Matumizi katika Njia ya Mwenyezi Mu...

Egypt's Dar Al-Ifta

Matumizi katika Njia ya Mwenyezi Mungu

Question

Matumizi katika Njia ya Mwenyezi Mungu 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, shukrani zote anastahiki Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimuendee Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W

Baada ya Utangulizi…

Utafiti huu ni katika kuelezea matumizi katika njia ya Mwenyezi Mungu na maelezo ya Madhehebu ya Wanachuoni katika hili.

Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema:

{Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni wajibu uliowekwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hekima} [AT TAWBAH: 60].

Neno njia katika lugha: Ni njia na vinavyopambanua njia hiyo, na njia ya Mwenyezi Mungu: Ni njia inayolingania kwake ([1]), kwani kila njia iliyotakiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni wema unaingia katika njia ya Mwenyezi Mungu ([2]).

Ibn Al-Athiir amesema: Njia kwa asili: Ni njia inayopelekea huchukuwa dhamira ya neno la kike na kiume japo kuwa mara nyingi huchukuwa dhamira ya kike, na hii njia ya Mwenyezi Mungu ni pana zaidi inapatikana katika kila matendo yaliyofuata njia ya kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutekeleza mambo ya faradhi au lazima na yale ya Sunna na aina mbalimbali za kujitoa, mara nyingi hutumika kwa maana ya jihadi, hutumika sana katika maana hiyo mpaka imekuwa kana kwamba inahusishwa na jihadi tu ([3]).

Ama kwa upande wa maana ya kimsamiati kusudio la matumizi katika njia ya Mwenyezi Mungu, Wanachuoni wa zamani na wa sasa kumekuwa na Madhehebu, nayo ni kama yafuatayo:

SOMO LA KWANZA

Ufafanuzi wa matumizi katika njia ya Mwenyezi Mungu katika Madhehebu manne yanayofuatwa.

Madhehebu ya Imamu Abu Hanifa:

Kauli inayotegemewa ndani ya Madhehebu ya Abu Hanifa ni kuwa kusudio la matumizi “Katika njia ya Mwenyezi Mungu” ni kupigana vita ([4]), nayo ni kauli ya Imamu Abi Hanifa, na kauli ya Abi Yusuf pia, kwa sababu njia ya Mwenyezi Mungu pindi inapoitwa hivyo katika mazoea ya Sharia hufahamika hivyo ([5]), kisha kuna tofauti ndani ya Madhehebu: Muhammad anaona kuwa kusudio lake upande wa Hija, kutokana na yaliyopokelewa kuwa mtu mmoja alimtoa ngamia wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ndipo Mtume S.A.W akamuamrisha ngamia atumike kubeba Mahujaji ([6]), na imenukuliwa na Ibn Aabidiin katika kitabu chake Fatwa ya dhwahiiria kuwa kusudio lake ni kutafuta elimu ([7]), wakati ambapo Al-Kasaany anaona kuwa njia ya Mwenyezi Mungu ni ibara ya mambo yote yanayokuweka karibu na Mwenyezi Mungu, ndani yake anaingia kila mwenye kufanya juhudi na hatua katika kumtii Mwenyezi Mungu na katika njia ya mambo ya kheiri akiwa mwenye kuhitaji ([8]).

Pamoja na hayo lakini wanakubaliana mambo mawili:

Jambo la kwanza: Ni kwamba umasikini na kuhitaji ni sharti la lazima la kustahiki kila mwenye kuzingatiwa yupo kwenye njia ya Mwenyezi Mungu, ni sawa sawa ikiwa ni mpiganaji vita au mwenye kuhiji au mtafuta elimu au mwenye kuiendea njia ya Mwenyezi Mungu kwa mambo ya kheiri.

Ibn Najeem anasema katika kitabu cha Al-Bahri: “Wala haijifichi kuwa kigezo cha umasikini ni lazima kwenye sura zote” ([9]).

Wakachukuwa dalili ya hilo kauli ya Mtume S.A.W pale aliposema:

 “Haifai sadaka kumpa mtu tajiri” na kauli yake S.A.W:

 “Nimeamrishwa kuchukuwa sadaka kwa matajiri wenu na kuwapatia masikini wenu”, “Hapa dalili – kama alivyotaja Al-Kasaany – ni kuwa Mtume S.A.W amewaweka watu makundi mawili: Kundi moja huchukuliwa zaka kutoka kwao, na kundi la pili hupewa zaka, lau kama ingefaa kutumika sadaka kwa kumpa tajiri basi mgawanyo ungebatilika na hili halifai” ([10]).

Limejadiliwa hilo: Kuwa hiki kigezo kimebatilishwa kwa kuwa “Njia ya Mwenyezi Mungu” ni aina inayojitegemea, ambapo imerudishwa kwenye aina ya kwanza, nao ni Mafakiri na Masikini ([11]).

Kama yanavyojadiliwa yafuatayo:

Kwanza: Sharti la umasikini katika vita ni sharti halipo, mwenye kufikiri kigezo cha umasikini anapaswa kuleta dalili.

Pili: Limekuja tamko la wazi na sahihi linaonesha kufaa kumpa sadaka mpiganaji tajiri, kutoka kwa Atwaa Ibn Yasar kutoka kwa Abi Saidi Al-Khudry R.A amesema: Mtume S.A.W amesema:

 “Si halali sadaka kumpa tajiri isipokuwa kwa mambo matano: Mwenye kusimamia, au mpiganaji katika njia ya Mwenyezi Mungu, au tajiri aliyenunua kwa mali yake, au masikini amepewa sadaka kisha akatoa zawadi kwa tajiri au mwenye deni” ([12]).

Tatu: Masikini anachukuwa Zaka kwa nafasi yake, ama mpiganaji katika njia ya Mwenyezi Mungu kuchukuwa kwake kuna masilahi kwa Waislamu, kwa sababu anatetea Uislamu na Waislamu, An-Nawawy amesema katika kitabu cha Al-Mujmuui: “Amesema mtunzi kwa maana ya Shiirazy na watu wake: Hupewa mpiganaji vita pamoja na umasikini na utajiri kwa ushahidi wa Hadithi iliyopita kwa maana Hadithi ya Abi Saidi iliyotangulia kutajwa, kwani ndani yake kuna masilahi kwa Waislamu” ([13]).

Nne: Mwenyezi Mungu Mtukufu amewafanya mafakiri na masikini makundi mawili, hakuna faida kutaja makundi sita ambayo yametajwa baada ya makundi hayo mawili kwani inakuwa ni kurudia ambako hakuna maana.

Al-Kasaany ameelezea kwa kusema: “Kuvuliwa kwa mpiganaji vita kunachukuliwa hali ya kuwepo mahitaji na kuitwa tajiri kwa kuzingatia hali iliyokuwepo kabla ya kuwepo kwa mahitaji, nayo ni kuwa tajiri kisha akatokewa na mahitaji pamoja na kuwa na nyumba yake ya kuishi vitu mavazi ya kuvaa pesa kiasi cha kuwa hastahiki kupewa sadaka, kisha akaadhimia kutoka kwenda vitani akawa ni mwenye kuhitaji vifaa vya safari yake pamoja na silaha atakazotumia vitani na kipando atakachopigania vita pamoja na mtumishi wa kumsaidia ambaye hakuwa mwenye kumuhitaji wakati wa kuishi kwake nyumbani, katika hali hii inafaa kupewa zaka au sadaka itakayomsaidia kwenye mahitaji yake ambayo yatakuwepo kwenye safari yake, naye akiwa ni tajiri kwa mali anazomiliki ni si muhitaji akiwa nyumbani kwake lakini ni muhitaji akiwa safarini ndipo inapofanya kazi kauli ya Mtume S.A.W:  “Si halali tajiri kupewa zaka isipokuwa akiwa vitani kwa ajili ya kupigania njia ya Mwenyezi Mungu” kwa aliyekuwa tajiri kwake hupewa baadhi ya mahitaji ya safari yake kwa ajili ya dharura yeyote safarini hivyo anapewa wakati wa kupewa akiwa tajiri, vile vile kuitwa mwenye deni ni tajiri katika Hadithi ni kwa kuzingatia hali aliyokuwa nayo kabla ya kuwa na deni kwani alikuwa na mahitaji ndio ikawa sababu ya hili deni, kwani tajiri ni jina la mwenye kujitosheleza kutokana na anachomiliki ambapo alikuwa hivyo kabla ya kutokewa na mahitaji ama baada ya hapo hapana” ([14]).

