Ulipaji kwa Mfumo wa “Kukodisha Huduma au Kazi”.
Question
Tumepitia ombi lilifikishwa kutoka katika Bankul-Misri Al-Khaliji – tawi la Al-Azhar la miamala ya Kiislamu, likiwa lina maswali yafuatayo:
Je, yafaa kulipa kwa mfumo wa: “kukodisha huduma au kazi”, ambapo benki inanunua haki ya manufaa au huduma mbalimbali kutoka kwa mkodishaji wake, kama vile: Shirika la Umeme, gesi, simu, ndege, wakala wa utalii na safari, shule, vyuo vikuu, mahospitali, maofisi ya ushauri na makampuni ya ufundi, au kutoka katika vitengo vya serikali, kwa mfano: Kitengo cha ushuru wa forodha na kodi. Na hilo ni kwa thamani maalumu ya fedha, kisha benki hiyo inafanya kazi ya kuiuza haki hiyo kwa wateja wake kwa mikataba ya kukodisha sawa na malipo ya baadaye au kwa malipo ya awamu pamoja na kujipatia faida?
Ifahamike kuwa mteja wakati mwengine anatanguliziwa huduma, kisha benki inatoa hundi ya benki moja kwa moja kwa mteja anayepata huduma (kwa jina lake na si kwa jina la mteja) kupitia risiti halisi za manunuzi au kile kinachomthibitishia mteja kutanguliziwa huduma, pasi na kulipia thamani ya fedha kwa mteja.
Na katika hali ya mteja kulipa kabla ya muda uliopangwa benki inampatia zawadi ya fedha kwa kulipa kwake mapema, na katika hali ya kuchelewa kulipa mteja anabeba jukumu la faini kwa kuchelewa kulipa, na faini hiyo inakuwa imeainishwa hapo nyuma kwenye mkataba, na mkataba huo lengo lake ni kuwajibika mteja kutelekeza malipo ya deni lake ndani ya wakati uliopangwa hapo nyuma ndani ya mkataba.
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Kwanza: kisheria huwa inafaa kuuza ambacho atakimiliki mnunuzi wa kinachouzwa na atalipa hapo baadaye malipo yote au sehemu ya malipo hayo kwa awamu zenye kufahamika na kwa muda wenye kufahamika pia.
Na dalili ya hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenyezi Mungu Ameihalalisha biashara} [AL BAQARA 275]. Na imepokelewa na Imamu Bukhari Hadithi kutoka kwa Bi. Aisha R.A. kuwa Mtume S.A.W. alinunua chakula kutoka kwa Yahudi kwa malipo ya baadaye na kuweka dhamana ya ngao ya chuma.
Na amesema Ibn Batal katika sherehe ya Bukhari (6/208, chapa ya Maktabat Al-Rushd huko – Riyadh): “Wanachuoni wamekubaliana juu ya kufaa kuuza kwa malipo ya baadaye”.
Ikiaa muuzaji atazidisha thamani ya mauzo kwa malipo ya siku za usoni zenye kufahamika, basi hilo pia linafaa kisheria, kwa sababu hilo linazingatiwa kuwa ni katika kuuza kwa faida, ambayo ni moja ya aina za biashara zenye kufaa kisheria ambayo inafaa kuweka sharti la kuongeza thamani ya bei kwa ulipaji wa baadaye, kwa sababu ulipaji wa baadaye hata kama hautakuwa mali ya sahihi isipokuwa ni katika mlango wa biashara kwa faida huongezwa bei kwa sababu ya faida, unapotajwa muda maalumu katika mkabala wa ongezeko la bei, kwa kukusudia kupata ridhaa kati ya pande mbili katika jambo hilo, na kutokuwepo kitakacholazimisha kuzuia, na watu wawe na hitajio kubwa la bidhaa hiyo wawe wauzaji au wanunuzi, na wala halizingatiwi hilo kuwa ni sehemu ya riba, kwa sababu kuuza kumepatikana kwa kuitikia na kukubali na imepatikana thamani na kitu cha kuwekewa thamani (cha kuuzwa). Hizi ndizo nguzo za biashara. Mwisho wa jambo lake ni kuwa malipo yatafanyika baadaye au sasa, na kuingia kwenye ujumla wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara} [AL BAQARAH 275]. Na vile vile kanuni ya kisheria ni kuwa ikiwa bei ya bidhaa ni ya kati na kati, basi hakuna riba.
Na kauli ya kufaa kuongeza bei kwa malipo ya baadaye ni katika yaliyokubaliwa na wanachuoni kuanzia Imamu Abu Hanifa, Imamu Malik, Imamu Shafi na Imamu Hanbal: Na amesema Imamu Al-Kasaniy katika kitabu cha Badaai As-Sanai miongoni mwa vitabu vya Imamu Hanbal [5/224, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah]: “Kwa malipo ya baadaye kunafanana na mauzo hata kama hayatakuwa mauzo ya kweli, kwa sababu ni yenye kutakiwa, kama unavyoona bei inazidi kwa sababu ya malipo ya muda wa baadaye, ikawa inafanana kukubaliana na thamani, na inakuwa kama vile mnunuzi amenunua vitu viwili kisha akauza kimoja wapo kwa faida baada ya thamani yote”.
Amesema Sheikh Ahmad Al-Dardiir katika sherehe ya kitabu chake Al-Kabir ufupisho wa Sayidi Khalil katika madhehebu ya Imamu Malik [3/58 – pamoja na Hashiyat Al-Dusuqiy – chapa ya Dar Ihyaa Al-Kutub Al-Arabiya]: “ikiwa itatokea – kwa maana: kuuza kwa sarafu kumi taslimu au zaidi lakini kwa malipo ya baadaye – si kwa lazima na akasema mnunuzi: nimenunua kwa bei fulani, hakuna kiziuizi”.
Na akasema Imamu Abu Is-haq As-Shiraziy Al-Shafi katika kitabu cha Al-Muhadhab [1/289, chapa ya Dar Al-Fikr – Beirut]: “Malipo ya baadaye yanachukua sehemu ya thamani”.
Na amesema mwanachuoni Ibn Muflih Al-Hanbaliy katika kitabu Al-Mubdii sherehe ya Al-Muqnii [4/103, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya]: “Malipo ya baadaye yanachukua sehemu ya thamani”.
Imenukuliwa kutoka kwa Taus, Hakam, Hammad na Al-Auzai katika wanachuoni waliopita [Maalim As-Sunan cha Abu Sulaiman Al-Khattaby, 3/123, chapa ya Al-Matbaa Al-Elmiya – Halab], ameelezea Kadhi As-Shaukaniy masuala haya kuyagawa katika sehemu ya peke yake na kuelezea madhehebu ya wanachuoni, na kuita: “Tiba ya matatizo katika hukumu ya ongezeko la thamani kwa mauzo ya baadaye” imetajwa katika [Sharhu ya Al-Muntaqa 5/181, chapa ya Dar Al-Hadith].
Haya ndiyo maazimio yaliyofikiwa na Jopo la Wanachuoni wa Fiqhi wa Kiislamu kwenye Kongamano la Kiislamu lililofanyika mjini Jiddah katika kikao chake cha sita cha mwezi 17 mpaka 23 shaaban 1410 sawa na tarehe 14 – 20 March 1990, ambapo yalifikiwa kwenye maamuzi ya mkutano nambari: (53 /2 /6), yanasema: “Inafaa kuongeza bei kwa malipo ya baadaye ukilinganisha na mauzo ya malipo ya hivi sasa, kama ambavyo inafaa kutaja bei ya kinachouzwa kwa malipo taslimu na pia malipo ya awamu kwa muda maalumu, na wala haifai kuuza isipokuwa watakapokubaliana muuzaji na mnunuzi kwa malipo taslimu au ya baadaye, ikiwa yatafanyika mauzo pamoja na kusitasita kati ya kufanyika malipo taslimu au kwa njia ya malipo ya baadaye. Ikiwa hawatafikia makubaliano juu ya bei moja iliyopangwa, basi hiyo biashara haitafaa kisheria”.
Hakuna tofauti kati ya manufaa na vitu katika kufaa kukubaliana kibiashara na kuvikuza. Amesema Imamu Ibn Qudama Al-Hanbali katika kitabu cha: [Al-Mughniy 5/251, chapa ya Dar Ihyaa Al-Turath Al-Arabiy]: “Manufaa ni sehemu ya vitu, kwa sababu yanafaa kumilikiwa katika kipindi cha uhai wa mtu na hata baada ya kufa kwake. Manufaa yanakusanya vitu vya kukabidhiana mkononi na katika hali ya kuharibika kwake, na kunakuwa na fidia ya malipo katika hali ya kuharibika kwa ima kitu au deni, ambapo huhusishwa kwa jina kama vile zinavyohusishwa baadhi ya biashara kwa jina”.
Na amesema mwanachuoni Ibn Hajar Al-Haitimiy Al-Shafiy katika fatwa yake [3/93, chapa ya Al-Maktaba Al-Islamiya]: “Manufaa ni kama vitu, yana thamani yake ikiwa amepatikana mtu mwenye kuyahitaji au hajapatikana”.
Kukodisha – ni makubaliano jumla ya kisheria – ni moja ya aina za makubaliano katika vitu vyenye manufaa lakini kwa malipo mbadala. Amesema Al-Khatib As-Sherbiniy katika uelewa wake: “Ni makubaliano juu ya manufaa yanayokusudiwa yenye kufahamika yanayokubali kutumika na halali kwa gharama yenye kufahamika” Kitabu cha Mughniy Al-Muhtaj, 3/438, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah.
Na amesema Ibn Qudama katika kitabu cha: [Al-Mughniy 5/250]: “Wamekubaliana wanachuoni katika zama zote ndani ya miji yote mikubwa kwamba kukodisha kunafaa, ila Abdulrahman Ibn Al-Aswamm amesema: (haifai kufanya hivyo kwa sababu ni udanganyifu), kwa maana ya kuwa mtu anaingia mkataba wa manufaa ambayo bado hayajatengezwa, na hili ni kosa. Haizuii kukubaliwa na wanachuoni ambao wamepita ndani ya zama tofauti na kuenea kwenye miji mbalimbali”.
Na vile vile katika zile hukumu zilizopitishwa kifiqhi ni kuwa inafaa kwa mwenye kukodi kukodisha sehemu aliyoikodi kwa mtu mwengine ikiwa ameshakabidhiwa, kwa sababu kukabidhiwa kitu kunachukua hukumu ya kukabidhiwa manufaa. Amesema Ibn Qudama katika kitabu cha: [Al-Mughniy 5/ 277]: “Imamu Ahmad ameizungumzia kauli hii, nayo ni kauli ya Said Ibn Al-Musayyab na Ibn Syreen, Mujahid, Ikrama, Abu Salma Ibn Abdulrahman, Al-Nakhiy, Al-Shaabiy, Shafiy na wanafikra wengine”.
Na vile vile inafaa kwake kumkodisha mtu mwengine kabla ya kukabidhiwa, kwa kauli ya baadhi ya wanachuoni. Amesema mwanachuoni Shihab Ramly katika maelezo yake juu ya kitabu cha: [Asnaa Al-Matalib cha Sheikh wa Kiislamu Zakaria Al-Ansariy katika vitabu vya Wanachoni wa Madhehebu ya Shafi 2/82, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Islamy -maelezo ya pembeni ya kitabu cha Asnaa Al-Matalib-]: “Ikiwa mtu atakodi nyumba, basi analazimika kulipa kodi yake kabla ya kukabidhi kwa kauli iliyosahihi, ni tofauti kati yake na biashara: kitu kilichoingiliwa na makubaliano: manufaa, nacho hakiwi chenye kukabidhiwa kwa kukabidhiwa kitu kingine, hakuna athari yoyote ya kukabidhi kitu ndani yake”.
Ikiwa itafaa kukodisha kitu ambacho ni sehemu ya manufaa kabla ya kukikabidhi – kwa maana ya: kitu – kwa kufaa katika huduma na manufaa kwa hatua ya kwanza, au ikasemwa: makabidhiano ya kweli hayafanyiki katika manufaa na huduma, makabidhiano huwa yanafikiwa kwa makubaliano na kwa kuingia mikataba, ambapo kukabidhi kwa kitu chochote hutokea kwa mujibu wa kitu hicho – kama ilivyoelezwa na mwanachuoni Nourdeen Al-Shabramallisy katika maelezo yake ya kitabu cha: [Nihayatul-Muhtaj 5/303, chapa ya Dar Al-Fikr].
