Swala ya Tasbihi.
Question
Ni nini Swala ya Tasbihi? Na huswaliwa vipi? Na ni nini hukumu yake?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Swala ya Tasbihi: Ni moja ya aina za Swala ya hiyari na kujitolea, yenye utaratibu maalumu, nayo huwa inaswaliwa rakaa nne, mwenye kuswali huleta tasbihi ndani yake katika kila rakaa mara sabini na tano, na inakuwa na salamu moja ikiwa itaswaliwa mchana na huwa na salamu mbili ikiwa itaswaliwa usiku. Na kilicho bora zaidi ni kuiswali kila siku mara moja, na kama kutakuwa na uzito basi angalau iswaliwe kwa wiki mara moja, au kwa mwezi mara moja au kwa mwaka mara moja, na ikishindikana kabisa basi kwenye umri wa mtu aiswali angalau mara moja, na Swala hii imeitwa kwa jina hilo kutokana na kuwemo ndani yake Tasbihi nyingi.
Swala hii ya Tasbihi ni sunna iliyokokotezwa, kutokana na mapokezi yake kutoka kwa Mtume S.A.W, aliposema kumwambia baba yake mdogo Abbas Ibn Abdul Mutwalib: “Ewe Abbas, ewe baba yangu mdogo, je nikupe? Je nikupatie? Je nikuzawadie? Je nikuoneshe upendo? Je nikufanyie mambo kumi? Ikiwa utayafanya mambo hayo, basi Mwenyezi Mungu Atakusamehe dhambi zako, kuanzia dhambi ya kwanza mpaka ya mwisho, ya zamani na ya havi karibuni, uliyoifanya kwa makosa au kwa makusudi, iwe ndogo au kubwa, umeifanya kwa siri au kwa wazi, mambo hayo kumi: ni kuswali rakaa nne, utasoma katika kila rakaa surat Al-Fatiha na sura nyingine, utakapomaliza kusoma hizo sura katika rakaa ya kwanza hali ya kuwa umesimama, basi useme: Subhana Allah, Wa Alhamdu lillah, Wala ilaaha illa Allah, Wa Allaahu Akbar, mara kumi na tano, kisha utarukuu na utasema maneno hayo hali ya kuwa umerukuu mara kumi, kisha utainuka kutoka katika rukuu na utayasema hayo maneno mara kumi, kisha utakwenda kusujudu utayasema pia maneno hayo mara kumi huku ukiwa umesujudu, kisha utainuka kutoka kwenye kusujudu na utayasema maneno hayo mara kumi, kisha utasujudu tena na utayasema hayo maneno mara kumi, kisha utainuka kutoka sujudu na kusimama utayasema tena maneno hayo mara kumi, hivyo yanakuwa yamesemwa mara sabini na tano katika kila rakaa utafanya hivyo kwenye rakaa nne, ikiwa utaweza kuisali kila siku mara moja basi fanya hivyo, ikiwa utashindwa basi iswali kila Ijumaa mara moja, na ikiwa utashindwa basi kila mwezi swali mara moja, na ikiwa pia utashindwa basi kwa mwaka swali mara moja, na kama pia utashindwa basi kwenye umri wako swali angalau mara moja”.
Na Hadithi imepokelewa kwa njia nyingi, na idadi kubwa pia ya Masahaba ambao ni: Abdillah Ibn Abbas, Abu Rafi’, Abdillah Ibn Amr, Abdillah Ibn Omar, Abbas Ibn Abdul Al-Muttalib, Ja’afar Ibn Abu Twalib, Ummu Salma (radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote) na imepokelewa na Ikrema, Muhammad Ibn Kaab Al-Qardhiy, Abu Al-Jauzaa, Mujahid, Ismail Ibn Rafi’, A’rwa Ibn Ruwaim.
Na imetolewa na wapokezi wengi wa Hadithi kama vile Abu Daud, Tirmidhiy, Ibn Maja katika sunna yake na Hakim katika Mustadrak.
Na dalili kwenye Hadithi hii ni kuwa yale aliyoyasema Mtume S.A.W, kwa baba yake mdogo Abbas kuhusiana na Swala hii ni dalili ya wazi ya kukokotezwa kwa Swala hii.
Amesema Imamu An-Nawawiy katika kitabu cha [Tahdhib Al-Asmaa wa Al-Lughat, 3/136 chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya] kuwa “yenyewe ni sunna iliyo nzuri”.
Na akasema pia katika kitabu cha: [Al-Adhkar. uk. 232 chapa ya Dar Ibn Hazmi]: “Jopo la Maimamu wetu limezungumza kuwa Swala ya Tasbihi imekokotezwa, miongoni mwao ni Abu Muhammad Al-Baghwiy, Abul Mahasin Ar-Rauyaany”.
Na akasema Al-Khatwib As-Sherbiniy katika kitabu cha: [Mughniy Al-Muhtaj, 1/458, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya]: “Sala ya Tasbihi ni sunna iliyo nzuri, na aliyeithibitisha kuwa ni sunna kauli yake inakubalika kama alivyosema hayo Ibn Salah na wengine”.
Na amesema Ibn Abdiin katika kitabu chake: “Kauli yake, Swala ya Tasbihi ni rakaa nne ….mpaka mwisho”na huwa inaswaliwa wakati wowote na wala hakuna chukizo lolote ndani yake, au kila siku au kila usiku mara moja, na kama mtu atashindwa basi kila wiki au kila Ijumaa, au wiki au mwezi, au kwenye umri mara moja, na Hadithi hii ni sahihi kwa njia mbalimbali na sio sahihi mtu kuidhani kuwa ni ya kuzushwa” [Kitabu Radd Al-Muhtar ala Dur Al-Mukhtar cha Ibn Abdiin, 2/27 chapa ya Dar Al-Fikr].
Al-Hatwab Al-Malikiy ameyahesabu mambo yaliyo bora baada ya kuigawa Swala kwenye sehemu sita na akasema: “Na yaliyo bora: ni pamoja na rakaa mbili za kabla ya Swala ya Al-Fajiri… Swala ya Tasbihi kama alivyotaja Kadhi Iyadh katika kitabu chake” [Mawahib Al-Jalil, 1/381, chapa ya Dar Al-Fikr].
Na akasema Ibn Qudama Al-Hanbaliy: “Ikiwa ataiswali mtu, basi hakuna ubaya” [kitabu Al-Mughniy cha Ibn Qudama, 1/438, chapa ya Maktabat Al-Kahera] na kauli yake: “hakuna ubaya” maana yake ni kuwa inafaa.
Na imepokelewa na baadhi ya wanachuoni kuwa Hadithi iliyopokelewa kuhusu Swala ya Tasbihi ndani yake kuna udhaifu, na wakasema wengine kuwa Hadithi ni maudhui (ya kutungwa) na kwa sababu hiyo wamehukumu kutokuwa na usahihi wa kisheria, lakini hata hivyo wanajibiwa kuwa: Swala hii imepokelewa kwa njia nyingi, zikijipa nguvu zenyewe kwa zenyewe, na hiyo Hadithi imeshikamana na vitendo vingi vya waja wema waliotangulia kuiswali na kudumu nayo.
Amesema Ibn Hajar: “Ukweli ni kuwa Swala hii ipo katika kiwango cha ubora, ni kutokana na wingi wa njia zake ambazo zinaimarisha njia ya kwanza, Mwenyezi Mungu Anajua zaidi”. (Majibu ya Hafidh Ibn Hajar Al-Asqalaniy kuhusu Hadithi kumi na nane alizozioana Imamu Abu Hafs Al-Qadhawaniy kuwa siyo sahihi, na kuunganishwa kwenye kitabu cha: [Masabiih As-Sunna cha Baghawiy, 1/83 chapa ya Dar Al-Maarifa].
Amasema Imamu At-Tarmidhiy: “Ameiona Ibn Mubarak na zaidi ya wanachuoni Swala ya Tasbihi na kutaja ubora uliomo ndani yake” [Sunan ya Tirmidhiy 2/348, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy].
Na akasema Al-Baiqiy kuhusu Swala hii: “Na alikuwa Abdillah Ibn Mubarak akiiswali na kusaliwa na waja wema, na ndani yake inapewa nguvu na Hadithi iliyo sahihi” [Kitabu Shu’ab Al-Iman, 1/427, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya].
Na katika walioipitisha Hadithi hii ni pamoja na Al-Hafidh Abu Bakr katika kitabu chake An-Nasiha, na Ibn Mandaha na akatunga katika marekebisho yake kitabu, na Abu Sa’ad As-Sam’aaniy mwenye kitabu cha: [Al-Ansab], na Abu Muhammad Abdulrahman Al-Masry, na Abu Al-Hassan Al-Maqdisy, na Ibn Nassr Ad-din Ad-Demashqy katika kitabu chake: [Hadithi ya Swala ya Tasbihi Ina nguvu] na Ibn Salah katika fatwa zake na Al-Balqiny na Hafidh Al-Mundhiriy katika kitabu chake [At-Targhib wa At-Tarhib].
Na akasema Al-Laqnawiy: “Nikasema: ibara hizi zinapatikana kwa watu wakubwa wenye kuaminika wamelingania kuwa kauli ya kusema Hadithi siyo sahihi ya Swala ya Tasbihi ni kauli batili na ya kupuuzwa wala haikubaliki kiakili wala kwa kutamkwa, isipokuwa yenyewe ni Sahihi au ni Bora yenye kuchukuliwa kama hoja, na wazungumzaji wote ukiondoa Ibn Al-Juziy na mitazamo yake - hakika wametofautiana katika usahihi na udhaifu wake lakini hakuna hata mmoja aliyefikia kusema kuwa ni Hadithi ya kuzushwa” [Athar Al-Marfuua fi Akhabar Al-Maudhua, 1/137, chapa ya Maktabat Al-Ashark Al-Jadid- Baghadad].
Na amesema Imamu As-Suyutiy katika kitabu cha [Quut Al-Mughtadha ala jami’ At-Tirmidhy 1/208 – 209 chapa Chuo Kikuu cha Umm Al-Quraa]: “Amesema Ibn Al-Juziy na kuiweka Hadithi hii kwenye Hadithi za uzushi, na kuizungumzia Musa Ibn Ubaida, na sio kama alivyosema, Hadithi hata kama itakuwa ni dhaifu lakini haijafikia kiwango cha kuwa ya uzushi, na Mussa akaifanya kuwa ni dhaifu, na akaisemea Ibn Saad: ni yenye kuaminika na wala siyo hoja, na akasema Yakub Ibn Shaiba: ni ukweli lakini Hadithi ni dhaifu sana, na imetajwa na Ibn Habban katika wapokezi wake ni wenye kuaminika, na akasema Adhahaby katika Mizan: imepokelewa na wengi ukiondoa Musa Ibn Abiidat”.
Ama yaliyonukuliwa kutoka kwa Imamu Ahmad katika kuikana kwake Hadithi hii kuna maelezo yaliyokuja kusema kuwa aliifuta kauli yake hiyo, amenukuu Hafidh Ibn Hajar katika majibu yake kuhusu Hadithi iliyomo kwenye kitabu cha Al-Masabih, 1/83, kutoka kwa Aly Ibn Said An-Nisaai amesema: “Nilimwuliza Ahmad kuhusu Swala ya Tasbihi, akasema: kwangu haifai chochote, nikasema: kutoka kwa Ibn Rayyan toka kwa Abu Al-Jauzaa toka kwa Abdillah Ibn Amr. Akasema: nani aliyekwambia? Nikasema: Muslim Ibn Ibrahim, akasema: Rayyan ni mwenye kukubalika, kama kwamba amefurahishwa naye”. Mwisho.
Kisha akasema Hafidhi Ibn Hajar: “Nukuu hii toka kwa Ahmad inaonesha kuwa alirejea nyuma na kuipendezesha Swala hii, na ama yaliyonukuliwa toka kwa wengine yanapingana juu ya yule aliyoipa nguvu Hadithi na kuifanyia kazi, wamekubaliana kuwa yenyewe haichukuliwi kuwa katika Hadithi za uzushi, lakini inafanyiwa kazi kama Hadithi dhaifu kwenye mambo yaliyo bora na katika yale ya kupendezesha na kuogopesha”.
Na kutokana na maelezo yaliyotangulia: Swala ya Tasbihi ni aina ya Swala za kujitolea yenyewe ina utaratibu wake maalumu, nayo ni katika ibada zinazopendeza.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.