Namna ya Ndoa Baina ya Mwanamume Mw...

Egypt's Dar Al-Ifta

Namna ya Ndoa Baina ya Mwanamume Mwislamu na Mwanamke Mkristo

Question

Mimi ni mwanamke Mkristo kutoka Marekani lakini siamini suala la Utatu ninavyoamini mimi ni kuwa Mungu ni Mmoja tu, vile vile siamini kwamba Issa ni mwana wa Mungi kwani yeye ni Mtume aliyetumwa na Mungu, kwa hivyo basi nilikutana na mwanamume Mwislamu mzuri sana nikampenda, naye alinielekeza jinsi ya kusoma Quraani Tukufu pamoja na kuzielewa maana zake.
Sisi tunafikiria kuoana hivi karibuni. Lakini yeye ni Mmisri na kanuni za hapa zinalazimisha kwamba mkataba wa ndoa uandikwe na mwanasheria wakati mimi nahisi kwamba ndoa kwa njia hii haitabarikiwa, mimi nataka niolewe kwa jina la Mwenyezi Mungu, na hao wanasheria wa hapa wanaamini Utatu.
Je kuna njia yeyote ya kuandika mkataba wa ndoa kwa mfumo wa Kiislamu wakati mimi ni Mkristo?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Mkataba wa ndoa lazima uandikwe kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu; kwani Uislamu ni mfumo wa wazi ambao wafuasi wake wanalazimika kuwaamini Manabii na Mitume wote waliotumwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; maana kuamini kwamba Muhammad S.A.W. ni Mtume kwa watu wote kunamaanisha kuamini kwamba Issa A.S. ni Nabii wa Mwenyezi Mungu.
Hali kadhalika ili Mtu awe Mwislamu lazima awaamini Manabii na Mitume wote na miongoni mwa Manabii Wakuu na Wabora zaidi ni Bwana Issa A.S. pamoja na Nabii wa Umma huu wa Waislamu ambae ni Muhammad. Mtume wetu S.A.W. alisema: “Mimi nina haki zaidi kwa Nabii Issa bin Mariam katika dunia na akhera kuliko watu wote; hakuna nabii baina yangu na yeye”.
Ndoa inatimizwa kisheria kwa Ijaabu (tamko la kuoa au kuozesha) na Qabuul (tamko la kukubali); wewe utamwambia: (Kwa Baraka za Mwenyezi Mungu, nakuozesha nafsi yangu, kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wetu Muhammad S.A.W. na kwa mahari tuliyoafikiana, na Mwenyezi Mungu ni Shahidi juu ya niliyoyasema), naye atasema: (Kwa Baraka ya Mwenyezi Mungu, nakubali kukuoa, kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wetu Muhammad S.A.W. na watu wake, kwa mahari tuliyoafikiana, na Mwenyezi Mungu ni Shahidi juu ya niliyoyasema), sharti kuwepo mashahidi mawili Waislamu. Ama kufungisha ndoa katika ofisi ya mwanasheria, basi ni suala la kuthibitisha kiserikali mkataba wa ndoa na wala sio zaidi ya hapo. Nasi tunakuombeeni Mwenyezi Mungu aibariki ndoa yenu.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas