Toba ya kweli.

Egypt's Dar Al-Ifta

Toba ya kweli.

Question

Ni nini Toba ya kweli? 

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Neno “Toba” kilugha lina maana ya “Kurejea”, mfano, mtu amerejea makosa yake na kujivua nayo”. Na iwapo mja atarejea kwa Mwenyezi Mungu, ina maana kuwa, huruma ya Mwenyezi Mungu na upole wake upo juu ya mja huyo kwa kuwa amerudi kwake. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema {na wakayakinika kuwa hapana pa kumkimbia Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwake Yeye. Kisha akawaelekea kwa rehema yake ili nao waendelee kutubu. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu} [AT TAWBAH, 118]
Ama katika istilahi, Toba maana yake ni: Kujutia na kujivua na maasi, kwa kuwa ni maasi na si kwa ajili ya kuwa na madhara ya kimwili au katika mali, na kuwa na nia ya kutorudia tena kadiri mja awezavyo. Na wengine wakasema, ni kurudi kutoka katika njia iliyopinda na kwenda katika njia iliyo sahihi.
Imam Ghazali amesema; kujua ukubwa wa kosa, na majuto, na kuwa na nia ya kuacha pale ujuapo kosa hilo, na kutolirudia tena baadae.
Kupitia istilahi hizo pamoja na kuwapo tafauti kimaelezo, lakini lengo lake ni moja. Pia kuomba Toba inasemwa ni ile hali ya kujutia pekee, kwani kufanya hivyo utakuwa kama kwamba umeshajua kosa lako na hutofanya tena, na kwa ajili hiyo Mtume (Rehma na amani zimshukie) anasema “Kujuta ni kuomba Toba” (Imetolewa na Ahmad katika kitabu chake na Ibn Majah). Na kujutia ni kule kuuhuzunisha moyo wako kwa kujuta kuwa usingelifanya kosa hilo.
Toba inatokana na makosa na ni wajibu kisheria tena kwa haraka sana. Haya ni maafikiano ya Wasomi. Kwani ni katika misingi muhimu ya kiislamu na nguzo ya Dini, na ni njia ya mwanzo ya wachamungu. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema {Natubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa} [AN NUR 31].
Toba ni hali ya kuihakiki nafsi na ni uchunguzi wa ndani na kuirudi nafsi. Maneno kama haya ya uhakiki wa nafsi na kuirudi nafsi hiyo na uchunguzi wa ndani wa nafsi itaonekana kama kwamba hayana uhusiano na kutubu kwa mja, kwa kuwa ufahamu wa wengi ni kuwa neno “Toba” ni ile hali ya kuacha maasi tu na si vyenginevyo; lakini ukweli ni kuwa Toba ni sifa ya kiroho na kimoyo iliyomo ndani ya mwisilamu mwenye pupa juu ya mambo ya Dini yake.
Na kutubia kwa Mwenyezi Mungu ni mfungamano kati ya mja na Mwenyezi Mungu, Mola wake, baada ya kulirudia kosa kwa mara nyengine, kwani kutofanya kosa haiwezekani kwa yeyote, kwani hilo ni jambo pekee ambalo Mwenyezi Mungu huwahusisha awatakao. Kwa ajili hiyo, Mwenyezi Mungu akaweka Toba. Katika Toba kuna msaada, nao ni kumtaka Mwenyezi Mungu akusaidie kwa kukusamehe, kisha uweze kurudi katika njia iliyo sahihi na kuchunga mwenendo wako ili usije kuivunja ahadi ya kutorejea tena makosani, na kutoacha kumuomba Mwenyezi Mungu akusaidie ili uweze kufanikisha jambo hilo.
Na mwanadamu anahitaji kutubu kila siku, kwani Mwenyezi Mungu ameamrisha Toba maalumu, nayo ni ile ya kweli akasema; {Enyi mlio amini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati yake, siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Nabii na walio amini pamoja naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za kulia, na huku wanasema: Mola wetu Mlezi! Tutimilizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kilakitu.}(AT TAHREM;8)
Na wanazuoni wametafautiana juu ya Toba ya kweli. Na kauli iliyo maarufu ni ile iliyopokelewa na Omar na Ibn Masuud na Abi Kaabna Muadh Bin Jabal – Mwenyezi Mungu awawie radhi – Na imepokelewa kutoka kwa Muadh kuwa Mtume (Rehma na amani zimshukie) amesema: “Toba ya kweli ni kujutia mkosaji juu ya dhambi ambayo mja ameitenda. Anatubia kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kisha harudii tena kosa au makosa yake kama isivyowezekana kwa maziwa kurejea tena katika chuchu.” (Ameitaja Twabary na Al aswbahaniy). Kwa kuwa toba ya kweli ni kutorejea makosa baada yake kama isivyowezekana kwa maziwa kurudi tena katika chuchu ya (mnyama). Pia imesemwa kuwa: Toba ni majuto ya moyoni, na utubiaji wa mja ni kwa ulimi, na kujivua makosa na kuwa na matumaini kuwa mja huyo kamwe hatayarudia tena.
Hivyo, hapana budi ya kutubu kila siku, kwani kufanya hivyo kuna manufaa mengi ya kumyanyua mwanadamu na kumtakasa kutokana na udhalili. Na Mtume wetu S.A.W, ametupigia mfano mzuri wa kudumu katika hali ya kutubu kwa Mwenyezi Mungu, ingawa hakuwa amefanya kosa, kwani yeye amelindwa na Mola wake, amesema Mtume (Rehma na amani zimshukie): “Enyi watu, tubuni kwa Mwenyezi Mungu, kwani mimi ninatubia kwake mara mia kwa siku.” (Imamu Muslim).
Pia maumbile ambayo Mwenyezi Mungu amemuumbia Mwanadamu katika Ulimwengu, yanapelekea kumtaka atubie kila siku (kwa kudumu kufanya hivyo), na wala hatakiwi kuhisi uzito wa kufanya hivyo. Na pasipatikane hali ya kuionea aibu nafsi na pia pasiwe na uzito wa kujivua na makosa.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu mtukufu atuwezeshe kuwa ni wenye kutubia kwake Toba ya kweli na ya ya kudumu, atusamehe makosa yetu yote, na azikubali toba zetu kwani yeye ni mweza wa hilo. Na mwisho wa maombi yetu ni Alhamdulillah.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote
Chanzo: Kitabu Simaat Al asr, cha Mufti wa Misri, Profesa Ali Juma.

Share this:

Related Fatwas