Maswali ya Kiafya.

Egypt's Dar Al-Ifta

Maswali ya Kiafya.

Question

1- Ni ipi hukumu ya kisheria katika Kutenganisha chombo cha kupumulia kwa mgonjwa ambaye hali yake ya kiafya inakatisha tamaa )Terminally ill patient clinical death) pamoja na kuchunga kwamba hatua hiyo italeta manufaa kwa mgonjwa mwingine anayehitaji chombo hicho na kulinda mali?
- Na ni ipi hukumu ya Kusitisha matumizi ya madawa mengine yanayosaidia kuuamsha moyo na kulinda shinikizo lake (vaso pressol)?
- Na je, Daktari ambaye aliichukua hiyo hatua anazingatiwa amesaidia katika kifo cha mgonjwa (physician–assisted death)?
- Na daktari huyo anahitaji mwafaka kutoka kwa mgonjwa au mwenye wasia au ndugu wa karibu wa mgonjwa?
- Na je, inajuzu kwa mgonjwa kuwa na wasia kwa ajili ya jambo hilo?

2- Ni ipi Hukumu ya Kutumia madawa ya kuleta Utulivu na matumizi ya madawa ya kupunguza maumivu kwa Mgonjwa ambaye hali yake inakatisha tamaa?

3- Ni ipi Hukumu ya Kutumia vifaa vya kupumzisha viungo ambavyo husitisha pumzi wakati wa kumtenganisha mgonjwa na chombo cha kupumulia, na je ni wajibu kukisitisha na kufanya kinyume na kazi yake kwa kuzingatia kwamba mgonjwa huyo yuko katika hali ya kukatisha tamaa na kwa ajili ya kurahisisha kifo chake? Na ni ipi hukumu yake ikiwa haiwezekani kugeuza kazi yake?

4- Ni ipi Hukumu ya mgonjwa ambaye hali yake ya kiafya inakatisha tama kama atakataa kula na kunywa kwa hiyari yake?


5- Na ni ipi hukumu ya kuondosha viungu mwilini? Na nini hukumu yake ikiwa mgonjwa ambaye hali yake ya kiafya inakatisha tamaa? Na je, panahitajika mwafaka wa mgonjwa au jamaa yake?

6- Ikiwa Hali ya mgonjwa ni ya kukatisha tamaa kiukamilifu, Je inajuzu kutojaribu kuuamsha moyo wa mgonjwa wakati anapofariki na kumuacha mgonjwa afe bila ya kuuamsha moyo wake?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Kwa kurejea kwa wabobezi tumejua kwamba mfumo wa kupumua wa bandia mpaka ufungwe na kuanza kutumiwa na mgonjwa, mgonjwa huwa lazima apewe kile kinachojulikana kama dawa za kutuliza misuli. Na kazi ya madawa hayo ya kutuliza misuli ya mwili ni ya kuifanya misuli ya mfumo wa kupumulia iache kufanya kazi yake ili mfumo wa bandia uweze kufanya kazi yake na iwapo daktari atataka kuutenganisha mfumo huo wa kupumulia na mgonjwa pale mgonjwa anapokuwa hahitaji tena chombo cha kupumulia basi daktari atalazimika kumdunga sindano mgonjwa itakayomaliza kazi ya madawa ya kupumzisha misuli ya mfumo wa kupumulia na kubadilisha kazi yake ili iwezekane Kuondosha chombo cha kupumulia na kurejea kama kawaida kazi ya misuli ya mfumo wa kupumulia, upya.
Kutokana na hayo; ni kwamba inajuzu kumtenganisha mgonjwa na chombo cha kupumulia kwa sharti kuwa daktari ampe mgonjwa dawa inayogeuza kufanya kazi ya kutulizi misuli ili misuli ya kupumulia irude katika kazi yake ya kawaida.
Na pia inajuzu kusitisha madawa mengine yanayosaidia kuuamsha moyo na kutunza shinikizo; na tulichokiamua katika kujuzu kwa yote yaliyotangulia lengo lake ni kuwa matumizi ya njia zote hizi ni katika mlango wa kutibiana na kuponyana. Na kinachokubalika kisheria na ambacho Jamhuri ya Wanachuoni wa Fiqhi wanakifuata ni kwamba kutibiana sio wajibu, kwa maana kwamba atakayeamua kuacha dawa hatapata dhambi au hatakuwa amefanya kitendo cha Haramu. Kwa hivyo imepokelewa na Al Bukhariy na Muslim katika vitabu vyao viwili Sahihi, kwamba mwanamke mmoja alikuja kwa Mtume S.A.W., na akasema: "Mimi ninaugulia kifafa na mimi huwa ninajifichua uchi ninapojiwa na kifafa, niombee kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Akasema Mtume S.A.W: ukitaka vumilia na utalipwa pepo, na ukitaka nitamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akuponye. Akasema yule Mwanamke: mimi ninavumilia. Na akasema: hakika mimi ninajifichua mwili wangu ninapojiwa na kifafa. Niombee kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu nisijifichue mwili wangu, akamwombea".
Na Hadithi hii ina dalili ya kuwa inajuzu kuacha matibabu. Kwani Mtume S.A.W., amemhiyarisha mwanamke huyu baina ya kuvumilia balaa na kuingia peponi, na kuomba dua kwa ajili ya kuponywa, na mwanamke huyo alihiari kusubiri na kuingia Peponi.
Kwamba daktari halazimiki kuchukua maamuzi ya kusitisha chombo hicho kwa mgonjwa kwa kujiamulia yeye mwenyewe, bali anayeweza kutoa maamuzi hayo ni mgonjwa mwenyewe, kama kwa mfano anapousia hivyo, au wasimamizi wake, na hakuna jukumu lolote la kisheria wakati huo linalomuelemea daktari.
Na hiyo inatofautiana na kile kinachoitwa "Mauaji ya huruma", na ndani yake mgonjwa au msimamizi atamtaka daktari kusitisha uhai wa mgonjwa huyo au daktari ataamua au mtu mwingine yeye mwenyewe kwa sababu ya ulemavu wa mgonjwa au ukali wa maumivu yake, na jambo hilo ni Haramu moja kwa moja. Kwani hapa, maisha ya mgonjwa yanaendelea na hayategemei vifaa vya kupumulia isipokuwa mgonjwa au daktari anataka kuyamaliza kutokana na maumivu makali mno kwake, kwani kuyasitisha Maisha katika hali kama hiyo kunahesabika kuwa ni mauaji yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu isipokuwa yale aliyoyahalalisha.
Na tofauti kati ya hali hii na hali ile ni kwamba kutibiana hakumaanishia kuwa njia ya kupona, bali mtu anaweza kupona bila ya dawa yoyote, na mfano wake miongoni mwa njia mbalimbali za kujichagulia, bali kwa nguvu anazozijaalia Mwenyezi Mungu Mtukufu mwilini mwake na mfano wa hayo, basi kuyaacha matibabu ni kuacha jambo halali, ama mauaji yanayojulikana kama "Mauaji ya huruma", ni kwamba matokeo yake ni hayo na mauti ya mgonjwa yana hukumu inayojulikana.
Ama kwa upande wa matumizi ya dawa za kutuliza mwili na kuelewesha mwili kwa ajili ya kumpunguzia mgonjwa maumivu makali, mgonjwa ambaye hali yake inakatisha tama, asili yake ni uharamu wa matumizi ya kila kinachopelekea upotezaji wa akili au kuzorotesha viungo vya mwili, kwa sababu ya Hadithi ilipokelewa na Abu Dawud na Ahmad kutoka kwa Um Salamah R.A., kwamba alisema: "Mtume S.A.W amekataza kila kilevi na kila kinachoivuruga akili".
