Kushiriki Katika Mashindano ya Simu...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kushiriki Katika Mashindano ya Simu.

Question

 Tunataka kujua kuhusu hukumu ya kushiriki katika mashindano yanayofanyika kupitia simu katika vipindi vingi vinavyoenezwa kwa satalaiti, ambapo mshiriki huwa analipa gharama kubwa kwa maongezi ya dakika moja, wakati anajibu maswali kupitia simu yake, kisha majibu sahihi huwa yanachaguliwa na kukusanywa, na mshindi hupatikana kwa njia ya kura, miongoni mwa waliotoa majibu sahihi, na kuwatenga wote waliokosea.

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Asili ya mashindano ni kuwa yanajuzu kisheria yakiwa na lengo jema, na kuinufaisha jamii kwa ujumla, pamoja na kuleta kheri, ustawi, na kuwa mbali na kamari, rehani, udanganyifu, kugushi, na kutoelewana na watu; kwa Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Aisha R.A akisema: “Nilishindana na Mtume S.A.W, kukimbia nikamshinda, nilipokuwa mnene tulishindana tena, akanishinda, nikasema: Hii ni mbadala wa ile”. [Imamu Bukhari].
Inajuzu kisheria kuainisha tuzo kwa anaefuzu na kuwatangulia wengine katika kujibu maswali ya mashindano yenye lengo zuri, na yanayoruhusiwa kisheria, sharti tuzo husika itolewe kwa mali za wanaoyapanga mashindano hayo, au upande mwingine unaoweza kuitoa kwa washindi.
Kwa hiyo haijuzu mali ya tuzo hiyo kutolewa na wanaoshindana, hukumu hii ni kwa makubaliano ya wanachuoni. Ni kama vile kila mshiriki mmoja analipa kidogo kwa ajili ya kuja kupata fedha nyingi, na kwa hiyo basi, atakusanya alichokilipa yeye mwenyewe na kilicholipwa na washiriki wengine; kwa sababu huu ni mlango wa kuweka rehani na kamari ambavyo vinakatazwa katika Uislamu, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi na kamari na kuabudiwa (na kuombwa) asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kupiga ramli (na kwa vinginevyo); (vyote hivyo) ni uchafu (ni) katika kazi ya Sheteni. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufaulu (kutengenekewa)}.[AL MAIDAH: 90].
Kwa mujibu wa yaliyotanguli na katika uhalisia wa swali: Twasema kuwa: Mashindano ya simu kupitia radio na Televisheni na vyombo vingine vya habari, iwapo yataambatana na masharti na vigezo vya kisheria vilivyoashiriwa hapo juu, basi hakuna zuio lolote la kisheria.
Lakini yakikusanya hadaa, udanganyifu, kamari na kuweka rehani, na kukawa na kusudio kwa upande wa mashirika yanayoandaa mashindano hayo kwa ajili ya kupata faida na kuchukua mali za watu kwa njia ya udanganyifu, na kutoa sehemu ndogo ya mali iliyokusanywa kama tuzo, basi mashindano hayo ni haramu kisheria.
Na kwa jinsi ilivyoelezwa, jawabu limefahamika kutokana na maelezo yaliyotangulia katika swali, na ikiwa hali iliyopo ndiyo hiyo.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.
 

Share this:

Related Fatwas