Kulisha Chakula- Kilicho kizuri zai...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kulisha Chakula- Kilicho kizuri zaidi kwa Mtazamo wa kimaadili katika Uislamu

Question

  Ni zipi sababu za kuenea kwa tabia mbaya Duniani, na je, chakula anachokila mtu kina athari yoyote katika hilo?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Watu wengi huuliza tabia mbaya iliyoenea katika kila sehemu Duniani kote, na moja kati ya sababu muhimu – kwa Rai yangu – ni ubaya wa chakula, na Mtume S.A.W, anasema: kipendezeshe unachokila basi utajibiwa maombi yako. Na hii ni Hadithi yenye sehemu mbili, sehemu ya Kwanza: Kipendezeshe unachokila, nayo ni amri anayotutaka Mtume tupendezeshe chakula katika viwango viwili:
Kiwango cha Kwanza: Lazima chakula kiwe Halali, na maana yake ni kuwa chanzo cha pato kiwe Halali hakina rushwa ndani yake au wizi au udokozi au unyang’anyi au hata udanganyifu wa aina yoyote au gushi, na chanzo hicho kiwe mbali na vilivyoharamishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu katika vyakula kama vile pombe, nguruwe, mzoga na damu chafu. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Sema: Sioni katika yale niliyo funuliwa mimi kitu kilicho haramishwa kwa mlaji kukila isipo kuwa kiwe ninyamafu, au damu inayo mwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu}. [AL ANA'AM 145]
Bali Kisa cha Adamu katika Qur'ani kilibainisha adhabu ya kula chakula kisicho sahihi na ikajaalia kuwa sababu ya kufukuzwa peponi, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Basi akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti, tupu zao zilifichuka na wakaingia kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao Mlezi akawaita: Je, sikukukatazeni mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui yenu wa dhaahiri?} [AL A'ARAAF 22]
Na Al Hassan Al Baswriy amesema: "Mtihani wa Baba yenu Adamu ulikuwa chakula, na huu utaendelea kuwa mtihani mpaka siku ya Kiyama. Chakula kinapokuwa kinatokana na chumo la Halali, nalo ni lile alilolihalalisha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika vyakula, ingizo la mlishaji ni kwa kiwango cha kukubaliwa Dua yake".
Kiwango cha Pili: Chakula chenyewe kiwe kizuri kwa kukionja kwake na katika kukiandaa kwake na anayetaka aina hii ya chakula ana moyo mwema na anahisia nzuri ambapo njaa haimpelekei kulijaza tumbo lake bila ya kupata ladha ya chakula kwa kuonja na kuuhisi uzuri, nayo ni sifa tuionayo katika Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu Watu wa Pangoni baada ya kuwa kwao pale kwa miaka 309 usingizini. {Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao:Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu aende mjini, akatazame chakula chake kipi kilichobora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote}. [AL KAHF 19]
Njaa haikuwapelekea wao kutaka chakula chochote hata kama chenyewe ni Halali, na katika chanzo chake, bali waliomba kiwe na mfungamano na Usafi, kisha Aya inaashiria Kiasi cha Chakula na kwamba chakula hicho ni kuwa kwake riziki kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na wala hawakusema: akuleteeni chakula hicho, na hapa tunaona uhusiano na chakula unaotokana na usafi wa Nafsi. Na tunaona katika Hadithi ya Mtume S.A.W, kwamba kuitakasa Nafsi ni katika chakula kizuri, ambapo anasema: Mtu ana safari ndefu, akiwa amechafuka kwa vumbi, anaunyoosha mkono wake mbinguni akisema: Ewe Mola wangu, ewe Mola wangu, ewe Mola wangu. Wakati chakula chake ni cha Haramu, vinywaji vyake ni vya Haramu, nguo zake ni za Haramu na amekula Haramu, atajibiwa vipi.
Ulaji wa chakula lazima udhibitike kwa sababu una athari katika maisha yetu ya kila siku kwa pande zake zote za Kijamii, Kisiasa na kiuchumi. Na njia hizi za kudhibiti zinatolewa ndani ya Qur'ani Tukufu na Sunna. Na miongoni mwake:
1- Kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {{Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu}. [AL A'ARAAF 31]
Kwa hiyo Kiwango ni muhimu sana kama inavyopangwa na Mtume S.A.W. katika Hadithi inavyopokelewa kutoka kwa Miqdaam bin Muudi Karab, ambapo anasema: "Mwanadamu hajawahi kujaza chombo chochote Shari kuliko tumbo lake, kinachomtosha mwanadamu ni vijitonge vichache vinavyompatia uwezo wa kusimama na ikiwa Nafsi yake itamshinda, basi theluthi moja ni ya chakula na theluthi moja ni ya kunywa maji na theluthi moja ni ya kupumulia".
2- Na Wema waliotangulia wanaidiriki maana hii vyema. Anasema Bin Maasawiihi Twabiib alipoisoma Hadithi hii: Kama watu wangeyatumia maneno haya basi wangesalimika na magonjwa ya kila aina, na maduka yote ya madawa yangesitisha kazi zake. Na Marouzi anasema akimwambia Imamu Ahmad Bin Hanbali: Je, mtu atakuwa na ulaini moyoni mwake hali ya kuwa ameshiba? Akasema: sioni kama hilo linatokea. Na Ibrahim Bin Ad-ham anasema: Mtu atakayelidhibiti tumbo lake atakuwa ameidhibiti Dini yake, na atakayeimiliki njaa yake atakuwa anamiliki Usafi wa nia wenye wema na kumuasi Mwenyezi Mungu Mtukufu kuko mbali na mtu mwenye Njaa na kuko karibu na mtu mwenye Shibe, na Shibe huufisha moyo. Na Kauli hii inafupisha ule uhusiano uliokuwa unaonekana na ulipokosekana tukakosa Vitu vingi mno.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia Kulisha chakula kuwa ni katika Maadili mema. Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa}. [AL INSAAN 8]. {Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani}. [AL INSAAN 9].
3- Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia Kulisha chakula kuwa ni katika Maadili mema. Basi Kulisha chakula kizuri kipendezacho moyoni – Na hapana budi pawepo sifa hii – miongoni mwa sifa ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu anazipenda.
Bali amekifanya chakula kiwe kama njia ya kuzifikiria dhambi, ba akashurutisha chakula hicho kiwe kile kizuri kabisa na bora zaidi, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Kafara ya Kiapo: {Mwenyezi Mungu hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakushikeni kwa mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini yamini zenu. Namna hivyo Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake ilimpate kushukuru}. [AL MAIDAH 89]
Na ya Uwastani maana yake ya Juu, kama katika kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume aweni shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulichokuwa nacho ila tupate kumjua yule anaye mfuata Mtume na yule anaye geuka akarejea nyuma. Na kwa yakini hilo lilikuwa jambo gumu isipo kuwa kwa wale alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa watu na Mwenye kuwarehemu.} [AL BAQARAH 143].
4- Bali hapana budi chakula hicho kiwe Halali na chenye ladha nzuri na kizuri zaidi katika vile ambavyo mtu anawalisha watu wake wa nyumbani.
5- Na hivyo ndivyo tulivyoona katika zama zetu nzuri watu wanashughulikia zaidi chakula kizuri na kukiandaa na kukaa kwa ajili ya kukila na kutofanya israfu katika chakula hicho na kutokidharau, mpaka wakajaalia kudharau chakula ni kukufuru neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Mwanadamu. Na tumewaona wakifanya hivyo kwa ustadi mkubwa pamoja na ukawaida wa chakula, Na Wamisri na Watu wa Shamu na wengine wao wanajulikana mno katika kushughulikia maharagwe (fuulu) - kwa mfano – na Maharagwe haya ni katika vyakula mashuhuri sana vilivyoenea na vya kawaida, nao huviandaa kwa maandalizi mbalimbali na njia tofauti tofauti, na jambo hili linahusiana nini na “Kula huku unakimbia”? Au “Take away”, na hili linahusianaje na zama za hambaga na kikombe cha Kinywaji Baridi.
6- Na Mtume S.A.W, ametuwekea sisi Maadili ya chakula na akamwambia Ibnu Abbas R.W: "Ewe mvulana, Mtaje Mwenyezi Mungu, na ule kwa mkono wako wa kulia, na ule chakula kilicho upande wako". Na anasema Mtume S.A.W: Mtu yoyote atakayekula chakula na akamshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kusema: Ninamshukuru Mwenyezi Mungu aliyenilisha chakula hiki na akaniruzuku bila ya ujanja au nguvu zangu, basi Mtu huyu atasamehehewa madhambi yake yote aliyoyachuma.
Sheria imetuasa kula kwa utulivu na taratibu na kutoharakisha kwa kula haraka haraka, na kuna mwanamke mmoja aliyemkemea mume wake juu ya mazoea haya mabaya katika Hadithi ya Mama Zar’aa iliyosimuliwa na Mama Aisha R.A, kwa Mtume S.A.W, kwamba alisimulia kuhusu mke huyu: "Akasema Wa sita: Mume wangu anapokula huwa anakomba na anapokunywa huwa anakunywa maji kwa pupa na anapolala hujifunika gubi gubi" . Na yote hayo yanamaanisha kwamba sifa mbaya ya kula na kunywa ni katika mambo ya majanga ya kimaadili na sifa mbaya za wengi.
Na Mtume S.A.W akasema: Muumini anakula kwa tumbo moja na Kafiri anakula kwa matumbo Saba. Na Anasema Mtume S.A.W: Chakula cha wawili kinawatosha watatu, na chakula cha watatu kinawatosha wanne.
Na yeyote anayeukana Mfumo huu na akafanya israfu katika ulaji wake, na akawa hajali alikoipata riziki yake, wala hajali uzuri wa chakula chake, na wala hatafuti kujibiwa Dua zake na kuwa na Maadili mema, basi hakika mambo yalivyo, anakuwa mtu aliyejiweka katika kuacha, na Falsafa ya Kuacha katika Qura'ni ni jambo kubwa sana na lina mfumo wake tunauona katika suala la chakula, ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa.Watakuja jua}. [AL HIJR 3]
7- Na huwenda sisi tukapanua zaidi maelezo ya Falsafa ya Kuacha, na Msimamo wa Qur’ani unaoihusu; kwani inamnufaisha Muislamu katika zama zetu hizi.
Kwa hivyo sisi tunalazimika kurejea katika vyakula Halali mpaka tufanikiwe kuondosha Shari katika Nafsi zetu, na ufisadi katika Jamii zetu, na kuondosha kwenda kombo kwa Ulimwengu. Ni wito ambao baadhi yao wanaweza kuuona kama uko mbali, lakini sisi tunapaswa kuuhangaikia, na hatulazimiki sisi kuyadiriki mafanikio. Mtume S.A.W. amesema: Nilioneshwa Mataifa mbalimbali, nikamuona Mtume akiwa na kundi la watu, na Mtume mwingine akiwa na mwanaume mmoja, na wanaume wengine wawili na Mtume mwingine akiwa hana mtu yeyote. Maana yake hiyo wala haimdhuru kwamba yeye alikuwa na Haki, na hapana budi kufanya mabadiliko "Anza kwanza na Nafsi yako kisha aliye kuliani kwako". Na Dua yetu ni kuwa, tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mola wa Viumbe Vyote
Chanzo ni Kitabu cha Sifa za zama za sasa, cha Mheshimiwa Mufti wa Misri: Dkt. Ali Juma

 

Share this:

Related Fatwas