Jambo la Pili: Ni kuwa Zaka ni lazima kumilikiwa na mtu hivyo haifai kuitumia kwa ajili ya ujenzi.

Katika kitabu cha Durru Al-Mukhtar na Hashiyatu Ibn Abidiin imesemwa: “Inashurutishwa matumizi ya zaka kuwa ni miliki na si uhalali, hivyo haipaswi kutolewa Zaka kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti na mfano wake kama vile kujenga Mabwawa ya maji, Manywesheo, Matengenezo ya barabara, Mifereji ya mito ya maji, mambo ya Hija, jihadi na yote yasiyomilikiwa kama vile kukafini maiti na kumlipia deni lake” ([15]).

Linazungumziwa hili kuwa lina mtazamo, kwa sababu ugawaji ambao umelezewa na Qur`ani Tukufu kwa herufi ya “Fii” hakuna sharti la umiliki, tofauti na kielezo cha herufi “Laam” ya umiliki, kutokana na hilo wapo Wanachuoni waliotoa Fatwa ya kufaa kugawa Zaka ili kuachiwa huru mtumwa na kumlipia deni maiti katika mali ya Zaka pamoja na kutokuwepo umiliki, kisha umiliki unafikiwa kwa kupewa Zaka msimamizi wa mambo ya watu na wala sio lazima mmiliki kuiweka Zaka mkononi mwa masikini, ikiwa atapewa kiongozi au makamu wake basi anaweza kuitumia au kuigawa katika mambo haya ([16]).

Madhehebu ya Imamu Maliki:

Wamekubaliana watu wa Madhehebu ya Imamu Maliki kuwa “Njia ya Mwenyezi Mungu” inaendana na kupigana vita, jihadi na yaliyo na maana hiyo kama vile Farasi, na wanaona yafaa kumpa Zaka au Sadaka mpiganaji na mpiganaji mpanda Farasi hata kama watakuwa ni matajiri, na Jamhuri wamepitisha matumizi au ugawaji wa Zaka katika masilahi ya jihadi kama vile kununulia silaha, Farasi, Meli ya kivita, uzio na mfano wake, wala hawajahusisha matumizi kwa watu wa jihadi tu, wala hawakuweka sharti la umiliki wa Zaka kwa watu maalumu.

Mtazamo wa watu wa Madhehebu ya Imamu Maliki unakubaliana na maelezo ya Qur`ani kuhusu huu ugawajji kwa herudi ya “Fii” na wala si herufi ya “Laam” ya umiliki, kwa sababu uwazi wa maelezo haya ni matumizi kuwa katika masilahi ya jihadi kabla ya kuwa kwa wapiganaji jihadi.

Sheikh Dardiir anasema katika sherehe yake kubwa ya kitabu cha Mukhtasar Khalil: “Akaashiria kwa kauli yake “Na mpiganaji jihadi” kwa maana mwenye kuwa ndani ya hiyo jihadi akiwa miongoni mwa waliowajibikiwa jihadi kwa sifa ya kuwa mtu huru, Muislamu, mwanamme, mwenye kubaleghe, mwenye uwezo wa jihadi, ndani yake naingia mpiganaji wa kutumia Farasi na zana zake kama vile upanga mshale ananunuliwa hata kama mpiganaji jihadi ni mtu tajiri wakati  anapigana vita kama vile mpelelezi anayepelekwa kwa ajili ya kuchunguza kasoro na aibu za adui na kutujuza hali hiyo atapewa fungu la Zaka hata kama atakuwa kafiri, hakuna fungu la Zaka kwa ujenzi wa ukuta pembezoni mwa nchi ili kujikinga na makafiri, wala fungu kutengenezea chombo cha kumpigia adui”.

Dusuqy amelezea katika kitabu chake kauli ya mtunzi katika sherehe hii “Hakuna fungu la Zaka kwa ajili ya ujenzi wa ukuta pembezoni mwa mji ili kuzuia makafiri, wala fungu la Zaka kwa ajili ya ujenzi wa chombo cha kupigana na adui” kwa kauli yake: “Hii ni kauli ya Ibn Bashiir, na ina karibiana na kauli ya Ibn Abdulhakim, kwao wao inafaa kutolewa fungu la kazi za ujenzi wa ukuta na chombo cha kivita, na Ibn Salaam akasema: Hiyo ni kauli sahihi, hivyo Al-Mawaq amepinga maelezo ya mtunzi kwa kuwa yanalenga kumjengea umaarufu Ibn Bashiir, na akasema: Hajaona kizuizi zaidi ya kauli ya Ibn Bashiir kuongezea na kujijengea umaarufu” ([17]).

Madhehebu ya Imamu Shafi:

Watu wa Madhehebu ya Imamu Shafi wanaona kuwa matumizi haya yanahusisha upande wa jihadi na wapiganaji jihadi, na wanaona inafaa kumpa mpiganaji jihadi kile kitakachomsaidia kwenye jihadi hiyo, hata kama ni tajiri, kwa sharti la kuwa mwenye kujitolea, kwa maana hana fungu au mshahara kwenye hazina ya taifa, na inafaa pia kugawa fungu kwa ajili ya mahitaji ya wapiganaji jihadi kama vile silaha na zana za kivita.

Katika kitabu cha Al-Minhaj na sherehe yake cha Khatibu Sharibiny: “Na njia ya Mwenyezi Mungu – Mtukufu – wapiganaji” wanaume wasio na majina katika kundi la mamluki bali wanajitolea kupigana vita ambapo wanafanya harakati na wakishughulishwa na kazi za mikono na utengenezaji hivyo wanapewa katika mali ya zaka pamoja na utajiri walionao kwa sababu ya ujumla wa Aya na kuwasaidia dhidi ya adui, tofauti na wanajitosheleza nao wakiwa mamluki majina yao yakiwa yamesajiliwa, hivyo hawapewi katika fungu la Zaka hata kama hawajitoshelezi kwa kauli ya wazi, bali ni lazima matajiri Waislamu kuwasaidia” ([18]).

Na katika kitabu cha Rawdha cha An-Nawawiy: “Ama mpiganaji vita hupewa gharama na mavazi wakati wa kwenda na kurudi na wakati wa kukaa vitani hata kama muda utakuwa mrefu, je hupewa gharama zote au kinachozidi kwa sababu ya safari? Kuna mitazamo miwili kama vile msafiri, hupewa kile ambacho anaweza kununua farasi ikiwa ni mpiganaji wa kutumia farasi, na atakacho nunulia silaha na zana za kivita, na vinakuwa ni miliki yake, na inafaa kukodiwa farasi na silaha, hali inakuwa tofauti kutokana na uwingi wa mali na uchache wake, ikiwa anapigana chini kwa miguu hawezi kupewa fungu la Zaka kununua farasi” ([19]).

  Madhehebu ya Imamu Hambal:

Watu wa Madhehebu ya Imamu Hambali wanaona kuwa kusudio la “Njia ya Mwenyezi Mungu” ni kupigana vita kwa kujitolea kwa wale ambao hawana mshahara, au wanacho kidogo kisichowatosha, hivyo hupewa mpiganaji jihadi miongoni mwao kile kinachomtosha vitani, hata kama atakuwa ni mtu tajiri, ikiwa hapigani vita kitarudishwa kile alichopewa, na mtazamo wao ni kuwa: Uzio kwenye eneo linalohofiwa adui kushambulia ni kama vita kamili vyote viwili ni katika njia ya Mwenyezi Mungu, masikini atapewa kinachomtosha nafsi yake kwa Hija au Umra au kitakachomsaidia kati ya ibada hizo mbili.

Katika sherehe ya kitabu cha Muntaha Al-Iradaat cha Bahwaty: “Mtu wa saba: Mpiganaji” kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  {Na katika njia ya Mwenyezi Mungu} bila ya kuwa na kitu au anacho kisichotosheleza kuingia vitani hivyo hupewa katika fungu la zaka hata kama atakuwa tajiri, kwa sababu ana haja kwa Waislamu anayohitajia kwa ajili ya kupigana kwake vita kwenda na kurudi, na kupewa thamani ya silaha ngao na farasi ikiwa ni mpiganaji farasi, na wala haitoshi ikiwa atanunua mwenye mali kisha akalipia kwa ajili ya vita, inakuwa ni kama kulipa thamani, na inatosha kupewa fungu katika mali ya zaka kwa ajili ya hija na umra hivyo hupewa kitakachomuwezesha masikini kuhiji au kufanya umra au kumsaidia katika ibada hizo mbili kwa Hadithi ya Mtume S.A.W:

 “Hija na Umra ni katika njia ya Mwenyezi Mungu” imepokewa na Ahmad ([20]), amesema katika kitabu cha Furuui: Kuwa farasi ni zana ya kivita hivyo haitoshi kununua kwa aliyewajibikiwa na kupewa fungu la Zaka farasi na kumfunga katika njia ya Mwenyezi Mungu au kununua nyumba anaitumia kivita kwa kutopea amri ya hilo, wala haitoshi kwa aliyewajibikiwa kupewa Zaka kupigana vita juu ya farasi au kwa ngao na mfano wake kwa mali ya Zaka aliyopewa, kwa sababu nafsi yake si yenye kupaswa kutoa Zaka yake, kama vile halipi deni lake, ama kiongozi anapaswa kununua farasi kwa Zaka ya mtu na kumtoa, kwa maana ya farasi kwa mwenye Zaka na kuingia vitani kwa sababu yeye hausiki kwa kule kutoa kwake Zaka na kumpa kiongozi, na kiongozi anaweza kurudisha zaka kwa mtu tuliyochukuwa kwake ikiwa hapigani vita mwenye kuchukuwa farasi au mfano wake kutokana na Zaka kumrudishia kwa kiongozi, kwa sababu amepewa kwa ajili ya kazi lakini hakufanya kazi, imenukuliwa na Abdillah: Pindi anapotoka katika kupigania njia ya Mwenyezi Mungu hula katika mali ya Zaka” ([21]).

Mazingatio ya jumla:

Tuliyoeleza kuhusu Madhehebu manne tunazingatia yafuatayo:

Kwanza: Jamhuri yao imekubaliana mambo matatu.

Jihadi ipo ndani ya njia ya Mwenyezi Mungu moja kwa moja.

Uhalali wa kutumika mali ya Zaka kwa watu wapigania jihadi, tofauti na kutumika kwenye masilahi ya jihadi na zana za zaka, kwani kumekuwa na tofauti kwa watu wa Madhehebu.

Kutofaa kutumika mali ya Zaka katika pande za kheri na marekebisho ya umma ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabwawa, kuanzisha Misikiti, shule, kurekebisha barabara, kukafinia maiti na mfano wa hayo, bali uzito wa mambo haya ni kutumika vyanzo vya hazina zingine kama vile mali zilizopatikana kwa makafiri bila ya kupigana vita na mali itakonayo na kodi za ardhi na zisizokuwa hizo.

Kwa hakika haifai kutumika Zaka katika mambo haya kwa kukosekana umiliki, kama anavyosema Imamu Abu Hanifa, au kwakuwa kwake nje ya pande nane za matumizi ya mali ya Zaka kama wanavyosema Maimamu wengine.

Pili: Yaliyonukuliwa kuhusu Al-Kasaany kutoka kwa Abu Hanifa kwenye tafasiri yake ya neno “Njia ya Mwenyezi Mungu” kwa ukaribu wa aina zote na utiifu, ameweka sharti la kumilikiwa Zaka na mtu, kwani haitolewi na kupewa pande za umma, kama alivyoweka sharti la mtu kuwa masikini, kwa maelezo haya mtazamo huu haupo nje ya wigo wa waliobanwa katika maana ya “Njia ya Mwenyezi Mungu”.

Tatu: Imamu Abu Hanifa ameelezea peke yake kuweka sharti la umasikini kwa mpiganaji jihadi, kama alivyoelezea Ahmad katika moja ya mapokezi mawili ya kufaa kutumika zaka kwa mtu masikini, ili kutekeleza ibada ya Hija au Umra au kumsaidia katika ibada hizo mbili, nayo ni kauli ya Madhehebu ya Imamu Hambali – kwa maana Ibada ya Hija imo ndani ya njia ya Mwenyezi Mungu.

Nne: Wamekubaliana Imamu Shafi na Imamu Hambali juu ya sharti la kuwa wapiganaji jihadi ambao wanachukuwa mali ya Zaka ni wale wanaojitolea sio wenye mishahara katika hazina ya nchi.

Tano: Wamekubaliana wote – tofauti na Imamu Abu Hanifa – juu ya uhalali wa kutumika mali ya Zaka kwenya masilahi ya jihadi kwa ujumla ([22]).

SOMO LA PILI

Wapanuzi wa maana ya “Njia ya Mwenyezi Mungu” wa zamani na wasasa.

Wanachuoni - zamani na sasa – wapo waliopanua maana ya “Njia ya Mwenyezi Mungu” wala hawakuishia kwenye jihadi na yanaoendana na jihadi, bali wamefasiri kwa maana pana zaidi ya jihadi, miongoni mwao wapo waliofanya inakusanya mambo yote yanayomuweka mtu karibu na Mola, na wengine wameifanya inakusanya masila yote ya umma, na hilo ni kwa mujibu wa hali ya neno kilugha, na wapo miongoni mwao waliosema inafaa kutoa mali ya Zaka katika fungu hili kwa mwenye kusimamia masilahi ya umma katika masilahi ya Waislamu na mfano wake, na wengine wapo walioingiza ibada ya Hija ni katika njia ya Mwenyezi Mungu, na yafuatayo ni maelezo na ufafanuzi wa hizi kauli.

Kwanza: Kauli ya kuwa “Njia ya Mwenyezi Mungu inakusanya mambo yote ya kheri:

Imamu Razy ameelezea katika tafasiri yake juu ya hilo na akasema: Fahamu kuwa maana ya wazi wa tamko katika kauli ya Mola Mtukufu:  {Na katika njia ya Mwenyezi Mungu} hapaswi kuhusisha kila mpiganaji vita tu, kisha akataja yaliyosemwa na Al-Qaffal akinukuu baadhi ya Wanachuoni: Ni kuwa wao wamepitisha matumizi ya Zaka katika mambo yote ya kheri kuanzia kukafini maiti kujenga ngome na kujenga Misikiti kwa sababu kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  {Na katika njia ya Mwenyezi Mungu} inakusanya na kujumuisha vitu vyote ([23]).

Linalofahamika ni kuwa Imamu Razy hakuleta maelezo zaidi katika nukuu ya Al-Qaffal jambo linalonesha kuegemea kwake, kauli kama hii imesemwa na Al-Kasaany Al-Hanafy katika kitabu cha Al-Badaaii kama ilivyoelezwa, isipokuwa sharti lake la mtu kumiliki Zaka, hivyo haiwezi tolewa Zaka kwa kupewa upande wa umma, na huyo mtu awe ni masikini kama ilivyoelezwa, umasikini ambao unamfanya kutokuwa nje ya mzunguko wa watu waliodhikika.

Na miongoni mwa aliyoyasema pia Sheikh Swiddik Hassan Khaan yamekuja katika kitabu cha Rawdah Nadiya: “Ama njia ya Mwenyezi Mungu, kusudio lake hapa: Ni njia ya kumuelekea Yeye Mola Mtukufu, na Jihadi – pamoja na kuwa ni miongoni mwa njia kubwa ya kumueleke Mola Mtukufu – lakini hakuna dalili ya kuhusisha hili fungu kwenye hilo, bali inafaa kugawa na kuitoa mali ya Zaka kwa kile iliyokuwa njia ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hii ndio maana ya Aya kilugha, na nilazima kusimama kwenye maana za kilugha ambapo hapa haifai kunukuu maana ya Kisharia, kisha akasema: Na katika jumla ya “Njia ya Mwenyezi Mungu” ni kugawa kwa Wanachuoni ambao wanasimamia mambo na masilahi ya Waislamu ya kidini, kwani wao wanafungu katika mali ya Mwenyezi Mungu, ni sawa sawa wakiwa ni matajiri au masikini, bali kugaiwa mali ya Zaka katika upande huu ni katika mambo muhimu sana, kwa sababu Wanachuoni ndio warithi wa Mitume na ndio wabeba dini, na kwao wao kunahifadhia kiini cha Uislamu na Sharia ya Bwana wa viumbe” ([24]).

Miongoni mwa wanaona hivyo pia ni Sheikh Jamalu Diin Al-Qaasimy kwani ametaja katika tafasiri yake yaliyotajwa na Imamu Razy kuwa maana ya wazi ya tamko halipaswi kuhusishwa na hali ya kupigana vita tu, na yaliyonukuliwa na Al-Qaffal kutoka kwa baadhi ya Wanachuoni katika hilo, kisha akataja kauli ya mwenye kitabu cha Taju: “Kila njia inayokusudiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu – nayo jambo jema- inaingia katika njia ya Mwenyezi Mungu” ([25]).

Akainyamazia nukuu hii wala hakuongeza maelezo yeyote, jambo linalonesha kutopingana nayo.

Wakachukuwa dalili ya hilo kuwa tamko “Katika njia ya Mwenyezi Mungu” ni pana, hivyo haifai kuhusisha baadhi ya watu bila ya wengine isipokuwa kwa dalili, na wala hakuna dalili juu ya hilo.

Pili: Kauli ya masilahi ya umma ni katika “Njia ya Mwenyezi Mungu”:

Madhehebu haya ya Sheikh Muhammad Rashid Ridhwa – Mwenye kitabu cha Al-Manaar – amesema katika tafasiri yake ya Aya ya matumizi ya mali ya Zaka: “Ukweli hapa ni kuwa njia ya Mwenyezi Mungu: Ni masilahi ya Waislamu wote ambayo masilahi hayo ni nguzo ya dini na nchi bila ya watu binafsi.

Kisha baada ya hayo akasema: Njia ya Mwenyezi Mungu inakusanya masilahi mengine halali ya umma ambayo yenyewe ndio yanasimamia mambo ya dini na nchi, ya kwanza yake na yaliyobora kutangulizwa ni maandalizi ya kivita kwa kununua silaha chakula cha askari vifaa vya kusafirishia na kuwaandaa wapiganaji, na hii ni kwa upande wa vita vya Kiislamu na majeshi ya Kiislamu ambayo yanapigana ili kuinua juu neno la Mwenyezi Mungu, na yameelezwa kama hayo na Muhammad Ibn Abdilhakam, lakini ambaye anaandaa wapiganaji baada ya vita atarejesha kwenye hazina ya taifa ikiwa kuna masalio yaliyobaki kama vile silaha farasi na visivyokuwa hivyo, kwa sababu havimilikiwi siku zote kwa kazi za kivita tu ambavyo vimepiganwa, bali vinatumika pia katika njia nyingine ya Mwenyezi Mungu, na vitabakia baada ya kuondoka kwa sifa ya hiyo njia ya Mwenyezi Mungu na kuingia katika majukumu mengine kama vile kwenye ujenzi wa mahospitali ya kijeshi, vile vile mambo ya kheri ya umma, ujenzi wa mabarabara na marekebisho, kujenga reli za kijeshi – si za kibiashara – pia ujenzi wa minara ya kijeshi na viwanja vya ndege za kivita ngome na mahandaki, na katika muhimu yanaogharamiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu ndani ya zama zetu hizi ni kuandaa walinganiaji katika Uislamu, na kuwapeleka kwenye nchi za kikafiri kupitia taasisi zilizoandaliwa zinazofadhili fedha kama wafanyavyo makafiri katika kusambaza dini yao ([26]).

 Mwenye kitabu cha Al-Manaar ni miongoni mwa waliokubaliana na yaliyoelezwa na Sheikh Mahmoud Shaltuot ambapo amefasiri “Njia ya Mwenyezi Mungu” kuwa ni: “Maslahi ya umma ambayo hayamilikiwi na mtu yeyote, na ambayo hayahusishwi kunufaika nayo yeyote, umiliki wake humilikiwa na Mwenyezi Mungu na wanufaika wake ni waja wa Mwenyezi Mungu, ya kwanza yake na iliyo na haki zaidi: Muundo wa kivita ambao unaondoa kwenye jamii uovu na kulinda heshima, inajumuisha vifaa na zana mbalimbali za kisasa ikiwa ni pamoja na hospitali za kijeshi na kiraia, inajumuisha pia kazi za ujenzi wa barabara, kupanua mtandao wa reli na isiyokuwa hiyo ambayo inafahamika na watu wa vita na viwanja vya vita, inajumuisha pia kuandaa kundi lenye weledi la Waislamu walinganiaji wanaonesha uzuri wa Uislamu na usamehevu wake, wanaofasiri hekima za Uislamu, wanafikisha hukumu zake, na kufuatilia shambulizi la adui kwa kuangalia misingi ya Uislamu inayopelekea kurudisha vitimbi vyao shingoni mwao, vile vile inakusanya kazi endelevu ambazo wanaendelea nazo Wahifadhi wa Qur`ani ambao wanasoma – na kusomewa – kama ilivyoteremshwa katika zama za kushushwa kwake mpaka hii leo, na mpaka siku ya malipo Mungu akipenda” ([27]).

Na kwa msingi huu imetoka Fatwa kwa mwenye kuuliza kuhusu kufaa kutumika fungu la zaka katika ujenzi wa Msikiti jibu lake limekuwa: “Msikiti ambao unaokusudiwa kuanzishwa kwake au kujengwa kwake ikiwa ndio Msikiti pekee kijijini au kukawa na mwingine lakini mdogo kwa idadi ya watu wake, na wanahitaji Msikiti mwingine, basi inafaa Kisharia kutolewa fungu la Zaka ili kujenga huu Msikiti au kuufanyia marekebisho, na kutumia fungu la Zaka kwa ajili ya Msikiti katika hali hiyo inakuwa ni katika matumizi ambayo yametajwa ndani ya Aya ya ugawaji wa Zaka iliyokuja ndani ya Suratu Tawbah kwa jina la “Njia ya Mwenyezi Mungu”.

Na hii imejengeka katika kuteua kuwa makusudio ya neno “Njia ya Mwenyezi Mungu” ni masilahi ya umma, ambayo wananufaika nayo Waislamu wote wala haihusishi mtu mmoja, inajumuisha Misikiti mahospitali vituo vya elimu viwanda vya chuma risasi na vifaa vingine ambayo manufaa yake yanarejea kwa wengi, na ninapenda kusema hapa kuwa masuala haya yanatofauti kati ya Wanachuoi (Kisha Sheikh akataja aliyonukuu kwa Imamu Razy katika tafsiri yake kwenye matumizi ya Zaka katika njia zote za kheri….) mpaka aliposema: “Haya ndiyo aliyoyapitisha na kuyatolea Fatwa, lakini pamoja na kutaja kigezo ambacho tumekitaja kwa upande wa Misikiti, nacho ni kipengele cha Msikiti kuwa Misikiti mingie hautoshelezi, na kama unajitosheleza kutumia mali ya Zaka kwa mradi mwingine usiokuwa Msikiti ni bora zaidi na kustahiki” ([28]).  

Wala hatujamuona yeyote kwa waliotangulia aliyesema mfano wa kauli hii isipokuwa aliyonasibisha Ibn Qudama katika kitabu cha Al-Mughny rai hii kwa Anas Ibn Malik na Hassan Al-Baswary ambapo amesema: “wala haifai kutumia mali ya Zaka kinyume na pande zilizotajwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu – kwa maana ya pande nane – Anas na Hassan wamesema: Kilichotolewa katika ujenzi wa madaraja na barabara ni Zaka, na ya kwanza ndio sahihi zaidi” ([29]).

Ibara hii imeonesha kufaa kutumia mali ya Zaka katika kuanzisha madaraja barabara na kufanyia marekebisho, kwani ni zaka inayokubalika…. Kwa maana inafaa na kukubalika.

Lakini Sheikh Qardhawy ameelezea kuwa maelezo yaliyopokelewa hapo mwanzo kutoka kwa Anas na Hassan yamepokelewa na Abu Ubaid katika kitabu chake cha mambo ya mali, lakini inaonesha maana nyingine, kwani Abu Ubaida amesema kuwa Muislamu pindi anapopita na Zaka yake kwa watu wa fungu la kumi na akaikabidhi basi inamtosha kuwa ni Zaka, na hawa watu wa fungu la kumi ni wale wanaohusika na kukusanya mali kwa amri ya mkuu wa nchi wanasimama kwenye madaraja na barabarani ili kuchukuwa kwa wafanya biashara wasikuwa Waislamu wanaoishi kwa amani pamoja na kwa watu wa dhima miongoni mwa Waislamu kile kilicho lazima kwao katika kodi za kibiashara, kwa zama za hivi sasa inafanana sana na mfumo wa “Ushuru wa forodha” kwani mara zote walikuwa wanasimama maeneo ya mipakani.

