Kuwaua Watalii na Kujibu Shaka ya W...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuwaua Watalii na Kujibu Shaka ya Walioruhusu Jambo Hilo.

Question

Je, faradhi ya Jihadi imesitishwa? Je, viza ni usalama unaolinda kumwaga damu na mali? Na ipi Hukumu ya vitendo vya kulipua mabomu na shughuli za kujitoa mhanga? 

Answer

 Sifa zote njema ni za Allah pekee, na swala na salamu ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad Mtume wa Mwenyezi Mungu, na pia juu ya jamaa zake (watu wa Nyumbani kwake) na maswahaba zake, na juu ya wale wanaowafuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.
Kuhusu madai ya kusitishwa kwa Jihadi:
Kwanza kabisa, inapaswa kusisitiza kwamba Jihadi ni haki na ni faradhi ambayo hawezi yeyote kuisitisha wala kuizuia, lakini ikiwa Sheria zitakiukwa na nguzo na masharti yaliyotajwa na Wanazuoni wa Sheria yakawa hayakutekelezwa, basi hiyo haitakuwa Jihadi iliyoruhusiwa; papo hapo inakuwa ni uharibifu katika ardhi, na mara nyingine inakuwa ni uhaini na usaliti. Siyo kila kupigana ni jihadi, na wala sio kila mauaji katika vita yanaruhusiwa.
Ni lazima kupambanua kati ya dhana mbili muhimu: “Jihadi” na “Irjaf”:
Istilahi ya (Jihadi kwa ajili ya Allah) ni istilahi ya kiislamu yenye maana pana katika Uislamu; na inaitwa Jihadi ya nafsi, matamanio, na Shetani, na inaitwa kupigana na adui ambapo inatakiwa kuondosha uadui na kuzuia udhalimu, na aina hii ya Jihadi ina masharti yake ambayo haiwezi kuwa sahihi isipokuwa kwayo, kuwepo kwa khalifa Mwislamu anayewahamasisha Waislamu miongoni mwa raia wake kwa ajili ya Jihadi, kuwepo kwa bendera ya wazi ya kiislamu, na uwezeshaji kijeshi kwa Waislamu. Jihadi ni miongoni mwa faradhi za kutoshelezeana ambayo jambo la kuipanga linarudia kwa Watawala na wakubwa waliochukua madaraka ya nchi na waja na wenye uwezo zaidi kuliko wengine kujua matokeo ya maamuzi haya, ambapo wanafikiria udharura unaopelekea Jihadi, wa kuzuia uadui au kuzuia udhalimu. Basi uamuzi wa Jihadi unadurusiwa kwa njia ya kisayansi kutoka pande zake zote na matokeo yake, na njia hii ina uwiano kati ya maslahi na uharibifu, bila ya woga au unyonge, bila ya uholela au vurugu au mhemuko ambao hautawali kwa kuwepo uthibiti wa akili timamu. Watu hawa watalipwa thawabu kwa ajili ya jitihada zao kwa kila hali, kama wakishinda na kuyafikia yanayotakiwa basi watalipwa thawabu mara mbili, na kama wakishindwa watalipwa thwabu mara moja tu, na kama hawakujitahidi basi watapata dhambi, na hakuna yeyote anayeweza kuwafanyia lolote isipokuwa kutoa shauri kama atakuwa miongoni mwa washauri, na iwapo hatakuwa miongoni mwao, basi asiseme chochote kuhusu jambo asilolijua. Na asijianzishie Jihadi yeye mwenyewe, na iwapo atafanya hivyo basi hali hii itakuwa ni ukiukaji wa haki za Ukhalifa, na pengine katika hali hiyo, madhara ya kutoka kwa ajili ya Jihadi yatakuwa makubwa zaidi kuliko maslahi, na atapata dhambi ya matokeo ya kazi yake.
Kama watu wote watalazimishwa kutoka kwa ajili ya Jihadi, mtu mmoja mmoja bila ya kuhamasishwa na Khalifa, basi maslahi ya watu yatazoroteshwa na maisha yao hayatakuwa sawa sawa. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Wala haiwafalii Waumini kutoka wote} [AT TAWBAH : 122], Ingawa hali hii inapelekea maangamizi, kutojali matokeo, inasababisha kuwashambulia mataifa juu ya Waislamu, inayaangamiza mabustani yao, na ni sababu ya kuingia katika fitna na mgogoro unaowaangamiza Waislamu, sababu ya mambo haya yote ni maumivu ya kupigana mmoja mmoja yasiyosomwa vizuri. Inafahamika kwa upande wa Sheria na akili na kupitia hali halisi kwamba hali ya mtawanyiko na kutokuwepo kwa bendera hupoteza nidhamu yake kwa upande mmoja, na huondosha thamani yake na kuvuruga heshima ya lengo lake kwa upande mwingine.
Imepokelewa kutoka kwa Imam Al-Qurtubi katika kitabu cha: [Hukumu za Qur`ani 5/259] kutoka kwa Imamu Sahlu Ibn Abdullah At-Tostariy -Mweneyzi Mungu amrehemu- amesema kuwa : “Tiini kauli ya Khalifa katika mambo saba: kutengeneza pesa, vipimo na mizani, hukumu, kuhiji, kuswali ijumaa, kuswali Idi mbili, na kusimamisha jihadi”.
Imamu Abu Bakr Ibn Al-Arabiy Al-Malkiy alisema katika kitabu cha: [Hukumu za Qur’ani 1/581, Ch. ya Darul Kutub Al-Elmiyah] kwamba: “Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaamuru watu kupigana Jihadi katika vita vidogo vinavyotawanyika au vinavyokusanyika kwa Mfalme, vita hivi vidogo vikitokea, basi havifanyiki isipokuwa kwa idhini ya Khalifa; ili awatafutie habari, nguvu, na pengine wanahitaji kumwepusha mbali”.
Imepokelewa katika kitabu cha: [Mawahibul Jaliil cha Imam Al-Hattab Al-Malki 3/349, Ch. ya Darul Fikr] kuwa: “Ibn Arafah Al-Sheikh aliuliza Swali: Je, Inaruhusiwa kupigana vita pasipo na idhini ya Khalifa? akasema: Ama kuhusu Jeshi haliruhusiwi kubigana vita isipokuwa kwa idhini ya Khalifa na litaongozwa na mkuu wa Jeshi hilo”.
Vile vile, katika kitabu hicho (3/350) imepokelewa kutoka kwa Bwana wetu Ahmad Zarruuq miongoni mwa Wanazuoni wakubwa wa Madhehebu ya Imamu Maliki na miongoni mwa watu wema sana, alisema kuwa: “Kuiendea Jihadi pasipo na idhini ya kundi la Waislamu na Khalifa wao ni njia ya kuleta fitna, na hakuna wengi waliolishughulikia jambo hilo ila wameshindwa”.
Imamu wa Misikiti Miwili Mitakatifu alisema katika kitabu chake cha: [Ghaithul Umam fii Al-Tiyaath Al-Dhulam 155-156] kuwa: “Inapasa kujua kuwa: faradhi nyingi za kiutendaji ni za kutoshelezeana husimamiwi na Makhalifa, na ni wajibu kwa wote wenye madaraka kuzijali faradhi hizi, kama vile; kuwaandaa wafu, kuwasalia na kuwazika. Ama kuhusu Jihadi, hii inategemeana na Khalifa”.
Ibn Qudamah Al-Hanbali alisema katika kitabu cha: [Al-Mughni 9/166, Ch. ya Daru Ihyaa Al-Turaath Al-Arabiy] kuwa: “Mambo ya Jihadi yanamtegemea Khalifa na jitihadi yake tu, na raia wanalazimika kumtii jinsi anavyoona”.
Kwa upande mwingine, istilahi ya Jihadi haina maana ya kupigana tu, bali maana yake ni kutayarisha majeshi, kulinda mipaka, na kuhifadhi mianya; na mambo hayo ni miongoni mwa faradhi za kutoshelezeana katika Jihadi. Kama hali hii ikifanyika kulingana na uwezo basi wakati huo haitasemwa kuwa: Jihadi imezoroteshwa. Wakuu wa Madhehebu ya Imamu Shafiy walisema kuwa: “Faradhi ya kutoshelezeana -yaani Jihadi- inatekelezwa na Khalifa anapokusanya idadi ya watu katika mianya iliyo sawa na idadi ya makafiri pamoja na kulinda Usalama na mahandaki, na kuwaiga wafalme, au Jihadi inatekelezwa pia kupitia kuingia Khalifa na makamu wake nchi za makafiri pamoja na majeshi kwa ajili ya kupigana nao”. [Mughni Al-Muhtaaj 4/210, Ch. ya Al-Halabi].
Vile vile kutayarisha kwa “njia za kuzuia uhalifu” ni muhimu zaidi kuliko vita venyewe; kwa sababu njia hizi huasitisha umwagikaji wa damu. Qur`ani imeashiria hali hii katika kauli yake, Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi walio fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu} [AL ANFAAL: 60].
Imamu Shafiy -Mwenyezi Mungu amridhie, naye- alisisitiza kwamba kulinda mianya na mipaka ya Uislamu ni muhimu zaidi kuliko kupigana vita na nchi za makafiri. Kupigana vita nao wakati huo, kuna masharti ya kutowadanganya Waisalmu, na kuna matumaini makubwa ya kushinda. Kutokana na hayo, inafahamika kwamba shughuli za kujitoa mhanga zinazosababisha maangamizi ya Waislamu zaidi kuliko wasio Wasilamu haziruhusiwi kamwe, kwa sababu ya maangamizi yake kwa Waislamu pasipo na kuwashinda maadui. Imamu Shafi anasema katika kitabu cha: [Al-Um 4/91-92] kuwa : “Kwanza kabisa, ni wajibu kulinda mipaka ya Waislamu, mahandaki na kuwazuia maadui, na kabla ya kurudi kwa maadui nchi zao waislamu wote wapigane vita na Washirikina … kama ikifanyika hivyo, ni wajibu wa Khalifa kuwaingiza Waislamu katika nchi za Washirikina na ni kipindi cha kutowahadaa Waislamu, na awe anatarajia kushinda”. Vilevile, Imamu huyo anatakiwa asisitize kuwa hairuhusiwi kuwahamasisha Waislamu kupigana vita itakayowaangamiza wao wenyewe, akisema katika kitabu cha: [Al-Um 4/91-92] kuwa: “Haipaswi kwa Khalifa kumwamuru yeyote kupigana vita ila mwenye imani, jasiri, mwenye akili katika vita, siyo mwenye haraka haraka, na Khalifa amwambie yule aliyemwamuru asipigane na Waislamu kamwe”
Al-Qaadhi Abdulwahab Al-Malkiy anasema katika kitabu cha: [Al-Maunah 1/393] kuwa: “Nayo -Jihadi- ni miongoni mwa faradhi za Kutoshelezeana siyo faradhi za lazima kwa kila mtu, anayeitekeleza inawaondoshea waliobakia lawama ya kutotekelezwa, na lengo lake ni kulinda mianya na kuihifadhi kwa nguvu za kijeshi na idadi ya kutosha ya watu”.
Imamu Ibn Jazi Al-Malkiy anasema katika kitabu cha: [Al-Qawaniin Al-Fiqhiyah uk. 126] kuwa: “Kuhusu hukumu ya Jihadi, ni faradhi ya Kutoshelezeana kwa mujibu wa Wanazuoni wengi ..., kama mipaka ya nchi italindwa, na mianya ikahifadhiwa, faradhi ya Jihadi itakuwa imeondoshwa na itakuwa ni Sunna tu kwa wakati huo”.
Kutokana na matini hizi zilizotangulia inafahamika kwamba faradhi ya Kutoshelezeana katika Jihadi kwa kuilinda mipaka inatofauti katika nchi nyingi za Waislamu kwa ujumla, na Jihadi haikusitishwa kama wanavyodai wale.
Jihadi ni faradhi ya lazima katika nchi ambazo ndani yake utukufu wa Waislamu unazodhalilishwa na wapiganaji vita ambao ni madhalimu, na kwamba wenye nchi hizi ni lazima wazilinda. Katika wakati huu Jihadi ni faradhi ya Kutoshelezeana kwa wanaokaa nje ya nchi hizi kwa mujibu wa kauli ya Wanazuoni wa Fiqhi.
Mwanachuoni Al-Shirbini Al-Khatib anasema katika kitabu cha: [Al-Iqnaa] nacho ni miongoni mwa vitabu vya Madhehebu ya Shafiy [4/254, 255], na Kitabu cha: [Hashiat Al-Bijermi, Ch. Ya Darul Fikr] kuwa : “Na hali nyingine ya Makafiri ni kuingia nchini mwetu, wenye nchi hii wanalazimika kuilinda kwa kadiri wanavyoweza. Jihadi katika hali hii ni faradhi ya lazima, na hukumu yake ni ile ile kwa wanaokaa mbali kidogo lakini ndani ya nchi hii. Ama wanaokaa nje ya nchi hii wanalazimishwa kurudi Nchini mwao kama watahitajika, kwa ajili ya kuilinda, basi ni faradhi ya lazima kwa wanaokaa ndani, na ni faradhi ya Kutoshelezeana kwa wanaokaa nje”.
Kutokana na hayo, inafahamika kwamba Jihadi inategemea haja kwa wanaokaa ndani ya nchi iliyoshambuliwa, na kama wanaokaa ndani ya nchi hii wakihitajiwa kwa ajili ya kuilinda ni lazima waende huko, kama hawakutosha, basi wanaokaa mbali zaidi waongezwe n.k. Lakini kutekeleza hukumu ya Kisheria kwa njia hii ni lazima pawepo na njia sahihi inayohusishwa na pande zinazojua ukweli wa mambo ya vita, siasa, pande zinazokadiria mahitaji, zinazoangalia hisabu za matokeo, maslahi, ufisadi unaohusiana na hali ya kitaifa, mikataba ya kimataifa, kujua mizani ya nguvu za Kimataifa, na kila kinachohitaji bajeti maalumu, mafunzo ya kina ya kivita, ya kisiasa, yanayoangalia chaguo la amani lililoashiriwa na Mwenyezi Mungu katika Aya hii: “Na wakiielekea amani nawe pia ielekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua” [AL ANFAAL : 61]. Na kulinda usalama wa nchi za Kiislamu, raia wao, maslahi yao kwa upande mwingine, uwezo wao wa kupambana na kuhimili chaguo la vita kwa upande wa tatu, ili jambo hili lifanyike kwa njia rasmi na inayoainishwa umbo lake kuaminiwa watakao pigana Jihadi ili wasiwe mateka wa pande zinazotiliwa shaka, zinazowatumia kihisia, na hamasa zao kwa kuhudumia malengo yao ya nje kwa jina la Jihadi kwa upande wa nne. Hayo yote ni masuala yanayohusiana na fiqhi ya umma, ambayo yanaangaliwa na mifumo, majeshi, taasisi kubwa tu. Na hayahusiani na fiqhi ya watu, na hawawezi kuamua kuhusu hatima ya mataifa. Viongozi wa Waislamu tu ndio wenye mamlaka ya masuala hayo, hata kama hawakujitahidi, na kwa hivyo basi hali hii haiifanyi Jihadi isitishwe pamoja na kulinda mianya na mipaka. Na hakuna sababu yoyote kwa kukiuka mipaka ya mfumo jumla wa kundi la Waislamu ili maumivu ya vita yawe holela kwa watu, hali ambayo inasababisha kuangamiza nchi kavu na ya kijani kibichi, licha ya vitendo hivi vya ulipuaji holela wa mabomu ambavyo havihusiani na Jihadi ya Kiislamu wala vita vyenye kuheshimika.
Kisha Jihadi ambayo ina maana ya kupigana haikusudiwi yenyewe, kupigana na wasio Waislamu hakukusudiwi hivyo pia, kinyume na wanavyofikiri wenye mitazamo mikali inayofanya asili kwa wasio Waislamu kuwa damu yao ni halali, wakati ambapo wanazuoni wa Sheria wamebainisha kwamba Waislamu wanapofanya faradhi ya Kutoshelezeana kupitia kulinda mianya na mipaka ya nchi za Kiislamu, basi ulinganiaji unatosha badala ya kupigana na wasio Waislamu, na ulinganiaji unapokuwa sahihi, basi hakuna haja ya Jihadi, na kwamba kumwua kafiri kamwe sio kusudio la vita, na jihadi ni njia tu na wala haikusudiwi yenyewe kama ilivyo. Wanazuoni wamesema: “Umuhimu wa Jihadi ni umuhimu wa njia tu, kwani kinayokusudiwa kupitia kupigana ni kuwaongoza watu katika haki, lakini hali ya kupigana na makafiri haikusudiwi hata kama ikiwezekani kutoa uongofu kupitia dalili pasipo na Jihadi itakuwa ni bora zaidi kuliko Jihadi”. [Mughni Al-Muhtaj 4/210].
Ama kuhusu wanayoyasema wale ni “Irjaf” siyo Jihadi, nayo ni istilahi inayotajwa katika Qur`ani katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kama wanaafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao fitna katika Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako ila muda mchache tu (60) Wamelaanika! Popote watakapo onekana watakamatwa na watauliwa kabisa (61) Hii ni ada ya Mwenyezi Mungu iliyo kuwa kwa wale walio pita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika ada ya Mwenyezi Mungu.(62)” [AL AHZAAB : 60-62], nalo ni neno linalo na maana yake mbaya, maana yake ni kueneza fitna kupitia kuhalilisha kumwaga damu na kushambulia mali kati ya wanajamii chini ya madai tofauti, miongoni mwao ni : kudai kuwa mtawala akatoka katika Uislamu, au serikali ya nchi, au makundi maalumu ya watu, na miongoni mwa madai hayo ni kuhalilisha kumwaga damu za wasio Waislamu chini ya dai la kuamrisha mema na kukataza maovu, au kuhalilisha kumwaga damu za wasio Waislamu katika nchi zao, au wale walioingia nchi za Kiislamu kwa kudai kuwa nchi zao zinapigana na Uislamu…n.k kuhusu madai ya kueneza fitna zinazoshawishwa na Shetani kwa waenezao fitna, na ambazo baadhi yake zilikuwa sababu ya kujitokeza kwa Khawarij katika wakati wa Masahaba na wanaokuja baada yao wakatoa sababu za ufisadi wao katika ardhi na kumwaga damu ambazo ni haramu.
Katika wakati huu utawala unatofauti kufuatana na dhana yake; wanavyofanya wenye mitazamo mikali katika nchi za Kiislamu kuhusu kuwaua watalii, au katika nchi zisizo za Kiislamu miongoni mwa shughuli za kutoa mhanga, au vitendo vengine vya ufisadi vinavyotokea mbinu za “Irjaf”, vitendo vyote hivi ni haramu, navyo ni aina ya udhulumu iliyoharimishwa kwa Sheria, na kuwapigana na wenye mitazamo hii kama hawajiepushi na kuwadhuru Waislamu na wasio Waislamu wakiwa wananchi waliopewa amani, na kuitoa jina la Jihadi ni uwongo ili wenye akili dhaifu wasadiki ufisadi wao na kueneza fitna zao, na hali hii ni jeuri katika nchi bila ya haki, wenye jeuri hii ni madhalimu wapigwe kama wakiwa na nguvu mpaka waepushe udhalimu wao na kueneza fitna.
Hivyo vinabainishwa kwa hukumu ya aliyepewa amani, kueleza viza na athari yake kwa mujibu wa Sheria :
Siku hizi watalii ni wasafiri waliokuja kwetu miongoni mwa wanaume na wanawake wakaingia nchi zetu kwa usalama, na hukumu yao katika hali hii ni kama (Musta’man) kafiri aliyepewa amani. Maana ya (Musta’man) katika lugha : ni yule aliyepewa amani. Na maana yake katika istilahi : “Ni yule aliyeingia nchi nyingine kwa amani akiwa ni Mwislamu au adui wa kivita”. [Al-Darul Mukhtar kwa Imam Al-Haskafi Al-Hanafiy pamoja na Hashiyat Ibn Abdiin 4/166].
Amani ni ahadi ya Kisheria na mkataba unaolazimisha uharamu wa kumwua mtu yule na uharamu wa kuiba mali yake. Sheria imeamuru kutimiza ahadi, na dalili za Kisheria zimesisitiza kutimiza ahadi zote.
Imamu Shafiy R.A. alisema katika Kitabu cha: [Al-Um 4/106, Ch. Ya Darul Shaab] kuwa : “Kutimiza ahadi katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi mlio amini! Timizeni ahadi} [AL MAIDAH :1], na kauli yake pia {Wanatimiza ahadi} [al insaan: 7], vile vile Mwenyezi Mungu ametaja maudhui ya kutimiza ahadi katika aya nyingi za Qur`ani, nayo ni pamoja na ahadi zote…”
Hukumu ya kafiri aliyepewa amani ni : kuthibitishwa kwa amani kwake na inalazimishwa kuhifadhi nafsi yake, mali yake, na heshima yake kama walivyo wananchi. Kama Khalifa au mwingine akimpa yeyote amani, Waislamu wote wanalazimishwa kutimiza ahadi hii na hairuhusiwi kumwua wala kumteka, wala kuchukua chochote kutoka mali yake, wala kumwudhi.
Imamu Shafiy R.A. alisema katika Kitabu cha: [Al-Um 4/107] kuwa : “Kama ikiwa hivyo -yaani kama Khalifa akiwapa watu ahadi au akiwachukulia Jizyah- hairuhusiwi kwa Mwislamu yeyote kuchukua mali zao au kumwaga damu zao”.
Imamu An-Nawawiy katika Kitabu cha: [Rawdhatul Talibiin 7/474]: “Kama Kafiri akipewa amani, basi hairuhusiwi kumwua wala kutekwa”.
Amani inafanyika kwa mujibu wa Sheria kwa vyovyote; ikiwa ni neno, maandishi, ishara, desturi, na kwa njia yoyote ikiwa kwa uwazi au kwa ishara, au kwa lugha yoyote. Pia amani anapewa kwa yeyote aliyedhani hata kwa makosa kwamba amepewa amani, basi hairuhusiwi kumsaliti, iwapo Wanazuoni wa Sheria wamesema kwamba kufahamu kuwa asiye Mwislamu ana amani kwa hali yoyote, hali hii inalazimisha kuihifadhi damu yake na mali yake.
Ibn Al-Hajib alisema katika kitabu chake cha: [Jami’ul Umahaat] kutoka vitabu vya maimamu wa madhehebu ya Imamu Malik [246-247, Ch. Ya Darul Yamamah] kuwa : “Kama adui wa kivita akidhani kuwa ana amani, na Khalifa akiwakataza watu wakaasi au wakasahau au hawakujua hivyo, adui huyo arudishwe kwa amani yake”.
Imamu Ibn Juzayya Al-Malikiy alisema katika kitabu chake cha: [Al-Qawaniin Al-Fiqhiyyah Uk. 134, Ch. Ya Darul Fikr] kuwa: “Kama kafiri akidhani kuwa Mwislamu alitaka kumpa amani, lakini Mwislamu huyo hakutaka hivyo, basi hairuhusiwi kumwua. Na kama akihitaji amani kwa jamaa zake na mali yake, inalazimishwa kutimiza ahadi yake hii… na aliyeingia ubalozi wowote hakukosea amani, lakini makusudi yake haya ni amani kwake tu”.
Sheikh Al-Khatib As-Sherbini alisema katika kitabu chake cha: [Mughni Al-Muhtaj] kutoka vitabu vya Maimamu wa Madhehebu ya Shafiy [6/52, Ch. Ya Al-Halabi] kuwa : “Inaruhusiwa kumpa amani kupitia neno lolote lina maana hiyo kwa uwazi ; kama vile kumwambia nimekupa ulinzi na amani, au usiogope wewe utakuwa kama unavyopenda, au uwe kama unavyotaka, na inaruhusiwa kwa kuandika hivyo pia”.
Wanazuoni wa Fiqhi walisema kwamba ikiwa asiye Mwislamu yeyote akipewa idhini ya kuingia nchi za Kiislamu, hali hii ina maana ya kumpa amani pia, basi hairuhusiwi kuivunja ahadi hiyo :
Al-Hafidh Abu Omar Ibn Abdulbar Al-Malkiy alisema katika kitabu chake cha: [Al-Istidhkar fi Sharh Madhab Ulamaa Al-Amswaar 5/35] kuwa : “Kila kinachofahamika na adui wa kivita kuhusu amani ikiwa kupitia maneno au ishara au idhini, basi ni amani na inapaswa kwa Waislamu wote kutimiza ahadi hiyo”.
Siku hizi kuingia nchi kwa njia rasmi kupitia viza ya kuingia au ya kupita, na viza hii ni kibali cha kuingia nchi kwa amani kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa na desturi za ubinadamu. Kuruhusiwa kwa kuingia nchi tu kuna maana ya kupa amani, na imetajwa kwamba amani inapewa kupitia chochote kinachomaanisha hivyo. Kwa hivyo, imethibitishwa kuwa viza ina maana ya kupewa amani, na ahadi zote zinazofanyika kupitia viza zitimizwe. Ahadi inafanyika kwa chochote kinachomaanisha hivyo, yaani asiye Mwislamu yeyote akiingia nchi za Kiislamu kwa haja yoyote - ikiwa kwa ajili ya utalii au haja nyingine- akapewa amani, basi hairuhusiwi kumwaga damu yake wala kuiba mali yake. Na hivyo ndivyo Wanazuoni walivyosema kuhusu kudhani amani kunailazimisha kwa asiye Mwislamu hata akiwa ni adui wa kivita, hata akidhani kwa kosa kuwa akipewa amani.
Mkataba wa amani kwa jumla inafanyika kwa Makhalifa, lakini mkataba wa amani kwa idadi maalumu ya ujumbe wa watalii au wa kibiashara, mkataba huu unafanyika kwa Mwislamu muungwana, mwenye akili timamu, na baleghe kwa mujibu wa maafikiano ya Wanazuoni. Amani hii haitegemee Khalifa pekee yake, lakini kama Mwislamu yeyote alimpa asiye Mwislamu amani, ni lazima Waislamu wote watimize ahadi hii na hairuhusiwi kumsaliti asiye Mwislamu huyo kufuatana na kauli ya Mtume S.A.W., kuwa : “Dhima ya Waislamu ni moja ; hata aliyechukua dhima hiyo ni Mwislamu aliye chini kabisa, basi Mwislamu anayevunja dhima aliyechukua Muislamu mwingine juu ya kafiri, basi atalaaniwa na Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote. Haitapokelewa ibada yake ya faradhi wala ya sunna siku ya Kiama”. Hadithi hii imeafikiwa na Wanazuoni kutoka katika Hadithi ya Ali Ibn Abi Talib Mwenyezi Mungu auheshimu uso wake.
Kauli yake Mtume S.A.W. “dhima ya Waislamu” ni: ahadi yao, na kauli yake : “aliyechukua dhima hiyo ni Mwislamu aliye chini kabisa” yaani : aliyehusika na dhima yao ni aliye chini kabisa miongoni mwao katika hali na idadi. Basi kama Mwislamu mmoja -au Khalifa- akampa mwengine ahadi, hairuhusiwi kuivunja. Na kauli yake “Haitapokelewa ibada yake ya faradhi wala ya Sunna” yaani: haitapokelewa kazi yoyote.
Al-Hafidh Ibn Hajar Al-Asqalaniy katika kitabu chake cha: [Fathul Bari 4/86, Ch. Ya As-Slafiyyah] kuwa : “Na maana ya kwamba : dhima ya Waislamu ni ikiwa imepewa na Mwislamu mmoja au Waislamu wengi, mheshimiwa au mwenye hali ya chini. Kama Mwislamu mmoja akampa kafiri amani, hairuhusiwi kwa yeyote kuivunja ahadi hiyo, wote ni sawa katika jambo hili mwanamke, mwanamume, muungwana, na mtumwa, kwa sababu Waislamu wote ni kama nafsi moja”.
Kufuatana na hivyo, matini za Wanazuoni wa Fiqhi zimetajwa kama zifuatazo :
Imamu Shafiy – Mwenyezi Mungu awe radhi naye – alisema katika kitabu chake cha: [Al-Um 4/196] kuwa : “Kama Mwislamu baleghe akampa amani kwa muungwana au mtumwa anayepigana au asiyepigana au mwanamke, basi amani inaruhusiwa.. kama Mwislamu akiwashiria watu hawa kwa kinachomaanisha amani akisema : nimewapa amani kwa ishara, basi hii ni amani”.
Al-Qaadhi Abdulwahab Al-Malkiy alisema katika kitabu cha: [Al-Maunah ala Madhhab Alam Al-Madinah 1/408, Ch. ya Darul Kutub Al-Elmiyyah] kuwa: “Amani iliyopewa na Mwislamu muungwana baleghe hairuhusiwi kuivunja akiwa Mwislamu huyo ni mwanamume au mwanamke”.
Imamu Ibn Juzayya Al-Malikiy alisema katika kitabu chake cha: [Al-Qawaniin Al-Fiqhiyyah Uk. 134, Ch. ya Darul Fikr] kuwa: “amani ni aina tatu : ya kwanza na ya pili ni amani ya kijumla nayo inahusiana na Khalifa tu, nazo ni mapatano na dhima, ya tatu ni : inahusiana na kafiri mmoja au idadi maalum, inapewa na Mwislamu yeyote mwenye akili, akiwa ni mwanamke kwa mujibu wa madhehebu manne, na pia mtumwa kwa mujibu wa madhehebu tatu tu (yaani madhehebu yote isipokuwa madhehebu ya Imamu Ahmad Ibn Hanbal )”.
Ibn Al-Hajib alisema katika kitabu chake cha: [Jami’ul Umahaat 247-246] : “Inaruhusiwa amani inapewa na mkuu wa jeshi kwa ujumla na kwa sharti.. Vile vile kila Mwislamu, muungwana, baleghe, anaweza kupa amani… Pia mwanamke, mtumwa na mtoto akiwa na akili timamu wanaweza kupa amani kwa mujibu wa mtazamu mashuhuri wa Wanazuoni”.
Watalii hawa wasio Waislamu walipewa amani na Khalifa kupitia viza, pia hawa waliofanya mkataba pamoja na jumbe hizi za kiutalii na walipanga safari zao na waliwakaribishwa katika nchi zao pia waliwapa amani, waliowafikisha miongoni mwa Waislamu mpaka nchi zao waliwapa amani, na waliowapokea katika uwanja wa ndege, wakawaingiza katika nchi wakawapa amani, hali hizi zote zina hukumu ya amani iliyohifadhi damu zao na mali zao.
Kama mtu asiye baleghe au asiye na akili timamu akiwapa amani, wakadhani kuwamba hii ni amani, hairuhusiwi kuwaua, lakini ni lazima kuwapa amani na ulinzi wao, kwa sababu ya kutopambanua baina aliyeruhusiwa kupa amani na asiyeruhusiwa.
Imamu Shafiy R.A. alisema katika Kitabu cha: [Al-Um 4/196] kuwa : “Kama kafiri moja akipewa amani na wasio baleghe au mwenye wazimu hairuhusiwi kuivunja ahadi yake kabisa, vile vile mwenye dhima akipewa amani hairuhusiwi kuivunja ahadi yake kabisa. Kama yeyote miononi mwa hawa akitoka kwa amani ni lazima kuihifadhi amani yao wala hairuhusiwi kuiba mali zao au kumwaga damu zao”.
Vitendo vya uharibifu vya makundi dhalimu dhidi ya watalii na kuwaua ni ukiukaji wa watawala Waislamu na ukiukaji wa umma wote na kuivunja ahadi zao.
Dalili zao kuhusu kuruhusiwa kwa vitendo vya mabomu kama ilivyothibitika katika Sunna Tukufu kuhusu kuwashambulia washirikina dalili hizi ni kosa kubwa na upimaji mbovu; kwa sababu kushambulia hakuruhusiwi isipokuwa kwa kuivunja ahadi na amani au inayofahamika siku hizi kwa azimio la vita, na hairuhusiwi kabisa kushambulia pamoja na kutimiza ahadi na amani.
Imamu Shafiy R.A. alisema katika Kitabu cha: [Al-Um 4/107] kuwa : “Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema : {Na ukichelea khiana kwa watu fulani basi watupilie ahadi yao kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini} [AL ANFAAL : 58], Imamu ShafiY alisema: Kama ikitajwa dalili zenye maana ya kutotimiza watu ahadi yao ya kusitisha uadui, basi dalili hizi zinarudishwa kwao, (4/108) “Kama wenye kusitisha uadui walikuwa miongoni mwa wanaoruhusiwa kuchukuliwa Jizya hairuhusiwi kuwadanganya. Baada ya kuivunja ahadi na azimio la vita, Khalifa anaruhusiwa kuwashambulia waliovunja ahadi katika wakati wowote na kuwachukua mateka kama wakimdanganya”.
Upimaji wa kudanganya katika vita ni upimaji mbovu ; kwa sababu ni upimaji tofauti ; kwani ipo tofauti kubwa kati ya kuivunja ahadi na uhaini unaoruhusiwa katika vita, kuhusu jambo hili Imamu Ibn Jazi alisema katika katika kitabu cha: [Al-Qawaniin Al-Fiqhiyah Uk. 135] akisisitiza tofauti hii kuwa: “Tofauti kati ya kuivunja amani na uhaini unaoruhusiwa katika vita ni kwamba amani hutuliza nafsi ya kafiri, udanganyifu ni utaratibu wa mafumbo ya vita kwa njia iliyowadanganya adui kugeuka kutoka kwake hivyo kuna nafasi, basi kudanganya na kuficha kwa njia ya kinaya inaruhusiwa, na hairuhusiwi kuwafahamisha makafiri kwamba yeye amekuja kwa ajili ya kuwashauri, hali hii ni uhaini nayo hairuhusiwi”.
Imamu Al-Nawawiy alisema kuwa : “Wanazuoni wameafikiana juu ya kuruhusiwa kwa kuwadanganya makafiri katika vita kwa kadiri inavyoweza, ila kwa kuivunja ahadi au amani, hali hii hairuhusiwi”.
Yaliyotangulia yanathibitisha utukufu wa damu, mali, na heshima ya wasio Waislamu wakati wa kuingia nchi za Waislamu kwa amani. Hairuhusiwi wakati huu kuwashambulia kabisa. Hali ile ile kuhusu kuingia kwa Mwislamu nchi za wasio Waislamu kwa viza : kama kwamba hairuhusiwi kuwadanganya wasio Wasilamu wakati wa kuingia nchi za Waislamu kwa amani, hali ile ile kuhusu Mwislamu akiingia nchi za wasio Wasilamu kwa viza, basi ana haki ya kupewa amani, na hairuhusiwi katika wakati huu kukiukwa utukufu wake au kumshambuliwa. damu zao, mali zao, na heshima yao ni haramu, hali kumshambulia ni uhaini kwa mujibu wa yaliyotajwa na Wanazuoni; kwani tumetaja kwamba viza ya kuingia nchi za Waslamu ni amani kwa wasio Waislamu, hali ile ile kwa Mwislamu wakati wa kuingia nchi za wasio Waislamu, kwa sababu wasio Wasilamu hawakumpa Mwislamu viza ila kwa sharti ya kuacha kuwadanganya na kuhifadhi nafsi zao, ingawa sharti hii haikutajwa kwa uwazi, lakini inafahamika katika maana kama alivyosema Imamu Ibn Qudamah Al-Hanbali katika kitabu chake cha: [Al-Mughni], maneno yake yatatajwa baadaye. Mkataba wa amani una maana ya kuwa na haki ya kupewa amani pande zote mbili, na kwamba kila upande umeupa upande mwingine amani, kwa hivyo, Mwislamu wakati huu haruhusiwi kumdanganya mwingine asiye Mwislamu kabisa.
Imamu Shafiy R.A., alisema katika Kitabu cha: [Al-Um 4/164-165, 188] kuwa : “Kama wasio Wasilamu wakimpa Mwislamu amani, wakamruhusishia kuingia nchi zao kwa wema, nao wana uwezo juu yake, ni lazima kwake kuwapa amani pia, yaani kumpa amani kwake ni amani kwao, Mwislamu katika wakati huu haruhusiwi kuwaua au kuwadanganya ... Kama watu miongoni mwa Wasilamu wakiingia nchi za kivita kwa amani, basi adui ni lazima kupewa amani mpaka watoke au kufikia muda ya amani, na hairuhusiwi kwao kuwadhulumu maadui au kuwadanganya .. na hatujui mtazamo mwingine unaopinga mtazamo huu”.
Imamu Mohammad Ibn Al-Hassan Al-Shibaniy alisema katika kitabu chake cha: [Al-Sair Al-Kabiir maa Sharhul Sarkhasi 2/66-67, Ch. ya Darul Kutub Al-Elmiyyah] kuwa : “Kama baadhi ya Waislamu wakija mahali pa adui wa kivita wakiwaambia kuwa : sisi ni wajumbe wa Khalifa, wakitoa barua inayofanana na barua ya Khalifa au hawaitoi, na jambo hili lilikuwa hila kutoka wao kwa washirikina, maadui wakawaambia : ingieni, Waislamu wakaingia nchi ya kivita, basi Waislamu hawaruhusishwi kumwua yeyote miongoni mwa maadui wa kivita wala hawaruhusishwi kuchukua mali zao kama wakiwepo katika nchi zao.
Aliyeeleza mtazamo huu alisema : “Kwani makafiri hawajui nia ya Waislamu wanaoingia nchi, basi hukumu inategemea wanaoonesha; kwa sababu ni lazima kuepuka kudanganya, hivyo kwa sababu suala la amani ni nguvu na uchache wake unatosha”.
Imam Ibn Qudamah alisema katika kitabu chake cha: [Al-Mughni 12/587, Darul Hadith] kuwa: “Suala la: anayeingia nchi ya adui kwa amani haruhusiwi kuwadanganya katika mali yao, kwa sababi udanganyifu wao ni haramu, kwani wamempa amani kwa sharti la kuacha kuwadanganya na kuwapa amani, ingawa sharti hili halikutajwa kwa uwazi, lakini linafahamika katika maana”.
Kutokana na hayo, kosa kubwa linalofanywa na hawa madhalimu katika nchi za wasio Waisalmu la shughuli za kujitoa mhanga zenye sifa ya uhaini zitadhihirika, madhalimu hawa wanawatisha wanaowaamini kwa shughuli hizi na wakawaruhusisha kuingia nchi zao, na kwamba vitendo hivi haviruhusiwi kabisa, bali vinapingana na mafunzo ya Kiislamu na utukufu wake ambayo yanakataza uhaini hasa kwa walioturuhusu kuingia nchi zao kwa amani.
Na sababu zinazotajwa na hawa kwa ajili ya kuhalalisha vitendo vyao vyenye kueneza fitna, ufisadi na vya ulipuaji wa mabomu katika nchi zinazopigana vita na Waislamu au zinazopinga wananchi Waislamu wanajibiwa kuwa vitendo hivi vya uhaini havitofautishi kati ya raia na mwanajeshi, na kwa mujibu wa Sheria, hairuhusiwi kukaribia kuwaua raia wakiwa ni wanaume au wanawake, na kama ikitangazwa Jihadi ni jambo la lazima tutofautishe kati ya mwanajeshi na asiyekuwa mwanajeshi, hasa ikijulikana kwamba mara nyingi wananchi katika nchi za demokrasia za wasio Waislamu wanapinga vita vinavyopiganwa na serikali zao dhidi ya baadhi ya nchi za Kiislamu, maandamano yanayopinga vita hivi yanachangia jitihada za kuondosha serikali hii iliyotangaza vita. Maana ya hayo ni kwamba siyo wananchi wote ni maadui wa kivita kufuatana na serikali zao, kwa hivyo, kuwaua pasipo na kutofautisha kati ya raia na mwanajeshi hakutokani na mafunzo ya Kiislamu. Na imethibitika kwa mujibu wa Misingi ya Sheria Tukufu kwamba hairuhusiwi kumwadhibu mtu kwa sababu ya kosa la mwingine. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na kila nafsi haichumii ila nafsi yake. Na habebi mwenye kubeba mzigo wa mwenziwe.} [AL ANA'AM : 164].
Imamu Shafi anasema katika kitabu cha: [Al-Um 4/108] kuwa : “Kama wakitofautiana au baadhi ya watu hawakukubaliana nao, na baadhi yao wakaonesha nia njema na wengine wakaonesha kinyume na hivyo, inaruhusiwa kupigana nao Vita lakini siyo wote, inaruhusiwa kuwaita wenye nia njema watoke, wakitoka wanatimiziwa ahadi na waliobakia wanauawa, lakini wenye nia njema kama hawakuweza kutoka wanaepushwa, na hairuhusiwi kuchukua mali zao au kumwaga damu zao”.
Kutokana na kauli yake “inaruhusiwa kupigana nao lakini siyo wote” inadhihirisha kuwa wakiwepo watu miongoni mwao hawakupigana nasi (nao ni wengi miongoni mwa wananchi wa dunia wasio Waislamu wanaokataa kushiriki katika kupigana vita pamoja na serikali zao dhidi ya nchi za Kiislamu) watu hawa hairuhusiwi kupigana nao wote kwa vitendo vya kulipua mabomu au kwa shughuli za kujitoa mhanga. Na kupitia maneno ya Shafi unajulikana ubatili wa dalili za watu hawa wanaosema kuwa shughuli za kujitoa mhanga zinaruhusiwa dhidi ya wasio Waislamu katika wakati ambao hakuna vita pasipo na kupambanua kati ya adui wa kivita na asiyekuwa adui.
Kutokana na maelezo yaliyotangulia inadhihirika kuwa kuwadhuru watalii wageni walioingi nchi za Waislamu kwa kuwaua ni maovu makubwa na ni dhambi kubwa mno, kwa sababu hali hii inapingana na amani waliopewa nasi kupitia viza ya kuingia nchi zetu kwa njia za kisheria. Hali ile ile kwa wasio Waislamu katika nchi zao hairuhusiwi pia kuwauawa kwa vitendo vya kujitoa mhanga au kwa vitendo vya mabomu, kwa sababu vitendo hivi ni haramu, kwani vinapingana na amani waliyopewa nasi tulipowaruhusu kuingia nchi zetu kwa nija ya kisheria, Na Sheria ilituamuru kutimiza ahadi na mikataba; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Enyi mlio amini! Timizeni ahadi} [AL MAIDAH:1].
Na imepokelewa kutoka kwa Imamu Bukhari katika Sahihi yake kutoka kwa Abdullah Ibn Umar R.A. kwamba Mtume S.A.W. amesema: “Mambo manne mwenye kuwa nayo basi huwa ni mnafiki wa kweli, na mwenye kuwa na moja tu katika hayo basi huwa na sifa moja ya unafiki mpaka aiache: Anapo zungumza husema uongo na anapochukua miadi hatekelezi, na anapotoa ahadi hufanya hiana na anapo gombana hupindukia mipaka”.
Sheria imewatishia kama hawa wasiotimiza ahadi ya amani pamoja na waliowapa amani na wakawaruhusishia kuingia nchi zao kuwa watabeba bendera ya uhaini Siku ya Kiyama. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Majah kutoka kwa Amr Ibn Al-Hamq Al-Khuzai R.A. alisema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. alisema “aliyeamini mwanamume juu ya damu yake akamwua, akabeba bendera ya uhaini Siku ya Kiyama”.
Vitendo hivi ni miongoni mwa madhambi makubwa, kwani ni kumwaga damu iliyo haramu kumwagwa, kuua nafsi za Waislamu wasio na hatia, na nafsi za wasio Waislamu zilizoharamishwa kuuawa isipokuwa kwa haki. Sheria Tukufu imeiipa heshima kubwa damu ya Mwislamu na ikakemea sana kuimwaga bila ya haki. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu, na humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa.} [AN NISAA : 93]. Imepokelewa kutoka kwa Al-Nasaa’i kutoka kwa Abdullah Ibn Umar R.A. kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema kuwa: “kuangamizwa kwa dunia ni jambo jepesi kwa Mwenyezi Mungu kuliko kumwua Mwislamu”, vile vile Mwenyezi Mungu Mtukufu ameharamisha kabisa kuua nafsi bila ya haki, Mwenyezi Mungu Mtukufu alisema: {Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha kuiuwa, ila ikiwa kwa haki.} [AL ANA'AM :151], bali Mwenyezi Mungu amefanya kuua nafsi - iwe ni ya Mwislamu au asiye Mwislamu - ni sawa na kuwaua watu wote. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote.} [AL MAIDAH : 32].
Pia kuna kuwaua wasio waangalifu. Imepokelewa kutoka kwa Abu Dawud na Al-Hakim katika kitabu cha: [Mustadrak] kutoka kwa Abu Hurairah R.A. alisema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. anasema: “Muumini hamuui mtu yoyote, Imani ni kizuizi cha kuua”. Ibn Al-Athir amesema katika kitabu cha: [Al-Nihayah]: “Kuua maana yake ni mtu kumshambulia mwenzake wakati wa kutoangalia na kumwua”. Maan aya Hadithi ni kwamba Imani inazuia kuua kama kizuizi kinavyozuia kutenda, kwani kuna hila na udanganifu. Na kauli ya Mtume S.A.W: “Muumini haui” hili ni katazo au ni Hadithi yenye maana ya katazo.
Katika hukumu za Jihadi inathibitika kwamba hairuhusiwi kumwua mtu ambaye hakumfikiwa na Ulinganiaji wa Dini hata akiwa ni adui wa kivita asiyepewa amani, fidiya ya mauaji yake ni juu ya aliyemwua, Imam Shafii anasema katika Kitabu cha: [Al-Um 4/157] kuwa: “Kama Mwislamu akiua mwengine mshirikina ambaye hakufikiwa na Ulinganiaji wa Dini, akamwangamiza”, hali itakuwaje kwa yule aliyemwua mtu aliyepewa amani na akamdanganya, akaifanyia uhaini dhima ya Allah, Mtume wake S.A.W., ya Waislamu na watawala wao.
Na kwamba vitendo hivi vinapinga makusudio ya Sheria ya kuu:
Sheria Tukufu inasisitizia kuhifadhi vitu vitano ambavyo dini zote zimekubaliana umuhimu wa kuvihifadhi, navyo ni: Dini, Nafsi, Akili, Heshima, na Mali, na hayo ndio makusudio matano ya Kisheria.
Ni wazi kwamba vitendo hivyo vya ulipuaji wa mabomu vinayabatilisha makusudio hayo, miongoni mwao ni kuhifadhi nafsi; basi aliyeuawa kama akiwa ni yule aliyejitoa mhanga na aliyetenda vitendo vya kujilipua mabomu aliyejisababishia kifo kwa kujilipua n.k. basi ataingia chini ya kauli yake Mtume S.A.W: “Mwenye kujiua kwa kitu chochote duniani, ataadhibiwa kwa kitu hicho hicho Siku ya Kiyama”. Hadithi hii imekubaliwa kutoka kwa Hadithi ya Thabit Ibn Al-Dhahak R.A.
Na kama aliyeuawa ni mwingine, basi kama aliyeuawa ni Mwislamu, kumwua kwa makusudi ni uadui mkubwa, na hakuna dhambi kubwa zaidi kuliko dhambi hii baada ya ukafiri. Kuhusu kukubaliwa toba yake au kutokubaliwa; kuna tofautia kati ya Masahaba na waliokuja baada yao. Na Kama mtu aliyeuawa si Mwislamu, kama alikuwa ndani ya nchi zetu, basi yeye alipewa ahadi ya amani, na kama alikuwa nchini mwake, basi yeye ni mwananchi asiye na hatia na hana dhambi yoyote. Katika hali zote hizi nafsi zao zinahifadhiwa na hairuhusiwi kuwavamia na ni lazima walindwe.
Vile vile vitendo hivi vya ulipuaji wa mabomu vinabatilisha makusudi ya kuhifadhi mali: ambapo matokeo ya vitendo hivyo yako wazi sana. Miongoni mwa matokeo hayo ni kupoteza mali, majengo, mali za umma na za watu binafsi, na kupoteza mali ni suala lililoharamishwa na Sheria, ambapo uharamu huo unazidi marudufu kama mali hizi zilizopotezwa si za mwenye kuzipoteza bali ni mali za mwingine - kama hali ilivyo katika suala hili – uharamu unahusiana na ukiukwaji wa katazo la Sheria kwa upande mmoja, na uharamu unahusiana pia na haki za viumbe kwa upande mwengine.
Pia vitendo hivi vinasababisha madhara na ufisadi mkubwa: Lengo la Sheria Tukufu ni kuleta maslahi na kuondosha ufisadi. Ni wazi kwa mtu mwenye akili kwamba vitendo hivi vinaleta uharibifu kwa Waislamu kote duniani; Na katika uharibifu huu ni kuvitumia kama sababu ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi za Kiislamu, kuzitumia heri za Waislamu, kuzipora rasimali zao kwa kisingizio cha kutafuta ugaidi au kwa ajili ya kuhifadhi maslahi ya kiuchumi, au kuwakomboa wananchi. Na mwenye kuwasaidia hawa ili kutekeleza makusudio yao na kufikia malengo yao kupitia vitendo vyao viovu, kwa sababu ya vitendo hivyo atakuwa amewasababishia shari nyingi Waislamu, pia vitendo hivyo vitakuwa vimesaidia kupunguza nguvu ya Waislamu, na hali hii ni uhalifu mkubwa.
Miongoni mwa ufisadi mkubwa ni vitendo hivi ambavyo viko mbali na mafunzo ya Uislamu na utukufu wake, vitendo hivi vinazidisha vumi na shutuma za uongo ambazo maadui wa Uislamu wanazibandika katika dini ya Uislamu kwa nia ya kuivuruga sura yake, na kusisitiza kuwa Uislamu ni dini ya kinyama na ya umwagaji damu, lengo lake ni kuwashinda watu na kueneza ufisadi katika ardhi, na hali hii ni miongoni mwa aina za uzuiaji wa njia na dini ya Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwa ufisadi mkubwa ni yale yanayotokana na vitendo hivyo kama vile; unyanyasaji wa Waislamu katika baadhi ya nchi za kigeni, unaofanywa na wenye mtazamo mkali, kutokana na hali hiyo, Waislamu wanapata madhara makubwa katika nafsi zao, mali zao, heshima zao, na baadhi yao wanalazimika kuitekeleza dini yao kwa siri au kuziacha baadhi ya Ibada zikiwemo za faradhi.
Mambo hayo yote yalisababishwa kwa vitendo hivi vilivyofanywa na hawa wajinga wasiojua wanachokitaka wala wanachotakiwa kukifanya, na wanaharibu rasimali na kuangamiza wakidhani kwamba wanatekeleza Sheria, nao kwa vitendo hivyo watapata kile alichokisema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Ni wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kwamba wanafanya kazi nzuri} [AL KAHF: 104].
Wanazuoni wamesema kuwa kama maslahi yakikinzana na madhara, basi kuondosha madhara ni bora zaidi kuliko kuleta maslahi. Na maneno haya ya Wanazuoni yanahusisha maslahi ya kweli. Je, hali inakuwaje kwa yale maslahi yanayodhaniwa kuwepo au yale ambayo hayapo?
Ama kuhusu yanayosemwa na wajinga hawa juu ya vitendo hivi kwamba eti ni miongoni mwa Sehemu ya Jihadi dhidi ya adui, na baadhi ya Wanazuoni wanaiita vita, na jina hilo ni ujinga na ni kosa kubwa sana; kwa sababu Jihadi iliyoruhusiwa katika Uislamu ni ile iliyo chini ya bendera ya Khalifa na kwa idhini yake, au kama sio hivyo, itakuwa fujo na umwagaji mkubwa sana wa damu bila ya haki na kwa kisingizio cha Jihadi, lakini Jihadi kwa mujibu wa Uislamu ni kwa ajili ya kuyatekeleza malengo mawili, nayo ni:
La kwanza ni: kuwatetea Waislamu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanao kupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao uadui} [AL BAQARAH: 190].
La pili ni: kutetea uhuru wa watu katika kuamini Dini ya Uislamu au kubakia kama walivyo, nayo ni fitna tuliyoamuriwa kupigana kwa ajili ya kuiondosha; ili watu wachague dini yao kwa uhuru kamili, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha basi pasiwepo uadui ila kwa wenye kudhulumu.} [AL BAQARAH: 193].
Ni wazi kwamba Jihadi inayokuwa kwa ajili ya kutekeleza malengo mawili hayo haikuwa ila dhidi ya adui wa nje.
Ama kuhusu kutumia mauaji, vitisho, kuharibu mali za jamii ya Kiislamu, kama ilivyokuwa kwa vitendo vya kulipua mabomu katika nchi za Waislamu, hali hii inaitwa “Al-Hirabah” kwa mujibu wa Wanazuoni wa Fiqhi. “Al-Hirabah” ni dhuluma na uharibifu katika dunia, mwenye kufanya hivyo anastahiki adhabu kubwa sana, kama vike adhabu ya kuua, kuiba, na kuzini, kwani ni uharibifu unaopangwa na kuandaliwa, na mwenye kuufanya uharibifu huu anaufanya dhidi ya jamii. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
{Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuawa, au kusulubiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchini. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa} [AL MAIDAH: 33].
Hairuhusiwi hivyo katika nchi na jamii zisizo za Kiislamu, kama ikiongezwa mikataba ya kimataifa kati yao na Waislamu, na kwamba wataruhusiwa Waislamu kulingania Waislamu wengine kama wanavyofanya hivyo pamoja na wasio Waislamu, basi kufanya shughuli za uhalifu ni haramu na ni ufisadi zaidi, lakini hata pamoja na kutangaza vita halisi hairuhusiwi kuua watu hovyo kwa ujumla wao; ambapo hairuhusiwi kuwaua wanawake wasio wa kivita wala watoto wala wazee wanyonge na waajiriwa wanaofanya kazi zisizo husiana na vita, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaokupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao uadui} [AL BAQARAH: 190]. Imepokelewa kutoka kwa Imam Al-Tahir Ibn Ashour katika Tafsiri yake kutoka kwa Ibn Abbas na Umar Ibn Abdulaziz na Mujahid kuwa Aya hii haikufutwa, akasema: “Kwani maana ya wale wanaokupigeni ni wale wanaojiandaa kukupigana vita nanyi, yaani msipigane na wazee, wanawake na watoto”.
Imepokelewa kutoka kwa At-Termidhiy kutoka kwa Sulaiman Ibn Buraidah kutoka kwa baba yake alisema kuwa: Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. wakati alipokuwa akimtuma mkuu wa jeshi akamwusia kumcha Mwenyezi Mungu na kuwafanyia wema Waislamu ambao ni pamoja naye akisema: “Piganeni vita kwa jina la Mwenyezi Mungu katika njia ya Mwenyezi Mungu, piganeni na aliyekufuru, piganeni vita wala msichupe mipaka, wala msifanye uhaini, wala msikate kate viungo, wala msiue mtoto”.
Imepokelewa kutoka kwa Ahmad kutoka kwa Al-Muraqa Ibn Saifi kutoka kwa babu yake Rabah Ibn Rabii ndugu yake Handhalah Al-Katib alimwambia kuwa alienda vitani pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, ambapo Khalid Ibn Al-Waliid alipokuwa mbele, Rabah na Masahaba zake Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. walipitia mwanamke ambaye aliuawa, wakasimama kumwangalia, wakashangaa hali yake, mpaka Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. alipowafuata akiwa amepanda ngamia wake, Masahaba wakaenda kando, Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. akasimama karibu naye, akisema: “Inakuwaje mwanamke kama huyu apigane vita”, akamwambia mmoja wao: “Mfuate Khalid, mwambie: usiwashambulie watoto wala waajiriwa wanaofanya kazi ambazo sio za kivita”.
Imamu Nawawi anasema katika Sharhul Imamu Muslim: “Wanazuoni wamekubaliana juu ya uharamu wa kuwaua wanawake na watoto kama hawakupigana vita”.
Tukifahamu kwamba sababu ya kupigana ni vita, basi kila asiyepigana anafuata yaliyotajwa katika Matini za Kisheria, kama vile; kipofu, mgonjwa, mwenye wazimu, mshamba, na mifano yao, hawa wote wanaoitwa “Raia” kwa istilahi ya kisasa, basi hairuhusiwi kuwadhuru, wala kuzipoteza mali zao, pia hairuhusiwi kuwaua, kwani kuwaua raia ni dhambi kubwa.
Miongini mwa makosa yao wanayohalilishia ufisadi wao ni: kupima suala la kuua watalii, wanawake na watoto na suala la kujikinga kwa maadui nyuma ya wasioruhusiwa kuuawa lililotajwa na Wanazuoni.
Upimaji huu ni mbovu; kwani tofauti iko wazi kati ya suala la kujikinga kwa maadui lilitajwa na Wanazuoni na suala ambalo watu hawa wanajitahidi kulitumia katika kuhalilisha shughuli zao za uhalifu, wakati wa vita ambapo maadui wanapojikinga nyuma ya wanawake, watoto, au Waislamu kwa ajili ya kuzuia mashambulizi ya majeshi ya Waislamu, hali hii ni ya dharura tu, hata hivyo, kama hakuna dharura ya kuwaua maadui wanaojikinga nyuma ya wasioruhusishwa kuuawa ni bora tusiwaue. Na dharura hii ina masharti yake yaliyoainishwa kwa uwazi na yaliyotajwa na Wanazuoni. Ama kulishambulia kundi la watalii wakiwa pamoja na wanaume, wanawake, na watoto na kuwaua kwa ujumla na kwa uhaini pasipo na kujikinga kwa maadui wala hakuna dharura ya kuwaua, basi kitendo hiki ni uadui mtupu. Katika suala hili hakuna kujikinga na maadui, wala hakuna maana yoyote ya kuzingatiwa, kama wakiwaacha wote wakiwemo wanawake na watoto, basi hali hii haitasababisha kuzuia Jihadi wala kuifanya iwe ni njia ya kushindwa kwa Waislamu. Wanazuoni wa Sheria wamelizungumzia suala la kujikinga kwa maadui nyuma ya Waislamu, kuwa kama kuna dharura tu, wakati wa vita, na hakuna uhusiano wowote kati ya maneno haya na yanayoenezwa na wajinga hawa.
Kwa kweli wale wanaofanya shughuli za kujitoa mhanga wanaichezea Dini, Sheria, na misingi yake iliyoimarishwa, wanategemea makosa ya kifiqhi, kuwavuruga watu, pamoja na ujinga wa wazi wa kutoijua misingi ya kutoa dalili na kuchagua kati ya dalili za kisheria, na wanafuata matamanio katika kufahamu Sheria kwa masharti yake na pasipo na masharti kinyume na walivyofuata Wanazuoni wa Sheria. Fikra zao ni mbovu, zimepotoka na wanajitahidi kuzitumia ili kuhalilisha umwagaji damu, na fikra zao hizo zinalindwa na Sheria ya Kiislamu.
Ingawa kuna madai mapana ya Jihadi na Usambazaji wa shutuma za jeuri juu ya wanaopinga katika maoni, matokeo ya vitendo vya madhalimu hawa ni kuanguka kwa nchi za Kiislamu chini ya utawala wa ukoloni wa kijeshi, kuwajaza Waislamu kwenye makaburi na jela wakiwa hawana dhambi yoyote, na vitendo vyao hivyo viovu vinaimarisha maslahi ya maadui wa Umma wa Kiislamu. Vitendo hivi vilileta maafa na misiba iliyosababisha vifo vya mamia ya maelfu ya Waislamu. Kusema kuwa wanatetea Waislamu ni dai la uongo, bali wanawaua Waislamu na kuwatoa katika makazi yao kama wanavyofanya wasio Waislamu, nao hawakumzuia adui na Waislamu kwa mujibu wa dai lao hilo la Jihadi, bali waliuleta uadui wa mataifa ya Waislamu na wakapata uadui wao, mpaka udhaifu wa Umma ukazidi kutokana na vitendo vyao.
Ukweli ambao Waislamu hawawezi kuukanusha, ni kwamba hawa ni wazushi, madhalimu, na wenye matamanio, na haichukukuwi Elimu yoyote kutoka kwa watu wa aina hii, kwani wao ni wazushi na wenye matamanio, na wanaenda kinyume na itikadi za watu wa Sunna, na hasa kwa kuutia uzushi wao, matamanio yao, wanayoyapigania. Ni lazima watawala Waislamu wamrejeshe mjinga asiyebeba silaha kwa akili yake kwa hekima na kauli njema. Ama kuhusu mtu aliyebeba silaha huyu anaendelea kuwa dhalimu mpaka ashindwe, Uislamu na Waislamu waepukane na shari zake.
Kutokana na maelezo yaliyotangulia katika swali hili: inajulikana kuwa viza ni sawa na mkataba wa amani inayolazimisha kuwepo kwa amani kwa pande mbili, na hairuhusiwi kuivunja ahadi hii wala kuzifanyia uhaini kutoka pande mbili hizi, na kwamba Jihadi ni faradhi isiyotetereka na itaendelea kuwepo mpaka Siku ya Kiyama, na kwamba kulinda mipaka, kuhifadhi mianya na kuhifadhi nguvu za Ulinzi wa majeshi ni faradhi ya Kutoshelezeana na ni jukumu la wanavyoona kufanya kwa mujibu wa uwezo wao, na kwamba kufanya hivyo inaondosha sifa ya faradhi isiyokuwepo kwa Jihadi. Hata kama kuna kasoro katika Jihadi kutoka kwa Watawala Waislamu, basi shughuli za uhalifu zinazoangamiza nchi kavu na ya kijani hazihalalishwi kwa hali zote, na kwamba ulinganiaji wa Uislamu ukiwezeshwa na ukawa hauzuiliwa, basi hakuna haja ya kupigana vita, na kwamba vitendo vya ulipuaji wa mabomu na shughuli za kujitoa mhanga zinazowakusudiwa wasio Waislamu wanaozuru nchi za Waislamu kwa lengo lisilo la kivita au katika nchi zao tulizoingia kwa viza, vitendo hivi ni haramu, na ni uvunjifu wa ahadi, na uhaini ambao hauna uhusiano wowote na Uislamu, navyo si miongoni mwa Jihadi Takatifu au vita iliyoruhusiwa katika Uislamu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.
Ofisi ya kutoa Fatwa

 

 

 

 

Share this:

Related Fatwas