Kuhudhuria Mazishi ya Ndugu Wasio W...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuhudhuria Mazishi ya Ndugu Wasio Waislamu

Question

Mimi ni msichana kutoka Scandinavia, niliingia katika Uislamu (nilisilimu) tangu miaka mitano iliyopita. Hakuna yeyote katika familia yangu ambaye ni Mwislamu, na kwa hivyo basi mmoja wa jamaa zangu alifariki dunia, je inajuzu kwangu kuhudhuria taratibu za kuzika zitakazofanyika kanisani?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Hakuna kizuizi cha kisheria katika kuhudhuria jeneza za ndugu wasio waislamu au hata marafiki kwa mujibu wa yaliyopokelewa na Ali R.A. aliposema: “Alipokufa Abu Twalib nilikwenda kwa Mtume S.A.W. nikamwambia: Hakika ami yako mwenye kupotea amekufa, basi nani atamzika? Mtume S.A.W. akasema: “Nenda ukamzike, kisha usifanye chochote mpaka urudi kwangu”, nilisema: Amekufa mshirikina, Mtume S.A.W. akasema: “Nenda ukamzike”, akasema: Nilikwenda kumzika kisha nikarudi, Mtume S.A.W. akasema: “Nenda ukaoge kisha usifanye chochote mpaka urudi kwangu”, akasema: Nilikoga kisha nikarudi kwake. Mtume S.A.W. akaniombea kwa Mwenyezi Mungu nipate wanyama wekundu na weusi” (Hadithi hii imesimuliwa na Ahmad na Abu Daud na Al Baihaqiy).
Imamu Al Nawawiy alisema katika kitabu cha: [Al Maj-muu vol. 5, uk. 281, chapa cha Mak-tabat Al Irshad]: “Haichukizi kwa Mwislamu kulisindikiza jeneza la ndugu aliye kafiri, na kauli hii ameifuata Imamu Al Shafi katika kitabu cha: [Muhtasari wa Al Mazniy]”.
Halikadhalika, jambo la kulisindikiza jeneza la ndugu hata akiwa kafiri linaingia katika uhusiano wa kutazama jamaa ulioamrishwa kisheria licha ya kutendeana kwa wema, tabia zilizo njema na kutekeleza wema. Tena mwenye swali akihudhuria jeneza la nduguye ni jambo linaloleta heshima zaidi katika Uislamu wake mbele ya jamaa zake. Aidha haidhuru kisheria kutoa rambirambi; kwani jambo hili linatokana na uhusiano wa kutendeana kwa wema na uadilifu unaotajwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenyezi Mungu hakukatazeni kuwafanyia ihsani na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini wala hawakukufukuzeni katika nchi zenu. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wafanyao uadilifu}[AL-MUMTAHINAH, 8], tena hayo ni miongoni mwa mema yaliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliposema: {Na semeni na watu kwa wema}[AL BAQARAH, 83].
Kutokana na hayo, tunamnasihi mwenye swali awe mwepesi kwa watu na jamaa zake pamoja na kuhifadhi utambulisho wake wa Kiislamu, tena Uislamu haupendelei Mwislamu awe katika hali ya kujitenga mbali na waliomzunguka; kwani Uislamu umeenea kwa kutendeana kwa wema, kushirikiana na watu katika furaha na huzuni zao, kuwasaidia wengine pamoja na kuwahurumia.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas