Kuacha Kulala Usingizi Minaa kwa Wa...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuacha Kulala Usingizi Minaa kwa Wanyonge, Wagonjwa na Wanawake Wakati wa Hija.

Question

 Nini hukumu ya kutolala usingizi Minaa kwa wanyonge, wagonjwa na wanawake miongoni mwa Mahujaji, na nini hukumu ya kuwawakilisha wengine watekeleze kwa niaba yao, ibada ya kutupia mawe minara mitatu?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Kuihifadhi nafsi ya mtu ni miongoni mwa makusudio muhimu ya Sharia kama inavyojulikana. Na kama masilahi na maovu yakikinzana, hakika katika maamuzi ya kanuni za fiqhi kuwa: kuyazuia maovu hupewa kipamumbele zaidi kuliko kuyaleta masilahi, na kama masilahi yenyewe yakipingana basi yapimwe kwa kadiri maalumu, na hayo yenye fadhila zaidi hupewa kipaumbele cha mengine.
Na nafsi ya Muumini hutamani siku zote kuitekeleza faradhi ya Hija, lakini Mwenyezi Mungu amefaradhisha hilo kwa huyu awezae njia ya kwenda, kwa hiyo amejaalia kizuizi kiwe udhuru wa kuacha kuyakamilisha matendo ya Hija.
Na kuzihifadhi nafsi za Mahujaji ni wajibu wa kisharia, na inalazimika kwa wote wafanye juhudi zao kwa ajili ya kuzihifadhi; kwa sababu ya utukufu wa heshima ya nafsi hizi. Na kutoka kwa Ibn Abbas alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, alipotazama Kaaba alisema: “Karibu katika Nyumba, Utukufu Mkuu ni Wako, Heshima Kuu ni Yako, na kwa Muumini ni mwenye heshima zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu”. Al-Baihaqiy ameipokea.
Na siku hizi haja imeongezeka zaidi kurahisisha mambo ya watu kuhusu Fatwa za Hija na hukumu zake; na hakika hekima ni kuziangalia hali za watu katika kuyatekeleza matendo ya Hija ili kuwaepusha na maradhi na majanga wanayoyapata, ili warudi kwa jamaa zao wakiwa salama na afya nzuri, Mwenyezi Mungu akipenda, hasa katika mahali pa msongamano, ambapo Mwenyezi Mungu alimejaalia ndani yake upana kwa waja wake.
Na jambo la kulala usingizi Minaa wakati wa siku za Hija linahitilafu kati ya wanazuoni: wengi wa wafuasi wa madhehebu ya Imamu Shafi, Hanbal, Malik wanaona kuwa ni wajibu, na Madhehebu ya Hanafi wanaona kuwa ni Sunna, ambapo baadhi ya wafuasi wa Madhehebu manne walikubali rai ya wafuasi Madhehebu ya Hanafi, ingawa haitambuliwi katika Madhehebu zao.
Mwanzuoni Damad mfuasi wa madhehebu ya Hanafi katika kitabu cha; [Majamaa’ Al-Anhur: 1/282, Ch. ya Dar Ihiyaa At-Turath Al-Arabiy] anasema: “inachukiwa kuacha kulala usingizi Minaa, siku za Minaa, hata akilala usingizi mahali pengine bila ya udhuru, hapo hana kosa, kwa rai yetu”. [mwisho].
Na Mtaalamu Al-Mirghinaniy mfuasi wa madhehebu ya Hanafi katika kitabu cha: [Al-Hidayah: 2/501-502, pamoja na Al-Hidayah na Al-Babirtiy, Ch. ya Dar Al-Fikr] anasema: “Inachukiwa kutolala usingizi Minaa nyusiku za kutupia mawe Minara Mitatu; kwa sababu Mtume S.A.W., amelela usingizi Minaa, na Umar R.A., alikuwa akiadhibu kwa mwenye kuacha kukaa ndani yake. Na akilala usingizi mahali pengine halazimiki kitu kwa rai yetu, kinyume cha rai ya Imamu Shafiy, Mwenyezi Mungu Amrehemu; kwa sababu kulikuwa ni wajibu ili kurahisisha kutupia mawe Minara Mitatu katika siku zake, kwa hiyo hakukuwa miongoni mwa matendo ya Hija, na kuacha kwake hakuwajibiki malipo”. [Mwisho]
Na kauli ya kuwa kulala usingizi Minaa ni Sunna, ni kauli moja ya Imamu Shafiy. Na Sheikh Abu Is-Haaq Ash-Shiraziy katika kitabu cha: [Al-Muhadhab: 8/222], pamoja na kitabu cha: [Al-Majmuu’, Ch. ya Al-Muniriyah] anasema kwa maelezo: “Kwa sababu ni kulala usingizi, kwa hiyo hakulazimiki, mfano wake kulala usingizi usiku wa Arafah”. [Mwisho].
Na Imamu Al-Mardawiy mfuasi wa madhehebu ya Hanbal amenukulu katika kitabu cha [Al-Insaaf: 4/60, Ch. ya Dar Ihiyaa At-Turath Al-Arabiy]: kauli kutoka kwa Imamu Ahmad kuwa pia ni Sunna.
Na dalili ya kauli kuwa ni Sunna, ilivyopokelewa na Maimamu Bukhari na Muslim, kutoka kwa Ibn Umar R.A., kuwa Al-Abbas amemtaka idhini Mtume S.A.W., kwa ajili ya kulala usingizi Makah nyusiku za Minaa kwa ajili ya kunywesha Mahujaji maji, na Mtume S.A.W. akampa idhini. Basi ikiwa kulala usingizi Minaa ni wajibu, Mtume S.A.W., asingempa ruhusa ya kuacha kulala kwa ajili ya kunywesha maji, kwa hiyo inafahamika kuwa ni Sunna. [Rejea: Fat-h Al-Qadiir, na Mhakiki Al-kamaal Ibn Al-Humaam: 2/ 501-502, Ch. ya Dar Al-Fikr].
Na miongoni mwa kutegemeza kauli ya kuwa ni Sunna kusemwa: suala la kulala usingizi halikusudiwa kidhati, lakini limeamuliwa kwa maana ya kufaa, nayo ni huruma kwa Haji ili awe mahali karibu na kutupia mawe siku ifuatayo, kwa hiyo ni jambo linaloamuliwa kwa jambo jingine na siyo kwa dhati yake, na ikiwa hali ni hivyo basi haiwi wajibu.
Na tukiongeza kwa yaliyotangulia ni kuwa kuzingatia wanayoyapata Mahujaji kutokana na taabu kubwa, dhiki ya mahali, na hofu ya maradhi: inaonekana kuwa suala la kulala usingizi ni Sunna na sio wajibu ni rai inayochaguliwa kwa kutoa Fatwa.
Na tukisema kuwa jambo hilo sio wajibu, basi aliyeacha kulala usingizi muda wa siku tatu kamili, baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa: ni Sunna achinje na siyo wajibu; na aliyeacha kulala usingizi muda wa usiku mmoja, basi ana malipo ya kutoa sadaka ya kitu cha chakula, na hayo ni kutokana na kauli nyingine ya Imamu Shafiy kuwa kulala usingizi Minaa ni Sunna.
Imamu An-Nawawiy katika kitabu cha: [Al-Majmuu: 8/223] anasema: “Tukisema kuwa kulala usingizi ni wajibu basi kuchinja ni wajibu, na ikiwa ni Sunna basi malipo yake pia ni Sunna’. [Mwisho].
Na wafuasi wa madhehebu ya Hanafi na Imamu Ahmad katika mapokezi kuwa: hailazimiki kitu kutokana na kutolala usingizi Minaa.
Na Imamu Ahmad alisema: (halazimiki kitu, lakini amekosa). [Mwisho: Al-Mughniy na Ibn Qudamah: 3/232].
Hata kwa kauli ya wengi wa wanazuoni kuwa: kulala usingizi Minaa ni wajibu, kwa hivyo wanaruhusu yule mwenye udhuru wa kisheria aache kulala usingizi, bila ya kupata dhambi wala chukio, na pia halazimiki kitu. Na bila shaka kuogopa maradhi ni miongoni mwa udhuru wa kisheria unaotakiwa.
Na Imamu An-Nawawiy katika [Mansak yake: Uk. 399-402, pamoja na Hashiyat Mtaalamu Al-Haitamiy, Ch. ya Dar Al-Hadith, Bairut] anasema: “kuhusu kuacha kulala usingizi Muzdalifah au Minaa kwa sababu ya udhuru, basi hana kosa; na udhuru huu ni wa aina kadhaa:… wa tatu: Ni wa yule anayeo udhuru kwa sababu nyingine, mfano wake… anayehofia nafsi yake au mali yake… rai sahihi: inajuzu kwao waache kulala usingizi, na waondoke baada ya machweo, bila ya kosa kwao”. [Mwisho].
Na Sheikh Al-Khatib Ash-Shirbiniy mfuasi wa madhehebu ya Shafiy katika kitabu cha [Mughniy Al-muhtaj: 2/266, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah] anasema: “Anapewa udhuru yule kuacha kulala usingizi na kutolazimika kuchinja kwa mwenye hofu ya nafsi, mali au kupoteza haja; kama vile: anayetafuta mtumwa mwenye kutoroka, kumtunza mgonjwa; kwa sababu yeye ana udhuru, na mfano wake; mchungaji wanyama, na mwenye kunywesha Mahujaji maji; na ana haki ya kuondoka baada ya machweo, kama inavyofakamika katika hali ya wenye kunywesha Mahujaji maji”. [Mwisho].
Imamu Ibn Qudamah katika kitabu cha: [Al-Mughniy: 5/257] anasema: “Watu wenye udhuru isipokuwa wachungaji wanyama, kama vile: wagonjwa, wenye mali wakihofia kuipoteza na wengineo, ni sawa na wachungaji kuhusu kutoacha kulala usingizi; kwa sababu Mtume S.A.W., aliwaruhusu, na kuna ishara kwa wengine; au twaweza kusema kuwa: Aliainisha hivyo kwa maana inayohusu wengine, kwa hiyo inawajibika kuungana nao”. [Mwisho].
Hivyo ruhusa ya sharia wamepewa watu wa kuchunga wanyama na wenye kunywesha Mahujaji maji waache kulala usingizi Minaa. Imamu Malik katika kitabu chake Al-Muwattaa, kutoka kwa Asim Ibn Adiy R.A, kuwa Mtume S.A.W., aliwaruhusu wachungaji wa ngamia walale usingizi nje ya Minaa; watupe mawe siku ya kuchinja , kisha wakatupa mawe siku ya kesho, na baada ya kesho muda wa siku mbili, kisha wakatupa mawe siku ya kuondoka.
Na Maimamu Bukhari na Muslim walipokea kutoka kwa Ibn Umar R.A, alisema: “Al-Abbas Ibn Abdul Mutwalib amemtaka Mtume S.A.W., idhini alale usingizi Makah nyusiku za Minaa kwa ajili ya kunywesha Mahujaji maji, na Mtume S.A.W., akampa idhini”.
Na hailazimiki kuizingatia matini yenyewe iliyotajwa hapa, lakini ni afadhali kuuzingatia muradi wa sharia kutoka kwake, isijekuwa ni ujinga kamili. Al-Hafidh Ibn Hajar katika kitabu cha [Fat-h Al-Bariy: 3/579, Ch. ya Dar Al-Maa’rifah] anasema: “Je, idhini hii inahusu kunywesha maji au kwa Al-Abbas tu au sifa zingine zinazohusu hukumu hii? Imesemwa: inamhusu Al-Abbas tu, na huu ni ujinga, na imesemwa: pamoja na jamaa zake, na imesemwa: watu wake nao watoto wa Hashimu, na imesemwa: kila anayehitaji kunywesha maji ana hukumu hii. Na imesemwa pia hukumu hii inahusu kunywesha maji kwa Al-Abbas tu, hata ikiwa kwa mwingine haruhusiwi kwake kulala usingizi kwa ajili ya kazi hii. Na baadhi ya wanazuoni wanaona kuwa hukumu hii ni kwa watu wote, na ni sahihi katika hali hizi mbili, na sababu yake ni kuyatayarisha maji kwa Mahujaji.
Na je, hukumu hii inahusu maji tu au inambatana na vitu vingine kama vile chakula na vinginevyo? Mahali pa uwezekano, lakini wafuasi wa madhehebu ya Shafi walisisitiza kuunganisha kwa watu wa kunywesha wafuatao: aliyekuwa na mali na akaogopa kuipoteza, jambo analolihofia kulipoteza, au mgonjwa anayemtunza”. [Mwisho].
Al-Hafidh Abu Omar Ibn Abdul Bar katika kitabu cha: [At-Tamhiid: 17/ 263, Ch. ya Wizrat Umum Al-Awqaf Wash-Suun Al-Islamiyah, Morocco] anasema: “Imepokelewa kutoka kwa Ataa, kutoka kwa Ibn Abbas R.A, alisema: kama mtu akiwa na mizigo Makkah, akaogopa kuupoteza kutokana na kulala usingizi Minaa, hakuna kosa alale usingizi Makkah kwenye mizigo hii, na mapokezi haya ni sawa; kwa sababu ni mwenye hofu na dharura, kwa hiyo anaruhusiwa”. [Mwisho].
Na inajulikana kuwa kulazimika kulala usingizi kwa haji pamoja na matendo mengine ya Hija bila shaka huzidisha kumchosha na kumdhoofisha, mwili wake utakuwa hali dhaifu kiasi kikubwa. Na kwa kuongeza hayo yote yaliyowashukia watu siku hizi ulimwenguni kote kama vile majanga na maradhi hatari yanayohamishwa kwa urahisi kupitia mikusanyiko ya watu na misongamano, hakika mwili wa mtu utakuwa shabaha ya kupata maradhi na maambukizo.
Na bila shaka watu ambao huathiriwa zaidi ya hayo ni wanawake, watoto, wagonjwa, na wakongwe; kwa hiyo inafaa kwao wapate hukumu ya walioruhusiwa, hasa kuwa suala la kulala usingizi sio miongoni mwa nguzo za Hija kwa madhehebu yote yanayofuatwa.
Kuhusu niaba katika kutupia mawe kwa wakongwe, wagonjwa, na wanawake hakika inajuzu, na dalili yake kuwa: inajuzu kumwakilisha mwingine atekeleze Hija, basi mfano wake ni kumwakilisha katika kutupia mawe, kwa sababu Hija ni kutupia mawe na matendo mengine.
Na hii ni ruhusa kwa wenye udhuru miongoni mwa wagonjwa na wengineo, waliokuwa na sababu. Kwa hiyo wengi wa wanazuoni walitaja mambo mengine yasiyotajwa katika matini, kwa njia ya kuyaambatanisha matawi na asili; kama vile: anayehofia nafsi au mali yake, au alikuwa na mgonjwa wa kumtunza, au kuwa na mahitaji ya Mahujaji, na pia aliyehofia mali au nafsi yake, kama ilivyotangulia.
Imamu An-Nawawiy katika kitabu cha [Al-Majmuu: 8/ 219-220] anasema: “Imamu Shafi na wenzake, Mwenyezi Mungu awarehemu, alisema: Asiyeweza kutupa mawe kwa nafsi yake, kwa sababu ya maradhi au kizuizi au mengineyo, basi anaweza kumwakilisha mwingine kwa ajili ya kutupa mawe badala yake”. [Mwisho].
Na akasema pia: kama mtu akiwa mgonjwa au anakizuizi, au ana udhuru, inajuzu kumwakilisha atakayetupa mawe badala yake”. [Mwisho].
Na kwa mujibu wa maelezo hayo yote yaliyotangulia: Inajuzu kwa wakongwe, wagonjwa, na wanawake, kuacha kulala usingizi Minaa, na pia inajuzu kwao wawakilishwe na wengine katika kutupa vijiwe, na hawana kosa, na hawalazimiki kulipa.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas