kuunga ukoo wa wazazi, imepokewa kutoka kwa Ibn Umar amesema: Nimemsikia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) akisema: “Hakika katika wema mkubwa sana ni kuunga ukoo wa familia ya wazazi baada ya kutoweka.” Pindi wakitoweka au kufariki basi atawahifadhi familia ya wazazi na kuwafanyia wema kwani ni katika mambo yatakiwayo. Abu Usayd amepokea –Miongoni mwa walioshuhudia vita ya Badri- Amesema: “Nilikuwa nimekaa na Mtume (S.A.W), akaja kijana katika Maanswari akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wazazi wangu wamekwishafariki, je kuna kitu ninaweza kuwafanyia ili kiwe ni wema kwao?” Mtume akasema: “Ndio, wasalie, waombee msamaha, nakutekeleza ahadi zao, kuwakirimu watu wao, kuunga familia kwa yule ambaye ameacha watu wake, haya ndio yaliyobakia kwako.” (Abu Daudi). Na Mtume (S.A.W) alikuwa akitoa sadaka kwa ajili ya Bi. Khadija mke wake kama kumfanyia wema, sembuse kwa wazazi wawili?!
Na maelezo haya yote ya kisheria yanahimiza umuhimu wa kuwatendea wema wazazi wawili, kuwatii na kuunga familia, na vilevile zinasisitiza kuwa jambo hili ni kubwa sana na lina nafasi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na hii ina maana kuwa linahitaji kupewa nafasi kubwa.
Na sisi tunakumbusha juu ya ukubwa wa jambo hili na uwepo wa haki kwa wazazi wawili na kuunga familia (ukoo) ili kheri ienee katika jamii ya kiisilamu, na inatosha kuwa wema kwa wazazi wawili ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kuwakasirisha ni kupata hasira zake pia.tunamuomba Mwenyezi Mungu mtukufu atuongoze katika njia iliyonyooka na atusamehe na waislamu wote.
Na sasa tunazungumzia suala jingine linahusu haki kwa wanadamu nalo ni kuunga ukoo.
Pili: Kuunga Ukoo (Jamaa): Kuunga ukoo ni nguzo muhimu sana miongoni mwa nguzo katika dini ya kiislamu, nayo ni tabia njema aliyoihimiza Mwenyezi Mungu ndani ya kitabu chake na kwa kupitia pia ulimi wa Mtume wake (S.A.W).
Waarabu kabla ya uislamu walikuwa wakitilia mkazo sana uungaji Ukoo, na ulipokuja uislamu ukalikubali jambo hili, na wala haukukanusha isipokuwa kwa yale mambo ya chuki za kijinga, lakini hakika walilitilia mkazo sana jambo hili, kwani kuunga Ukoo na kuwa karibu ilikuwa ni kama kuinusuru na kuweka upendo wa karibu na kuukinga na kusambaratika na udhalili na kutotaka mgeni kuweza kuwatawala na kuwakandamiza.
Kwa ajili hiyo, waarabu walihifadhi koo zao ili kumzuia adui asiweze kuwatawala na kujikinga na makero yao, mpaka ukaribu (upendo) ukafikia kuwapa ushindi wa kuwa pamoja na kuweza kuhukumu juu ya adui aliyetaka kuwadunisha.
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu Nabii Lut (R.A) alisikitika pale watu wake walipoacha kumsaidia akasema kuwaambia watu wake {Akasema: Laiti ningeli kuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu!} (HUUD. 80) akikusudia watu wake. Imepokewa na Abu Salama kutoka kwa Abu Hurayra (R.A) amesema: "Hakika Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema: “Mwenyezi Mungu amrehemu Nabii Luti, kwani alikuwa akitegemea nguzo iliyo madhubuti yaani Mwenyezi Mungu." [Bukhari na Muslim]
Kuunga ukoo ni lazima (Wajibu) na kukata ni katika mambo yaliyoharamishwa, Mwenyezi Mungu anasema {Basi yanayo tarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na mwatupe jamaa zenu? 23. Hao ndio Mwenyezi Mungu alio walaani, na akawatiauziwi, na akawapofoa macho yao.} [MUHAMMAD. 22-23]. Na akasema (S.A.W) kuhusu kauli hii, “Je huridhii kuunga waliokuunga na kuwatupa waliokutupa? Akasema: “Ndio, akasema: “Hivyo ndivyo itakiwavyo. [Bukhari na Muslim]. Na akasema (S.A.W)” Wafanyieni wema jamaa zenu hata kwa salamu.” [Bayhaqi].
Na katika yajulikanayo miongoni mwa sifa za bwana Mtume (S.A.W) ni kuwa alikuwa akiamrisha kuunga jamaa, na kwa hili kuna Hadithi nyingi sana, ila tutazitaja baadhi tu. Mtume (S.A.W) anasema: “Mwenyezi Mungu anasema” Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, na Mimi ndiye mwenye kurehemu, na rehema imetokana na jina miongoni mwa Majina Yangu, mwenye kuiunga basi Nami nitamuunga, na mwenye kuikata Nami nitamkata.” (Abi Daudi).
Na kutoka kwa Aisha (R.A) amesema: Amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W): “Ukoo umetundikwa kwenye arshi ya Mwenyezi Mungu, inasema: “Mwenye kuniunga basi naye ataungwa na Mwenyezi Mungu, na mwenye kunikata naye atakatwa na Mwenyezi Mungu.” [Muslim].
Na kutoka kwa Abdillah Bin Salama amesema, Mtume baada ya kufika Madina watu walikusanyika kwa kumpokea kwa shangwe, na nikamuangalia usoni nikaelewa kuwa si muongo, na kitu cha kwanza nilichomsikia ni: Enyi watu, toleaneni salamu, ungeni jamaa, na lisheni chakula na salini usiku hali ya kuwa watu wamelala.” ]Ibn Majah].
Na mtunzi wa kitabu cha: [Durar Ahkaam] “Kuunga jama ni wajibu hata kwa salamu, maamkizi na kwa zawadi, nao ni msaada na wema kwa walio karibu na kukaa nao na kuzungumza nao pia kuwatembelea. Jambo hili huzidisha upendo na hasa ikiwa utawatembelea kila Ijumaa au kila mwezi, na kwa koo zote ziwe kama mkono mmoja katika kusaidiana na kuwa pamoja na wale walio kinyume nao katika kuonesha haki na si katika mambo yachukizayo, na wala haitakikani kuikataa zawadi itokayo katika upande mwingine kwani husababisha mtengano.” [Durar Hukaam Sherh Ghurar Ahkaam.1/323].
Kukata jamaa ni haramu kwa tamko moja la wanazuoni, Mwenyezi Mungu anasema: {Wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada yakwisha ifunga, na wakayakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; Hao ndio wenye khasara.} (AL BAQARAH. 27). Na aliposema: {Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga, na wanakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya ufisadi katika nchi: Hao ndio watakao pata laana, na watapata nyumba mbaya.} (ARAAD: 25). Na ibn Hajar Alhaythamiy –Madhehebu ya Imam Shafi- Ameweka wazi yale yanayosababisha ukataji wa ukoo na mtunzi wa kitabu cha [Tahdhib Al Furuuq] –Madhehebu ya Imam Malik- Amekubaliana naye. Imepokewa kutoka kwa Imam Ibn Hajar kuwa kuna rai mbili, ya kwanza; hujulikana kuwa ni uovu juu ya jamaa, na ya pili: Ni hupelekea kuacha wema, mtu aliyebaleghe akiacha kuunga jamaa na kuwatendea wema bila ya udhuru wa kisheria hujulikana kuwa ameitendea uasi familia (ameikata), na baadhi ya wasomi huona hili kuwa ni katika madhambi makubwa, kama ilivyotangulia.
Ama udhuru wa kuacha kuwatembelea wanafamilia unatafautiana kutokana na aina ya familia, kuna vidhibiti vimewekwa na Imamu Shafi na Imamu Malik kama ule udhuru wa kutohudhuria sala ya Ijumaa, ingawa hali zote hizo ni za lazima na kuziacha ni katika makosa makubwa, ikiwa katika kuunga familia kunahitajika kutumia mali na hakuweza kutumia kwa sababu ya haja kubwa aliyonayo ya mali hizo basi huu hujulikana kuwa ni udhuru wa kisheria.
Na kuandikiana, iwapo hakuna muaminifu katika kuandikiana barua, pia hujulikana kuwa ni udhuru, na katika udhuru aliousema Imamu Malik ni kule kuwa na jeuri mwanafamillia aliye tajiri kwa mwanafamilia aliye masikini.
Kuunga jamaa ni wajibu hata kama ni mtu muovu- kama ilivyoelezwa katika [Fatawa Asabakiy]. Haki yake haianguki kwa uovu wake, na Mtume (S.A.W) anasema: “Si katika anayeunga jamaa yule anayehitaji malipo, lakini anayeunga jamaa ni yule ambaye hata wakimkata basi yeye huunga.” [Bukhariy]. Na Hadithi hii inasisitiza wajibu wa kumuunga hata kama mtu ni muovu. Kwani kukata undugu ni katika uovu na uovu umekatazwa kisheria. Pia Mtume (S.A.W) alimwambia aliyesema: “Mama yangu amekuja naye ni katika wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu je nimuunge? Akasema: “Ndio, muunge mama yako.”
Na jambo hilo pia ni wajibu hata kwa wasio waislamu na linatakikana kisheria kama vile kuwatendea wema wazazi wawili. Mtu hana budi kuunga ukoo kwa wasio waislamu hata kama ni watu wake wa mbali, kwani uungaji ukoo ni katika maadili mema ambayo yameletwa na sheria tukufu, na ni jambo lenye kuingia akilini mwa kila mtu, nayo ni tabia murua, Mtume (S.A.W) anasema: “Hakika nimetumwa kuja kutimiza maadili mema.” (Ahmad). Tukaelewa kuwa jambo hili ni haki kwa muisilamu na asiye muislamu.
Na Mtume (S.A.W) ametuma Makka dinari mia tano wakati wa ukame, na akaamrisha apewe Abu Sufiyan bin Harb na Sufwan bin Umayah ili wawape mafakiri wa Makka, Abu Sufiyani akakubali na Abu Swafwan akasema: “Muhammad amefanya hivi ili kuwahadaa vijana wetu.” [Sherhi sayri kabiir]
Jamaa ni tofauti na hawako katika ngazi moja, kuna wazazi wawili, ndugu, wajomba na mashangazi, na watoto wao, na Imamu Shafi ameeleza kuwa ngazi za ujamaa hutofautiana kutokana na ukaribu. Kwa upande wa wazazi wawili kuna msisitizo zaidi, na si katika kuunga iwapo utamuunga aliyekuunga, hii itajulikana kama kwamba unalipa, lakini kuwaunga hata kama wanakutenga. Nayo ni kama alivyosema Mtume (S.A.W) “Si katika anayeunga jamaa yule anayehitaji malipo, lakini anayeunga jamaa ni yule ambaye hata wakimkata basi yeye huunga.” (Bukhariy) Na mambo mengi hupelekea kuunga ujamaa mfano:- Kutembeleana, kusaidiana, kusalimiana, kama alivyosema (S.A.W) Wafanyieni wema jamaa zenu hata kwa salamu.” (Bayhaqiy) Na salamu pekee haitoshi kwa mtazamo wa Abi Khutab, na kama kuunga kunapatikana kwa kuandikiana iwapo wahapo karibu na hili limeelezwa na Imam Hanafi, Maliki na Shafii. Na hili si kwa wazazi wawili kwani wao wakikuhitajia uende basi ni lazima uende. Pia kutumia mali kwa ajili ya jamaa, kwani hilo huzingatiwa kuwa ni miongoni mwa kuunga jamaa, kama alivyosema Mtume (S.A.W) “Kutoa sadaka kwa masikini ni sadaka (moja), na kutoa kwa jamaa ni ni sadaka mbili, ni sadaka na kuunga ukoo. (Tirmidhiy) Na kwa mtazamo wa Imamu Shafii na Hanafi ni kuwa, kwa mtu tajiri haitohesabika kuwa anaunga undugu iwapo atatuma mali tu na kuacha kwenda kumtembelea jamaa yake iwapo ni masikini. Na uungaji ukoo unaingia katika aina zote za wema.
Na katika kuunga ukoo kuna faida nyingi nzuri. Na Hadithi za Mtume (S.A.W) zimeelezea umuhimu wake akasema: “Anayetaka riziki zake au ambariki katika athari zake basi na aunge ukoo wake.” (Bukahariy na Muslim)
Na katika faida walizozitaja wasomi wa dini (R.A). Ni kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha kuunga ukoo ili furaha ipatikane na kuongezeka kwa utulivu na kupata malipo mema baada ya kifo, kwani wanafamilia huombeana baada ya mmoja wao kufariki na kumtaja kwa wema.
Na sheria imefanya kuwa ni jambo la kupendeza kutembelea jamaa hasa katika siku za sherehe na kulifanya jambo hilo kuwa ni katika ibada. Imetajwa katika kitabu cha imam Nawawiy “Almajmuu`” kuwa jambo hilo ni katika Sunna za sikukuu ya Iddi akasema: “Inapendeza kuwatembelea watu wema na wenye kheri, jamaa na ndugu na majirani na kuwatendea wema na kuwakirimu pia kuwaunga, na inatakikana matembezi yawe kwa mujibu wa hali inavyoruhusu, na Hadithi zenye kuelezea hili ziko nyingi. [Al Majmuu` Sherh Muhadhab 4/478-479].
Na katika matunda ya kuunga undugu kati ya waislamu ni kupatikana kwa nguvu, uimara wa kijamii, ukaribu na upendo, kila mtu atakuwa na imani thabiti hapatakuwa na khiyana na wote watasimama kama kwamba ni mtu mmoja katika kupambana na maovu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuwafikishe, mwisho wa neno letu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu.
Chanzo: kitabu cha “Simat Al asri”. Mwandishi: Mufti wa Misri. Prof. Ali Juma.

Share this:

Related Fatwas