Maelezo ya Anas na Hassan pia yamepokelewa na Ibn Abi Shaibah katika kitabu chake kuwa wamesema: “Kilichochukuliwa kwake kwa ajili ya ujenzi wa madaraja na mabwawa ya maji hiyo ni zaka inayokubalika” katika mlango wa mwenye kusema: Huzingatiwa kilichochukuliwa na watu wa fungu la kumi, kama alivyofanya Abu Ubaida, na kwa maelezo haya hakusimami kunasibishwa rai ambayo ameitaja Ibn Qudama kwa Anas na Hassan Mola awe radhi nao ([30]).

Ama dalili ya watu wa kauli hii, imehusishwa na yaliyotajwa katika tafasiri ya neno “Njia ya Mwenyezi Mungu” kuwa ni masilahi ya umma, kama ilivyowazi kwenye maelezo yao.

Tatu: Kauli ya kumpa zaka mwenye kusimamia masilahi ya umma katika masilahi ya Waislamu na mfano wake ni katika “Njia ya Mwenyezi Mungu”:

Tofauti kati ya hii na kipengele kilichotangulia ni kuwa kilichotangulia kusudio lake ni masilahi ya umma wa Waislamu ambayo kwa masilahi hayo ndio muhimili wa dini na nchi bila  ya watu binafsi, kwani ndani yake hakuna umiliki wa watu, tofauti na hii kwani kusudio lake ni umiliki wa watu ambao wanasimamia masilahi ya umma katika masilahi ya Waislamu na mfano wake.

Katika kitabu cha Subuli-Salaam cha Swanaany: “Na hupewa mpambanaji ni yule mwenye kusimamia masilahi ya umma katika masilahi ya Waislamu kama vile kazi za kimahakama utoaji Fatwa na ufundishaji, hata kama atakuwa ni mtu tajiri, na Abu Ubaidi akaingiza mtu mwenye kuwa katika masilahi ya umma katika wafanyakazi, akashiria Imamu Bukhary ambapo amesema: “Mlango wa rizki kiongozi na wafanyakazi” anakusudia riziki ni fungu linalotolewa na Imamu katika mali ya umma kumpa mwenye kusimamia masilahi ya Waislamu kama vile kazi za uhakimu Fatwa na ufundishaji, anapaswa kuchukuwa katika mali ya Zaka kwa kazi anayofanya, kwa kipindi ambacho anasimamia masilahi hata kama atakuwa ni tajiri” ([31]).

Kuna baadhi ya Wanachuoni wameongeza maana hii, kwani wapo waliopitisha kutolewa mali ya Zaka kwa kuwapa wanafunzi wanaosomea elimu ya Sharia ambao wamezifunga nafsi zao katika kuipata elimu hiyo.

Katika vitabu vya Madhehebu ya Imamu Maliki – Kama ilivyoelezewa – Ezza Ibn Aabideen katika kitabu chake kuna kauli ya kufaa kutoa mali ya Zaka kwa kuwapa wanafunzi walimu ikiwa ni sehemu katika njia ya Mwenyezi Mungu ([32]).

Akasema katika sehemu nyingine: “Haifai kutolewa mali ya Zaka kwa kupewa mwenye kumiliki fungu la Zaka isipokuwa kwa mwenye kutafuta elimu, mpimbanaji katika njia ya Mwenyezi Mungu na aliyekatikiwa katika ibada ya Hija, kwa kauli ya Mtume S.A.W: “Inafaa kutolewa fungu la Zaka kwa kupewa mtafuta elimu hata kama atakuwa na gharama za matumizi ya siku arobaini”…..

Na akasema: Assaruujiy katika watu wa madhehebu ya Imamu Abu Hanifa, amelikataa swala la kufaa kutoa fungu la Zaka na kumpa mtafuta elimu, kwa sababu Aya inayoelezea pande za kupewa zaka ilipoteremka hakukuwa na watu wanaoitwa watafuta elimu. Mwenye kitabu cha Shurnablalia [33]katika watu wa Madhehebu ya Imamu Abu Hanifa akajibu kwa kusema: Kuliacha kwake kabisa, kwa sababu mwenye kutafuta elimu hakuwa isipokuwa ni mwenye kunufaika na hukumu mbalimbali, je mwenye kutafuta elimu anafikia daraja na kiwango cha aliyelazimika kuambatana na Mtume S.A.W ili kupokea hukumu kutoka kwake kama vile watu wa Al-Suffah”([34]).

Na Al-Mardawy katika watu wa Madhehebu ya Imamu Hambali ametaja katika sherehe ya kitabu cha Al-Muqnai kuwa Sheikh Taqiyyudeen Ibn Taimia ameteua kufaa kuchukuwa mali ya Zaka ili kunuua vitabu vitakavyotumika kwa yale yanayohitajiwa katika vitabu vya elimu ambavyo vinaulazima kwa masilahi ya dini yake na dunia, kisha akamalizia kwa kauli yake: “Nayo ni sahihi” ([35]).

Na mwenye kusema kauli hii ameichukulia dalili kuwa wenye kusimamia kazi hizi zenye masilahi kwa umma wa Kiislamu basi kusimamia kazi hizi ni katika masilahi ya umma ([36]).

Nne: Kauli kuwa Hija ni katika “Njia ya Mwenyezi Mungu”:

Mtazamo huu Muhammad katika wasomi wa Madhehebu ya Imamu Abu Hanifa amesema, kama ilivyotangulia na tukataja kuwa kusudio la “Njia ya Mwenyezi Mungu” ni pamoja na mkatikiwa Hija, kwa sharti la umasikini kama ilivyo kwenye Madhehebu yao.

Kauli kuwa Hija ni katika “Njia ya Mwenyezi Mungu” ni mapokezi ya Imamu Ahmad, katika kitabu cha Al-Muqnaa na sherehe yake ya Mardawy kwenye kauli ya mtunzi katika ukurasa wa saba miongoni mwa wanaostahiki fungu la Zaka: “Kundi la saba: Katika njia ya Mwenyezi Mungu, nao ni wapambanaji ambao hawana msharaha, wala hawapewi fungu la Zaka katika hija” amesema: “Hii ni moja kati ya kauli mbili ameichukuwa mtunzi, na mshereheshaji, wamesema: Ni sahihi na kuipitisha katika kufaa, na kutoka kwake pia anasema masikini hupewa kitakachomuwezesha kutekeleza ibada ya Hija, au kumsaidia katika ibada hiyo, nayo ni kauli iliyoelezewa na katika maelezo ya Abdillah, Al-Marwadhy na Al-Maimuuny amesema katika kitabu cha Furuui: Hija ni katika njia iliyoelezewa” ([37]). Na yamelezwa haya na Ibn Abbas na Ibn Omar R.A pia na Is-haq ([38]).

Wakachukuwa dalili ya hilo Hadithi ya Ummu Maaqal Al-Asadiya iliyopokelewa katika musnad ya Imamu Ahmad, na katika Sunani ya Abi Daud kama ilivyoelezewa, ndani yake amesema: Pindi Mtume S.A.W alipohiji Hija ya kuaga tulikuwa na ngamia Abu Maaqal akamtoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, lakini tuliumwa na Abu Maaqal alifariki, Mtume S.A.W akatoka alipomaliza Hija yake nilimuendea na akasema: “Ewe Mama Maaqal nini kimekuzuia kutoka pamoja na sisi?” akasema: Tulijiandaa lakini Abu Maaqal akafariki, na tulikuwa na ngamia ambaye huwa tunamtumia kuhiji lakini Abu Maaqal aliacha usia atumike katika njia ya Mwenyezi Mungu. Akasema: “Hivi kilichotolewa je ibada ya Hija ni katika njia ya Mwenyezi Mungu? Ikiwa utapitwa na Hija hii pamoja na sisi basi tekeleza ibada ya Umra ndani ya Mwezi wa Ramadhani kwani ni kama Hija ([39]), na katika maelezo mengine ya Ahmad: “Hija na Umra ni katika njia ya Mwenyezi Mungu” ([40]).

Pia wakajenga hoja kwa maelezo yaliyopokelewa katika Sunani ya Abi Daud kutoka kwa Ibn Abbas amesema: Mtume S.A.W alitaka kutekeleza ibada ya Hija, mwanamke mmoja alisema kumuambia mume wake: Niwezeshe nikahiji pamoja na Mtume S.A.W kwa kutumia ngamia wako, akasema: Sina cha kukuwezesha kuhiji, akasema: Niwezeshe kwa ngamia wako fulani, akasema: Huyo amewekwa kwa ajili ya njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, akaenda kwa Mtume S.A.W akasema: Mke wangu anakutakia amani na rehma za Mwenyezi Mungu, kwani ameniomba aende Hija pamoja na wewe alisema: Niwezeshe Hija pamoja na Mtume S.A.W nikamuambia: Sina cha kukuwezesha, akasema: Niwezeshe Hija kwa ngamia wako fulani, nikasema: Huyo ngamia yupo kwa ajili ya njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mtume S.A.W akasema: “Ama lau ungemuwezesha kutekeleza ibada ya Hija ilikuwa ni katika njia ya Mwenyezi Mungu” akasema: Na yeye amenitaka nikuulize kinacholingana na Hija ya pamoja na wewe, Mtume S.A.W akasema: “Mtakie amani ya Mwenyezi Mungu rehma zake na baraka zake, na mfahamishe kuwa inafanana Hija pamoja na mimi “Kwa maana kufanya Umra ndani ya Mwezi wa Ramadhani” ([41]).

Sharti la umasikini katika Hija halikupokelewa kwenye pande nane za matumizi ya zaka yaliyoelezewa katika Aya ya zaka kwa sababu limechukuliwa kwa kuzingatia kuwa kwake masikini.

Ikiwa patasemwa: Ni ipi faida ya tamko la Ibada ya Hija ni katika njia ya Mwenyezi Mungu ikiwa mwenye kuhiji anachukuliwa kwa umasikini wake?

Jibu: Ni kuwa baadhi ya mahujaji wanaweza kupata shida katika Hija kwa mali za Zaka, hivyo tamko linaondoa mfano wa shika kama hii kwa mwenye kuhiji na kwa mtoa Zaka. Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua zaidi ([42]).

Tano: Upana wa maana ya Jihadi:

Sheikh Yusuf Qardhawy amelezea Madhehebu mpya amefanya ukati na kati, na kupendelea kutokunjua zaidi maana ya “Njia ya Mwenyezi Mungu” ambapo inakusanya masilahi yote na matendo mema yakujiweka karibu na Mungu, kama vile ameipa nguvu kauli ya kutolibana sana ambapo haliishii kwenye jihadi ya maana ya kijeshi tu.

Akasema: Mwenye kulifuatilia neno “Njia ya Mwenyezi Mungu” lina ambatishwa na matumizi, atakuta lina maana mbili:

Maana ya yote: Sawa na maana ya neno asili linakusanya aina zote za wema utiifu na njia za mambo yak kheri.

Na maana maalumu: Nayo ni kutetea dini ya Mwenyezi Mungu na kupigana vita na maadui zake pamoja na kuliinua neno la Mwenyezi Mungu duniani, ili kusiwe na fitina na dini yote iwe ya Mwenyezi Mungu.

Kisha akasema: Kauli ambayo naipa nguvu ni kuwa maana jumla ya njia ya Mwenyezi Mungu haifai kupokelewa hapa kwa sababu ujumla huu unapanuka kwenye pande nyingi, hazina kikomo pande zake kuongezea pia watu wake, na hii inapingana na kikomo cha ugawaji wa Zaka kwa pande nane kama ilivyo kwenye Aya.

Kama vile njia ya Mwenyezi Mungu kwa maana ya jumla inakusanya kuwapa watu mafakiri na masikini pamoja na makundi mengine saba yaliyobakia, kwa sababu makundi yote ni katika wema na utii kwa Mwenyezi Mungu, hivyo ni ipi tofauti kati ya makundi haya na yale yaliyopita na yajayo?

Maneno ya Mwenyezi Mungu ni ufikishaji kwa ufupi yanapaswa kuepushwa na kujirudiarudia bila ya faida, hivyo ni lazima kukusudiwa maana maalumu inayojipambanua na makundi mengine yaliyobaki, na haya ndiyo yaliyofahamika na Wafasiri pamoja na Wanachuoni wa zama za nyuma, wakaitumia maana ya njia ya Mwenyezi Mungu katika jihadi, na wakasema: Kusudio lake wakati wa kutamkwa tamko.

Akaishia hili kwa kusema: Jihadi inaweza kuwa kwa kalamu na ulimi, kama vile inaweza kuwa kwa upanga na meno, jihadi inaweza kuwa kifikra au kimalezi au kijamii au kiuchumi au kisiasa, kama vile inaweza kuwa kijeshi, na aina zote hizi za jihadi zinahitaji ufadhili.

Jambo muhimu ni kufikiwa sharti la msingi la hayo yote, nalo ni kuwa “Katika njia ya Mwenyezi Mungu” kwa maana katika kunusuru Uislamu na kuinua neno lake duniani, jihadi zote zinazokusudia neno la Mwenyezi Mungu kuwa juu basi hiyo ni katika njia ya Mwenyezi Mungu, aina yeyote ya jihadi itakayo kuwa na silaha zake.

Kwani kutetea dini ya Mwenyezi Mungu na njia yake pamoja na Sharia yake kunafikiwa kwa vita na mapigano wakati mwingine, bali inaweza kutumika njia hii baadhi ya nyakati na sehemu ili kutetea dini ya Mwenyezi Mungu, lakini inaweza kuja wakati – kama wakati wetu huu – vita ya kifikra na kisaikolojia ni muhimu zaidi na hatari na yenye athari zaidi kuliko vita vya mizinga na kijeshi.

Ikiwa Jopo la Wanachuoni katika Madhehebu manne ya zamani wameweka kikomo cha fungu hili katika kuandaa wapiganaji na kuwekwa mipakani, na kupewa mali wanayohitaji miongoni mwa farasi kondoo na silaha, basi sisi tunawaongezea katika zama zetu hizi hawa wapiganaji aina nyingine, hao ndio ambao wanafanya ya kupigana vita vya akili na nyoyo kwa mafundisho ya Uislamu, na kulingania kwenye Uislamu, hao ndio wapiganaji kwa juhudi zao na kauli zao pamoja na kalamu zao ili kutetea Imani ya Uislamu na Sharia ya Uislamu.

Dalili yetu kwenye upana wa maana ya jihadi:

Kwanza: Jihadi katika Uislamu haikomei kwenye mapigano ya kivita na mauaji kwa upanga, Hadithi sahihi kutoka kwa Mtume S.A.W alipoulizwa: Ni jihadi gani iliyobora? Akasema: “Neno la haki mbele ya Kiongozi dhalimu” ([43]).

Kama ilivyopokelewa kutoka kwa Ibn Masoud Mtume S.A.W amesema: “Kila Nabii aliyeletwa na Mwenyezi Mungu kabla yangu kwa umma wake isipokuwa katika umma wake alikuwa na wanafunzi pamoja na Maswahaba wakijifunza mwenendo wake na kufuata amri zake, kisha wakafuata baada yao umma nyingi wanasema wasioyafanya, na wanafanya wasioamrishwa, basi mwenye kupambana nao hao kwa mkono wake huyo ni Muumini, na mwenye kupambana nao kwa ulimi wake huyo ni Muumin, na mwenye kupambana nao hao kwa moyo wake huyo ni Muumini, wala hakuna imani hata kidogo baada ya hayo” ([44]).

Na akasema S.A.W: “Pambaneni na washirikina kwa mali zenu nafsi zenu na kauli zenu” ([45]).

Pili: Tuliyoyataja miongoni mwa aina za jihadi na harakati za Kiislamu kama zisingeingia ndani ya maana ya jihadi kwa andiko, ingelazimika kukutanishwa na uoanisho, kwani vyote viwili ni kazi inayokusidia kutetea Uislamu na kuulinda, pamoja na kupambana na maadui wake na kuinua neno lake juu duniani.

Tumeona kwa Wanachuoni Waislamu waliowaunganisha wasimamizi wa Zaka wanaofanya kazi katika masilahi ya umma wa Waislamu.

Hakuna la kushangaza kuunganisha na jihadi – kwa maana ya kupigana – kila kinachopelekea lengo la jihadi, na kusimama kwenye jukumu lake kwa kauli au kitendo kwa kuwa sababu ni moja, nayo ni kutetea Uislamu.

Kabla ya hapo tumeona kwenye uiano utangulizi katika milango mingi ya Zaka, wala hatujaona Madhehebu yeyote isipokuwa yamezungumzia katika moja ya sura yake.

Hivyo tuliyoteua hapa katika maana ya “Njia ya Mwenyezi Mungu” yanakuwa ni rai na mtazamo wa Jamhuri ya Wanachuoni pamoja na baadhi ya upana wa maana zake.

Na akasema pia: Yanayopelekea uzito wa kuandaa jeshi la serikali na kulipatia silaha pamoja na kuligharamia yalikuwepo tokea mwanzo wa Uislamu mpaka ndani ya zama zetu hizi – gharama hizo zikibebwa na hazina kuu ya nchi, na wala si mali katika mali za Zaka, kwa sababu hili linahitaji gharama kubwa ni mzigo mkubwa katika mapato ya Zaka, hivyo sisi tunaona kuwa kuelekezwa matumizi haya kwenye jihadi ya kitamaduni kimalezi kihabari ni bora zaidi katika zama zetu kwa sharti ya jihadi kuwa ya Kiislamu kabisa na Uislamu sahihi, wala isiwe jihadi iliyochafuliwa na uchafu wa kikabila na kitaifa, wala isiwe jihadi ya Kiislamu iliyoingizwa mambo ya Kimagharibi au Kimashariki, inakusudiwa sio jihadi inayohudumia Madhehebu au mfumo au nchi au tabaka au mtu, kwani Uislamu mara nyingi huchukuliwa anuwani ya taasisi yenyewe ndani yake ni taasisi ya kisekula wala si ya kidini, hivyo ni lazima Uislamu uwe ndio msingi na chanzo, nayo ndio lengo na muelekeo, mpaka hiyo taasisi istahiki heshima ya kunasibishwa kwa Mwenyezi Mungu, na kuzingatiwa kazi ndani ya taasisi hiyo ni sehemu ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Tunaweza kutoa mifano mbalimbali kwa kazi nyingi ambazo zinahitaji Ujumbe wa Uislamu ndani ya zama hizi, nazo ni muhimu kuzingatia ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Kuanzisha vituo vya kazi za ulinganiaji katika Uislamu sahihi, na kufikisha Ujumbe wake kwa wasiokuwa waislamu ndani ya mabara yote ndani ya dunia hii ambayo kumekuwa na mvutano wa dini na Madhehebu, ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Kuanzisha vituo vya Kiislamu vyenye uelewa ndani ya nchi za Kiislamu vinavyochukuwa vijana Waislamu, na kufanya kazi ya kuelekeza muelekeo sahihi wa Kiislamu na kuulinda kutokana na upagani wa akida, na fikra potofu, uharibifu wa maadili, na kuandaliwa ili kutetea Uislamu, na kupambana na maadui zake, ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Kuanzisha gazeti maalumu la Kiislamu, linapambana na magazeti haribifu na potoshi, ili kuinua neno la Mwenyezi Mungu, na kuipa nafasi kauli ya haki pamoja na kujibu uzushi na uwongo dhidi ya Uislamu na shaka za wapotoshaji, na kufundisha hii dini watu wake likiepukana na kuzidisha na kuchafua, hiyo ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Kuchapisha kitabu asili cha Kiislamu kinachoelezea uzuri wa Uislamu, na kuelezea yaliyomo ndani yake pamoja na kuonesha uzuri wa mafundisho yake na ukweli wake, kama vile kuweka wazi ubatilifu wa wapinzani wa Uislamu, na kusambaza kitacha kama hiki kwa sehemu kubwa, pia ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.  

Kuleta watu wenye nguvu waaminifu katika kufanya kazi kwenye maeneo yaliyopita kwa umuhimu mkubwa na kwa mipango ili kuhudumia hii dini, na kupanua nuru yake katika anga, na kujibu vitimbi vya maadui wa Uislamu wanaovizia, na kuwaamsha vijana wa Uislamu waliolala, pamoja na kupambana na mawimbi ya usambazaji Ukiristo na upagani, ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Kusaidia walinganiaji katika Uislamu wa kweli, wale ambao wanafanyiwa njama na nguvu ya uadui wa Uislamu wa nje, wakitumia waovu na walioritadi wa ndani, wakifanyiwa kila aina ya mateso ikiwa mauaji kuadhibiwa kuhamishwa na mateso ya njaa – kuwasaidia hawa ili kuweza kupambana na kuthibiti mbele ya makafiri wa waovu, pia ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Kutumia mali ya zake katika njia hizi mbalimbali ni bora zaidi na kupaswa Muislamu kutoa katika hayo Zaka yake, na ziadi ya Zaka yake, kwani hakuna katika Uislamu – baada ya Mwenyezi Mungu – isipokuwa Waislamu wenyewe, na hasa katika wakati wa ugeni wa Uislamu.

Na katika yanayopaswa kuelezewa ni kuwa kuna baadhi ya kazi na miradi inaweza kuwa ndani ya nchi fulani, na wakati fulani na hali fulani ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hilo lisiwe ndani ya nchi nyingine au wakati mwingine hali nyingine.

Kuanzisha shule katika mazingira ya kawaida ni jambo jema na juhudi za kushukuriwa zinazopendwa na Uislamu, lakini haizingatiwi ni jihadi, ikiwa nchi imekuwa na mafundisho na taasisi za kielimu zipo mikononi mwa Wamisionari au Wakomunisti au watu wasio na dini wasekula, basi katika jihadi kubwa ni kuanzisha shule za Kiislamu zinazotoa mafunzo kwa watoto na vijana wa Waislamu, na kuwalinda na vitendo vya uharibifu wa kifikra na kimaadili, na kuwalinda na sumu inayopulizwa katika mitaala na vitabu, na katika akili za walimu, na ndani ya roho ya umma ambao inaelekezwa mashuleni na mafunzo yote.

Mfano wa hilo husemwa katika kuanzisha maktaba ya Kiislamu ili kujisomea katika kupambana na maktaba haribifu.

Vile vile kuanzisha hospitali ya Kiislamu ili kutibia Waislamu, na kuwaokoa na kutumika jumbe mbaya na potofu za Kimisionari, na ikiwa taasisi za kifikra na kitamaduni ndio hatari zaidi na zenye athari mbaya ([46]).

Ufupisho wa Utafiti

 Kutokana na maelezo yaliyotangulia ni wazi kuwa kauli ya kusudio la matumizi ya Zaka katika “Njia ya Mwenyezi Mungu” ni jihadi na kupambana na yale yanayoendana na hayo, hiyo ndio kauli ya Jamhuri ya Wanachuoni, isipokuwa kauli za wapanuzi wa maelezo ya kusudio la matumizi haya hapo zamani na hivi sasa, na kauli ya wapanuzi katika maana ya jihadi ni kauli zenye kuzingatiwa, na kila mmoja miongoni mwao ana mtazamo, hivyo inafaa kuchukuwa kauli ya watu waliopanua maana ya jihadi hasa ndani ya zama zetu hizi.

Na kanuni ambayo wameitaja Wanachuoni ndani ya vitabu vyao: Ni kuwa inafaa kuiga rai yeyote na Madhehebu inayokubalika kunukuliwa, na maana ya kanuni hii ni kuwa: Kiwango cha Fiqhi kimejengeka juu dhana wala si rai thabiti ya moja kwa moja kwa sababu hii yenyewe ndio kusudio la Mwenyezi Mungu, kwa vile rai ina chanzo cha Kisharia na wala haiwi nje ya Sharia, basi inafaa kuifuata, wala haizingatiwi hili isipokuwa ni kuhama kutoka rai yenye nguvu kwa Mwanachuoni na kwenda kwenye rai inayopewa nguvu kwa mtazamo wake, inaweza kuwa yenye nguvu kwa mtazamo wa mwingine, na imelezwa kuwa Ofisi ya Mufti wa Misri ilitoa Fatwa mbili katika zama za Fadhila Sheikh Abdul-Majiid Salim – Mungu amrehemu – na kuelezea katika Fatwa hizo mbili kuipanua tafasiri ya matumizi katika njia ya Mwenyezi Mungu, Fatwa ya kwanza ni kufaa kutoa Zaka kwa ajili ya jumuiya za mambo ya kheri iliyotolewa mfungo tano mwaka 1360H – sawa na mwezi Marchi mwaka 1940, na Fatwa ya pili ni kuhusu kufaa kutumika mali ya Zaka kwa kujengea Misikiti iliyotolewa mfungo nne mwaka 1363H – sawa na mwezi January mwaka 1944.

 Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

            Imeandikwa Na:

Mustafa Abdulkarim Muhammad

               04/06/2007.

 

 

[1] Kamusi ya Lisaanu Al-Arab ya Ibn Mandhur 11/319.

[2] Kitabu cha Taajul-Aruusi cha Zubaidy.

[3] Kitabu cha An-Nihaayatu fii Ghariib Al-Athar 2/846.

[4] Kitabu cha Lubab katika sherehe ya kitabu cha Al-Maidany 1/78, Ad-Durru Al-Mukhtaa 2/343.

[5] Kitabu cha Al-Inaya sherehe ya kitabu cha Al-Bidaya 2/264, na kitabu cha Badaaii fii Tartiibi Sharaaii 2/45.

[6] Marejeo ya mwisho kwa upokezi huo huo, na Hadithi imo katika kitabu cha Sunan Abi Daud 1988.

[7] Raddul-Mukhtar 2/343.

[8] Kitabu cha Badaaii Swanaaii 2/45.

[9] Kitabu cha Bahru Raaiq sherehe ya Kanzu Dakaik 2/260.

[10] Kitabu cha Badaii Swanaai fii tartiibu sharaaii 2/46, na Hadithi ya kwanza: Inapatikana katika Sunani ya Imamu Tirmidhy 652 na akasema Hadithi na nzuri, na Hadithi ya pili imekubaliwa na Wanachuoni wa Hadithi kwa tamko:

“Akawapa habari kuwa Mwenyezi Mungu amelazimisha kwao sadaka huchukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kupewa masikini wao” Sahihi Bukhary Hadithi nambari 1425. Sahihi Muslimu Hadithi nambari 19.

[11] Tafasiri ya Al-Manaar ya Sheikh Rashiid Ridhaa 10/580.

[12] Imepokewa na Daud katika Sunani yake Hadithi nambari 1635, imepokewa pia na Ibn Maja Hadithi nambari 1841 na mfano wake katika Musnad ya Ahmad 3/56. Imamu An-Nawawy amesema: “Hadithi hii ni nzr au sahihi imepokewa na Abu Daud kwa njia mbili, ya kwanza kutoka kwa Atwai Ibn Yasar kutoka kwa Abi Saidi Al-Khudry kutoka kwa Mtume S.A.W, njia ya pili kutoka kwa Atwa kutoka kwa Mtume S.A.W na upokezi wake mzuri kwa njia mbili, Baihaqy amekusanya njia yake ndani yake ni kuwa Maliki na Ibn Ayiina wameipokea na Muammar pamoja na Thaury wakaendeleza nao hao wawili ni katika jumla ya wahifadhi wa Hadithi wanaotegemewa, kuna kanuni maarufu kwa watu wa Hadithi inasema kuwa: Hadithi iliyokatika mpokezi mmoja hukumu inakuwa ni kwa kuungana na madhehebu sahihi, na tumeelezea pia kuhusu Imamu Shaafy R.A kuwa amepinga Hadithi iliyokatika mmoja wa wapokezi ikiwa itakuwa inafungamana na moja ya mambo manne: Ima Hadithi Musnad, ima Hadithi imekata mmoja wa wapokezi kwa njia nyengine, ima kauli ya Swahaba, ima kauli ya Wanachuoni wengi, na hii mara nyingi inakutwa hivyo, kwani imepokelewa Hadithi na wazungumzaji na Wanachuoni Maswahaba na wengine” kitabu cha Al-Majimuui 6/191.

[13] Kitabu cha majimuuu 6/200.

[14] Kitabu cha Badaai Swanaaii 2/46.

[15] Hashiyatu Ibn Abideen “Raddul- Muhtar alaa Durril-Mukhtar 2/344.

[16] Kitabu cha Fiqhi ya zaka cha Sheikh Qardawy.

[17] Kitabu cha Sherhu Al-Kabiir cha Dardiir na Haashiyatu ya Dusuuqy 1/497.

[18] Kitabu cha Mughny Al-Muhtaaj ilaa maarifatu al-Faadhi al-Minhaaj 4/181.

[19] Kitabu cha Rawdhatu Twalibiin na Umdatu Muftiin 2/188.

[20] Musnad Ahmad 6/450.

[21] Kitabu cha Daqaiq Uli-Nnuhaa ni sherehe ya kitabu cha Al-Muntaha 1/458.

[22] Kitabu cha Fiqhi ya zka cha Sheikh Qardawy.

[23] Mafatiihul-Ghaibu Tafasiri ya Imamu Razy 16/115.

[24] Rawdhat Nadiya 1/206/207.

[25] Kitabu cha Mahaasinu Taawiil 8/3181.

[26] Kitabu cha Tafsiri ya Manaar 10/585, 587.

[27] Kitabu cha Uislamu Imani na Sharia ukurasa wa 104, 105 chapa ya Dar Al-Sharqi.

[28] Kitabu cha Al-Fatawa cha Sheikh Shaltuut ukurasa wa 119 chapa ya Al-Azhar.

[29] Kitabu cha Al-Mughny 2/280.

[30] Kitabu cha Fiqhi ya zaka cha Sheikh Qardawy, na maelezo ya Abi Ubaida katika kitabu cha mali ukurasa wa 573, 575 kwenye marejeo yaliyopita, na maelezo yamepokelewa na Ibn Abi Shaiba katika kitabu chake 2/392.

[31] Kitabu cha Subuli-Salaam 1/145.

[32] Kitabu cha Raddul-Muhtaar alaa Darrul-Mukhtaar 2/343.

[33] Naye ni: Hassan Ibn Ummaar Ibn Yusuf Al-Shurnilalii Mmisri, na kunasibishwa kwake na Shabry Balulah kutoka Munifiya nchini Misri: Ni mwanachuoni wa madhehebu ya Imamu Abu Hanifa, alifariki nchini Misri mnamo mwaka 1069H. Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na: Tahkiikaatul- Qudusia na vyengine vingi.

[34] Marejeo yaliyopita 2/340, 343.

[35] Kitabu cha Al-Inswaaf 3/218.

[36] Utafiti uliokusanya matumizi katika njia ya Mwenyezi Mugu kwa mtazamo wa kisasa sawa na maelezo mbalimbali ya Dr. Omar Sulaiman Al-Ashqar – ni katika jumla ya tafiti na kazi za kongamano la kwanza la kadhia za zaka za kisasa lilofanyika Jijini Cairo mnamo mfungo sita mwaka 1409H, sawa na mwezi October 1988, ukurasa wa 208.

[37] Kitabu cha Al-Inswaaf cha Mardawy 3/235.

[38] Kitabu cha Al-Mughny 6/334.

[39] Kitabu cha Sunani Abi Daud 1989.

[40] Musnad Ahmad 6/450.

[41] Sunani ya Abi Daud 1990.

[42] Utafiti umekusanya matumizi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mtazamo wa kisasa kwa mujibu wa ibara mbalimbali za Dr. Omar Suleiman Al-Ashqar – ni katika jumla ya tafiti na kazi za kongamano la kwanza la kadhia za zaka za kisasa lilofanyika Ciaro mfungo sita mwaka 1409H, sawa na mwezi October 1988 ukurasa wa 206, 207.

[43] Sunani An-Nisaai 4209 na Musnad ya Ahmad 4/315, na Muujam Al-Kabiir ya Twabary 8/282, na kitabu cha aina za imani cha Baihaqy 6/93, na akasema Al-Minawy katika kitabu cha Taisiir sherehe ya Al-Jaamii As-Swaghiir 1/77, na katika kitabu cha Taisiir pia 1/365.

[44] Sahihi Muslimu 188..

[45] Sunani Abi Daud 2504 na mfano wake katika Sunani An-Nisaai 3096 na mfano wake katika sahihi Ibn Habban 11/6 na kitabu cha Mustadriku Al-Haakim 2/91: Hadithi hii ni sahihi kwa maelezo ya Imamu Muslimu na kukubalika na Dhahby katika kitabu cha Talkhisw, na Musnadi Ahmad3/124.

[46] Kitabu cha Fiqhi ya zaka cha Sheikh Qardawy.

Share this:

Related Fatwas