Usawa Kati ya Mwanamume na Mwanamke...

Egypt's Dar Al-Ifta

Usawa Kati ya Mwanamume na Mwanamke

Question

Je, Uislamu umeweka usawa kati ya mwanamume na mwanamke, au umemfanya mwanamke kuwa chini ya mwanamume?

Answer

Miongoni mwa haki za Ibnadamu zilizo wazi kabisa katika Uislamu ni haki ya usawa kati ya mwanamume na mwanamke katika haki na wajibu. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita mito kati yake.} [Al-Imran: 195].

Aya hii imethibitisha usawa kati ya mwanamume na mwanamke katika malipo, kama ilivyothibtisha usawa kati yao katika matendo. Ama makusudio ya kauli ya Mtume (S.A.W): ((... Sijaona miongoni mwa wenye upungufu wa akili na dini walio washindi zaidi kwa wenye akili miongoni mwenu)) basi ni kile alichokielezea Mtume (S.A.W) mwenyewe wakati mwanamke alipomuuliza:

((Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ni nini upungufu wa akili na dini? Akasema: Ama upungufu wa akili: basi ni ushahidi wa wanawake wawili unalingana na ushahidi wa mwanamume mmoja, huu ndio upungufu wa akili, na hukaa masiku haswali, na hufuturu katika Ramadhani, huu ndio upungufu wa dini)).  Upungufu huu unatokana na asili ya uumbaji kwa mwanamke, na unahusiana na yale yanayomfika miongoni mwa kusahau; na kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu akafanya ushahidi wake kuwa ni nusu ya ushahidi wa mwanamume, huu ndio upungufu wa akili, na yale yanayomfika miongoni mwa ada ya kila mwezi "Hedhi" inayomzuia kuswali na kufunga, hivyo hakuna lawama kwa wanawake katika hilo, na huu ndio upungufu wa dini; Hadithi hii inahimiza huruma na upole kwa wanawake na kuwatendea wema.

Maelezo

Miongoni mwa haki za Ibnadamu zilizo wazi kabisa katika Uislamu ni haki ya usawa kati ya mwanamume na mwanamke katika haki na wajibu; baada ya mwanamke kuwa kabla ya Uislamu katika baadhi ya jamii hana thamani yoyote, bali alikuwa akidharauliwa na kuwa mnyonge, Uislamu ukaja na kunyanyua nafasi yake na kutukuza hadhi yake na kumpa haki ya kushiriki katika nyanja zote za maisha sawa na mwanamume, na hilo ni kama ifuatavyo:

Ana haki ya kuchagua dini yake.

Ana haki ya kutoa maoni yake katika kuchagua mwenza wa maisha yake.

Ana haki ya kusoma na elimu.

Ana haki ya kurithi baada ya kuwa alikuwa harithi.

Ana haki ya kumiliki na kufanya miamala ya kiraia na kibiashara.

Ana haki kamili ya kushiriki katika maisha ya kijamii na kisiasa kulingana na asili yake na bila kuharibu haki za wengine juu yake; awe mume, baba, watoto au wengineo.

Haki hizi zote na nyinginezo Sharia ya Kiislamu imemdhamini mwanamke jambo ambalo mwanamke hakulifikia katika ustaarabu wowote miongoni mwa staarabu wala dini yeyote miongoni mwa dini.

Dalili za kisharia zimethibitisha usawa huu kati ya mwanamume na mwanamke katika ubinadamu na katika haki na wajibu:

Miongoni mwazo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi} [An-Nisa: 1]. Aya hii inathibitisha asili ya mwanamume na mwanamke na kwamba wote wanatoka katika nafsi moja ambayo ni Adam (A.S).

Na miongoni mwazo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mola Mlezi wao, akayakubali maombi yao akajibu: Hakika sipotezi kazi ya mfanya kazi miongoni mwenu, akiwa mwanamume au mwanamke, kwani ni nyinyi kwa nyinyi. Basi walio hama, na walio tolewa makwao, na wakateswa katika Njia yangu, na wakapigana, na wakauliwa, kwa yakini Mimi nitawafutia makosa yao, na kwa yakini nitawaingiza katika Mabustani yanayo pita mito kati yake.} [Al-Imran: 195]. Aya hii imethibitisha usawa kati ya mwanamume na mwanamke katika malipo, kama ilivyothibitisha usawa kati yao katika matendo.

Na miongoni mwazo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini,tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.} [An-Nahl: 97], na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zaka, na humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.} [At-Tawbah: 71], na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wanaume wana fungu katika walio vichuma, na wanawake wana fungu katika waliovichuma} [An-Nisa: 32]. Wanaosemeshwa katika Aya zilizotangulia wamejumuishwa mwanamume na mwanamke bila ubaguzi wala upendeleo.

Na miongoni mwazo ni kauli ya Mtume (S.A.W): ((Hakika wanawake ni ndugu wa wanaume)  [1].

Hapa linajitokeza Swali: Kuna wale wanaojaribu kuchafua taswira ya mwanamke katika Uislamu na kudai kuwa Uislamu umemfanya mwanamke kuwa chini ya mwanamume; wakitolea dalili kwa yale aliyoyapokea Ibn Majah katika kitabu chake cha Sunan Ibnu Majah, kwamba Mtume (S.A.W) amesema: ((... Sijaona miongoni mwa wenye upungufu wa akili na dini walio washindi zaidi kwa wenye akili miongoni mwenu)), basi vipi tunajibu maneno haya?

Tunajibu hilo na kusema:  Hakika Mtume (S.A.W) ameelezea upungufu huu katika Hadithi mwenyewe, wakati mwanamke alipomwambia: ((Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu na ni nini upungufu wa akili na dini? Akasema: Ama upungufu wa akili: basi ni ushahidi wa wanawake wawili unalingana na ushahidi wa mwanamume mmoja, huu ndio upungufu wa akili, na hukaa masiku haswali, na hufuturu katika Ramadhani, huu ndio upungufu wa dini)). Tunapata faida kutokana na Hadithi hii kwamba upungufu huu unatokana na asili ya uumbaji wa mwanamke, na unahusiana na yale yanayomfika miongoni mwa kusahau, na kwa hiyo Mwenyezi Mungu akafanya ushahidi wake kuwa nusu ya ushahidi wa mwanamume basi huo ndio upungufu wa akili, na yale yanayomfika miongoni mwa ada ya kila mwezi (Hedhi) inayomzuia kuswali na kufunga, hivyo hakuna lawama kwa wanawake katika hilo, na huu ndio upungufu wa dini; Hadithi inahimiza huruma na upole kwa wanawake na kuamiliana nao vizuri.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuumba mwanamume na mwanamke kutokana na nafsi moja, na akaweka usawa kati yao katika haki na wajibu, na Uislamu umenyanyua hadhi ya mwanamke na nafasi yake baada ya kuwa alikuwa akidharauliwa katika baadhi ya jamii kabla ya Uislamu, na Uislamu umesisitiza juu ya kuwatendea wema wanawake na kuwaonea huruma wote.

 

[1] Imepokelewa na Abu Dawud.

Share this:

Related Fatwas