Damu Imtokayo Mwanamke Aliyetolewa ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Damu Imtokayo Mwanamke Aliyetolewa Kizazi

Question

 Nini hukumu ya damu inayomtoka mwanamke aliyetolewa kizazi? Je, ni damu ya hedhi au damu ya maradhi?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema ni zake, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu na Jamaa zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya utangulizi huu..
Kizazi cha baadhi ya wanawake hutolewa kwa sababu mbali mbali. Na kwa maana hiyo, wanawake wasio na kizazi huwa hawana hedhi, kutokana na kutolewa sehemu yote ya kizazi hicho, kwa hivyo pengine mwanamke huyo anaona damu inayotoka kutoka kwake, hapo anauliza; je, ni damu ya hedhi au siyo?
Ni wazi kuwa sura hii inahusiana na mlango wake wa msingi wa hedhi; ambapo wanazuoni wa Fiqhi wa madhehebu mbali mbali walifafanua hedhi, kwa hiyo linaweza kufahamika suala hili kupitia ufafanuzi huo, ingawa hakuna matini ya suala hili lenyewe.
Hedhi ni: damu itokayo kwenye fuko la uzazi la mwanamke, akifikia kuvunja ungo, kisha akizoea inakuwa katika nyakati maalumu. [Al-Mughniy na Ibn Qudamah: 1/322, Ch. ya Maktabat Al-Qahirah].
Hukumu ya suala hili kuwa: damu hii itokayo kwenye tupu ya mwanamke, baada ya fuko lake la uzazi likiwa limeng’oliwa, haihesabiwi kuwa ni hedhi kwa njia yeyote iwayo, kwa hiyo mwanamke huishi maisha ya unadhifu siku zote, aswali, afunge saumu, aingiliwe na mumewe, na hakatazwi kwa kitu kilichokatazwa wakati wa siku za hedhi; na eda yake inahesabiwa kwa miezi na si kwa hedhi.
Dalili ya hayo ni kuwa: hedhi ni matukio ya kazi ya Ovari katika fuko la uzazi, na pasipokuwa na kazi hii kwa sababu ya udogo au uzee, basi hakuna hedhi, kwa mujibu wa hayo wanafiqhi walisema juu ya umri wa chini na wa juu ambamo mwanamkea hupata hedhi ndani yake, na Mwenyezi Mungu amesema: {Na wale waliokoma na kutoka hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayo shaka (katika muda wao wa Eda), basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, na (pia ndiyo eda kwa wale) ambao hawajapata hedhi bado}. [ AT TALAQ: 4].
Tulivyotaja ni waliyotaja wanafiqhi katika ufafanuzi wao wa hedhi, iliyokuwa ni: damu itokayo kwa fuko la uzazi, na hali ya kutokuwepo fuko la uzazi, basi haipo hedhi, kwa mujibu wa ufafanuzi, na suala kama hili linajulikana kwa (kutokuwepo mahali), na lina mifano mingi katika Fiqhi.
Miongoni mwa dalili za Sunna tukufu ni Hadithi ndefu kuhusu Kiyama, kutoka kwa Abi said Al-Khudriy alisema: Mtume S.A.W, alisema: “Mwenyezi Mungu anasema: Malaika waliomba, Manabii waliomba, waumini waliomba, na hakubaki ila Mwenye rehema kabisa kuliko wote, na anashika sehemu ya Moto ambamo ndani yake watu ambao hawakufanya heri katu, na miili yao kama makaa ya moto, akawatupa katika mto mbele ya Pepo iitwayo: Mto wa uhai, wakarejea uhai kama chembe inayoota kutokana na mafuriko ya maji, je, wanaonaje mifano yake ni kama mawe au miti, zikikabili Jua, basi rangi yake ni karibu ya manjano au kijani, na zikikabili kivuli, basi rangi yake ni nyeupe? Wakasema: ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, wewe kama kwamba huchunga wanyama jangwani”. [Wameipokea Bukhariy na Muslim, na lafudhi ni ya Muslim].
Mwelekeo wa dalili kuwa: Mtume S.A.W, aliashiria kuchunguza uhalisia wa vitu na mabadiliko yake kutokana na sababu za kuathirika kwake, na zaidi ya hayo akaashiria kuwa ukweli na uwongo wa vitu hivi unaambatana na uhalisia wake na alama zake, kama ilivyotajwa katika Hadithi ya Sahl Ibn Saad As-Saidiy katika Hadithi ya (Mulaa’nah) kuwa Mtume S.A.W, alisema: “Kama mwanamke akizaa mtoto mwekundu tena mfupi, kama kwamba mnyama, basi mwanamke alisema kweli na mwanamumme alisema uongo, lakini akizaa mtoto mweusi, macho yake mapana, na mwenye vitako, basi mwanamume alisema kweli, na mwanamke alizaa kitu makuruhi”. [Ameipokea Bukhariy].
Kutokana na hayo hapo juu inabainika kuwa Sharia inatambua maneno ya watu wenye ujuzi, kwa hiyo tulitambua kutokuwepo kwa hedhi kutokana na kutokuwepo fuko la uzazi.
Kuhusu yaliyotajwa katika baadhi ya vitabu kuwa hedhi ni damu inayotoka kwenye tupu, hakika imefasiriwa kuwa maana yake ni damu itokayo kwenye fuko la uzazi, kwa hiyo hakuna hitilafu katika kauli za wanazuoni kuhusu suala hili.
Na zifuatazo ni fafanuzi za Madhehebu manne ya kifiqhi:
Al-Kasaniy anasema: “Hedhi katika kawaida ya Sharia ni: damu itokayo kwenye fuko la uzazi, na haifuatiliwi na kuzaa, yenye kadiri maalumu, na wakati maalumu, basi lazima kujua rangi ya damu, hali yake, kutoka kwake, kadiri yake na wakati wake”. [Badaii’ As-Sanaii’ Fi Tartiib Ash-Sharaii’: 1/39, Ch. ya dar Al-Kutub Al-ilmiyah].
Abu Abdillahi Al-Mawaq Al-Malikiy anasema: “Ibn Arafah; Hedhi ni damu itokayo kwenye fuko la uzazi huweza kupata mimba, na bila ya kuzaa”. [At-Taj wal-Iklil Li Mukhtasar Khalil: 1/539, Ch. ya Dar Al-kutub Al-Elmiyah].
Sheikh Zakariya Al-Ansariy anasema katika: “(Kitabu cha hedhi) ni damu ya inayomtoka mwanamke kwenye uzio wa fuko la uzazi kwa wakati maalumu”. [Asna Al-Matalib Fi Sharh Rad At-Talib: 1/99, Ch. ya dar Al-Kitab Al-Islamiy].
Abun-Naga Al-Hijawiy anasema: “Hedhi ni damu ya kimaumbile inayotoka katika uzio wa fuko la uzazi, na ni ya kawaida kwa mwanamke aliyevunja ungo, na huwa kwa nyakati maalumu”. [Al-Iqnaa’ fi fiqh Al-Imam Ahmad ibn Hanbal; 1/63, Ch. ya dar Al-Maa’rifah].
Wanazuoni wa Fiqhi walitambulia walivyosema waganga kwa ujumla, na kuna matini ya kutambua hasa elimu ya Anatomia. Kwa mfano suala la tohara ya manii na kutoka kwake pamoja na mkojo kupitia njia moja, Sheikh wa Uislamu Zakariya Al-Ansariy anasema: “Ilivyosemwa kuwa ni najisi kama mkojo kwa sababu njia ya kutoka ni moja, Maimamu wetu walijibu kuwa: manii ni asili ya binadamu, na ni mfano wa udongo, kinyume cha mkojo, na njia ya kutoka kwa hizi mbili si moja, Al-Qadhi Abut-TWayib anasema: tupu ya mtu wa Kirumi ilipasuliwa, na imedhihirika kuwa njia ya kutoka kwa manii na mkojo si moja, basi hatutoi hukumu ya unajisi kutokana na mashaka tu. Na sheikh Abu Hamid anasema: ikiwa njia ni moja unajisi haulazimiki; kwa sababu kuchanganua unajisi huathiri katika dhahiri na si katika batini. Na Ibn As-Sabbagh anasema: ikiwa njia ni moja basi unajisi hapa ni kusameheka, kwa sababu ya dharura”. [Al-Ghurar Al-Bahiyah Fi Sharh Al-bahjah Al-Wardiyah: 1/45, Ch. ya Al-Matbaa’ah Al-Maimaniyah].
Kwa muhtasari: Kutolewa kwa kizazi huondosha uwepo wa hedhi, kwa sababu ya kutokuwepo kizazi hicho, na mwanamke akiona damu baada ya hapo basi haihesabiwi kuwa ni hedhi, na hukumu yake ni kujitwaharisha kwa kutawadha tu. Na kuhusu eda ya mwanamke asiye na kizazi katika hali ya talaka, huwa inahesabiwa kuwa ni miezi tu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.
 

Share this:

Related Fatwas