Ushiriki wa Wanawake Katika Baraza la Ushauri la Msikiti na Kutambulika Kura Zao.
Question
Liliundwa Baraza la Ushauri katika Msikiti wa Chuo Kikuu cha East Anglia Mjini Norwich, nchini Uingereza. Baraza hili lina baadhi ya wanawake Waarabu na Waingereza, na maamuzi hupitishwa katika Baraza hili kwa njia ya kupiga kura.
Je,inaruhusiwa kwa wanawake kupiga kura katika Baraza hili, au hairuhusiwi isipokuwa kwa wanaume tu?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Na kutokana na usawa huo kati ya mwanamume na mwanamke ni ushauri wao wa mambo ya umma na binafsi, mambo ya kidini na yasiyo ya kidini, na dalili ni nyingi, miongoni mwazo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu} [AT TAWBAH: 71]. Aya hii haipambanua kati ya wanawake na wanaume katika mambo hayo mawili, kupiga kura ni aina moja ya ushauri, kuamrisha mema na kukataza maovu.
Vile vile ahadi ya wanawake, ambapo walimwahidi Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W kuhusu kuinusuru dini katika nafsi zao, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Ewe Nabii! Watakapo kujia wanawake Waumini wanakuahidi ya kwamba hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatawauwa watoto wao, wala hawataleta uzushi wanao uzua tu wenyewe baina ya mikono yao na miguu yao, wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana nao ahadi, na uwatakie maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi maghfira, Mwenye kurehemu}[AL MUMTAHINAH: 12]. Pia wakati Mtume S.A.W alipomshauri mke wake Umu Salamah R.A kuhusu Mkataba wa upatanishi wa Al-Hudaibiah, na ushauri wa Asmaa binti Abi Bakr kwa mwanawe Abdullah Ibn Al-Zubair kuhusu juhudi zake kwa ajili ya Uislamu.
Miongoni mwa dalili hizi ni kwamba kumkataza mwanamke kupiga kura ni kama kumwamuru kuificha elimu yake na kukataza ushauri wake, na mambo mawili hayo ni maovu kwa mujibu wa Sheria na akili, na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na pale Mwenyezi Mungu alipofungamana na waliopewa Kitabu kuwa: Lazima mtawabainishia watu, wala hamtokificha, walikitupa nyuma ya migongo yao, na wakanunua kwacho thamani duni. Basi ni kiovu hicho walicho nunua}[AALI IMRAAN:187].
Inaeleweka kuwa waliopewa Kitabu ni wanaume na wanawake siyo wanaume tu. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema katika Hadithi yake kuwa: “Mwenye kuulizwa juu ya elimu akaificha, atafungwa mdomo na kifungo cha moto siku ya Qiyaamah” Hadithi hii imepokewa kutoka kwa Abu Dauud, At-Tirmidhiy, Ibn Majah, Ahmad, na Abu Hurairah, R.A. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema kuhusu kuhimiza juu ya kushauri kadiri unavyoweza na kwamba jambo hili miongoni mwa dini: {Hapana lawama kwa wanyonge, wagonjwa, na wasio pata cha kutumia, maadamu wanamsafia niya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hapana njia ya kuwalaumu wanao fanya wema.} [AT TAWBAH:91]. Basi kutokuwepo kwa lawama kwa wasiokwenda Jihadi pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa wanyonge na wagonjwa kwa sharti ya kumsafia niya Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W. Mtume S.A.W alisema: “Hakika dini ni nasaha, hakika dini ni nasaha, hakika dini ni nasaha, wakasema: Kwa nani? Akasema: “Kwa Mwenyezi Mungu, Kitabu Chake, Mtume Wake, kwa viongozi wa Waislamu na watu wa kawaida.” Hadithi hii imepokelewa kutoka kwa Muslim, Abu Dauud, An-Nasaai, Ahmad kutoka kwa Tamiim Ad-Dari R.A, At-Tirmidhi, An-Nasaai, na Abu Hurairah R.A.
Wakati usawa huu katika haki na wajibu ulipothibiti kwa Wanavyuoni wa Uislamu na wamefahamu Maandiko mengi ya kidini umejitokeza msingi maarufu sana ambao ni “Wanawake ni ndugu wa wanaume” Andiko hili ni Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa At-Tirmidhi, Ibn Majah, Ahmad, Abu Dauud, Ad-Darami kutoka kwa Aisha R.A, Al-Minyawi alisema kuwa Hadithi hii ina mapokezi ya Daraja la Hasan, pia imepokelewa kutoka kwa Abu Dauud, Ad-Darami, Abu Awnah, na Al-Bazzar kutoka kwa Anas R.A, Ibn Qahtan alisema Hadithi hii ina mapokezi ya Daraja la Sahihi.
Kama mmoja wao akidhani kwamba wanawake hawana elimu ya kuwawezesha kupiga kura katika mambo ya kisheria hasa, tutampelekea Mama wa Waumini Aisha R.A na madrasa yake ya kifiqhi ambayo Wanavyuoni wengi wamejifunza miongoni mwa wanaume, vile vile tutampelekea binti Said Ibn Al-Musaib, Karimah Rawit Al-Bukhari, na wengi ambao hawana idadi miongoni mwa wanawake wa Wanavyuoni katika Umma mtukufu.
Pia inafahamika kwamba miongoni mwa hekima za mitaala ya Mtume S.A.W ni kufikisha idadi kubwa ya wake zake watukufu wanavyosikia na wanvyoona kutoka kwa Mtume S.A.W kufuatana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu {Na kumbukeni yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za Mwenyezi Mungu na hikima. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya siri, na Mwenye khabari} [AL AHZAB: 34].
Kwa mujibu wa Swali hili na kwa mujibu wa yaliyotangulia hapo juu: Inaruhusiwa kwa mwanamke kupiga kura katika Baraza lililotajwa kama wanavyopiga kura hiyo wanaume.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi ya wote.