Kukusanya Swala kwa Sababu ya Mazin...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kukusanya Swala kwa Sababu ya Mazingira ya Kazi na Eneo

Question

Mmoja wa ndugu zangu anafanya kazi ya kuendesha trekta katika eneo la Tundra (eneo ambalo hufuatia eneo la ncha ya kaskazini (Arctic)) na hakuna katika eneo hili uwezekano wowote ule wa kusali kwani nyakati zote kuna matope na unyevunyevu. Sasa anauliza, je, inafaa kusali hali ya kuwa amekaa kitako ndani ya trekta? Na je, inafaa kukusanya Swala?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Masahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Swala ni nguzo katika nguzo za Uislamu, na nafasi yake kwa upande wa imani ni kama kichwa kwenye mwili, na Uislamu umeisisitizia katika Kitabu chake na kuijali ipasavyo na pia kuitilia mkazo mkubwa wa kuwa itekelezwe na isaliwe kwa nyakati zake maalumu. Mwenyezi Mungu anasema: {kwani hakika Swala kwa waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu } [AN NISAA: 103]. Na imetahadharishwa sana kutoiacha. Imepokewa kutoka kwa Ibn Umar –radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie –kuwa Mtume – rehma na amani zimshukie– amesema: "Uislamu umejengwa kwa nguzo tano: Kushuhudia kuwa hapana Mola mwingine apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, kusimamisha Swala tano, kutoa Zaka, kuhiji Makkah na kufunga mwezi wa Ramadhani".
Na Uislamu umesisitiza na kuwataka waislamu kuzihifadhi Swala tano wawapo kazini au safirini, katika hali ya hofu au ya amani, katika hali ya utulivu au vita na hata katika sehemu zenye usumbufu na wakati wa hofu kubwa ya kivita ambapo waislamu huwa mbele ya maadui zao. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Angalieni Swala, na hasa Swala ya katikati, na simameni kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. * Na kama mkiwa na hofu basi (salini) mkitembea au mmepanda (wanyama); na mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyowafunzeni yale mliyokuwa hamyajui.} [AL BAQARAH: 238-239] Kwa maana; Salini katika hali ya hofu na ya vita, mkiwa katika mwendo au vipando kwa namna yeyote muwezayo bila ya kurukuu au kusujudu lakini inatosha ishara na bila ya kushurutisha kuelekea kibla. Mwenyezi Mungu anasema: {Na mashariki na magharibi ni ya Mwenyezi Mungu, basi mahali popote mgeukiapo ndipo (mtaukuta) mwelekeo wa Mwenyezi Mumgu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.} [AL BAQARAH:115]
Na sheria inakubali kukusanya Swala utokeapo udhuru, utaswali Swala ya Adhuhuri pamoja na ya Alasiri, kwa kutanguliza au kuchelewesha, na Swala ya Magharibi utaswali pamoja na Swala ya Isha kwa sharti ya kunuia kufanya hivyo kabla ya kuingia wakati wa Alasiri au wa Isha. Na miongoni mwa nyudhuru ni huo udhuru wa matope, kwa kukisia (kulinganisha na) safari ambayo ina usumbufu (mashaka) katika hali zote hizo mbili. Imamu Bukhari na Muslim wameitoa Hadithi kutoka kwa Anas – radha za Mwenyezi Mungu zimshukie – amesema: Mtume –rehma na amani zimshukie – alipokuwa akisafiri, kabla ya kupetuka kwa jua, mwisho wa wakati wa Adhuhuri kuelekea wakati wa Alasiri, huteremka na kukusanya Swala hizo. Na Hadithi aliyoitoa Muslim kutoka kwa Muadh –radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie– amesema: "Tulitoka pamoja na Mtume –rehma na amani zimshukie – katika vita ya Tabuk, na alikuwa akisali Swala ya Adhuhuri na Alasiri pamoja, na akisali Swala ya Magharibi na Isha pamoja".
Imamu Nawawiy anasema katika kitabu cha: [Al majmuu 4/383, chapa, Dar Al fikr]: Ar Rafii amesema: Amesema Malik na Ahmad, inafaa kukusanya kwa sababu ya udhuru wa ugonjwa na matope. Na maneno kama haya wamesema baadhi ya wanazuoni wetu miongoni mwao ni Abu Suleiman Al khatwabiy na kadhi Husein na akapendezeshewa nayo Ar rubbani katika [Al hiliyyah], nikasema: Mtazamo huu una nguvu sana. Na hutolewa ushahidi kutoka kwa Ibn Abbas amesema "Mtume –rehma na amani zimshukie– amekusanya (Swala pamoja) alipokuwa Madina bila ya (sababu ) ya hofu au mvua." Imepokewa na Muslim kama ilivyokwisha elezwa. Na ufafanuzi wake ni kwamba; kukusanya huko ima kutakuwa kwa sababu ya ugonjwa au kwa sababu nyengine iliyofanana na ugonjwa, na kwa kuwa udhuru wa ugonjwa na wa mtu mwenye hofu ndio wanaohofiwa zaidi kuliko hali ya mvua.
Hivyo basi, iwapo rafiki yako hataweza kusali katika ardhi (kavu) kwa kuwa matope na unyevunyevu umezagaa kila mahala basi atatafuta kitu kigumu na kikavu cha kutandikia ili akisimamie anaposali pindi akiweza, na kama haikuwezekana hivyo basi atasali katika sehemu iliyonyoka katika trekta, na kama haitawezekana hayo yote basi atakusanya Swala kwa kuswali ima kwa kutanguliza au kwa kuchelewesha katika moja ya nyakati za Swala hizo, na pale ambapo ataweza kuswali hali ya kuwa yupo katika eneo la ardhi kavu au katika sehemu iliyonyooka, na iwapo haikuwezekana kuswali katika hali hizo tulizozitaja basi itafaa kuswali hali ya kuwa amekaa kitako kwenye trekta hilo; kwa sababu ya udhuru wa matope, kwani hakuna tofauti baina ya wanazuoni kuwa kukaa ni badala ya kusimama katika Swala za lazima pale unaposhindwa kusimama.
Kwa asiyeweza kusimama anaweza kuswali hali ya kuwa amekaa, kama ilivyopokewa na Bukhari kutoka katika Hadithi ya Umran bin Huswayn –radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie– kuwa amesema: Amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu –rehma na amani zimshukie – "Swali ukiwa umesimama na kama huwezi basi uswali ukiwa umeketi, ukiwa huwezi swali kwa ubavu." Shekh Saleh Al aliy amesema katika kitabu cha: [Jawahir Al ikliyl Sharhu Mukhtasar Khalily Al Malikiy 1/55, chapa, Dar Al Fikr]: "Ni lazima kusimama katika Swala za faradhi, isipokuwa kwa maradhi (machofu - mashaka) makubwa au hofu ya mtu pindi akisimama ndani ya Swala au kabla ya Swala kwa kuepusha madhara. Shihab akasema: Itamlazimu kukaa ndani ya Swala na dini ya Mwenyezi Mungu ni nyepesi." Mwisho.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas