Jinsi mtu mwenye dini anavyotendean...

Egypt's Dar Al-Ifta

Jinsi mtu mwenye dini anavyotendeana na familia yake

Question

Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 18, ni mwanafunzi, bado sijaolewa, nina shida na familiya yangu ni kama yafuatayo:

"Mimi ninashikamana na dini yangu zaidi kuliko familia yangu; familia yangu ni ya Waislamu wa kawaida (wa mila). Wanaamini tu kile walichoambiwa na mababu zao hata kama ni makosa. Wanatazama filamu, nyimbo, na vitu kama hivyo. Wanatumia maneno yasiyo na adabu mara nyingi, na pia wananilazimisha nifanye hivyo. Wanatumia maneno ya kufuru, shirki, na unafiki, nami ninaishi nao.

Tafadhali nisaidieni nijue jinsi ya kuishi nao katika maisha ya kila siku kwa matumaini ya kuwaongoza! Nimewafahamisha kuhusu lililo sahihi lakini hawajanisikiliza hadi sasa, bali wamenitukana kwa sababu ya kufanya da‘wah (kuwaita kwenye dini).

Kwa kweli ninahisi maumivu makubwa ninapoona mtu akifanya kosa mbele yangu.

Tafadhali nisaidieni nijue namna ya kuishi na familia yangu"

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:

Dada mpendwa,

Uwe mpole na mwepesi kwa familia yako. Uislamu haupendi Muislamu kuwa mtu wa kujitenga na watu wanaomzunguka. Na jihadhari kujiona kuwa wewe ni mwenye dini zaidi kuliko familia yako, kwani hujui – huenda wao ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko watu wengi walio kama wewe, hata kama wanafanya mambo ambayo wewe unayaona kuwa ni maasi, ambapo kutazama filamu pekee siyo maasi, isipokuwa maasi ni mtu kuangalia yale yanayomkasirisha Mwenyezi Mungu ndani yake. Na kusikiliza nyimbo pekee siyo dhambi, kwani nyimbo ni maneno – yaliyo mazuri ni mazuri, na yaliyo mabaya ni mabaya. Vilevile, maneno mengi ambayo unadhani kuwa ni ya shirki, kufuru au unafiki, huenda hayana uhusiano wowote na hayo – kwa karibu au mbali. Basi jihadhari kuwahukumu familia yako kwa mambo ambayo si sahihi kisharia. Wala usidhani kuwa wewe ni bora kuliko wao; kwani kipimo mbele ya Mwenyezi Mungu ni ukweli, yakini na ikhlasi – hata kama matendo ni machache. Mche Mwenyezi Mungu kuhusu wazazi wako, na uwe na huruma kwao. Muislamu hujaza huruma kwa wale waliomzunguka. Wala usijione kama wewe ndiye utakayerekebisha ulimwengu mzima – kwani uongofu uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu pekee.

Hata hivyo, hilo halikupi ruhusa ya kugombana au kukereka nao. Ikiwa Uislamu umeamrisha kuwafanyia wema wazazi hata kama ni makafiri, basi vipi ikiwa ni Waislamu?

Tunakuomba ewe dada mpenzi uwe na subira na utulivu, na usisikilize kila mtu anayeongea tu bila elimu. Bali wasikilize wale wanaoelewa dini vizuri – wanazuoni waliobobea – ili njia yako iwe sahihi na iliyonyooka.

Na tunamuomba Mwenyezi Mungu akufanikishie na akuongoze kwenye yale anayoyapenda na kuyaridhia.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi

Share this:

Related Fatwas