Haki za Binadamu Zinazoendana na Makusudio ya Nafsi.
Question
Je, Haki nini za binadamu katika Uislamu zinazoendana na makusudio ya nafsi katika Usawa?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wafuasi, na baada ya utangulizo huo:
Watu wote wanarejea kwenye asili moja, kisha ni lazima wawe sawa katika thamani ya ubinadamu, watu wote wanarejea kwa Adam A.S. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutokanafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwake mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukuangalieni}( ).
Na Adam asili yake inarejea kwenye udongo kwani Mola Anasema: {Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam, Alimuumba kwa udongo kisha Akamwambia: Kuwa! Basi akawa}( ).
Na katika hili anasema Mtume S.A.W.: “Nyinyi nyote mnatokana na Adam na Adam anatokana na udongo”( ).
Ikiwa wanadamu katika asili wapo sawa hivyo hakuna mizani ya ubora isipokuwa ni kwa matendo ambayo hufanywa na kila mmoja miongoni mwao: {Na wote watakuwa na daraja zao mbali mbali kwa waliyoyatenda}( ).
Ni lazima kwa mtu kumcha Mwenyezi Mungu kwenye matendo haya anayoyafanya. Mola Anasema: {Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na Tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliyemcha-Mungu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari} [AL-HUJRAAT: 13].
Ikiwa watu wapo sawa katika thamani ya ubinadamu hivyo haifai mwanadamu kufikwa na hatari au madhara kwa zaidi ya vile wanavyofikwa nayo watu wengine, kwa sababu “Waislamu damu zao zipo sawa”.
Ikiwa hali ipo hivyo, basi wala hakuna sababu wala mfumo wa kutenganisha watu kwa misingi ya rangi au taifa au kabila au lugha au dini, na tofauti yoyote ya sura hii inakuwa ni yenye kwenda kinyume, na yenye kubomoa msingi wa usawa ambao umepitishwa na Uislamu wa mfumo wa kati na kati.
Katika Hadithi Takatifu Mtume S.A.W. anasema: “Mwenye kuchelewa kwa matendo yake, basi nasabu yake haitamharakisha”( ).
Hivyo si kwa misingi ya utaifa au ukoo mwanadamu anakuwa na sifa ya kipekee.
Ikiwa watu mbele ya Uislamu wapo sawa katika thamani ya ubinadamu hivyo ni lazima wawe sawa katika utekelezaji wa Sheria ya Mwenyezi Mungu kwao, hakuna yeyote wa kuvuliwa katika hilo kwa nafasi yoyote aliyo nayo, au utukufu wake, au utajiri wake au heshima yake na nasaba yake, kwani watu mbele ya utekelezaji wa Sheria na kanuni zake ni sawa, kwa hili amesema Mtume S.A.W. kumwambia mtu ambaye alikuwa akiomba kwa Mtume kuondolewa adhabu mwanamke mmoja wa kabila la Ban Makhzuom ambaye aliiba na akasema: “Hivi unamuombea kuondolewa hukumu ya adhabu katika hukumu za adhabu za Mwenyezi Mungu? Fahamu wameangamia watu waliokuwa kabla yenu kwa sababu walikuwa pindi anapoiba miongoni mwao mtu mwenye heshima walikuwa wanamwacha, lakini akiiba miongoni mwao mtu mnyonge wanamhukumu adhabu. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu lau Fatuma Binti Muhammad ataiba, basi nitamkata mkono wake”( ).
Sheria ya Uislamu inamlinda mtu mwenye heshima mwenye mamlaka na wale wasio na sifa hizo, na inamlinda mtu tajiri na masikini, inamlinda mwenye nguvu na mnyonge sawa kwa sawa, haitofautishi kati ya mwanadamu na mwengine, kwa sababu ni Sheria inayomheshimu mwanadamu vyovyote atakavyokuwa mwanadamu huyu, na katika hili anasema Sahaba Abu Bakr As-Swidik R.A. katika hotuba yake pindi aliposhika ukhalifa: “Fahamuni kuwa mnyonge wenu kwangu mimi ndio mwenye nguvu mpaka nimpatie haki, na mwenye nguvu zaidi kwenu kwangu mimi ndio mnyonge mpaka nichukue haki kwake”.
Maadamu watu wapo sawa katika thamani ya ubinadamu, na mbele ya utekelezaji wa Sheria kwao pasi na kuondolewa yeyote na kuwalinda kwa Sheria hiyo, hivyo inalazimisha kuwa sawa katika haki ya kunufaika na vyanzo vya mali ya jamii kupitia uwiano wa nafasi za kazi, kwani kila mwanadamu anapaswa kuchukua fursa yake katika kazi kama anavyochukua mtu mwingine nafasi yake, na hasa vyanzo vya mapato Mwenyezi Mungu Amegawa kwa wote, kwa kauli yake: {Basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katikariziki zake}( ).
Ikiwa juhudi zinazochukuliwa ni moja, na kazi inayopelekea juhudi hiyo ni moja kwa upande wa idadi na namna, hivyo haifai kutofautisha kwenye malipo kwa mwanadamu na mwingine, kwani Mola Mtukufu Anasema: {Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona! Na anaye tenda chembe ya uovu atauona!}( ).
Hivyo basi hakuna maana kabisa ya mwanadamu kuchukua malipo zaidi ya mwanadamu mwingine anayefanya kazi hiyo hiyo, kama inavyofanyika wakati mwingine ndani ya baadhi ya nchi kwa sababu za ubaguzi wa rangi au wa kidini.
Hii ndiyo haki ya usawa ambayo Uislamu umetangulia tangazo la haki ya binadamu( ) ambalo limepitishwa na Umoja wa Mataifa na imekuja kwenye tangazo: “Kila mtu ana haki kutumia haki zote pamoja na uhuru vilivyo ainishwa kwenye tangazo hili pasi na kutofautisha au kubagua kwa aina yoyote, kama vile kubagua kwa sababu za ukoo, au rangi, au utaifa, au lugha, au dini, au mtazamo wa kisiasa, au mitazamo mengine, au asili za kabila, au za kijamii, au za mali, au watoto au visivyokuwa hali hizo”( ).
Usawa katika Uislamu una Sura Nyingi:( )
1. Usawa mbele ya Sheria:
Inaonesha wazi katika maelezo yaliyotangulia kuwa hakuna ubaguzi na tofauti ya matabaka ya kijamii mbele ya Sheria, kwani wote hao wanafuata Sheria moja ikiwa ni pamoja na kiongozi mkuu mwenyewe, kwani Sheria ya Kiislamu haitambui ulinzi wa yeyote mbele ya Sheria, kama vile haihusishi mtu au kundi kuwa na Sheria inayotofautiana na kinachotekelezwa kwa Waislamu wengine, kwani msingi ni umoja wa Sheria.
Utekelezaji wa msingi huu Mtume S.A.W. na Makhalifa waliokuja baada yake walifuata hukumu za Sheria na kuzitekeleza kwa kuanzia wao wenyewe.
Kwani Mtume S.A.W. wakati wa kuumwa kwake alitoka akiwa na Fadhl Ibn Abbas na Ally Ibn Abi Talib na kukaa juu ya mimbari kisha akasema “Enyi watu, kama yupo ambaye niliwahi kumchapa mjeledi mgongoni kwake basi mgongo wangu leo huu hapa na aje kulipiza, na kama yupo niliyewahi kumtukana na kumvunjia heshima yake basi leo na aje heshima yangu hii alipize, na kama yupo niliyewahi kuchukua mali kwake basi hii mali yangu na achukue, kwani mtu anayependeza sana kwangu ni yule mwenye kuchukua haki yake kwangu akiwa anayo haki hiyo, ili niweze kukutana na Mola wangu nikiwa na nafsi safi”, kisha Mtume S.A.W. akateremka na akasali Sala ya Adhuhuri kisha akarejea nyumbani kwake na kurudia maneno yake( ).
Mtume S.A.W. alijiwa na Amirah Al-Makhzuomiya ambaye aliiba na kutakiwa afanyiwe hukumu ya wizi baadhi ya Masahaba walitaka kumwombea kwa sababu alikuwa bado ni mgeni katika Uislamu, na wakamtuma Sahaba Usama Ibn Zaidi katika hilo ndipo Mtume S.A.W. alipokasirika sana na kusema kumwambia Usama “Hakika waliangamia waliokuwepo kabla yenu, walikuwa pindi anapoiba mtu mwenye kuheshimika huwa wanamwacha, na akiiba miongoni mwao mtu mnyonge, basi wanamtekelezea hukumu ya wizi. Ni naapa kwa Mwenyezi Mungu lau Fatuma binti Muhammad ataiba, basi nitamkata mkono wake”( ).
Vilevile kiongozi au Khalifa Abu Bakr na waliofuata baada yake akiwemo kiongozi mkuu wa Waumini Umar Ibn Al-Khattab wote hao walikuwa wanasimamia usawa wao wenyewe, kwani siku moja Umar aliwahi kumpiga mtu na yule mtu akamwambia Umar: Hakika nilikuwa mmoja wa watu wawili, ima mtu mjinga mwisho akafahamu au alifanya makosa akasamehewa, akasema Umar: Umesema kweli, wasiokuwa wewe basi wafuate( ). Hivyo Sahaba Omar alikuwa anatoa shime kubwa ya kusisitiza usawa mbele ya Sheria.
Kwani Umar alibomoa ubaguzi mbele ya Sheria kati ya kiongozi na mwenye kuongozwa pale alipotoa amri ya kulipiza kisasi kwa mmoja wa Mkoptiki wa Misri kwa mtoto wa Amr Ibn Al-‘As pindi mwanawe alipompiga, kama vile aliwataka watu wa majimboni kufahamu wanayoyapitia kutoka kwa viongozi wao ili kulipiza kisasi kwao( ) na hilo alikataa kukubali sifa yoyote ya kipekee kuwa nayo kiongozi kwa raia.
2. Usawa mbele ya Mahakama:
Mfumo wa Uislamu unakaribia kuwa ndio mfumo pekee ambao haumuondoi yeyote vyovyote alivyo kufikishwa mbele ya Mahakama hata akiwa ni Khalifa kwa maana ya kiongozi mkuu wa nchi, ni sawa sawa akiwa ameshawahi kuhukumiwa yeye mwenyewe au kuhukumiwa kwa sifa yake, kama vile kwenye Uislamu hakuna jambo linalozuia kuhukumiwa kimahakama, katika hili kuna usimamizi wa dhati wa uadilifu katika Uislamu wenye sifa ya pekee dhidi ya mifumo mingi ya kisasa ambayo huzuia kufikishwa Mahakamani au kuhukumiwa na Mahakama Rais wa nchi au Mawaziri au kuanzishwa Mahakama maalumu kwa ajili ya kusikiliza kesi zao, vilevile Mahakama inazuiliwa kuangalia baadhi ya matendo na hatua zingine( ).
Katika Uislamu kumefanyika hatua za hukumu kwa Makhalifa na wasimamizi wa majimbo sawa na zilivyofanyika hukumu hizo kwa watu wengine mbele ya hakimu( ) miongoni mwa hayo ni Khalifa Ally Ibn Abi Talib alipoteza ngao na akaikuta kwa Myahudi akidai kuwa ni miliki yake akamwambia: Kati yangu mimi na wewe kuna hakimu Mwislamu hivyo atatoa hukumu kati yetu kwenye hii ngao, hakimu akatoa hukumu kwa masilahi ya Myahudi kwa sababu yeye ndiye anayeishikilia ngao na kushikilia ndio kibali cha umiliki( ).
Kiongozi Umar Ibn Al-Khattab aliwahi kuchukua farasi kutoka kwa mtu na kumbebesha mizigo na mwenye farasi akamkasirikia Umar, akasema Umar: Mlete mtu asimamie kati yangu mimi na wewe, yule mtu akasema mimi ninaridhia watu wa kutoka upande wa Iraq. Akasema huyo mtu wa Iraq kumwambia Umar: Umemchukua akiwa mzima basi jukumu lako kuhakikisha unamrudisha akiwa mzima na salama, ndipo Umar alilipa thamani ya mnyama kwa yule mtu kisha akamteua yule mtu wa Iraq kuwa jaji( ).
Kuna kundi la watu walimshitaki Khalifa Al-Mansour kwa hakimu Muhammad Ibn Umar At-Talahy ndipo hakimu alituma ujumbe wa kumwita Khalifa, naye Khalifa aliitikia wito na kuhudhuria kikao cha mashitaka yake, baada ya kuhudhuria mlalamikaji ndipo hakimu alisikiliza maelezo ya pande zote mbili zenye mvutano mwisho alitoa hukumu dhidi ya Khalifa, baada ya Khalifa kurudi alitoa amri ya kumwita hakimu baada ya kuondoka kwenye kikao chake na baada ya kufika mbele ya Khalifa ndipo aliposema kumwambia hakimu: Mwenyezi Mungu Akulipe kutokana na dini yako na Mtume wako na kwa Khalifa wako malipo yaliyokuwa mazuri( ).
Ndiyo hivyo, Waislamu walitekeleza msingi wa usawa kwenye Mahakama kwa utekelezaji ambao hatuoni mfano wake kwenye mfumo wowote, huenda utekelezaji huu unaonekana wazi katika katiba ya Mahakama ambayo aliiweka Umar Ibn Al-Khattab katika wasia wake ambao alimuusia Aba Musa Al-Ashaarii pindi alipompa jukumu la usimamizi wa Mahakama.
Kwa msingi wa katiba hii, hivyo haifai kwa hakimu kutofautisha kati ya pande mbili zenye kuvutana katika mtazamo wake akamkubalia huyu na kumkatalia mwingine, wala katika kikao chake akaangalia upande mmoja na upande wa pili akaupa mgongo, wala katika utoaji wake wa hukumu akaegemea kwa mgomvi mmoja dhidi ya mgomvi mwengine.
3. Usawa kwenye Nyadhifa za Umma:
Uislamu umekuja katika kusimamia nyadhifa bila ya kutenganisha kati ya kundi na kundi lingine, au wadhifa na wadhifa mwingine, wala haujapendelea kwa yeyote wala kumwathiri Mwarabu dhidi ya asiyekuwa Mwarabu, kwani watu wote wapo sawa katika kushika wadhifa wa Umma kwa mujibu wa kutosheleza kwao elimu yao pamoja na uwezo na wala si kwa sababu nyengine( ).
Wala haina maana ya usawa ni kuwa sawa kati ya msomi na mjinga aumwana stadi na mvivu bali ukweli kufikiwa kwa usawa ni pale panapokuwa na usawa katika vigezo jambo ambalo leo linaelezewa kama usawa wa KiSheria, na wala sio usawa wa kihesabu. Mola Mtukufu Anasema: {Sema: Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale wasio jua?}( ).
Katika hilo pia anasema Mtume S.A.W. kumwambia Abi Dharr pindi alipomtaka ampe kazi: “Hakika wewe ni dhaifu na hii kazi ni amana siku ya Kiyama ni udhalili na majuto isipokuwa kwa mwenye kuichukua kwa haki yake”( ).
Na Mtume S.A.W. aliwapa baadhi ya Masahaba kazi za usimamizi wa mambo ya Waislamu kama vile alivyompa Sahaba Bilal na Zaid Ibn Haritha aliiongoza Madina kwa niaba yake wakati alipotoka kwenda vitani na wala hakukuwa na mazingatio yoyote ya kutokuwa kwao Waarabu( ).
Kama vile Usama Ibn Zaid alishika uongozi wa jeshi kwa sababu Mtume alikuwa anaangalia watu wenye uwezo zaidi kwenye wadhifa huo, na pindi Umar Ibn Al-Khattab alipopinga Msikitini amri ya Suhaib Ar-Rumy kuongoza watu naye akiwa ni katika waliachwa huru na utumwa na wala si Mwarabu.
Na kutoka kwa Umar pia aliwahi kusema wakati wa kupendekeza kwake watu sita ambao wanaweza kushika Ukhalifa baaada yake: Lau angelikuwepo Salim, basi ningemteua.
4. Usawa katika Kutoa:
Mfumo wa Uislamu umekuwa na sifa ya pekee ni kwa sababu wenyewe ni mfumo wa aina yake katika ulimwengu ambao umelazimisha kila mtu nchini kuwa na haki katika mali ya hazina kuu, tokea kuzaliwa kwake mpaka kufa kwake ambapo jambo linalofahamika katika mfumo wa kisasa ni kuwa nchi hailazimishi katika mali ya hazina kuu mishahara isipokuwa ni kwa wafanya kazi na wale wasiokuwa na uwezo wa kufanya kazi( ). Katika hilo anasema Umar Ibn Al-Khattab: Ni naapa kwa Mwenyezi Mungu Ambaye hakuna Mola wa haki isipokuwa ni Yeye, hakuna mtu yeyote isipokuwa ana haki katika hazina hii kuu iwe amepewa au hajapewa( ).
Uislamu wala hautenganishi kati ya watu katika haki hizi hivyo hapewi mtu na kunyimwa mwingine, wala kutofautisha kati ya mwanamume na mwanamke, au kati ya Mwislamu na mtu Dhimmiy, kwa hakika tumeona kuwa Umar Ibn Al-Khattab alimchukua Myahudi masikini na kumpeleka kwenye hazina kuu na kuwaambia wafanya kazi wake: Mpeni fungu yeye na wa mfano wake kutoka hazina kuu( ).
Khalifa Abu Bakr pindi alipo lazimisha kwa Waislamu mafungu yao, alimpa kila mtu ambaye Mtume S.A.W. alimwahidi kitu, na mali iliyobakia aligawa kwa watu sawa sawa kwa mdogo na mkubwa mtu huru na mtumwa mwanamume na mwanamke, ukafika mwaka mmoja kila mmoja alipewa dirhamu saba, na ikafikia mwaka uliofuata dirhamu ishirini kwa kila mtu, wakasema baadhi ya watu kumwambia Abi Bakr: Ewe Khalifa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika yako umegawa hii mali na kugawa sawa kwa watu, miongoni mwao wapo wenye uwezo na waliotangulia kwenye Uislamu, ungewazidishia watu waliotangulia katika Uislamu na kuacha wenye uwezo kwa uwezo wao, akasema: Ama mliowataja watu waliotangulia katika Uislamu na wenye uwezo, basi ni kitu gani kitanijulisha hilo bali jambo hili thawabu zake ni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na hii ni kiinua mgongo hivyo kigezo katika hili ni bora zaidi kuliko nafasi ya mtu( ).
Hivi ndivyo Abu Bakr alifanya usawa katika kutoa kati ya watu usawa, na akaacha malipo ya kazi hiyo ni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hilo ni kwa msingi kuwa kutoa lengo lake kuimarisha maisha na wala sio malipo, na kiwango cha maisha ni sawa kwa wote, pindi Umar aliposhika utawala alifuata njia nyengine katika kugawa, akawapa fungu watu wazima miongoni mwa Muhajirina na Ansar miongoni mwa wale walioshiriki vita vya badri walipewa elfu tano kila mmoja, na ambaye hajashiriki vita hivyo alipewa elfu nne dirhamu, na akagawa fungu kwa yule aliyeingia kwenye Uislamu kama vile kuingia kwenye Uislamu kipindi cha vita vya Badr, akawapa kiasi cha wale waliotangulia katika Uislamu, pindi alipoulizwa kuhusu hilo akasema: Sifanyi kwa mwenye kupigana na Mtume S.A.W. sawa na aliyepigana kwa kushirikiana na Mtume, kama vile alivyohusisha watu wa nyumbani kwa Mtume S.A.W. na kuweka fungu la wake za Mtume kiasi cha dirhamu elfu kumi na mbili kwa kila mmoja, na akagawa fungu kwa watu wa Abbas kiasi cha elfu tano dirhamu, na kwa Hassan na Hussein dirhamu elfu tano.
Jambo ambalo linaonesha ni kuwa Umar pindi alipogawa alichunga misingi mitatu:
Msingi wa Kwanza: Kuwafadhilisha watu wa nyumbani kwa Mtume S.A.W. kwa ukaribu wao kwa Mtume S.A.W.
Msingi wa Pili: Alifadhilisha baadhi ya watu kwa ukaribu wao na Mtume S.A.W. ambapo alimpa fungu Usama Ibn Zaid la dirhamu elfu nne, mtoto wake Abdillah Ibn Umar alisema kumwambia Umar: Umenipa mimi dirhamu elfu tatu, na ukampa Usama dirhamu elfu nne, na baba yake hakuwa na uwezo zaidi kama alivyokuwa baba yangu, wala yeye hakuwa nacho kama nilivyokuwa nacho mimi, Umar akasema: Mzidishie kwa sababu alikuwa anapendwa zaidi na Mtume S.A.W. kuliko wewe, na baba yake alikuwa anapendwa sana na Mtume S.A.W. kuliko baba yako.
Msingi wa Tatu: Aliwafadhilisha waliotangulia katika Uislamu na kupigana jihadi, ambapo Umar alimpa Safwan Ibn Umayah na Harith Ibn Hisham pamoja na Suhail Ibn Umar miongoni mwa watu waliofungua mji wa Makka chini ya kiwango cha waliochukua wa kabla yao, na wakajizuia kuchukua na wakasema: Hatutambui kuwa kuna yeyote aliye mbora zaidi ya sisi, akasema: Kwa hakika nimekupeni kwa kutangulia katika Uislamu wala si kwa sababu ya hesabu, wakasema kama hivyo basi sawa.
Hivi ndivyo kanuni zilikuwa ambazo ziliwekwa na Umar kwenye kutoa na kugawa mali ya hazina kuu ya serikali pamoja na kutofautiana makundi isipokuwa watu walikuwa sawa ndani ya kila kundi hakuna tofauti kwa mtu dhidi ya mtu mwingine, bali kupewa kulikuwa ni lazima kwa Mwislamu na asiyekuwa Mwislamu, kama vile hilo halikuishia kwa Waarabu ndani ya Kisiwa cha Waarabu, bali kupewa kulikuwa ni haki kwa kila Mwislamu popote alipo bali Umar alichukua na kuwapa wenye mahitaji miongoni mwa watu wa dhimma kama alivyolazimisha fungu kwa wageni kutoka kwenye hazina kuu ya serikali( ).
5. Usawa kwenye Kodi:
Waislamu wanakuwa sawa kwenye uzito wa kodi uliopitishwa kwao, kwani kodi kuu ni zaka, ambapo Waislamu wanakuwa sawa katika kuitoa kwa asilimia moja kwenye zaka ya fedha, matunda, wanyama, mazao ya kilimo, mali ya kuokota na visivyokuwa hivyo, kama vile Uislamu umeweka fungu la kodi kwenye mali iliyofichwa ardhini na kuokotwa, na Zaka ni ibada ya mali hailazimishwi kwa wasiokuwa Waislamu, na wala haifai kusamehe kwa mwenye vigezo vya kulipa Zaka, kwa kauli yake Mola Mtukufu: {Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe nauwatakase kwazo} [AT-TAWBAH: 103].
Kama vile haifai kupunguza viwango vyake ambapo Mtume S.A.W. ameviainisha.
Mali ya Zaka na mali iliyofichwa ardhini na kuokotwa ni sawa, ni kodi mbili muhimu pindi linapotokea jambo katika nchi linalohitaji gharama, basi watu hulazimishwa kulipia kodi wanayoona kulipa ili kuchunga msingi wa usawa kati ya wale wenye kipato kinachofanana, katika hilo anasema Imamu Shafiy( ): “Pindi hazina kuu ya nchi inapokosa fedha na mahitaji ya fedha kwa askari jeshi yakaongezeka ili kupata kiwango kinachotosheleza, basi Imamu au kiongozi akiwa ni mwadilifu anatakiwa kuwapa majukumu matajiri kwa maana ya kuwataka kulipa kodi kwa kiwango anachoona kitawatosha kwa hivi sasa mpaka pale zitakapopatikana fedha kwenye hazina kuu ya nchi”.
Na kutawekwa malipo mengine (Al-Jizyah) kwa watu wa Kitabu badala ya wao kutoa zaka ambayo imelazimishwa kwa Waislamu, nayo hayo malipo yatawekwa kwa kichwa kwa kiwango cha kawaida tu, kwa kuchunga pia hali ya mtu tajiri na masikini, gharama hizo ni kwa ajili ya ulinzi wao pamoja na kupata haki zao na usalama wao wa nafsi zao na mali zao, wakati huo huo wale masikini wanasamehewa kulipa pamoja na wale wasio na uwezo, wanawake, watoto na watu wazima, ikiwa watasilimu hawa watu wa Kitabu, basi malipo haya yanakuwa hayapo tena kwao na watawajibika na utoaji wa Zaka, katika muhimu kuangalia ni kuwa kiwango cha malipo siku zote kwa watu wa Kitabu ni cha chini sana na viwango vya Zaka ya lazima kwa Waislamu, na kumeachwa makadirio ya kiwango chake yafanywe na Mismamizi Mkuu wa mambo ya nchi kwa masilahi anayoyaona,na kwa mujibu wa hali za kiuchumi, kwani malipo ya Jizyah kwa watu wa Kitabu hata siku moja hayajawahi kuwa kwenye kiwango cha ukandamizaji au cha dhuluma, kama ilivyokuwa kawaida mara nyingi huondolewa malipo haya pindi hali ya kiuchumi inapokuwa mbaya kwa kuwepo hali ya ukame au mafuriko au mfano wa hayo katika majanga ya Umma, wakati ambapo Zaka inaendelea kuwa ni lazima tu kwa Mwislamu kwa masharti yake, wala haiwezekani kuondolewa Zaka madamu sharti na vigezo vyake vimekamilika kama vile kigezo cha kufikia kiwango cha kulipiwa pamoja na kufikisha mwaka.
6. Usawa kwenye Huduma za Kijeshi:
Mwenyezi Mungu Amelazimisha Jihadi kwa Waislamu lengo ni kulinda Dini nafsi na nchi, katika hilo Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinachushakwenu. Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kherikwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu Anajua na nyinyi hamjui}( ).Nayo Jihadi ni jambo la lazima pindi nchi ikiwa katika tishio la kiusalama, hivyo haifai mtu yeyote kukiuka Jihadi. Mwenyezi Mungu Anasema: {Nendeni mtoke, mkiwa wepesi na wazito, na piganeni Jihadi kwa mali zenu na nafsi zenu katika Njia yaMwenyezi Mungu}( ).
Kama vile Mwenyezi Mungu Anatahadharisha kujivua na kujiondoa kwenye Jihadi, ambapo watu wote wenye uwezo kwenye Jihadi wapo sawa ambapo haifai mtu kujiondoa au kundi au jinsia kwenye ulazima wa Jihadi maadamu ni mwenye uwezo, yenyewe Jihadi si lazima kwa wasiokuwa na uwezo kwa sababu za KiSheria, katika hilo Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Hapana lawama kwa wanyonge, wagonjwa, na wasiopata cha kutumia, maadamu wanamsafia niya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hapana njia ya kuwalaumu wanao fanya wema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu}( ).
Kama vile Jihadi si wajibu kwa wanawake na hiyo ni kutokana na udhaifu na unyonge wa miili yao na asili ya maumbile yao, kwani alipata kuulizwa Mtume S.A.W. je kwa mwanamke anapaswa kupigana Jihadi akasema: “Ndiyo ni Jihadi isiyo na mapigano ndani yake nayo ni Ibada ya Hija na Umrah”( ).
Ama kwa upande wa nchi kutokuwa kwenye kitisho, basi Jihadi inakuwa ni jambo la lazima yenye kutosheleza pindi ikiendeshwa na baadhi ya watu basi waliobaki wataendelea na mambo mengine na wala hakuna dhambi yoyote kwao.
7. Usawa kati ya Mwanamume na Mwanamke:
Uislamu umefanya usawa kati ya mwanamume na mwanamke katika thamani ya ubinadamu na katika thawabu na malipo na kubainisha vigezo tofauti kati yao ni matendo na wala sio ujinsia, na hiyo ni kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na hakika tumewatukuza wanadamu}( ).
{Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi}( ).
{Kila mtu lazima atapata alicho kichuma}( ).
{Wanaume wana fungu katikawalio vichuma, na wanawake wana fungu katika walio vichuma}( ).
Kutokana na maandiko haya Uislamu haujabomoa nafasi ya mwanamke kwa upande wa mwanamume katika mfumo wa Kiislamu na hilo katika mambo yafuatayo: Kwenye Haki - Siasa - Elimu - Matumizi ya Sheria - Mfumo wa familia - Mirathi.
Na msingi wa utawala katika Uislamu ni uwezo wa kutekeleza majukumu kwa mtu mwenye uwezo wa kusimamia hilo( ) katika hilo haki ya mwanamke inatokana na uwezo wake wa kusimamia kwa sura bora zaidi ya mwengine.
Katika hilo pia anasema Imamu Shafi( ): “Mwenye kuwa na uwezo wa kuongoza basi huyo anatakiwa kuongoza, na asiye na uwezo wa hilo ni mwenye kutakiwa kwa kazi nyengine nayo ni kusimamia uongozi kwa mwenye kuweza na kumlazimisha kuchukua jukumu hilo”.
Usawa kamili kati ya mwanamume na mwanamke si wenye kuwezekana kwa tofauti zilizopo kwa kila mmoja kati yao na uwezo wake pamoja na kufaa kwake, sifa ya ubinadamu na asili ya kuumbwa pamoja na kiwango cha elimu ndio vigezo vya kuteuliwa mtu kufanya kazi awe ni mwanamume au mwanamke, katika hilo anasema Sheikh Bukhariy Al-Hanafiy( ): “Hakika Mwenyezi Mungu Amezungumza na waja wake kwenye suala la ibada, wala hakuna maandalizi ya kusimamisha ibada isipokuwa kwa kusimamisha masilahi ya mwili na masilahi yanayotokana nje ya nyumba na ndani yake, ikiwa mwanamume atajishughulisha na masilahi ya nje ya nyumba, basi atapoteza masilahi ya ndani ya nyumba, na ikiwa atajishughulisha na masilahi ya ndani ya nyumba basi haiwezekani kwake kuyafikia masilahi ya nje ya nyumba, hivyo haijawa lazima kukusanya kati ya mwanamume na mwanamke ili mmoja wao asimamie masilahi nje ya nyumba na mwanamke thamani ni masilahi ya ndani ya nyumba”.
Kwa vile mwanamke amekuwa ni mshirika wa mwanamume katika maisha hivyo uhusiano kati yao ni uhusiano wa kusaidiana na kushirikiana na wala si uhusiano wa kujirudiarudia na kufanana( ). Inakuwa kila mmoja na sehemu yake katika kutumia haki.
Nafsi ya mwanamke katika jamii kwa upande wa haki na wajibu Uislamu umeziainisha na wala hatuna haja ya kutaja kuwa Uislamu umefanya kazi ya kumkomboa mwanamke kutokana na utumwa kabla ya kufikiria jamii ya sasa jambo hili kwa zaidi ya karne ishirini, kinachowezekana kusema ni kuwa Uislamu umefanya usawa kati ya mwanamke na mwanamume katika haki na wajibu tofauti ni kwenye mambo machache ambayo Uislamu umeangalia asili ya mwanamke kama Alivyoumbwa na Mwenyezi Mungu na majukumu yake endelevu ya kijamii kwa upande wa kuwa kwake Mama wa kizazi kipya( ).
Mwanamke pamoja na kuwa amezuiliwa kuongoza maeneo makubwa kama vile kuwa Khalifa au kuongoza serikali ya jimbo kuongoza Jihadi kwa makubaliano ya kauli za Waachuoni vile vile kuwa Imamu kwenye Swala kwa kauli pia za Wanachuoni pindi maamuma wasipokuwa wanawake( ) isipokuwa ana haki yeye mwanamke kwa mujibu wa desturi za Uislamu kufanya kazi kwenye baadhi ya majimbo ambayo yanaendana na asili yake basi anaweza kufanya kazi ya uwaziri mtendaji ikiwa kazi zake zitaendana na mambo ya familia kutokana na kuhitajika upole na huruma, kama vile amepitisha Imamu Abu Hanifa mwanamke kuongoza Mahakama katika mambo ambayo inafaa kuonekana kwake( ).
Katika hali ya mwanamke kufaa kuonekana kwake - ukiachana suala la mali - katika mambo ambayo hayawezi mwanamume kama vile mambo ya familia, watoto, unyonyeshaji na mengineyo basi sisi tunaona inafaa kusimamiwa na mwanamke kama vile kuwa kiongozi kwenye mambo ya matukio na mambo ya wanawake kwani yeye ni mwenye uwezo zaidi kuliko mwanamume ya kuyafahamu mambo hayo na kuyaelewa.
Kama vile wamepitisha Wanachuoni mwanamke kuwa na haki ya kuchaguliwa na haki ya kuwa mbunge pindipo ikiwa nafasi hiyo itamwezesha kutoa maoni yake basi hali yake katika hilo ni kama hali ya mwanamume sawa sawa( ). Kwani imewahi kutokea mwanamke alimkusudia Sahaba Umar Ibn Al-Khattab akiwa Msikitini akizungumzia masuala ya mahari za wanawake, mwanamke mmoja alipingana naye na Umar akabadilisha rai yake na kufuata rai ya huyo mwanamke.
Hakuna mwenye kupinga kwa mwanamke kuwa na haki katika usimamizi, kama vile hakuna anayepinga haki yake ya kuwa mwana jitihada, kisha anamiliki haki ya kushiriki katika kutengeneza kanuni.
