Kuondosha Nembo Baada ya Kuingia ka...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuondosha Nembo Baada ya Kuingia katika Uislamu. Swali:

Question

 Mimi ni mwanamke niliesilimu tangu miezi minne iliyopita. Na nilikuwa nikichora nembo (mchoro wa mwili) juu ya mgongo wangu kabla ya kuingia katika Uislamu tangu miaka kumi iliyopita, na mwishoni nikajua kwamba nembo ni haramu, nifanyeje na nembo hii? Hali ya kuwa uondoshaji wake unakuwa na maumivu makali na ni gharama kubwa sana, na nembo hii haitaonekana kwa yeyote isipokuwa kwa mume wangu?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Nembo inatengenezwa kwa namna mbili;
ya kwanza: ni kudunga ngozi kwa sindano mpaka damu itoke, kisha inawekwa rangi ndani ya mianya hii na majeraha mwilini ili ibakie na wala isitoke.
Ya pili: Ni mchoro uliopatikana kwa kitendo kilichotajwa.
Nembo ni haramu kwa mujibu wa Hadithi sahihi zinazomlaani aliyechora nembo na aliyechorwa nembo, na miongoni mwa Hadithi hizo ni ile iliyopokelewa na Imamu Bukharin na Muslim kutoka kwa Ibn Umar R.A. alisema: "Mtume S.A.W alimlaani mtu aliyevaa nywele za bandia, na aliyechora nembo na aliyechorwa nembo".
Al-Hafidh Ibn Hajar alisema katika Kitabu cha: [Fathu-Albari 10/372, chapa ya Dar Al-Maarifa]: "Na kuifanya ni haramu kwa dalili ya Hadithi iliyotajwa katika mlango huu na pahala pa mwili palipochorwa na nembo pamekuwa najisi kwani damu ilifungwa ndani yake na inapaswa kuiondosha kwa jinsi iwezekanavyo hata kwa jeraha ila ikiwa kitendo hicho kitaleta madhara au kupoteza manufaa ya kiungo, basi katika hali hii inajuzu kuiacha nembo na kutosheka na toba ili kufuta dhambi, na mwanamke ni sawa na mwanamume katika suala hili”.
Na hii ni moja ya haki za Mwenyezi Mungu ambazo zinafutwa kwa kuingia katika Uislamu; kwani dhambi zote katika haki za Mwenyezi Mungu zinafutwa baada ya mtu kiingia katika Uislamu, kama alivyotaja Ahmad katika kitabu chake cha: [Musnad] kutoka kwa Amru Ibn Al-A's R.A. alisema: Mtume S.A.W alisema: "Uislamu unafuta yaliyokuwa kabla yake" na Hadithi hii ilitajwa pia na Imamuu Muslim kwa maneno haya: "je unajua kwamba Uislamu unafuta yaliyokuwa kabla yake", na Imamu Al-Karafi katika kitabu cha: [Al-Fourok 3/184, chapa ya A’lam Al-Kotub] alisema: "Haki ni za aina mbili: Haki za Mwenyezi Mungu, na haki za wanadamu, na haki za Mwenyezi Mungu hazimtenzi nguvu (mtu aliyeingia katika Uislamu) kama vile dhihari, nadhiri, kiapo / yamini yeyote, kulipa Sala au Zaka zilizopita, wala kitu kinachoachwa katika haki za Mwenyezi Mungu, kwa kauli yake Mtume S.A.W: "Uislamu unafuta yaliyokuwa kabla yake", na tofauti kati ya haki za Mwenyezi Mungu na haki za wanadamu inakuwa katika pande mbili: Moja yake ni kwamba: Uislamu ni haki kwa Mwenyezi Mungu, ya pili: Mwenyezi Mungu ni Mwenye ukarimu na Mwenye Ihsani na Mwenye Usamehevu, na mja ni bahili na mdhaifu, na sifa hizo zimeafikiana na kushikamana kwake na haki yake huyo mja, basi haki zote za Mwenyezi Mungu (zilizokuwapo kabla ya mtu kuingia katika Uislamu) zilifutwa kwa ujumla wake baada ya kusilimu".
Kitendo cha kuondosha nembo, kinaposababisha jeraha la mwili au madhara, basi haipendekezwi kuiondosha, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu: {Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini}[AL HAJJ, 78], na kauli yake: {Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito} [AL-BAQARAH, 185], na kadhalika kauli yake: {Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yeyote ila kwa kadiri ya iwezavyo} [AL-BAQARAH, 286] {Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu} [AN-NISAA, 28].
Vile vile Maulamaa waliamua kanuni ya: ‘Hakuna madhara’ na ‘Hakuna hasara’, na asili yake inatokana na Hadithi iliyopokelewa na Ahmad, na Ibn Majah kutoka kwa Ibn Abas [As-Suyuti, Al-Ashbah wal-Nadhai'r, uk.86, chapa ya Dr Al-Kotub Al-Imiya].
Na Sala ya mtu mwenye kujichora nembo, inakubalika; kwani nembo ni najisi inayosamehewa, na Al-Nafarawy Al-Maliki alisema: "nembo ikiwa kwa namna inayokataliwa, basi mwenye nembo halazimishwi kuiondosha kwa kutumia moto, na nembo katika hali hii inakuwa miongoni mwa najisi zilizosamehewa, kwa hivyo basi, Sala inasihi nayo" [2/314, Al-Fawakih Al-Dwani, maelezo ya risala ya Al-Kairawany na Al-Nafarawy, chapa ya Dar Al-Fikr], na kadhalika saumu yake inasihi kwani hakuna uhusiano baina ya saumu na kitendo cha kuharamishwa kwa nembo.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

 

Share this:

Related Fatwas