Kuchinja Mnyama wa Kujistrehesha Ka...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuchinja Mnyama wa Kujistrehesha Kabla ya Siku ya Idi Kubwa.

Question

Mtu alichinja mnyama wa kujistarehesha baada ya kuutekeleza ibada yake ya Umra, lakini kabla ya Siku ya Idi kubwa, na sisi tulimpinga kwa kufanya hivyo, lakini yeye alituambia kuwa yeye aliwauliza baadhi ya wanazuoni ambao walitoa fatwa kuwa kufanya hivyo inajuzu, kwa hiyo akaamua kufanya. Je, ni sahihi hivyo alivyofanya?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Mwenye kujistarehesha katika Hija anachinja mnyama kwa sababu anazikusanya ibada mbili pamoja katika safari moja, na kwa kwaida waislamu wanachinja wanyama wao katika Siku ya Idi kubwa au katika siku moja ya siku tatu zinazoifuata Siku ya idi kubwa ziitwazo siku za kusherehekea (Siku za Tashriiq); kwa hiyo watu, kwa urahisi, wanampinga mtu anayefanya kinyume na hivvyo, bila ya kujaribu kutafuta asili ya hukumu ya suala hili, huenda kuna wanazuoni wenye jitihada zao walioeleza kuwa kufanya hivyo inajuzu.
Asili ya suala hili ni kuwa uwajibikaji wa kuchinja mnyama wa kujistarehesha katika Hija una sababu, nayo ni kuzikusanya ibada mbili katika safari moja; kwa hiyo mkusanyaji (Qaarin) katika Hija analazimika vile vile kuchinja mnyama, kwa kuwepo sababu ile ile.
Kwa hiyo ingawaje ni bora kuchinja katika Siku ya Idi kubwa na Siku za Minaa kwa ajili ya kujiepusha na hitilafu, lakini pia inajuzu kuchinja mnyama kuanzia Ihramu ya Hija; hasa swali hili limeulizwa baada ya kuchinja na kurejea katika Msikiti Mtakatifu.
Dalili ya hayo ni kwamba uwajibikaji wa kuchinja mnyama katika Hija unakwenda sambamba na Ihramu ya Hija, kwani hiyo ni sababu ya uwajibikaji wake, nayo ilikuwepo, na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndiyo akahiji, basi achinje mnyama aliyesahilika}. [AL BAQARAH: 196], na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ile ile: {Na asiyepata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakaporudi (kwenu)}.
Yaani kufunga siku tatu katika Hija, ndani ya siku za kushughulika na Hija, baada ya Ihramu na kabla ya kuvunja ihramu. Na kuchinja huwa kunafanywa ndani ya siku hizi; kwa sababu ni jambo la msingi ya msingi, na kufunga ni mbadala, na hakuna kutofautisha kati ya hukumu isipokuwa dalili ya maandiko. Kwa vyovyote iwavyo, damu ya kustarehesha katika Hija ni karibu sana na fidia kuliko damu ya Kichinjo (Udh-hiya), ambayo baadhi ya wanazuoni waliilinganisha na damu ya kustarehesha.
Na huu ni mwelekeo wa wafuasi wa madhehebu ya Imamu Shafi; Al-Khatwib As-Shirbiniy katika kitabu cha: [Sharh Al-Minhaj [Mughniy Al-Muhtaj: 2/290, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah] anasema: “(Wakati wa uwajibikaji wa damu) kwa mtu ni (Ihramu yake ya Hija); kwa sababu hapo anakuwa mtu huyu ni mwenye kujistarehesha kwa Umra mpaka Hija.
Na huenda ikafahamika kuwa haijuzu kuitanguliza, na huu si muradi, lakini ni sahihi zaidi kumchinja mnyama wake atakapomaliza Umra. Na inasemaekana kuwa inajuzu akiitekeleza Ihramu ya Umra bila ya kuainisha wakati maalum wa kuchinja, mfano wa damu zote za fidia. Lakini (ni bora zaidi kumchinja katika Siku ya Idi Kubwa) kwa ajili ya ufuasi, na kutoka kwa hitilafu ya Maimamu Watatu; ambao walisema: haijuzu kuchinja katika wakati mwingine, na hii haikunukuliwa kutoka kwa Mtume S.A.W., wala mtu kati ya waliokuwa naye kuwa aliwahi kuchinja kabla ya wakati huu”. [Mwisho}.
