Usahihi wa Udhu Pamoja na Kupaka r...

Egypt's Dar Al-Ifta

Usahihi wa Udhu Pamoja na Kupaka rangi za kucha

Question

          Je, Udhu unasihi iwapo kucha zimepakwa rangi?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema ni zake, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya hayo:

        Neno Udhu limechukuliwa kutokana na maana ya kung'aa na hiyo inamaanisha uzuri na usafi, na udhu ni maji yanayotumika kutawadhia. [Lesaan Al Arab, kidahizo cha (w-dh-a)].

        Na maana ya kisharia; Udhu ni twahara inayopatikana kwa maji na inaambatana na viungo mahsusi mwilini, na idadi ya viungo hivyo ni vinne. [Hashiat Ala Alsharh Al Sagheer, 1/104, Ch. Dar Elmaaref]

        Kwa kuwa Udhu huvihusishia viungo maalumu mwilini, inashurutishwa katika udhu kuondosha vinavyoyazuia maji kufika (ngozini) mwilini, ili lengo la kutawadha litimie, la si hivyo udhu huo utakuwa umebatilika.

        Al Sharnablaliy Al Hanafiy anasema katika masharti ya udhu: "Sharti la tatu miongoni mwa masharti hayo ni kuondosha yanayozuia kuwasili maji katika mwili kama vile nta au mafuta, na ameainisha nta na mafuta kwa kuwa kubakia athari ya mafuta na mfano wake hakuzuii maji kwa kutokuwepo kizuizi chochote, [Maraqi Al Falah, Uk.34, Ch. Mustafa Al Halabiy].

        Al Zaraqaaniy alisema katika kitabu chake cha (Sharh Mukhtasar Khalil) juu ya masharti ya usahihi wa udhu: "Na miongoni mwa masharti ya kusihi kwa udhu ni kutokuwepo kizuizi chochote juu ya viungo vya mwili"  [Sharh Al Zarqaaniy Ala Mukhtasar Khalil, 1/54, Ch. Dar Al Fikr].  

        Na Al Bajiramiy Al Shafiy anasema katika (Hashiatahu Ala Al Iqnai) juu ya masharti ya Udhu: "Na kutokuwepo kizuizi kama vile mafuta yaliyoganda, ama kimiminika (uowevu) hakizuii maji kugusa (ngozi ya) kiungo cha mwili hata kama haikuthibitika hivyo juu yake" [Al Bajiramiy Ala Al Iqnai, 1/115,, Ch. Mustafa Al Halabiy.

        Al Haitamiy anasema katika (Tuhfat Al Muhtaj): "Na sharti la udhu ni kutokwepo juu ya kiungo cha mwili kitu kinachoyageuza maji na kuyafanya yawe na madhara, au tabaka (kitu kigumu) gumu linalozuia maji kufika katika ngozi", [Tuhfat Al Muhtaj Bisharh Al Minhaj, 1/180, Ch. Ihiyaa Al Turaath Al Arabiy].

        Na Al Rahibaniy Al Hanbaliy anasema: "Na inashurutishwa katika udhu kuondosha kitu chochote kinachozuia kufika maji katika viungo vya udhu ili yafike maji hayo katika ngozi". [Mataalib Uli Al Nuhaa, 1/104, Ch. Al Maktab Al Islamiy].

        Na rangi ya kucha ni kimiminika (uowevu)) kinachoganda na hutengeneza gamba gumu juu ya kucha ambazo huyazuia maji kuwasili katika kucha hizo. Na kucha ni sehemu ya mikono na miguu ambayo ni viungo vinavyotakiwa kuoshwa katika udhu na katika kuoga. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Enyi mlioamini! Mnapotaka kusimama kwa ajili ya kuswali, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na (osheni) miguu yenu mpaka vifundoni}, [Al MAIDAH, 6].

        Mweyezi Mungu Mtukufu ameamrisha kuosha hii mikono miwili na hii miguu miwili, na viungo hivyo ni miongoni mwa viungo vya udhu, na kucha ni sehemu ya mkono au mguu unaotakiwa kuoshwa; kwani amri ya kuosha kiungo kizima ni amri ya sehemu ndogo inayoungana nacho, na iwapo kizuizi kitazuia kufika maji katika sehemu hiyo ya kiungo basi udhu hautakuwa sahihi. Kwa hivyo ni lazima kizuizi hicho kiondoshwe kisha sehemu hiyo ioshwe, na wala si sharti kuosha tena sehemu ya mkononi au mguu inayobakia, kwani kuosha viungo vyote vya udhu kwa mfululizo bila ya kukatisha ni Sunna na siyo faradhi kwa mujibu wa wanavyuoni wengi. Basi inapendeza kutawadha upya iwapo utenganishaji kati ya viungo wakati wa udhu wa kwanza utakuwa mrefu. Na inajuzu kuosha sehemu iliyokuwa imepakwa rangi ya kucha pasina kutawadha upya iwapo utenganishaji utarefuka.

        Na asipoiosha sehemu hiyo basi itakuwa ni sehemu ya kiungo ambayo haijaoshwa, nayo inaubatilisha udhu pamoja na Swala. Na iwapo mtu ataswali kwa udhu huo basi inampasa kutawadha tena na kuswali upya. Laa si hivyo inampasa kuondosha rangi hiyo ya kucha katika sehemu hiyo na kuiosha.

        Na iwapo itasemwa: kwamba rangi ya kucha ni kama piopio (hogo) inajuzu kupaka maji juu ya rangi hiyo ya kucha iwapo kuna ugumu wa kuiondosha. Hapa jibu la kutofautisha kati ya piopio (hogo) na rangi ya kucha linatolewa; Inajuzu kupaka maji juu ya piopio (hogo) kwa sababu ya kuwepo udhuru (unaokubalika kisharia); imepokewa na Ibn Majah kutoka kwa Aliy Ibn Abiy Twalib alisema: "Mkono wangu mmoja ulivunjika, na nikamwuliza Mtume S.A.W. akaniamrisha nipake maji juu ya piopio (hogo). Kwa hivyo kupaka maji juu ya piopio (hogo)  ni ruhusa, na ruhusa huwa inakadiriwa kiasi chake.

        Basi kutokana na maelezo yaliyotangulia hapo juu, tunaona kwamba udhu juu ya rangi ya kucha hausihi. na ni lazima kuondosha rangi hiyo, kisha kutawadha upya, kwa kuepukana na kinyume cha Wanavyuoni waliyoona kuwa kufululiza kati ya viungo wakati wa kutawadha ni faradhi, na inajuzu kuwafuata wale Wanavyuoni wanaoona kuwa kufululiza sio faradhi. Haiwi wajibu isipokuwa kuosha mahali ambapo maji hayajafika kwa sababu ya rangi ya kucha iliyoyazuia maji hayo.

        Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi

 

 

 

Share this:

Related Fatwas