Jinsi ya Kutendeana na Jamaa Wasioshikamana na Sheria.
Question
Ninakaa na jamaa zangu, lakini ninashikamana na Sheria zaidi kuliko wao, kwani wao wanatazama filamu na wanasikiliza nyimbo n. k. Vile vile wanatoa maneno yasiyo na adabu na wananilazimisha na mimi kusema maneno hayo hayo, pia wanatumia maneno ya kikafiri na kishirikina. Je? Ni namna gani ninaweza kutangamana nao kimaisha, kila siku kwa ajili ya kuwaongoza?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Unatakiwa uwe mwepesi wa kutangamana na jamaa zako, Uislamu haumpendi Mwislamu anaejitenga na wengine. Huna haja ya kujisifu kuwa wewe ni mfuasi wa dini zaidi kuliko wao, pengine wao ni bora zaidi kuliko wengi sana walio kama wewe. Hata kama wakifanya mambo hayo unayodhani ni dhambi, basi kutazama filamu tu siyo dhambi, lakini kuvitazama vinavyomkasirisha Mwenyezi Mungu ndiyo dhambi. Kusikiliza nyimbo tu siyo dhambi, kwani nyimbo ni maneno, mazuri yake ni mazuri na mabaya yake ni mabaya. Yapo maneno mengi unayodhani kuwa ni ya ukafiri na ushirikina au ya unafiki na hayana uhusiano na ukafiri kwa mbali au hata kwa karibu. Tahadhari na kuwashutumu jamaa zako kwa sifa ambazo haziruhusiwi kwa mujibu wa Sheria.
Usidhani kamwe kuwa wewe ni bora zaidi kuliko wao, kwani msingi ni kusema kweli, yakini, na uaminifu hata kama kazi za ibada kwao ni chache, Muogope Mwenyezi Mungu kuhusu wazazi wako, na uwe na huruma kwao. Mwislamu ni mwingi wa huruma kwa watu wote, usidhani kuwa wewe ndio utakayerekebisha ulimwengu wote, bali Mwenyezi Mungu tu ndiye anayeweza kuurekebisha Ulimwengu huu. Na mambo hayo hayasababishi kupambana na watu.
Na kama Uislamu uliamuru kuwafanyia wema wazazi hata kama wakiwa makafiri, basi inakuwaje kama wazazi hao watakuwa Waislamu! Ewe dada, tunatarajia kuwa utakuwa na subra na kutoyasikiliza maneno ya mtu yeyote, bali usikilize maneno ya wanavyuoni tu waliobobea katika kuifahamu Sheria ili njia yako iwe iliyonyooka. Tunamwomba Mwenyezi Mungu akufanikishe na akuongoze kwenye njia iliyo njema.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.