Lakini zuio hili linaepukwa katika baadhi ya hali za dharura na haja yoyote ambayo inafikia hali hiyo, kwani dharura huwa zinahalalisha yaliyokatazwa, na haja huwa inaenda kuwa katika nafasi ya dharura kwa ujumla au kwa sifa maalumu, na kumpunguzia mgonjwa maumivu kama hakufikii kiwango cha dharura basi hakutakuwa miongoni mwa haja. Kwa hiyo matumizi ya dawa za kutuliza maumivu na za kulewesha mwili kwa ajili ya kupunguza maumivu zinaruhusiwa kisheria, lakini kuruhusiwa huko kunaendelea kuwa na mfungamano na kiwango cha haja inayotakiwa, na kinachozidi kinabakia katika kiwango cha kinachohitajika katika asili ya uharamu wa kutumia kwake; kwa msingi wa kisheria: kile kilichohalalishwa kwa sababu ya dharura hukadiriwa kwa kiasi chake, Na huendelea kuwa na mfungamano pia na upeo wa madhara ambayo yanaweza kumpata mgonjwa kutokana na kula dawa hizi za kupunguza maumivu au kutokana na kuongeza ulaji wake, kwa hiyo daktari analazimika kuainisha kiwango kinachotakiwa kwa ajili ya kulewesha kwa mujibu wa haja iliyopo kwa namna ambayo mgonjwa hawezi kudhurika kwa madawa hayo, na wala asizidishe.
Na wanachuoni wametoa maelezo ya kujuzu matumizi ya bangi kwa kiasi kitakacholewesha akili na kuitoa ikiwa kufanya hivyo ni kwa ajili ya kujitibu. Na Raafiiyu ametoa maelezo kinyume na hivyo katika kujuzu kujitibu kwa mvinyo, na Nawawiy amesahihisha kujuzu huko.
Ama kuhusu mgonjwa mwenye ugonjwa unaokatisha tamaa atakaposita kula na kunywa, kama kusita huko kunakusudiwa kujiletea madhara yeye mwenyewe na kumfanya aharakishe umauti wake, basi hapana shaka kuwa kufanya hivyo ni haramu kisheria, na hii ni aina ya kujiua. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anakataza mambo kama hayo, na anasema:{Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, walamsijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeniwema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema}[AL BAQARAH 195]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: {Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipo kuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe. Walamsijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenyekuwarehemuni.} [AN NISAA 29]
Na katika vitabu viwili vya Sahihi kutoka katika Hadithi ya Jundub Bin Abdulahai R.A, kwamba Mtume S.A.W. alisema: "Alikuwa katika wale waliokuwa kabla yenu mtu mmoja mwenye jeraha akashindwa kuvumilia na akachukua kisu na kuukata mkono wake na akashindwa kusitisha damu mpaka akafariki Dunia. Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Mja wangu amejiua mwenyewe, nimemuharamishia Pepo yangu".
Imamu Aj Jaswasw anasema katika Tafsiri yake: "Mtu aliyeacha kula na kunywa hali ya uwepo wa chakula na vya kunywa, mpaka akafa basi hufa katika maasi kwa Mwenyezi Mungu kwa kuacha kwake kwa kula".
Ama kuhusu kuondosha viungo vya binadamu, hapo kuna sura mbili:
Sura ya Kwanza: Anayechukuliwa viungo anatakiwa awe binadamu aliye hai na anayehamishiwa pia awe hai, kwani kiungo kinachohamishwa kinatakiwa kiwe kiungo mbadala kinachofanya kazi zake na kuhamishwa kwake kunapelekea kifo kwa mwenyewe, kama vile moyo, au maini kwa mfano, au iwe kinyume na hivyo kwamba pawepo kiungo mbadala kinachofanya kazi yake na mara nyingi hakipelekei kifo kwa kuhamishwa kwake, na hili linapatikana katika viungo vya kutibu, kama vile figo au vyenye kujengeka upya kama vile ngozi na damu. Kama kiungo kilichohamishwa kina sifa ya umoja basi ni haramu kwa mwanadamu kukitoa kwa mwingine au kukichukua kutoka kwa mtu mwingine katika watu walio hai, na vile vile inakuwa haramu kwa daktari kusaidia uhamishaji wake na upandikizaji wake; na hukumu hiyo ni kutokana na yale yanatojitokeza kutokana na hali hiyo kama vile mauti ya mtu aliyetolea kiungo hicho. Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, walamsijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeniwema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema} [AL BAQARAH 195]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: {Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma,isipo kuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe. Walamsijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenyekuwarehemuni.} [AN NISAA 29]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: {Na saidianeni katikawema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi nauadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Munguni Mkali wa kuadhibu} [AL MAIDAH 2].
Na msingi wa kisheria ni kwamba madhara bado yanaendelea kuwapo, basi haijuzu tukaondosha madhara kwa mtu mwenye kiungo kilichoharibika kwa kumharibia mtu mwingine kiungo chake na kumpotezea bure kiungo hicho, moyo wa mtu wa kwanza hauna haki zaidi ya kukihifadhi kiungo hicho kuliko moyo wa mtu wa pili na maisha yake.
Kama kiungo husika kinachohamishwa kitakuwa sio katika vile vimoja vimoja basi inajuzu kuhamisha na kukitumia kwa mtu mwingine pamoja na kuchunga masharti yake yafuatayo:
1- Kuwepo kwa hali ya dharura au hitajio la kisheria kwa yule anayehamishiwa kiungo ambayo hali hiyo upandikizaji wa kiungo hicho unakuwa ndio njia pekee iliyopo ya kumtibu, na kukadiria uainishaji kunarejeshwa kwa madaktari wabobezi.
2- Mwafaka wa mtu anayetoa kiungo pamoja na kuwa kwake na akili na awe amebaleghe.
3- Uhamishaji huu unatakiwa uwe wa kuleta manufaa yaliyothibishwa na daktari kwa anayehamishiwa kiungo hicho.
4- Uhamishaji wa kiungo usisababishe madhara yanayoweza kutokea kutokana na kiungo hicho kuhamishwa, ambayo yatamdhuru kwa ujumla au kwa kiasi Fulani, na kumuathiri vibaya hapo hapo au baadae kwa njia iliyothibitika kimatibabu; kwani masilahi ya anayehamishiwa kiungo husika sio bora zaidi kisheria kuliko masilahi ya anayetoa kiungo. Na madhara hayaondoshwi isipokuwa kwa madhara, na hakuna kudhuru wala kujidhuru katika uislamu, na inatosha katika hili masilahi mapana yenye nguvu zaidi. Na madhara machache yanayotegemewa kutokea kwa kawaida au kwa kujulikana kisheria pia hayazuii kujuzu huku katika kuruhusu iwapo itajulikana kikamilifu hapo mapema na kuwezekana kuvumilika au kukinga kifedha au kwa njia nyingie kwa upande wa mtu anayetolewa kiungo, na ambaye anaainisha hivyo ni katika wataalamu bobezi na wenye uzoefu wa kitabibu na waadilifu pia.
5- Uondoshaji huo wa kiungo lazima uwe mbali na kununua na kuuza.
6- Kutolewa kwa maamuzi yaliyoandikwa kutoka katika kamati ya kimatibabu kabla ya kuhamisha kiungo kwa kuyajua masharti haya yote na kumpa anayetakiwa kupewa kutoka katika pande mbili – anayetolewa kiungo na anayesaidiwa kiungo – kabla ya kufanyika upasuaji wa kimatibabu, ni kwamba kamati hiyo iwe ni bobezi na isiyopungua madaktari watatu waadilifu na hakuna yoyote miongoni mwao mwenye maslahi yoyote katika zoezi hilo la upasuaji wa kuhamisha kiungo na kupandikiza.
7- Inashurutishwa kwamba kiungo kinachohamishwa kisiwe ni chenye kupelekea mchanganyiko wa nasaba – kwa kuwa kwake ni katika viungo vya uzazi – kwa hali yoyote iwayo.
8- Uhamishaji huo wa kiungo ufanyike katika kituo bobezi cha afya kilichopitishwa na nchi na kina kibali cha kufanya hivyo moja kwa moja bila ya gharama zozote za kifedha baina ya pande zinazotoa viungo, na katika jambo hili, wanalingana watu wote, masikini na tajiri, kwa namna ambayo panawekwa masharti ambayo yanawalinganisha watu wote katika utoaji wa huduma za kimatibabu na hakuna yoyote kati yao anayetangulizwa dhidi ya mwingine isipokuwa kwa mujibu wa hali ya dharura ya kimatibabu tu ambayo ipo katika kuokoa maisha ya mtu kutokana na madhara halisi au kutokana na kifo au maangamizi.
Na dalili ya kujuzu ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewau wawatu wote.} [AL MAIDAH 32]. Basi aya hiyo inaingizwa ndani yake mchango wa binadamu kwa kaka yake kwa kutoa kiungo miongoni mwa viungo vyake ili ayaokoe maisha yake, kwani katika hali hiyo inamthitikia kwamba anatoa maisha kwa ajili ya roho ya kaka yake.
Na pia Mwenyezi Mungu Mtukufu amemsifu huyo ambaye aliyempenda ndugu yake kuliko nafsi yake kwa chakula au kinywaji au mali, na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: {Bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji} [AL HASHR 9].
Kama hiyo itakuwa katika mambo haya mepesi, yule atakayempendelea ndugu yake kwa kumpa kiungo chake au akachukua hatua ya kumuhifadhia ili amuepushe na maangamizi yanayoweza kutokea basi hapana shaka kuwa huyu ni mbora zaidi na ni wa kusifiwa na kupewa maneno mazuri, na kwa hivyo kitendo chake hicho kinazingatiwa kisheria kuwa ni kizuri mno.
Na Misingi Mikuu ya sheria haikubali hivyo; kwani kauli ya kujuzu inaafikiana na Msingi wa "madhara huondoshwa", na Msingi wa "dharura huhalalisha viliyoharamishwa", na Msingi wa "Jambo linapokuwa finyu basi hutanuka". Na jambo hili ndilo linalohukumia uwepo wa mizani ya kulinganisha baina ya madhara; kwa nmna ambayo madhara makubwa zaidi yanaondoshwa kwa madhara madogo, na panachaguliwa shari iliyo hafifu baina ya mbili kwa kuitumia iliyo hafifu.
Na katika suala letu hili kumetokea ukinzani baina ya uharibifu wa kuhamisha kiungo cha mtu aliye hai na kumsababishia baadhi ya machungu mtu huyo, na baina ya ubaya wa kuangamia mtu aliye hai anayesaidiwa kiungo. Na hapana shaka kwamba madhara ya kuangamia aliye hai anaesaidiwa kiungo ni makubwa kuliko madhara yanayotuka kwa mtoaji wa kiungo aliye hai, na kwa hivyo anatangulizwa huyo aliye mgonjwa; kwa sababu ndiye mwenye madhara makubwa zaidi na aliye hatarini zaidi.
Sura ya Pili: Anayetolewa kiungo anatakiwa awe mwanadamu aliayefariki, na anayepewa kiungo hicho ni hai, na sura hiyo ni halali pia lakini kwa masharti yafuatayo:
1- Anayehamishwa kiungo anatakiwa awe amethibitika kisheria kuwa amefariki dunia; na hali hiyo ni kwa kufa kikamilifu, ni kwamba viungo vyote vya mwili wake viwe vimesita kufanya kazi kikamilifu na haiwezekani kurejea tena katika uhai na utendaji wake kwa mara nyingine kwa ushahidi wa wataalamu bobezi walio waadilifu ambao wanategemewa kutoa taaarifa za kifo kinapotokea, kwa namna ambayo mtu huruhusiwa kuzikwa, na ushahidi huo uandikwe na kusainiwa na wataalamu hao.
2- Kuwepo hali ya dharura au hitajio ambavyo viwili hivi vinatambulika kisheria kwa nmna ambayo hali ya mgonjwa anayehamishiwa kiungo inaendelea kuzorota na hakuna kinachoweza kumwokoa kwa mtazamo wa daktari, na kulifikia lengo muhimu la kupona kwa kutokuwa na njia mbadala isipokuwa kumhamishia kiungo hicho kutoka kwa mtu mwingine.
3- Maiti inayochukuliwa viungo iwe ya mtu aliyeusia kuchukuliwa viungo vyake alipokuwa hai na mwenye nguvu zake kamili za kiakili na bila ya kulazimishwa na mtu mwingine yoyote, kifedha au kimaana, na anajua kwamba yeye anausia kuchukuliwa kiungo maalumu cha mwili wake na kuhamishiwa kwa mtu mwingine baada ya kufa kwake, au aliidhinisha wasimamizi wake kufanya hivyo.
4- Uondoshaji huo lazima uwe mbali na kununua na kuuza.
5- Inashurutishwa kwamba kiungo kinachohamishwa kisipelekee mchanganyiko wa nasaba – kwa kuwa kwake ni katika viungo vya uzazi – kwa hali yoyote iwayo.
6- Uhamishaji huo wa kiungo ufanyike katika kituo bobezi cha afya kilichopitishwa na nchi na kina kibali cha kufanya hivyo moja kwa moja bila ya gharama zozote za kifedha baina ya pande zinazotoa viungo, na katika jambo hili, wanalingana watu wote, masikini na tajiri, kwa nmna ambayo panawekwa vidhibiti ambavyo vinawalinganisha watu wote katika utoaji wa huduma za kimatibabu na hakuna yoyote kati yao anayetangulizwa dhidi ya mwingine isipokuwa kwa mujibu wa hali ya dharura ya kimatibabu tu ambayo ipo katika kuokoa maisha ya mtu kutokana na madhara halisi au kutokana na kifo au maangamizi.
Na dalili tuliyoipata katika jambo hili ni kwamba inajuzu kuhamisha viungo kutoka kwa mtu aliye hai na kuvihamishia kwa mtu aliye hai, na kujuzu huko kunatokana na upatikanaji wa dalili kunakofaa pia katika sehemu hii, na vile vile hakika mambo yalivyo katika matawi ya Fiqhi ya kale ni kile kinachothibitisha kujuzu; kutokana na hayo, ni kile walichokisema wanachuoni wa Fiqhi kuhusu kujuzu upasuaji wa tumbo la mfu kwa lengo la kutoa mali ya mwingine ambayo maiti aliimeza kabla hajafa.
Kwa kuwa inajuzu kuhamisha viungo vya maiti ni bora na ni vizuri zaidi kufanya hivyo; kwa kuwa ni katika nafasi ya kuokoa nafsi inayoheshimika ambayo ina hadhi kuliko mali.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

 

 

Share this:

Related Fatwas