Mwanamke ana haki ya kuwakilisha na kuwakilishwa, kwa hivyo inafaa kuwakilisha kwenye baraza la Wananchi kwa maana ya bunge wanawake wenzake, ikilinganishwa na usimamizi wa majukumu yake ya kimahakama kwa kauli za baadhi ya Wanachuoni.
Tofauti na tuliyotaja katika nyadhifa kwa upande wa wajibu kwa mwanamke katika kusimamia nyumba yake na familia yake hakuna kinachomzuia kufanya kazi inayomhitaji na anayohitaji inayomfaa yeye na kukubaliana na asili ya maumbile yake, wala haipelekei kwenye uharamu wala kuchukiza kutokana na kuwa kwake wazi na kuwa maeneo ya siri na asiyekuwa haramu kwake, ambapo kazi yenye heshima inayozalisha inamzuia mwanamke na udhalili na kumuweka mbali na kukumbana na taabu( ).
Katika historia ya Uislamu inaonesha kuwa mwanamke alikuwa anafanya kazi ukiacha kazi zake za msingi za kusimamia nyumba yake na familia. Huyu hapa ni Asmaa binti Abi Bakr aliyeolewa na Zubeir Ibn Al-Awaam anasema: Nilikuwa nabeba miche ya mitende kichwani kwangu kutoka kwenye shamba la Zubeir ambalo linapatikana karibu na Madina, siku moja nikiwa nimebeba miche ya mitende kichwani kwangu nikakutana na Mtume S.A.W. akiwa na kundi la Masahaba kisha akaniita( ).
Kama walivyoshiriki baadhi ya Masahaba wa kike( ) pamoja na Mtume S.A.W. katika vita kama vile Mama Imarah alishiriki kwenye vita vya Uhdi. Mama Suleim alishiriki katika vita vya Hunain. Ummayah Binti Qais alishiriki katika vita vya Khaibar, na walikuwa wakigawa maji ya kunywa kwa majeruhi na kuwafunika wakati mwingine walikuwa na wao wanapigana vita.
Kisha Umar Ibn Al-Khattab alimpa nafasi ya uongozi As-Shifaa Binti Abdillah ya kusimamia masuala ya uhasibu katika soko la Madina, nayo ni nafasi ambayo inapelekea kuzuia kughushi udanganyifu riba na ukiritimba, na inasemwa kuwa alikuwa pia anasimamia masuala ya wanawake sokoni.
Kutokana na hayo ambapo mwanamke anakuwa ni mwenye uzoefu sana wa kazi, na uelewa zaidi ya mwanamume, na mwenye uchunguzi zaidi wa habari kuu, hivyo katika Uislamu hakuna kinachozuia kuendesha na kusimamia majukumu mbali mbali kama vile kufanya kazi za kufundisha katika shule za wasichana, hasa kwenye kitengo cha watoto wadogo, vile vile kufanya kazi kwenye sekta ya tiba kama kuwa daktari muuguzi kwa wanawake na watoto wadogo, na kufanya kazi kwenye nyadhifa za tafiti za mambo ya kifamilia na misaada kwa familia.
Ama kazi mbazo zinahitaji uwezo wa kimwili na mwanamke hakuandaliwa na kazi hizo kama vile kazi za uaskari jeshi ulinzi na kazi za usalama: Hivyo haifai kwa mwanamke kufanya kazi hizo ili kulinda afya yake.
Vile vile haifai mwanamke kufanya kazi za kutumikia nyadhifa na majukumu yanayopelekea kwenye hali za riba na dhana mbaya pasi na masilahi binafsi wala masliahi ya Umma, kama vile wadhifa wa sekretari binafsi wa ofisi ya mwanamume, na kazi za kuhudumia wanaokuja kufuata vinywaji pamoja na mahoteli, kwa kauli ya Mtume S.A.W.: “Acha lenye kukujengea shaka na kufanya lisilo na shaka”( ). Na kauli yake Mtume S.A.W.: “Halali ipo wazi na haramu ipo wazi kati ya viwili hivyo kuna vitu vyenye kuleta shaka watu wengi hawavifahamu, basi mwenye kujitenga na mambo yanayoleta shaka atakuwa amejiweka mbali kwa ajili ya dini yake na heshima yake, na mwenye kuingia kwenye yanayojenga shaka ni kama mchunga anayechunga pembezoni mwa shimo inahofiwa kudondokea humo”( ). Kama vile amefanyia kazi kanuni ya KiSheria “Kuondoa ubaya hutangulizwa zaidi kuliko kuleta manufaa”( ).
Haki ya mwanamke kwenye Elimu:
Uislamu umehalalisha kwa mwanamke kupata elimu za aina mbalimbali na kwa hatua zake tofauti kama vile ulivyo halalisha kwa mwanamume, bali umefanya kwa mwanamke - katika mambo ya dini na mambo muhimu kwake katika mambo ya dunia - lazima kwake katika wigo wa hali ya dharura, katika hili anasema Mtume S.A.W.: “Kutafuta elimu ni jambo la lazima kwa kila Mwislamu mwanamume na Mwislamu mwanamke”( ).
Mama wa Waumuni Bi. Aisha R.A. alikuwa ni katika watu waliohifadhi sana Hadithi na Sheria, na alikuwa Mama wa Waumini Hafsa Binti Umar Ibn Al-Khattab R.A. akijifunza kuandika katika zama za ujinga kwa mwanamke mwandishi anaitwa Shafaa Al-Adawiyah baada ya kuolewa na Mtume S.A.W. alimtaka Shifaa kumfundisha mambo ya hati nzuri na kuzipamba kama alivyomfundisha msingi wa elimu ya kuandika( ).
Usawa katika matumizi ya Sheria:
Uislamu umeweka mazingira sawa kati ya mwanamume na mwanamke kwenye Sheria na katika haki zote za kiraia hakuna tofauti katika hilo kati ya mwanamke aliyeolewa na asiye olewa.
Kwani mwanamke haiba yake ya kiraia na ana uhalali wa kuingia makubaliano, na haki yake katika kumiliki kwani anamiliki hatua mbalimbali za makubaliano kuanzia makubaliano ya kuuza na kununua kuweka rehani kutoa zawadi na kuacha wasia, kama vile ana haki ya kubeba wajibu madamu ni mwenye akili na mtambuzi( ), na wala si mume wake wala mtu yeyote katika ndugu zake ana haki pamoja na yeye katika hilo, kama vile si halali kwa mume kutumia chochote katika mali yake isipokuwa akipewa ruhusa ya kufanya hivyo au akamuwakilisha katika kuingia mikataba kwa niaba yake, na ana haki ya kuvunja uwakala wake na kuwakilishwa na mwingine ikiwa atataka. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Wala si halali kwenu kuchukuachochote mlicho wapa wake zenu}( ).
Na Anasema tena Mola Mtukufu: {Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa nikipawa. Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha}( ).
Kwa hili Uislamu umetangulia mifumo mingine katika kupitisha uhuru wa mwanamke kwenye matumizi yake ya Kisheria na jukumu lake la mali, ambapo mwanamke hakupewa uhuru wa kumiliki mali ndani ya nchi za Ulaya isipokuwa ndani ya kipindi kifupi kilichopita.
Usawa katika mfumo wa Familia:
Mwanamke anamiliki kama mwanamume kazi za usia kwa wadogo na kusimamia mali na usimamizi wa mali za wakfu.
Katika masuala ya ndoa Uislamu umesimamia haki ya mwanamke ya kumkubali mume au kuto mkubali, kwani Wanachuoni wamekubaliana kuwa mwanamke aliyebaleghe mwenye kujitambua halazimishwi kumkubali mume pasi na ridhaa yake, bali ana uhuru moja kwa moja wa kuteua mume, kama vile hafanyiwi uzito kuhusu mume mwenye vigezo, ikiwa ndugu zake watamfanyia ubaya na kufanyiwa uzito kwa yule aliyemteua yeye basi atafungua kesi kwa kadhi kwa dhuluma hiyo, na kuondolewa kero hii pamoja na kuwezeshwa kuolewa na yule aliyemridhia yeye mwenyewe madam ni mwenye kigezo kwake.
Kwa upande wa talaka baadhi ya watu wanadhani kuwa Sheria ya Kiislamu imempa haki hii moja kwa moja mwanaume pasi na mke kuwa na haki katika hili, jambo ambalo linazingatiwa ni kinyume na msingi wa usawa kwa mwanamume, na kukiuka msingi wa wajibu wa makubaliano ambapo haifai kuvunja isipokuwa kwa ridhaa ya pande mbili zilizoingia makubaliano.
Asili katika makubaliano ya ndoa katika Sheria ya Kiislamu ni kuwa yanakamilika kati ya pande mbili na mwanamke anakubali mwanamume kushikilia peke yake hatua ya utoaji talaka katika mipaka ambayo imepitishwa na Uislamu, ikiwa mume atatumia haki yake katika talaka, basi matumizi hayo yanakuwa sawa na walivyokubaliana pande mbili wakati wa ndoa, isipokuwa Uislamu umeweka aina nyingine ya talaka ambayo ni( ):
- Kuna talaka inatoka kwa mwanamke, na hiyo ni pale kunapowekwa sharti katika ufungaji wa ndoa ya kuwa maamuzi ya mwisho yapo mikononi mwake, na mume anakuwa amekubali hilo, hivyo mwanamke anakuwa na haki ya kutoa talaka ikiwa masharti maalum yatakamilika( ).
- Mke kuweka sharti maalumu katika kufunga ndoa ikiwa mume atakiuka hilo sharti basi talaka inatoka, wala lisiwe hili sharti lenye uharibifu na kwenda kinyume na mipaka ya Mwenyezi Mungu na mambo yanayoimarisha maisha ya ndoa( ).
- Talaka inatolewa na Chief Kadhi kwa ugumu unaotokana na mume na kutokuwa na uwezo wa kuhudumia na kuepusha madhara na kujidhuru, au kwa kutokuwepo kwa mume kwa muda mrefu ikiwa mke atapeleka shitaka lake kwa Chief Kadhi akiwa anataka kuachika( ).
- Talaka inatoka kwa ridhaa ya mwanamume na mwanamke kwa pamoja, na mara nyingi inakuwa mwanamke anaachia na kusamehe mali zake zote kwa mume wake au baadhi yake au kwa njia ya kupewa sehemu ya mali wakiridhiana wote wawili, na ndio inaitwa Khuluu - kujivua( ).
- Kama vile mwanamke anaweza kudai talaka kwa vile tu anamchukia mume( ). Imepokelewa Hadithi na Imamu Bukhari( ) kuwa mke wa Thabit Ibn Qais alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Thabiti Ibn Qais wala sipingi kwake tabia wala dini, lakini mimi nachukia kufanya vitendo kinyume na Uislamu kwani ninamchukia kwa sura yake. Mtume S.A.W. akamuuliza: Je unaweza kumrudishia mahari yake? Akasema ndiyo naweza: Mtume S.A.W. akasema mpe mahari yake na umwache kabisa” Na kwa mahari hiyo amejivua mwenyewe kwenye ndoa.
Ni kama hivyo, mume pindi anapoitoa talaka atalazimika kwa mtalaka wake kulipa mahari aliyochelewesha kulipa matumizi yake na ulezi wa watoto, na mfano wa hivyo inakuwa kwa mke ambaye anataka talaka kusamehe haki zake zote au baadhi kabla ya kuachwa kwake.
Marejeo: Kitengo cha utafiti wa KiSheria ofisi ya Mufti wa Misri.