Ukeketaji wa wanawake
Question
Jumuia imepokea maswali kadhaa kuhusu hukumu ya Ukeketaji. Kutokana na mgongano na ufadhili kutoka pande mbalimbali za msaada ambazo zimefanya kazi hapo awali kuhimiza kuharamisha Ukeketaji wa wanawake, na kuna baaadhi ya Mashekhe wakubwa anasema kinyume na hilo; jambo linalotufanya kushindwa kutoa rai ya kisharia; hivyo basi tunatarajia mtupe Fatwa kuhusu maudhui hii.
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Sahihi kwamba Ukeketaji wa wanawake ni katika sehemu ya mila na si sharia, jambo ambalo ni sharia ni Ukeketaji wa wanaume kwa makubaliano ya wanazuoni. Imamu Ibn Al-Haj amesema: “Wametofautiana katika haki yao: je, wanapunguza moja kwa moja au wanatofautisha kati ya Mashariki na Magharibi” ([1]).
Imamu Ash-Shaukany anasema: “Pamoja na kuwa Hadithi haifai kutelea dalili basi hakuna dalili kwa kinachotakiwa” ([2]).
Na Abady anasema: “Na Hadithi ya Ukeketaji wa mwanamke imepokewa katika njia nyingi, na zote ni dhaifu, zina kasoro, hakusihi kuzitolea dalili kama ilivyojulikana. Ibn Al Mundhiri amesema: Hakuna katika Ukeketaji wa mwanamke Hadithi inayofuatwa. Na Ibn Abdil Bar amesema katika Tamhid: Waislamu wamekubaliana kwamba kutairi ni kwa wanaume, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi” ([3]).
Haya yote yanajulisha kwamba suala la Ukeketaji wa mwanamke si suala la kidini la kiibada katika asili yake, lakini ni suala linalorejea katika turathi za kitabibu na kiada. Na baada ya kutafiti tumekuta kwamba ada hii inafanywa kwa njia yenye madhara inayotufanya tuseme kwamba ni Haramu kisharia. Na wanazuoni wengi wameelezea hili baada ya kutafiti sana na kwa maelezo mbalimbali:
Miongoni mwao ni marehemu Shekhe Muhammad Arafa, mjumbe wa jumuia ya Wanazuoni wakubwa, amesema: “Ikithibiti kwamba yote hayo basi hakuna ubaya kwa mwanamke anayefanya Ukeketaji”. Kisha akaendelea akasema: “Na kama itapigwa marufuku hapa Misri kama ilivyopigwa marufuku nchi nyingine za Kiislamu, kama Uturuki na Moroco basi hakuna ubaya, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwafikisha vilivyo ndivyo” ([4]).
Muheshimiwa Imamu Mkuu Shekhe wa Al-Azhar Prof. Muhammad Tantawy anasema katika Fatwa yake: “Ama kwa upande wa wanawake hakuna andiko la kisharia sahihi linalotolewa Ushahidi wa Ukeketaji wa mwanamke, na rai yangu ni kwamba hii ni ada iliyoenea hapa Misri kutoka kizazi hadi kizazi kingine, na inakaribia kutoweka na kupotea kwa matabaka yote, hasa tabaka la Wasomi”, kisha anaendelea kusema: “Tunakuta nchi nyingi za Kiislamu zilizojaa Wanazuoni wa Fiqhi zimeacha Ukeketaji wa wanawake; miongoni mwa nchi hizi ni Saudia Arabia, na nchi za ghuba, pia Yemen, Iraq, Syria, Lebanon, Jodan, Palestina, Libya, Algeria, Morocco na Tunisia”.
Dkt. Yussuf Qardhawy anasema katika tafiti yake iliyotolewa kuhusu hukumu ya kisharia katika Ukeketaji wa wanawake: “Na kutokana na asili hii iliyopitishwa na kuafikiana (Inakusudiwa kuliacha umbo aliloumba Mwenyezi Mungu kama Alivyoliumba na kutolibadilisha) na Ukeketaji wa wanawake au kupunguza kwa kukata sehemu katika mwili wa mwanamke pasi na kuacha kunawajibisha jambo jingine linaloruhusiwa au lisiloruhusiwa kisharia.
Dkt. Slim anasema kwamba hukumu ya kisharia katika Ukeketaji wa mwanamke si wajibu, wala Sunna, wala kupendeza; kwa udhaifu wa Hadithi zote zilizopokewa katika hilo, bali ni ada, na ada yenye madhara ya wazi, Wanazuoni wa Fiqhi wamewajibisha kuwa ikiwa inakosesha starehe ya mwanamke anapokutana na mwanamume kwa sababu ya Ukeketaji wamewajibisha kisasi au fidia.
Huenda muulizaji anauliza: Kwanini ada hii imeendelea?
Tunasema kwamba imeendelea kwa kutodhihiri madhara yake, kwa hakika madhara yake yamedhihiri na madaktari wamethibitisha, basi kupiga marufuku wakati huo ni wajibu, na kutokea madhara wakati huo kumekuwa ni kwa Yakini; kwa kutofautiana mavazi na ufinyu wake, na kusambaa njia mpya za Maisha na kwa haraka, na kuchafuka mazingira, na kutofautina katika chakula, hewa na aina ya Maisha, na maendeleo ya tiba ambayo yamethibitisha madhara ya moja kwa moja, pia na kutofautiana umadhubuti wa mwili wa mwanadamu katika majeraha na mfano wa hayo.
Na mwenye kusoma vitabu vya Wanazuoni wetu waliotangulia atagundua ukweli wa jambo hili, hata kwa wale wanaosema kwamba Ukeketaji wa wanawake ni kama kutairi wanaume, ni kuweka jeraha tu katika ngozi ya juu ya tupu pasi na kukata ngozi.
Al Maroudy anasema: “Ni kukata ngozi kunakuwa juu ya tupu: kama ngozi ya kokwa ya tende au ngozi ya juu ya jogoo, kukata Ngozi hii ya juu pasi na kuiondosha yote” ([5]).
Annawawy amesema: “Kukata sehemu ya juu katika Ngozi ambayo ipo juu ya tupu” ([6]).
Hapa inabainika kuwa kukata maana yake ni kupasua na si kuondosha Ngozi yote, na hili ndilo linalojulishwa na Hadithi dhaifu “Ondoa sehemu iliyozidi wala usikate chote”, na jambo hili linahitaji daktari wa vidonda mbobezi katika masuala ambayo katika zama zetu yamekuwa yana madhara katika mwili wa mwanadamu moja kwa moja, pasi na haja ya kisharia.
Watu wangi wamelirudisha suala hili kwa madaktari, na madaktari wamethibitisha madhara yake, ikiwa ni lazima kusema kuwa ni haramu. Dr, Yussuf Qardhawy anasema: “Mambo halali yanaweza kuzuiwa yakiwa yanasababisha madhara kwa kuyafanya; kutokana na kanuni ya “Usidhuru wala usijidhuru”, na jambo hili la halali linazuiwa kwa kuepusha madhara na uharibifu”.
Na kwa wale wanaobisha hili wamche Mwenyezi Mungu, na wajue kwamba Fatwa inahusiana na ukweli wa uhalisia, na kwamba suala la Ukeketaji limebadilika na limekuwa linadhuru sana, kimwili na kisaiklojia jambo ambalo linalazimisha kusema kuwa ni haramu kwa makubaliano ya Wanazuoni katika hilo, pasi na kutofautisha neno, na tofauti isiyokuwa na utetezi.
Hakika anayechambua uhalisia wa jambo hana namna isipokuwa kusema ni Haramu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi
([1]) Al Madkhal, 3/310. Angalia Fathul Bary cha Ibn Hajar 10/340.
([2]) Nayl Al Awtaar. 1/19.
([3]) Aun Al- Maaboud. 14/126.
([4]) Makala yake katika jarida la Al-Azhar namba 24 la mwaka 1952, uk. 1242.
([5]) Fathu ALBary cha Ibn Hajar. 10/340.
([6]) Al Majmou. 3/148.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
