Kusoma Bismillah Kwa Sauti Katika S...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kusoma Bismillah Kwa Sauti Katika Swala.

Question

Je, nini hukumu ya kusoma Bismillah kwa sauti katika swala? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na jamaa zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Maana ya kusoma kwa sauti katika lugha: ni kukisema kitu kwa kupaza sauti, husemwa: “Nimesoma maneno kwa sauti” yaani nimeyasema maneno hayo kwa kupaza sauti, na mtu ana sauti ya juu, yaani sauti yake ni kubwa.
Abu Hilal Al-Askariy alisema: maana yake ni kupaza sauti, husemwa, “amesoma kwa sauti” yaani amepaza sauti yake katika kusoma, na maana yake ya kiistilahi haikuwa mbali na maana yake ya kilugha, nayo ni kutangaza.
Na kuna wakati maalumu wa kusoma kwa sauti katika swala na wakati mwingine hairuhusiwi kusoma kwa sauti, lakini jambo hili halitushughulishi na lengo kuu la swala nalo ni unyenyekevu na kuzingatia na kunong’oneza.
Kusoma Bismillah kwa sauti ni sehemu ya swala, Wanavyuoni wametofautiana katika suala hili.
Pengine tofauti hii inatokana na kiwango cha kuthibitisha kusoma Bismllah kwa sauti kama ni Aya miongoni mwa Qur`ani. Ibn Kathiir amesema, baada ya kutaja tofauti ya Wanavyuoni kuhusu kusoma Bismillah kwa sauti kama ni Aya miongoni mwa Qur`ani: “Hivi ndivyo nilivyotaja kuhusu kuwa Bismillah ni Aya moja miongoni mwa Aya za Suratul Fatiha au la, ama kuhusiana na suala la kusoma Bismillah kwa sauti linategemea tofauti ile.
Basi aliyesema kuwa Bismillah siyo Aya miongoni mwa Aya za Suratul Fatiha, alisema kuwa haisomwi kwa sauti. Vile vile waliosema kuwa ni Aya ya mwanzo katika sura wametofautiana kuhusu kusomwa kwake, ambapo Imamu Shafi Mwenyezi Mungu Amrehemu alifuata mtazamo wa kuwa inasomwa kwa sauti katika Suratul Fatiha na Sura zingine, nao ni mtazamo wa kundi la Masahaba, Tabiina na Maimamu wa Waislamu waliotangulia na waliokuja baada yao [Tafsiri ya ibn Kathiir 1 / 117, Dar Twaibah].
Pengine tofauti hii inatokana na tofauti dhahiri katika dalili, ambayo inahitaji kuangalia nguvu ya dalili kama ilivyo katika suala lolote la kifiqhi lenye utata. Imam Al-Nawawiy amesema kwamba: “Jua kwamba suala la kusoma Bismillah kwa sauti halitegemei suala la kuthibitisha kuwa Bismillah ni Aya katika Qur`ani au la; kwa sababu kuna kundi la Wanavyuoni wanaoona kuwa inasomwa kwa siri wanaamini kuwa Bismillah siyo miongoni mwa Qur'ani, lakini ni miongoni mwa Suna zake, kama vile; kujikinga na kusema mwishoni mwa Suratl Fatiha “Amin”. Na kundi lingine la Wanavyuoni wanaoona kuwa inasomwa kwa siri wanaamini kuwa Bismillah ni miongoni mwa Qur'ani, lakini hawa wamesema kuwa inasomwa kwa siri, na kundi lingine likasema kuwa inasomwa kwa sauti kufuatana na nguvu za dalili za kila kundi miongoni mwao” [Al-Majmuu’ Sharhu Al-Muhadhab 3/300, Dar Al-Fikr].
Hakuna kizuizi ya kuwa tofauti juu ya suala moja inategemea zaidi ya sababu moja, basi hukumu ya kuisoma Bismillah kwa sauti inategemea hukumu ya kuisoma Bismillah katika swala, na hukumu ya kuisoma ni sehemu ya tofauti kuhusu suala la kuthibitisha kuwa Bismillah ni Aya moja miongoni mwa Aya za Suratul Fatiha, hivyo pamoja na tofati ya Wanavyuoni kuhusu dalili zilizotajwa katika kuisoma kwa sauti au kwa siri.
Madhehebu ya Imam Shafiy na tunavyopendekeza ni kuisoma Bismillah kwa sauti katika Suratul Fatiha na katika sura zote, nao ni mtazamo wa wengi wa Wanavyuoni miongoni mwa Masahaba, Tabiina, na waliokuja baada yao miongoni mwa Wanavyuoni wa Fiqhi na Wasomi.
Ama kwa Maswahaba: Imepokelewa kutoka kwa Abu Bakr, Omar, Uthman, Ali, Ammar Ibn Yasser, Ibn Abi Kaab, Ibn Omar, Ibn Abbas, Abu Qatada, Abu Sa'eed, Qais Ibn Malik, Abu Hurayrah, Abdullah Ibn Abi Aufa, Shaddad Ibn Aws, Al-Hussein Ibn Ali, Abdullah Ibn Jaafar, Muawiyah, na kundi la Al-Muhaajiriyn (walio hama kutoka Makkah), na Al-Answaar (waliowasaida na kuwanusuru Muhaajiriyn katika wakazi wa Madina) waliohudhuria Muawiya aliposwali Madina na hakusoma Bismillah kwa siri wakakanusha hivyo akarudia kuisoma kwa sauti mara nyingine.
Ibn Abd Al-Barr alisema: “Hawakutofautiana kuhusu suala la kuisoma Bismillah (Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu) kwa sauti kutoka kwa Ibn Umar, nayo ni sahihi vile vile kutoka kwa Ibn Abbas, na kundi la wenzake wamefuata mtazamo huu; miongoni mwao ni Said Ibn Jubair, Atwaa, Mujahid, Tawous, nayo ni madhehebu ya Ibn Shihab Al-Zuhri, Amr Ibn Dinar , Ibn Juraij, Muslim Ibn Khaled, na wengine miongoni mwa watu wa Makka.” [Al-Insaaf fima baina Al-Ulamaa mina Al-Khilaaf uk. 160, Adhwaa Al-Salaf.]
Pia alisema: “Mtazamo huo ni wa Ibn Wahb mwenzake Malik”. [Al-Insaaf fima baina Al-Ulamaa mina Al-Khilaaf uk. 277].
Sheikh Abu Muhammad Al-Maqdisi alisema: “Kuisoma Bismillah kwa sauti ni rai iliyochaguliwa na Maimamu wakubwa, miongoni mwa ni: Mohammed Ibn Nasr Al-Marwazi, Abu Bakr Ibn Khuzaymah, Abu Hatim Ibn Hibban, Abu Al-Hassan Ad-Daaraqutni, Abu Abdullah Al-Hakam, Abu Bakr Al-Bayhaqi, Al-Khatib, Abu Omar Ibn Abdul Barr, na wengine. [Al-Majmuu Sharhul Muhadhab 3/342].
Zimepokewa Hadithi zinazoonesha usahihi wa kuisoma Bismillah, kwa sauti, miongoni mwazo ni: Hadithi ya Naim Ibn Abdullah Al-Mojmir alisema: Nimeswali nyuma ya Abu Hurayrah, R.A, akasoma: Bismillah (Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu), kisha akasoma Suratul Fatiha, mpaka akafika Wala dhwaaliin. {Wala waliopotea} akasema: Amina, na watu wakasema: Amina, na wakati aliposujudu alisema: Allahu Akbar (Mwenyezi Mungu ni mkubwa), na akisimama kutoka katika kikao alisema: Allaahu Akbar, na kisha alisema alipomaliza: Naapa kwa ambaye nafsi yangu iko mkononi mwake swala yangu ni mfano kwenu nyinyi wa swala ya Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.”. (Imepokelewa kutoka kwa Ibn Khuzaymah na Ibn katika Hadithi zao, na Ad-Darqutwniy, na alisema. Hii ni Hadithi sahihi, na wapokezi wao ni waaminifu, na imepokelewa kutoka kwa Al-Hakim katika Al-Mustadrak, na amesema: Hadithi hii ni sahihi kwa sharti la Maimamu wawili na hawakusimulia).
Al-Haafiz Ibn Hajar alisema: Hadithi hii ni sahihi zaidi kuliko nyingine. [Fath Al-Bari 2/267, Dar Al-Maarifah] anakusudia Hadithi inayohusu kuisoma Bismillah kwa sauti.
