Hukumu ya Ndoa ya Misyaar (Ndoa ya ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya Ndoa ya Misyaar (Ndoa ya Mwanamke kukubali kuacha baadhi ya haki zake)

Question

Tunatarajia kutoka kwenu wanazuoni waheshimiwa kutuelezea maana ya Ndoa ya Misiyaar, na mtubainishe hukumu yao?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Ndoa ni mkataba wa maneno baina ya watu wawili; mwanamume na mwanamke ambao hawana vizuizi vya kisharia, hali yake kama mkataba wowote ambao unasihi kisharia kwa kupatikana sharti na nguzo zake na kutokuwepo vizuizi vyovyote. kadhalika mkataba katika Fiqhi ya Kiislamu unakuwa kwa maneno.

Katika ndoa ya misyaar, mkataba unafungwa, sharti na nguzo zinatimizwa, ila mwanamke anaafikiana na mumewe aache haki yake ya makazi na kupata matumizi au mojawapo yao.

Kimsingi aina hiyo ya ndoa ni halali ikiwa mkataba umetimizwa sharti na nguzo zake zinazotakikana kisharia, nazo ni: ijaabu (makubaliano ya kuoana), kuwepo kwa walii, mashahidi na mke na mume kusalimika na vizuizi vya kisharia.

Mkataba huo ukitimizwa sharti na nguzo zake, basi unakuwa na haki zinazoambatana na mkataba wa kindoa kama nasaba, urithi, eda, talaka, kuingiliana, makazi, matumizi na wajibu na haki nyingine ziambatanazo na ndoa, lakini wanandoa wakiafikiana kwamba mke aache haki ya kukaa au kupata matumizi, basi mwanamke akiacha haki yake au baadhi yake inajuzu kisharia kwani yeye ndiye mwenye haki hiyo naye anaweza kuiacha bila ya kuathiri hali ya kusihi mkataba wa ndoa.

Ibn Qudama alisema katika kitabu chake “Al Mugh-niy” alipozungumzia aina za masharti ya ndoa: “Sehemu ya pili: yanayobatilisha sharti na mkataba unasihi, kama  Akishurutisha kutokuwa na mahari kwa mke au kutompa matumizi au mke ashurutishe asiingiliane na mumewe au mumee atumie kinga wakati wa kuingiliana (kinga za mimba) au mumewe ampe zamu siku chache kuliko mke mwingine au mumewe ashurutishe asimtembelee zaidi ya siku moja kila wiki au amtembelee mchana tu bila ya usiku au mumewe amshurutishe mkewe ampe matumizi au ampe kitu angalau hata kidogo, basi masharti hayo yote ni batili; kwani yanapingana na maana ya muktadha wa mkataba, na kwa kuwa zimekusanya kuondosha haki zinazopasa kwa kufunga ndoa kabla ya kufungwa kwake, kwa hiyo haijuzu kama ilivyo haki ya wamiliki wawili, mmoja hana haki ya kumshurutisha mwenzake aiache haki yake kabla ya mauzo.

 Ama mkataba wenyewe, basi unakuwa ni sahihi; kwani masharti yale yanaambatana na vitu vya ziada ambavyo havilazimishwi kuvitaja tena haidhuru kutovitaja kwa hiyo havibatilishi mkataba kama ikishurutishwa mahari iliyo haramu”[1].

Suala la kujuzu kwa mwanamke kuacha baadhi ya haki zake wakati wa kufunga mkataba wa ndoa yake lipo katika maneno ya Mwenyezi Mungu: (Na mwanamke akichelea kutupwa na kutojaliwa na mumewe, basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekwa machoni mwake tamaa na choyo. Na mkifanya wema na mkamchamungu basi hakika Mwenyezi Mungu Anazo khabari za yote mnayoyatenda) {AN-NISAA, 128}.

Imesimuliwa kutoka kwa Mama wa Waumini Bi. Aisha R.A ya kwamba sababu ya kushuka kwa Aya hiyo ni: “Mume anakuwa na mke hali ya kuwa amemchukia hamtaki anataka kuachana naye, na mkewe amwambie: “nakupa uhuru wa kuniacha”, basi ikashuka Aya hiyo katika suala hilo”.

Naye Ibn Abass R.A. alisema: “Bi. Sauda alihofia kuachwa na Mtume s.a.w. akamwambia: usinipe talaka niache niishi nawe na siku yangu mpe Bi. Aisha, basi Mtume S.A.W. akafanya na hiyo ikashuka Aya: (basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora)”.

Ndoa ya misyaar siyo mpya katika Fiqhi ya Kiislamu lakini jina lake ndilo jipya na aina hiyo ni ya zamani ambayo ilikuwa inajulikana kwa jina la ndoa ya “NAHARIYAT AU LAYLIYAT (ndoa ya kukutana mchana au usiku)”, na mazingatio hapa yanakuwa katika hukumu siyo majina.

Ilitajwa katika kitabu cha Fat-h Al Qadir kilichotungwa na Al Kamal bin Al Hamam Al Hanafiy: “Si vibaya kuwaoa AL NAHARIAT nao ni: kuwaoa wanawake sharti kukutana nao mchana sio usiku”.

Imamu Ahmad amesema - kama ilivyotajwa katika kitabu cha Al Mughniy - katika suala la mwanamume ambaye kamwoa mwanamke akamshurutisha akae naye mara moja kila wiki halafu mkewe akabadili kauli yake akasema: sikubali isipokuwa siku moja kwa siku moja, akasema Imam Ahmad: ana haki ya kuachana na ombi lake kwa hiari yake na hiyo inajuzu ama akisema: sikubali isipokuwa baada ya kugawanya masiku, basi ni haki yake anaweza kuiomba muda wowote akitaka. Aidha imesimuliwa na Al Athram katika suala la mwanamume anayemwoa mwanamke akampa sharti kwenda kwake siku maalumu kwamba inajuzu, na akitaka anaweza kubadili kauli yake, kadhalika amesema katika suala la mwanamume anayemwoa mwanamke kwa la sharti kumpa matumizi ya dirham tano au kumi kila mwezi, ndoa hiyo inajuzu kisheria, na mke ana haki ya kufuta maneno yake. Na imenukuliwa kutoka kwa Al Maruzi aliyoyasema Imam Ahmad katika ndoa za Al Nahariat na AL Layliyat akasema: aina hiyo ya ndoa haiafikiani na ndoa za Waislamu. Naye Hamad bin Abi Sulaiman na Ibn Shubruma ni miongoni mwa waliochukiza suala la kuwaoa AL NAHARIYAT. Na Al Thauriy alisema: hapa sharti ni batili. Ingawa Al Hassan na A’taa walikuwa hawaoni vibaya katika ndoa ya AL NAHARIYAT, naye Al Hassan alikuwa haoni ubaya kwa mtu kuoa mwanamke kwa sharti la kumpangia siku maalumu za kukutana naye kila mwezi. Hapa chukizo la wanaochukiza suala hilo linarejea kubatilisha sharti, na kujuzusha kwa walijuzisha kunarejea asili ya ndoa, kwa hiyo maoni yao yanaafikiana juu ya kusihi ndoa na kubatilisha sharti[2].

Maana ya kauli ya imamu Ahmad: aina hiyo ya ndoa haiafikiani na ndoa za Waislamu; si ndoa kamili, kama unavyosema: si Muumini asiyependa kwa nduguye apate anayoyapenda kupata yeye. Na maana yake: si Muumini mwenye imani kamili asiyependa nduguye apate anayoyapenda kupata yeye.

Na baadhi ya Wanazuoni wamesema kwamba hakujuzu aina hiyo ya ndoa, wakatolea dalili kadhaa kuthibitisha kauli yao, na miongoni mwa dalili hizo ni:

Ufungaji ndoa wa aina hiyo unakuwa unaambatana na baadhi ya masharti yanayohitalifiana na lengo “maana” la ndoa, kama sharti la mwanamke kuachana na haki yake katika kugawa zamu, matumizi n.k., masharti hayo ni batili yanaweza kubatilisha ndoa.

Na kumetangulia kujadili dalili hizo kutokana na kauli ya Imamu Ibnu Qudama kuhusu sehemu ya pili ya masharti ya ndoa, ambayo ilitaja kwamba ndoa inasihi, na sharti ni batili.

Ndoa kwa aina yake hiyo inapingana na makusudio ya Sharia ya Kiislamu yanayoelekeza kuleta utulivu, mapenzi pamoja na ulezi wa watoto.

Kiufupi: sisi hatusemi kwamba aina hiyo ya ndoa haiafikiani na ndoa sahihi ya Kiislamu inayotakikana, bali tunasema kwamba aina hiyo inahakikisha lengo kuu la ndoa ambalo ni kuleta kujizuia na machafu kama ilivyokuja katika Hadithi ya Mtume s.a.w.: “Enyi Kundi la vijana yeyote anayekuwa na uwezo wa ndoa, basi aoe kwani ndoa inainamisha macho na kulinda tupu”.

Ndoa ya Misyaar kimsingi inategemea hali ya usiri na kujifichika na asili ya ndoa katika Sheria ya Kiislamu ni kuitangaza.

Hili linajibiwa kwamba suala la usiri silo kitu cha msingi katika aina hiyo ya ndoa, bali inaweza kuwa na aina ya tangazo na kuandikwa na msajili rasmi, aidha suala la kuficha ndoa baada ya kukamilika masharti na nguzo zake haliifanyi kuwa ni batili kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni walio wengi.

Na yaliyonukuliwa na wafuasi wa madhehebu ya Malik kuhusu suala la kushurutishia mashahidi kuficha kunabaatilisha ndoa, hili ni maalum kama watausiwa kuficha wakati wa kufunga ndoa, ama wakiusiwa baada ya kufunga ndoa hakudhuru[3].

Ndoa hiyo inakuwa na aina nyingi za marufuku za kisharia, kwani baadhi ya wanawake wanaweza kuchukua aina hii ya ndoa kama njia ya kufanya machafu wakidai kwamba wameolewa kwa njia ya ndoa ya Misyaar, kwa hiyo inalazimika kukataza aina hiyo ya ndoa ili kujiepusha na maovu, hata kama imekamisha nguzo na sharti kwa kulinganisha na ndoa ya Mutaa na ndoa ya mtu aliemuoa mwanamke alieachika talaka tatu ili amuache na aolewe tena na mume wake (Al Muhallil).

Na huku ni kupetuka mipaka katika suala la kujiepusha na maovu, kwani aina hiyo ya ndoa inaweza kusaidia katika kujilinda na mambo machafu. Ama kuilinganisha na ndoa ya Mutaa na ndoa ya mtu aliemuoa mwanamke alieachika talaka tatu ili amuache na aolewe tena na mume wake (Al Muhallil) si sahihi pia. Mjadala wa hili utakuja hapo baadae.

Ndoa ya aina hiyo inaletea madhara kwa mke wa kwanza; kwani mumewe atakwenda kwa mkewe wa pili bila ya mke wa kwanza kujua, na atatumia wakati nae, na kulala nae na kuchukua muda wa mke wa kwanza jambo ambalo linapuguzia haki ya mke wa kwanza katika kustarehe.

Rai hiyo inajibiwa kwamba, si lazima ndoa hiyo ya Misyaar iwe ya pili, bali inaweza kuwa ya kwanza au ya pili na mke wa kwanza akawa anajua.

Tukikubali kuwa mume ameoa mke wa pili lakini analificha suala lake kwa mke wa kwanza, basi haidhuru ikiwa havunji haki yoyote katika haki za mke wa kwanza katika makazi na matumizi yake n.k.

Aina hiyo ya ndoa inavunja heshima ya mwanamke, na inatishia mustakbali wake kwa kuachwa kama ataomba haki yake kugawanya zamu sawa au akiomba haki yake ya kupata matumizi, aidha aina hiyo ya ndoa inakuwa kama njia ya kumkandamiza mke kutokana na hali yake ilivyo; kwani kama angepata ndoa ya kawaida asingekubali ndoa ya Misyaar.

Rai hiyo inajibiwa kwamba, hakuna uhusiano wa karibu kati ya hali ya kuomba mke haki yake katika kugawa zamu au kupata matumizi na kuachika, kwani talaka inaweza kutokea kwa sababu yoyote nyingine mbali na kuomba mke haki yake ya kupata matumizi au kugawa zamu.

Mume kwa mujibu wa ndoa hiyo anaweza kumkandamiza mkewe akiona ana mali na utajiri hali ya kuwa mke ana shida naye, basi anaweza kumkandamiza ili apate manufaa yoyote.

Rai hiyo inajibiwa kwamba, kumkandamiza mke kunaweza kutokea hata katika ndoa ya kawaida, bali jambo hilo linatokea mara nyingi, mume anamkandamiza mkewe halafu anamuhama au anampa talaka, na jambo hilo linaambatana zaidi na imani na tabia na halina uhusiano na aina ya ndoa.

Aina hiyo ya ndoa haiafikiani na yaliyotajwa na Mwenyezi Mungu kuhusu mume na haki yake ya kuwa mlinzi wa mkewe; kwani katika aina hiyo ya ndoa hatobeba jukumu la kutoa matumizi wala pahala pa kukaa, na Mwenyezi Mungu Amefanya mume awe msimamizi wa mkewe kwa mambo mawili;

La kwanza: Kwa alichofdhilisha kati yao, kwa maana kwa sababu ya sifa ambazo Mwenyezi Mungu Amewapa katika uwezo wa kuvumilia na subira.

 La pili: kwa wanachokitoa; mahari na matumizi.