Kwa maelezo hayo katika sura ya swali ni kuwa: Inafaa kisheria kwa benki kufanya kazi ya manunuzi ya haki ya kunufaika inayofungamana na huduma zilizotajwa na zenginezo miongoni mwa huduma mbalimbali, katika mambo yanayofungamana na kazi za uzalishaji madamu tu thamani inayohitajika imeshapangwa na kufikiwa makubaliano kwa njia ya uwazi kati ya pande mbili: upande wa benki na upande wa wateja wake miongoni mwa makampuni au watu binafsi, kwa sababu baadhi yake ni katika jumla ya vitu na baadhi yake nyingine ni katika aina ya huduma ambazo zinakuwa kuingia nazo mkataba ni sawa na kuingia mkataba kwenye manufaa, au manufaa na vitu kwa pamoja, na hili linafaa kisheria.
Huduma hii inachukua hukumu ya bidhaa yenye kuwezekana kuingia mkataba kwa malipo ya fedha taslimu au kwa awamu, kwa kutanguliza au kuchelewesha, na kwa kuongeza bei kwenye malipo ya awamu au kutoongeza bei, na inafaa wakati huo kuingia upande wa tatu au zaidi kwa ununuzi, uwakala au udalali, na kufanya malipo upande wa ununuzi kwa fedha taslimu na kujipatia kutoka kwa muuzaji ongezeko la thamani kwa sababu ya kufanya malipo kwa muda wa baadaye, hakuna kizuizi chochote cha kisheria, wakati huo hutolewa huduma inayofahamika kama sehemu ya bidhaa.
Hakuna kizuizi chochote kwenye makubalino haya kwa sababu ni makubalino ya kukodishana, ambapo benki inafanya kazi ya kukodi huduma hii kutoka kwa mhusika kisha yenyewe inaikodisha kwa wateja wake.
Ama kuhusu ulipaji wa deni kwa mdai kwa kulipa baadaye pamoja na ongezeko la thamani, kama vile benki kulipa kodi na ushuru wa forodha kwa mteja au kumlipia thamani ya huduma ambayo amehudumiwa hapo nyuma, hilo ni katika mlango wa kununua madeni, au inakuwa ni katika sehemu yake pamoja na kukubaliana kiwango na sifa. inawezekana kufuata na kuiga katila hilo pamoja na kuchunga masharti yaliyotajwa, ikiwa ni pamoja benki kupata fedha tofauti kutoka kwa mteja, ambazo amezilipa kwa upande wa tatu.
Amesema Sheikh Al-Dardiyir katika sherehe ya Al-Sagir juu ya kitabu cha: [Akarib Al-Masalik kuhusu madhehebu ya Imamu Malik 3/99, chapa ya Dar Al-Maarif]: “(Na sharti) ya kufaa (Kuuza deni: ni kuwepo mdaiwa) hilo linalazimisha kuwa kwake hai (na kukubali kwake) hilo, hapana ikiwa halitambui, na wala halijathibiti kwa dalili za wazi, kwa sababu hilo ni sawa sawa na kufanya biashara yenye ugomvi, (na kufanya malipo ya haraka), kinyume na hivyo inakuwa ni kuuza deni kwa deni, na hutangulizwa katazo, (na kuwa kwake) kwa maana: thamani (si katika uhalisia wake) kwa maana: ya deni, (au kuwa katika uhalisia wake) katika kisichokuwa kitu, (na kulingana na kiwango na sifa zake), sio inapokuwa chache, kutokana na kuwepo ulipaji mdogo katika vitu vingi, navyo ni kupitisha manufaa. (na wala siyo) deni kuuza (dhahabu) (kwa fedha na kinyume chake), ni kutokana na ulipaji wa baadaye”.
