Usafi wa Nguo Zenye Najisi Zikiwekwa katika Mashine ya Kujiendesha ya Kufulia
Question
Je nguo zenye najisi zikiwekwa katika mashine ya kufulia inayojiendesha yenyewe zitakuwa twahara?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema ni zake, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu na Jamaa zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya utangulizi huu..
Unajisi katika lugha ya Kiarabu ni: uchafu. Na katika Sharia ni: sifa ya dhahania ambayo inalazimu mtu ajiepushe na swala, muda wa kuwa na sifa hii. [Hashiyat Ad-Disuqiy Ala Ash-Sharh Al-Kabiir: 1/32, Ch. ya Dar Al-Fikr].
Inashurutishwa kwa usahihi wa swala, twahara ya mwili wa anayeswali, nguo yake, na mahali pake, kutokakuwa na unajisi; kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na nguo zako uzisafishe}. [AL MUDDATHIR: 4], na hii ni dalili ya uwajibikaji wa kuondoa unajisi kutoka kwenye nguo za mwenye kuswali, na kwa iliyopokelewa na Bukhariy, kutoka kwa Aisha alisema: Mtume S.A.W., alisema: “Ukipata hedhi, basi iache swala, na ukimaliza, basi ioshe damu na Swali”, na hii ni dalili ya uwajibikaji wa kuondoa unajisi kutoka kwa mwili wa mwenye kuswali, na kwa iliyopokelewa na Bukhariy, kutoka kwa Abi Hurairah, alisema: “Bedui alikojoa katika msikiti, na watu walimkataza, na Mtume S.A.W., aliwaambia: mwacheni na mwageni juu ya mkojo wake ndoo ya maji, na hakika ninyi mmetumwa ni wenye kurahisisha, na hamkutumwa ni wenye kutia uzito”, na amri yake S.A.W., kumwaga ndoo ya maji juu ya mahali, ni dalili ya uwajibikaji kuondoa unajisi kutoka kwenye mahali pa kuswali.
Unajisi unaondolewa kwa kutumia maji safi kabisa, hata ikaondolewa hukumu ya unajisi ambao ulikuwa sababu yake, kuhusu najisi nyenyewe utaondolewa kwa njia yeyote kama kusugua, na sharti la kuondolewa najisi ni kuondoa ladha yake, ama rangi na harufu yake ni sharti, kama iwezekanavyo.
na dalili ya kuondoa najisi kwa kutumia maji safi sana ni kauli ya Mwenyezi Mungu: {Na akakuteremshieni maji mawinguni ili kukutwaharisheni kwayo}. [AL ANFAAL: 11], na Bukhariy ameipokea kutoka kwa Asmaa alisema: “Mwanamke alikuja kwa Mtume S.A.W., akasema; unaonaje mwanamke kati yetu nguo yake imepatwa na sehemu ya hedhi, je, vipi anafanya? Akasema: ioshe kwa maji kisha aswali kwayo”.
Sheikh Ad-Dardiir anasema: “Unajisi unaondolewa kwa kutumia maji safi kabisa, nayo ni maji yanayojulikana, kinyume na aina zingine za majimaji, kama vile: siki, samli, maji ya waridi au maua, maji ya tikiti n.k., aina hizi za maji haijuzu kuzitumia kwa kusafishia, lakini inajuzu kutumia maji ya bahari, mvua, visima, kwa ajili ya kusafishia”. [Ash-Sharh As-Swaghiir, na Ad-Dardiir: 1/29, Ch. ya Dar Al-Ma’arif].
Sheikh As-sawiy katika Hashiya yake anasema: “Unajisi wenyewe huondolewa kwa kila njia, lakini haitoshi pekee kwa kuleta twahara ya kisheria”. [Ash-Sharh As-Swaghiir, na Ad-Dardiir: 1/27].
Sheikh Ad-Dardiir katika kitabu cha: [Ash-Sharh Al-Kabiir] anasema: “Sehemu ya unajisi inasafishwa kwa kuiosha hadi ikaondolewa ladha yake ya sehemu hii, hata ikiwa na ugumu, kwa sababu kuwepo ladha ni dalili ya kuwepo unajisi, kwa hiyo lazima uondoshwe, lakini si sharti kuondoa rangi na harufu, isipokuwa nyepesi”. [Hashiyat Ad-Disuqiy Ala Ash-Sharh Al-Kabiir: 1/78, Ch. ya Dar Al-Fikr]
Kuhusu kazi ya mashine ya kujiendesha ya kufulia katika kusafisha/kutwaharisha nguo, muda tu, wa kuanza kufanya kazi, maji yapite ndani ya mashine, kupitia sanduku la poda ya kusafishia, hapo ikachanganya na sabuni, kisha injini ikaanza katika pande mbili, ili nguo zigeuzwegeuzwe, kisha maji yakatoka kupitia mpira wa kutoa maji nje, na kufanya hivi kuna vitu viwili:
Kwanza; kuondoa unajisi wenyewe, pamoja na ladha, rangi na harufu yake, na kuhusu unajisi wenywe haishurutishwi kutumiwa maji safi kabisa, Pili: maji yanapochanganywa na sabuni, inatarajiwa maji yasiwe yamebadilika kwa najisi au hapana, kama hayakubadilika kwa najisi, basi unajisi wenyewe umeondolewa, na kubaki ni kuondoa hukumu itakayoondolewa katika mara ya nne au ya tano ya kazi ya mashine, ambapo hakuna sabuni, yaani kusafisha hapa ni kwa njia ya maji safi kabisa tu, lakini kwa mara ya pili na ya tatu ya kazi ya mashine, hukumu ya unajisi haiondoshwi kwa sababu ya kuchanganya na sabuni, na hapo basi maji yatakuwa safi tu, na si safi kabisa.
Kama maji yakipata unajisi katika mara ya kwanza, basi itakuwa najisi na si twahara. Sheikh Ad-Dardiir anasema: “Maji ya kufulia yanayopata sifa moja miongoni mwa sifa za unajisi ni najisi”. [Hashiyat Ad-Disuqiy Ala Ash-Sharh Al-Kabiir: 1/ 78], kueneza unajisi katika kila sehemu ya maji, basi nguo zote zitakuwa najisi, yaani mara ya kwanza ya kazi ya mashine imeeneza unajisi, ingawa unajisi mwenyewe umeondoshwa, na kubaki ni hukumu yake itakayoondoshwa katika mara ya nne na ya tano.
Wafuasi wa Madhehebu ya Hanafiy walijuzisha kuondoa najisi kwa mada nyingine isipokuwa maji safi kabisa, basi unajisi utasafishwa katika mara ya pili na ya tatu ya kazi ya mashine, ambapo maji huchangaywa na sabuni, na si katika mara ya kwanza, kama maji yatapata najisi katika mara hii.
Al-Mighinaniy, Al-Hanafiy anasema: “Inajuzu kusafisha unajisi kwa kutumia maji, na kila mada ya majimaji twahara, kama vile; siki, maji ya waridi n.k., na nyingine za majimaji”. [Sharh Fath Al-Qqdiir Ala Al-Hidayah; 1/133, Ch. ya Al-Amiriyah]
Kuhusu maji najisi, yanayochanganya na najisi, hii haijuzu kusafishwa kwake, kwa sababu ni majimaji siyo twahara.
Ash-Shurunbilaliy Al-Hanafiy anasema: “Maji yaliyonajisika ni yale yaliyochanganyika na najisi, kwa yakini au kwa kuishinda dhana”. [Maraqiy Al-Falah, Sharh Nur Al-Idhah, Uk. 16, Ch. ya Mustafa Al-Halabiy], nayo ni kauli ya Taqiy-Din ibn taimiyah, kama ilivyokuja katika [Majmuu’ Al-Fatawa; 21/475, Ch. ya Majma’ Al-malik Fahd].
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia: kusafisha nguo kwa kuzifua katika mashine ya kujiendesha ya Kufulia ni njia nzuri ya kufulia kuliko njia za kienyeji, kwa sababu ya kuondosha unajisi mwenyewe wa ladha, rangi, na harufu kwa mara kadhaa ya kufulia, na kuondosha hukumu yake kwa mara kadhaa pia, jambo linalosafisha nguo kutoka kwenye unajisi kikamilifu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.