Rai hiyo inajibiwa kwamba kukubali kwa mume suala la mkewe kuacha haki yake ya kupata matumizi hakumaanishi mume aache haki yake ya kuwa msimamizi kwa mkewe; hakuna uhusiano baina ya masuala hayo mawili.

(Upambanuzi katika tofauti zilizopo kati ya ndoa ya Misyaar na ndoa ya Mutaa’ “ndoa ya muda maalumu”)

Ndoa ya mutaa inakuwa mwanamume kumwambia mwanamke: nakupa kadhaa ili nitembee nawe kwa siku moja, mwezi mmoja au mwaka n.k. akiainisha muda kama ilivyotangulia katika mifano au akiuacha bila ya kuainisha yote ni sawa, kama kusema: Nakupa kadhaa nitembee nawe nawe msimu wa Hija au kwa muda nitakaobaki nchini au mpaka Zaidi arudi. muda ukiisha talaka inatuka.

Ndoa ya mutaa ni aina mojawapo wa ndoa za kijahiliya, nayo ilikuwa halali mwanzoni mwa Uislamu halafu ikaharamishwa, na hii ndio rai kwa mujibu wa makubaliano ya pamoja ya wanazuoni kwa wa Madhehebu ya Malik, Hanafi, Shafi na Hanbal.

Baadhi ya wanaopinga ndoa ya misyaar wamelinganisha baina ya ndoa ya mutaa na ndoa ya misyaar wakasema kuwa ndoa ya misyaar haramu, na kunakuwepo tofauti kubwa baina ya aina hizo mbili nayo ni kwamba:

Ndoa ya mutaa inakuwa na muda maulumu kwa ujira au mahari maalumu tena muda huo aghalabu unaainishwa kwa mujibu wa ujira au mahari tofauti na ndoa ya misyaar ambayo hapangiwi muda tena inakuwa na sifa ya kudumu inayoendelea mpaka talaka.

Halikadhalika mwanamke hapati talaka katika ndoa ya mutaa lakini anaachana na mumewe wakati wa kuisha muda waliouafikiana, ilhali anapata talaka yake katika ndoa ya misyaar ikitokea talaka.

(Upambauzi katika tofauti zilizopo kati ya ndoa ya Misyaar na ndoa ya Muhalalishaji)

Baadhi ya wanaopinga wa ndoa wa Misyaar wamelinganisha baina ya ndoa ya misyaar na ndoa ya muhalalishaji ambayo Mtume s.a.w. amelaani na akamlaani mwenye kuifanya.

Mtazamo huo unajibiwa kwamba. Ndoa ya Muhalil sio kusudio lenyewe; bali inakusudiwa kwa ajili ya kufikia lengo mwanamume mwingine mume wa kwanza kumrudisha mke wake.

 Ama ndoa ya Misyar, hapa lengo ni ndoa waliyokubaliana mume na mke na wakaikusudia ndoa baada ya kutambuana na kukubaliana nayo ni ndoa ya kudumu kama ndio zote wanazofunga Waislamu, asili ya ndoa ni nia ya kuendelea kwa ndoa na kudumu.

Kwa ufupi ni kwamba, misyaar ni ndoa sahihi na inajuzu kisharia ikiwa na nguzo za ndoa na masharti zake zinazotakiwa kisharia, aidha mwanamke kuacha baadhi ya haki zake za makazi au kupata matumizi ya nyumbani au mojawapo, ni jambo ambalo halibatilishi mkataba wa ndoa, pamoja na kujuwa kwamba mwanamke ana haki ya kuomba haki yake ya makazi na kupata matumizi ya nyumbani wakati wowote akitaka, naye mumewe analazimika kulitekeleza ombi lake.

Tena aina hii ya ndoa licha ya kuwa ni sahihi ila ikipatikana khofu ya kuwepo madhara au kuenea uovu katika jamii– kama watu kuacha ndoa ya kawaida ya kisharia wakafuata ndoa ya misyaar – hapo kiongozi anaweza kuizuia kwa sababu hiyo, na hilo linaingia katika mlango wa sera za kisharia kama alivyofanya Umar R.A. alipomwamrisha Huzaifa R.A. amwache mke wake Myahudi akisema: “Naogopa kuacha kuwaoa wanawake Waislamu na kuoa wanawake ambao hawakutulia”. Ingawa asili katika ndoa hiyo ni sahihi.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

[1] Al Mughny 7/72.

[2] Al Mughny 77.

[3] Fataawaa Muaasara cha Shekhe Qardhawy 3/300, Pamoja na Al Sharh Al Kabeer cha Sheykh Al Derdeer 2/236.

Share this:

Related Fatwas