Kuzigawanya Hukumu

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuzigawanya Hukumu

Question

Je, ni sahihi kuwa: Madhehebu ya Imamu Shafi yanakataza kutufu ndani ya Hijr, kuzingatia ni sehemu ya Nyumba, wakati yanakataza kuielekea kwa Swala, kwa kuzingatia siyo sehemu ya Nyumba? Na kama maneno haya ni sahihi, je, hayo yanahusiana na Istilahi iitwayo: (Kuzigawanya Hukumu)? Na nini ufafanuzi wa Istilahi hii? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Yaliyotajwa katika swali ni kuwa: Wanazuoni wa Madhehebu ya Shafiy wanakataza Swala kuelekea Hijr, wakati wanakataza Tawafu ndani yake, hilo lililotajwa ni sahihi kabisa ya Madhehebu yao.
Imamu An-Nawawiy katika [Al-Majmuu: 3/95, Ch. ya Al-Muniriyah] anasema: “Kama mwenye Swala akielekea Hijr, bila ya kuelekea Kaabah, kuna rai mbili mashuhuri, zilizopokelewa na Mtungaji wa [Al-Hawiy na Al-Bahr] na wengineo. Mojawapo: Swala yake inasihi, kwa sababu Hijr ni sehemu ya Nyumba, kwa mujibu wa Hadithi Sahihi kuwa: Mtume S.A.W., alisema: “Hijr ni sehemu ya Nyumba”, [Ameipokea Muslim]. Na kwa mujibu wa Pokezi lingine: “Mikono Sita ya Hijr ni sehemu ya Nyumba”, na pia kwa sababu akitufu ndani yake basi Tawafu yake haisihi. Na rai sahihi zaidi ya kauli ya pamoja: Swala haisihi, kwa sababu iko kutoka katika sehemu ya Nyumba ni jambo la dhana na halina nguvu ya kuhakikiwa. Hivyo basi, Imamu wa Swala akisimama karibu na Kaabah na walio nyuma yake wapo kuzunguka Kaabah: hiyo inajuzu, na wakisimama mwishoni mwa Msikiti kwa umbo la safu ndefu: hiyo inajuzu, na akisimama karibu na Hijr na ipo safu hapo inaangaliwa kuwa: Swala ya watu wasio pakana na Kaabah: ni batili”. [Mwisho]
Na hilo lililotajwa katika swali ni miongoni mwa Mlango uitwao: (Kuzigawanya Hukumu), ambao ufafanuzi wake ni: Tawi moja linagawanywa na Misingi Miwili, na hilo Tawi linahusiana nayo miwili, kwa sbabu hukumu yake inaambatana nayo miwili, na haiwezekani kufungua upande wa ufananaji, au kujaalia Tawi lichukue Hukumu ya mojawapo ya Misingi Miwili, kwa sababu ya uwazi wa ufananaji na kutothibiti upi ni nguvu zaidi kuliko Mwingine. Hivyo basi inatumiwa kanuni ya (Kuzigawanya Hukumu) na hapo pengine Tawi linachukua hukumu ya mojawapo ya Misingi Miwili, na pengine huchukua hukumu ya Msingi Mwingine.
Kuna inayonesha maana hii katika Hadithi Tukufu:
Miongoni mwake, iliyopokelewa na Bukhariy na Muslim katika Vitabu vyao Viwili Sahihi, kutoka kwa Ummul Muuminin Aisha RA, alisema: “Saad Ibn Abi Waqqas na Abd Ibn Zama’ah waligombana kuhusu kijana, na Saad alisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kijana huyu ni mtoto wa kaka yangu Utbah Ibn Abi Waqqas, naye aliniambia kuwa ni mtoto wake, mtazame sura yake. Na Abd Ibn Zama’ah alisema; Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Huyu ni ndugu yangu, alizaliwa juu ya kitanda cha baba yangu, na mamake. Na Mtume S.A.W., alimtazama akakuta sura yake ni karibu sana na Utbah, akasema: “Yeye ni wako Ewe Abd, na mtoto ni wa uhusiano wa kuoana, na mzinifu apigwe mawe, ujifiche naye ewe Saudah Binti Zama’ah”. Na Aisha alisema: “Hakumuona kamwe Saudah.
Katika Hadithi hii, Mtume S.A.W., aliamua kuwa mtoto ni ndugu ya Saudah kutokana na ukoo, wakati ambapo alimuamuru Saudah ajifiche naye, na kwa mujibu wa Hukumu za kuharamisha kutokana na ukoo halazimiki kujificha naye, lakini hapa Mtume S.A.W., hakika alizigawanya Hukumu.
Al-Hafidh Ibn Hajar Al-A’asqalaniy katika [Fat-h Al-Bariy: 12/38, Ch. ya Dar Al-Maa’rifah] anasema: “Baadhi ya wafuasi wa madhehebu ya Malik waliitoa hii ni dalili ya kisheria ya Hukumu kati ya Hukumu mbili; na maana yake ni: Tawi linachukua ufananaji kutoka katika zaidi ya asili moja, na hapo linachukua idadi ya Hukumu hizi, kwani uhusiano wa kuoana unalazimika kuunga kijana na Zama’ah kutokana na ukoo, na sura yake inalazimika kumuunga na Utbah, kwa hiyo Tawi limepewa Hukumu kati ya Hukumu mbili; yaani kuzingatiwa uhusiano wa kuoana kwa ukoo, na sura wazi kwa kujificha.
Anasema: Kujiunga kijana na mmoja wa wawili hata ikiwa kwa njia moja ni afadhali kabisa kuliko kutengua mmoja wao kikamilifu”. [Mwisho]
Pia miongoni mwa dalili: ilivyopokelewa kuwa: Mtume S.A.W., amejaalia Tawafu iwe Swala, basi inalazimika Tahara na kufunika tupu, wakati ameruhusu maneno ndani yake, na maneno yanapingana na Swala kwa maana yake ya kisheria. At-Tirmidhiy na An-Nasaiy walipokea- na Tamko hili ni la An-Nasaiy- kutoka kwa Tawuus, kutoka kwa mtu wa kumuona Mtume S.A.W., kuwa alisema: “Tawafu kuzunguka Nyumba ni Swala, basi punguzeni maneno ndani yake”.
Na Ibn Abdul Hadiy anasema: “Maana ya hayo kuwa: Tawafu ni kama Swala kwa njia kadhaa, kwa maana ya kuwa: Thawabu yake ni kama thawabu ya Swala, kama ilivyotajwa katika Habari ya: “Mmoja kati yenu angalikuwa katika Swala wakati angaliisubiri”.
Wanazuoni wa Misingi walisema: Msamiati wa kisheria kwa neno uko wazi kabisa kuliko msamiati wa kilugha, kwa hiyo Msamiati wa kilugha unaeleweka kama Msamiati wa kisheria, na kama msamiati wa kisheria ukiwa na shida basi je, utaeleweka kimajazi, kwa ajili ya kuhifadhi sheria iwezekenevyo, au ni ufupisho kati ya Majazi ya sheria na msamiati wa kilugha, kwa ajili ya kutanguliza Uhalisia mbele ya Majazi? Kuna kauli nyingi, na wanazuoni wengi walichagua ya kwanza, na wakatoa mfano wa Hadithi hii ambapo Tawafu ina ugumu wa kuiita Swala kwa Msamiati wa Sheria, kwa hivyo inaeleweka kimajazi, kwa kusema: kama Swala kwa kuzingatia Tahara na Nia; au inaeleweka Msamiati wa kilugha kama dua ya kuomba mambo mema, kwani Tawafu inakusanya dua, bila kuzingatiwa inavyotajwa; au ni ufupisho kutokana na kauli nyingi zinazoihusu”. [Mwisho, na Fat-h Al-Qadiir, na Al-Manawiy: 4/292-293, Ch. ya Al-Maktabah At-Tijariyah Al-Kubra].
Pia miongoni mwa dalili: ilivyopokelewa na At-Tirmidhiy na Ibn Majah, kutoka katika Hadithi ya Aisha kuwa: Mtume S.A.W., alisema: “Mwanamke yeyote aliyeolewa bila idhini ya walii wake hakika ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili, na kama mume wake atamwingilia basi Mwanamke huyo aliyeingiliwa, atapata Mahari ya mweziwe, kutokana na kuhalalishwa tupu yake”. Hapa Mtume S.A.W., alihukumu kuwa Mkataba wa ndoa hii ni batili, na hii inapelekea kubatilisha mambo yanayoambatana nao, bila kuzingatiwa chochote, lakini aliongeza suala la kuthibitisha Mahari, nayo ni miongoni mwa athari ya Mkataba Sahihi na wajibu wake.
Kuna Matawi mengine yaliyotajwa katika Vitabu vya madhehebu ya Shafi, ambapo walielekea njia ile ile, miongoni mwake ni:
Kuingia sehemu ya mwili ndani ya Kaabah hubatilisha Swala, wakati inajuzu kwa anayejitenga msikitini kwa ibada atoe kichwa chake kutoka katika msikiti hali ya kujitenga kwake. Yaani wanazuoni hawa kuna wakati wao wanazingatia kuwa kutoa sehemu ya mwili nje ya mahali pa kuitekeleza ibada kunabatilisha ibada, na na wakati mwingine wanazingatia si hivyo, kutokana na aina ya ibada.
Imamu Shafi katika kitabu cha [Al-Umma: 2/193, Ch. ya Dar Al-Maa’arifah] anasema: “Ukamilifu wa Kutufu ambako ni kuzunguka Nyumba ni: Mtu Kutufu nje ya Hijr, na kama akitufu ndani yake, basi Kutufu kwake hakuzingatiwi, na kama akitufu juu ya ukuta wa Hijr pia haizingatiwi, kwa sababu hakukamilisha Kutufu ambako ni kuizunguka Nyumba. Kwa hiyo Tawafu yoyote kupitia Jukwaa la Kaabah, ndani ya Hijr, juu ya ukuta wa Hijr haizingatiwi; na akianza Tawafu analazimika kuanzia Pembe ya Rukn ambayo iko kushotoni kwake kisha akamilishe Tawafu, lakini akianza na Pembe ya Rukni iliyo kuliani kwake kisha akatufu, hapo atageuza Tawafu na pia haizingatiwi kwa sababu ya kuifanya kinyume chake.
Na yeyoye aliyetufu (Mara saba) kwa njia iliyotangulia: yaani kugeuza Tawafu, kutufu kwenye Jukwaa la Kaabah, ndani ya Hijr, juu ya ukuta wa Hijr, basi Tawafu yake haizingatiwi, bila hitilafu”. [Mwisho]
Al-Khatwib Ash-Shirbiniy katika kitabu cha: [Mughniy Al-Muhtaj: 2/245, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah] anasema: “Inashurutishwa pia kutoa mwili wake mzima, yaani mwenye kutufu, nje ya Nyumba yote, kama alivyosema An-Nawawiy kwa kauli yake: (akitembea juu ya Shazarwan), nalo ni jukwaa nje ya upana wa kaabah lililopanda juu ya Ardhi karibu ya theluthi mbili ya mkono, na Quraish waliliacha jukwaa hili bila kuliingiza ndani ya eneo la Kaabah, kutokana na upungufu wa matumizi ya fedha.
Au aliingiza sehemu ya mwili wake katika sehemu ya Nyumba, kwa mfano kwa kugusa ukuta unaopakana naye, yaani: Jukwaa, au aliingiza sehemu ya mwili wake katika anga la Jukwaa au anga la mahali popote pa Nyumba, au aliingia kutokea upande mmoja wa Hijr na kutoka upande mwingine, au aliacha sehemu ya Hijr kutoka katika Nyumba, - nayo ni kiasi cha Mikono Sita - na kupanda ukuta na kutoka upande mwingine, hapo Tawafu yake haisihi katika yote yaliyotajwa. Na kuhusu mahali pasipo na Hijr, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {na waizunguke Nyumba ya Kale}. [AL HAJJ: 29], na hakika Tawafu ya Nyumba inazingatiwa hali ya kuwa nje yake, na isipokuwa hivyo itakuwa ndani yake.
Na kuhusu Hijr, Mtume S.A.W., alitufu nje yake, pamoja na kauli yake: “Zichukueni ibada zetu kutoka kwangu”, na kwa Hadithi iliyopokelewa na Muslim, kutoka kwa Aisha R.A., alisema: Nilimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.: kuhusu (Ukuta) yaani Hijr: Je, ni sehemu ya Nyumba? Akajibu; ndiyo, nikasema: Kwa nini hawakuiingiza katika Nyumba? Akasema: Hakika watu wako walikuwa na kasoro ya gharama. Nikasema: Kwa nini mlango wake uko juu? Akasema: Watu wako walifanya hivyo ili waingize wawatakao, na wawazuie wawatakao, na lau kama watu wako wasingalikaribia zama za Ujahili, pamoja na kuogopa kuwa nyoyo zao hukanusha, ningaliingiza ukuta katika Nyumba, na kuweka mlango wake ardhini’. Hapo ni wazi katika Habarii hii kuwa Hijr yote ni sahemu ya Nyumba”. [Mwisho kwa maelezo machache].
Na Al-Khatwib Ash-Shirbiniy pia katika kitabu cha: [Mughniy Al-Muhtaj; 2/200] anasema: “Haidhuru hali ya kujitenga kwa ibada msikitini kutoa baadhi ya viungo vyake nje ya msikiti, kama vile kichwa chake au mkono wake, kwa sababu hazingatiwi nje ya msikiti. Na katika Vitabu Viwili Sahihi kuwa Mtume S.A.W., alikuwa akitoa kichwa chake kwa Aisha kwa ajili ya kuzichana nywele wakati alipojitenga msikitini kwa ibada. Na lau angalitoa mguu mmoja tu basi haidhuru, kwa sababu asili ni kutotoka, lakini akitoa miguu yake miwili basi itadhuru, hata ikiwa kichwa chake ni ndani”.
Pia miongoni mwa Matawi: Suala la kumlazimisha kafiri kwa Matawi:
Imamu An-Nawawiy katika kitabu cha: [Al-Majmuu Sharh Al-Muhadhab: 3/5] anasema: “kuhusu kafiri halisi: Wanazuoni walikubali pamoja katika Vitabu vya Matawi kuwa: halazimiki na Swala, Zaka, Saumu, Hija, na nyinginezo miongoni mwa Matawi ya Uislamu. Katika Vitabu vya Misingi wanazuoni wasema: Kafiri anatakiwa kwa Matawi kama anavyotakiwa kwa asili ya Imani; na imesemwa: Yeye hatakiwi kwa Matawi. Na imesemwa: Anatakiwa kwa Makatazo ya uharamisho wa Zinaa, Kuiba, Pombe, Riba, n.k., na siyo Maamrisho kama vile Swala. Na rai sahihi ni ya kwanza.
Na rai hii haina hitilafu na kauli yao katika Matawi; kwa sababu muradi hapa sio muradi wa pale. Muradi wao katika Vitabu vya Matawi kuwa Makafiri hawatakiwi kwa mambo haya hapa duniani, pamoja na ukafiri wao, na hali ya mmoja wao akisilimu basi hatalazimika kuzitekeleza kazi zilizopita, na hawatapata adhabu za kazi hizi katika Akhera.
Na muradi wao katika Vitabu vya Misingi kuwa: watapata adhabu za kazi hizi katika Akhera, pamoja na adhabu ya Ukafiri, basi watapata adhabu za kazi na ukafiri pamoja, na sio Ukafiri peke yake, na wanazuoni hawa hawakutaja suala la kazi zao hapa duniani, hapo kwa Misingi walitaja hukumu ya upande mmoja, na kwa Matawi walitaja hukumu ya upande mwingine, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi”. [Mwisho]. Hapo Imamu An-Nawawiy alibainisha kuwa: upande umetatuka, kwa hiyo hakuna upingaji. Pia miongoni mwa Matawi: Suala la Baba kumnasinisha mke wa mtoto wake hali ya kutoelewa nasaba yake:
Sheikh wa Uislamu Zachariya Al-Answariy katika kitabu cha [Asna Al-Matalib: 3/149, Ch. ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy] anasema: (Tawi) Mtu ameoa mwanamke wa kutoelewa nasaba yake, na baba ya mtu huyu alijinasibisha mwanamke, basi nasaba yake itathibitika, na ndoa haivunjiki, yaani hali ya mume asipomsadiki, kama aliitaja Al-Muzaniy kisha akasema: habari hii ina kigeni. Na Al-Kadhi katika Fatwa zake anasema: hakuna sura ya kuwa mtu anaweza kumwingilia dada yake katika Uislamu isipokuwa hii. Na mfano wake: mwanamke akiolewa mtu wa kutoelewa nasaba yake, kisha baba ya mwanamke alijinasibisa huyu mtu, hapo nasaba itathibitika, na ndoa haivunjiki, hali ya mume asiposadiki”. [Mwisho]
Na miongoni mwake: Suala la kumkalifisha mlevi, kwa maoni ya wafuasi wa madhehebu ya Shafi, na yeye ana hukumu zote za asiye mlevi, hali ya kuwa mwenye dhambi kutokana na ulevi wake, isipokuwa kuhusu ibada ambazo Uisalmu si miongoni mwake. [Taz. Al-Ahkam As-Sultaniyah, na Al-Mawardiy, Uk. 285, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah; Al-Ashbah Wan-Nadhair, na As-Sayutiy: Uk. 237, Ch. ya Issa Al-Babiy Al-Halabiy].
Na miongoni mwake: ilvyotajwa kuhusu Hukumu za Khuntha, ambapo hukumu zake zimegawanywa kuwa: anayechukua hukumu ya mtu wa kikie, au kuchukua hukumu ya mwanaume, na ya tatu ambayo hukumu inagawanywa. Hapo kuna Matawi, miongoni mwake ni: Ndevu za Khuntha ambazo haitakiwi kuzinyoa, kwa sababu angekuwa kiume, kwa hiyo sura yake itabadilika. Lakini analazimika kuosha ndani ya ndevu hali ya udhu, kwa sababu angekuwa kike, kama walivyotaja Mashekhe Wawili, na wengineo. [Taz. Al-Ashbah Wan-Nadhair, na As-Sayutiy, Uk. 266]. Na miongoni mwake: Mtu wa mchanganyiko, yaani: nusu huru na nusu mtumwa, kwani ana hukumu ambazo pengine ni mtumwa na pengine ni huru, pia kuna hukumu inayogawanywa. Na kuna Matawi miongoni mwake ni: Zaka ya Fitri, ambapo hakuna mfanano, na kuhumu yake ni: Yeye na Bwana wake wanalazimika nusu Swaa’. [Taz. Al-Ashbah Wan-Nadhair, na As-Sayutiy: Uk. 255].
Na miongoni mwake ni kama alivyotaja Imamu As-Sayutiy katika kitabu cha [Al-Ashbah Wa-Nadhair: Uk. 119] kwenye maneno kuhusu kanuni ya: (Uhalali na Uharamu vinapokutana, basi Uhalali hushinda); amesema: (kama mtu akiweka sehemu ya ardhi isiyoainishwa iwe msikiti: inasihi, na inalazimika kuigawanywa, na hapo haijuzu kwa mtu mwenye janaba kukaa katika mahali popote pa ardhi hii, wala kujitenga ndani yake kwa ibada, kutangulia uharamu katika pande mbili. Alitaja hivyo Ibn As-Salah katika Fatwa zake”. [Mwisho].
Pia amesema katika kitabu hapo juu: [Uk.192]; “Talaka Rejea: Je, inakata ndoa au siyo? Kuna kauli mbili: Ar-Rafii’iy anasema: Uhakiki kuwa hakuna nguvu ya kauli hizi mbili, kwa sababu ya hitilafu ya Matawi… kwanza itatekelezwa katika kumwingilia, starehe zote, mtazamo, upweke, na kuchunguza uja uzito kama akiwa mjakazi na kumnunua. Na pili itatekelezwa katika urithi, Talaka, usahihi wa: Dhihar, Ilaa, Lia’an, na uwajibikaji wa matumizi ya fedha’. [mwisho].
Na miongoni mwake ni kama alivyotaja katika hukumu za mwanamke mwenye kukosa akili yake: Naye ambaye alisahau mazoeo yake kiasi na wakati na hana utambulisho; ambapo anasema katika kitabu cha: [Al-Ashbah Wa-Nadhair; Uk. 272]: “inaharamishwa kwake kuisoma Qur`ani nje ya Swala”. [Mwisho].
Kwa muhtasari: hakika (kuzigawanya Hukumu) ni njia moja ya kutatua tatizo katika Tawi linaloambatana na Misingi Miwili inayoligombania. Hivyo basi Tawi hili linapewa hukumu katika baadhi ya Matawi kutokana na mojawapo ya Misingi Miwili hii, wakati ambapo linapewa Hukumu zingine katika Matawi mengine kutokana na Msingi Mwingine. Na dalili ya Sharia inaonesha usahihi wa mwelekeo huu, na wanazuoni waliendelea kulikubali na kulitekeleza wakati wa kuwepo sababu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas