Matumizi ya Njia za Kisasa za Kufic...

Egypt's Dar Al-Ifta

Matumizi ya Njia za Kisasa za Kufichua Kasoro za Mtoto Tumboni na Kuzitibu.

Question

Tumelisoma ombi lililotolewa na muulizaji na ambalo lina maswali yafuatayo:
1- Ni ipi hukumu ya kutumia njia za kisasa za kugundulia kasoro za Mtoto tumboni? Kwa kujua kwamba zinaweza kuwa na athari mbaya kwa mtoto na kwa mama.
2- Ni ipi hukumu ya kutumia njia mbalimbali za kuzitibu kasoro za Mimba kama vile upasuaji wa mtoto ndani ya tumbo?
3- Ni ipi hukumu ya Kisheria ya kuharibu mimba yenye kasoro ya kimaumbile, kasoro ambayo inazuia kukamilika kwa maisha ya mtoto baada ya kuzaliwa, kama vile kukosekana kwa ubongo au figo zote mbili? Na ni ipi hukumu kama uharibifu huo wa mimba utafanyika baada ya kupita siku mia moja na ishirini za ujauzito huo?
 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Baadhi ya watoto huzaliwa wakiwa na baadhi ya magonjwa au kasoro za kimaumbile au kasoro ambazo zinaweza kutokea katika kiungo miongoni mwa viungo vya mwili wa Mtoto, na katika mazingira ya maarifa, elimu na vumbuzi mbalimbali za kisasa katika nyanja za tiba, na matibabu, pamekuwapo uwezekano wa kugundua magonjwa na kasoro hizo na kuzishughulikia wakati mtoto akiwa tumboni kwa mama yake ndani ya miezi ya mimba kwa kutumia njia za vyombo mbalimbali na chunguzi za kimaabara na ambazo zinasaidia kujua ukubwa wa tatizo.
Na ugunduzi huu wa mapema husaidia kuyawahi baadhi ya magonjwa kwa matibabu, na hasa ukiwa ugonjwa huo ulitokana na viambata vya ugonjwa vinavyoweza kutibika kwa viasilia au kwa teknolojia ya chembe hai na mfanowe, au kutokana na kasoro mbalimbali za kimaumbile ambazo zinatibika na kurekebishika, ima kwa njia ya upasuaji wa mimba au wa kawaida baada ya kuzaliwa kama upasuaji wa Mimba utashindikana.
Na njia hizi za kuchunguzia magonjwa ni za aina mbili: Njia zisizo za kupenyeza vifaa mwilini, na njia za kupenyeza vifaa mwilini; Kwa upande wa njia zisizo za kupenyeza vifaa mwilini ni zile zisizohitaji kuingiza kitu chochote mimbani kama vile kupima kwa mawimbi ya sauti ya mfumo wenye upeo wa pande mbili, au pande tatu, au hata pande nne, na kama mionzi ya tv na ya sumaku. Ama kwa upande wa njia za kupenya mwilini, hizo ni zile zinazokuwa kwa kuingiza chombo kidogo kama vile sindano kinapenya ndani ya mwili. Na njia hii hutumika katika hali maalumu; kama vile wanapohitaji kuchukua sehemu ndogo ya majimaji ya ujauzito au kutoka katika kondo au kutoka katika Damu ya mrija wa kitovu au kutoka katika chembe hai za mwili wa mtoto kutoka katika Damu ya mama au kuchukua chembe chembe kutoka katika Mimba yenyewe.
Na kutumia njia za matibabu na kupeana dawa au kujitibu ni jambo lililotakiwa na Sheria na kufanywa likawa ni Sunna na Mtume S.A.W amelisisitizia. Na Abu Dawud na At Tirmidhiy wamesimulia kutoka kwa Usama Bin Shuriak R.A., anasema: "Nilienda kwa Mtume S.A.W, na maswahaba wake kama walikuwa kama vile vichwani mwao kuna ndege, nikasalimia kisha nikaketi, wakaja mabedui kutoka hapa na pale na wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu: Je sisi tunaweza kupeana dawa? Akasema: Peaneni dawa; kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuweka ugonjwa isipokuwa aliuwekea dawa yake isipokuwa ugonjwa mmoja tu, nao ni uzee. Na uzee unaokusudiwa hapa ni utu uzima kiumri. Na katika Hadithi hii, limekuja sisitizo la kutibiana au kupeana dawa, kwa aina yoyote iwayo, hakuna kikomo kilichowekwa kwa kitu chochote, na Msingi uliopo hapa, ni kuendelea kuwa bila kikomo cha tiba mpaka ije dalili ya kuweka kikomo hicho".
Imamu Al Khatwabiy akasema katika kitabu cha: [Maalem As Sunan 217/4, Ch. Al Matwba'ah Al Elmiyah, Halab] "Katika Hadithi hii kuna uthibitisho wa tiba na matibabu, na kwamba kutibiana au kupeana dawa ni halali na hakuchukizi".
Na Imamu Ez Edeen Bin Abdulsalaam anasema katika kitabu cha: [Kawaeid Al Ahkaam 6/1, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]: " Hakika ya tiba ni kama sheria, imewekwa kwa ajili ya kuleta masilahi ya usalama na afya njema, na ni kwa ajili ya kuondosha mabaya ya maangamizi na magonjwa, na kuzuia kinachowezekana kuzuilika kwa njia hiyo, na kwa ajili ya kuleta kinachowezekana kuletwa kwa njia hiyo".
Na matumizi ya njia hizo za kugundulia magonjwa ni zile ambazo tiba haiwezi kufanyika isipokuwa kwa njia hizo, na ikiwa tiba yake imeidhinishwa basi njia zake na kila kinachoambatana nazo pia vimeidhinishwa; kwa kuwa Msingi wake ni kwamba kukiidhinisha kitu ni idhini katika vikamilishaji vinavyokusudiwa. [Tazama: Ihkaam Al Ahkaam kwa Ibn Daqiq Al Eid 288/2, Ch. Matwba'at As Sunna Al Mahamadiyah]
Kwa hiyo, asili ya kutumika moja kati ya njia hizi zilizotajwa ni kwamba zimeidhinishwa kama wanaofanya hivyo ni madaktari bobezi wenye uwezo wa kitaaluma, isipokuwa zikihusishwa na madhara ya kweli au dhana ya kutokea kwake ikawa kubwa zaidi kwa mama mjamzito au kwa mimba, basi kwa wakati huo zitazuiliwa, kwani kanuni ya kisheria ni kwamba madhara huondoshwa. Na asili yake ni kama ilivyopokelewa na Ibn Majah kutoka kwa Ibn Abbas R.A, kwamba Mtume S.A.W, anasema: "Hakuna kujidhuru wala kumdhuru mtu mwingine".
Na Imamu Al Baghawiy amesema katika kitabu cha: [Sharhu As Sunnah 147/12, Ch. Al Maktab Al Islamiy]: "Na kama tiba itakuwa na hatari kubwa ndani yake basi itakuwa Haramu na haitatumika".
Ama kwa upande wa njia za tiba zinazotumika kwa ajili ya tiba ya kasoro za mimba kama vile tiba kwa njia ya dawa au kwa uingiliaji kwa upasuaji zote zinaingia katika asili ya kutakiwa kwa tiba kulikokwisha amuliwa kisheria, na wala haikatazwi njia yoyote isipokuwa kukiwapo madhara ya Uhakika; kwa namna ambayo na madhara ya kuitumia yatakuwa makubwa kuliko madhara ya kuiacha kwa Uhakika au kwa dhana iliyo kubwa zaidi. Na katika misingi ya kisheria iliyopitishwa kisheria ni kwamba, yanapokutana madhara mawili, basi yataangaliwa zaidi yale yenye kuleta madhara makubwa zaidi kwa kuyafanya yaliyo chini yake, na kwamba Madhara hayaondoki kwa madhara yanayolingana nayo au kwa yaliyo makubwa zaidi yake. [Tazama: Al Ashbaah na An Nadhair kwa Asiyuti Uk. 86, 87, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]
Na ama kwa upande wa kuiharibu mimba yenye kasoro za kimaumbile zinazouzuia ukuaji kamili wa mtoto huyo baada ya kuzaliwa, kama vile kukosekana kwa ubongo au figo zote mbili, Al Bukhariy na Muslim walipokea kutoka kwa Ibn Masoud R.A, kwamba Mtume S.A.W, anasema: "Hakika mmoja wenu hukusanywa mwili wake tumboni mwa mama yake siku arubaini, kisha anakuwa pande la damu linaloning'inia, mfano wa hivyo, kisha likawa pande la nyama mfano wa lililotafunwa, kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu humtuma Malaika na kuamrishwa maneno manne, na akaambiwa amwandikie; Amwandikie kazi yake, na riziki yake, na muda wake wa kuishi, na ikiwa ni mwema au mwovu, kisha anapuliziwa roho". Kwa hiyo hii ni Hadithi tukufu ya Mtume S.A.W inayomaanisha kupuliziwa roho kiumbe tumboni kunakuwa baada ya siku mia moja na ishirini za Mimba.
Na kwa hivyo, hakika kiumbe kilicho tumboni ambacho uhakika wa kupatwa kwake na kasoro za kimaumbile unapatikana, kasoro ambazo zitazuia kukua kwake atakapozaliwa kwa kawaida baada ya kupita ujauzito huo siku mia moja na ishirini, hakika misingi ya Sheria ya Uislamu haimzuii mama kuchukua hatua ya kuiharibu mimba hiyo na katika hali kama hiyo, kwa kuwa hakuna madhara yoyote ya Uhakika kwa mama au yenye kutegemewa kutokea kutokana na kuiharibu mimba hiyo. Na hiyo ni kwa ajili ya kuondosha tabu ya mimba na ugumu wa kujifungua na hatari zake kutokana nayo au kwa kumuepushia matatizo hayo yanayosababishwa na maumivu ya kupoteza baada ya kuwa na matumaini na mwambatano wake pamoja na gharama zinazoambatana na jambo hilo ukiachana na ufuatiliaji wa ujauzito kimatibabu na uzalishaji wake kwa njia ya upasuaji. Na hii inakuwa ni kwa lengo la kuondosha madhara.
Na Jamhuri ya Wanachuoni wa Fiqhi inaona kuwa inajuzu kuiharibu mimba kabla ya kupuliziwa roho kama kuna madhara yanayozingatiwa, kama vile kukatika kwa maziwa yake baada ya kudhihiri ujauzito na baba akawa hana uwezo wa kumuajiri mnyonyeshaji, na akawa anachelea kuangamia kwa mkewe, kama alivyonukulu Ibn Aabidiin katika Hashia yake kutoka kwa Ibn Wahbaani ambaye ni miongoni mwa wanachuoni wa Fiqhi ya Madhehebu ya Imamu Hanafi. [Tazama: Radu Al Mehtaar 176/3, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]
Na yamekuja maelezo mengine ya kifiqhi yanayomaanisha kuwa inajuzu kwa hali yoyote iwayo hata kama haikuwa udhuru wowote. Basi Sheikh wa Uislamu Zakariyah Al Answariy wa Madhehebu ya Shafi anasema katika kitabu cha: [Sharhu Al Bahjat Al Wardiyah 331/3, Ch. Al Maimaniyah]: "Kutoa mimba huko kukiwa kabla ya kupuliziwa roho kutajuzu, au baada ya kutiwa roho kutakuwa Haramu".
Na imekuja katika matini ya kitabu cha: [Al Eqnaa] kwa Al Hijaawiy, miongoni mwa vitabu vya wanazuoni wa kihanbaliy, (pamoja na Sharhu ya kitabu cha: Kashfu Al Qinaa' 220/1. Ch. Dar Al Kutub Al Elimiyah]: "Na inajuzu kunywa dawa kwa ajili ya kutoa maji ya uzazi".
Na katika kitabu cha: [Al Furuugh' kwa Ibn Muflih 282/1, Ch. Alam Al Kutub] kwamba inachukuliwa kutoka katika tamko la Abu Al Wafaa' Ibn Aqiil katika kitabu cha: [Al Funun]: anasema: "Kwamba inajuzu kuharibu Mimba kabla ya kupuliziwa roho. Amesema Ibn Muflih. Na ana maoni yake".
Na ikiwa Mimba itapitisha siku mia moja na ishirini ikiwa tumboni kwa mama, basi haijuzu kwa hali yoyote ile kuitoa, kwani Wakati huo itakuwa imeshapuliziwa roho, na kuifanyia uadui wowote hakujuzu, na kuitoa Mimba wakati huo kunakuwa ni kuua alikokuharamisha Mwenyezi Mungu Mtukufu isipokuwa kwa haki. Isipokuwa pakiwapo hatari ya kuendelea kuwapo kwa Mimba hiyo dhidi ya maisha ya mama mzazi na jambo hili linaamuliwa na madaktari waliobobea. Basi hakuna kizuizi chochote kwa wakati huo kuiharibu mimba kwani Maisha yaliyopo yanatangulizwa mbele ya Maisha yanayodhaniwa kuwapo, lakini ruhusa ya kuharibu mimba hapa ilitokana na maana hii na wala sio kwa sababu ya sifa maalumu ya kuharibika kwa kiumbe tumboni. Na kwa ajili hiyo, Baraza la Taifa la Fiqhi ya Kiislamu, Katika Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu, katika kikao chake, liliupitisha uamuzi huu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas