Ukamilifu wa Tabia zake katika kuamiliana kwake na wale waliompinga, katika vita na amani.
Question
Vipimo vya utukufu havipimwi kwa wingi wa mali au wafuasi tu, wala kwa ukubwa wa ufalme, ushawishi wa utawala, au nguvu ya hadhi tu; bali, utukufu hupimwa kwa ukarimu wa nafsi, utakaso wa maadili, na ukubwa wa athari zinazoendelea. Hizi ndizo sifa zote zilizojumuika katika tabia ya Mtume mtukufu (S.A.W).
Answer
Vipimo vya utukufu havipimwi kwa wingi wa mali au wafuasi tu, wala kwa ukubwa wa ufalme, ushawishi wa utawala, au nguvu ya hadhi tu; bali, utukufu hupimwa kwa ukarimu wa nafsi, utakaso wa maadili, na ukubwa wa athari zinazoendelea. Hizi ndizo sifa zote zilizojumuika katika tabia ya Mtume mtukufu (S.A.W).
Tumeeleza mara mbili zilizopita kuhusu pande mbili za utukufu katika mtu huyu alietukuzwa; katika sehemu ya kwanza tulizungumza juu ya: "utukufu wa Lengo na Utukufu wa Madhumuni," na katika sehemu ya pili tulizungumzia: "Uzuri wa Tabia," na sasa tutazungumza juu ya: "Ukamilifu wa Tabia Zake (S.A.W) katika muingiliano wake na wanaompinga, katika Vita na Amani."
Hakika Qur'ani inaunga mkono dalili za upekee, tofauti, na utukufu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), si kwa ishara ya siri, bali kwa tangazo la wazi na dhahiri, lisilo na utata wala shaka. Wakati Qur'ani tukufu katika Surah Al-Qalam inamwambia bwana wetu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W): "Na hakika wewe una tabia njema kabisa." (Al-Qalam: 4), je, msomaji mpenzi ataona kitu kingine zaidi ya tangazo la ukamilifu wa tabia yake na ukamilifu wa sifa zake?
Jambo la kwanza linalopaswa kujulikana katika jambo hili ni kwamba ukamilifu wa tabia yake (S.A.W) unatoka kwenye ukamilifu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu hii, harakati zake zote na utulivu wake na ndugu na mgeni, na rafiki na adui, katika hali ya furaha na hasira, katika hali ya wepesi na shida, katika amani na vita, zilikuwa katika daraja la juu zaidi ya ukamilifu wa binadamu, na ishara za juu kabisa za heshima ya maadili. Hakuna ajabu katika hili, kwani yeye ni mwasilishaji wa ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anayetia saini kwa jina lake, akiongea kwa ufunuo wake. Je, Mwenyezi Mungu atamtuma asieweza kupokea wahyi?
Hili linathibitishwa kupitia mahusiano yake na wanaompinga, katika amani na vita.
Tangu Mtume (S.A.W) alipoutangaza wito wake, na Mwenyezi Mungu Mtukufu alipomwamuru kuufikisha kwa watu na viumbe, tunakuta ni wito uliokuja na seti ya kanuni za juu na maadili mema yanayoratibu mahusiano kati ya Uislamu na wengine, ambayo leo yanafahamika kama mahusiano ya kimataifa. Mfano: kanuni ya kutimiza ahadi, uharamu wa kuwaua wajumbe, kuchunga ujirani, kuheshimu haki za binadamu, kulinda utu wake, kuzingatia kanuni za kibinadamu katika mapigano, kutowadhuru wanyonge na watoto, na kujiepusha na kila kitu ambacho asili safi na nafsi nzuri hukikataa.
Kanuni hizi zilizokuwa katika wito wake (S.A.W) zilikuwa msingi wa ustaarabu wa Kiislamu, ambao ulianzishwa na kuchangia kujenga jengo lake kwa muda mfupi. Hili liliwavutia wasomi Mashariki na Magharibi, wa zamani na wa sasa.
Watu walijua desturi na mikataba mbalimbali, ambayo lengo lao lilikuwa kulinda kanuni na sheria za vita. Lakini mara chache sana zilifuatwa au kuzingatiwa.
Pia, katika vita kabla ya utume wake (S.A.W), kila kitu kilikuwa halali: kudhuru wapiganaji na wasiokuwa wapiganaji, uharibifu wa miji, na mauaji ya watu.
Alipokuja Mtume (S.A.W) na wito wake, alikuja na nadharia mpya ya vita, na akaweka sheria ambayo utu wa binadamu unaheshimiwa na nafsi ya binadamu inalindwa. Hili linathibitishwa na mwongozo wake Mtume (S.A.W). Alipokuwa akituma kikosi, aliwaambia: "Wafanyieni watu wema na waelewe. Msiwashambulie mpaka muwaite. Ni bora kwangu mniletee watu wote duniani wakiwa Waislamu, kuliko kuwaletea watoto wao na wanawake wao na kuwaua wanaume wao." ([1])
Maneno haya yanabainisha mwongozo wake Mtume (S.A.W) katika kuingiliana na wengine katika hali ngumu zaidi. Pia inavyobainisha seti ya sheria ambazo Mtume (S.A.W) aliziweka kwa ajili ya vita katika Uislamu, na miongoni mwa muhimu zaidi ni:
Kwanza: Mapigano ni dhidi ya wapiganaji: Hupaswi kupigana na mtu wa dini aliyejitenga katika nyumba yake ya ibada, wala mtu wa kawaida aliye njiani au amejifungia nyumbani kwake, wala mzee, wala mtoto, wala mwanamke.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: (Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaokupigeni, wala msivuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanaovuka mipaka.) [Al-Baqara: 190]. Na kauli Yake Mtukufu: (Hakika wale walio amini na wakahama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, na wale walio toa mahala pa kukaa, na wakanusuru, hao ni marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale walio amini lakini hawakuhama, nyinyi hamna waajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipo kuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.) [Al-Anfal: 72].
Na kauli Yake Mtukufu: (Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia) [Al-Hajj: 39]. Na Mtume (S.A.W) alisema: "Piganeni, wala msiibe, wala msifanye udanganyifu, wala msiharibu maiti, wala msimuue mtoto." ([2])
Pili: Kuzuia uharibifu: Kwa kuhifadhi jamii ya binadamu, usikate miti, wala minazi, wala usibomoe nyumba, wala usiharibu mazao, wala usivunje mahekalu au sehemu za ibada za wasiokuwa Waislamu, wala usichafue maji. Sayyidna Abu Bakr As-Siddiq (R.A) alipowatuma askari Syria alisema:
"Msiaharibu mitende wala msiichome, wala msimchinje wanyama, wala mti wenye matunda, wala msibomoe nyumba ya ibada, wala msiwaue watoto, wala wazee, wala wanawake. Na mtawakuta watu waliojifungia katika mahekalu, waacheni na yale waliojifungia." ([3])
Tatu: Kuamiliana kwa usawa: Kujibu mashambulizi kunapaswa kufanywa kwa wema, hakuna kuvunja hakuna kuvunja heshima. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: (Na mkilipiza basi lipizeni sawa na vile mlivyo adhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanao subiri.) [An-Nahl: 126]
Nne: Kuwalinda mateka na kuwatendea wema kulingana na ubinadamu wao: Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: (Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa.) [Al-Insan: 8]. Katika hadithi kutoka kwa Abu Aziz bin Umair - kaka yake Mus’ab bin Umair - amesema: "Nilikuwa miongoni mwa mateka siku ya Badr, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alisema: “Watendeeni wema mateka”. Nilikuwa pamoja na kundi la Ansari, na walipoandaa chakula chao cha mchana na cha jioni, walikula tende na kunilisha mkate, kama Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) alivyowaagiza kufanya ([4])”. ([5]).
Hakika mipaka hii iliyowekwa na Uislamu na kutekelezwa na Mtume wake (S.A.W) na akawafundisha Maswahaba zake na wote waliowafuata katika njia yao — imetokana na mtazamo wa Uislamu kuhusu vita; ambapo huiona kama dharura ya kipekee tu. Hata hivyo, dharura hii imefungwa na kanuni ya jumla inayozingatia udugu wa kibinadamu na heshima ya binadamu.
Dalili ya hili ni yaliyomo katika barua ya Sayyidina Ali bin Abi Talib kwa Al-Ashtar Al-Nakha’i: “Jiepushe na damu na kumwaga damu isivyo halali; kwani hakuna kitu kinachochochea hasira (ya Mwenyezi Mungu) zaidi, wala kisicho na madhara makubwa zaidi, wala chenye kuondoa neema na kukatisha muda haraka zaidi kuliko kumwaga damu isiyo ya halali. Na hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye ataanza kuhukumu baina ya waja Siku ya Kiyama kwa yale waliyomwagiana damu.”[6]
Na sababu ya hilo ni kuwa, vita katika Uislamu haikuwekwa isipokuwa kwa dharura; kwa ajili ya kuzuia uvamizi dhidi ya Waislamu, ardhi zao na mali zao, na kwa ajili ya kupambana na dhuluma na kuwasaidia wanyonge, au pale inapokuwa kuna hali ya kujiandaa kwa mapigano.
Wala hakuna shaka kuwa dharura hupimwa kwa kiwango chake; haiwezi kuwa njia ya kuendelea na batili, au kutenda dhuluma kwa wengine, au kutumia fursa kwa ajili ya uharibifu na uteketezaji, au kuridhisha matamanio ya kujikweza, kutawala na kujifanyia jeuri kwa viumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.[7]
Tunasema haya wakati huu tunaposhuhudia uvamizi wa kinyama wa Kizayuni ulioanzisha vita dhidi ya watu wasio na silaha, wanyonge; vita ambayo imehalalisha kila kitu ndani yake, ikatumia njia za halali na zisizo halali; jambo linaloonesha — bila shida — jeuri ya adui huyu na kutokujali haki za msingi za kibinadamu na utu.
Matendo yao yanafichua asili yao halisi na mtazamo wao maalumu kwa wengine; mtazamo ambao bila shaka ni wa kidhalimu, unaojengwa juu ya ubaguzi wa rangi, kujiona bora, kupenda nafsi na kukataa ubinadamu wa wengine. Na haya yamejidhihirisha waziwazi kupitia matamko yao katika vita vya mauaji ya halaiki wanayoendelea nayo hivi sasa dhidi ya watu wa Gaza — tunamuomba Mwenyezi Mungu awanusuru.
Hakika tunaposimama mbele ya maneno haya, lazima tushangazwe na kutahayari kwa sababu ya ukatili wa yale tunayoyaona, na ukubwa wa yale wanayoyaamini. Na hili linatufanya tukumbuke mwenendo na tabia aliyokuwa nayo Mtume (S.A.W) na akaiweka katika matendo halisi, na wakafuata Maswahaba baada yake. Tunageuza macho ya ulimwengu kuelekea kwenye mwenendo huo, huenda hilo likawa ni msukumo kwao wa kuunga mkono haki na kuipigania, na kuchukua hatua ya kupunguza maumivu ya wajane, wanyonge na waliodhulumiwa.
Basi huyu hapa Sayyidina Abubakar (R.A) alipotuma majeshi kwenda Shaam, alitoka akitembea pamoja na Yazid bin Abi Sufyan, akamwambia: "Hakika utakutana na watu wanaodai kuwa wamejitenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu — waache na yale wanayodai wamejitenga nayo kwa ajili Yake. Na utakutana na watu waliopunguza nywele katikati ya vichwa vyao — wapige hapo walipopunguza kwa upanga. Na ninakuusia mambo kumi: usimuue mwanamke, wala mtoto mdogo, wala mzee mkongwe, wala usikate mti unaozaa matunda, wala usiharibu miji iliyojengwa, wala usichinje kondoo wala ngamia isipokuwa kwa ajili ya chakula, wala usichome mitende, wala kuiangusha majini, wala usifanye khiyana, wala usiwe mwoga.”[8]
Na alikuwa Sayyidina Umar bin Al-Khattab (R.A) alipokuwa akiwatuma majemadari wa majeshi, alikuwa akiwausia kumcha Mwenyezi Mungu Mtukufu, kisha akisema wakati wa kufunga bendera:
“Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, nendeni kwa msaada wa Mwenyezi Mungu kwa ushindi na kushikamana na haki na subira. Piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu dhidi ya wanaomkufuru Mwenyezi Mungu. Wala msifanye uadui; hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafanyao uadui. Msikimbie katika mapigano, wala msifanye msiwaseme vibaya maiti wala msifanye israfu mtakaposhinda, wala msiue mzee mkongwe, wala mwanamke, wala mtoto mdogo. Na jihadharini na kuwaua hawa pindi majeshi yatakapokutana, na katika joto la mapambano, na wakati wa kufanya mashambulizi ya ghafula.”[9]
Top of Form
Bottom of Form
Na katika hili linaonekana wazi msimamo wa Uislamu na Mtume wake (S.A.W) kuhusu “mwingine” na namna alivyoamiliana naye, hata katika mazingira ya vita. Jambo hili linapelekea kuuliza swali — na hali ya kuwa tuna yakini kuwa halina jawabu, kwani dhamiri zimekufa, fadhila zimetoweka, na unafiki wa kisiasa umetawala ambao umeweka mbele maslahi — maslahi tu:
Vipi kama wangeoneshwa kwa Mtume wetu (S.A.W) watoto wa Gaza, ambao wamechanwa chanwa na risasi za adui na muovu? Na vipi kama angeona wanyonge na wagonjwa wa umma wetu ambao wameuawa kwa hila na khiyana? Vipi kama mwenye tabia njema kabisa — ambaye tabia yake njema ilimjumuisha kila mtu bila ubaguzi — angeona hali yetu, akauona umma wake umetapakaa na baadhi yao kwenda kinyume na wengine katika wakati ambao nusura na msaada vinahitajika? Na vipi kama angeshuhudia kuwa tumewaacha wanyonge mikononi mwa adui asiyejua dini, utu, mikataba wala maagano?
Hakika sisi tunapozungumza kuhusu mwonekano wa ukubwa katika utu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) tunawapa wasomaji nyanja za kumfuata na kumuigiza. Na je, jamii zinahitaji kitu kingine isipokuwa maadili yake (S.A.W) ili yafuatwe, na kuinuka kutoka kwenye hali yao ya kuporomoka kwa mali? Na je, tunajua wakati wowote ambapo nguvu za uovu zimetamalaki zinastahiki zaidi kuiga kwake tabia na mwenendo kuliko wakati huu?
Tunamuomba Mwenyezi Mungu atimize ndani yetu kile anachokitaka kutoka kwetu. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kufanikisha makusudio.
([1]) Ufafanuzi wa Wasifu Mkuu, Al-Sarakhsi (alikufa 483 AH), (1/79), Kampuni ya Utangazaji ya Mashariki, 1971 AD.
([2]) Musnad Ahmad, (38/136), Na.: (23030).
([3]) Al-Sunan Al-Kubra, Al-Bayhaqi, (9/145), No.: (18125).
([4]) Kamusi Kuu, Al-Tabarani, (22/393), Na.: (977).
([5]) Tazama: Mahusiano ya Kimataifa katika Uislamu, Muhammad Abu Zahra, uk. 417.
[6] Rabi' al-Abrār wa Nusus al-Akhyār, Jar Allah al-Zamakhshari (aliyefariki mwaka 583 Hijria), juzuu ya 4, ukurasa wa 133, Mu'assasat al-A'lami, Beirut, chapa ya kwanza, mwaka 1412 Hijria.
[7] Tazama: Ahkam al-Harb fi al-Islam wa Khasa'isuha al-Insaniyya, Dkt. Wahbah al-Zuhayli, ukurasa wa 8-9, Dar al-Maktabi — Syria, chapa ya kwanza, 1420 Hijria — 2000 Miladia.
[8] - Muwatta Malik, Kitabu cha Jihadi, mlango wa Kukataza Kuwaua Wanawake na Watoto katika Vita, (2/447), Hadithi namba: (10).
[9] - Uyūn al-Akhbār, Ibn Qutaybah, 1/185, Dār al-Kutub al-‘Ilmiyyah – Beirut, 1418 H.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
