Kusimama kwa Ajili ya Kuomboleza Roho za Mashahidi
Question
Je! Inaruhusiwa kusimama kimya kwa dakika moja, kwa mfano, kwa ajili ya kuomboleza na kuheshimu roho za watu kama vile Wanavyuoni, Wapiganiajia haki, Mashujaa, na viongozi waleta mabadiliko?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wafuasi, na baada ya hayo:
Sheria ya Kiislamu ilikuja waziwazi katika wito wake kwa kumtukuza mwanadamu na kuheshimu ubinadamu wake akiwa hai na akiwa amekufa, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri} [AL ISRAA: 70] Uislamu pia ulizingatia kujumuisha tabia nzuri na maadili mema na kuyaeneza katika jamii na kutia moyo kwa njia zote zinazopatikana kama vile kutoa mawaidha, elimu, utamaduni na sanaa zinazoruhusiwa. Mtume S.A.W. alisema: "Nimetumwa kwa ajili ya kukamilisha maadili mema". [Imepokelewa kutoka kwa Ahmad katika Musnad yake, na Al-Bukhariy kwenye Al-Adab Al-Mufrad, na Al-Hakim katika Al-Mstadrak], kueneza fadhila na kulilinda ni lengo kubwa miongoni mwa malengo ya sheria ya Kiislamu.
Mojawapo ya maadili yaliyotetewa na Uislamu ni kuwashukuru watu kwa matendo yao mema; katika Hadithi Tukufu: "Asiyewashukuru watu hamshukuru Mwenyezi Mungu". Imepokelewa kutoka kwa At-Tirmidhi, na Ahmad. Pamoja na maadili ya Uislamu kuwatukuza watu na kuwatendea kama wanavyostahili, na kuwaheshimu watu wenye fadhila; imepokelewa kutoka kwa Bi Aisha R.A. kwamba Mtu mwenye haja alipita kwa Bi Aisha R.A. akampa kipande cha mkate, na akapita mwingine amevaa nguo nzuri, na ana sura nzuri, akakaribishwa kuketi na akala, Bi Aisha aliulizwa kuhusu hali hiyo, alisema kwamba: Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema: "Wawekeni watu nafasi zao wanazostahiki". Imepokelewa kutoka kwa Abu Dawud, na As-Sakhawiy katika kitabu cha: [Al-Maqasid Al-Hasanah] alisema Hadithi hii ni Hassan. Ibn 'Omar vile vile R.A. alisema: Mtume wa Allah S.A.W. akasema: "Ikiwa mkarimu akija kwenu, basi mkirimu" Imepokelewa kutoka kwa Ibn Majah na Al-Bayhaqiy huko Sunnah Al-Kubra. Na Imepokelewa kutoka kwa Abu Musa Al-Ash'ariy .R.A. amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. alisema: "Hakika katika utukufu wa Allah kumkirimu Muislamu mwenye mvi, aliyehifadhi Qur`ani asiye mbali nayo, na kumkirimu mwenye ufalme ambaye ni mwadilifu" Imepokelewa kutoka kwa Abu Dawud katika kitabu chake cha: [Sunan], na Al-Bukhariy kwenye kitabu cha: [Al-Adab Al-Mufrad].
Na kuelezea kuheshimu na kukirimu kwa kusimama wakati wa ujio wa wenye fadhila miongoni mwa wanavyuoni na masharifu na kadhalika, imetajwa katika sheria dalili ya kuruhusiwa kufanya hivyo, bali baadhi ya wanavyuoni walisema kwamba jambo hilo linapendekeza, na miongoni mwa dalili za wanavyuoni wengi kuhusu jambo hilo ni Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Al-Bukhariy na Imam Muslim katika Sahihi zao kutoka kwa maneno ya Mtume S.A.W. kwa Al-Ansar: "Simameni kwa ajili ya bwana wenu" wakati alipokuja Saad Ibn Muadh R.A. akipanda punda.
Imam Al-Bayhaqiy alisema: “Inaruhusiwa kusimama kwa ajili ya heshima na kukirimu; kama Al-Ansar walivyomsimamia Saad na kama Talha alivyomsimamia Kaab, na haipaswi kwa anayesimamiwa kuamini kuwa kusimamiwa ni haki yake, kwa hivyo hata akiwa hakusimamiwa anakasirika au kulaumu au kulalamika” [Fathul Bari kwa Al-Hafidh Ibn Hajar 11/ 52, Ch. Dar Al Maarifa].
