Kufaidika na Kodi Zinazopatikana Kutokana na Vitu vya Haramu
Question
Serikali ya Tailendi imeainisha sehemu maalum ya kodi zinazohusu uzalishaji na biashara ya pombe na sigara nchini humo, na kiwango chake ni asilimia mbili kila mwaka, kwa ajili ya kuanzisha na kugharamia idara maalum iitwayo: (Mfuko wa kuimarisha Afya ya Umma). Idara hii inapiga vita kunywa pombe na kuvuta sigara katika jamii ya Tailendi, na imeigawanya bajeti iliyotolewa na serikali kwenda miji na kote vijijini nchini Tailendi, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya taifa, kwa lengo la kupunguza unywaji pombe na uvutaji sigara katika jamii.
Tatizo limetokea wakati Mfuko huu ulipotoa bajeti yake kwa jamii ya kiislamu ya nchini Tailandi; hapo ndipo ilipojitokeza hitilafu kuhusu: Je, bajeti hii ni halali au haramu? Kwani inajulikana kuwa kodi hii imechukuliwa hasa kutokana na uzalishaji na biashara ya pombe na sigara, na serikali haiweki bajeti hii miongoni mwa bajeti ya umma ili isije ikachanganya na aina nyingine za kodi.
Kwa hiyo baadhi ya waislamu wanaona kuwa hii ni haranu kwa sababu inahusiana na kazi haramu kisheria, na wengine wanaona kuwa ni halali kwa sababu nchi ya Tailendi si ya kiislamu, na haitazamiwi kuwa serikali yake inaweza kutekeleza kanuni za halali Na haramu kuhusu bajeti ya nchi; kwa kuongeza kuwa waislamu wasipoikubali, matatizo ya afya nchini humo yataongezeka.
Sasa je, nini hukumu ya kiislamu katika suala hili?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Fatwa yetu ni kama ifuatavyo: Kufaidika na kodi zinazohusu pombe na sigara inajuzu kisheria, na ushirikiano wa waislamu wa Tailandi na nchi nyingine katika jambo hili kwa ajili ya kuimarisha Afya ya Umma, na kupambana na unywaji wa pombe na uvutaji sigara pia inajuzu kisheria, na hakuna uharamu wowote ndani yake, kwa sababu zifuatazo:
1- Kuna tofauti kubwa kati ya thamani ya pombe na kodi inayoihusu, kwani thamani ya pombe ni: Mali inayolipwa kwa ajili ya kupata bidhaa hii yenye uharamu, na pombe ni haramu kwa kauli ya pamoja ya waislamu, na bei yake ni haramu kwa kauli ya pamoja ya waislamu katika nchi za kiislamu, kwa hiyo, haijuzu kuinunua wala kuiuza wala kuchukua thamani yake kati ya waislamu.
Kuhusu kodi kama inavyofafanuliwa na wanauchumi ni kuwa: Makato ya lazima ambayo nchi huyatoza kutoka katika mapato ya mashirika mbali mbali ya kiuchumi, kwa lengo la kukabiliana na mahitaji ya umma pamoja na kugawanya mahitaji haya kati ya mashirika yanayotajwa, kutokana na uwezo wake wa kulipa, yaani: Ni kiasi maalum cha mali ambacho dola hukitoza katika mali za raia wake, wawe ni watu wa kawaida au wa vyovyote vile, na kodi huwa inawekwa kwa miliki, kazi, mapato, aina zote za biashara, mashirika na maeneo mengine yenye kujiingizia pato ili kuimarisha huduma mbalimbali kwa raia. Na kodi hii ina tofautiana kutokana na sheria na hali. Serikali zote ulimwenguni zinafanya hivyo kwa ajili ya kukabiliana na matumizi na mahitaji ya lazima kwa wananchi, kwa kuzingatia kuwa huduma zote kwa umma zinahitaji malipo yanayoambatana na mapato imara, hasa katika enzi hizi ambapo nchi ina majukumu mengi ya kiraia, na nyanja zote zimepanuka.
Na hapo ndipo inapobainika kuwa: Kodi ya biashara ni haki ya kiraia inayotozwa kwa kiasi cha mapato ya kibiashara, na siyo bei ya bidhaa ambazo ni vyombo vya biashara; na kwa hivyo basi, hakuna uhusiano wowote kati ya kodi na kuwa bidhaa ni halali au haramu, na kwa hiyo kodi ya pombe na sigara siyo bei ya bidhaa hizi, na kufaidika nayo si haramu.
2-Kodi hizi zinapoingia Hazina ya Dola huwa zinakuwa miongoni mwa miliki yake na sehemu ya bajeti na mapato yake. Na iwapo mtu atasema kuwa: Kodi hizi ni haramu, kauli hii pia haiharamishi kufaidika nazo, kwa sababu huwa zinachanganywa na mapato mengine, na hazitenganishwi nayo, na hivi sasa njia mbadala kati inayotumiwa na watu ni Noti ambazo haziainishwi kwa sifa zake zenyewe, kwa sababu thamani yake ni katika nguvu yake ya kununua, wala si katika sifa zake zenyewe, na inayopendekezwa kisheria kuwa uharamu usipoainishwa huwa unakuwa halali, na wanachuoni wametaja kuwa: Haramu haiambatani na dhima mbili, na maelezo ya halali na haramu ndiyo yanayoambatana na watu, na siyo ya vitu na visivyokuwa hai.
Mtaalamu Ibn Abidiin mfuasi wa Madhehebu ya Hanafiy katika kitabu cha: [Raddel-Muhtaar Ala Durel-Mukhtaar: 2/292, Ch. ya Dar Al-Fikr] anasema: “Katika Hashiyat Al-Hamawiy na Adhakhira: Mwanachuoni Abu-Jaafar aliulizwa kuhusu mtu aliyechuma mali yake kutoka kwa wasaidizi wa Sultani na akakusanya mali hiyo kutokana na tozo haramu na vinginevyo, je inajuzu kwa aliyejua hivyo kula chakula chake, akajibu: Napendelea asile, lakini kwa njia ya hukumu inajuzu kukila chakula chake, sharti chakula hicho kisiwe kimepatikana kwa njia ya unyang'anyi au rushwa. [Mwisho].Yaani isipokuwa unyang'anyi au rushwa kama vilivyo; kwa sababu yeye hakuvimiliki, kwa hiyo vimekuwa haramu vyenyewe kama vilivyo, na kwa hiyo basi, havijuzu kwake yeye mwenyewe wala kwa mtu mwingine yeyote.
Imetajwa katika Al-Bazzaziyah kuwa: Asiyejuzu kwake kuchukuwa sadaka, ni bora kwake asichukue tuzo ya Sultani, kisha akasema: Mtaalamu wa Khuwarazm alikuwa hali chakula chao, lakini akapata tuzo zao, na alipoulizwa Na hizi tuzo inakuaje? Alijibu na akasema: Kutoa chakula ni hiari, na mwenye kukila anakitumia kama ni miliki ya mtoaji, na kwa hivyo basi, anakula chakula cha dhalimu. Lakini tuzo ni miliki kwa aliyepewa, na kwa hivyo basi anaitumia kama miliki yake. [Mwisho]. Mimi ninasema: Pengine rai hii imejengwa juu ya kauli isemayo kwamba: Haramu haizidi dhima mbili. [Mwisho].
Mwanazuoni Ibn Muflih, mfuasi wa madhehebu ya Hanbali katika kitabu cha: [Alfuruu’: 4/390, Ch. ya Muassasat Ar-Risalah] anasema: “Wengi waliipokea Hadithi kutoka kwa Ath-Thauriy, kutoka kwa Salamah bin kuhail, kutoka kwa Dhar bin Abdillahi, kutoka kwa Ibnu Masu’ud RA, kuwa mtu mmoja alimwuliza: Nina jirani anayekula Riba, na kila mara amekuwa akinialika chakula, akasema: “Manufaa ya chakula ni kwako, lakini dhambi anaipata yeye”.
