Salamu (maamkizi) ya mdogo kwa mkubwa
Question
Inapaswa — kama nilivyosoma — kwa Muislamu mdogo kumsalimu Muislamu mkubwa, na mpandaji kumsalimu anayetembea, na anayeingia kumsalimu aliyepo (anayepita kwa aliyekaa). Basi itakuwaje ikiwa mpandaji au anayeingia ndiye mkubwa zaidi, nani anapewa kipaumbele na nani inampasa kuanza salamu kwanza?
Na nimesoma pia kuwa Ali bin Abi Talib hakumsalimu Swahaba mmoja mkubwa zaidi yake wakati mmoja, na Swahaba huyo alipomuuliza kwa hasira: kwa nini Ali hakumsalimia, Ali alijibu kuwa alitaka kumpa nafasi mkubwa kuanza salamu, kwa sababu anayeanza salamu thawabu zake ni kubwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Je, simulizi hii ya Ali ni sahihi? Na ikiwa hivyo ndivyo, vipi mtu anaweza kupatanisha kati ya kitendo cha Ali na amri iliyotajwa hapo awali kwamba mdogo anatakiwa kumsalimu mkubwa?
Answer
Kwa jina la Mwnyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Aliyestahiki kuanza kwa salamu wakati huo ni anayepita au mpandaji, awe mdogo au mkubwa, kama walivyobainisha kundi la Wanazuoni miongoni mwao Imamu Ibn Rushd, Nawawiy na al-Muhallab. Na mazungumzo yote hapa ni kuhusu ustahiki si kuhusu wajibu, na kwa sababu hiyo Imamu Al-Maziriy — kama alivyonukuliwa kutoka kwake na Al-Hafidhi Ibn Hajar katika Fath Al-Bariy — alisema: “Hali hizi hazipingwi na matukio ya mtu mmoja yanayokwenda tofauti; kwa sababu hazikuwekwa kama sababu za lazima zinazopaswa kuzingatiwa kiasi kwamba haijuzu kutoka nje yake, hata ikiwa anayetembea ataanza akamsalimu mpandaji haizuiwi; kwa sababu anatekeleza amri ya kutoa salamu na kuieneza. Isipokuwa tu, kuzingatia yale yaliyothibiti katika Hadithi ni bora zaidi, na ni habari yenye maana ya amri kwa njia ya kupendekeza, na hailazimu kuacha jambo linalopendekezwa ni kuwa linachukiza (makruh), bali ni kwenda kinyume na lililo bora, hivyo ikiwa yule aliyekuwa ameagizwa kuanza salamu aliacha na mwingine akaanza, basi aliyekuwa ameagizwa ameacha jambo la kupendekezwa na mwingine amefanya Sunna, isipokuwa kama alitangulia (kabla ya wakati unaofaa) naye pia atakuwa ameacha lililo bora.”
Na juu ya hili huchukuliwa yaliyopokelewa kuhusu Sayyiduna Ali bin Abi Talib (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) na simulizi kama alivyoitaja Imamu Ibn Abi Jamrah katika Sharh Al-Bukhari ni kwamba Sayyiduna Ali bin Abi Talib (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) alikuwa kila alipokutana na Abu Bakr (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) alikuwa akianza yeye kwa salamu, kisha siku moja akamgeukia (hakumsalimia), basi Abu Bakr akaanza yeye kwa salamu. Kisha Abu Bakr akamwarifu Mtume (Rehma na amani zimshukie) kuhusu Ali kumgeukia, akamwita Mtume (Rehma na amani zimshukie) na kumwuliza. Ali (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) akasema: Niliona usiku wa jana ndotoni kasri (jengo kubwa), nikasema: Ni la nani hili? Ikasemwa: Ni la yule anayeanza kumtangulia mwenzake kwa salamu. Nikataka nimpe Abu Bakr (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie), fadhila hiyo kuliko nafsi yangu.
Basi maana ambayo Sayyiduna Ali aliacha kuanza kwa salamu kwa ajili yake — nayo ni kumpa mtu wa fadhila kipaumbele kwa fadhila — ni ya ziada zaidi katika adabu kuliko ile maana ambayo imependekezwa kwa ajili ya kuanza mdogo kwa salamu. Na ni jambo lililoamuliwa kuwa adabu ya juu inapewa kipaumbele juu ya kufuata amri isiyo ya lazima; ambapo Mtume (Rehma na amani zimshukie) aliwakubalia Maswahaba katika kuipa adabu kipaumbele juu ya ufuataji, akamkubalia Sayyiduna Ali kwa kutokufuta jina lake tukufu (Muhammad Rasulullah) walipomwomba washirikina afanye hivyo katika Suluhu ya Hudaybiyyah, akamuamrisha Ali alifute, lakini akakataa, na akamkubalia Sayyiduna Abu Bakr kwa kutotangulia na kukataa kwake kuswali Imamu pamoja na Mtume (Rehma na amani zimshukie) alipomwonesha ishara hiyo alipotoka katika chumba chake na Abu Bakr akiwa anawaongoza watu katika Swala. Atufundishe Mwenyezi Mungu na wewe, na atufanikishe na wewe katika anachokipenda na kuridhia.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
