Hukumu ya kukumbatiana kwa Mwanamke...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kukumbatiana kwa Mwanamke na Mwanaume wasio ndugu wa damu.

Question

Mimi ni mwanamke kutoka Marekani na ninaishi Ulaya, nina ndugu wengi. Tangu nilipoingia Uislamu ninapata ugumu wa kuwaelezea watoto wa mjomba wangu kuwa siruhusiwi kukumbatiana nao. Ninatarajia mnifahamishe hukumu ya Sheria katika suala hili. 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Hakuna kikwazo chochote katika kuamkia na kupeana mikono kwa ajili ya kukaribishana tu, kama hakuna matamanio na fitina. Dalili ya hayo ni Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Al-Bukhari kutoka kwa Anas Ibn Malik R.A. alisema kuwa: “Mjakazi mmoja miongoni mwa wajakazi wa Madinah alikuwa akimchukua Mtume kwa mkono wake mpaka anapomfikisha mahala anapotaka”.
Na katika mapokezi mengine kutoka kwa Imam Ahmad, kutoka kwa Anas pia alisema: “Mjakazi mmoja kati ya vijakazi wa Madinah alikuwa akimchukuwa Mtume kwa mkono wake naye Mtume hakuwa akiutoa mkono wake mpaka wanapofika mahala anapopataka.” Mtazamo huu ni kwa mujibu wa walivyosema Wanavyuoni wa siku hizi.
Imepokelewa kutoka kwa Imam Ahmad kuwa inachukiza sana kupeana mikono kati ya wanaume na wanawake. Al-Bahwati aliusema mtazamo huu katika kitabu cha Kashaf Al-Qinaa [2/154, 155, Darul Kutub Al-Ilmiyah]: “Imam Ahmad alisema katika mapokezi ya Ibn Mansur:- "Inachukiza kupeana mikono kati ya wanaume na wanawake".
Wengi wa Wanavyuoni – isopokuwa Wanavyuoni wa madhehebu ya Imam Shafi – hawaruhusu kupeana mikono kati ya wavulana na wasichana, ambapo Wanavyuoni wa madhehebu ya Imam Shafi wameruhusu hivyo kwa masharti mawili: kutokuwepo kwa fitina, na kuwepo kwa kikwazo. [Rejea: Tabiin Al-Haqaiq 6/18 Darul Kitab Al-Islami, Hashiyatul Sawi ala Sharhul Saghiir 4/760, Darul Maarif, Nihayatul Mihtaj 6/191, 192, Darul Fikr].
Kama kuna haja ya kukaa wanaume na wanawake pamoja, na hakuna fitina baina yao, basi hakuna ubaya wowote wa kupeana mikono kati yao kama kuna dharura; kama vile ya aliyerudi kutoka safarini, na kama jamaa akimzuru mmoja wa jamaa zake, nk.
Mola wetu ametukataza tusikaribie mambo machafu kama alivyosema: {Wala msikaribie mambo machafu, yanayoonekana, na yanayofichikana.}[AL ANAAM: 151]. Na miongoni mwa kukaribia mambo hayo ni kufanya mambo yanayoyapelekea kuyafikia, na hakuna shaka kuwa kukumbatiana kwa mwanamke na wanaume wasio maharimu (ndugu) zake ni kutokana na sababu za kiuasi zinazopelekea mambo machafu.
Ama kuhusu kukumbatiana na kubusu kati ya mwanamke na wanaume wasio (ndugu) maharimu – kama watoto wa mjomba – basi ni haramu kwa mujibu wa maafikiano ya Wanavyuoni, kwa sababu hao sio (ndugu) maharimu kwa mwanamke, naye siye maharimu kwao. Na kumkumbatia inadhaniwa kuwa - kunasababisha matamanio na ufisadi, na msingi wa kifiqhi unasema kuwa kinachodhaniwa ni sawa na kilicho kweli.
Na kama ukiwajulisha kuwa sababu za kukataza vitendo hivi ni za kidini, basi pengine wataheshimu hivyo na watajizuia.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

 

Share this:

Related Fatwas