Ath-Thauriy anasema: “Ukikiainisha chakula basi usikile”, na muradi wa ibn Masuud na maneno yake havipingani na hukumu hiyo.
Wengi waliipokea Hadithi kutoka kwa Ma`mar, kutoka kwa Abi-Ishaaq, kutoka kwa Zubairbin Al-Khirrit, kutoka kwa Salman RA, anasema: “Ukiwa na rafiki mwenye madaraka, akakualika chakula, basi kile, hakika manufaa ya chakula hicho ni yako, lakini dhambi ni yake”.
Ma’mar anasema: “Adiy bin Artaa ambaye ni liwali wa Basrah alikuwa akimpelekea Hassan chungu cha uji kila siku, na Hassan alikuwa akiunywa uji huo, na kuwanywesha pia marafiki zake, pia alikuwa akimpelekea Shaabiy na Ibn Siriin na Hassan, na Hassan na Ibn Siriin waliupokea na kuunywa, lakini Shaabiy aliukataa”.
Hassan aliulizwa kuhusu chakula cha wabadilishaji fedha akasema: “Mwenyezi Mungu alikuambieni kuhusu manasara na mayahudi kuwa wanakula riba, na alikuhalalishieni chakula chao”.
Mansuur anasema: Nilimwambia Ibrahim Al-Lakhmiy kuhusu mkubwa wetu ambaye alikuwa dhalimu, na yeye alikuwa ananialika mara kwa mara, na mimi nilikuwa nikiukataa mwaliko wake, na Ibrahim akasema: “Shetani ana lengo la kuwawekea uadui baina yenu, na maliwali walikuwa wanafanya hivyo, wakialika, mialiko yao inakubaliwa, kisha akanihalalishia, kwa kusema: Kubali mwaliko huo. Mimi nikamwambia: Akiwa mla Riba je? Yeye akasema: Kubali usipomwona yeye mwenyewe”. [Mwisho].
3-Kodi hizo zinazolipwa kwa biashara ya pombe na sigara ndizo zitakazotumiwa katika kupambana na unywaji pombe, na njia hii mpya inayopelekea kupunguza maovu ya unywaji pombe ni ya kisheria. Na kurekebisha upeo wa kuyaeneza maovu hayo, na kila ilipozidi maenezi na kuuza kwake, itazidi pia matumizi ya fedha kwa ajili ya kuzipigania na kupunguza kunywa kwake. Kwa hiyo hii ni njia nzuri na ya kiutendaji katika kukataza mabaya, na Sheria ya kiislamu iliamuru kuzuia mabaya kwa mbinu mbali mbali, na mbinu hizo ni nyingi, na ambazo hubadilika kwa mabadiliko ya zama, sehemu, mazingira na mila na desturi za watu. Na inaamuliwa kuwa mbinu zina hukumu za makusudio.
4-Kodi hata zikiwa haramu, lakini inajuzu kuzitumia katika masilahi ya umma; na wanachuoni walitaja kuwa mali haramu inajuzu kuitumia katika masilahi ya umma, na inafahamika kuwa kupambana na unywaji wa vitu haramu ni upeo juu wa masilahi ya umma; kwa sababu kupambana huko ni kulilinda kusudio muhimu miongoni mwa makusudio Makuu ya Uislamu, nalo ni kulinda akili ambayo ni umbile la binadamu. Na wanachuoni walitaja mifano ya masilahi ya umma kama vile: kujenga kivuko/daraja, barabara na mengineyo, na bila shaka kumjenga binadamu ni muhimu zaidi kiutu kuliko kuyajenga majengo.