Au inakuwa ni katika mlango wa wakala, kama vile mteja anatoa uwakilishi kwa benki wa kumlipia hizi stahiki, na zile fedha zinazolipwa na benki zinakuwa ni deni kwa mteja, na kiwango kilichopo kinakuwa malipo halali ya benki kwa wakala, na malipo kwa wakala yanafaa, amesema Ibn Farhun Al-Malikiy katika kitabu cha: [Tabsirat Al-Hukkam 1/184, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah]: “Uwakala unafaa kwa malipo au pasi na malipo, ukiwa kwa malipo basi wenyewe ni ukodishaji unaolazimisha makubaliano, wala haiwi kwa mmoja kati yao kujivua, na makubaliano hayo yanakuwa kwa malipo yanayotajwa na kwa muda uliopangwa na kwa kazi inayofahamika”.
Amesema Imamu Anawawiy katika kitabu cha: [Al-Raudha 3/56, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah]: “(Somo): muda gani tumesema: Uwakala unafaa, tumetaka pasi na kuwepo malipo, ama ikiwa pamewekwa masharti ya malipo yenye kufahamika na kukutana masharti ya ukodishaji na makubaliano, na kuingiwa makubaliano kwa tamko la ukodishaji hiyo ni lazima”.
Ama benki kumpa mteja zawadi ya fedha taslimu wakati wa kulipa deni lake mapema ni jambo linalofaa na hakuna ubaya wowote ndani yake, kwa sababu benki yenyewe inafanya hivyo pasi na malipo yaliyotangulia, kwa hiyo basi hiyo inazingatiwa kuwa ni kujitolea, na kujitolea ni jambo linalohitajika kisheria, na dalili za hilo zipo wazi, miongoni mwazo ni Hadithi iliyopokelewa na Al-Baihaqiy katika kitabu chake kutoka kwa Abu Huraira R.A. kuwa Mtume S.A.W, amesema: “Peaneni zawadi mtapendana”, bali kitendo hicho ni katika jumla ya mambo ya kujipamba nayo, kutokana na kuwepo ndani yake kumfanyia wepesi mtu mwengine.
Na imepokelewa na Imamu Muslim katika kitabu chake kutoka kwa Abu Huraira R.A. kuwa Mtume S.A.W, amesema: “Mwenye kumwepesishia mwenye mazito basi Mwenyezi Mungu atamwepesishia na yeye duniani na akhera”. Na katika mapokezi ya Al-Tabraniy katika kitabu cha Al-Ausat Hadithi hii imekuja kwa tamko jingine: “Mwenye kumwepesishia Mwislamu Mwenyezi Mungu atamwepesishia na yeye duniani na akhera”.
Ama ikiwa kwa makubaliano yaliyotangulia yenyewe yanafanana na ya mwenye kudai na mwenye kudaiwa ili mwenye kudai aweze kuweka sharti kwa baadhi ya deni lake kwa mwenye kumdai, kwa kumtaka alipe mapema, na haya ni masuala yanayofahamika katika Fiqhi ya Kiislamu kama ni: “Weka na fanya haraka” kama vile mwenye kudaiwa akasema kwa mdai wake: “Weka sehemu ya deni langu na nitakufanyia haraka kilichobaki”. Jamhuri ya wanachuoni imelipitisha jambo hili. Amesema Ibn Qudama: “Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas R.A, kuwa hajaona ubaya wowote, na limepokelewa hilo kutoka kwa Al-Nakhai na Abu Thaur, kuwa alichukua baadhi ya haki zake na kuacha baadhi yake, ikafaa, kama lingekuwa deni la kulipwa hivi sasa”. Kitabu cha: [Al-Mughniy, 4/52], na kunukuliwa na Al-Sarkhasiy katika kitabu chake cha: [Al-Mabsuut kutoka kwa Zaidi Ibn Thabit R.A. 21/31, chapa ya Dar Al-Maarifa].
Nayo pia ni mapokezi toka kwa Imamu Ahmad katika baadhi ya madeni ya muda na kuondoa maelezo yaliyobaki ya Ibn Abi Mussa, na amepitisha Ibn Taiymia na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim katika wafuasi wa Imamu Hanbal. [Kitab Iilaam Al Muuqiin, 3/358, chapa ya Dar Al-Jil – Beirut].
Wakachukua dalili katika Hadithi iliyopokelewa na Al-Baihaqiy na wengine kutoka kwa Ibn Abbas R.A. kuwa Mtume S.A.W. pindi alipotoa amri ya kutolewa Bani Al-Nadhir katika mji wa Madina walikuja watu miongoni mwao, wakasema: ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, umetoa amri ya kutolewa watu lakini wao wanadaiwa na watu mbalimbali ambayo bado hayajalipwa. Mtume S.A.W, akasema: “Yawekeni na yalipwe baadaye” au akasema “na yafanyeni malipo yake baadaye”.
Na akasema Ibn Al-Qayyim katika kitabu cha: [Ilaam Al-Muwaqiin 3/358]: “Haya ni kinyume cha riba, kwani riba inakusanya ongezeko la moja ya malipo mawili kukabiliana na malipo ya baadaye, na hili linakusanya kujivua jukumu lake kutokana na baadhi ya malipo katika kukabiliana na kwisha kwa muda wa malipo, na kunufaika na kila mmoja kati ya wawili, na wala haikuwa hapa riba si kwa uhalisia, kilugha wala kufahamika kwake, kwani riba ni nyongeza. Na katika deni wanazuoni wameharamisha hivyo japo kuwa wamelinganisha na riba. Na tofauti haijifichi bali ipo wazi kati ya kauli yake: “Ima kuikuza au kuilipa”. Na kauli yake: “Nilipe haraka nitakupa mia”, ipo wapi moja wapo toka kwa nyengine, hakuna andiko katika uharamu wa hilo wala makubaliano ya wanachuoni wala uwiano sahihi”.
Amesema Imamu Abu Is-haq Al-Shiraziy katika kitabu cha: [Al- Muhaddhab 1/204): “Ikiwa ameweka sharti la kumlipa zaidi ya kile alichokopesha, kuna mitazamo miwili: Mtazamo wa pili: inafaa, kwa sababu kukopa kumerahisishwa kwa mkopaji, na sharti la kuongeza linalokuwa nje ya maudhui yake halifai, na sharti la kupunguza pale pasipoachana na maudhui yake linafaa”.
Amesema Ibn Abdul Bar Al-Malikiy katika kitabu cha: [Tamheed 4/91, chapa ya Wizara ya Waqfu na Mambo ya Kiislamu – Morocco]: “Mwenye kuruhusu –kwa maana ya: weka na fanya haraka– hayupo kwenye mlango huu – kwa maana ya: riba – na kuwa kwenye mlango unaofahamika”.
Ama kuhusu yanayofahamika kwa jina la fidia ya kuchelewesha kulipa deni au malipo ya kuchelewa ambayo yanakuwa kwa mdaiwa katika hali ya kuchelewa kwake kulipa deni ndani ya muda uliokubaliwa na kulazimika kulipa sehemu ya mali kwa mdai, hilo halifai, kwa sababu limejengeka katika misingi ya nyongeza ya mali kutokana na kuongezeka kwa muda wa kulipa deni. Na hiyo ni riba ambayo ilikuwa ikifahamika sana kwa Waarabu, na kuteremka Aya za Qurani Tukufu kwa ajili ya kuikataza.
Amesema Imamu Al-Qurtubiy katika tafsiri yake [3/348, chapa ya Dar Ashaab]: “Mara nyingi – kwa maana ya riba – ni ile waliyokuwa Waarabu wakiifanya kwa kauli yake kwa mdaiwa: “utalipa au utazidisha kwa riba!” Akawa mwenye deni anazidisha idadi ya mali na kumsubiri mwenye kuhiitaji. Haya yote ni haramu kwa makubaliano ya Jamhuri ya wanachuoni”.
Ni jukumu la benki wakati huo kutafuta njia halali ili kudhamini haki yake ya kulipwa, kama vile kuweka kitu rehani, au mdhamini, au dhamana yoyote pale yatokeyapo madhara wakati wa kulipa na kutakiwa kulipa kutokana na madhara hayo, na malipo hayo yanakuwa sawa na uhalisia wake.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.