Tofauti Baina ya As-Salam na Al-Ist...

Egypt's Dar Al-Ifta

Tofauti Baina ya As-Salam na Al-Istisnaa na Kuuza Kitu Kisichokuwepo Mikononi mwa Mtu.

Question

 Nini tofauti kati ya makubaliano ya uuzaji wa As-Salam au Al-Istisnaa ambapo wanafiqhi wamesema inafaa kisharia, na kuuza kitu ambacho hakipo mkononi mwa mtu ambapo imekuja Hadithi ikikataza uuzaji huu?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Hukumu za fiqhi zimeweka sharia za miamala ya kifedha na mengineyo ili watu kufikia manufaa na kukidhi mahitaji yao kupitia miamala hiyo, hivyo basi kufanya hivyo katika wigo wa amri na makatazo ya kisharia ambayo yanafanya kazi kwa lengo la kufikia usawa kwa kila upande kupata manufaa yake kwa kushirikiana na upande mwengine, na kuzuia yale yatakayopelekea mpasuko na tofauti pamoja na mvutano kati ya pande mbili, kwani kuondoa migongano na mivutano ni jambo muhimu, ambapo hiyo mivutano ndiyo sehemu ya uharibifu. [Kitabu Badaii As-Sanaii, 5/143, 7/2. Dar Al-Kutub Al-Elmiya], anasema mwanachuoni Al-Qarafiy katika kitabu cha: [Al-Furuq, 3/290, chapa ya Alam Al-Kutub]: Na hii hapa kanuni: Kinachotakiwa na Sharia ni masilahi ya pande mbili na kuondoa uharibifu na fitina, hilo linafikiwa kwa kauli ya Mtume S.A.W. “Hamtaingia Peponi mpaka mpendane”.
Imepokelewa na watu wa Sunna kutoka kwa Hakiim Ibn Hizam R.A. kuwa amesema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ananijia mtu na anataka nimwuzie kitu ambacho siko nacho, je nimwuzie kutoka sokoni? Mtume S.A.W. akasema: Hapana usiuze kitu ambacho hauko nacho”.
Hadithi imeonesha ujumla wa katazo la kuuza kitu chochote kabla mtu hajakuwa nacho na kuwa mikononi mwake, na kabla ya kuwa na uhakika wa uwezo wa kukikabidhi, katika mlango huu linaingia katazo zaidi la kuuza kitu kisichokuwepo, na maana hii inasisitiza yale yaliyokuja katika Hadithi nyengine inayotokana na Ahamd katika musnad yake kutoka kwa Hakiim Ibn Hizam amesema: “Niliuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi naweza kununua kitu cha kuuza, basi ni ipi halali kwangu na ipi haramu kwangu? Mtume akasema: Pindi unaponunua kitu cha kuuza basi usikiuze mpaka uwe nacho mkononi”.
Kuenea katazo hili katika kila kitu cha kuuzwa ndiyo kulivyoeleweka na mfasiri wa Qurani Tukufu Ibn Abbas R.A. kutokana na Hadithi ya Mtume S.A.W. imepokelewa na Imamu Bukhari na Muslim kutoka kwa Ibn Abbas amesema: Amesema Mtume S.A.W.: “Mwenye kutaka kuuza chakula basi na asiuze mpaka kiwe mikononi mwake”. Amesema Ibn Abbas: Ninazingatia kila kitu sawa na utaratibu wa chakula.
Ikiwa kusudio la Sharia ni kuziba mlango huu ili kufikia masilahi na kuondoa madhara kwa kuondoa viashiria vya mivutano na magomvi, hivyo hakuna shaka kuwa masilahi na hitajio kubwa ni vyenye kuhitaji wepesi kwenye baadhi ya miamala ambayo imekuwa ni kawaida matatizo, lakini mara nyingi bila ya kupelekea dhuluma au uharibifu au mivutano, uwekwaji Sharia mfano katika miamala kama hii huitwa: Sharia kinyume na asili, au kinyume na kipimo, au kinyume na kanuni, miongoni mwa Sharia hizo ni pamoja na makubaliano yanayofahamika kama makubaliano yenye udanganyifu ambayo yamepitishwa na Sharia pale panapo kuwepo hitajio kubwa, mfano huu ni sawa na makubaliano ya biashara ya As-Salam na Al-Istisnaa. [Kitabu Al-Ashbah wa An-Nadhair cha Ibn Najeem, 1/293 – 294, pamoja na kitabu Ghamz U’yuun Al-Basair, chapa ya Dar Al-Kutub Al- Elmiya, na kitabu Hashiyat Ar-Ramliy ala Asna Al-Matalib, 2/122, chapa ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy].
Neno As-Salam kwa upande wa lugha lina maana nyingi: miongoni mwa maana hizo ni pamoja na Kutoa na Kuacha lakini pia huitwa As-Salaf (ukopaji), misamiati yote ina maana ya kutoa dhahabu au fedha kwa bishaa zinazofahamika na kwa muda unaojulikana, kama kwamba unakuwa umekabidhi thamani ya kitu kwa maana umefanya malipo hivi sasa kwa mtu atakayekuwa na bidhaa hapo baadaye. [Angalia Kamusi ya Lisan Al-Arab, 12/259, 9/158, chapa ya Dar Sadir].
Lakini Kwa upande wa Sharia neno As-Salam lina maana: Kuuza kitu kilicho kwenye wajibu wako, na hii ni sifa yake ya kufikiwa makubaliano, imeitwa uuzaji wa aina hii kwa jina la As-Salam kwa sababu unaweza kukabidhi mtaji kwenye kikao, na imeitwa kwa jina la Salaf kwa sababu unaweza kukabidhi mtaji hapo baadaye, [Kitabu cha Mughniy Al-Muhtaj, 3/3–4, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya]. Na pamesemwa tena As-Salam ni: Kununa kitu kwa kipindi kijacho malipo yanafanyika sasa hivi kwenye kikao, au kuuza kitu sasa hivi makabidhiano yake ni hapo baadaye. (Rejea Hashiyat Ibn Abideen, 5/209, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya, na Kashaf Al-Iqnaa cha Al-Bahutiy, 3/285, chapa ya Dar Al-Kutub Al- Elmiya).
Na asili ya uhalali wa biashara kwa njia ya As-Salam ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi mlioamini! Mnapokopeshana deni kwa muda uliowekwa, basi andikeni}[AL BAQARAH, 282].
Amesema Ibn Abbas R.A.: “Aya hii imeteremka katika masuala ya biashara ya As-Salam”. Na Hadithi iliyopokelewa na Imamu Bukhari na Muslim katika vitabu vyao kutoka kwa Ibn Abbas R.A. kuwa: “Mtume S.A.W.. alipofika Madina aliwakuta watu wakifanyiana biashara ya kukopeshana matunda kwa muda wa miaka miwili na miaka mitatu, Mtume akasema: Mwenye kufanya biashara ya kukopesha basi akopeshe katika kipimo kinachofahamika uzito wenye kufahamika na kwa muda unaofahamika”. Na imethibiti makubaliano ya wanachuoni uhalali wa biashara ya As-Salam. [Kitabu cha Mughniy Al-Muhtaj, 3/3 na Kitabu cha Kashaf Al-Qanaa, 3/285].
Makubaliano ya biashara kwa njia ya As-Salam ni yenye kuhitajika, kutokana na hali hiyo kuhalalishwa kwake kunakusudia kuondoa uzito na matatizo kwa watu, kwa mfano mkulima anakuwa hana fedha ambazo atazitumia katika kazi za kilimo, na kilimo chake kinachukua muda mpaka kufikia mavuno na kunufaika na thamani ya mavuno yake, kipindi chote anakosa mtu wa kumkopesha fedha anazozihitaji kwa kazi zake za kilimo, hivyo basi anakuwa ni mwenye kuhitaji sana aina ya miamala itakayomwezesha kupata fedha kwa ajili ya kazi zake, kinyume na hivyo basi anaweza kupitwa na masilahi ya kuwekeza kwenye ardhi yake au shamba lake, na kuwa katika mazingira magumu na shida, kwa sababu hiyo imehalalishwa biashara ya As-Salam, amesema Ibu Quddama katika kitabu cha: [Al-Mughniy, 4/185, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy]: “Kwa vile watu wanahitaji, na kilimo cha nafaka, matunda na biashara mbalimbali ni zenye kuhitaji kugharamiwa, na kwa gharama hizo ndizo hukamilika, wakati mwengine mtu hushindwa kugharamia, hivyo ikaruhusiwa kwao kufanya biashara ya As-Salam ili wapate kugharamia kilimo chao kwa wepesi”.
Wanachuoni wametofautiana kwenye uhalali wa makubaliano au mkataba wa As-Salam kwa mujibu wa kipimo cha Sharia na kanuni kuu za Sharia, kuwa je As-Salam imekuja katika hali ya dharura tu tofauti na kipimo cha Sharia kutokana na kuhitajika sana na watu makubaliano haya? Jopo la wanachuoni wameona kuwa As-Salam ni makubaliano yaliyo halali tofauti na kipimo cha Sharia, amesema Al-Kassaniy katika kitabu cha: [Badaii As-Sanaii 5/212, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmliya]: “Ruhusa katika Sharia ni jina linalobadilisha kitu asili kwa kutokea udhuru au dharura ili kurahisisha na kufanya wepesi, kama vile ruhusa ya kula kilicho kufa, kunywa pombe kwa kutenzwa nguvu njaa na mfano wa hayo, ruhusa kwenye biashara ya As-Salam ni kubadilisha hukumu asili, nayo ni uharamu wa kuuza kitu ambacho hakipo mikononi mwa mtu na kuwa halali kwa kutokea udhuru au dharura ili kuokoa mtu kufilisika”.
Na akasema Ibn Najeem katika kitabu cha: [Al-Bahr Ar-Raiq 6/169, chapa ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy: “As-Salam ni tofauti na kipimo cha Kisharia, ambayo ni kuuza kitu kisichokuwepo, badala yake As-Salam ni wajibu kwa Aya na kauli za wanachuoni kutoka na kuhitajika kwake sana kwa watu”.
Katika kitabu cha: [Minah Al-Jalil] miongoni mwa vitabu vya wafuasi wa Imamu Malik [5/331, chapa ya Dar Al-Fikr]: “Amesema katika kitabu kuwa kazi za As-Salam ni ruhusa ya dharura ya kuuza kitu kisichokuwepo kwa muuzaji”.
Amesema Sheikh wa Kiislamu Zakaria Al-Answariy katika kitabu cha: [Asna Al-Matalib 2/122, chapa ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy]: “biashara ya As-Salam ni makubaliano yasiyokuwa wazi lakini inafaa kutokana na kuhitajika kwake”.
Amesema Al-Bahutiy Al-Hanbaliy katika kitabu cha: [Sharehe ya Muntaha Al-Iradaat 2/92, chapa ya Alam Al-Kutub]: “Biashara ya As-Salam imeruhusiwa kwa ajili ya kuwepesisha”.
Amesema Ibn Taimiah na Ibn Al-Qayyim katika wafuasi wa Imamu Hanbal kuwa: As-Salam ni makubaliano halali Kisharia kulingana na kipimo cha Sharia, na wala hakuna ndani yake ukiukaji wa kanuni halali za Kisharia. Amesema Ibn Al-Qayyim katika kitabu cha “Iilam Al-Muwaqqiina”: “Ama As-Salam, kwa mwenye kudhani kuwa ipo kinyume na kipimo cha Sharia anafahamika kuingia kwake kwenye uelewa huu wa kauli ya Mtume S.A.W.. inayosema: “Usiuze kitu usichokuwa nacho” huu ni uuzaji wa kitu hakipo, na kipimo cha Sharia inazuia kufanya biashara kwa sura hiyo. Killicho sahihi ni kuwa, As-Salam ipo sawa na kipimo cha Sharia, kwani yenyewe ni uuzaji wenye dhamana mara nyingi ni wenye kuwezekana kukabidhi bidhaa au mazao ndani ya wakati wake, nayo ni kama vile ulipaji fidia katika manufaa ya upangishaji, na imeshaelezewa kuwa As-Salam ni sawa tu na viwango vya Sharia.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amewafungulia watu wenye akili na fikra kutofautisha kati ya uuzaji wa mtu kitu asichomiliki wala hana uwezo nacho, na kati ya As-Salam yenye mazingira yaliyo na dhamana katika jukumu lake mtu, na kawaida anakuwa ni mwenye uwezo wa kukabidhi mazao ya kilimo”. (1/301, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya) Amezungumzia mwanachuoni Al-Kamal Ibn Al-Hamam mtazamo huu katika kitabu cha: [Fath Al-Qadir] na kurefusha maelezo yake. [7/71 – 72, chapa ya Dar Al-Fikr].
Ama kwa upande wa Al-Istisnaa, ambapo kilugha ni chanzo cha neno: kutaka kutengenezewa kitu: Kwa maana ya kutoa wito wa kutengenezwa kwake, na inasemwa kwa mfano: fulani ametaka kutengenezewa mlango: maana yake ni pale mtu anapotaka kutengenezewa huo mlango. [Kitabu cha Taj Al-Arus, 21/375, chapa ya Dar Al-Hidaya].
Na katika istalahi - sawa na maelezo ya baadhi ya wafuasi wa Imamu Abu Hanifa na kusahihishwa na Al-Kasaniy - ni kuwa: makubaliano ya mauzo kwa sharti la kufanya kazi. [Kitabu cha Al-Badaii' 5/2]. Ikiwa mtu atasema kumwambia mwenzake katika watu wa utengenezaji: nitengenezee kitu fulani cha dirhamu fulani, mtengenezaji akakubali kutengeneza, kwa upande wa watu wa Imamu Abu Hanifa, hapo makubaliano ya kutengenezwa hicho kitu yameshafanyika. Watu wengi wafuasi wa Imamu Abu Hanifa wanasema: Al-Istisnaa ni uuzaji wa kitu kwa sharti la kufanya kazi, au ni uuzaji wa kitu lakini mnunuzi anakuwa na hiyari ya kukiangalia, ni uuzaji lakini siyo kama inavyofahamika, imekwenda kinyume moja kwa moja na uuzaji kwa kuwepo sharti la kazi katika Al-Istisnaa, kinachofahamika ni kuwa uuzaji wa kitu hauna sharti la kazi. Na wamesema pia baadhi ya watu wa Imamu Abu Hanifa: Hakika Al-Istisnaa ni uajiri moja kwa moja, na ikasemwa: yenyewe ni ajira kwa hatua ya kwanza, uuzaji kwa hatua ya mwisho. Na wakasema baadhi ya watu wa Abu Hanifa kuwa, lau utatolewa muda kwa mtengenezaji basi hiyo inakuwa ni As-Salam. (Kitabu cha Fath Al-Qadir, 7/115 – 116, chapa ya Dar Al-Fikr, Na Kitabu cha Ibn Abideen, 5/223 – 225, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya)
Ama kwa upande wa wafuasi wa Imamu Malik na Shafii wameikutanisha na kazi za As-Salam. [Kitabu Hashiyat As-Sawiy cha Ash-Sharh As-Saghir, 3/287, chapa ya Dar Al-Maarif, Na kitabu Al-Muhaddhab cha Shiraziy, 1/297 – 298 chapa cha Isa Al-Hanbali]
Ama kwa upande wa wafuasi wa Imamu Hanbal, wametofautiana katika Al-Istisnaa, wakasema: Haisihi kwa sababu ni uuzaji wa kitu ambacho hakipo tofauti na sura ya As-Salam. Na ikasemwa: Inafaa ikiwa itakusanywa kati ya uuzaji na kufanyiwa kazi kwa mkataba mmoja, kwa sababu ni kuuza na kukabidhi, au kuwa na sharti ndani yake lenye manufaa kwa muuzaji. [Kitabu cha Al-Insaf cha Mardawiy, 4/300, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy].
Na anasema Imamu As-Sarkhasiy katika kitabu cha Bayan kuwa: Al-Istisnaa ni halali pamoja na tofauti na kipimo cha Sharia. [Kitabu cha Al-mabsut, 12/138, chapa ya Dar Al-Maarifa]: “Kipimo cha Sharia ni kuwa haifai kufanya hivyo, kwa sababu kinachotengenezwa ni chenye kuuzwa ambacho hakipo, na kuuza kitu kisichokuwepo haifai, kwa katazo lake Mtume S.A.W., kuuza kitu asichokuwa nacho mtu, kisha hukumu hii ni pamoja na kuuza kitu hata kama kitakuwepo lakini hakimilikiwi na mwenye kuuza haifai kukiuza, ni sawa na kinapokuwa hakipo, bali kisichomilikiwa ni bora zaidi kisiuzwe na muuzaji, lakini tunasema: Sisi tumeacha kipimo cha Sharia kwa ajili ya kuchunga miamala ya watu katika kazi hiyo ya Al-Istisnaa, kwa sababu miamala hiyo ilifanyika tokea enzi za Mtume S.A.W. mpaka leo hii pasi na kupingwa na mpingaji, na miamala ya watu pasi na kupingwa inakuwa ni msingi katika misingi mikubwa ya kukubalika”.
Kutokana na maelezo yaliyotangulia: tunaweza kusema kuwa biashara kwa njia ya As-Salam pamoja na Al-Istisnaa ni halali na inaruhusiwa ili kukidhi mahitaji pamoja na kuwa zinaingia katika jumla ya katazo la uuzaji wa kitu asichokuwa nacho mtu, isipokuwa makusudio ya katazo hili ni kuondoa yale yanayopelekea mivutano na uharibifu, lakini imekuwa ni kawaida watu kufanya miamala ya As-Salam na Al-Istisnaa pasi na kupelekea au kutokea hiyo mivutano wala uharibifu, na kubakia miamala mingine isiyokuwa aina hizo mbili ni katika inayoingia kwenye uuzaji wa kile kisichokuwepo mikononi mwa mtu ambapo asili yake ni kutofaa.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi


Share this:

Related Fatwas