Hukumu ya Mwanamke Kuvaa Suruali na Sifa za Mavazi ya Mwanamke
Question
Kwanza: Ni nini hukumu ya kuvaa suruali iliyobana kwa mwanamke?
Pili: Ni yapi masharti ya lazima yanayotakikana kwa mavazi ya mwanamke katika Sharia ya Kiislamu? Na ni sehemu zipi zinazoruhusiwa kuonekana katika mwili wa mwanamke?
Tatu: Ni ipi hukumu au adhabu ya kuvunja masharti na vidhibiti vya mavazi ya mwanamke?
Nne: Ni nini hukumu ya mwanamke kuweka mapambo na (Make up), uturi wakati anapotoka nje ya nyumba yake hata kwa muda mchache?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Kwanza: Kuvaa suruali ikiwa ni pana, haibani, haidhihirishi wala haioneshi sehemu za mwili, wala haioneshi sehemu za siri, wala haisababishi fitina kwa wanaume na wanawake, basi hakuna tatizo kisheria katika hilo, na inaruhusiwa kuvaa suruali hiyo kwa ajili ya mahitaji ya maisha ya kila siku. Lakini ikiwa suruali ni ya kubana, inaonesha maumbile ya mwili na inaweka wazi sehemu za siri, basi kuvaa suruali hiyo ni haramu kisharia kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu: {Wala msijionyeshe uzuri wenu kama walivyofanya wanawake wa enzi ya ujahiliya wa kwanza} [Al-Ahzab: 33].
Pili: Masharti yanayopaswa kupatikana katika vazi la kisharia la mwanamke: Haramu kwa mwanamke kuvaa nguo ambazo dhihirisha (maumbile ya mwili) au zinazoonesha yaliyo chini yake, au zinazobana sehemu za mwili hasa zile sehemu zenye kuleta fitina. Mwanamke anaruhusiwa kuvaa apendavyo kwa sharti kwamba nguo hizo zifunike mwili wake wote isipokuwa uso na viganja vya mikono; anaweza kuviacha wazi kama atataka, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu: { Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao...} [An-Nur: 31].
Tatu: Adhabu ya kukiuka masharti haya ni adhabu kali, na kiwango cha adhabu hiyo kiko katika elimu ya Mwenyezi Mungu na matakwa Yake. Kujipamba kupita kiasi na kujiachia wazi ni miongoni mwa madhambi makubwa kisheria, kwa sababu kunapelekea ufisadi na kueneza maovu katika jamii. Ni wajibu kwa muulizaji kumnasihi mhusika kwa hekima na mawaidha mema, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: {Lingania kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri} [An-Nahl: 125].
Kuhusu mwanamke kutumia vifaa vya mapambo – kama vipodozi na marashi – ikiwa nia yake ni kujipamba kwa ajili ya mumewe, basi hakuna tatizo lolote kisharia, mradi tu vifaa hivyo vimetengenezwa kwa vitu halali. Lakini ikiwa nia yake ya kujipamba ni kwa ajili ya kujionesha na kujiachia wazi nje ya nyumba yake, basi jambo hili ni haramu na limekatazwa kisheria.
Kwa yaliyotajwa hapo juu, jibu la swali lililoulizwa huwa limebainika.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