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah pia kutoka kwa Mtume, S.A.W “Alikuwa akiisoma wakati aliopokuwa akiwaswalisha watu akianza kwa Bismillahi Rahmani Rahiim. kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu”, Abu Hurayrah akasema: “Hii ni Aya miongini mwa Qur`ani, Someni kama mkitaka Suratul Fatiha, ni Aya ya saba”. [Imepokelewa kutoka kwa Ad-Darqutwniy na Al-Baihaqiy).
Katika Hadithi nyingine “Kwamba Mtume S.A.W alikuwa akiwaswalisha watu akisoma Bismillah. Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu” [Imepokelewa kutoka kwa Ad-Darqutwniy].
Na imepokelewa kutoka kwa Qatada alisema: Anas aliulizwa namana gani Mtume wa Mwenyezi Mungu akisoma? Alisema: kwa kurefusha (herufi), kisha akasoma Bismillah (Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu) akirefusha (herufi za) (Kwa jina la Mwenyezi Mungu) na akirefusha (Mwingi wa rehema) na akirefusha (Mwenye kurehemu). (Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhaari katika Sahihi yake).
Al-Hafiz Abu Bakr Muhammad Ibn Musa Al-Hazmi akasema: Hii ni Hadithi sahihi, ambayo hatujui ila (kasoro) kwake. Na ina dalili inayothibitisha kuisoma Bismillah kwa sauti wakati wowote katika swala au katika hali yoyote, kwani kusoma kwa Mtume, S.A.W. kulitofautisha kusoma kwa sauti katika hali mbili katika swala na katika hali nyingine. Anas akaibaianisha hali hii, anasema hivyo kwa ujumla, na Anasa akajibu kwa Bismillah, hii ni dalili ya kuwa Mtume S.A.W. alikuwa akisoma Bismillah kwa sauti, na lau Mtume hakufanya hivyo, Anas alikuwa akijibu kwa “Alhamdu lillah Rabil Alamiin” (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote) au Aya nyingine. [Al-Majmuu Sharhul Muhadhab 3/347].
Sheikh Abu Muhammad Al-Maqdisi alisema: “Hakuna udhuru kwa wale ambao wameacha uwazi wa Hadithi hizi kutoka kwa Abu Hurayrah, na wanategemea Hadithi ya: “Swala imegawanywa”, na wakaichukua Hadithi hiyo kwamba ni kuacha Bismillah kabisa, na Hadithi hizi zote zimepokelewa kutoka kwa Sahaba mmoja tu, kupatanisha kati ya Hadithi hizi ni bora zaidi kuliko kuamini kuwa zinatofautiana na Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Ad-Darqutwniy kwa mapokezi ya Hadithi “Swala imegawanywa”, inapaswa kuzifahamu Hadithi hizi mbili kufuatana na yalivyosemwa katika moja yao”. [Al-Majmuu Sarhul Muhadhab 3/346].
Kwa mujibu wa madhehebu ya Imam Abu Hanifa kuwa kusoma Bismillah kwa siri pamoja na Suratul Fatiha ni Sunna. Vile vile kwa mujibu wa Imamu Ahmad ni kuwa kuisoma Bismillah kwa siri pamoja na Suratul Fatiha ni Sunna. [Ad-Durr Al-Mukhtar 1 / 490-491, Dar Al-Fikr, Kashful qinaa 1 / 335-336, Dar Al-Kutub Al-Elmiyah].
Imam Malik amezuia kusomwa Bismillah katika swala za faradhi iwe kwa sauti au kwa siri, iwe mwanzoni mwa Suratul Fatiha au katika Sura nyingine, na ameruhusu kusomwa katika Swala za Sunna; hivyo inatokana na kusema: kuwa Bismillah siyo Aya miongoni mwa Aya za Suratul Fatiha, na kwa sababu anategemea Hadithi zinazothibitisha kutoisomwa katika Swala. [Sharhu Mukhtasar Khalil kwa Al-Kharashi 1/289 na kurasa zilizo baada yake].
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia hapo juu, tunaona kwamba inapendekezwa kuisoma Bismillah kwa sauti katika swala katika Suratul Fatiha na Sura zingine, kufuatana na dalili tulizozitaja, na kukumbusha kwamba suala hili ni la utata, basi, Waislamu hawaruhusiwi kugombana kwa sababu ya suala hili.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.
 

Share this:

Related Fatwas