Imamu An-Nawawiy, mfuasi wa madhehebu ya Shafi katika kitabu chake [Al-Mjmuu’ Sharhul-Mhuadhab: 9/352, Ch. ya Dar Al-Fikr]: “Al-Ghazaliy anasema: Mtu akiwa na mali ya haramu, na akitaka kutubu na kujiepusha nayo, ikiwa mali hiyo ni ya mtu maalumu basi lazima amrudishie mtu huyo, au mwakilishi wake. Na kama mwenye mali akiwa amekufa basi amrudishie mrithi wake. Lakini mali hiyo ikiwa ya mtu asiyejulikanwa na hakuna uwezekano wa kumjua, basi ni bora kuitumia mali hiyo katika masilahi ya umma wa kiislamu, kama vile: kujenga daraja, nyumba za mafakiri, misikiti, kutengeneza barabara za kwenda Makkah, na mifano ya hayo ambayo waislamu wanahusika nayo, au aitoe kama sadaka kwa mafakiri. Na akimpa fakiri, haitakuwa haramu kwake, bali ni halali na ni nzuri. Na inajuzu kwake kuitumia yeye mwenyewe na kwa watoto wake, akiwa fakiri, ambapo watoto wake wana sifa ya ufakiri, na kwa hivyo wao wana haki zaidi kuliko watu wengine. Na kuhusu yeye mwenyewe, atachukuwa kadiri ya haja yake, kwani yeye pia ni fakiri”.
Na hivi ndivyo ilivyosemwa na Al-Ghazaliy katika mlango huu, imetajwa pia na wengine miongoni mwa wanachuoni. Na hivi ni kama walivyoisema. Na Imamu Ghazali amenukuu na Muawiyah bin Abi-Sufiyan na wengineo miongoni mwa Salaf, kutoka kwa Ahmad bin Hanbal, Al-Hariyh Al-Muhasabiy, na wengineo miongoni mwa wachamungu; kwa sababu haijuzu kuharibu mali hii na kuitupa baharini, lakini ni kuitumia katika masilahi ya waislamu.
Al-ghazaliy anasema: Mtu akipata mali ya haramu na mikononi mwa Sultani, baadhi ya wanachuoni walisema: Amrudishie Sultani; kwani yeye anajua zaidi anavyovimiliki. Na wala hawezi kuitoa mali hiyo kama sadaka. Na wengine walisema: Aitoe kama sadaka hasa akijua kuwa Sultani hatamrudishia mwenye mali.
Nasema kuwa: Rai iliyochaguliwa ni kuwa akijua kuwa sultani ataitumia katika njia batili, au alikuwa na dhana hii kwa uwazi, basi lazima aitumie yeye mwenyewe katika masilahi ya waislamu, kama vile kujenga daraja n.k. Lakini akishindwa kufanya hivvyo au kuwa na shida kwa kumwogopa mtu yeyote, basi ni bora aitoe kama sadaka kwa anayehitaji” . [Mwisho].
Licha ya hayo, wafuasi wa madhehebu ya Hanbal, na Dhahiri wanaona kuwa: kukubali mali ya haramu ambayo imetolewa na mwenye mali ni wajibu; kwa sababu ni kushirikiana katika mema na mazuri.
Mwanazuoni Ibn muflih, mfuasi wa madhehebu ya Hanbali anasema katika [Al-Furuu’ : 4/398]: “Akiitoa kama zawadi kwa mwingine, huyu lazima akubali zawadi; kwa kuwa ni kushirikiana katika mema na mazuri, na kurudisha ni kushirikiana katika dhulma na uadui, lakini anaweza kuitoa kwa mwenye mali au mrithi wake, au kumpa hakimu au kuitoa kama sadaka, kuna tofauti, na huu ni mfano wa alivyotaja Ibn Hazam, na akaongeza: Akiirudisha amefanya maasi, na kama akijua mwenye mali basi maasi yake yanazaidi, na atafanya dhambi kubwa zaidi, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yote”. [Mwisho].
5-Ilivyoamuliwa kisheria ni kuwa: Inajuzu kukubali zawadi na tuzo kutoka kwa wasio waislamu; kwa sababu kimsingi, uhusiano kati ya waislamu na wengineo ni kuishi pamoja kama katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenyezi Mungu hakukatazeni kuwafanyia ihsani na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini wala hawakukufukuzeni katika nchi zenu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao uadilifu}. [AL MUMTAHINAH: 8], na hii inakusanya aina zote za uhusiano wa kibinadamu kama vile: kushikamana na kushirikiana kwa kuchukua au kutoa, na ni sawa sawa iwe kwa mtu binafsi au wengi.
Sunna ya Mtume S.A.W, iliamua kukubali zawadi za wasio waislamu: kutoka kwa Ali R.A alisema: “Kisra Mfalme wa Waajemi alimpatia Mtume S.A.W zawadi, na Mtume S.A.W, akaiikubali. Na Qaisar Mfalme wa Warumi alifanya hivyo, na Mtume S.A.W, akaikubali. Vile vile Wafalme wengi walitoa zawadi na Mtume S.A.W, akazikubali”. [Hadithi hii imepokelewa na Ahmad na At-Tirmidhiy, na huyu amesema:ni Hadithi yenye hukumu ya Hassan.
Na kutoka kwa Anas bin Malik R.A, kuwa: “Mfalme wa Duma alimpa Mtume S.A.W, juba la Hariri nzito”. Muttafaq.
Na kutoka kwake pia amesema kuwa: Mfalme wa Dhi-Yazan alimpa mtume S.A.W, vazi ambalo thamani yake ni ngamia thelethini na watatu, na Mtume S.A.W, akalikubali”. [Ameipokea Hadithi hii Abu-Dawuud].
Na kutoka kwa Amir bin Abdillahi bin Zubair alisema: “Qutailah binti ya Abdil-Uzaabin Abdi-Asa’d, kutoka kwa Bani-Malik bin Hasal alikuja kwa binti yake Asmaa binti ya Abu-Bakari RA, kwa zawadi za nyama, jibini, na samli, na Qutailah alikuwa mshirikina, na Asmaa akaikataa zawadi yake na pia kumwingiza nyumbani kwake, basi Aisha akamwuliza Mtume S.A.W, kuhusu hali hiyo, na hapo Mwenyezi Mungu akateremsha: {Mwenyezi Mungu hakukatazeni kuwafanyia ihsani na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini}, mpaka mwisho wa Aya. Hapo Mtume S.A.W, akamwamuru Asmaa akubali zawadi ya mama yake na kumwingiza nyumbani kwake”. [Ameipokea Hadithi hiiAhmad].
Pia wanachuoni walitoa dalili ya kukubali Mtume S.A.W, zawadi ya Salman Al-Farisiy R.A, kabla hajasilimu; Al-Hafidh Al-Iraqiy katika kitabu cha: [Tarikh At-Tathriib: 4/40, Ch. ya Dar Ihiyaa’ At-Turaath Al-Arabiy] anasema: “Ndani yake ni kukubali zawadi ya kafiri; kwa kuwa Salman R.A, alikuwa hajasilimu bado, hakika alisilimu baada ya kujua alama tatu alizozijua miongoni mwa alama za Unabii”. [Mwisho].
6-Wanachuoni walitaja kuwa: mwislamu anakubali kuwa na deni kutoka kwa kafiri, hata ikiwa deni hilo ni kwa thamani ya pombe, kwa kuwa kuuza pombe ni sahihi kwa kafiri, na hii inamaanisha kuwa: inajuzu kukubali zawadi yake hata kama ikiwa imetokana na thamani ya haramu aliyoiuzia.
Imamu Haskafiy, mfuasi wa madhehebu ya Hanafiy katika kitabu cha: [Ad-Durul Muktaar: 6/385, Ch. ya Dar Al-Fikr] anasema: “Inajuzu kuchukua deni kutoka kwa kafiri, asili yake ya thamani ya pombe; kwa usahihi wa kuuza, kinyume cha deni la mwislamu, kwa ubatili wake, isipokuwa mwislamu anamwakilisha asiye mwislamu katika kuuza, basi inajuzu kwa rai yake, kinyume cha rai ya wengine”. [Mwisho].
7-Inayotolewa fatwa katika zama hizi ni, mwelekeo wa madhehebu ya wafuasi wa hanafiy, kuwa: Inajuzu kuamiliana/kutendeana kwa mikataba isiyo sahihi na wasio waislamu katika nchi za waislamu; ambapo Maimamu Abu-Hanifa na Muhammad wanaona kuwa: hakuna Riba kati ya mwislamu na asiye mwislamu katika nchi zisizo za kiislamu, na kuwa mwislamu katika nchi hii ana haki ya kuchukua mali zao kwa njia yeyote iwayo; hata kama ni kwa mkataba usio sahihi kama vile; kamari, kuuza nyamafu, au Riba n.k, kwa kuwa tu ni kwa maridhiano ya nafsi zao.
Imamu Muhammad bin Al-Hassan Ash-shaibaniy anasema:
“Mwislamu akiingia nyumba ya vita (nchi ya Adui) kwa mkataba wa amani, hakuna kosa kuchukua mali zao kwa kuridhiana nao kwa njia yo yote iwayo, kwa sababu yeye amechukua mubaha kwa njia iliyo mbali na hadaa, kwa hiyo itakuwa njema kwake, na mfungwa na mwenye ahadi ya amani ni mamoja, hata akiwauzia Dirham moja kwa Dirham mbili, au kuwauzia nyamafu kwa Dirham, au akichukua mali zao kwa njia ya kamari, basi vyoyote iwavyo ni vyema kwake”. [Mwisho]. Hii imenukuliwa na Hashiyat ya Mtaalamu Ibn Abidiin (Radul-Muhtaar Ala Ad-Duril-Mukhtar: 5/186].
Hakika Imamu Muhammad na wengineo waliita nchi zisizo za waislamu kuwa ni nyumba ya vita kutokana na mgawanyo uliokuwepo katika zama za maimamu tunaowanukulu hukumu hii, ambapo ulimwengu wote ulikuwa ukipambana na waislamu, hivyo wanachuoni walizigawanya nchi zote ziwe aina mbili: nyumba ya uislamu ambapo unasimamishwa uislamu na maamrisho yake yanatekelezwa, na nyumba ya vita ambapo hukumu za waislamu hazitekelezwi.
Lakini mgawanyo wa kisasa wa wanachuoni wa Uislamu baada ya hali ya vita vinavyochochewa dhidi ya waislamu baada ya kumalizika ni nchi za waislamu na nchi zisizo za waislamu, na hukumu zake ni zilezile za nyumba ya vita, isipokuwa mambo yanayohusu vita vyenyewe, ambapo havipo kwa sasa, basi lazima tuangalie hivi.
Hivyo tuzingatie maana ya maneno ya wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy kuwa: Maana ya nyumba ya vita ni nchi zisizo za waislamu, ni sawa pawepo vita au la, na dalili yake kuwa hoja zao nyingi zilihusiana na nyumba ya ukafiri bila ya kuwepo vita, yaani wanakusudia Makkah kabla ya Al-hijrah, kama itakavyokuja, na haikuwepo nyumba ya vita ulimwenguni kote, na lengo la dalili ni kushirikiana na uwajibikaji wa hukumu kwa pamoja.
Imamu As-Sarkhasiy, mfuasi wa madhehebu ya Hanafiy katika kitabu chake cha: [Al-Mabsuut: 14/98, Ch. ya Dar Al-Fikr], baada ya kutaja Hadithi Mursal ya Makuhuul anasema: “Hakuna riba kati ya waislamu na watu wa nyumba ya vita katika nyumba ya vita”: na kuhusu Hadith Mursal ya Makuhuul ni dalili kwa Abi-Hnifa na Muhammad, Mwenyezi mungu awarehemu, kuwa inajuzu kwa mwislamu kumwuzia kafiri dirham moja kwa dirham mbili katika nyumba ya vita..Vile vile akiwauzia nyamafu au akacheza kamari nao, na akachukua mali zao kwa njia hiyo, na mali hii ni halali, kwa mtazamo wa Abi-hanifa na Muhammad, Mwenyezi Mungu awarehemu”. [Mwisho].
Na kauli za maimamu wawili Abi-Hanifa na Muhammad ndiyo inayotegemewa na kuchaguliwa na wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy.
Imamu As-Sarkhsiy baada ya matini yake iliyotangulia [14/100] anasema: “Hoja ya wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy ni Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abbas RA na wengineo kuwa Mtume SAW alisema katika hotuba yake: “Kila riba iliyokuwa katika wakati wa ujahili sasa imetenguliwa, na riba ya kwanza kutenguliwa ni riba ya Al-Abbas ibn Abdel-Muttalib”, hivyo kwa sababu Al-Abbas R.A baada ya kusilimu, akarejea Makkah na alikuwa anakula riba, na tendo lake hili halifichiki kwa Mtume S.A.W, na Mtume S.A.W hakumkataza, na hii ni dalili ya kujuzu. Kuhusu riba iliyotenguliwa nayo ni riba ambayo haikukabidhiwa hadi wakati wa kufungua Makkah na - ikawa nyumba ya Uislamu-, na hii ni kauli yetu.
Wanachuoni wa madhehebu ya hanafiy walitoa dalili ya maoni yao kama zifuatazo:
1- Kama Ilivyopokelewa katika Hadithi ya Makuhuul kutoka kwa Mtume SAW: “Hakuna riba kati ya waislamu na watu wa nyumba ya vita katika nyumba ya vita”, As-Sarkhasiy anasema katika kitabu cha: [Al-Mabsuut; 14/98]: “Ikiwa Hadithi hii ni Mursal, basi Makuhuul ni mjuzi na mwaminifu, na Hadithi Mursal kwa upande wake ni kukubaliwa”.
2- Imamu Muhammad, Mwenyezi Mungu amrehemu, alitoa dalili ya Hadithi ya Bani-Qainuqaa’, ambapo Mtume S.A.W aliwahamisha, walisema: “Tuna madeni na bado hatujapokea”, akasema: “Zichukueni upesi au ziacheni”, na ambapo aliwahamisha Bani-Nadhiir walisema: “Tuna madeni kwa watu”, akasema: “Ziacheni au zichukueni upesi”.
Imamu As-sarkhasiy alibainisha maana ya dalili katika [Sharhus-Siyar Al-kabiir: 4/184-185, Ch. ya Dar Al-kutub Al-Ilmiyah]: kuwa: “Inajulikana kuwa matendeano kama hayo, yaani Riba, iliyopo katika kauli yake Mtume SAW: “Acheni au pokeeni upesi” hayajuzu kati ya waislamu, kwa sababu mwenye deni kwa mwingine kwa muda maalum haijuzu kuiacha sharti apokee baadhi yake upesi, kwa kuwa Umar, zaid ibn Thabit na Ibn Umar R.A walichukia hivi, lakini Mtume SAW alijuzisha kwa mayahudi kwa sababu wao ni watu wa vita katika wakati huu, kwa hiyo aliwahamisha, hivyo tulijua kuwa inavyojuzu kati ya kafiri na mwislamu haijuzu kati ya waislamu wenyewe kwa wenyewe”. [Mwisho].
3- Na ilivyotokea katika kupigana mieleka kwa Mtume S.A.W na Rukanah alipokuwa katika Makkah, na Mtume S.A.W alimshinda, kila mara kwa theluthi ya kondoo wake, na lau tendo hilo ni la kukatazawa basi Mtume S.A.W asingelifanya, na Mtume alipomshinda kwa mara ya tatu Rukanah alisema: “Hakuna yeyote aliyeweza kunishinda na hata wewe hukuweza”, lakini Mtume S.A.W alimrudishia kondoo wake. Imamu As-sarkhasi katika [Sharhus-Siyar Al-Kabiir: 4/184] anasema: “Hakika Mtume SAW alirudishia kondoo kwa njia ya kufadhili, na Mtume S.A.W alifanya hivi siku zote na washirikina ili awapendezesha akawavutia ili waingie Uislamu”. [Mwisho]. Na haifichiki kuwa Makkah katika wakati huu haikuwa nyumba ya vita bali ilikuwa nyumba ya ukafiri.
4- Na Hadithi aliyoisema Mtume S.A.W, na ile iliyopokelewa na Ibn Abbas R.A na wengineo kuwa Mtume S.A.W, anasema: “Hakika kila kitu cha mambo ya ujahili kimetenguliwa na kimo chini ya miguu yangu miwili, na Riba ya ujahili ni ya kutenguliwa, na riba ya kwanza nina ya tengua ni Riba ya Al-Abbas in Abdel-muttalib nayo ndiyo ya kutenguliwa kwa jumla”.
Upande wa dalili katika Hadithi hii kuwa: Al-Abbas R.A baada ya kusilimu alipokuja mateka katika vita vya Badr, wakati alimuomba ruhusa Mtume S.A.W arejee Makkah baada ya kusilimu, na Mtume alimpa ruhusa, na Al-Abbas alikuwa anakula riba katika Makkah mpaka wakati wa kuifungua, na tendo lake hili halifichiki kwa Mtume S.A.W, na kwa kuwa Mtume hakumkataza basi ni dalili ya kujuzu, hivyo riba iliyotenguliwa katika nyumba ya vita ni ile haikuchukuliwa mpaka wakati wa kuifungua Makkah, na ikawa nyumba ya Uislamu, kwa hiyo Mtume S.A.W alitengua Riba wakati wa Kuifungua Makkah.
5- Kwa kuwa Abu-Bakr R.A alicheza kamari na washirikina wa Quraish kabla ya Al-Hijrah wakati Mwenyezi Mungu alipoteremsha kauli yake: {Alif Lam Mym. Warumi wameshindwa}.Aya hii…, Quraish walimwambia: Waona kuwa Warumi watashinda? Akajibu: Naam, wakasema: Unakubali kuweka rehani? Akajibu: Naam, hapo wakapigana rehani, akamwambia Mtume S.A.W, Mtume akamwambia: “Waendee, uzidishe kiasi cha rehani”, akazidisha, kisha Warumi walishinda Waajemi, Mtume S.A.W alijuzisha hivi, na hii ndiyo ni kamari yenyewe iliyopo kati ya Abu-Bakr na washirikina wa Quraish, na Makkah katika wakati huo ilikuwa nyumba ya ushirikina, pia haifichiki kuwa Makkah katika wakati huo haikuwa nyumba ya vita, kwa sababu tokeo hili lilitokea kabla hata kutunga sheria ya Jihaad.
6- Kwa sababu mali ya makafiri ni halali, basi mwislamu ana haki ya kuichukua bila ya hadaa kwani hadaa ni haramu.
Kwa mujibu wa maelezo hayo: Inajuzu kuzitumia mali hizi ambazo zinachukuliwa kama kodi ya pombe na sigara katika (mfuko wa kuimarisha Afya ya Umma) ambao unapambana na unywaji wa pombe na uvutaji sigara katika jamii ya Tailendi.
Na hakuna uharamu kuhusu ushirikiano wa waislamu kwa njia ya Sheria, kwa sababu kuitumia mali katika kazi hizi ni miongoni mwa ushirikiano kwa mema, na kazi ya kiutendaji katika kuzuia mabaya, kwa njia ya kuwafahamisha wananchi madhara ya vitu hivi vya haramu, pia ni ushirikiano wa kivitendo wa waislamu katika jamii yao, bila ya ugomvi usio na sababu, kuchangia kwao katika kupambana na kuuondoa ufisadi, na kuthibitisha mema ambayo Dini Tatu zimeyaasisi. Na wote wenye akili wamekiri. Na hakuna sababu yeyote ya kuharamisha hivyo.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.