Al-U’mraniy katika kitabu cha: [Sharh Al-Muhadhab], miongoni mwa vitabu vya madhehebu ya Shafiy, anasema: “Kuhusu wakati wa uwajibikaji wa damu ya kustarehesha kwa yule mwenye masharti yake, kwa rai yetu, inawajibika anapoanza Ihramu ya Hija, na hii ni rai ya Imamu Abu Hanifa. A’ataa’ anasema: haiwajibiki mpaka anasimame A’rafa. Na Imamu Malik anasema: "Haiwajibiki mpaka anatupa Jiwe la A’aqaba", anazingatia ukamilifu wa Hija.
Na dalili yetu ni kauli ya Mwenyezi Mungu: {basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndiyo akahiji, basi achinje mnyama aliyesahilika}. [AL BAQARAH: 196], na huyo alifanya hivyo; kwa sababu inatosha mwanzo kwa kulifikia lengo, kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu: {Kisha timizeni Saumu mpaka usiku}. [AL BAQARAH: 187]; kwa sababu masharti yapo ambapo ipo Ihramu ya Hija, kwa hiyo uwajibikaji uaambatana nayo. Na kuhusu wakati wa kuchinja: ni bora asichinje isipokuwa katika Siku ya Idi kubwa, na kama akichinja baada ya Ihramu na kabla ya Siku ya Idi kubwa, basi inajuzu kwa rai yetu. Na Maimamu Malik na Abu hanifa wanasema: (Haijuzu).
Dalili yetu kuwa ni damu inayoambatana na Ihramu, basi inajuzu kuitoa kabla ya Siku ya Idi Kubwa, mfano wa damu ya manukato na nguo. Na kama akichinjwa baada ya kuitekeleza ibada ya Umra na kabla ya Ihramu ya Hija.. basi kuna rai mbili, ambazo alizitaja Abu Ali katika kitabu cha: [Al-Ifswaah], na pia alizozitaja Al-Masu’udiy, nazo ni: Kwanza: haijuzu, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndiyo akahiji, basi achinje mnyama aliyesahilika}. [AL BAQARAH: 196].
Na kama asipoitekeleza Ihramu ya Hija basi kustarehesha hakupo; na uchinjo wa mnyama unaambatana na kazi ya mwili, nayo ni kuzigawanya nyama zake, kwa hiyo haijuzu kuitanguliza, ingawa ni wajibu, kama vile kufunga. Pili: inajuzu, nayo ni rai sahihi; kwa sababu ni haki ya mali inayoambatana na sababu, na kama sababu moja au zaidi zikipatikana, basi inajuzu kuitanguliza sana kuliko mabaki yake, kama vile Zaka baada ya kumiliki sehemu maalum ya mali na kabla ya kupita mwaka kamili, na pia kafara ya yamini baada ya kuiapa na kabla ya kuivunja. Na kama akitaka kuchinja baada kuitekeleza Ihramu ya Umra na kabla ya kuimaliza; wanazuoni wa Baghdad wanasema: haijuzu kwa kauli moja, lakini Al-Masu’udiy alisema: kama tukisema: inajuzu kuchinja baada ya kuimaliza Umra na kabla ya Ihramu ya Hija, Je, inajuzu kuchinja kabla ya kuumaliza Umra? Kuna rai mbili:
Kwanza: inajuzu kufanya hivyo; kwa sababu ya kupatikana baadhi ya sababu za uwajibikaji, nazo ni kuanzia Umra, akawa kama kwamba alichinja baada ya kumaliza Umra.
Pili: haijuzu kufanya hivyo, nayo ni sahihi; kwani sababu moja ya uwajibikaji kamili, nayo ni Umra, haikupatikana, akawa kama kwamba alichinja kabla ya Ihramu ya Umra”. [Mwisho]. [Al-Bayaan: 4/91, Ch. ya Dar Al-Minhaj, Jeddah]
Al-Mawardiy katika kitabu cha: [Sharh Mukhtaswar Al-Muzaniy], miongoni mwa vitabu vyao, anasema: “Kama yakipatikana masharti ya kustarehesha yanayowajibisha damu basi kuna hali mbili: Hali ya utajiri na hali ya ufakiri. Kama akiwa tajiri basi analazimika kumchinja kondoo, ambapo analazimika kwake baada ya kuumaliza Umra, na kwenye Ihramu yake ya Hija, na akiitekeleza ihramu ya Hija atalazimika na damu; kwa sababu masharti yanayolazimisha damu hayapatikani ila baada ya kuanzia Hija, na kama akitaka kumchinja mnyama , basi ana hali nne:
Kwanza: ni hali ya hiari: nayo itakuwa katika Siku ya Idi Kubwa.
Pili: hali ya kujuzu, nayo itakuwa baada ya Ihramu ya Hija, na kbla ya Siku ya Idi Kubwa, na hii inajuzu kwa rai yetu. Imamu Abu Hanifa anasema: haijuzu ila katika Siku ya Idi Kubwa, kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjioni mwao}. [AL BAQARAH: 196], na machinjioni mwao ni Siku ya Idi Kubwa; na kwa sababu ya kumchinja mnyama, basi haijuzu kabla ya siku ya Idi Kubwa, kulingana na mnyama wa kufukia na vichinjo, na dalili yetu ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndiyo akahiji, basi achinje mnyama aliyesahilika}. [AL BAQARAH: 196].
Kwa hiyo tulijua kuwa analazimika au anajuzu kwake kuchinja mnyama atakapojistarehesha Umra kwa Hija, kutokana na dalili zote tulizozisema; na kwa sababu ni fidia ya kustarehesha, basi inajuzu itekelezwe kabla ya Siku ya Idi Kubwa, na asili yake ni kufunga, na kwa sababu ni kichinjo cha kafara, basi inajuzu kufanywa baada ya uwajibikaji wake, na kabla ya siku ya Idi Kubwa, kulingana na Kafara ya maradhi na malipo ya mawindo. na kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {mpaka wanyama hao wafike machinjioni mwao}, maana ya mahali hapa ni: damu na siyo Siku ya Idi Kubwa, kwa dalili ya kauli yake mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kisha mahali pa kuchinjwa kwake ni (karibu na) ile nyumba kongwe ya Kale}, na kulingana na mnyama wa sadaka na vichinjo, hakika maana yake ni kuwa hakuna mbadala wake.
Tatu: Kumchinja mnyama baada ya kutimiza Umra, na kabla ya Ihramu yake ya Hija, kuna kauli mbili: iliyo sahihi zaidi na kutajwa katika kitabu cha: [Al-Imlaa’]: ni kujuzu; kwa sababu haki za mali zikiambatana na vitu viwili, inajuzu kuvitanguliza hali ya kuwepo kitu kimoja kati yake, kama vile; aina za Zaka, aina za kafara, na pia damu ya kustarehesha, ambapo inawajibika kwa vitu vinne; kwa kutimiza Umra basi vitu viwili vimepatikana, navyo ni kuwepo kwake katika Msikiti Mtakatifu, na kabla ya Umra ndani ya miezi ya Hija, kwa hiyo inajuzu kutanguliza damu. Na kauli ya pili: haijuzu, kulingana na kufunga, na hii iliyonukuliwa na Ibn Khairaan kuhusu kustarehesha.
Nne: Kumchinja mnyama kabla ya kuutimiza Umra, hapo hakuna hitilafu ya madhehebu kuwa: haijuzu kabisa, kwa sababu ya kutokuwepo sababu nyingi sana”. [Mwisho]. [Al-Hawiy Al-Kabiir Fi Fiqh Madh-hab Al-Imam Ashafiy: 4/51, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah, Bairut, Lebanon].
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia na katika uhalisia wa swali: Kazi iliyofanywa na mtu huyo kwa kumchinja mnyama wake kabla ya Siku ya Idi Kubwa, inajuzu kisheria, na ina-kubaliwa ibada yake; kutokana na kauli ya wanachuoni walioijuzisha.
Na mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas