Haki za Binadamu.
Question
Je, kuna dhana maalumu yoyote ya Haki za Binadamu katika Uislamu? Na ni upi msingi wake wa kifalsafa ikiwa Dhana hiyo ipo? Na kuna uhusiano gani baina yake na Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu na yaliyofuatia kutokana na Maazimio na Mikataba mbalimbali? Na je, hali ya Waislamu siku hizi inazingatiwa kuwa ni hoja juu ya Uislamu katika nyanja hizo?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wafuasi, na baada ya utangulizo huo:
Leo hii, Suala la Haki za Binadamu limekuwa ni miongoni mwa maudhui zinazoongoza katika vipaumbele vya Jamii ya Kimataifa na kuna mitazamo mingi ndani yake na kutofautiana kwa wingi jambo ambalo linazishawishi akili na kufungua nyanja za uchupaji mipaka na mambo ya udanganyifu.
Suala la Haki za Binadamu, kwa baadhi ya makundi mbalimbali, na baadhi ya pande mbalimbali, limekuwa kama lango la kuichafua sura ya Ulimwengu wa Kiislamu na kuleta madhara ya Utambulisho wa Waislamu, bali hata kuugusa Uislamu wenyewe na kuitia dosari Sharia yake. Na inatosha sisi kuyarejea mambo ya fasihi ya kisasa inayozungumzia haki za binadamu na Historia yake na ilianza lini, tunakuta makubaliano yanayoonekana kama ni ya wengi kwamba ilianza Majnakarta mwaka wa elfu moja mia mbili, kumi na tano (1215), iliyotolewa baada ya mapinduzi ya watu dhidi dhulumu ya Mfalme wa Uingereza na waraka wa haki uliotolewa mwaka wa elfu moja mia sita, ishirini na sita (1628), na Azimio la Haki za Binadamu lililotolewa mwaka wa elfu moja mia sita, thamanini na sita (1686) nchini Uingereza pia, halafu Tangazo la Uhuru nchini Marekani mwaka wa elfu moja mia saba, sabini na saba (1776), halafu Azimio la Haki za Binadamu na Raia lililotolewa baada ya mapinduzi ya Kifaransa mwaka wa elfu moja mia saba, thamanini na tisa (1789), na kadhalika hadi inafikia Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu lililotaolewa mwaka wa elfu moja mia tisa arobaini na nane (1948). [Dhana ya Haki za Mwanamke na Uhusiano wake na Haki za Binadamu, kwa mwandishi Haadi Mahmoud, Taarifa katika Gazeti la Mazungumzo ya Kistaarabu, toleo la mia nne, kumi na tisa (419) Uk. 3]
Na kama kwamba kuzilinda Haki za Binadamu na Kumtambua na kuutambua utukufu wake hakukuzalika wala kuiona nuru isipokuwa katika nchi za Magharibi, ni Magharibi peke yake bila ya kuutambua Umma mwingine au ustaarabu wowote kuwa na mchango katika upande huu na hasa Umma wa Kiislamu na hiyo si sahihi. [Uislamu na Haki za Binadamu, Dkt. Mohammad Emarah Uk. 4, miongoni mwa mfululizo wa vitabu vya Alam Al Maarifah namba 89].
Ambapo Uislamu ndio Ustaarabu pekee ulioleta maana iliyo kamili ya Haki za Binadamu. Na inatosha tukauchunguza mtazamo wa Uislamu kwa Mwanadamu, Mtazamo ambao unazingatiwa kuwa ni kiungo muhimu sana cha akili ya Mwislamu unaotokana na Msingi wa Mwislamu kwa Ulimwengu huu, kwani mwislamu ameona ulimwengu unamtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake.} [AL ISRAA 44]. Na ameona ulimwengu wote ukimnyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na mimea yenye kutambaa, na miti, inanyenyekea} [AR RAHMAAN 6]. Kwa hiyo mtu mwaminifu anamwona kwamba mwanadamu ni bwana katika ulimwengu huo, na siye bwana wa ulimwengu, kwani Bwana wa ulimwengu ni Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama alivyosema Mtume S.A.W. katika Hadithi yake: "Hakika kwamba Bwana ni Mwenyezi Mungu Mtukufu" [Imepokelewa na An Nassa'iy katika kitabu cha As Sunan Al Kubra, na Al Baihaqiy katika kitabu cha Dala'il Al E'jaaz];
Kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu ameuumba Ulimwengu huu na akamuumba mwanadamu, akampa riziki na akampa uhai na akamfisha, na yeye ndiye bwana wa Ulimwengu huu, na kwa kuwa mwanadamu ndiye Bwana wa Ulimwengu huu amemjaalia sifa za kipekee na akampa akili na Elimu na akambebesha Amana ya Dunia hii. Na suala hili linatumika kama katika tamko la Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba} [AL ISRAA 70].
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akamwumba mwanadamu kwa umbo lilio bora kabisa {Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa} [AT TIIN 4]. Na akampulizia roho inayotokana naye: {Na nitakapo mkamilisha na kumpulizia roho inayotokana nami, basi muangukieni kwa kumtii} [Swwad 72]. Na akawaamuru Malaika kumsujudia: {Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipokuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri.} [AL BAQARAH 34].
Ibn Kathiir amesema katika maana ya Aya hiyo: "Na huu ni Utukufu mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenda kwa mwanadamu, na akauandalia kizazi chake" [Tafsiri ya Ibn Kathiir 80/1]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akamjaalia mwanadamu ni Khalifa katika ardhi kama katika kauli yake: {Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi),} [AL BAQARAH 30]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akampa mwanadamu elimu: {Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote,} [AL BAQARAH 31]. Na akampa amana kama katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na milima; na vyote hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanaadamu akaichukua} [AL AHZAAB 72].
Siyo hiyo tu, bali Mwenyezi Mungu Mtukufu amefanya vimtumikie vilivyomo mbinguni na ardhini: {Kwani hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni vilivyomo mbinguni na Ardhini} [LUQMAAN 20]. Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu pia: {Na akavifanya Jua na Mwezi kwa manufaa yenu daima dawamu, na akaufanya usiku na mchana kwa manufaa yenu.} [IBRAHIMU 33].
Kwa hiyo, zoezi la kudhalilishiwa huku limeijenga akili ya Mwislamu kwamba yeye ndiye Bwana katika Ulimwengu huu na kwamba yeye ndiye Mja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya Ulimwengu huu. {Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.} [ADH DHARIYAAT 56].
Na kwamba Mwislamu hamwangalii mwanadamu kama ni sehemu ya ulimwengu huu, kwani kuwa kwake mwenye kutukuzwa, amemjaalia akawa na upekee wa Sifa akiwa bwana juu ya kilele cha viumbe vyote vilivyo haina mimea pamoja na vitu vingine vyote na kwa ajili hiyo, amemjaalia mwanadamu akawa katika hali isiyofaa kutumia mifumo ya takwimu utekelezaji wake unaofanyika kwa vitu mbalimbali kama ni Maada tu. Na mwanadamu akawa katika hali isiyofaa kutumia mfumo huo, basi mwanadamu sio kipande cha mbao na wala sio tu pande la nyama; kwani mwanadamu anaumbika pia kwa kuwa na akili na moyo na roho na nafsi na viungo vinginevyo. Utangulizi huu unazingatiwa kuwa ni Falsafa ya Uislamu kumwelekea mwanadamu na ni mtazamo wa mwislamu kumwelekea mwanadamu kama mwanadamu huathiri moja kwa moja yale yanayolinganiwa na Mataifa mbalimbali kwa kile kinachoitwa haki za binadamu.
Na tunapozungumzia Haki za Binadamu, lazima tujue neno la Haki ambalo ni umoja wa (Hukuk), kwani maana ya haki katika lugha kama alivyosema Aj Jawhariy ni: "Haki ni kinyume cha Ubatili, na haki ni umoja wa mahaki" [Kamusi cha: Mukhtaar As Swahah, kidahizo cha: Haqaq]. Aj Jurjani amesema: "Haki ni kinyume cha Ubatili, Na kila Haki inakabiliana na Wajibu nayo ni hukumu inayoendana na uhalisia, na hili ni jina miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na haki ni kitenzi cha kuamrisha katika lugha ya Kiarabu, na mnyumbuliko wake pia ni kustahiki haki na haki nyingi, na mwisho ikawa haki na ikathibiti. [Kitabu cha: At Taarifaat Uk. 120, Ch. ya Dar Al Kitaab Al Arabiy, Na Kamusi ya Lisanu Al Arab kwa Ibn Mandhuur, Kidahizo cha: Haqaq].
Na Al Fairuz Abadi akasema: "Al Haqu: ni katika majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu au sifa zake, na ni jina la Qur'ani Tukufu, na dhidi ya batili, na ni Jambo lililopitishwa tayari, na Uadilifu, na Uislamu, na Mali, na Ufalme, na Uwepo, na Thabiti, Kweli, Mauti, na uthabiti wa maamuzi". [Al Qamuus Al Muhiitw, Kidahizo cha Haqaq]
Na katika Istilahi, maana ya Haki inaashiria kwa jumla ya vigezo ambavyo vinalenga upangiliaji wa mahusiano ya kibinadamu na kuweka usalama wa masilahi ya kibinadamu. Na imeelezwa kwa Maana yake kuwa ni: Ni masilahi yaliyopitishwa na Sharia ili yamnufaishe muhusika na afaidike nayo. Na Haki inaweza ikawa ni ya kupitishwa na iliyo thabiti kwa nidhamu au kanuni au sheria maalumu au azimio la kimataifa au makubaliano ya mwisho, [Kusoma katika risala ya haki kwa Ali Zein Al Abdiin kwa Hedar Adel, Taarifa katika Gazeti la An Naba' toleo la 63, Uk, 3]. Au hiyo ni kwa maana ya madaraka yaliyojengewa kisheria au kwa maana ya takwa ambalo mtu anawajibika kulitekeleza yeye au mwingine.
Na hivyo ndivyo tunavyoweza kusema kwamba Haki inafungamana na mkusanyiko wa Watu na maana zake na inaendelea kukua kwa kukua kwao, na kuendelea kuwa daima ni jambo maalumu la kijamii lenye jumla ya vigezo na sharia mbalimbali, nalo kwa hivyo sio msemo mtupu wa kibinadamu bali ni maneno ya kihistoria na muhimu sana kwa ajili ya kupangilia mahusiano ya kijamii.
Na kufuatana na vyanzo vya kiislamu tunajua kuwa Uislamu umempa mwanadamu kwa jumla –kama binadamu bila ya utofautisho baina ya rangi au jinsi wala dini- kundi la haki linamhifadhia mtazamo wa Uislamu tulioutaja hapo juu kwa binadamu, na haki hizo ni nyingi sana; haki za kisiasa, za kiuchumi, za kijamii, za kiutamaduni, na haki za familia, haki za mwanamke, haki za mtoto na nyinginezo.
Vilevile Uislamu katika mtazamo Wake wa Haki hizi haukuzizingatia tu kama Haki zinazofaa kwa mtu au kwa wote kwamba anaweza Mtu akaziacha zote au baadhi yake, bali ni katika mambo ya dharura na ya lazima kibinadamu, iwe Mtu mmoja au Watu wote, na hakuna uwezekano wowote wa Maisha ya binadamu bila ya uwepo wa Haki hizo, Maisha yanayostahili kuwa na maana halisi ya Maisha. Na kwa ajili hiyo, hakika sio tu kuzilinda haki ya mtu bali ni wajibu juu yake pia atapata dhambi ikiwa atazipuuzia – awe mmoja au Watu wote – ukiongezea na madhambi yanayomwandama kila mwenye kuzuia mtu katika kuyafikia mambo hayo ya lazima. [Uislamu na Haki za Binadamu Uk. 15]
Na haki inayokuja mwanzoni mwa orodha ya haki za binadamu ni haki ya kuishi kwani hiyo ni msingi wa Haki nyingine zote na inazitangulia zote, na bila ya haki hii basi haki nyingine zote zinakosa thamani yake. [Akida ya Haki za Binadamu, kwa Dkt. Ahmad Omar Buzqiyah, Uk. 47, Utafiti katika Jarida ya Masomo ya Kisharia ya Kilibiya, Toleo Na. 17]
Na tunaangalia umbali ulio wazi baina ya Tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu lililotolewa mwaka wa elfu moja mia tisa, arobaini na nane (1948) katika jambo hilo, ambapo mada yake ya tatu imetaja kwamba: "Kila Mtu ana haki ya Maisha na Uhuru pamoja na Usalama wake, na Uislamu umeweka wazi Ulezi wa Uislamu katika Haki za Binadamu na ukajaalia ulinzi wa maisha ya mtu ni jambo la wajibu kwa kila mtu na jamii na nchi pia, bali na kuziweka salama njia zote zinazotakiwa kwa ajili ya binadamu kama vile; chakula, madawa, usalama, na ukaamrisha kwa kutilia mkazo {Walamsiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa, ila ikiwa kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini}. [AL ANAAM 191]
Vilevile mwanadamu hatakiwi kujiua yeye mwenyewe au kusogelea vitu vinavyoweza kuyapoteza maisha yake na kuangamia, na akifanya hivyo atakuwa anastahiki laana ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na ghadhabu zake na ya jamii yake. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Walamsijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni} [AN NISAA 29].
Na mtu yeyote bila kujali nafasi yake au madaraka yake hana haki ya kumtoa Maisha mtu mwingine na yoyote atakaye fanya hivyo bila haki atakuwa amewaidhinisha watu wote wapambane naye kivita pamoja na Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye amejiwekea yeye peke yake sifa ya Kuhuisha na Kuua. Na kila mtu anaungana na mwenzake katika kuepusha mkono wa yoyote kumuua nduguye binadamu, kwani watu wote ni ndugu, na iwapo mtu mmoja atakusudia kufanya hivyo basi wote watakuwa makosani kwa kulikubali kosa hilo la mauaji lifanyike, na zingatia tamko jumuishi katika Kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote.} [AL MAIDAH 32].
Halafu ni kwamba Uislamu haukuweka Sheria ya mpaka wa Kisasi katika kuua isipokuwa ni kwa ajili ya kuilinda haki hiyo tukufu: {Mtakuwa nao uhai mzuri katika kulipiza kisasi enyi wenye akili, ili msalimike} [AL BAQARAH 179].
Pia Uislamu umewakana wanaowaua watoto wao kwa sababu ya ufakiri au kuogopa njaa. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Wala msiwauwe watoto wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni kosa kubwa}. [AL ISRAA 31]
Na wala sio maisha tu bali maisha huru na mazuri na kwa hivyo haijuzu kwa yeyote awaye kumtia mtu utumwani. Na katika Hadithi Tukufu: "Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: watu watatu Mimi ni mwenye kugombana nao siku ya Kiama, … miongoni mwao ni mtu aliyemuuza mtu huru na akala thamani yake". Pia Waislamu Wanachuoni wa Fiqhi wametaja kwamba kiasili, mtu aliye huru haiingizwi utumwani. [Kitabu cha: Fat-hu Al Aziz kwa Ar Raafi'y 263/11, Ch. ya Dar Al Fikr]
Na miongoni mwa yanayoihifadhi hadhi ya mwanadamu ni kukataa kuitana kwa majina ya kejeli kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala msivunjiane heshima, wala msiitane kwa majina ya kejeli} [AL HUJURAAT 11]. Kwa maana ya kwamba mtu asimwite mwenzake kwa namna inayomchukiza, iwe kwa majina au sifa yoyote, na vile vile ni haramu kumteta. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi} [AL HUJURAAT 12]. Na pia Uislamu umeharamisha kumdharau mwanadamu yoyote kwa ujumla kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao} [AL HUJURAAT 11] Bali Uislamu ukaita kwa kuhifadhi heshima ya mwanadamu hata baada ya kifo chake, Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema: "Kuvunja mfupa wa maiti ni kama kuuvunja wakati wa uhai wake". [Imepokelewa na Abu Dawud na Ibn Majah]
Na kwa kurejesha wepesi kwa Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu lililotolewa mwaka wa elfu moja mia tisa na arobaini na nane (1948), na linalozingatiwa na wengi kuwa ni mapinduzi na mhamo wa aina yake katika nyanja za haki za binadamu tunakuta kuna Haki tatu za Msingi; Undugu, Usawa na Uhuru. [Haki za Binadamu Baina ya Uislamu na Umoja wa Mataifa, kwa Sheikh Muhamad Al Ghazaliy Uk. 7].
Na Undugu, Uislamu uliutilia mkazo, hasa alipokuja Mtume S.A.W, na alipohama kutoka Makka kwenda Madina, aliweka undugu baina ya kabila la Ausi na Kabila la Khazraji, na Muhajiruun na Answaari; tajiri na fakiri wao, mwenye nguvu na mnyonge wao, ukianzia na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu} [AL HUJURAAT 10].
Qura'ni inauashiria Undugu wa wanadamu kwa ujumla ikisema; {Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliyemchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari} [AL HUJURAAT 13]. Basi wanadamu wote wanarejea kwa baba mmoja; naye ni Adamu na mama mmoja naye ni Hawaa, na Imamu Ali R.A. alikazia kauli hiyo katika wasia wake kwa Malik Al Ashtwar alipomtumia Wali wa Misri akasema: "Watu ni aina mbili; Ama ni ndugu yako katika dini, au mwenzako katika uumbaji". [Kitabu cha: Nahj Al Balagha wa Asanidah kwa Abduzahraa Al Huseiniy Al Khatwib 391/3]
Ama kwa upande wa Usawa: ni kulingana kikamilifu mbele ya sharia na kulingana kikamilifu katika fursa za ajira na kuwepo uuwiano baina ya wale ambao bahati zao zimetofautiana na fursa zilizopo. [Kitabu cha: Uislamu na Usalama wa Kijamii kwa Dkt. Mohamad Imarah Uk. 25, Ch. ya Dar As Shuruq, na Kitabu cha: Uislamu na Haki za Binadamu kwa Dkt. Khedher Uk. 11]
Na kwa kuanzia na Msingi wa Undugu wa Kiutu, tulioutaja hapo kabla, Uislamu umejenga uhusiano mtu na mtu mwingine kwa msingi wa Usawa halisi mbele ya Sharia mpaka Uadilifu utulizane na haki kuenea kwa wote na kuzifuta athari zake zote za dhuluma na ukandamizaji, hakuna ubaguzi baina ya mtu na mtu isipokuwa kwa uchamungu na matendo mema. Na hata uzingatiaji huu haumpi muhusika haki ya ziada dhidi ya mtu mwingine lakini unalazimisha jamii imjali na kumheshimu bila ya kujipendekeza au kupata kisichokuwa haki, Mtume S.A.W. amesema: "Hana mwarabu juu ya mwajemi, na wala mwajemi juu ya mwarabu ubora wowote, au mweusi juu ya mweupe au mweupe juu ya mweusi, hakuna yeyote aliye bora isipokuwa kwa uchamungu". [IImepokewa na At Twabaraniy katika Al Mu'jam Al Kabiir]
Na katika zama hizi, mapinduzi ya Kifaransa yalichangia kuinua Kiwango cha Usawa lakini majaribio ya kiutendaji yanamfundisha mwanadamu kwamba misingi peke yake ya kuinua hadhi ya haki za binadamu haitoshi, bila ya kuwepo kinachoyaainisha madhumuni, na kufungua njia ya utekelezaji wake na kuwajibisha adhabu kwa kukiuka, na hiki ndicho tunachokikuta katika Uislamu. Huu ni utatuzi wa kiasili kwa hukumu ya Sharia, na madhumuni yake ni maalumu na njia za utekelezaji wake ziko wazi na kuna adhabu pale sharia inapokiukwa, na hiyo ni adhabu ya kidunia na ya kiakhera. Na imetajwa kwamba Abu Dhari alimdharau Bilal kwa upande wa mama yake akimsema Ewe mwana wa mweusi! Na Mtume S.A.W, alipolisikia neno hilo baya alilikana kabisa kisha akasema: "Wewe ni mtu ambaye una Ujahili ndani yako". Abu Dhari akajutia na akalisikitikia tendo lake na maneno ya Mtume S.A.W, yalimwathiri mno katika nafsi yake na akalilaza shavu lake juu ya ardhi na akasema akimwambia Bilali: simama na unikanyage shavuni! Na Al Baihaqiy ametaja kisa hicho katika kitabu cha Shua'b Al Imaan. [Rejea kitabu cha: Haki za Binadamu Baina Uislamu na Umoja wa Mataifa Uk. 16]
Huo ni Usawa katika Uislamu, na hali za wanadamu zinapotofautiana na tabia zao, na nyakati zao zinapotofautia na pia mahali pao, na ipo tofauti katika jinsia, rangi, lugha, na yupo tajiri, fakiri, mwanachuoni, na mjinga, na kiwango cha kijamii na cha kiuchumi kinatofautia baina ya watu wakati huo. Jamii huweka vigezo vya kujikweza baina ya watu kutokana na uwepo wa tofauti mbalimbali, na hapana budi kuweka vigezo vya kujiona bora zaidi, kwani usawa halisi hauwi isipokuwa kwa utu wenyewe na tatizo huanzia pale vinapowekwa vigezo hivyo kwa namna ambayo inavuruga msingi wa Usawa katika uhalisia wa Usawa. Na hicho ndicho kinachoutofautisha Uislamu na zama mbalimbali, na nyaraka zinazohusiana na haki za binadamu ambapo Uislamu umeweka uchamungu kama ndicho kigezo cha Ubora wa Mtu na mtu mwingine. Kwa hiyo, Kigezo cha mtu kuwa bora hapa, kila Mtu anaweza kupanda daraja kwa kukitumia, na wala hakiwagawi watu wakawa matabaka mpaka mtu akawa juu ya mwingine. Hiki ni kigezo kinachowapandisha watu juu zaidi na zaidi na kumfanya mwanadamu awe kama mwanadamu, na Kigezo hicho kimemfanya awe bora zaidi kwa nafsi yake na jamii yake anayoishi nayo, na kwa hiyo Uislamu umeondosha vigezo vyote vya bandia ambavyo vilikuwa vimeenea katika jamii za kibinadamu. [Kitabu cha: Haki za Binadamu katika Uislamu kwa Abdulla Abdulmuhsen At Turkiy Ku. 34-44].
Ama Haki ya Uhuru, kama Uhuru huo utakuwa ni wa Kidini, Uhuru wa Kifikira, Uhuru wa Kiraia au Uhuru wa Kisiasa, basi hakika ni kwamba Uislamu umeutangulia Uhuru huo, na inatosha kuisoma mada ya kwanza katika Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu ambalo limesema: "Watu wamezaliwa huru, wenye usawa katika heshima na katika haki, na mada ya pili imesema: hakika kwamba kila mwanadamu anaweza kushika haki zake zote na uhuru wake wote, hakuna tofauti baina ya mtu na mtu mwingine."
Ama katika Uislamu, basi umemjaalia mlango wa Uhuru ukifungua wazi kabisa, basi katika Uhuru wa Kidini unamjaalia mwanadamu ni mwenye uhuru kamili katika kuchagua akida yake; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hapana kulazimisha katika Dini} [AL BAQARAH 256], Na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae, [AL KAHF 29] Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akaainisha kazi ya Manabii katika neno moja lenye balagha wazi katika kauli yake: {Haimlazimu Mtume ila kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnacho kidhihirisha na mnachokificha} [AL MAIDAH 99] [Rejesha kitabu cha: Uislamu na Haki za Binadamu kwa Sheikh Zakariya Al Biriy Uk. 15]
Imetajwa katika waraka wa Omar Bin Al Khatwab R.A. kwa watu wa Iliya; Akawapa amani kwa nafsi zao, mali zao, makanisa yao na misalaba yao… "Ni kwamba makanisa yao yasikaliwe wala yasivunjwe na wala kisiharibiwe chochote ndani yake, au mali iliyopo, wala msalaba wake usiguswe na kisiguswe chochote katika mali zake, na wala waumini wake wasilazimishwe chochote kinachoikiuka Dini yao na yeyote miongoni mwao asidhuriwe". Na imetajwa kama hivyo katika mkataba wa Omar R.A, kwa watu wa Misri. [Kitabu cha: Uislamu na Haki za Binadamu kwa Sheikh Zakariya Al Biriy Uk.26, na Kitabu cha Haki za Binadamu katika Uislamu kwa Rashed Al Ghanushiy Uk. 4]
Ama Uhuru wa Kifikira: Endapo Uislamu umejenga Itikadi sahihi juu ya mtazamo katika ulimwengu kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu} [AL ANKABUUT 20] Na kauli yake Tukufu: {Sema: Mimi nakunasihini kwa jambo moja tu –ya kwamba msimame kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wawili-wawili na mmoja-mmoja; kisha mfikiri} [SABA 46].
Na mara nyingi tunaona katika Qur`ani Tukufu Aya zinazotutaka tufikirie, tutumie akili, au tuzingatie jambo ambalo tunalifanya, kufikiria kuwe ni lazima katika Uislamu na wala sio tu uchangamfu wa akili peke yake.
Kama ambavyo unazuia kufuata kile ambacho mtu hana ujuzi nacho, na wala hana uwezo wa kukiwekea dalili, na unawatia kasoro wenye kuwafuata wengine hata kama baba zao wangelikuwa hawajui kitu wala hawana mwongozo wowote au Kitabu chochote kinachowaangazia njia. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa}. [AL ISRAA 36] Na hiyo haihusu mlango wa Akida, bali katika mlango wa rai na Itikadi, tunamkuta Imamu Aba Hanifah akisema: "Hiyo ni rai ya Abu Hanifah, Nayo ni bora tuliyokadiriwa na Mola, na yeyote atakaye tujia na kheri basi huyo atakuwa bora zaidi ya kupatia. Na Imamu Maliki anasema: Mimi ninakosea na ninapatia. Basi iangalieni rai yangu, ikiafikiana na Sunna basi ichukueni. Na ikiwa haitaafikiana na Sunna, basi iacheni. [Uislamu na Haki za Binadamu kwa Sheikh Zakariya Al Biriy Uk.24]
Uislamu ulikuwa na Shime pia katika Uhuru wa kiraia kwamba mtu awe na uhuru wa kujifanyia mambo yake binafsi na kifedha na wala asikabiliane na utumwa wa aina yoyote dhidi yake ambao utamkosesha Uhuru wake wa kujiamulia na hatakuwa na Uhuru wa kujichukulia hatua yeye mwenyewe. Uislamu umempa kila mtu uongozi wa kujiongoza akawa anamiliki mali na anarithi, anauza na kununua, anaweka rehani, analea, anatoa, na anaweka wakfu anaishi na anafanya atakavyo, na anatoa. Na hivi ndivyo ilivyo katika kila jambo linalomletea masilahi yake binafsi au ya wote. [Uislamu na Haki za Binadamu kwa Sheikh Zakariya Al Biriy Uk.46, na Haki za Binadamu baina ya Uislamu na Umoja wa Mataifa kwa Sheikh Muhamad Al Ghazaliy Uk. 84]
Na msimamo wa Uislamu katika utumwa na juhudi yake ya kuumaliza na kukausha vyanzo vyake ni wazi kabisa kwa kila mwenye akili na mwenye uadilifu. [Kitabu cha Uislamu na Haki za Binadu kwa Dkt. Muhamad Imarah Uk. 17]
Pia Uislamu umeshughulikia Uhuru wa Kisiasa na ukajaalia kwa kila mwanadamu haki ya kupata wadhifa wa kiidara, mdogo au mkubwa hata Urais wa nchi na pia ana haki kushiriki kutoa rai yake pasipo kitisho au hofu. hakika Mtume S.A.W. ameamuru kushauriana, bali iko Sura katika Qur`ani inaitwa Ushauri (As Shura) imetaja kuwasifu waumini kwamba jambo lao ni kushauriana baina yao.
Uislamu umeushughulikia Uadilifu kwa Kiwango kikubwa na ukampa kila mtu bila ya kujali nafasi yake ya kijamii au cheo chake, haki ya Uadilifu na ukaamrisha utekelezwaji wake wazi wazi. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Hakika Mwenyezi Mungu Anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani. [AN NAHL 90] Siyo hiyo tu, bali Uislamu umekana kwamba uadui au hitilafu imekuwa katika akida au rai ni sababu ya kuharibu uadilifu. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu, Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu} [AL MAIDAH 8].
Kutokana na hayo, basi dhana ya Haki za Binadamu katika Uislamu zilikuwa wazi kabisa kama uwazi wa mchana, na pia zimejipambambanua zaidi kuliko matangazo, ahadi na mikataba ya kimataifa kwa faida kadhaa; miongoni mwazo:
Ya kwanza: Kwa upande wa kutangulia na kuwajibika ambapo imepitiwa na zaidi ya karne kumi na nne na nyaraka za kimataifa ni zao la zama hizi mpya. Vilevile haki za binadamu katika nyaraka za kimataifa ni kama nyasia na maazimio au hukumu za kukanya, wakati ambapo katika Uislamu ni faradhi yenye dhamana ya kutokea Malipo ambapo Madaraka ya Serikali Kuu ina haki ya kulazimisha utekelezaji wa faradhi hiyo.
Ya Pili: Na kwa upande wa undani wake na ujumuishaji kwani mzizi wake ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Sunna ya Mtume wetu S.A.W. Ama kwa upande wa chanzo cha Haki katika Kanuni na Nyaraka ni fikra ya kibinadamu, na wanadamu wanakosea zaidi kuliko kupatia na wanaathirika zaidi kwa maumbile yao ya kibinadamu ukiwemo unyonge, mapungufu na kushindwa kuyatambua Mambo, bali mara nyingi humili upande wake, vile vile katika Uislamu, inazikusanya haki zote.
Ya Tatu: Kwa upande wa Ulinzi, ni dhamana mbalimbali ambapo hizo katika Uislamu ni sehemu ya Dini zimekuja katika Hukumu za Mwenyezi Mungu Mtukufu na ni za kufuatwa na watu. Zina utukufu wake unaozuia zisichezewe na kuzifanya ziwe Amana kwa kila muumini. Kuwa kwake haki za binadamu zinawakilisha Akida na mwenendo wa kimaumbile kwa mwanadamu, hii ni dhamana pekee ya kuziheshimu Haki hizo.
Bali hakika Uislamu una mazuri mengi juu ya haya kwamba haukikatai kitu chochote chenye masilahi kwa binadamu na chenye kumletea furaha kidini na kiakhera bali kinyume na hivyo, Uislamu unaharakisha katika kushiriki ndani yake na kwa hiyo, Jamii ya Kimataifa ilipohangaikia ukombozi wa Watumwa na kuufuta utumwa huo: Waislamu walikuwa wa kwanza kusaini mkataba wa kuuharamisha utumwa kwani walifahamu kutoka kwa Mtume S.A.W. alipozungumzia mkutano katika nyumba ya Ibn Jada'an ambapo Makuraishi walikutana na wakaahadiana kumnusuru aliyedhulumiwa alipo sema: Mimi nikiitwa kuhudhuru mkutano kama huo katika Uislamu basi nitakubali. [Imepokelewa na Al Baihaqiy katika kitabu cha As Sunan]
Kwa hiyo, Waislamu walikubali, Mikataba yote na nyaraka za kimataifa ambazo zinahimiza kuheshimiwa kwa Haki za Binadamu si lolote isipokuwa baadhi ya Makatazo ya baadhi ya vipengele vya vifungu mbalimbali ambavyo ni matawi tu na ambavyo haviafikiani na sharia ya Uislamu.
Vilevile tunalazimika kukumbusha kwamba Waislamu sio hoja ya Uislamu ambapo Hukumu za Uislamu hazijulikani kupitia mwenendo wa kivitendo wa baadhi ya Waislamu na hasa hasa katika zama za Ujinga, Unyonge, Mgawanyiko, kuathirika na Kuibua hisia kali kwa jinsi maadui zao wanavyowatendea na kuwapiga vita vinavyowatoa katika usahihi wao na Heshima ya Dini yao.
“Na wala siuzingatii sana wakati wa baadhi ya Waislamu walipoenda kinyume na Hukumu hizi pale unyonge ulipoanza kujitokeza katika umoja wao na kubanwa vifua vyao kutokana na ukawaida wa mnyonge, na hilo ni katika mambo yasioambatana na maumbile yao na wala hayachanganyiki na maumbile yao. [Kitabu cha: Uislamu na Ukristo Uk. 20 na Kitabu cha: Uislamu na Haki za Binadamu kwa Sheikh Zakariyah Al Biriy Uk. 10]
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.