Hukumu ya Kuvaa Mapambo ya Dhahabu ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya Kuvaa Mapambo ya Dhahabu au Fedha kwa Wanaume na Wanawake

Question

Je, Kunajuzu kwa wanaume au wanawake kuvaa pete, bangili, mkufu, saa, au vitu vingine vilivyotengenezwa kwa dhahabu, fedha, shaba, chuma au vinginevyo, au haifai?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:

Hakika Mwenyezi Mungu – Subhanahu wa Ta‘ala – amesema katika Kitabu chake Kitukufu: {Sema: Ni nani aliyeharamisha mapambo ya Mwenyezi Mungu aliyowatolea waja wake, na riziki nzuri?} [Al-A‘arāf: 32]. Asili yake ni kwamba ni halali kwa mwanadamu kujipamba kwa vitu vyote ambavyo Mwenyezi Mungu ameviumba katika dunia hii. Lakini imekuja Hadithi kubainisha baadhi ya mambo katika ujumla huu, na ikaharamisha kwa wanaume kuvaa au kutumia dhahabu isipokuwa pale panapolazimu, kama inavyothibitishwa katika Hadithi ya ‘Alī – Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake – amesema: "Nilimwona Mtume wa Mwenyezi Mungu – S.A.W.  – akichukua hariri akaiweka mkono wa kulia, na dhahabu akaweka mkono wa kushoto, kisha akasema: 'Hakika hivi viwili ni haramu kwa wanaume wa umma wangu'." Na Ibn Mājah ameongeza: "Lakini ni halali kwa wanawake wao." Kadhalika katika Hadithi ya Abū Mūsā al-Ash‘arī – R.A. – Mtume wa Mwenyezi Mungu – S.A.W. – amesema: "Kuvaa hariri na dhahabu kumekatazwa kwa wanaume wa umma wangu, na kumehalaishwa kwa wanawake wao." Na zipo hadithi nyingine nyingi katika mlango huu, ikiwa ni pamoja na Hadithi ya Al-Barā’ bin ‘Āzib aliyesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu – S.A.W. – alitukataza mambo saba, ikiwa ni pamoja na pete ya dhahabu, au akasema: duara la dhahabu."

Kwa mujibu wa hayo, Wanzuoni wengi wa Fiq’hi wamekubaliana kuwa ni haramu kwa wanaume kuvaa au kutumia dhahabu, tofauti na wanawake, kwa kufuata maandiko haya. Hawakutoa ruhusa kwa wanaume katika matumizi ya dhahabu isipokuwa pale panapokuwa na dharura, kama vile mtu aliyekatwa pua yake – kwa sababu imesimuliwa kwamba: "‘Arfajah bin As‘ad alikatwa pua yake siku ya vita vya al-Kilāb, akajitengenezea pua ya fedha, lakini ikaanza kutoa harufu mbaya. Mtume – S.A.W.  – akamwamuru atengeneze pua ya dhahabu."

Kadhalika, kufunga meno kwa dhahabu kwa mwenye haja ya kufanya hivyo; kwa kuwa al-Athram amepokea kutoka kwa Abū Ḥamzah, Mūsā bin Ṭalḥah, Abū Rāfi‘ na Ismā‘īl bin Zayd bin Thābit kwamba walifunga meno yao kwa dhahabu.

Na Ahmad amesema: "Imesimuliwa kuwa katika upanga wa ‘Uthmān bin Ḥanīf kulikuwa na msumari wa dhahabu" na akasema: "‘Umar alikuwa na upanga uliokuwa na vipande vya dhahabu," kwa kauli ya Ibn Umayyah kutoka kwa Nāfi‘.

Imepokewa katika Sunan At-Tirmidhiy kuwa: "Hakika Mtume (S.A.W.) aliingia Makkah na juu ya upanga wake kulikuwa na dhahabu na fedha." Na kuna athari nyingine nyingi zilizopokelewa ambazo zinaonyesha kuwa inaruhusiwa kwa wanaume kutumia dhahabu endapo kuna dharura inayolazimu hilo.

Na hii ndio rai Wanazuoni wa Madhehebu ya Hanafiy, kwani imeandikwa katika juzuu ya tano ya Tanuwir al-Absar na maelezo yake katika mlango wa "Mambo yaliyokatazwa na kuruhusiwa," kwa muhtasari: “Haifai kwa mwanaume kujipamba kwa dhahabu au fedha, isipokuwa kwa pete, mshipi wa kiunoni, au mapambo ya upanga kwa fedha ikiwa hajakusudia kujipamba. Inaruhusiwa pia kutengeneza pua ya dhahabu na kushikilia jino kwa dhahabu kulingana na kauli ya Muhammad, na ni riwaya kutoka kwa Abu Yusuf.” Na maoni haya yanapatikana pia katika madhehebu ya Shafi’iy. Al-Nawawiy alisema katika al-Majmū‘: “Inajuzu kwa mtu aliyevunjika pua kutengeneza pua ya dhahabu hata kama inawezekana kuitengeneza kwa fedha. Na katika hukumu hiyo hiyo ni jino na ncha ya kidole, inajuzu kuvifanya kwa dhahabu bila kutofautiana.” Kisha akasema: “Ikiwa kuna ulazima wa kutumia dhahabu basi inaruhusiwa kwa makubaliano ya madhehebu; kwa hivyo pua na jino la dhahabu ni halali.”

Halikadhalika, madhehebu ya Malikiy na Hanbal wamekubaliana juu ya hili.

Kwa hiyo, dhahabu ni haramu kwa wanaume, isipokuwa pale ambapo kuna dharura ya matumizi yake.

Na haitahesabiwa kuwa ni dhahabu iliyokatazwa kile kilichopakwa (kutiwa) dhahabu kwa sababu haiwezi kutolewa kutoka humo, na pia hakuitwi dhahabu.

Vivyo hivyo, inachukiza kwa wanaume kutumia fedha, tofauti na wanawake, isipokuwa katika pete. Kwa kuwa, maimamu wanne wameruhusu wanaume kuvaa pete ya fedha; kwa sababu imepokewa kwamba Mtume (S.A.W.) alikuwa na pete ya fedha, nayo ilikuwa katika mkono wake mtukufu mpaka alipofariki dunia. Kisha ikawa katika mkono wa Abu Bakr (R.A.) mpaka alipofariki, kisha kwa ‘Umar (R.A.) hadi alipofariki, kisha kwa ‘Uthman (R.A.) mpaka ilianguka kutoka mkononi mwake kwenye kisima, akatumia mali nyingi kuitafuta lakini hakuipata. Na halali kutumia fedha kwa wanaume inabakia tu pale ambapo kuna dharura ya kuitumia. Tumeshaeleza kilichoandikwa katika Tanwir al-Absar kuwa: "Haifai mwanaume kujipamba kwa dhahabu wala fedha isipokuwa kwa pete, mshipi wa kiunoni, au mapambo ya upanga kwa fedha ikiwa hajakusudia kujipamba.". Na maoni haya pia ndiyo yaliyochukuliwa na wafuasi wengi wa wa madhehebu ya Shafi’iy. Al-Rafi‘iy amesema katika Sharh al-Wajīz: "Inajuzu kwa mwanaume kuvaa pete ya fedha kwa kuwa imepokewa kwamba Mtume (S.A.W.) alitengeneza pete ya fedha. Na halali kwake kuvaa mapambo mengine ya fedha kama bangili, kidani au mkufu." Lakini maandiko ya kitabu yanaonesha kuwa inakatazwa, kwani alisema: "Haifai kwa wanaume isipokuwa pete tu." Na haya ndiyo maoni ya wengi. Abu Sa‘īd al-Mutawalliy alisema: "Ikiwa imehalalishwa pete ya fedha, basi hakuna tofauti kati ya vidole na sehemu nyingine za mwili, kama ilivyo kwa wanawake na mapambo ya dhahabu. Hivyo, mwanaume anaweza kuvaa bangili katika mkono wa juu, mkufu shingoni, na bangili ya mkononi, na mengineyo." Na hayo ndiyo aliyoyajibu mwandishi katika vitabu vya fatwa, akisema: "Hakuthibiti kuhusu fedha isipokuwa uharamu wa vyombo (kama vikombe, sahani) na uharamu wa mapambo yanayopelekea kufanana na wanawake."

Wafuasi wa Madhehebu ya Hanafiy walichukia kuvaa pete isiyokuwa ya fedha. Imeandikwa katika Al-Durr al-Mukhtār: "Asivae pete isipokuwa ya fedha kwa sababu ya kutosheka nayo; hivyo, ni makruh kuvaa pete ya chuma, shaba, au risasi."

Na imeandikwa katika Haashiyat Radd Al-Muhtār ‘ala Al-Durr: "Imepokewa na mwenye Sunan kwa isnadi yake kutoka kwa ‘Abdullah bin Buraydah kutoka kwa baba yake kuwa mtu mmoja alikuja kwa Mtume (S.A.W.) akiwa na pete ya shaba, Mtume akasema: ‘Mbona nasikia harufu ya masanamu kutoka kwako?’ Basi akaiondoa. Kisha akarudi akiwa na pete ya chuma, Mtume akasema: ‘Mbona nakuona umevaa mapambo ya watu wa Motoni?’ Basi akaiondoa. Akasema: ‘Ewe Mtume wa Allah, nichukulie nivae nini?’ Akasema: ‘Chukua ya fedha, lakini isizidi uzito wa mithqaal (kiasi maalum cha fedha).’”

Na kwa muhtasari, tunapata yafuatayo:

Dhahabu ni haramu kwa wanaume na halali kwa wanawake kwa mujibu wa maoni ya wanazuoni wengi wa wa fiqhi, isipokuwa pale dharura inapolazimu, basi inaruhusiwa kwa wanaume. Na vyombo vya dhahabu ni haramu hata kwa wanawake vilevile.

Fedha ni makruh (haipendelewi) kutumika na wanaume kwa mujibu wa maoni ya Hanafiyya na wanazuoni wengi wa Shafi‘iyya, isipokuwa katika pete, kwani inajuzu mwanaume kuvaa pete ya fedha bila makruh, na pia inajuzu kutumia fedha katika hali ya dharura. Kwa wanawake, ni haramu kutumia vyombo vya fedha kwa mujibu wa maandiko ya wazi. Na baadhi ya wanazuoni wa Shafi‘iyya waliona kuwa inaruhusiwa kwa wanaume kutumia fedha bila makruh mradi tu haitumiki kwa namna ya kuiga wanawake.

Vyombo au mapambo ya madini mengine kama chuma, shaba, n.k., yanabakia katika hukumu ya asili ambayo ni uhalali. Hakuna aliyepinga hilo isipokuwa wafuasi wa madhehebu ya Hanafiyya, ambao walichukia wanaume kuvaa pete ya aina yoyote ya madini hayo.

Na kwa kwa haya, jibu la swali huwa limebainika.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi

Share this:

Related Fatwas