Imam An-Nawawiy anasema katika maelezo yake kuhusu Imam Muslim [12/93, Ch. Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy]: “Kauli ya Mtume S.A.W: "Simameni kwa ajili ya bwana wenu" ni kuwakarimu wenye fadhila na kuwakaribisha kwao kwa kusimama wakati wanapokuja, kwa hivyo wengi wa wanavyuoni walitoa dalili hii kwa ajili ya kubainisha pendekezo la kusimama huko, Al-Qadhi alisema: hali hii ya kusimama siyo katika hali iliyokatazwa, lakini hali iliyokatazwa ni ile ya kusimama watu fulani muda mrefu hali ya kuwa yeye ni mwenye kukaa. Nimesema inapendelewa kusimamia kwa ajili ya wenye fadhila, na kuna Hadithi zaidi ya moja zimetajwa kuhusu suala hili, na hakuna Hadithi sahihi kuhusu kukataza suala hilo, na nilikusanya maoni ya wanavyuoni kuhusu sual hilo vile vile nimejibu kuhusu masuala yanayofikiriwa kuwa yamekatazwa, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi.”
Wanavyuoni wanasema: Inapendekezwa kuwasimamia wazazi, Imamu mwadilifu, na wenye fadhila katika watu. Hali hii ya kusimama ilikuwa kama kauli mbiu kati ya wenye fadhila. Kama mtu hakusimama kwa anayestahiki kusimamiwa, basi hushutumiwa na kutukanwa, na hali hii inapelekea chuki. Hali ya kupenda kwa mwenye kusimama haimzuii yule anayesimamiwa kuichukia hali ile, na kuona kwamba yeye hastahiki kusimamiwa [Mukhtasar Minhaj Al-Qasidiin kwa Ibn Qudaamah Uk. 230, Ch. Dar Al Bayan]. Ukaribishaji (kusimama) wa aina hii umekuwa ni mazoea yanayojulikana katika baadhi ya nyakati, ambapo mwenye kusimama anaonesha ukarimu, na kuiacha hali hii inaonekana ni kupuuzia, na kwa sababu hizo baadhi ya wanavyuoni wametaka kuilazimisha hali hii ili kuepuka chuki, wivu na makutano. Rejea: [Hashiyatul Sheikh Al-Qalioubi juu ya Sharul Mahali 3/213, Ch. Issa Al-Halabiy. Na Al-Fatawa Al-Kubra kwa Ibn Hajar Al-Haitami 4/284, Ch. Al-Maktaba Al-Islamiya].
Iliyotangulia ni kuhusu kuheshimu walio hai kwa kuwasimamia, lakini kufanya hivyo kwa ajili ya wafu - hata kwa ajili ya kuheshimu kifo na hali ya kifo – imepokelewa Hadithi inayoruhusu kusimama wakati Jeneza linapopita, na maburini, hata akiwa marehemu alikuwa ni Myahudi au kafiri. Katika Hadithi hii kwamba: Jeneza lilipita mbele ya Mtume S.A.W naye akasimama, na ikasemwa kwake: Ni mazishi ya Myahudi, akasema: "Je! Sio ni roho?". Hadithi hii imekubaliwa na, Al-Hafidh Ibn Hajar anasema katika [Fathul Bariy 3/181]: maana ya hivyo ni kwamba inapendeza kusimamia kila mazishi.”
Katika [Kashaaf Al-Qinaa, kwa Al-Bahwatiy Al-Hanbaliy 2/150, Ch. Dar Al Kutub Al-Elmiyah]: “(Na inaruhusiwa) kuzuru (kwa kaburi la kafiri) na kulisimamia kaburi lake, kama vile ziara yake Mtume S.A.W. katika kaburi la mama yake lilikuwa baada ya ushindi, ama kuhusu Aya hii: {Wala usisimame kaburini kwake} [AT TAWBAH: 84], Aya hii iliteremshwa kwa sababu ya Abdullah Ibn Ubai kwamba inamaanisha kwa wingi wa wanavyuoni wa tafsiri kuwa: kusimama kwa ajili ya kumwombea dua na kumwombea msamaha.”
Al-Mardawi alisema katika kitabu cha: [Al-Insaf 2/562, Ch. Dar Ihyaa At-Turaath Al-Arabiy]: “Inaruhusiwa kuzuru kaburi la kafiri … na inapaswa kulikaribia kaburi hilo kama vile Mtume S.A.W, alivyomzuru mwenye kaburi hilo katika maisha yake, mtazamo huu umetajwa katika kitabu cha: [Al-Wasilah wal Talkhiis]”.
Tuliyoyataja ni kutoka Maandiko ya Sheria na maneno ya wanavyuoni yanaonesha asili ya ruhusu ya kusimama kwa heshima na kumthamini yule anayestahiki, akiwa hai au amekufa, haswa ikiwa hali hii ni tabia ya watu, na kwamba jambo hili linahusishwa, na kile kinachoendelea katika mila na desturi za kijamii, na kwamba hakuna chochote kinachopingana na Sheria ya Kiislamu, isipokuwa ikiwa hali ya kusimama inaambatana na jambo lililokatazwa, au kuna pingamizi yoyote katika Sheria.
Inawezekana kusemwa: Hakika Hadithi zilizopokelewa zinaonesha kuwa inaruhusiwa kusimama kwa ajili ya kutazama mazishi, lakini katika swali letu hakuna mazishi yaliyopo wakati wa kusimama, lakini hiyo ikitokea kwamba mmoja wa waliohudhuria huwataka wale waliohudhuria kusimama dakika kwa ajili ya maombolezo kwa wale waliokufa, na hakukuwa na mazishi, je dalili hizi zilizotajwa hapo juu zilikuwaje?
Tulisema: Ndio, hali ya kusimama iliyomo kwenye Hadithi ilikuwa wakati wa kushuhudia Jeneza, lakini haikusemwa kwamba hali ya kusimama iliyomo ndani yake ilikuwa kwa ajili ya mwili wa marehemu haswa, lakini hali ile ilikusudiwa kwa lengo maalumu na mapokezi mengi yamepokelewa kwa ajili ya makusudi hayo, ambayo ni: kutukuza amri ya Mwenyezi Mungu, na sio siri kuwa kusimama kwa ajili ya kuogopa kifo au kupata mazingatio kutoka kwake hali hii ina utukufu wa agizo la Allah, na kuheshimu wale waliotekeleza amri yake, nao ni Malaika, na dalili ya hivyo ni: kwamba wakati masahaba walipomwuliza Mtume – S.A.W- kwa sababu ya kusimama kwake, alisema: kifo ni hofu, kama mkiliona jeneza, basi simameni, na katika mapokezi mengine: Kwani Sio roho? Na katika mapokezi mengine: na katika mapokezi mengine: "Tunasimama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu", na katika mapokezi mengine: "Tunasimama kwa ajili ya Malaika walio pamoja na Jeneza", na hakuna ubishi kati ya mapokezi hayo ambayo yalitaja kusudi la kusimama. Al-Hafidh Ibn Hajar alisema katika maelezo yake juu ya Al-Bukhaariy [3/180]: “Kauli yake: ((Kwani Sio roho?)) Hii haipingani na sababu zilizotajwa hapo juu; ambapo alisema: (Hakika kufa ni hofu), na vile vile imepokelewa kutoka kwa Al-Hakim kutoka kwa Qatada kutoka kwa Anas alisema: "Tulisimama kwa ajili ya Malaika" na Hadithi kama hiyo imepokelewa kutoka kwa Ahmad kutoka kwa Hadithi ya Abu Musa kutoka kwa Ahmed na Ibn Hibban na Al-Hakim kutoka kwa Hadithi ya Abdullah Ibn Amr kwamba Mtume S.A.W alisema: "Hakika mnasimama kwa ajili ya kumtukuza yule anayeshika roho", na kutoka kwa Ibn Hibban kwamba Mtume S.A.W alisema: "Kwa ajili ya kumtukuza Allah anayeshika roho" , Hadithi hizi hazipingana na sababu zilizotangulia hapo juu; kwa sababu hali ya kusimama kwa ajili ya hofu ya kifo ina kutukuza kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na kuheshimu kwa wale waliotekeleza amri yake, nao ni Malaika."
Hii inaungwa mkono na yale yanayosemwa na Ibn Batal katika maelezo yake juu ya Sahihi Al-Bukhariy [Ch. Maktabat Ar-Rushd 3/291]: “Al-Muhallab alisema: Kusimama kwa ajili ya mazishi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi, kwa ajili ya kutukuza jambo la kifo, na kuheshimu amri ya Mwenyezi Mungu; kwa sababu kifo ni hofu, inapaswa kipokewe na kusimama na sio cheko, ameelezea maana hii kutoka kwa Mtume S.A.W.”
Kwa mujibu yaliyotangulia hapo juu: haikusudiwi kusimama hapa ni kwa ajili ya wafu haswa hata kuhitaji kuwepo kwa mwili wa wafu wakati wa kusimama, lakini kuna makusudi mengine nyuma yake, pamoja na: kuchukua funzo, na kutukuza amri ya Mwenyezi Mungu. Kusimama kwa muda wa dakika moja pamoja na ukimya uliochukuliwa na watu kama dhihirisho la heshima kwa walio kufa mashahidi au watu maarufu, na ni njia ya kuheshimu na kuchukua funzo, na kwa mujibu wa Sheria njia zina hukumu ya makusudi.
Baadhi ya watu wanaweza kufikiria kuwa hairuhusiwi kusimama kwa ajili ya kuomboleza roho za watu wenye fadhila, kwa sababu ni sawa na mila za jamii za Magharibi zisizo za Waislamu; lakini hii inajibiwa kwa asili ya msimamo wa kumheshimu marehemu katika Sheria kama yaliyotangulia hapo juu. Vile vile katika jamii hizi Uislamu uliingia na wengi wa watu wake wakawa Waislamu, kwa hivyo ada hizi hazikuwa zinahusiana na wasio Waislamu tru, au kauli mbiu za makafiri, kisha kutokea kwa ufanano katika jambo linaloruhusiwa lenyewe – kama vile ada ambazo hazipingani na Sheria – haulazimishi kutokea ufanano uliokatazwa, Uislamu hautafuti; ubora tu, lakini unawaamuru wafuasi wake kujipambanua kwa maadili mema na ukarimu wakizingatia heshima ya mwanadamu na kutimiza maagano na ahadi, na kuwaheshimu watu, kuwapenda na kuwahurumia, na kuheshimu mila na desturi zao zinazoruhusiwa, lakini ni jambo baya kuwaiga wasio Waislamu katika moja ya masharti mawili haya: La kwanza: Hakika kitu cha kuigwa ni haramu, kama vile kutositiri uchi na kunywa pombe. La pili: Hakika Muislamu anakusudia kuiga asiye Muislamu kwa ajili ya kuiga tu pasipo na kusudi la maslahi linayozingatiwa, na kwamba utegemezi huu una ubaya kwa mujibu wa Sheria vile vile una ubaya kwa mujibu wa maumbile ya kila mwanadamu mwaminifu na mwenye tabia nzuri, ikiwa hali hizi mbili zimepotea, kufanana sio haramu; Ibn Nujaim Al-Hanafiy anasema katika kuelezea kitabu cha: [Kanzu Ad-Daqiq 2/11, Ch. Dar Al-Kitab Al-Islamiy]: “Ujue kuwa kuwaiga watu wa kitabu hakuchukizi katika kila kitu, tunakula na kunywa kama wanavyofanya, lakini jambo ambalo ni haramu ni kukiiga kitu ambacho ni kibaya, na kinalokusudiwa kuigwa tu”.
Kwa hivyo, inaruhusiwa kuiga mila zenyewe ambazo zinaruhusiwa na hakuna kusudi la kuiga. Kwa hivyo, Mtume S.A.W. alisali akiwa amevaa nguo ya Kishamu, kama ilivyopokelewa katika Al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Hadithi ya Al-Mughira ibn Shu'bah, R.A, na hii ilfasiriwa na Imam Al-Bukhari kwa kauli yake “Sura katika kuswali kwa nguo ya Kishamu”. Al-Hafidh ibn Hajar katika kitabu cha: [Al-Fathi 1/473] alisema: Tafsiri hii ni sawa kwani inaruhusiwa kuswali katika nguo za makafiri kama uchafu haupatikani, ametaja neno la Shamu, kwa sababu Shamu katika wakati huo ilikuwa nchi ya makafiri”. Bwana wetu Omar ibn Al-Khatwab – R.A – akawaiga waajemi katika kufanya “Diwani” yaani ofisi ya serikali, na hakuelezwa kuwa kawaiga wasio Waislamu. Rejea: [Al-Ahkaam Al-Sultaniyah kwa Al-Mawardi, uk. 249 – Ch. Dar Al Kutub Al-Elmiyah].
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia hapo juu: hakuna pingamizi kwa mujibu wa Sheria kusimama kimya kwa dakika moja, kwa mfano; kwa ajili ya kuomboleza na kwa ajili ya kuziheshimu roho za wanavyuoni na mashahidi na viongozi waleta mabadiliko na walio na heshima katika jamii, na jambo hili silo uzushi mbaya ambao umekatazwa na Sheria, lakini jumla ya Hadithi zilizomo katika Sunna ya Mtume S.A.W zinaonesha kuwa kitendo kama hicho kipo katika sheria ya Kiislamu kuhusu kupendeza kusimama kwa ajili ya Jeneza na kuwakirimu watu wenye fadhila na kadhalika.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.