Kukusanya Sala kwa Udhuru wa Ugonjw...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kukusanya Sala kwa Udhuru wa Ugonjwa

Question

Je, inafaa kukusanya sala kwa sababu ya ugonjwa? Na iwapo inafaa ni kwa masharti gani? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Sala ni nguzo katika nguzo za kiisilamu, na nafasi yake kwa upande wa imani ni kama kichwa kwenye mwili, na uislamu umeisisitiza katika kitabu chake na kuijali ipasavyo na pia kuitilia mkazo mkubwa wa kuwa itekelezwe na isaliwe kwa nyakati zake maalumu, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {kwani hakika sala kwa waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu} [AN NISAA: 103].
Na imetahadharishwa sana kutoiacha, imepokewa kutoka kwa Ibn Omar – radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie –kuwa mtume – rehma na amani zimshukie – amesema: "Uislamu umejengwa kwa nguzo tano: Kushuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, kusimamisha sala, kutoa zaka, kuhiji na kufunga Ramadhani."
Na uislamu umesisitiza na kuwataka waislamu kuzihifadhi sala wakiwa ni wakazi au wasafiri, katika hali ya hofu au ya amani, katika hali ya utulivu au vita na hata katika sehemu zenye usumbufu na wakati wa hofu kubwa ya kivita ambapo waislamu huwa mbele ya maadui zao, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Angalieni (zihifadhini) Sala, na hasa Sala ya katikati, na simameni kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. * Na kama mkiwa na hofu basi (salini) mkitembea au mmepanda (wanyama); na mtakapokuwa katika amani, basi Mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama Alivyowafunzeni yale mliyokuwa hamyajui.} [AL BAQARAH: 238-239]
Kwa maana; Salini katika hali ya hofu na vita, mkiwa katika mwendo au vipando kwa namna yeyote muwezayo bila ya kurukuu au kusujudu lakini inatoosha ishara na bila ya kushurutisha kuelekea kibla. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na mashariki na magharibi ni ya Mwenyezi Mungu, basi mahali popote mgeukiapo ndipo (mtaukuta) uso wa Mwenyezi Mumgu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.} [AL BAQARAH:115]
Na sheria inakubali kukusanya sala utokeapo udhuru, utasali sala ya adhuhuri pamoja na ya alasiri, kwa kutanguliza au kuchelewesha, na sala ya magharibi utasali pamoja na sala ya isha kwa sharti ya kunuia kufanya hivyo kabla ya kuingia wakati wa alasiri au wa isha. Na miongoni mwa udhuru huo ni matope, kwa kukisia (kulinganisha na) safari ambayo ina usumbufu (mashaka) katika hali zote hizo mbili. Imamu Bukhari na Muslim wametoa kutoka kwa Anas – radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie – amesema: "Mtume –rehma na amani zimshukie- alipokuwa akisafiri, kabla ya kumili kwa jua, mwisho wa wakati wa Adhuhuri kuelekea wakati wa Alasiri, huteremka na kukusanya sala hizo."
Na Hadithi aliyoitoa Muslim kutoka kwa Muadh – radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie – amesema: "Tulitoka pamoja na Mtume –rehma na amani zimshukie – katika vita ya Tabuk, na alikuwa akiswali sala ya Adhuhuri na alasiri pamoja, na akisali sala ya Magharibi na Isha pamoja."
Imamu Nawawiy anasema katika kitabu cha: [Al majmuu 4/383, chapa, Dar Al fikr]: "Ar Rafii amesema: amesema Malik na Ahmad, inafaa kukusanya kwa sababu ya udhuru wa ugonjwa na matope. Na maneno kama haya wamesema baadhi ya wanazuoni wetu miongoni mwao ni Abu Suleiman Al khatwabiy na kadhi Hussein na akapendezeshewa nayo Ar Rubbani katika [Al hiliyyah], nikasema: Mtazamo huu una nguvu sana.
Na hutolewa ushahidi kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Mtume – rehma na amani zimshukie – amekusanya (sala pamoja) alipokuwa Madina bila ya (sababu ) ya hofu au mvua." Imepokewa na Muslim kama ilivyokwisha elezwa. Na ufafanuzi wake ni kwamba; kukusanya huko ima itakuwa kwa sababu ya ugonjwa au kwa sababu nyingine iliyofanana na ugonjwa, na kwa kuwa udhuru wa ugonjwa na mwenye hofu wanahofiwa zaidi kuliko hali ya mvua.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.


 

Share this:

Related Fatwas