Swala ya Raghaib.
Question
Ni ipi hukumu ya Swala ya Raghaib ambayo husaliwa na baadhi ya watu ndani ya usiku wa kwanza wa mfungo kumi?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Kilugha, neno Raghaib: lina maana ya kutoa kwa wingi, au kile kinachohimiza kufanya mambo ya heri, neno hili limekuja ndani ya vitabu vya fiqhi ya Imamu Malik, na linakusudiwa kile kinachohimizwa na sharia na kupangiliwa ambapo ikiwa kitaongezwa au kupunguzwa kwa makusudi basi huwa kinabatilika, na wala hakifanywi kwa pamoja, na huwa ni mbadala kati ya msamiati huu na Sunna pamoja na vitendo vya ziada. Wanazuoni wanalichukulia neno Raghaib kuwa ni chini ya Sunna na zaidi ya ziada inayopendelewa. [Kitabu Hashiyat Al-Dusuqiy, 1/312, chapa ya Dar Al-Fikr, na sharhu ya Kharshiy 2/2, chapa ya Dar Al-Fikr].
Wamesema: Hakuna Swala ya Raghaib isipokuwa ni moja tu nayo ni rakaa mbili za Al-Fajir. Anasema Sheikh Alish: (Raghaib imekuwa ni kama jina maarufu la rakaa mbili za Al-Fajir, [1/348, chapa ya Dar Al-Fikr]. Huu ni msamiati maalumu wa Imamu Malik.
Neno Raghaib katika misamiati ya kifiqhi: ni Swala maalumu inayosaliwa kati ya Magharibi na Isha usiku wa Ijumaa ya kwanza ya mfungo kumi, na idadi ya rakaa zake ni kumi na mbili.
Ama Hadithi iliyopokelewa kuhusu ubora wa Swala ya Raghaib imetolewa dalili ya hukumu yake na zaidi ya Imamu mmoja, miongoni mwao ni Al-Iraqiy katika kitabu cha: [Takhrij Ahadith Al-Ihyaa 2/366, chapa ya Dar Al-shaab], na Al-Ajlouniy katika kitabu cha: [Kashf Al-Khafaa 2/31, chapa ya Al-Maktaba Al-Asriya], na Ibn Al-Juuzy katika kitabu cha: [Al-Maudhuat 2/125, chapa ya Al-Maktaba Al-Salafia Al-Madina Al-Munawara).
Swala hii ni uzushi wenye kupingwa umeonekana hivyo kupitia ibara za fiqhi kwa kauli ya kutotambulika kisharia, na pia haina dalili.
Anasema Ibn Abideen katika kitabu chake [2/26, chapa ya Dar Al-Fikr]: Amesema katika kitabu Al-Bahr: “Mpaka hapa inaonesha kuchukiza kukutana kwa pamoja na kuswali Swala ya Raghaib ambayo huswaliwa ndani ya mfungo kumi usiku wa kwanza wa Ijumaa yake, yenyewe ni uzushi.
Na kupitia mwanachuoni Nur Al-Din Al-Maqdisiy kuna kitabu kizuri alichokiita “Rad Al-Raghaib” ameelezea maelezo mengi ya wanachuoni wa zamani na waliofuata baada yao miongoni mwa wanachuoni wa madhehebu manne”.
Anasema Imamu An-Nawawiy katika kitabu cha: [Al-Majmuu, 4/56, chapa ya Dar Al-Fikr]: “Swala inayofahamika kwa jina la Swala ya Raghaib, ambayo ina rakaa kumi na mbili na huswaliwa kati ya Magharibi na Isha ndani ya usiku wa Ijumaa ya kwanza ya mfungo kumi, na Swala ya usiku wa nusu ya mwezi wa Shaaban kwa kuswaliwa rakaa mia moja, Swala hizi mbili ni uzushi mtupu na zenye kuchukiza na mbaya, wala hazizingatiwi kutajwa kwake ndani ya kitabu cha Qut Al-Qulub na Ihyaa Ulum Al-Din wala Hadithi zilizotajwa ndani ya vitabu hivyo, vyote hivyo ni batili, wala haizingatiwi kwa baadhi ya yaliyofanana hukumu zake kutoka kwa Maimamu, kwa kuandikwa kwenye makaratasi juu ya kupendezeshwa kwake ni makosa, Sheikh Abu Muhammad Abdulrahman Ibn Ismail Al-Maqdisiy ametunga kitabu kizuri kinachoelezea ubatilifu wa Swala hizo, Sheikh ameandika vizuri na kufafanua vyema”.
Amesema pia Imamu An-Nawawiy katika kitabu cha: [sharhu ya Muslimu 8/20, chapa ya Dar Ihyaa Al-Turath Al-Arabiy]: “Ni adui wa Mwenyezi Mungu mwandishi wake na aliyezivumbua Swala hizo, kwani zenyewe ni uzushi wenye kupingwa ni miongoni mwa uzushi ambao ni upotovu na ujinga, ndani yake kuna machukizo ya wazi. Jopo la Maimamu wametunga vitabu kuelezea ubaya wake na upotovu wa mwenye kuziswali na yule aliyezivumbua, na dalili za ubaya wake na ubatilifu wake pamoja na upotovu wa mwenye kuzitekeleza ni nyingi mno”.
Na anasema Ibn Hajar Al-Haitamy katika fatwa zake [1/217, chapa ya Dar Al-Fikr]: “Ama Sala ya Raghaib yenyewe ni kama Sala inayofahamika ya usiku wa nusu ya mwezi Shaaban zenyewe ni uzushi mbaya na Hadithi zake ni za kuwekwa, basi inachukiza kuziswali mtu mmoja mmoja au kuziswali kwa pamoja”.
Katika utangulizi wa kitabu cha: [Ibn Haj (1/293, chapa ya Dar Al-Turath]: “Na katika uzushi ambao umezushwa ndani ya mwezi huu mtukufu - kwa maana ya mwezi wa mfungo kumi - ni kuwa, usiku wa Ijumaa ya kwanza ya mfungo kumi watu huswali ndani ya usiku huo kwenye Misikiti ya Ijumaa na ya kawaida Swala ya Raghaib, wanakusanyika ndani ya baadhi ya Misikiti ya Ijumaa na ile ya kawaida ndani ya miji mbalimbali wakiwa wanatekeleza uzushi huu na wakiuonesha ndani ya Misikiti kwa kuswali pamoja wakiwa wanaongozwa na Imamu, kana kwamba ni Swala inayokubalika kisharia…. Ama madhehebu ya Imamu Malik R.A. yanasema Swala ya Raghaib inachukiza kuiswali, kwa sababu haikuwa yenye kuswaliwa huko nyuma, na mambo ya heri yote yapo kwenye kuwafuata wao R.A.”.
Na anasema Imamu Al-Bahutiy katika sherehe ya kitabu cha Al-Muntaha (1/252, chapa ya Aalam Al-Kutub): “Swala ya Raghaib na iliyozoeleka ile ya usiku wa nusu ya mwezi wa Shaaban ni uzushi mtupu hazina asili wala msingi, ameyasema haya Sheikh Taqiy Al-Din”.
Amenukuu Al-Taj Al-Sabaky katika ufasiri wa Al-Izz Ibn Abdulsalam kuzuiliwa kwa Swala hizi na kauli ya uzushi wake, kumepokelewa mapokezi kumi na tatu ya kauli za kutokuwa halali kisharia Swala hizi, amesema kwenye kitabu cha Tabaqat Al-Shafiya Al-Kubra (8/252 - 254, chapa ya Dar Hijr):
Kauli ya Kwanza: Mwanachuoni ikiwa ataziswali Swala hizi inadhaniwa na kuchukuliwa na jamii kuwa ni katika ibada za Sunna, basi anakuwa ni mwenye kumsemea uongo Mtume S.A.W. kwa kauli za hivi sasa, na kauli za hivi sasa huenda ikawa ndiyo kauli zinazosemwa.
Kauli ya Pili: Mwanachuoni ikiwa ataziswali anakuwa ni mwenye kusababisha umma kumfanyia uongo Mtume S.A.W. - wanasema hii ni Sunna miongoni mwa Sunna, na kusababisha uongo kwa Mtume S.A.W. - ni jambo lisilofaa.
Kauli ya Tatu: Kitendo cha uzushi ambacho kinatoa nguvu kwa wazushi waliokiweka na kukizusha pamoja na kuzama katika ubatilifu na kusaidia hali hiyo ni jambo lisilokubalika katika sharia, kufanyia kazi uzushi na maudhui zake ni jambo la kukemewa kwa wawekaji na wazushi wake, na kukemea uovu ni katika mambo makubwa yaliyoletwa na sharia.
Kauli ya Nne: Swala yenyewe inakwenda kinyume na Sunna katika kuleta utulivu ndani ya Swala, kwa kuleta kwa wingi surat Al-Ikhlas mara kumi na mbili na kusoma kwa wingi pia surat Al-Qadr, mara nyingi idadi yake haiji isipokuwa kunapelekea kukosekana utulivu wa baadhi ya viungo, na kuonekana kwenda kinyume na Sunna katika kuleta utulivu wa viungo.
Kauli ya Tano: Swala yenyewe inakwenda kinyume na Sunna katika kuleta unyenyekevu wa moyo na kuuhudhurisha kwenye Swala pamoja na kuutenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuzingatia utukufu wake na ukubwa wake pamoja na kusimama kwenye maana za Aya zinazosomwa na katika kumtaja Mwenyezi Mungu, hivyo anapozingatia idadi kadhaa ya sura kwa moyo wake anakuwa ni mwenye kumgeukia Mwenyezi Mungu akitekeleza amri ambayo haina uhalali kwenye Swala, na kugeuka kwa sura ni kubaya kisharia, basi inakuwaje kugeuka kwa moyo ambao ndiyo makusudio makubwa.
Kauli ya Sita: Swala yenyewe inakwenda kinyume na Sunna za ziada, kwani Sunna kwa mwenye kuitekeleza nyumbani ni bora kuliko kuitekeleza msikitini isipokuwa ile iliyovuliwa na sharia kama vile Swala ya kuomba mvua na Swala ya kukamatwa kwa jua na mwezi, na Mtume S.A.W. Amesema: “Swala ya mtu kuswali nyumbani kwake ni bora zaidi kuliko kuswali msikitini isipokuwa Swala za lazima”.
Kauli ya Saba: Swala yenyewe inakwenda kinyume na Sunna, ni kuwa na muundo wa pekee katika ibada za ziada, Swala za Sunna huswali mtu peke yake isipokuwa zile zilizovuliwa na sharia, na wala uzushi wa aina hizi mbalimbali kwa Mtume hazitoki kwake.
Kauli ya Nane: Swala yenyewe inakwenda kinyume na Sunna, katika Sunna ni kuharakisha kufuturu ambapo Mtume S.A.W, Amesema: “Umma wangu hautoacha kuwa kwenye heri kila wanavyoharakisha muda wa kufuturu na kuchelewesha muda wa kula daku”.
Kauli ya Tisa: Swala yenyewe inakwenda kinyume na Sunna katika kuuweka moyo huru na mambo yenye kuleta hali ya wasi wasi kabla ya kuingia kwenye Swala, kwani Swala hii anaingia mtu akiwa ni mwenye njaa na kiu hasa ndani ya masiku ya joto kali, Swala za kisharia haingii mtu katika hali hiyo pamoja na kuwepo jambo la kushughulisha linawezekana kuondoshwa.
Kauli ya Kumi: Ni kuwa sijda zake ni zenye kuchukiza, kwani haijapokelewa kwenye sharia mtu kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kwa kuleta sijda ya kipekee isiyo na sababu, kwani kujiweka karibu kuna sababu, masharti, nyakati na nguzo ambapo haifai kinyume na hivyo, ni kama vile hakuna kujiweka karibu kwa Mwenyezi Mungu kwa kusimama kisimamo cha Arafa, Muzdalifa, kurusha vijiwe kwenye jamarati, kutembea kasi kati ya eneo la Saffa na Marwa pasi na utaratibu ulio ndani ya wakati wake, na si kwa sababu na masharti ya mtu mwenyewe, na vile vile hakuna kujiweka karibu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa sujudu ya kipekee, na ikiwa ni kujiweka karibu basi kuna sababu zilizo sahihi, na vile vile hakuna kujiweka karibu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Swala na funga ndani ya wakati wote na muda wote, kwani huenda kujiweka karibu kwa Mwenyezi Mungu kwa wajinga ni kuleta mambo yanayowaweka mbali na Mwenyezi Mungu pasi na wenyewe kujitambua.
Kauli ya Kumi na Moja: ikiwa sijda zake mbili zingekuwa ni halali basi zingetofautiana na Sunna katika unyenyekevu na utulivu kutokana na idadi ya tasbihi ndani ya sijda.
Kauli ya Kumi na Mbili: Hakika Mtume S.A.W. Amesema: “Msihusishe usiku wa Ijumaa pekee kwa ibada kati ya siku mbalimbali, wala msihusishe siku ya Ijumaa kwa kuifunga kati ya masiku mengine mbalimbali isipokuwa ikiwa imeangukia siku ya funga ya mmoja wenu”. Hadithi hii imepokelewa na Muslim katika sahihi yake.
Kauli ya Kumi na Tatu: Katika Swala hizo kuna kwenda kinyume na Sunna katika yale yaliyoteuliwa na Mtume S.A.W. kwenye utajo unaotumika ndani ya sijda kwani pindi ilipoteremka kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Litakase jina la Mola wako Mlezi Aliye juu kabisa} [AL AALA, 01].
Akasema Mtume S.A.W.: “Litajeni kwenye sijda zenu” na kauli yake: “Subbuh Quddus” ikiwa ni sahihi kutoka kwa Mtume S.A.W. basi isingefaa kwa Mtume kuihusisha kipekee pasi na kusema “Subhana Rabbiya Al-a’laa” wala kuwapa umma wake, kinachofahamika ni kuwa, hayafanyiwi kazi isipokuwa maneno yaliyo bora, na katika kauli yake S.A.W.: “Subhana Rabbiya Al-A’laa” kuna sifa zisizokuwepo kwenye kauli ya: “Subuh Quddus” kisha akasema: “Hakuna yeyote kuchukua kama ushahidi na dalili kwa Hadithi iliyopokelewa toka kwa Mtume S.A.W. kuwa Amesema: “Swala ibada bora iliyowekwa”, kwani maneno haya yanahusisha Swala zilizo halali kisharia.
Kutokana na maelezo yaliyotangulia yanafahamisha kuwa, Swala ya Raghaib inayoelezewa hukumu yake ni uzushi wenye kuchukiza katika Uislamu hakuna dalili ya uhalali wake kisharia, wala haifai kuiswali kama ilivyoonesha hivyo kupitia madhehebu ya wanachuoni pamoja na ibara mbalimbali za Wanafiqhi.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukuf ni Mjuzi zaidi.