Utafiti wa Upatanishaji Baina ya Madhehebu ya Kifiqhi
Question
Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, na swala na salamu zimshukie Bwana wetu Muhammad, Muaminifu, na jamaa zake na Maswahaba zake wote, na baada ya hayo:
Answer
Hakika Sharia ya Muhammad ni nyepesi, samehevu na pana mno, inawaenea na kuwatosha watu wote waliokalifishwa kisharia, kwa hali zao tofauti tofauti na mahitaji yao, katika kila zama na kila mahali, na haiwezekani kwa Mujtahidu Mmoja akaweza kuizingira yote bali kila Mujtahidu anachota kiasi chake cha elimu katika Bahari Pana ya Sharia kwa uwezo wa Elimu yake, na upeo wa ufahamu wake. Na kama watu wote wangepita njia moja ya Madhehebu basi jambo lingekuwa finyu kwa waumini kutokana na Madhehebu moja kutozingira kila kitu katika vyote vilivyoletwa na Sharia takatifu. Hakika imenukuliwa kutoka kwa Omar bin Abdul-Aziiz kwamba yeye alikuwa akisema: {Hainifurahishi kwamba Maswahaba wake Mtume S.A.W, hawakuhitilafiana; kwani kama wao hawakuhitilafiana pasingelikuwapo ruhusa "[1].
Na kadhalika Al Khatweeb Al Baghdadiy alitoa kwamba Haruun Ar Rasheed akasema kwa Malik Bin Anas: " Ewe Baba Abdillah sisi tunaandika kitabu hiki -Yaani Kitabu cha Al Muatw'- tunachokiandika, na tunakigawa katika peo za Kiislamu ili tuubebe Umma kwacho, akasema: Ewe Kiongozi wa Waumini: Hakika kutofautiana kwa Wanazuoni ni rehma kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Umma huu, kila mmoja na afuate kilicho sahihi kwake, na wote wamo katika uongofu na kila mmoja wao anakusudia Mwenyezi Mungu Mtukufu"[2]
Al Qasim Bin Mohammad akasema: "Kuhitalifiana kwa Maswahaba wa Mtume S.A.W, kulikuwa ni njia aliyoitumia Mwenyezi Mungu Mtukufu kunufaisha kwayo, na ulichokifanya katika matendo yako nafsi yako haijapata chochote"[3]
Na kutoka kwa Omar Bin Abdulaziz R.A akasema: "Kisichonifurahisha ni kwamba lau Maswahaba wake Mtume S.A.W, hawakuhitilafiana,"[4]
Na alikuwa akisema, yaani Omar Bin Abdulaziz, "Kisichonifurahisha ni kwamba lau Maswahaba wake Mtume S.A.W, hawakuhitilafiana, kwani wao kama wasingelihitilafiana basi pasingelikuwepo ruhusa".
Na Sufiaan Athauriy alisema: "Uhitilafiano wa Mswahaba wa Muhammad ni rehema kwa waja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, Na Al Laith kutoka kwa Yahiya Bin Saied akasema: Wanavyuoni wana upana wa Elimu"[5]
Na kutoka kwa Yahiya Bin Saied akasema: "Wanavyuoni wana upana wa Elimu, na Mamufti wanaendelea kutofautiana, huyu anahalalisha hiki na huyu anakiharamisha kile, na wala huyu hamkosoi yule anapojua kasoro hiki ajuapo kike yule akijua vile"[6] Na hiyo ni kutoka Fiqhi yao R.A, wote.
Anapaswa mtu anaeongoza katika utoaji wa Fatwa asijifunge na Madhehebu maalumu bali kinachozingatiwa ni kile kilichopitishwa na Dalili na kikawa kinaendana na mahitaji ya watu katika zama zao. Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema katika Kitabu chake Kitukufu: {Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim} [AL HAJ 78], Na Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: {Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo} [AL BAQARAH 286].
Na imetaja katika Bukhari na Muslim kutoka kwa Abi Musa akasema: Mtume S.A.W., alikuwa akituma mmoja wa Maswahaba katika jambo fulani husema: "Peaneni habari njema na wala msipeane habari mbaya na fanyeni wepesi na wala msifanye ugumu"[7]
Na imekuja katika Bukhari na Muslim kutoka kwa Saied Bin Abi Bardah kutoka baba yake, kutoka babu yake kwamba Mtume S.A.W. alimtuma yeye na Mu'az kwenda Al Yamen, basi akasema: "Peaneni habari njema na wala msipeane habari mbaya na fanyeni wepesi na wala msifanye ugumu, na jitoleeni wala msihitilafiane" [Imetolewa na Bukhariy 2269/5, Na Muslim 141/5]
Basi Fatwa inatofautiana kutokana na utofauti wa nyakati na mahali, na kutokana na utofauti wa Mufti, kwa hiyo tunakuta Ahmad Bin Hambal ana Fatwa kadhaa katika suala moja. [Tazama kwa mfano, kitabu cha: "Al Iswaaf" kwa Al Mardawiy, kina mifano mingi katika jambo hilo].
Na kuanzia hapo, ndipo ilipojitokeza haja ya kile kinachoitwa upatanishaji wa Fatwa; kwa lengo la kuwarahisishia Waumini. Na baadhi ya watu walitumia vibaya uelewa wa upatanishaji, na kudhani mwenye kufuata ruhusa za Wanachuoni kama ni matamanio.
Na kwa ajili hiyo pamekuwepo uhitaji mkubwa wa kuandika tafiti inayofafanua vyema maana ya Upatanishaji, na hukumu ya Upatanishaji, na kubainisha kinachojuzu katika hukumu hiyo na kinachokatazwa, na udhibiti wa kila hukumu pamoja na kuweka wazi utekelezaji wa kifiqhi.
Muhtasari wa kijumla wa maana ya Upatanishaji:
Kwanza: Maana ya Upatanishaji katika lugha na Istilahi:
Na kwa hiyo, Upatanishaji kilugha ni: ukusanyaji, ulinganishaji, udanganyaji na upambaji, na ukusanyaji wa moja ya pande mbili na kuiunganisha na nyingine na kisha kuziambatanishaji pamoja[8], na pia husemwa kwamba mtu fulani ameambatanisha ombi la jambo kadhaa na hakulidiriki, na ukusanyaji wa pamoja na kuchanganya, na husemwa pia kuchukua upatanishaji katika masuala, husemwa pia ameziambatanisha nguo mbili au amezikunja pamoja kwa maana ya kushona pamoja, Na Hadithi imepambwa na kupotoshwa kwa uongo, kwa hiyo ni kubambika.
Na maana katika Istilahi: "Kuna wakati Istilahi ya Talfiq inatumika katika vitabu vya Fiqhi kwa maana ya kukusanya na wakati mwingine hutumika kwa maana ya kupatanisha na kukusanya"
Basi inatumiwa kwa maana ya kukusanya, Ibn Qudamah amesema katika kitabu cha: [Al Mughniy]: "Na maana yake nyingine ni kuunganisha damu na damu nyingine ambayo kati yake kuna Twahara" [9]
Na kwa maana ya kupatanisha na kukusanya baina ya mapokezi mbali mbali katika suala moja ilivyo katika mapokezi yanayowajibisha malipo kumrejesha mtumwa aliyetoroka katika Madhehebu ya Hanafi.[10]
Na upatanishaji katika elimu ya Balagha: Ni aina ya upeo wa kilugha, na udhibiti wake, na hakika huko ni kukusanya jambo na kile kinachonasibiana nacho sio kwa kinyume chake. Kama mfano wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Jua na mwezi huenda kwa hisabu} [AR RAHMAAN 5], Basi Hakika Jua na Mwezi vinanasibiana na siyo kwa kinyume.[11]
Na kusudio letu hapa ni lengo la utafiti wetu; upatanishaji katika Fatwa, na maana yake ni kuleta kwa namna ambayo Mujtahidi hasemi chochote kuhusu jambo hilo.[12]
Na imesemwa kuwa maana inayokusudiwa kwa neno hili la Upatanishaji (Talfiiq) kati ya madhehebu ni kuchukua kilicho sahili katika matendo kutoka katika madhehebu mbili kwa pamoja baada ya hukumu ya ubatili wake kwa kila moja katika madhehebu hayo.[13]
Na inasemwa ni: "Kuchagua hukumu za madhehebu ya Fiqhi yanayozingatiwa kwa lengo la kuiga na kufuata".[14]
Na imesemekana kwamba ni: "Kuja na kitu kinachoigwa au kufuatwa katika suala moja lenye matawi mawili yenye mfungamano au zaidi kwa namna ambayo hakuna katika wale walioigwa Mujtahidi yeyote anayelizungumzia suala hilo. [15]
Na maana yake ni kupangika katika kazi kwa kuiga madhehebu na kuchukua katika suala moja kauli mbili au zaidi. Na kufikia ukweli uliojengeka ambao hakuna yeyote anaoukiri, iwe Imamu ambaye alikuwa katika madhehebu yake, na Imamu aliyeuiga, kwani kila mmoja miongoni mwao anaamua kubatilika kwa ukweli huo uliopatanishwa.
Na jambo hilo linapatikana ikiwa mwigaji atafanya kazi ya kuiga katika jambo moja kwa kauli mbili tofauti, au kwa kauli moja pamoja kubakia athari ya kauli ya pili na kuendelea.
Kwa hivyo, Talfiq au Upatanishaji ni: Kukusanya baina ya kuiga maimamu wawili au zaidi katika kitendo chenye nguzo zake au katika sehemu zenye mfungamano zenyewe kwa zenyewe, lakini ndani yake kuna hukumu maalumu ilikuwa ni sehemu ya jitahada zao, na kufafanua rai zao, na yeye akaamua kumwiga mmoja wao katika hukumu fulani, na kumwiga mwingine katika hukumu nyingine, na kwa njia hiyo kitendo cha kupatanisha kinatimia baina ya madhehebu mbili au zaidi.
Kwa mfano, mtu kuiga au kufuata katika udhu madhehebu ya Shafi katika kutosheka na ufutaji wa sehemu tu ya kichwa, kisha kufuata madhehebu ya Hanafi au Maliki katika kutotengukwa na udhu kwa kumgusa mwanamke bila ya kizuizi chochote na bila kukusudia matamanio na kuwepo kwake matamanio hayo, kisha akaswali, basi hakika udhu huo alioswali nao hakuna yeyote katika wanachuoni aliouzungumzia, kwani Imamu Shafi anauzingatia kuwa ni batili kwa kutenguka kwake kwa kugusa, na Abu Hanifa hajuzishi kwa kutopaka robo ya kichwa, na Maliki hakubali kwa kutopaka kichwa chote au kwa kutosugua viungo vya udhu na mfano wa hayo. Au ni Mtu kumfuata au kumuiga Maliki katika kutotengukwa na udhu kwa kukohoa kohoa ndani ya Swala, na Abu Hanifa katika kutotengukwa na udhu kwa kugusa utupu, na akaswali. Basi hakika Swala hii wote wawili wamekubaliana ya kuwa imeharibika.
Na mfano wake ni mtu kumkodisha mtu mwingine sehemu iliyowekwa Wakfu wa miaka Sabini na zaidi bila ya kumuona, kwa kuiga na kufuata Madhehebu ya Imamu Shafi kwa muda mrefu sana pamoja na Imamu Ahmad, na katika kutoona katika madhehebu ya Abuu Hanifa, basi inajuzu.[16]
Na mfano wake vilevile: Mtu aliyetawadha amemgusa mwanamke asiyemuhusu bila ya kizuizi chochote na akatokwa na najisi kama vile damu ambayo haikutoka moja ya njia mbili, hakika udhu huo umeharibika kwa kumgusa mwanamke kwa mujibu wa madhehebu ya shafi, na umeharibika udhu huo kwa kutokwa na damu ambayo haikutoka katika moja ya njia mbili kwa mujibu wa madhehebu ya Hanafi, na wala hatengukwi na udhu kwa kutokwa na najisi hiyo ambayo haitoki katika moja ya njia mbili kwa mujibu wa madhehebu ya Shafi na wala udhu huo hautenguki pia kwa Imamu Hanafi kwa kugusa, na ikiwa mtu ataswali kwa udhu huo basi hakika mambo yalivyo, kusihi kwa Swala yake kunaambatanishwa ma madhehebu mawili.
Na katika mifano ya Upatanishaji wa hukumu katika Mambo ya ndoa na Familia: Ni mtu kuoa mwanamke bila ya Walii au mahari au mashahidi, kwa kuiga na kufuata kila dhehebu kile kisichosemwa na mwingie lakini ni katika Upatanishaji wa hukumu unaopelekea uharamu, na kwa hivyo haijuzu kufanya hivyo, kwani ni kwenda kinyume na Wanachuoni wote, na sura hii haijasemwa na mwanachuoni yeyote.
Nyanja na Upatanishaji wa Huku ni kama nyanja za kuiga zinaishia katika masuala ya kujitahidi kwa Wanachuoni na kukisia. Ama kuhusu yale masuala yajulikanayo katika Dini kwa dharura – kwa maana kiakili – ni katika yaambatanayo na hukumu ya kisharia, nayo ni yale ambayo Waislamu wote wamekubaliana na ayeyapinga anakuwa kafiri kwa kuyapinga, na wala haisihi ndani yake ufuasi wala Upatanishaji wa Hukumu, na kwa ajili hiyo haijuzu aina yoyote ya upatanishaji wa hukumu unaopelekea uhalalishaji wa mambo yaliyoharamishwa kama vile mvinyo na uzinifu kwa mfano. Na hii ni kwamba hakika suala la upatanishaji wa hukumu baina ya madhehebu umeshurutishwa kutokuwepo kwake kwa kujuzu uigaji wa madhehebu ya wengine zaidi kuliko waliokuja baadaye miongoni mwa Wanachuoni baada ya kumalizika kwa karne ya kumi Hijiriya, na hawakuizungumzia kabla ya karne ya saba.[17]
Hitilafu za Wanavyuoni katika upatanishaji:
Na kabla ya kuingia katika kuyazungumzia Madhehebu katika suala hili kwanza kabisa tunapaswa kupaacha huru mahala pa mzozo.
Wanachuoni wamekubaliana ya kwamba haijuzu kuleta upatanishaji wa hukumu katika yale mambo yanayojulikana katika Dini kwa dharura kama vile masuala ya Upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na Nguzo za Uislamu na mfano wake.[18]
Wamekubaliana katika kuurudi Upatanishaji wa hukumu ulio batili wenyewe kwa wenyewe kama vile anavyochanganya msemaji: Irakiyu amehalalisha mvinyo na kuunywa mvinyo na akasema: Vyote viwili ni pombe na ulevi, na akasema Hijaazi: Vinywaji vyote viwili ni kitu kimoja na ndipo tulipopata sisi pombe baina ya hitilafu hizi mbili.[19]
Nitachukua kutoka katika kauli zao wao wote wawili na kunywa pombe hakuna tofauti baina ya pombe na mnywaji katika hukumu ya Uharamu wake, na Abu Hanifa anaona kuwa inajuzu kunywa mvinyo, na Imamu Shafi anaona kuwa Mvinyo ni pombe na akasema kwamba huyu mpatanishaji yuko baina ya kauli mbili: Kwa hiyo pombe ni halali. Wamekubaliana wanachuoni kumrudi na kuirudi hukumu hii ya Upatanishaji ambao inalazimu kuitengua hukumu ya hakimu kwani hukumu yake inaondosha hitilafu iliyopo. wamekubaliana wanachuoni katika kuurudi upatanishaji wa hukumu unaowajibisha kurejea nyuma kwa yale yaliyofanyiwa kazi kwa kuiga au kufuata au yaliyofuatwa na wanachuoni wote.[20]
Na upatanishaji una aina kadhaa, tunapasa kuuelezea kabla ya kutaja hitilafu.
Aina ya Kwanza: kwamba upatanishaji ulikuwa baina ya vitabu na milango mbali mbali, kama vile anapatanisha baina ya madhehebu ya Kihanafi katika ibada na madhehebu ya Kishafi katika matendeano, au madhehebu ya Kimaliki katika kuosha na madhehebu ya Kihanbali katika hedhi.
Aina ya Pili: Upatanishaji huo wa hukumu uwe katika mlango mmoja, kwa mfano kama atachukua madhehebu ya Hanafi katika yanayowajibisha josho na madhehbu ya Shafi katika sifa zake.
Aina ya Tatu: na Upatanishaji huo wa hukumu uwe katika sehemu za Hukumu moja na mfano wake ni kama ilivyotangulia kuelezwa nao ni kwa yule aliyetawadha akafuta sehemu ya nywele zake kwa kuiga madhehebu ya Imamu Shafi na baada ya udhu akaugusa utupu wake kwa kuyaiga madhehebu ya Abu Hanifa.[21]
Pia aina za upatanishaji haramu:
Ni mtu kumwacha mke wake mara tatu, kisha mwanamke huyo akaolewa na mtoto wa miaka tisa kwa lengo la kuhalalisha, kwa kumuiga mume wake katika kusihi kwa ndoa katika Madhehebu ya Imamu Shafi, na akamuingilia kisha akamwacha kwa kuiga kusihi kwa talaka, na kutokuwepo haja ya eda kwa mujibu wa Madhehebu ya Imamu Ahmad, basi inajuzu kwa mume wake kufunga naye ndoa haraka iwezekanavyo. Na upatanishaji huu wa hukumu umekatazwa kwa sababu unapelekea katika kuyachezea chezea masuala ya Ndoa.
Kwa hivyo amesema Sheikh Ajhuryi mfuasi wa Madhehebu ya Imamu Shafi: Hii inakatazwa katika zama zetu na haijuzu na wala haisihi kulifanyia kazi suala hili, kwa sababu katika madhehebu ya Imamu shafi panashurutishwa kwamba lazima anapoozeshwa mtoto awe na mzazi wake au babu yake na awe mwadilifu, na iwe kuna masilahi katika kumwozesha mtoto huyo, na katika uozeshaji wa mwanamke awepo walii wake mwadilifu kwa kuhudhuria waadilifu wawili, na ikiwa moja kati ya masharti haya litakiukwa basi hautasihi uhalalishaji wake kwa kuharibika ndoa hiyo.
Aina za Upatanishaji unaozuiwa kwa kwenda kwake kinyume na Wanazuoni wote: Ni mtu kumuoa mwanamke bila ya mahari, walii au mashahidi, kwa kuiga kila madhehebu katika yale ambayo mwingine hayazungumzii, huu ni upatanishaji unaopelekea uharamu, kwani unaenda kinyume na Wanachuoni wote, na hakuna yeyote miongoni mwao aliouzungumzia.[22]
Na katika aina zilizoharamishwa ni upatanishaji uliokatazwa unaohusiana na Haki za Mwenyezi Mungu au haki za jamii kwa ajili ya kulinda mfumo mkuu wa sharia na kwa kujihimiza na uchungaji wa masilahi ya watu wote. Vilevile haijuzu kuleta upatanishaji katika vitu vilivyopigwa marufuku vinavyohusiana na haki za waja, kwa maana ya haki ya watu maalumu, kama zuio la kushambulia haki za watu na kuwasababishia madhara na kuwafanyia uadui.
Na vilevile: Adhabu za Kisharia, kama vile Adhabu maalumu na adhabu zinazokadiriwa na Makadhi, na kutoa Zaka ambako ni wajibu kisharia kama vile kutoa sehemu ya kumi na mazao, na kulipa kodi ya ardhi, na kulipa sehemu ya tano ya madini yaliyogundulika, na masuala ya ndoa. Kwa hiyo, mikataba ya ndoa na yanayoifuatia miongoni mwa aina za mtengano wa wanandoa: lengo lake ni furaha ya wanandoa wawili na watoto wao. Na hili linawezekana kutokea kwa kulinda mfungamano wa wanandoa, na kuwa na maisha mazuri ndani ya ndoa, kama ambavyo Qur'ani Tukufu inavyosema: {T'alaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa wema} [AL BAQARAH 229]
Kwa hivyo kila kinachoiunga mkono hii asili kinafanyiwa kazi, hata kama kitapelekea katika baadhi ya matukio Upatanishaji unaojuzu, ama ukichukuliwa upatanishaji kama kisingizio au njia ya kupenyea kwa ajili ya watu kuchezea masuala ya ndoa na talaka, basi hapo inakuwa Upatanishaji mwovu unaozuiwa. Ni lazima kuchunga msingi wa kisheria: Nao ni kwamba Asili katika mambo ya ndoa ni uharamishaji kwa lengo la kuchunga haki za wanawake na nasaba.
Matendeano, na matumizi ya fedha, na adhabu zilizowekwa na sharia na visasi kwa ajili ya kulinda Damu na mfano wake miongoni mwa mambo ya majukumu yanayotumika kuyachunga ndani yake masilahi ya Watu na Taasisi muhimu, na kwa hiyo ni wajibu kuchukua ndani yake kila madhehebu yale yaliyokaribiana na masilahi ya watu na furaha yao, na kama italazimika kufanya upatanishaji, kwa namna ambayo ndani yake kuna juhudi za kuunga mkono masilahi ambayo Sharia inayakusudia.
Na kwamba masilahi ya watu yanabadilika kwa kubadilika zama na mila na desturi zao na makuzi ya ustaarabu na ujenzi miji. Na kigezo cha masilahi au uainishaji wa kinachokusudiwa ndani yake: ni kwamba kila kinachojumuisha utunzaji wa Misingi Mikuu Mitano ya Asili: ambayo ni kuilinda Dini, Nafsi, Akili, Kizazi/Ukoo na Mali. Na kulinda kila masilahi yanayolengwa kisharia kutoka katika Qur'ani na Sunna na Ijmaa ya Wanachuoni. Nayo ni masilahi Mursala yanayokubalika.[23]
Na kuna anayegawa kwa zingatio jingine na anasema: Sehemu ya Kwanza: Upatanishaji baina ya hukumu kuu bila ya kuangalia hukumu ndogo ndogo kama vile mfano wa yule anayemuiga Abu Hanifa katika ndoa ya bila ya Walii wa mwanamke na akamwiga Shafi katika hukumu zingine zilizobakia za ndoa bila ya kuangalia suala la ndoa bila ya Walii kwa sehemu yake japo ndogo.
Sehemu ya Pili: Upatanishaji baina ya madhehebu kwa kuhama hama baina ya madhehebu hayo na haya katika kauli yake ni mengi mno kwa wanachuoni na Alqaraafiy ameyataja hayo kwamba hiyo inajuzu kwa masharti matatu:
Ni kutokusanya baina ya madhehebu kwa sura inayoenda kinyume ya wote kama vile mfano wa yule aliyeoa bila ya kutoa mahari au bila ya walii wa mwanamke au bila ya mashahidi.
Kwamba Aamini katika yule aliyemfuata na kumwiga kuwa ni fadhila.
Asiwe anataka kufanya hivyo kwa ajili ya ruhusa.
Na ikiwa ya kwanza katika mfano huu wa zuio ni kwa ajili ya kuzipa pengo fulani la mlango wa kuchezea chezea Sharia lakini kama itatokea hivyo kwa makubaliano basi haizuiliki isipokuwa pindipo itakapoonekana ya kwamba Mwigaji anawajibika kufuata madhehebu maalumu na hili ni suala ambalo ni mashuhuri sana na kilichosahihi ndani yake ni kutokuwepo wajibu wa hilo.
Sehemu ya Tatu: Hukumu zinachaguliwa kwa ajili ya kuzitekeleza katika suala moja na hii ndio njia iliyotajwa hapo kabla katika sura ya tatu nayo zaidi inanasibishwa na hitilafu katika uhalisia wake baina ya wanachuoni.
Na ikibainika katika yaliyotangulia basi watu wa elimu wamehitilafiana katika Upatanishaji kwa kauli mbili: Na wanachuoni wa zama za karibuni wengi wao wamezuia Upatanishaji wakishurutisha kusihi kwa uigaji na kutopatanisha na baadhi yao wakasema: kutofuatani ruhusa, na inaambatana na uhakika wowote pale ausemapo mmoja wao na vilevile usahihi wa Mwigaji unaaminika na kwa hitajio la kuiga kwake idadi imetimia.[24]
Ya Kwanza: Zuio lisilo na kikomo.
Ya Pili: Kujuzu.
Kwanza: Dalili za wale wasemao: Zuio lisilo na kikomo;
Kwamba hakika mambo yalivyo ni kuzua kauli ya tatu pale wanachuoni wanapopishana katika hukumu ya suala fulani, kwa wanachuoni wengi ni kwamba: Haijuzu kuleta kauli ya tatu.[25]
Kauli ya kujuzu kwake inapelekea katika mgongano na kutoka katika udhibiti kwa namna ambayo majukumu hayatulizani ipasavyo kama ambavyo inapelekea katika ufunguzi wa mlango wa Haramu na uharibifu wa mfumo wa Sharia na kila kinachopelekea katika Haramu na chenyewe ni Haramu.
Kuna Ijmaa ya wanachuoni juu ya zuio la Upatanishaji.[26]
Na Kauli ya Pili: ni kujuzu. Na wametoa dalili kwa:
Kitendo cha Maswahaba wa Mtume R.A, ambapo Mufti katika wao alikuwa anamuuliza Mujtahid katika suala fulani kisha anatafuta kulifutu kwa mwingine na hakuna yeyote aliyekana kitendo hicho na huu ndio ukweli wa upatanishaji katika kuiga, kama ambavyo haikunukuliwa kutoka kwa Maswahaba wa Mtume S.A.W, pamoja na Taabiina kwamba walimlazimisha mtu yeyote kuchukua madhehebu ya Mujtahid katika kauli zake zote ili ajikute katika upatanishaji.
Hakika kauli ya kuzuia kwake analazimika nayo ulazima wa ubatili kama vile:
kuondoka kwa faida ya kuiga.
Kwamba hatua hii inavunja yaliyokwishaamuliwa ya kuwa kwamba Wanachuoni wote wako katika uongofu kwa yale wanayojitahidi ndani yake iwapo watapita njia ya jitihada sahihi na hii inatengua hali ya kuwa hitilafu ni rehma.
Hakika jambo hili linapingana na wepesi wa Sharia.
Hakika jambo hili litapelekea kuharibu ibada za waja na matendeano yao.
Hakika mambo yalivyo ni kuwa hakuna kinachozuia kiakili au kisharia na kwa ajili hiyo asili yake ni kujuzu.[27]
Mjadala wa Dalili za makundi mawili:
Ama kuhusu wasemao kwa kuzuia:
Dalili yao ya kwanza ni: Hakika kwamba hiyo ni kuleta kauli ya tatu na hilo halijuzu. Kwani Upatanishaji sio uletaji wa kauli ya tatu kwani huko sio kuja na hukumu mpya bali uhakika ni kwamba haikutoka nje ya kauli mbili za awali, kwa hivyo Mpatanishaji hakuja na kipya.
Dalili yao ya Pili ni: Kauli ya kujuzu kwake inapelekea katika mgongano na kutoka katika udhibiti kwa namna ambayo majukumu yake hayatulizani kama ambavyo pia inapelekea kufungua mlango wa Haramu na kuharibu mfumo wa Sharia na kila kinachopelekea katika haramu nacho ni haramu.
Na hili hakika ya mambo yalivyo ni kwamba linadhibitika kwa sisi kuweka sharti katika Upatanishaji ya kutofuata Ruhusa kwa matamanio katika kuchukua Hukumu. Nayo wakati huo inakuwa haina uharibifu ndani yake.
Dalili yao ya Tatu ni: Ijmaa ya Wanachuoni: Ni madai ya Ijmaa ya Wanachuoni juu ya kuzuia Upatanishaji, kuna mtazamo.
Na hiyo ima ni kwa kuzingatia madhehebu kadhaa, au kwa kuzingatia kilicho zaidi, au kwa kuzingatia usikivu, au kwa kuzingatia makisio, kwani kama ingelikuwa suala hili limekusanywa basi Wanachuoni wa Fiqhi wa madhehebu mengine wangelilizungumzia kwa pamoja, kwani kilichozungumzwa na wanachuoni wote hapana budi kiwe mashuhuri tena wazi baina ya watu wake kimeelezwa vyema na wala haitoshi kukinyamazia na kukisia na hakuna dalili yenye nguvu kuliko hivyo kutoafikiana zaidi kuliko uhitilafiano wazi wa wengi wa wanavuoni wa kisasa.[28]
Na mimi nitataja hapa kwa ufupi kauli za Wanavyuoni wa madhehebu katika kuhalalisha kwa Upatanishaji:
Wanavyuoni wa Kihanafi: Al Kamal Bin Al Hamam na mwanafunzi wake Ibn Amir Al Haj wameema katika kitabu cha At Tahrir na Sharhu yake.[29] Hakika mwigaji anapaswa kuiga atakavyo, na mtu wa kawaida achukue katika kila suala kauli ya Mujtahid iliyo nyepesi kwake, sielewi kinachozuia kunukulu au akili, na kwa kuwa mtu hufuata kilicho na wepesi kwake miongoni mwa kauli za wanachuoni wanaojitahidi, sijawahi kujua Sharia zinazozuia jambo hili kwa kulisema vibaya, na Mtume S.A.W, alikuwa anapenda kuurahishia umma wake.
Na yamekuja katika Kitabu cha Tanqiihul Fataawaal Haamidiyah cha Ibnu Aabidiin, [30] maelezo yanayomaanisha kuwa katika nia ya Mufti kuna kinachomaanisha kujuzu kwa hukumu iliyopandanishwa, na kwamba Kadhi Twarsuur aliyefariki mwaka wa 758 Hijiriyah amefuata kujuzu kwake. Na Mufti wa Rum Abu Suudil Amaadiy aliyefariki mwaka wa 983 Hijiriyah katika Fatwa zake amejuzisha. Na Ibnu NAjiim Mmisri aliyefariki mwaka wa 970 katika risala yake inayohusu uuzaji wa mali ya Wakfu ametaja kuwa Madhehebu yake yanajuzisha Upatanishaji, na akanukulu kutoka katika Fatwa za Albazaziyah. Na Amir Bad Shaah aliyefariki dunia mwaka wa 972 anaona kuwa inajuzu kupatanisha kwa nguvu zake zote. Na Mufti wa Nablus Munib Afande Hashimi aliandika risala yake katika Uigaji mwaka wa 1307 Hijiriya na ndani ya risala hiyo akaunga mkono Uigaji bila kikomo, na akasema mwanachuoni wa zama zake Sheikh Abdul Rahman Bahraawiy: Kwamba Mtunzi amebainisha vyema ukweli.
Na Ufupisho ni kwamba: Kilichoenea na kuwa mashuhuri ni kuwa Upatanishaji ni batili, lakini Wanachuoni wanaona kinyume na hivyo na kwamba Upatanishaji unajuzu kwa dalili nyingi mno zinazouzungumzia usahihi wake.
Wanavyuoni wa Kimaliki: Na kilicho sahihi zaidi na kinachokubalika kwa Wanachuoni waliokuja baadaye wa Madhehebu ya Maliki ni kujuzu Upatanishaji, kwani Ibnu Arafa wa Madhehebu ya Maliki amerekebisha katika kitabu chake cha ushereheshaji wa Sharhul Kabiir cha Dardiir, na akatoa Fatwa Mwahachuoni Mkubwa Aladawii kujuzu kwake, naye Mwanachuoni Dusuqi akajuzisha, na Amirl Kabiir akanukulu kutoka kwa Mashekhe zake kwamba Usahihi wa Upatanishaji ni kuivunja kwake.
Wanavyuoni wa Kishafi: Baadhi yao wamezuia aina zote za upatanishaji, na baadhi yao wakaishia katika kuzuia hali za upatanishi zilizokatazwa na ambazo ufafanuzi wake utakuja baadaye, na baadhi yao wakajuzisha upatanishaji kama utakusanywa katika suala moja kwa masharti ya Madhehebu yanayoigwa.
Wanavyuoni wa Kihanbali: Twarsuus amenukulu ya kwamba Makadhi wa Madhehebu ya Hanbali walitekeleza hukumu ya upatanishaji.[31] na waliojuzisha waliweka masharti ya kusihi kwake: 1-Ni kwamba yule anayepatanisha asikusudie kufuata ruhusa kwani kufanya hivyo kunakatazwa na wanachuoni wote.[32] 2- pasiwepo katika upatanishanji huo muundo wa kauli unaokubaliana na ubatili wake. 3- kutorejea katika kuutumia upatanishaji kwa kuiga. 4- Ni yeye kuitikadi usahihi wa Kauli anayoihamia kwa sababu ya nguvu ya dalili yake, na hapo upatanishi unakuwa kwa kuwepo kauli sahihi zaidi na baadhi ya wanachuoni wameirudisha sharti hii ya kutokuwa na uwezo wa mwigaji kuelewa kilicho sahihi zaidi ya kilicho sahihishwa kwa kutokuwa kwake na elimu yakutosha. 5- kwamba upatanishaji huo usipelekee utenguzi wa hukumu; kwani kufanya hivyo kunapelekea katika mgongano wa kuhukumu na kutotulizana kwake: na baadhi ya wanachuoni wakaweka masharti ya kuwepo sababu za dharura yake na wengi hawakushurutisha.
Na ufupisho wa yote ni kwamba: Hakika udhibiti wa kufaa kwa Upatanishaji au kutofaa kwake ni kwamba kila kinachopelekea kuvunja nguzo za Sharia na kuangamiza sera zake na hukumu zake kimeharamishwa na kinakatazwa, na hasa zile hila za kisharia zilizokatazwa. Na kwamba kila kinachounga mkono nguzo za Sharia, na kila kinachotupiwa juu yake hekima na sera yake kwa ajili ya kuwafurahisha watu duniani na akhera kwa kuwepesisha Ibada juu yao. Na kulinda masilahi yao katika miamala, basi hilo linajuzu.
Utafiti huu umeletwa na Mtafiti Hatem Yusuf Muhammad.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.
[1] - Tazama: Kitabu cha: Al Faqiih Al Mutafaqeh, kwa Al Khatwebu Al Baghdadiy 404/1, Na Kitabu cha Al Maqaswed Al Hasanah kwa As Sakhawiy 70/1.
[2] - Tazama kitabu cha: Kasfu Al Khafaa 67/1.
[3] - Tazama: Kitabu cha: Al Faqiih Al Mutafaqeh 404/1.
[4] - Rejeo lenyewe lilopita.
[5] - Kitabu cha: Kashfu Al Khafaa 66/1
[6] - Tazama Kitabu cha: Al Maqaswed Al Hasanah kwa As Sakhawiy 65/1
[7] - Imetolewa na Al Bukhariy 38/1, Na Muslim 141/5
[8] - Tazama kamusi ya: Taji Al A'arus toka Jawaher Al Qamuus 361/26, Na kitabu cha: Al Mu'jam Al Wasetw 283/2, na Kitabu cha: Tahzeebu Al Lugha 228/3, na kitabu cha: Mukhtaar As Swahah 612/2.
[9] - Tazama kitabu cha Al Mughniy kwa Ibn Qodamah Al Maqdisiy 227/1
[10] - Tazama kitabu cha: Fat-hu Al Qadeer 435/4
[11] - Tazama kitabu cha: Adhwaa Al Baiaan katika Iydhaah Qura'ni kwa Qur'ani 214/21
[12] - Tazama gazeti la Baraza la Fiqhi ya Kiislamu 33/8, na Fiqhi ya Kiislamu na Dalil zake 85/1
[13] - Tazama kitabu cha: Al Mausoa Al Fiqhiyah 293/13
[14] - Tazama kitabu cha: Al Ijtihadi wa madaa Hajatinah Ilaihi , Dkt. Said Muhammad Musa 549
[15] - Tazama maazimio ya Baraza la Kifiqhi zama ya nane, Uk. 160.
[16] - Tazama kitabu cha: Al Fiqh Al Islamiy na Dalili zake 85/1, na kitabu cha: Aomedat At Tahaqiq fi At Taqlid wa At Talfiq kwa Al Baniy 91.
[17] - Tazama kitabu cha: Al Fiqh Al Islamiy na Dalili zake 86/1
[18] - Kitabu cha: Aomdatu At Tahqiq Uk. 104, na Kitabu cha Ar Rkhsah As Shari'ah Dkt Omar Abdullah Kamel 217
[19] - Kutoka matamshi ya Ibn Ar Rumiy, yamenukuliwa na Al Imam Azu'biy katika kitabu cha Seir A'lam An Noblaa 459/3.
[20] - Tazama kitabu cha: Aomdatu At Tahqiq Uk. 121
[21] - Tazama kitabu cha: At Talfiq katika Al Ijtihadi wa At Taqlid Uk. 16
[22] - Kitabu cha : Sharhu At Tanqieh kwa Al Qarafiy Uk, 386
[23] - Kitabu cha: Al Fiqh Al Islamiy na Dalili zake 93/1
[24] - Kitabu cha: Aomdat At Tahqiq kwa Al Baniy, Uk. 183
[25] - Wenye zama moja wakihitilafiana katika suala juu ya kauli mbili, basi inajuzu kwa wengine kuzuka kauli ya tatu, na katika jambo hilo maoni matatu: ya kwanza: Zuio lisilo na kikomo, na juu yake Jamhuri wa wanavyuoni. Ya Pili: ni kujuzu bila ukomo na katika hili kuna kundi la Wanachuoni wa Madhehebu ya Hanafi na Shia pamoja na Dhwahiriy, na Ya Tatu: Nayo ni kweli kwa Wachuoni waliokuja baadae akiwemo Imamu na wafuasi wake Al-Amidiy ya kwamba Tatu ni kulazimika kuondosha kile walichokusanyika nacho katika hukumu hakikujuzu kuileta kwake na kufupisha mfano wa Matumaini pale mtu anapofariki na akaacha babu na nduguze baadhi ya Wanachuoni wanaona ya kwamba kuna kushirikiana, na wengine wanaona ya kwamba ndugu wanadondoshwa kwa kuwepo Babu na kama angelisema kwa kumuangusha Babu basi kauli yake isingelijuzu kwani yeye anakuwa ni mwenye kulinyanyua jambo la ambalo wanachuoni wote wameafikiana na kwa kunufaika na kauli ya wanachuoni wa zamani nalo ni kwamba Babu anaweza akawa yuko peke yake au akashirikiana na ndugu, na ikiwa tutamdondosha babu tutakuwa tumeondosha jambo walilokubaliana wanachuoni wote, na mfano huu mwandishi Imamu pamoja na Alaamidiy nao ni sahihi, Tazama kitabu cha: Al Ibhaaj 2075/5, Al Ahkaam kwa Al Amaadiy 329/1, At Taqreer wa At Tahbeer 141/3, Al Mahswul kwa Ibn Al Arabiy 132/1, Al Mahswul kwa Ar Raziy 197/4, Al Maswadah 292/1, na Rawdhat Ak Nadher 149/1.
[26] - Tazama kitabu cha: Rasmu Al Mufti katika Hashiyat Ibn Abdeen 69/1, na kitabu cha: Al Ahkaam fi Tameez Al Fatawa an Al Ahkaam kwa Al Qarafiy, Uk. 250
[27] - Kitabu cha: Aomdatu At Tahqiq K.98-105, At Tahqiq fi Butwlaan At Taufiq K 160-169, "At Tankiil" kwa Al Mua'limiy 384/2
[28] - Kitabu cha: Aomdatu At Tahqiq Uk.106
[29] - Tazama kitabu cha: At Taqrir wa At Tagrir fi Elimu ya Ak Oswul 469/3.
[30] - Kitabu cha: Al Uquud Ad Duria fi Tanqiyh Al Fatawa Al Hamediyah 109/1
[31] - Kitabu cha: Rasmu Al Mufti 69/1, At Tahrir wa Sharhuh 350/3 na yanayoifuatia,. Al Ihkaam fi Tamiiz Al Fatawa an Al Hakaam kwa Al Qarafiy uk.250 na unaoufuatia, Aomdat At Tahqiq fi At Taqlid wa At Talfiq kwa Al Baniy Uk. 106 na unaoufutia, Mkutano wa Kwanza kwa Baraza Kuu la Utafiti wa Kiislamu, Utafiti wa Sheikh Profesa AS Sanhuriy Uk. 83 na unaoufuatia, Na Utafiti wa Sheik Abdulrahmaa Al Qalhuud Uk. 95 na uanaoufuatia.
[32] - Tazama yaliyoyataja Ibn Abdulbar katika Kitabu cha: Jame' Bayan Al Elmu wa Fadhlahu 91/2, Na Ibn As Swalah katika kitabu cha: Adabu Al Mufti Uk.125, Na Ibn Hazm katika kitabu cha: Marateb Al Ijmaa' Uk. 87, Na As Shatwebiy katika kitabu cha: Al Muafqaat 140/4.