Kutumia Silaha za Maangamizi
Question
Siku hizi baadhi ya maandishi na tafiti zilizoandikwa na baadhi ya makundi zimejitokeza zikidai kuwa inaruhusiwa kutumia silaha za maangamizi dhidi ya nchi zisizo za Kiislamu wakisema kuwa kauli yao hii inaafikiana na Sheria, wakitoa dalili kutoka baadhi ya matini za Kifiqhi, na wakipima na suala la “Al-Tatarus” (yaani kujikinga maadui kwa Waislamu ambao hawaruhusiwi kuuawa), “Al-Tabiyit” (yaani kuwashambulia maadui usiku kwa nia ya kuiba mali zao), na “Al-Tahriiq” (yaani kuunguza nyumba za maadui kama hakuna Mwislamu yeyote ndani yake), masuala hayo yaliyotajwa katika vitabu vya fiqhi, je maneno hayo ni sahihi na yanaafikiana na Sheria?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Silaha za maangamizi katika istilahi ya kijeshi ina maana ya aina ya silaha zisizo za kawaida zenye maangamizi makubwa, zikitumiwa zinasababisha madhara makubwa sana katika eneo linaloangamizwa. Viumbe hai, wakiwa wanadamu na wanyama na hata mazingira yanaangamizwa kwa silaha hizi.
Silaha hizi zina aina tatu: Silaha za nyuklia, kama vile, bomu la nyuklia, bomu la haidrojeni, na bomu la nyutroni. Aina hii imetengenezwa ili kueneza vifaa vya mionzi vinavyoangamiza wanadamu, majengo, na huchafua nchi nyingi kwa muda mrefu, na baadhi ya silaha hizi zinaangamiza watu tu, na haziangamizi majengo.
Silaha za kemikali, kama vile: Gesi za vita zinazotumiwa mara nyingi na vifaa vya kuunguza vyenye madhara makubwa -pengine madhara hayo yanafikia mpaka kifo- juu ya viumbe, mimea, na mara nyingi vifaa hivi vina sumu vikiwa vya gesi au vya maji vinavyovukizwa haraka, na mara chache vinakuwa yabisi.
Silaha za biolojia; nazo ni vimelea na virusi vinavyotumika kwa ajili ya kueneza magonjwa makubwa kati ya maadui, kufanya hasara ya rasimali yao ya wanyama au ya kilimo.
Inaruhusiwa kwa nchi za kiislamu kutumia silaha kama hizi kwa ajili ya kuzuia uadui, na dalili ya hivyo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi walio fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu} [AL ANFAAL : 60], Al-Alusi alisema katika tafsiri yake kuwa : “yaani : Kila kinachochukuliwa kama nguvu katika vita.” [10/24, Daru Ihyaa Al-Turaath Al-Arabi], Mwenyezi Mungu Mtukufu aliamuru katika aya iliyotangulia kuzuia uadui ili maadui wasishambulie Waislamu.
Msingi wa kuzuia uadui ni msingi wa kisheria na pia ni msingi wa kisiasa unaotegemewa kwa nchi katika siasa zao za kujitetea kama ilivyoamuliwa katika mikakati ya kijeshi. Basi kutumia silaha kama hizi ni jambo linalozingatiwa miongoni mwa mambo ya ukamilifu, na ukamilifu huu unatakiwa. Na ruhusa katika kitu fulani ni ruhusa katika ukamilifu wake pia, na hali hii ina faida kubwa sana kuhusu uwiano wa mikakati ya kijeshi kati ya nchi. Hali ya kutumia silaha kama hizi ni kama sababu ya ushawishi wa nchi maalum ambayo pengine inafanya kazi ya uadui dhidi ya nchi nyingine ya Kiislamu, jambo ambalo linatuepusha kupigana vita ovyo.
Suala linalotangulia linahusiana na kutumia silaha kwa ajili ya kutishia na kuzuia uadui, ipo tofauti kati ya kutumia silaha kwa ajili ya kuzuia uadui na kuanza uadui kupitia kutumia silaha hizi, na swali hili linahusu kuanza kutumia silaha hizi, na kwamba kutumia silaha hizi kunategemea hukumu za mtu binafsi au maoni yanayohusu baadhi ya makundi, na hali hii hairuhusiwi kisheria, kuhusu mtazamo wa kuruhusiwa ni mtazamo wa uwongo na kisingizio juu ya Sheria na Dini. Dalili za hali hii ni mambo yafuatayo :
La Kwanza: Asili ya kupigana vita ni lazima kuwa chini ya bendera ya Khalifa, na kwamba hali ya vita inategemeana na jitihada za Khalifa mwenyewe. Vile vile raia wanapaswa kumtii katika uamuzi huu. Hali ya vita imetegemea jitihada za Khalifa kwa sababu ya ujuzi wake wa mambo yote yanayohusu matendo na matokeo ya vita na masilahi ya raia wake. Kwa hivyo, kutangaza vita na kufanya mikataba ya jumla au ya kimataifa inategemewa kwake baada ya kuchaguliwa moja kwa moja, naye haamui uamuzi wowote kwa matamanio yake, bali haamui ila baada ya kushauriana na wenye ujuzi katika kila nyanja inayohusiana na uamuzi wake, kama wataalam wa kijeshi na washauri wa kisiasa wanaoshirikiana naye katika uamuzi huu, ambapo hawezi kuamua uamuzi huu pekee yake pasipo na kushauriana nao.
Kama mtu mmoja au watu miongoni mwa Waislamu wakiamua kutumia silaha hizi basi hali si kisingizio juu ya Khalifa tu, bali ni kisingizio juu ya Waislamu wote, kwa sababu watu hawa wamejipa haki ya kufanya maamuzi yanayohusu hatima ya taifa pasipo na kurejea wenye ujuzi, na hali hii ambapo nchi na wananchi watapata hatari kubwa.
Al-Bahutiy alisema katika kitabu cha [Sharhu Muntaha Al-Iradaat] kuwa: “Hairuhusiwi kupigana vita pasipo na ruhusa kutoka Khalifa, kwani yeye mwenyewe ni mwenye majukumu ya kupigana vita, kwa sababu anajua wingi wa maadui au uchache wao, mahali pao pa kujificha na vitimbi vyao (Ila kama maadui wakiwashtua Waislamu) na walikuwa wakiogopa shari zao, katika wakati huu inaruhusiwa kupigwa vita pasipo na kuomba ruhusa kutoka Khalifa kufuatana na masilahi yao” [1/636, Alamu Al-Kutub].
La Pili: Mambo yanayosababisha kuvunja ahadi na mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na nchi za Kiislamu kwa hiari yao, na kwa mujibu wa jamii ya kimataifa, ili kufanikisha usalama na amani ya kimataifa kufuatana na wajibu wa nchi zilizotia saini juu ya mikataba na ahadi hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema : {Enyi mlio amini! Timizeni ahadi} [AL-MAIDAH: 1]. Ahadi ni mkataba unaofanyika kati ya pande mbili katika kitendo kimoja. Al-Tunisi Ibn Ashour ambaye ni Sheikh wa Uislamu alisema kuhusu tafsiri ya aya hii : “Ahadi ni pamoja na ahadi ya Waislamu na Mola wao, nayo ni kutii Sheria yake… na kama Mtume S.A.W alivyowaahidi Waumini ya kwamba hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini. Vile vile ahadi ni pamoja na ahadi ya Waislamu na Washirikina, na ahadi ya Waislamu kati yao” [Al-Tahrir Wal-Tanwir 6/74, Darul Tunisiah Lelnashr].
Imepokelewa kutoka kwa Al-Tirmizi kutoka kwa Amr Ibn Auf Al-Mazni R.A kwamba Mtume S.A.W. amesema: “Waislamu ni wenye kutimiza masharti isipokuwa sharti linaloharimisha jambo la halali au sharti linalohalilisha jambo la haramu”, Al-Jassas amesema : “Maana ya hivyo ni lazima kutimiza masharti yote kama hakuna dalili ya kuainisha” [Ahkam Al-Quran 2/418, Darul Fikr].
Imepokewa kutoka kwa Al-Bukhari kutoka kwa Ali R.A kwamba Mtume S.A.W, amesema : “Dhima ya Waislamu ni moja ; hata aliyechukua dhima hiyo ni Mwislamu aliye chini kabisa, basi Mwislamu anayevunja dhima aliyechukua Muislamu mwengine juu ya kafiri, basi atalaaniwa na Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote. Haitapokelewa ibada yake ya faradhi wala ya Sunna siku ya Kiama.”
Na kauli yake Mtume S.A.W – “Dhima ya Waislamu” yaani: Ahadi yao, na kauli yake : “Aliyechukua dhima hiyo ni Mwislamu aliye chini kabisa” yaani: Aliyehusika na dhima yao ni aliye chini kabisa miongoni mwao katika hali na idadi. Basi kama Mwislamu mmoja -au Khalifa- akampa mwingine ahadi, hairuhusiwi kuivunja. Na kauli yake “Haitapokelewa ibada yake ya faradhi wala ya sunna” yaani: Haitapokelewa kazi yeyote.
Imepokewa kutoka kwa Al-Bukhari kutoka kwa Abdullah Ibn Omar R.A kwamba Mtume S.A.W amesema: “Mambo manne mwenye kuwa nayo basi huwa ni mnafiki khalisi, na mwenye kuwa na moja tu katika hayo basi huwa na sifa moja ya unafiki mpaka aiwache: Anapo zungumza husema uongo na anapochukua miadi hatekelezi, na anapotoa ahadi hatekelezi na anapogombana hupindukia mipaka”. Imepokelewa kutoka kwa Al-Baihaqi kutoka kwa Amr Ibn Al-Hamq Al-Khuzai kwamba Mtume S.A.W. amesema : “Kama mtu akimwamini mwingine juu ya nafsi yake kisha akamwua, basi ninatakasika kutoka aliyeua hata akiwa aliyeuawa ni kafiri”.
Kwa hivyo, pande mbili zinazoahidiana wanakaa katika usalama na wanaacha kupigana vita kwa mujibu wa ahadi yao, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na wakielekea amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua} [AL ANFAAL: 61].
La Tatu: Pia kuna kuua kwa wasio waangalifu, imepokelewa kutoka kwa Abu Daud na Al-Hakim katika Mustadrak kutoka kwa Abi Hurairah R.A. amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema: “Muumini haui mwingine, Imani ni kizuizi cha kuua”. Ibn Al-Athir amesema katika kitabu cha Al-Nihayah : “Kuua maana yake ni kwamba mtu anamshambulia mwenzake wakati wa kutoangalia na kumwua”. Maana aya Hadithi ni kwamba Imani inazuia kuua kama kizuizi kinavyozuia kutenda, kwani kuna hila na udanganifu, na kauli ya Mtume S.A.W.: “Muumini haui” hili ni katazo au ina maana ya katazo.
Wakati Khubaib alipotekwa na Washirikina Wakamchukua na wakamwuza katika Makkah. Khubaib akanunuliwa na watoto wa Al-Haarith Ibn Amir Ibn Nawfal Ibn Abdi Manaaf. Na Khubaib ndiye aliye muuwa Al-Haarith bin Amir siku ya vita vya Badr, na akabaki kwao hali ni mateka. Siku moja Khubaib alimtaka binti wa Al-Haarith amuazime wembe ili ajisafishe sehemu zake za chini, na yeye akamuazima, na alimchukua mtoto wake mwanamme naye binti wa Al-Haarith ameghafilika alipomjia kumchukua. Akasema: Nikamkuta amempakata pajani pake na wembe mkononi mwake. Nikafadhaika mfazaiko wenyewe hata Khubaib akaujua usoni mwangu. Akasema: Unakhofu kuwa nitamuuwa? Mimi sitakuwa wa kufanya hayo. Wallahi katu sikupata kumwona mateka mtu wa kheri kuliko Khubaib… nk. Mtu huyo ni mateka Mwislamu kwa maadui wake wanaopanga kumwua ambapo yeye anakaribia kuuwa, inagwa hivyo, alipokuwa na nafasi ya kuwahuzunisha Washirikina kwa kumwua mtoto wao anatoa msamaha kwao; kwa sababu tabia ya Mwislamu haina udanganyifu wala haina kuwashangaza wanaoghafilika.
La Nne: Vitendo hivi vinasababisha kuua na kudhuru kwa wanawake na watoto. Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Abdullah Ibn Omar R.A. kwamba mwanamke alikutwa akiuawa, basi Mtume S.A.W. alikana kuhusu kuuawa kwa wanawake na watoto, na katika Hadithi nyingine: Mtume S.A.W. alikana kuhusu kuuawa kwa wanawake na watoto. Imam Al-Nawawi alisema katika Sharhul Imam Muslim: “Wanazuoni wamekubaliana juu ya uharamu wa kuwaua wanawake na watoto kama hawakupigana, lakini kama wakipigana, Wanazuoni walisema: Inaruhusiwa kuwauwa”. [Sharhu Muslim 12/48, Ihyaa Al-Turath Al-Arabiy].
La Tano: Vitendo hivi ni miongoni mwa vitendo vya kuua na kudhuru Waislamu wanaokwepo kwenye nchi hizi miongoni mwa makazi wake au miongoni mwa waliorudishwa kwake. Sheria Tukufu imeadhimisha damu ya Mwislamu na ikatishia sana kuimwaga bila ya haki. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: {Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa.} [AN NISAA: 93]. Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema pia: {Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote.} [AL MAIDAH: 32].
Imepokelewa kutoka kwa An-Nasaa’i kutoka kwa Abdullah Ibn Umar R.A. kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. alisema kuwa : “kuondoka kwa dunia ni nyepesi kwa Mwenyezi Mungu kuliko kumwua Mwislamu”, pia imepokelewa kutoka kwa Ibn Majah kutoka kwa Ibn Omar R.A amesema: Nimemwona Mtume S.A.W. wakati alipotufu Kaabah akisema: “Namna gani wewe ni nzuri, na harufu yako ni nzuri, namna gani wewe ni mtukufu na namna gani utukufu wako, naapa kwa Mwenyezi Mungu ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake kwamba utukufu wa muumini kwa Mwenyezi Mungu ni kubwa zaidi kuliko utukufu wako, mali yake na damu yake, na kumdhani kwake ni kheri tu”
Basi kumwua kwa makusudi ni uadui mkubwa hakuna dhambi baada ya ukafiri ni kubwa zaidi kuliko ile. Kuhusu hali ya kukubali toba yakekuna tofauti kati ya masahaba na waliokuja baada yao wametofautiana.
La Sita: Vitendo hivi vinasababisha madhara na ufisadi mkubwa kwa Waislamu wote ; kwa sababu nchi iliyoshambuliwa pengine mmenyuko wake utakuwa sawa au kwa nguvu zaidi. Na kwamba madhara makubwa yanayosababishwa kwa silaha hizi labda yatapita mipaka ya nchi hii mpaka yafikie nchi nyingine ambazo hazina kosa lolote. Madhara yote ya vitendo hivi ni makubwa sana zaidi kuliko maslahi yake. Na Miongoni mwa misingi ya Sheria Tukufu ni kwamba kuondosha madhara ni bora kuliko kuleta maslahi.
La Saba: Matokeo ya kutumia silaha kama hizi ni kuharibu mali, majengo, mali ya umma na ya binafsi, kuharibu mali na kuzipotea zisizoruhusiwa kwa Sheria, uharamu unazidi na kuwa marudufu ikiwa mali hizi hazimilikiwi na mwenye kuzipotea bali zinamilikiwa na mwengine -kama iliyokuwa katika suala hili- basi uharamu unahusiana na kukiuka Sheria kwa upande mmoja, na pia unahusiana na haki za watu kwa upande mwengine.
La Nane: Hali ya kutumia silaha hizi kwa njia fulani labda inamuingiza mtendaji nchi zinazokusudiwa baada ya kutimiza taratibu za viza, na kukubali kwa nchi hizi juu ya kuingia kwa mtu mmoja ndani ya nchi hizi kwa sharti kutofanya ufisadi ndani yake, hata kama haitajwa hivi kwa maneno inafahamika kwa maana. Wanazuoni wa Fiqhi walisema kama hivyo.
Imam Al-Khirqi alisema katika Muhtasari yake: “Aliyeingia nchi za maadui kwa amani hairuhusiwi kuwadanganya katika mali zao”, Ibn Qudamah alieleza maneno ya Imam Al-Khirqi akisema: “Ama kuhusu udanganya wao ni haramu, kwani wamempa amani kwa sharti la kuacha kuwadanganya na kuwapa amani, ingawa sharti hili halikutajwa kwa uwazi, lakini linafahamika katika maana, kwa hivyo, aliyekuja kwa amani kwetu miongoni mwao kisha akatudanganya, basi alivunja ahadi yake. Ikithibitika hivyo, hairuhusiwi kuwadanganya kwa sababu alivunja ahadi, na katika dini yetu hairuhusiwi kuvunja ahadi” [Al-Mughni 9/237- Daru Ihyaa Al-Turaath Al-Arabi].
Ama kuhusu matini za Kisheria na za Kifiqhi zinazotegemewa ili kueneza fikra mbovu ni matini zimekatwa kutoka muktadha yake ambayo ni tofauti. Kwa hivyo, hali ya kuchukuwa matini hizi kama dalili ni aina ya fujo, ambapo kuna kupoteza kwa tofauti zinazozingatiwa kati ya hali mbalimbali, kama vile tofauti kati ya hali ya vita na hali ya usalama. Na kwamba hali ya vita ina hukumu zake hasa kinyume na hali ya usalama ambayo inalinda damu, mali, na heshima. Nayo ni tofauti kubwa ambayo inapinga na kutumia silaha hizi kufuatana na yaliyotajwa katika vitabu vya Fiqhi kuhusu kuruhusiwa kuwashambulia washirikina na kujikinga kwa maadui nyuma ya wasioruhusishwa kuuawa, dalili hizi ni kosa kubwa na upimaji mbovu kabisa, hata kama masuala hayo yaliyotajwa na masuala sahihi katika muktadha yake ya kifiqhi. Lakini kosa ni kubadilishwa hukumu hizi kutoka muktadha yake kwa muktadha nyingine ambayo inatofauti kabisa katika hali na hukumu.
Pia hairuhusiwi kupima silaha hizi na kupigana na “Al-Swaail” yaani aliyepita mipaka na kumwua, kwa sababu ipo tofauti kati ya hukumu za kumzuia aliyepita mipaka na hukumu za Jihadi yenyewe. Miongoni mwa hukumu hizi ni kwamba aliyepita mipaka anazuiliwa kwa mamabo ambayo ni rahisi zaidi, yaani kama akizuiliwa kwa maneno basi kumpiga ni haramu, na kama akizuiliwa kwa mkono hairuhusiwi kuzuiliwa kwa upanga, hali ambayo hailingani na kutumia silaha za maangamizi kama ilivyotajwa hapo juu.
Kuhusu hadithi zinazotajwa juu ya kuhusu kuruhusiwa kuwashambulia washirikina au kuwachoma, upimaji wa kutumia silaha za maangamizi kwa njia hii kwa kweli ni upimaji mbovu kabisa. Kwa sababu ipo tofauti kubwa na wazi kati ya hali hizi mbili, na kwamba Hadithi hizi zimetajwa katika hali ya vita, na ipo tofauti kubwa kati ya hali ya vita na hali nyingine. Vile vile ipo tofauti kubwa sana kwa upande wa athari kati ya kutupa mawe na kutumia silaha za maangamizi ; kwani kutupa kwa mawe siyo kama kutumia silaha za maangamizi, pia matukio hayo yaliyotajwa katika Sunna yametokea chini ya bendera ya Khalifa, nayo ni tofauti ya msingi kati ya hali hizi mbili.
Vile vile kama tukidhani usahihi wa Hadithi hizi, basi ni matukio maalum yana muktadha yake hasa, baadhi ya Wanazuoni wamesema kuwa asili ni kutoruhusiwa kwa kuwashambulia washirikina, kuwachoma na kuharibu kutegemea matini za kauli katika maudhui hii zinazo na sifa ya ujumla.
Mtazamo sahihi ni kutotumia aina za silaha za maangamizi zinazosababisha kuangamiza kwa ujumla kufuatana na katazo la kuangamiza kwa moto baada ya kuamuru Mtume S.A.W, kisha alikataza kabla ya kutukia, ingawa hali ilikuwa ya vita. Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhari kutoka kwa Abu Hurairah R.A kuwa Mtume S.A.W. alisema : “Hakika haadhibu kwa moto ila Mwenyezi Mungu tu”, Mtume S.A.W alikataza kuangamiza. Inafahamika kuwa silaha nyingi za maangamizi zinasababisha moto mkubwa. Kwa hivyo, mtazamo sahihi ni kutotumia silaha hizi kabisa hata katika hali ya vita kwa katazo hili la ujumla.
Ama kuhusu upimaji wa suala hili na suala la kuwashambulia washirikina, basi ni aina ya kosa, kwani Wanazuoni waliporuhusishia kuwashambulia washirikina walitaja masharti maalum miongoni mwao ni : Inapatikana hali ya vita, kwamba maadui wanaoshambuliwa ni maadui wanaoruhusiwa kupigwa vita, kinyume na maadui ambao wana ahadi nasi ; basi hairuhusiwi kuwashambulia washirikina wanao na ahadi au dhima na kama hivyo miongoni mwa mikataba ya Kimataifa, kama kila upande uwe na amani kuhusu mali na heshima.
Kama hairuhusiwi kuwashambulia washirikina, basi kutumia silaha za maangamizi pamoja nao ni haramu zaidi. Ama kuhusu suala la kujikinga kwa maadui nyuma ya wasioruhusishwa kuuawa, basi haliruhusiwi isipokuwa katika hali ya vita na kwa masharti na kwa namna maalum kama Wanazuoni walivyotaja kinaganaga. [Rejea : Al-Bahr Ar-Raiq 5/80, Hashiyat Ibn Abdein 3/223, Rawdatul Taalibiin 10/239, Mughni Al-Muhtaj 4/223, Al-Mughni kwa Ibn Qudamah 8/449, 10/386].
Kutokana na yaliyotangulia hapo juu, basi hili ni dai miongoni mwa madai batili, kusema kwa dai hili na kulieneza ni kisingizio, kosa na ufisadi katika ardhi, hali iliyokatazwa na Mwenyezi Mungu na atakayefanya hivyo ataadhibiwa adhabu kubwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Kama wanaafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao fitna katika Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu.} [AL AHZAAB; 60], Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema pia: {Wala msifanye uharibifu katika nchi, baada ya kuwa imekwisha tengenea. Hivi ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.} [AL AARAF: 85], Vile vile Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: {Basi yanayo tarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na mwatupe jamaa zenu? (*) Hao ndio Mwenyezi Mungu alio walaani, na akawatia uziwi, na akawapofoa macho yao} [MUHAMMAD: 22,23].
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote